Simulizi ya kusisimua ya Prof. Mark Mwandosya: Salaam kutoka Comoro

Hivi punde

JF-Expert Member
Apr 1, 2017
2,554
8,552
Nimeona niandike waraka huu kutoka ughaibuni, ingawa si ugenini sana, nikiwa Jamhuri ya Comoro. Nimebahatika kusafiri sana kikazi duniani kote, kuanzia Japan mpaka Brazil, kuanzia Guyana mpaka Australia. Nimeiwakilisha nchi kikazi katika mabara yote isipokuwa Aktiki na Antaktika. Namshukuru Rabuka kwa kuniwezesha kulitumikia Taifa langu kwa zaidi ya miaka arobaini. Nimetembelea nchi zote jirani isipokuwa Jamhuri ya Comoro.

Mara nyingi tumezoea kusema Tanzania inapakana na nchi nane; Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Watu ya Congo, Zambia, Malawi, na Msumbiji. Tunasahau kwamba watu wa Visiwa vya Comoro ni jirani zetu. Badala ya mpaka wa ardhi tunatenganishwa na Bahari ya Hindi. Inawezekana hii ikawa ndio sababu ya nchi zetu kutokuwa na ushirikiano wa karibu kiuchumi na kiutawala, pamoja na kwamba kijamii na kiutamaduni sisi, na hasa watu wa mwambao wa pwani na Zanzibar, Wacomoro wamekuwa ni sehemu yetu. Mara nyingi utasikia fulani na fulani wametutangulia mbele za haki na wamezikwa katika makaburi ya waComoro.

Nakiri kwamba pamoja na kusafiri sana nje ya nchi, sikuwahi kubahatika kufika nchi ya jirani ya Comoro. Hivyo basi nikiwa mstaafu, na ilhali Mwenyezi Mungu amenijalia siha njema, moja ya nchi ambazo nimeamua kutembelea ni nchi jirani, Comoro.

Nikiongozana na mke wangu Lucy, kijana wetu Emmanuel, tuliondoka Dar es Salaam kuelekea Moroni, mji mkuu wa Comoro, jumanne kwa njia ya anga kupitia ndege aina ya Bombadier, De Havilland Dash 200, Q400, ndege ya Shirika la ATC ambayo iliondoka kama ilivyopangwa, asubuhi saa 2 barabara. Muda mfupi baada ya ndege kufika usawa wa anga uliopangwa kwa safari hii, wahudumu wakatupatia, soda, kahawa au chai kwa jinsi kila msafiri alivyohitaji, vinywaji hivi vikiambatana na karanga na korosho. Hakika ndege ilijaa. Wasafiri wengi walikuwa ni wafanyabiashara wa Comoro wakitoka Dar es Salaam wakiwa na bidhaa mbali mbali. Hicho ni kielelezo cha jinsi ATC ilivyohodhi soko. Na kama itashindwa kuhudumia soko hili basi itakuwa ni kutokana na makosa yake na si vinginevyo.

Kufumba na kufumbua, tukatangaziwa tufunge mikanda na kuweka viti vizuri kwani tulikuwa kukaribia uwanja wa ndege wa Hahaya, Comoro. Kuangalia muda, tulitua baada ya safari ya saa moja na nusu hivi. Maana yake ni kwamba iwapo tungetumia ndege aina ya jet basi safari ingetuchukua saa moja tu, muda wa safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi, au kwenda Mbeya. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba bado tuna kile waingereza wanaita “goodwill”. Kwani baada ya kumtaarifu, Mheshimiwa Balozi Sylvester Mabumba mwenyewe alikuja kutupokea na kutukaribisha Comoro.

[https://4]Jengo la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Prince Said Ibrahim, Hahaya, Moroni (Picha:Emmanuel Mwandosya).
Jengo la abiria kiwanja cha Prince Said Ibrahim, Hahaya ni dogo lakini ni zuri na la kisasa. Ingekuwa ni miaka 17 iliyopita ningewashauri Wakala wa Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA waangalie usanifu wake. Chumba cha watu mashuhuri ni kidogo. Mheshimiwa Balozi katika unyenyekevu wake isiyo na mfano anasikitika kutukaribisha katika chumba cha wageni ambacho ni finyu. Kwani kuna kingine kikubwa zaidi cha wageni maarufu zaidi. Namkumbuka Mwalimu, Baba wa Taifa alipojengewa nyumba kubwa kiasi pale Butiama akasema “ mnanijengea nyumba kubwa namna hii, kwani mimi tembo”. Huwa nawambia wenzangu na wananchi kwamba kama huna uhakika na jinsi ya kukabiliana na hali fulani kumbuka Mwalimu kwa hekima zake angesema nini? Suala jingine lajitokeza. “Vipi pasi zenu za kusafiria ni za raia wa kawaida?” Baada ya kumaliza vipindi vitatu mfululizo vya ubunge, hakika hatustahili pasi za kidiplomasia. Hivyo basi tulizirudisha mara moja na kupatiwa pasi za kusafiria za kawaida. Wenyeji wetu wanatushangaa. Kwani wanapokea viongozi wengi waliostaafu, ikiwa ni pamoja na wabunge na mawaziri, wakiendelea kutumia pasi za kidiplomasia.

