Sitta na Lowasa waitesa CCM

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,174
Gazeti la Tanzania Daima linatuhabarisha ya kuwa misuguano kati ya Waziri wa Afrika Mashariki Samweli Sitta na Mbunge wa Monduli Edward Lowassa inainyanyasa CCM na kuleta migawanyiko na mifarakano ndani ya chama hicho cha siasa kikongwe nchini...........

Kwingineko pia.................

Kwenye gazeti la Mtanzania tunataarifiwa ya kuwa yupo kada wa CCM ambaye amenuia kumfikisha Spika Mstaafu kwenye vikao vya juu vya chama kwa minajili ya kumfukuza uanachama kwa kile kiitwacho kauli ya Sitta ya kudai ilitumika nguvu kubwa ya fedha katika mizengwe ya kumzuia kuwa Spika...................................

Kada huyo anadai kauli hiyo ililenga kuleta migawanyiko na kukichafua chama hususani Kamati Kuu ambayo ndiyo iliyofanya maamuzi ya kutolirudisha jina lake...........................
Sitta, Lowassa waitesa CCM
• Vita vya urais, makundi yashamiri

na Bakari Kimwanga


amka2.gif
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kiko katika wakati mgumu wa kudhibiti makundi ya makada wake ambao wameanza vita vya kuwania madaraka na malumbano yanayotafsiriwa kukiweka njia panda chama hicho kikongwe, Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa.
Miongoni mwa makada wanaonekana kukipa wakati mgumu chama hicho ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye wiki hii aliibuka na kauli nzito iliyopingwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusufu Makamba.
Mwanasiasa mwingine anayeonekana kukiumiza kichwa chama hicho ni spika wa zamani wa Bunge na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye kauli zake za siku za hivi karibuni zimeibua maneno mengi ya chini chini na ya wazi.
Wakati Lowassa ameingia katika mzozo na Makamba kutokana na kauli yake ya kuvitaka vyama vya CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao zilizosababishwa na mzozo wa umeya katika mji wa Arusha, Sitta ameibua mjadala baada ya kudai kwamba alienguliwa katika mchuano wa uspika kutokana na hofu ya viongozi wa juu wa CCM walioshindwa kwenda sambamba na kasi na viwango vyake.
Makamba katika matamshi yake dhidi ya Lowassa, alipinga wazo la kukutana na CHADEMA kujadili mzozo huo akisema chama chake kilikuwa hakina sababu ya kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba kilikuwa kimeshinda kihalali kinyang'anyiro cha umeya wa Arusha.
Kama hiyo haitoshi, Makamba alieleza kushangazwa na kitendo cha Lowassa kutoa matamshi hayo hadharani wakati akiwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ambako ndiko alikokuwa akipaswa kuwasilisha hoja yake hiyo.
Lowassa kwa upande wake aliieleza Tanzania Daima kwa simu juzi kushangazwa kwake na matamshi ya Makamba dhidi yake akisema lilikuwa ni jambo lisiloingia akilini kwa kiongozi wa juu wa CCM kukataa kukaa meza moja na CHADEMA wakati akijua kwamba chama hicho kimekaa katika meza ya mazungumzo na Chama cha Wananchi (CUF) katika mzozo wa Zanzibar.
"Nimeshangazwa na Makamba kwa sababu anaona hakuna sababu ya kuzungumza na CHADEMA kuhusu mzozo wa umeya Arusha ambao katika kauli yangu niliwaonya wanasiasa kutojaribu kuugeuza mji huo kuwa Ivory Coast nyingine. Mbona katika mzozo wa Zanzibar tumekaa na CUF kwa nini iwe vigumu kuzungumza na CHADEMA?" alihoji Lowassa.
Kwa upande wake, Sitta anaingia katika mzozo na makada wenzake ndani ya CCM kutokana na kile ambacho baadhi yao wanakiona kuwa ni kinyongo dhidi ya wanachama wenzake ambao anaamini ndiyo waliokuwa na mkono katika kuenguliwa kwake katika nafasi ya uspika aliyoishikilia kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Inadaiwa kuwa kutokana na kinyongo hicho Sitta, anawatuhumu makada hao kuhusika na kashfa mbalimbali za ufisadi ikiwemo ile ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambayo mkataba wake wa kulipwa kiasi cha sh milioni 152 kwa siku ulirithiwa na Dowans Tanzania Ltd.
Sitta, hivi karibuni, aliitaka serikali isilipe kiasi cha sh bilini 185, ilizoamuliwa iilipe kampuni ya Dowans baada ya kuvunja mkataba wa kununua umeme na kampuni hiyo.
Kutokana na hatua ya Sitta, kutoa kauli za utata, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja, ameweka wazi nia yake ya kupeleka hoja za kumshitaki kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).
Mgeja anamtuhumu Sitta, kwa kuendeleza mgawanyiko ndani ya CCM huku akimtaka kufuta kauli yake kuwa aliondolewa kugombea uspika kwa mizengwe na Kamati Kuu ya chama hicho tawala.
Mapema wiki hii, Mgeja, alimjia juu Sitta, akimtuhumu kwa kuendeleza mgawanyiko ndani ya CCM huku akimtaka kufuta kauli yake kuwa kuondolewa kugombea uspika aliondolewa kwa mizengwe na Kamati Kuu ya chama hicho tawala.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa njia ya simu Khamis Mgeja, alisema kuwa yeye kama kada mwaminifu wa CCM, anajua nachokifanya Sitta, kwani hivi sasa ameanza mipango yake ya urais kupitia Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM).
Akizungumzia kwa undani mipango hiyo ya Sitta, na kundi lake alisema hivi sasa wameamua kuanza maandalizi hasa kwa kumuandaa mmoja wa vigogo katika serikali ili agombe urais Mwaka 2015, kwa kupitia nguvu ya vijana.
"Mimi ni kada mwaminifu kwa chama changu na msimamo wangu wa kuwasilisha hoja utabaki palepale ni lazimka Sitta, aeleze ukweli ndani ya vikao, na ninajua hivi sasa yeye na kundi lake wameanza maandalizi ya kumuandaa mmoja kati ya kigogo ili awanie nafasi ya urais mwaka 2015," alisema Mgeja.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili jana, Sitta, alisema alikuwa akimtakia baraka Mgeja katika hoja yake hiyo ambayo amesema ina mikono ya watu wengine nyuma yake.
"Sina cha kusema katika hilo, ila namshangaa Mgeja acha aendelee na mipango yake ambayo ninajua nyuma yake kuna kina nani, ila ipo siku nitasema kama anahitaji niseme," alisema Sitta.
Ukiacha kauli hiyo ya Sitta, nyingine ambayo imeibua mjadala ni ile inayohusu Dowans ambayo aliitoa siku chache baada ya kutolewa kwa hukumu na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kimataifa (ICC) ambayo iliipa ushindi kampuni hiyo dhidi ya TANESCO iliyotakiwa kuilipa faini ya shilingi bilioni 185.
Katika hilo Sitta, alisema hukumu ya Dowans dhidi ya TANESCO ni mbinu zagenge la mafisadi watatu (ambao hakuwataja kwa majina) wanaohujumu nchi kuandaa mpango wa kutafuta fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Waziri Sitta, alisema ataendelea kupambana na ufisadi hata kama kuna mbinu chafu zinafanywa dhidi yake na mafisadi ambao anaamini hawatafanikiwa kwa sababu hawaungwi mkono na watu wengi.
Alisema genge hilo ambalo halina huruma na nchi na umaskini wa Watanzania na kama likiachwa lijiimarishe, Watanzania wasubiri matatizo makubwa zaidi huko mbele.
Sitta ambaye katika bunge la tisa alikuwa Spika aliyeruhusu mjadala mkali kuhusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond iliyosababisha Lowassa, kulazimika kujiuzulu uwaziri mkuu na kisha akafuatiwa na mawaziri wengine wawili, alisema kinachofanyika sasa ni genge hilo kujiandalia mazingira ya kujikusanyia mabilioni ya fedha chafu za uchaguzi wa 2015.
Sitta alionya na kuwataka Watanzania kutofanya mchezo kwa kuwa macho na genge hilo ambalo alisema limekuwa na mazoea mabaya hali iliyopelekea taifa kuwa katika wakati mgumu hasa katika ulipaji wa fidia wa Dowans.
Alisema kwa kutumia nafasi yake kama waziri atajitahidi hasa kwa kushauriana na mamlaka za serikali ili kuzua hali hiyo yoyote yenye dalili ovu kwa taifa.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Sitta ilipingwa kwa nyakati tofauti na Mwanasheria Mkuu wa kwanza, Jaji Mark Bomani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambao walisema itakuwa ni jambo gumu kutoilipa Dowans hasa iwapo hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji itasajiliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wachambuzi wa mambo ndani na nje ya CCM wanaielezea mizozo hiyo inayowahusisha Lowassa na Sitta katika maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na mtikisiko unaoukumba Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), kuwa ni dalili za mwanzo za vita ya urais wa mwaka 2015.
Baadhi ya makada waliopo ndani ya chama hicho, wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili, kuwa hivi sasa kuna vita kubwa ya uongozi ndani ya CCM, ambapo vigogo wa chama hicho wamekuwa wakihaha kuunda mitandao itakayowasaidia kutimiza malengo yao Walidokeza kuwa hata UVCCM kuna hali tete licha ya Katibu Mkuu wake Martin Shigela kupinga jambo hilo kwa madai kuwa linachochewa na watu fulani kwa malengo binafsi Chanzo hicho kilidokeza kuwa UVCCM, hivi sasa kimemeguka ambapo yapo makundi yanayolenga kuwaandalia mazingira mazuri baadhi ya makada ili wawanie rais mwaka 2015 au ujumbe wa vikao vya juu vya chama utakaofanyika mwaka 2012.
 
Eti kuna cha chama kuchafuliwa, ni chama gani hicho cha kuchafuliwa huko???

Ama kweli akina Mgeja wa CCM inaelekea wako wengi mno lakini kibaya zaidi ni kwamba sasa ni dhahiri kwetu kwamba ambavyo mwenyekiti wao hajui ni kwa nini Wa-Tanzania bado tu masikini, na hawa jama pia nawao wana hawajui hisia zetu zinatutuma nini hata ikawafanya kuendelea kutunyea kwenye sahani hivi.


Ama kweli sasa nimeafiki ya kwamba hawa MAFISADI wa CCM wao hawaishi pamoja na sisi katika taifa hili iliojaa dhuluma, udini, upendeleo na kila aina ya uchafu na usanii.

Kwa masikitiko makubwa tunaendelea kushuhudia jinsi ambavyo akina Mgeja hawa kweli wanavyoishi katika syari nyingine kabisa kama katika nchi ya KUSADIKIKA kiasi kwamba yeyote anayediriki kutoa kauli yenye lengo la kuumuonea huruma Mtanzania masikini basi moja kwa moja huyo ni wa kusulubiwa haraka sana.

Lakini si neno, endeleeni kwa kasi zaidi hiyo hiyo na kwa jeuri ya akina Makamba bila kusahau kwamba taifa zima hivi sasa tumewakodoleeni macho ile mbaya!!!!!!
 
Inavyoonekana tayari kampeni za 2015 ndiyo zimeashaanza rasimi.
Nashindwa kuelewa hasa ni lini Tanzania tutapata maendeleo tunayohitaji! manake Tanzania ni nchi moja ambayo watu wanakampeni nonstop!
 
