Spika aweza kutofika 2015 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Spika aweza kutofika 2015

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by ByaseL, Aug 3, 2011.

 1. B

  ByaseL JF-Expert Member

  #1
  Aug 3, 2011
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 2,223
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 135
  [TABLE="class: MsoNormalTable, width: 599"]
  [TR]
  [TD]
  Joseph Magata ​

  Tuliipuuza kauli ya Pius Msekwa anayeonya hivi: (“Spika anayeonyesha kupendelea upande mmoja au kundi moja dhidi ya jingine, basi hatadumu sana katika nafasi hiyo.”)

  Badala yake wiki chache zilizopita tukavamia kauli ya “watu wa Kariakoo” kama ilivyokimbiliwa kauli ya “wivu wa kike” mwaka 2002. Pius Msekwa ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara).
  Katiba ya Jamhuri (Ib. 89) imelipa Bunge mamlaka ya kujitungia kanuni zake linapojiendesha. Humu nitazitumia za mwaka 2007.
  Tulijulishwa kuwa swali la Tundu Lissu halikujibiwa ili kuheshimu kesi inayolihusu: (Kan. 64(1)(c)).

  Hivyo, Tundu Lissu amefikisha maelezo kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge akipinga kwamba kesi ile haihusiani na swali lililozuiwa: (Kan. 5(4)).