NGAZIDJA (NGAZIJA au GRANDE COMORE)

Kiwanja cha ndege cha Prince Said Ibrahim kiko wilaya ya Hahaya ya mji wa Moroni. Kutoka Hahaya mpaka Moroni barabara ni finyu na majumba yako sehemu zote za barabara, yakikaribiana kabisa na barabara. Wangefuata sheria zetu zilizotungwa wakati wa ukoloni, nyumba zote hizi zingewekwa alama nyekundu na wakaazi kuamriwa kuzibomoa au serikali izibomoe na wao walipe gharama za kazi hiyo! Mji wa Moroni, kama ulivyo Stone Town, Zanzibar, usingekuwepo. Inanikumbusha yule kijana aliyetoa pendekezo kwa Tume ya Warioba ya mapendekezo ya Katiba Mpya kwamba Katiba itamke wazi kwamba Waziri mwenye dhamana ya ujenzi anyang’anywe rangi na “brush” ili asiweke alama ya X kwenye nyumba nchi nzima!

Kama ilivyo ada Mtanzania anapofika ugenini mahala pa kwanza kupitia ni Ubalozi wa Tanzania. Kuufikia Ubalozi inabidi kupita katika njia finyu na kupiga honi ili usigongane na gari linalokuja kwenye kona. Ndipo anapojitokeza mkaazi mmoja na kusema kwa hasira “Hanu Hatu”. Tunauliza maana yake nini, mwenyeji wetu anatwambia anasema “Hapa ni nyumbani kwangu” kwa hiyo tusimpigie honi.

[https://4]Ofisini kwa Mheshimiwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

Ukarimu wa mtanzania hauishii ndani ya mipaka ya nchi. Kwani pale Ubalozi mjini Moroni unapokelewa kama vile uko nyumbani. Hakika uko nyumbani. Kufuatana na Mkataba wa Kimataifa wa Vienna, ubalozi ni sehemu ya Tanzania ndani ya Comoro. Tulipokuwa wanafunzi nje ya Tanzania kwa baadhi yetu ilikuwa nadra kutembelea ubalozi. Baadhi ya maafisa wa ubalozi, kwa jinsi walivyotupokea tulihisi walikuwa wakituona kama vile tunafika kuwabughudhi tu. Lakini baada ya kuwa watumishi wa umma, tukiwa nje ya nchi Ubalozi ilikuwa ni mahala pa kwanza kufika. Tuliuliza “kuna Watanzania wangapi wanaishi Comoro?” “Ah” tukajibiwa, “waliojiandikisha ni kama 250, lakini tunapokuwa na sherehe, au Maulid, hujitokeza Watanzania kati ya 20 elfu na 30 elfu kwa ajili ya pilau”. Kwa ufupi wako wengi tu.

[https://2]Kreta za Volkano ya Mlima Karthala, Ngazija (Picha: Emmanuel Mwandosya)

Kuufikia msikiti wa maajabu ulio Bangoi-Kouni, njia moja ni kutumia barabara ambayo unapanda kuelekea kaskazini mashariki kuzunguka Volkano ya Karthala. Kisiwa kizima cha Ngazidja au “Grand Comoro” au “Grande Comore” ni matokeo ya volkano iliyo hai ambayo kwa mara ya mwisho ililipuka mwaka 1985. Mwaka 2007 Volkano ilifumuka kwa kutoa moshi na majivu yaliyosambaa kisiwa chote. Sio lazima uwe mtaalam wa jiolojia kutambua kuwa vkisiwa cha Ngazija kinatokana na Volkano ya Milima ya Karthala. Kwani mbali na mashimo mengi ya volkano, zinaonekana, hasa kutoka angani, njia dhahiri ambamo, lava, jivu nene la moto linalotokana na volkano, lilipita.

