Sitta: Wasomi liokoeni taifa na ufisadi

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,147
Waandishi Wetu Dar na Mwanza

SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta amewataka wasomi kuwa waadilifu na wazalendo kwa nchi yao ili kumaliza tatizo la ufisadi ambalo linaelekea kulitumbukiza taifa kwenye machafuko.

Sitta aliyasema hayo kwenye mahafali ya 11 ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) yaliyofanyika mjini hapa jana.

Sitta alisema kwa hali ambayo nchi imefikia sasa inahitaji wasomi wenye nidhamu, uzalendo na maadili mema kwa sababu ndio watakaochangia kuijenga katika misingi endelevu ya utu, upendo na kutanguliza mbele maslahi ya wengi hususan wanyonge na maskini.

"Ni dhahiri kuwa matatizo na kero nyingi tunazozishuhudia hivi sasa kama vile rushwa, ubadhilifu wa mali za umma, yanatokana na kupungua kwa uthabiti wa uzalendo na uadilifu miongoni mwa jamii," alisema Sitta.

Alisema migogoro na machafuko katika nchi mbalimbali duniani yanachangiwa na baadhi ya viongozi kupuuza sauti za wananchi, mahitaji yao na kukumbatia maslai yao binafsi pamoja na marafiki zao.

"Hali hii ikiachwa iendelee, huwafanya wananchi kukosa imani kwa utawala uliopo, hatimaye wananchi baada ya kuchoshwa na mfumo huo hujiingiza katika vitendo vya kupinga waziwazi mfumo huo na matokeo yake ni chuki ndani ya jamii na hata umwagaji damu," alionya Sitta.

Spika Sitta alisema yeye binafsi anaunga mkono jitihada za Rais Jakaya Kikwete alizotangaza za kuleta mabadiliko katika sheria ya maadili na uchaguzi kwa lengo la kuwabana viongozi wote ili wazingatie uadilifu.

Alielezea hayo akionya juu ya viongozi ambao hutumia madaraka yao ili kujitajirisha kifisadi kwa mikataba mibovu, kujipatia uongozi kwa kutumia fedha na matumizi mabaya ya madaraka.

Sitta alisema katika hali ya sasa ya utaandawazi wanafunzi wanapohitimu elimu ya juu hujikuta wakikabiliwa na changamoto kubwa tatu ambazo alizitaja kuwa ni kuwa na nidhamu ya kazi, kumtii Mungu, njia za mkato za kujitajirisha kimaisha na wajibu wa kusimamia haki na kupinga dhuluma.

Awali makamu mkuu wa chuo hicho, Padri Charles Kitima alipokuwa akifungua mahafali hayo alianza kwa kunukuu maneno ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambayo yalikuwa yakihimiza usawa katika elimu.

Alisema kwa sasa nchi inahitaji dira sahihi juu ya kutumia elimu ili liwe taifa huru la kiteknolojia kiuchumi na kijamii.

"Uhuru wa kisiasa bila uhuru wa kiuchumi, kijamii na kiteknolojia ni kujenga taifa maskini na ombaomba, Hii hali ya kutegemea wengine imekuwa ni ugonjwa wa taifa hili kwa sasa," alisemaPadri Kitima.

Aliitaka serikali iweke mkakati wa kuwaandaa wawekezaji wa ndani na kudai kuwa hata wakiwa bilionea hela zao zikiwekwa ndani ya nchi watalifaa zaidi taifa letu.

Katika mahafali hayo ya 11, wanafunzi 1,648 wa vitivo mbalimbali walihitimu wakiwemo wahariri watatu wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd ambayo inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Wahitimu hao wa shahada ya uzamili ni Mhariri wa Habari wa Mwananchi, Yahaya Charahani, Mhariri wa Mwanaspoti, Frank Sanga na Mhariri wa Makala za Siasa, Hawra Shamte.

Wakati huu huo, jana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ilimtunuku Waziri wa Mendeleo ya Mifugo na Uvuvi, John Magufuli Shahada ya Uzamivu katika taaluma ya kemia.