  Hivyo, hii si vita ya U-CHADEMA na U-CCM. Wala si vita ya mfumo jike na mfumo dume. Asiyependa neno “mdanganyifu” limfike mmoja wa hawa, basi asiifuatilie kesi hii.
  Kanuni zinamwajibisha Spika kuitisha kikao cha kamati ile na kulijulisha Bunge uamuzi uliofikiwa: (Kan. 5(5)). Kamati ambayo Tundu Lissu naye ni mjumbe (Hansard: February 08, 2011). Sijui kama atashiriki kama mjumbe au mlalamikaji au vyote.
  Kwenye Kanuni, neno “adhabu” limetokea mara 12 likimkabili mbunge. Wakati neno “Spika” limetajwa mara 441, lakini halibanwi na neno “adhabu”.
  Wasomaji wengi tuna ugonjwa uitwao “Skimming” unaotufanya tudhani sentensi moja inatosha kutuelewesha habari nzima, na tusihitaji kuendelea hadi mwisho.
  Kanuni ya 63 inaitwa “Kutosema Uongo Bungeni”. Ugonjwa ule unaweza kumfanya anayeiona akabishana mitaani ukisema “Spika akithibitika kadanganya “Bungeni”, basi kanuni hii itamshughulikia kama inavyowashughulikia mliowahi kuwaona”.
  Wakati ukiisoma kanuni hii hadi mwisho utaona kuwa nayo haigusi jina “Spika”, japo yumo ukumbi uleule ambao “wasema uongo” huadhibiwa nayo wanaposhindwa kuthibitisha kauli zao.
  Kanuni (Kan. 60 (15)) inasema: (..Katika mjadala wowote, mawaziri watatajwa kwa majina ya nyadhifa zao na wabunge watatajwa kwa kutumia neno “Mheshimiwa” kabla ya majina yao.). Hapa, pia jina “Spika” halitajwi.
  Je, mahakama ililitaarifu Bunge kuwepo kesi za wabunge wale? Taarifa hiyo ingekuwa kigezo kwa yeyote aliyeiona asimamie “ukweli” kwamba swali la Tundu Lissu halikutakiwa.
  Kanuni 63(2) inasema: (mbunge yeyote anapokuwa akisema bungeni hatachukuliwa kuwa anasema uongo iwapo anafanya rejea ya habari kuhusu jambo fulani lililotangazwa au lililoandikwa na vyombo vya habar).
  Habari yoyote iliyowahusisha kina Tundu Lissu, hata ingekosewa, isingemfanya mbunge awe muongo anapoinukuu. Kanuni hii ingemlinda. Hata hivyo, jina ’Spika’ hapa haliguswi pia.
  Spika Anne Makinda ni Mbunge wa Njombe Kusini. Ukitetea kwamba Kanuni inapomgusa ’mbunge’ naye anaguswa, basi uwe tayari kujibu kwa maswali utakayoulizwa?
  Swali kama hili, kwa nini huo ubunge wake haumtumbukizi kwenye hatua na matokeo yaleyale kama yanayowawajibisha wabunge? Kwa nini yeye isubiriwe Kamati ya Kanuni, tena katika hatua ya mwisho ya kutangaziwa tu.
  Tutarajie nini kutoka kamati hii? Kanuni zina “Nyongeza ya NANE”, Ibara ya 3(3) (c) inayotaja moja ya majukumu ya Kamati hii ni: {kuchunguza na kutoa taarifa juu ya malalamiko yote kuhusu uamuzi wa Spika ambayo yamepelekwa mbele ya Kamati na Mbunge yeyote.}
  Tunapowasifu Wabunge kwa maamuzi safi, haraka tunakumbuka walivyoyapitisha, hasa zile sauti zao ’ndiyooo’ na ’siyooo’. Hatujafika kipindi cha kushuku sauti hizi zilingane mara kadhaa.
  Kikifika, basi iko siku maamuzi yaweza yasifanywe na wabunge kwa sababu kura zimelingana{Kan. 79(2)}, na hivyo Spika akayafanya kwa kura yake (tiebreaker vote).
  Mabere Marando wa CHADEMA angemshinda Anne Makinda, basi siku kura zingelingana, kanuni hii ingemfanya apige kura itakayoleta maamuzi licha ya kwamba CCM wamo zaidi ya asilimia 78 bungeni.
  Inapoanza ibara ya 66 ya Katiba, kuna maneno ’wajumbe wa Bunge’. Kiingereza kina maneno ’Members of the National Assembly’. Mwenzako anaweza kukusimulia “Nimesoma Katiba nikaelewa kwamba tafsiri ya maneno ’National Assembly’ ni ’Bunge’.
  Kwenye Sheria ya Kinga za Bunge {Na. 03, (1988)}, unaposoma Ibara yake ya 2 huvuki maneno 92 bila kukutana na sentensi hii {“the Speaker is not a member of the National Assembly”}.
  Katiba {Ib. 62(1)} imetumia neno “Wabunge” ambalo kwa kiingereza limeandikwa “National Assembly”.
  Wataalamu wetu wa Kiswahili walitutengenezea Kamusi ikiwa na jina NATIONAL ASSEMBLY pia jina PARLIAMENT. Yote mawili imeyatafsiri kwamba ni “Bunge” {TUKI/English-Swahili Dictionary, ISBN: 9789976911299; uk. 589 na 639}.
  Nina kitabu cha Pius Msekwa {Reflections on the First Decade of Multi-Party Politics in Tanzania, ISBN: 9987-9092-1-3}. Msekwa ametumia jina “Parliament” na jina “House of the Parliament” kwa kifupi “House”. Hatumii jina “National Assembly”.
  Zile kanuni zimeandikwa Kanuni za Kudumu za Bunge. Sheria ya Kinga imetumia jina Standing Orders of the Assembly. Pius Msekwa ametumia jina Standing Orders of the House {ISBN: 9987-9092-1-3, uk. 184}.
  Kwenye Kamusi za Uingereza, jina “National Assembly” halifananishwi na jina “Parliament”{Oxford Dictionary of Law: ISBN 9780192806987, uk. 381, 350, 574}. Nchini Ufaransa “National Assembly” ni sehemu ya “Parliament”.
  Tumeona Sheria ya Kinga {Sheria Na. 03, (1988): Ib. 2} lilivyotumika neno hili. Hapo, kamusi yetu (TUKI) inatufundisha tutamke “Spika siyo sehemu ya Bunge”.
  Matokeo ya kesi nyingi duniani hayaishii kuipata ile haki inayotafutwa. Ukitafakari alichokifanya Tundu Lissu kuiendea Kamati ile, husiti kutafakari pia kuibuka kwa maswali haya mawili: “Je, Spika ni sehemu ya Bunge (National Assembly)?” au “Je, Spika ni sehemu ya Wabunge?”.
  Mjadala wa maswali hayo hautakosa wanaosema ni Spika sehemu ya “Bunge” au sehemu ya “Wabunge”. Wenye kusema hivi watasaidia kujibu hoja nne zifuatazo.
  Hoja ya kwanza ni kwamba mbona tumedokezwa humu hali ya Kanuni kuchunga sana jina “wabunge” na si jina “Spika”?
  Hoja ya pili inayofanana, ni rungu la Kanuni kushukia “wabunge” wanaotuhumiwa, tena kwa kuzitaja adhabu. Wakati tuhuma zinazomhusu Spika kama hizi za Tundu Lissu, tunasubiri hadi isomwe taarifa ya Kamati ya Kanuni. Na siku itakaposomwa, sijui ni lini, anaisoma Spika mwenyewe mlalamikiwa: {Kan. 5(5)}.
  Hoja ya tatu inatokana ukweli kwamba mle ukumbini anayegundua ukiukwaji hahitaji aelekezwe mwongozo wakati anaujua. Anatakiwa kusimama atamke maneno “Kuhusu utaratibu”. Hii inamnyamazisha na kumkalisha mbunge aliyekuwa anaongea ili huyu aliyesimama aitaje kanuni iliyokiukwa: {Kan. 68(1-3)}.
  Tatizo ni kwamba anayesimamama anaweza kujikuta naye anakosea badala ya kurekebisha. Matokeo yake ni kuaibika, kupoteza muda na hata kuonekana amedanganya.
  Hivyo, huwa ni nafuu kujilinda na mbinu ya kutumia Kanuni 68(7) ya kuomba “Mwongozo” kutoka kwa Spika {Pius Msekwa, ISBN: 9987-9092-1-3, uk. 181-182}.
  Nimeshaona hata watoto wakiigiza kufanya Bunge lao michezoni, wanamchagua “Spika” awape “Mwongozo”. Sijawahi kuona watoto wakitumia neno “Kuhusu utaratibu”, dalili kwamba linatumika mara chache hadi kudhaniwa kuwa halipo.
  Je, ni lini ilithibitika kwamba unapokalia kiti cha u-Spika, basi na akili yako inaongezeka hadi wenzako wakuombe “Mwongozo” mara nyingi?
  Si kwamba Spika anawazidi akili, bali ni tahadhari kwa matokeo ya kukosea kanuni. Tumeziona Kanuni zinazoweza kulibana jina “Mbunge” na hapohapo zisitaje jina “Spika”. Tumeiona Kanuni 63 inayoitwa “Kutosema Uongo Bungeni”. Inamwajibisha mbunge, lakini haimwajibishi Spika.
  Je, Spika na wabunge wako taasisi moja wakinufaika au kuwajibika kwa kanuni zilezile za hiyo taasisi?
  Hoja ya nne inatokana na Kanuni {Kan. 5(1)} inayolazimisha kuheshimu Katiba. Katiba yetu {Ib. 13(2)} inakataza ubaguzi. Je, unauonaje utaratibu mzima wa kuwajibishwa mle ukumbini? Je, utaratibu uko sawa kwa Spika na wabunge?
  Nimechagua hizi hoja nne tu ili wale wenzetu watufafanulie tunapobishana nao.
  Mbunge waweza kumtania “kwa nini mlipitisha maamuzi kama yale bungeni?”. Hivi, Spika ukimuuliza halafu akakujibu “sikuwahi kuyapigia kura”, utampinga kwa hoja gani?
