Sione ukadhani, umetumwa?

Sione ukadhani, umetumwa?

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2012
Posts
1,985
Reaction score
1,286
Sione nimenyamaza, mwenzio sina furaha,
Mambo ulo yatangaza, mie yanipa karaha,
Allah aniongoza, ulidhani nitahaha,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.

Sione nimetulia, moyoni nahangaika,
Mwenzio nafikiria, namna ya kuongoka,
Ubaya wanifanyia, inshallah tastirika,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.

Sione natabasamu, moyoni naungulika,
Nikiwaza sina hamu, mambo yalivyo pinduka,
Mie nimepigwa bomu, najuta kumchunuka,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.

Sione nimeduwaa, ujue ninayajenga,
Hata niipate taa, lipendeze langu anga,
Wajashikwa na butwaa, zipotee zako ngenga,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.

Sione sijakujibu, sidhani sijalipata,
Umetumwa si ajabu, fikisha umenikuta,
Sema halinipi tabu, si joto likafukuta,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.

Sione abwata juu, yupo alo mfundisha,
Yuko na yake miguu, na ngazi ya kuegesha,
Kobe yu mtini juu, yupo alo mpandisha,
Waja ndio walewale, hakika hayana budi.

Dotto Rangimoto Chamchua.(Njano5
mzalendo.njano5@gmail.com
0762845394/0784845394
Morogoro Tanzania.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom