BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,015
Slaa: Fedha za EPA kiinimacho
Atamba anao ushahidi kuthibitisha
na Edward Kinabo, Moshi
Tanzania Daima~sauti ya Watu
Atamba anao ushahidi kuthibitisha
na Edward Kinabo, Moshi
Tanzania Daima~sauti ya Watu
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, amesema fedha zilizodaiwa kurejeshwa baada ya kuibwa kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni Nje (EPA), hazikupelekwa kwenye Mfuko wa Pembejeo za Kilimo kama ilivyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete na kisha kuidhinishwa na Bunge, Januari, mwaka huu.
Dk Slaa, mmoja wa majemedari wakuu wa mapambano dhidi ya ufisadi ukiwamo huo wa EPA, alisema amebaini hilo kutokana na taarifa za uhakika alizozipata.
Akifafanua zaidi, alisema taarifa alizo nazo zinaonyesha kuwa fedha hizo za EPA zilikuwa zimeshatumiwa na serikali tangu Oktoba mwaka jana, zikielekezwa katika matumizi mengine.
Kutokana na ukweli huo, Dk. Slaa alisema serikali imelihadaa Bunge kwa kuliomba liidhinishe fedha hizo kiasi cha sh bilioni 53, kwenda kwenye Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, wakati ilijua fika kwamba fedha zilishatumika kinyume na taratibu tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Dk. Slaa, aliyekuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mbwera, Kata ya Masama, mkoani Kilimanjro, alisema ana ushahidi kuwa fedha hizo zilishatumiwa kinyume na utaratibu kabla hata Bunge halijakutana katika mkutano wake wa Januari, mwaka huu, ulioidhinisha fedha hizo kwenda kwenye Mfuko wa Pembejeo za Kilimo.
Ndugu zangu nina taarifa na ushahidi kwamba zile fedha za EPA mlizoambiwa zimerejeshwa...zile bilioni 53 ambazo Rais Kikwete alisema zitaelekezwa kwenye pembejeo, zilishatumika tangu Oktoba mwaka jana.
Nina taarifa kuwa fedha hizo zililiwa kabla Bunge halijakaa Januari mwaka huu. Zilishatumika kabla Bunge halijaidhinisha fedha hizo kwenda kwenye pembejeo fedha zile hazikwenda kwenye pembejeo za kilimo, Bunge lilikuwa tu linaidhinisha makaratasi lakini fedha zenyewe zilikuwa hazipo...Bunge liliidhinisha fedha hewa, alisema.
Tulimwambia Kikwete tangu mwanzo watuambie hizo fedha zilizorejeshwa zilikuwa zinarejeshwa na nani na ziliwekwa kwenye akaunti gani, lakini walificha. Nina ushahidi fedha hizo zilishaliwa tangu Oktoba mwaka jana. Mwenye uwezo wa kukanusha akanushe, alisema Dk. Slaa.
Alisema CHADEMA inaendesha kampeni maalumu ya kuhakikisha fedha zote zilizoibwa na mafisadi zinarejeshwa na zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Aliwataka wananchi hao wasirudie tena makosa ya kumchagua mbunge na chama ambacho hakiwezi kusimamia rasilimali zao, na akawataka kujiunga na CHADEMA na kujipanga kushinda viti vyote vya eneo hilo katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba.
Januari mwaka huu, Bunge liliidhinisha fedha hizo zitumike kwenye Mfuko wa Pembejeo kama alivyoaagiza Rais Kikwete. Kutokana na hatua hiyo, Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, alisema fedha za EPA zilizorejeshwa hivi karibuni na watuhumiwa mbalimbali, zimekuwa msaada mkubwa katika kutekeleza mpango wa serikali wa kuboresha sekta ya kilimo.
Wasira alisema wakulima nchini wameshaanza kunufaika na fedha hizo kupitia programu mbalimbali kama ilivyoelekezwa na Rais Jakaya Kikwete. Wasira alisema kuwa fedha hizo zimesaidia katika kutekeleza mpango wa serikali wa kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima na katika msimu huu, zaidi ya wakulima 700,000 wanatarajiwa kunufaika na fedha hizo.
Kwa mujibu wa Wasira, fedha hizo zimetolewa kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi na kupelekwa moja kwa moja kwenye Wizara ya Kilimo na Chakula. Hata hivyo, Wasira hakuwa tayari kueleza ni kiasi gani cha fedha kilichotolewa kusaidia mpango huo.