Somo la Utafiti katika fasihi simulizi

Tanzania Nchi Yetu Sote

JF-Expert Member
Mar 12, 2017
505
854
FB_IMG_1492103076614.jpg


Mada hii inalenga kukuwezesha:
(a) Kufafanua maana ya neno "utafiti"
(b) Kueleza historia fupi ya utafiti katika bara la Afrika
(c) Kuorodhesha vifaa vinavyopaswa kuwepo ili utafiti ufaulu
(d) Kuonesha vidato vinavyopaswa kufuatwa ili utafiti muafaka utimizwe
(e) Kueleza manufaa ya utafiti

Kulingana na ufafanuzi wa A standard English - Swahili Dictionary, maana ya neno utafiti ni uchunguzi, ni ngeni. Nayo Kamusi ya Kiswahili Sanifu inaueleza utafiti kuwa ni uchunguzi wa kisayansi. Utafiti ni mbinu ya udadisi wa hali ya juu. Maana inayoelezwa na Kamusi ya Kiswahili Sanifu inafaa zaidi. Sababu ni kuwa inafungamana na neno Utafiti kitaaluma.

M.M. Mulokozi ametoa historia fupi juu ya utafiti wa fasihi simulizi katika Makala za Semina ya Waandishi wa Kiswahili (1983). Mhakiki huyu anaonesha kwamba lengo la utafiti huathiriwa na itikadi ya mdhamini wa mtafiti fulani. Aghalabu, mdhamini hutaka utafiti unaofanywa kuridhishha mapendekezo na mapendeleo yake.


Jadili maoni ya watafiti weupe juu ya bara la Afrika katika karne ya kumi na tisa.......................................................................................................................................................
Jambo hili laelekea kuwa kweli hususani tukizingatia kipindi cha ukoloni. Kwa miaka mingi utafiti wa nyanja mbalimbali za maisha ya Mwafrika ulielekezwa kwa nia na kwa sababu zisizokuwa na mantiki. Unaweza kukumbuka visa asili vyovyote vinavyochukiza juu ya utu wa Mwafrika?

Mulokozi anadondoa ithibati nyingi kudhihirisha kwamba utu wa Mwafrika haukuthaminiwa kwa lolote lile. Chambilecho mwandishi Frantz Fanon, Mwafrika alichukuliwa kuwa kinyume cha utubora. Maoni makali sana yanayothibitisha madai haya yamedondolewa na Mulokozi (1983) kutoka kwenye maandishi ya G.F. Hegel alipokuwa akiandika historia ya ulimwengu. Ijapokuwa Mulokozi ameitoa tafsiri ya Hegel, nasi pia tumewajibika kuitoa yetu: Hegel anasema:

Afrika halisi, yaani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara haijaingiliana wala kuhusiana historia kwa lolote lile na sehemu nyingine za ulimwengu. Afrika ni kama nyumba iliyojifunga kwa ndani na kujisahaulisha kusijulikane chochote kilichomo. Afrika ni eneo lililozaliwa juzi inayobarizi nje ya mipaka ya historia inayofahamiwa na kujulikana. Ni eneo ambalo limefunikwa gubigubi kwa giza totoro, giza la usiku. Na ijapokuwa Mwafrika bado anaishi porini na hawezi kamwe kufugwa, anasawiri kwa mbali ishara za kibinadamu kama tunavyozifahamu. Hata hivyo, huwezi kutarajia ustaarabu wa aina yoyote kutokana na kiumbe wa aina hii. Kwa hiyo, unaliacha bara la Afrika na hatutalitaja tena daima dawamu. Afrika si sehemu ya ulimwengu kihistoria. Kile tunachofahamu kuwa Afrika ni roho ambayo haijabadilika wala kukua tangu hapo na uumbaji. Tumegusia Afrika hapa kunasawiri angalau kwa kifupi sura ya ulimwengu ulivyokuwa kabla athari zozote za kihistoria kutokea. Historia ya ulimwengu husonga ikitokea Mashariki kuelekea Magharibi. Uropa ni mwisho wa historia; Asia chanzo chake. (Tafsiri ni yangu toka Uk. 178 Katika Zirimu & Andrew Gurr). Utafiti wa mwanzo kumhusu Mwafrika katika vipengele vyake vyote ulielekezwa na maoni kama haya.

Fasihi simulizi ya Kiafrika ilianza kushughulikiwa tangu mwaka wa 1850. Hapo ndipo watumishi wa kwanza wa serikali za kikoloni walipoanza kuzungumzia utamaduni wa Mwafrika. Hii ina maana kwamba fasihi simulizi ya Waafrika ilitajwa bila kutarajia. Iliangaliwa kama sehemu ya utamaduni wa Wafrika.