  Pius Msekwa amesema, duniani, Maspika hujulikana kama refa {ISBN: 9987-9092-1-3, uk. 181}. Ile Sheria ya Kinga {Ib. 2} tumeona ikitamka {“the Speaker is not a member of the National Assembly”}. Ingeigwa mpirani ingetamka {“refa sio sehemu ya wachezaji”}.
  Kuna haja ya kutolitegemea neno moja tu “Bunge” linalozaa maneno “Wabunge” au “Bungeni”. Hauonekani utata linapotajwa neno “Parliament” likionyesha mfumo mzima unaomgusa hadi rais.
  Ile kauli ya Pius Msekwa inapatikana humu kitabuni mwake. Tuichambue kauli ile kwa kuanza na Kanuni 68(10) inayosema hivi: {Uamuzi wa Spika kuhusu suala lolote la utaratibu utakuwa ni wa mwisho}. Tunapotafakari hata kile kitendo cha kumtoa nje Ezekiah Wenje au kama ilivyokuwa kwa John Cheyo, basi tuzingatie kuwepo kwa kanuni hii.
  Je, uamuzi wa Spika, ambao ni wa mwisho mle ukumbini, ni uamuzi wa haki au uonevu? Ndipo hapa Msekwa anapotuambia kwamba tusijidanganye kuwa uamuzi wa Spika ni wa mwisho. Uamuzi ule unaweza kukatiwa rufani kwenye Kamati ya Kanuni:{ISBN: 9987-9092-1-3, uk. 196}.
  Hivyo, wabunge watueleze ngazi ya juu wanayodhamiria kuifikia iwapo kamati kama hii nayo imeshindwa kushughulikia rufani dhidi ya Spika. Kamati ambayo Kiongozi Mkuu wa Kambi ya Upinzani ni mjumbe.
  Siyo tuendelee kusoma habari za ubabe wa Spika, kama vile kuukalia utetezi fulani wakati hajafikishwa kwenye kamati hii. Haitofautiani na kulalamika kuhusu mhalifu, wakati hujamshtaki kortini.
  Tumeona Msekwa akisema Spika atakayeendekeza tabia ya kuwaonea baadhi ya wabunge au kikundi fulani, ili kuupendelea upande mwingine, basi hatadumu katika nafasi hiyo.
  Je, kuna dalili zozote za kutokea alichoonya Msekwa? Taarifa zinaonyesha kuwa Tundu Lissu hayuko peke yake. John Mnyika naye ameripotiwa kunuia kufikisha malalamiko kwenye kamati ileile. Haijajulikana ni nini hatima ya matukio haya.
  Sizungumzii sana suala la Ezekiah Wenje kwani limekuja nikiwa najiandaa kutuma makala hii. Hata hivyo, hadi hapa tumeshaona kuwa, njia ya kumrekebisha Spika si kubishana naye mle ukumbini au kwenye vyombo vya habari. Fursa iliyopo ni kumfikisha kwenye kamati hii kama alivyofanya Tundu Lissu.
  Hata hivyo, Pius Msekwa hajatutafunia kila kitu hadi jinsi Spika anavyoweza kuondoka kwenye nafasi hiyo.
  Uhalali wa kumuondoa Spika unapatikana kwa kuletwa hoja itakayoungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge {Kan. 134(1-5)}. Inawezekana Spika akapendwa hata na asilimia 99 ya wabunge wote. Hivyo, ikija hoja ya kumuondoa ni wazi kuwa Spika atakuwa na uhakika wa kubaki kitini kwani wingi wa kura uko kwake.
  Je, uhakika huo unampa Spika uhalali mwingine wa kubagua wengine na kuwapendelea wengine? Kama jibu ni “ndiyo” basi tafsiri ni kwamba wale wengi wamemtuma Spika akamilishe kazi ya ukandamizaji kwa wale wachache.
  Lakini, wabunge na Spika wana kiapo cha kuitetea na kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano: {Kan. 9(20), 24(1)}. Katiba ambayo ibara yake 9(h) na 13 zimekataza ubaguzi au upendeleo.
  Ni mbunge gani anaweza kusimama aipinge hoja ya kuilinda Katiba? Anayeipinga hoja hiyo, haishii kukiuka kiapo chake, bali pia, ni analishawishi Bunge zima likiuke viapo vyao kisha waivunje Katiba.
  Hivyo, inapothibitika kwamba Spika kafanya maamuzi ya upendeleo au ubaguzi, basi haishangazi suala hilo kuhusishwa na kukiuka vipengele vile vya Katiba yaani 9(h) na 13 . Kama Mbunge mmoja akiujengea hoja uthibitisho huo, basi Spika anaweza kujiuzulu kabla hata uamuzi wa hoja hiyo haujafikiwa {Kan. 134(6)}.

  [/TD]
  [/TR]
  [/TABLE]
  Source: Tanzanu Daima Jumapili
   
Loading...