Katika CCM hakuna wakumgusa Lowassa maana yeye ni kitu kimoja na Kikwete labda mpaka kina Kingunge,Chenge, Rostam na kina Anna watakapoondoka kamati kuu ya ccm
 
hivi iko kizazi kitakufa lini watuhachie nchi yetu.ingetokea wakafa pamoja wote,tuanze upya tumewachoka
 
Vita kati ya Sita na Lowasa ni vya kudumu maana wote wanawania kumridhi JK. Karata ya Lowasa katika vita hivyo ni kwamba anao wafuasi wengi katika vikao vya juu vya chama na amekuwa akijaribu kutumia karata hiyo kuhengua Sita kwenye chama. Uenda angelikwisha fanikiwa isingelikuwa kuwekewa kifua na JK. Kwa upande wake Sita amekuwa akitumia karata ya kuhusika kwa Lowasa na ufisadi kumpunguzia umaarufu. hivi sasa uenda vita kubwa ikaamia katika kujaribu kuhengua watu wanao muunga mkono Lowasa katika uchaguzi mkuu wa chama ujao.
 
Wacha wakaangane wenyewe kwa wenyewe wakijichokea CDM tunachukua madaraka come next uchaguzi
 
kuna kitu Lowassa kakizungumza ambacho kitaibua mapya. Alimuuliza mwalimu (mfukuzwa) Makamba, kwa nini CCM ilikubali kuketi meza moja na CUF ikatae kukaa meza Moja na Chadema? Swali hilo ni muhimu sana, ila nikaelewa tu kuwa wanawakataa CHM kukaa meza moja sababu CDM sio wengi maustaadh
 
kuna kitu lowassa kakizungumza ambacho kitaibua mapya. Alimuuliza mwalimu (mfukuzwa) makamba, kwa nini ccm ilikubali kuketi meza moja na cuf ikatae kukaa meza moja na chadema? Swali hilo ni muhimu sana, ila nikaelewa tu kuwa wanawakataa chm kukaa meza moja sababu cdm sio wengi maustaadh

i think you have a point! Kwa sababu muafaka wa zanzibar ulivyofikiwa ni kisanii mno kwa watu wanaofuatilia siasa za zanzibar! Isitoshe hakuna detail za mazungumzo ya karume na hamad isipokuwa ilisemwa tu wamekubaliana kwenye msiba [or something like that!]
 
Ukitafakari hizi kauli utajua ya kuwa......kweli mambo siyo shwari ndani ya Chama Cha Mafisadi..................
Wakati Lowassa ameingia katika mzozo na Makamba kutokana na kauli yake ya kuvitaka vyama vya CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao zilizosababishwa na mzozo wa umeya katika mji wa Arusha, Sitta ameibua mjadala baada ya kudai kwamba alienguliwa katika mchuano wa uspika kutokana na hofu ya viongozi wa juu wa CCM walioshindwa kwenda sambamba na kasi na viwango vyake.
Makamba katika matamshi yake dhidi ya Lowassa, alipinga wazo la kukutana na CHADEMA kujadili mzozo huo akisema chama chake kilikuwa hakina sababu ya kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba kilikuwa kimeshinda kihalali kinyang'anyiro cha umeya wa Arusha.
Kama hiyo haitoshi, Makamba alieleza kushangazwa na kitendo cha Lowassa kutoa matamshi hayo hadharani wakati akiwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ambako ndiko alikokuwa akipaswa kuwasilisha hoja yake hiyo.


Lowassa kwa upande wake aliieleza Tanzania Daima kwa simu juzi kushangazwa kwake na matamshi ya Makamba dhidi yake akisema lilikuwa ni jambo lisiloingia akilini kwa kiongozi wa juu wa CCM kukataa kukaa meza moja na CHADEMA wakati akijua kwamba chama hicho kimekaa katika meza ya mazungumzo na Chama cha Wananchi (CUF) katika mzozo wa Zanzibar.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Sitta ilipingwa kwa nyakati tofauti na Mwanasheria Mkuu wa kwanza, Jaji Mark Bomani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambao walisema itakuwa ni jambo gumu kutoilipa Dowans hasa iwapo hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji itasajiliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Waswahili husema......................panapofuka moshi panaficha moto...................................
 
Back
Top Bottom