Tokea miaka ya 1930, Waafrika wengi walianza kuzungumzia mambo yaliyohusu utamaduni wao. Walipewa motisha ya kuzungumzia mambo yaliyohusu utamaduni wao kutokana na uandishi wa Uafrika na pia kutokana na mwamko wa utaifa.

Baada ya uhuru kupatikana, somo la fasihi simulizi lilianza kushughulikiwa kwa mapana zaidi. Waandishi kama Ruth Finegan, Rose Mwangi, Taban Lo Liyong. Okot p'Bitek, J. Nandwa, A. Bukenya, B.M. Lusweri, N.Kipury na Wanjiku Kibira walijitokeza. Huko Tanzania Marehemu Bi. Matteru ameishughulikia fasihi hii sana. Afrika ya Magharibi nayo imezaa vigogo kama Ben Dan Amos, Boscom na Isidore Okpewho.

Kwa wakati huu kuna watafiti wengi wa fasihi simulizi wageni kwa wenyeji. Mara nyingi watafiti hawa hutumia njia za kimseto kutafitia fasihi simulizi. Na wageni si lazima wawe watu weupe. Wanaweza kuwa Waafrika wanaotoka maeneo tofauti na yanayotafitiwa.

Licha ya kwamba mtafiti anaweza kwenda uwanjani na kutumia ama njia za wenyeji au njia za kigeni au mchngamano wa zote kutafiti, mtafiti huyo anatazamiwa kuingiliana na wanajamii wa fasihi anayoitalii. Nao utafiti si ukusanyaji wa data tu; utafiti unapaswa kuchochewa na uadadisi fulani kwa upande wa mtafiti. Kutokana na udadisi huu, mtafiti anaweza kuwahoji wanajamii wa jamii inayohusika. Mtafiti anaweza kutumia hojaji. (Hojaji ni orodha ya maswali yanayoulizwa na mtafiti)

Eleza hatua za maendeleo zilizopigwa katika utafiti wa fasihi simulizi tangu kupatikana uhuru katika jamii za Afrika Mashariki.
Aghalabu, hojaji hutumiwa kukusanya maoni ya watu waliosoma. Maswali ya hojaji yana nafasi ya kuandikia majibu kwenye karatasi. Lakini mtafiti anaweza vilevile kutumia hojaji bila kuandika na kusambaza kwenye karatasi.

Inampasa mtafiti awafahamishe wahojiwa mapema kwamba atawahoji. Kama hafanyi hivyo huenda akashukiwa kuwa ama ni mdakuzi au mpelelezi wa siri.

Njia nyingine ya kutafiti ni kukutana na watu waliofahamu jambo analolitafuta mtafiti.

Jadili manufaa na upungufu wa njia mbalimbali za kukusanya data katika fasihi simulizi.Jambo litakalomsaidia. Pia, mtafiti anaweza kupata data kwa kushiriki katika sherehe mbalimbali na kujionea yale yanayotendeka. Hatimaye, mtafiti anaweza kuzungumzia jambo lolote kuhusu sherehe hizoo kutokana na msimamo wake. Namna ya kukusanya data hutegemea lengo la utafiti na jinsi utafiti huo unavyopaswa kutumiwa.

Lakini kutumia njia hizi au baadhi ya njia hizi kukusanya data hakuufanyi utafiti kuwa yakini. Ili ujuzi wa fasihi simulizi ukubalike kuwa kweli, unapaswa kuthibitishwa kisayansi.

Orodhesha na ujadili hatua zinazofuatwa katika kuthibitisha ujuzi wa kisayansi
K.S. Goldstein katika kitabu chake cha A guide For Fieldworkers in Folklore (1964) anasema kwamba utafiti wa kisayansi hufuata hatua zifuatazo:


  1. Lazima kuwa na tatizo analotaka kulitatua mtafiti. Tatizo hili huitwa kisio au haipothesia. Haipothesia ni jambo linalokubaliwa ijapokuwa halikuthibitika. Lengo la utafiti huwa ni kuyakinisha ukweli wa haipothesia. Haipothesia humwongoza mtafiti katika kuvibainisha vifaa vinavyohitajika na data zinazopaswa kuwepo ili utafiti wake ukamilike.
  2. hatua ya pili inahusiana na ya kwanza; nayo ni kutafuta data mwafaka na vifaa vinavyosaidia kuziwasilisha data hizo kutegemeana na aina ya utafiti unaofanywa. Mtafiti anaweza kuhitaji kalamu, karatasi, kinasa sauti, tepu video, kamera, kamera za sinema, mkalimani na kadhalika.
  3. Sehemu ya tatu ni ya ukusanyaji wa data. Data zinaweza kukusanywa kwa kutumia ama baadhi ya njia zilizotajwa hapo awali.
  4. Hatua ya nne inahusu uwasilishaji wa data. Data hizo zinaweza kuwasilishwa kwa njia mbili kulingana na jinsi utafiti ulivyofanywa.
  • Pengine matini itatafsiriwa neno kwa neno na baadaye kutafsiriwa kufungamana na maana iliyokusudiwa katika lugha asilia.
  • Data zinaweza kuwasilishwa moja kwa moja kulingana na lugha asilia ya mtafiti.
5. Baada ya uwasilishaji wa data kufanywa, uchambuzi wa hizo data hufuata. Katika fasihi simulizi, yaliyomo na jinsi yanavyowasilishwa ni baadhi ya mambo yanayozingatiwa. Mambo mengine kama vile mandhari na sherehe pia yanahitaji kutiliwa maanani.

6. Ulinganishaji wa makisio ya mwanzo na matokeo ya uchambuzi wa data ni hatua ya mwisho kudhihirisha ujuzi wa kisayansi. Kutokana na ulinganishaji, huenda makisio ya mwanzo yayakinishwe kuwa sahihi. Inawezekana pia kwa makisio kurekebishwa au kufutiliwa mbali. Ikitokea kwamba makisio ya awali yamefutiliwa mbali, tasnifu mpya zitaibuka kutokana na haipothesia zilizothibitishwa na uchunguzi wa kweli.

Onyo: Mtafiti anapaswa kukumbuka kwamba ili utafiti wake uzalishe matokeo yanayotegemewa, anapaswa kufahamu mazingira yote yanayozunguka mahali anapopafanyia utafiti wake na majaribio yake. Jambo hili litamwezesha kuainisha na kuzuia kadhia zinazoweza kuuingilia utafiti na kusababisha matokeo yasiyokuwa ya kweli kupatikana.

MATATIZO YANAYOWEZA KUMKABILI MTAFITI
Kuna matatizo mengi yanayoweza kumkabili mtafiti wa fasihi simulizi G. Kubik (1977) anaainisha mambo matano:


  1. Inawezekana kwamba mtafiti haelewi lugha inayosheheni tatizo analotafiti juu yake. Hivyo basi, atategemea mambo ya kuambiwa, mengine ambayo yatakuwa yamepotoshwa.
  2. Ni vigumu kupata miktadha inayochukuana vizuri na tanzu mbalimbali za fasihi simulizi kwa mfano, nyimbo za matanga huimbwa vizuri zaidi wakati mtu ameaga dunia. Haziwezi kuimbwa hovyo hovyo. Na muktadha wa matanga huenda usimsaidie mtafiti vizuri. Fikiria jinsi utakavyochukuliwa na watu wengine ikiwa wakati wakiomboleza, wewe utakuwa ukitembea huku na huko na kinasa sauti chako...ama sijui...Kamera ya sinema yako. Utachukuliwa kuwa mchawi.
  3. Ushirikina ni tatizo jingine, mtafiti anaweza kufikiria kwamba atalogwa na watu ambao jamii yao inatafitiwa inaweza kumshuku mtafiti hasa iwapo huyo mtafiti ni mgeni. Mgeni anaweza kufikiriwa anataka kujua siri za wenyeji.
  4. Tatizo lingine linaloweza kumkumba mtafiti ni mapendeleo ambayo huweza kuzuka pale ambapo mtafiti atadanganywa kuhusu asiyoyajua juu ya fasihi simulizi ya jamii fulani.
  5. Pia ikiwa mtafiti anatafiti juu ya jamii yake mwenyewe, kuna mambo atakayoyapunguza kwa kuwa hayaathiri matokeo ya utafiti wake. Mengine yatapuuzwa kwa sababu yanaeleweka. Haya ni mapendeleo.
  6. Tafsiri za matini ndilo tatizo la mwisho tutakalolizungumzia hapa. Iwapo data zinazowasilishwa, mtafiti atakuwa na shida ya kupata msamiati utakaowasilisha dhana zote kwa usawa kutoka lugha chanzi hadi lugha lengwa.
Kwa kutoa mifano inayofaa, jadili matatizo yannayoweza kumkabili mtafiti katika fasihi simulizi anapotafiti.
MANUFAA YA KUFANYA UTAFITI KATIKA FASIHI SIMULIZI

  1. Kusahihisha mielekeo mibaya kuhusu fasihi simulizi ya Kiafrika na utamaduni wa Mwafrika kwa ujumla.
  2. Kufahamu mambo yanayopatikana katika fasihi simulizi ya Mwafrika kwa njia ya utaalamu.
  3. Kuchanganua data tunazopata na kuhitamidi ukweli unaohusu maisha yetu kutokana nazo.
  4. Kuelewa matatizo ya uwanja yanayowakabili watafiti.
SOMA ZAIDI >>>>>UTAFITI KATIKA FASIHI SIMULIZI | MWALIMU WA KISWAHILI
 
Back
Top Bottom