Hekaya za abunuasi ..
Part three.3
SIKU moja alfajiri, wakati wananchi wa mji wenye
wakazi wengi walipokwenda kuchota maji mtoni,
walishangazwa kuuona mkono wa mtu ukiwa katikati ya
mto. Mkono huo wa ajabu ulikuwa umenyoosha vidole
viwili juu, kuonyesha alama ya mbili.
Wananchi walistushwa sana na kitendo hicho, wakaogopa
hata kuchota maji mtoni, kwani hawakuwahi kuona tukio
la kuogopesha kama lile. Wengine waliamini kuwa huo
ulikuwa mwili wa mtu aliyetupwa mtoni.
Lakini ishara iliyoonyeshwa na mkono huo iliwafanya
wananchi waamini kuwa huo ulikuwa mkono wa ajabu.
Katika kiza kinene kilichozunguka ndani ya vichwa vya
wananchi, habari zikamfikia Mfalme wao, naye akafika
haraka eneo la tukio.
Mfalme wa nchi hiyo baada ya kujiridhisha kuwa ulikuwa
mkono wa ajabu na uliwekwa na watu wenye imani za
kishirikiana, alitoa siku tatu mkono huo uwe
umeondolewe, vinginevyo ataleta wataalam kutoka
sehemu mbali mbali duniani kwa ajili ya kubaini wahusika.
Siku tatu zilizowekwa na Mfalme zikaisha, wataalam wa
mambo ya asili kutoka sehemu mbali mbali duniani
wakaanza kuwasili mtoni hapo kwa lengo la kuundoa
mkono huo wakashindwa.
Mfalme akatoa ofa nono, waganga wenye sifa na jeuri ya
mambo ya jadi wakamiminika eneo la mto, wakafanya
mitambiko na mambo yao kwa ufanisi zaidi, wengine
wakalala mtoni kuonyesha umahili wao lakini wakashindwa
na kuuondoa mkono huo wa ajabu...
Mfalme na wasaidizi wake wakakuna vichwa, wananchi
hawana jinsi ya kupata maji. Maji mtoni hayachoteki,
wananchi wanaogopa kutumia maji hayo. Ndipo Abunuwasi
akajitokeza mbele ya Mfalme. Akamwambia Mfamle,
"Mimi naweza kujaribu.
Mfalme akamfukuza Abunuwasi kwa hasira, akamwambia.
"Mpumbavu sana wewe, hapa wameshindwa waganga na
waganguzi, wewe Abunuwasi utaweza wapi, usitupotezee
muda wetu".
Abunuwasi akaondoka, waganga wakazidi kumiminika
mtoni wakitoka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na
sifa zao. Kila walichofanya kuuondoa mkono huo
wakachemka na kuondoka eneo hilo kimya kimya.
Abunuwasi akamrudi Mfalme, akamwambia, "Wacha
nijaribu mimi". Mfalme akamjia juu akamwambia.
"Nimesema huwezi Abunuwasi, wameshindwa waganga wa
dunia, utaweza wapi wewe?, Abunuwasi akasisitiza.
"Wacha nijaribu mimi kama walivyojaribu wengine na
kushindwa.
Mfalme kwa hasira akamwambia Abunuwasi, "Haya
jaribu, maana unataka kutupotezea muda tu hapa, lakini
ole wako ukishindwa, nitawaamru askari wakutie ndani".
Abunuwasi akaanza kuuzunguka mto huku umati wa
wananchi ukimwangalia kwa makini, alipita huku na huku
akikimbia kama mtu aliyepatwa na wazimu, Mfalme
akaanza kuchukia, hatmaye Abunuwasi akakaa sambamba
na mkono ule, Abunuwasi akachuchumaa chini na kuinua
mkono wake juu mfano wa mkono ule.
Mfalme na wananchi walikuwa kimya wakifuatilia kwa
makini tukio hilo, Abunuwasi aliuchezesha mkono wake
kushoto na kulia, mkono ule ndani ya maji nao ukafanya
vile, kama alivyofanya Abunuwasi. Wananchi
wakashangazwa mno na kitendo kile.
Abunuwasi akauvuta mkono wake nyuma, mkono huo pia
ukafanya hivyo, Abunuwasi akakunja kidole chake kimoja,
mkono ndani ya maji nao ukafanya vile. Hatmaye
Abunuwasi akaushusha mkono wake chini kama
anaudhamisha, mkono ule nao ukadhama na haukuonekana
tena.
Mayowe, vigelegele na shangwa vikasikika, Mfalme
akasimama akamfuata Abunuwasi, akamuomba radhi,
akamtukuza na kuonyesha kufurahishwa. "Ahsante sana
Abunuwasi, umetuondolea aibu, nisamehe kwa
kukudharau, sikutegemea kabisa".
Wananchi wakaja juu wanamtaka Abunuwasi apewe
Ufalme. Maana ameweza kufanya jambo lililowashinda
waganga na waganguzi. Mfalme akahamaki. Abunuwasi
akaula...