Dk Magufuli alitunukiwa shahada hiyo huku akijivunia ugunduzi wa kisayansi wa kutumia maganda ya korosho ili kuzalisha kemikali ambao huzuia kutu kwenye chuma alioufanya wakati akifanya utafiti akisoma masomo yake.

“Kwa kutumia utafiti wangu huu maganda ya korosho hayatatupwa tena na badala yake yatatumiwa katika kuzalisha bidhaa nyingine." alisema Magufuli ambaye amekuwa na rekodi nzuri ya utendaji wake katika uwaziri nchini.

Magufuli ambaye ni waziri wa kwanza nchini kuweza kufanikisha mkakati wa kuwakamata raia wa kigeni wanaotuhumiwa wa uvuvi haramu katika eneo la Tanzania, bahari ya Hindi.

Katika mahafali hayo ya 39 yaliyofanyika jana, wanafunzi 4,331 wa fani tofauti, miongoni wakiwemo wanaume 2,051 na wanawake 2,280 walihitimu katika ngazi mbalimbali za shahada.

Habari hii imeandaliwa na Frederick Katulanda, Mwanza na Fredy Azzah, Dar
 
wewe kama spikaumeshindwa kushugulikia mambo haya ya ufisadi maana umezidiwa nguvu unaenda kuwaambia graduates wasaidie kuondoa ufisadi?how ?we unafikiri mawazo yao yako wapi?wanawaza wakikamata chaka tu ni kununua Prado au kakosa kabisa basi GX 100 ndo mambo mengine yaendelee.kwa kifupi hakuna watakalotekeleza hao,they are too young to do that
 
issue ya kupambambana na Mafisadi sio ya wasomi pekeyao, Mafisadi wa Tanzania wengi wao ni wasomi haohao na hata wasio wasomi wanawatumia wasomi haohao kufanikisha mambo yao ya kifisadi
mi nilidhani angeonyesha njia ya kupambana na mafisadi na sio usomi tu
 
Mtu mwenye njaa hawezi kuwa na msimamo. Wasomi hawalipwi vizuri, unadhani kitu gani kitawafanya waswe mafisadi? Mishahara haiendeani kabisa na kiwango cha bei za vitu na hali ya maisha kwa ujumla.

Rushwa imekuwa kama jadi, kila mtu anategemea kupewa chochote. Ufisadi umekaa katika uzi unaotuunganisha sisi wote. mhudumu wa ofisi anategemea chochote kutoka kwako anapofanya kazi yake ya kupitisha kabrasha lako kutoka ofisi moja kwenda nyingine. Utasikia mzee kumbe unaomba likizo nililitoa jarida lako leo kutoka kwa mhasibu kwenda kwa mkuu wa utawala etc.

Kukemea ufisadi kunataka sisi wote tuwajibike.
 
issue ya kupambambana na Mafisadi sio ya wasomi pekeyao, Mafisadi wa Tanzania wengi wao ni wasomi haohao na hata wasio wasomi wanawatumia wasomi haohao kufanikisha mambo yao ya kifisadi
mi nilidhani angeonyesha njia ya kupambana na mafisadi na sio usomi tu
Yani wakuu nyote mnakuwa "wanasiasa"?

Tuache kwenda na upepo kama wanavyotaka kutupeleka na porojo za UFISADI!

Hawa hawa ndo walikataa tangu mapema kuwa hakuna kitu kama hicho. Ghafla hawa hawa ndo wanakuja kusema "Mafisadi wanawaelemea...". Hivi hata si wawataje hao mafisadi? Kazi kuwarubuni wananchi na neno "Mafisadi", watajeni basi!

Tatizo la Tanzania kwa sasa si ufisadi... Matatizo sugu yanayopelekea kila aina ya uozo ni Siasa Safi na Uongozi Bora!

Tukifanikisha kubadilisha siasa zetu, katiba ikapitiwa upya na ikaridhiwa na watanzania, tukafanikiwa kuwarekebisha au kuwabadilisha kabisa viongozi tulio nao katika sekta mbalimbali basi tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana. Haya yakitekelezwa basi neno "ufisadi" litabakia historia.

Heri nimesema!
 
Back
Top Bottom