[https://4]Msikiti wa Shiounda, Bangoi-Kouni, Ngazija. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

Maajabu ya Msikiti wa Shiounda yanatokana na maelezo ya Wazee wa Bangoi Kouni ambao nao wamerithishwa maelezo hayo kutoka vizazi na vizazi vilivyopita, tangu zamani za kale. Kufuatana na maelezo ya Mzee Mhoma Mbae na Mzee Ahamada Mohamadi Salim, mwanzoni hapakuwa na msikiti eneo hilo. Siku moja wananchi wa eneo hilo walilala na walipoamka alfajiri wakashangaa kukuta msikiti umesimama.

Imani iliyojengeka ni kwamba msikiti huo ulishushwa na Malaika kutoka Mbinguni. Waumini huenda hapo kuombewa dua na watalii hufika hapo kuushuhudia msikiti huo. Kwa mujibu Wazee hao, heshima kubwa na tahadhari inabidi ioneshwe na wote wanaofika msikitini hapo. Mzee Mhoma, katika simulizi zake, anasema mtu mmoja alijaribu kuondoa jiwe la ukuta wa msikiti, akajikuta akitupwa baharini na kupotea moja kwa moja. Aidha iwapo kwa kisa chochote kile ukafanya kitendo cha kuchukiza katika mazingira ya msikiti utapigwa vibao bila kutambua anayekuadhibu.

[https://3]Ndani ya Msikiti wa Shiounda, Bangoi-Kouni, Ngazija. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

Huwezi ukakamilisha ziara ya kaskazini mwa kisiwa cha Ngazidja bila kuona ziwa dogo lililotokana na mlipuko wa volkano, Ziwa la Bangoi-Kouni. Wenyeji huelezea chimbuko la ziwa hilo kama ifuatavyo: Zama za kale alipita bwana mmoja eneo hilo ambalo lilikuwa makazi ya watu. Akaomba maji ya kunywa. Kila mkaazi aliyemuomba akamyima kwa kusema hakuwa na maji ingawa walikuwa na maji. Alipofika kwa bibi kizee mmoja na kumuomba maji, yule bibi kizee akampa. Baada ya kunywa yule mgeni akamwambia yule bibi mzee kwamba yeye na ndugu zake waondoke mahali hapo. Yule bibi akamjibu hana ndugu. Akaambiwa aondoke mwenyewe. Alipoondoka, baada ya saa moja hivi eneo lote likafurika na maji na ziwa likatokea. Wakaazi wote waliomnyima maji yule mgeni wakazama, makaazi yao na mali zao. Wenyezi wanaamini maji ya ziwa hilo ni dawa.

[https://4]Ziwa la Volkano, Bangoi-Kouni, Ngazija. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

Simulizi hii inafanana sana na ile tunayoifahamu kama chanzo cha ziwa la aina hiyo linalojulikana kama Kyungululu, lililo Kata ya Itete, kilomita 3 hivi kutoka kijijini kwetu Lufilyo, Busokelo, Mbeya. Hapo Kyungululu kulikuwa na mkaazi aliyekuwa akiishi hapo. Baadaye kukatokea na mgeni mpita njia aliyekuwa na kiu. Akaomba maji ya kumywa na yule mwenyeji akamwambia hakuna maji. Inaelekea alimyima mgeni maji ingawa alikuwa nayo. Baadaye alipoondoka yule mgeni pale alipokuwa mkaazi, gharika ikatokea, mkaazi akazama, na ziwa likatokea. Simulizi hii ya Kyungululu, Tanzania, na ile ya Bangoi-Kouni zinafanana. Inashangaza.

Unaweza kurudi Moroni kupitia Amahame, au kwa barabara iliyotufikisha Bangoi-Kouni, ama kuchukua njia ya pwani ya magharibi ya kisiwa kupitia Mitsamouli, Fasi, Ndzaouze, Djomani, Nsaoueni, Domwajuu, na viunga vya Moroni vya Hahaya, Panambwani, Voijuu, Hantsanbou, Badamaji, na Isandra.

Moroni ni mji ulio pwani ya magharibi ya kisiwa cha Ngazidja. Ni mji wa kiutawala zaidi na huduma ikiwa ni pamoja na bandari. Sehemu nyingi zinafanana na mji wa Zanzibar, ikiwa ni pamoja na eneo la Medina, ambalo linafanana kiasi na Mji Mkongwe Zanzibar.

[https://2]Mtaa wa Medina, Badjanani, Moroni, Ngazija (Picha: Emmanuel Mwandosya)
Utamaduni wa vazi la kimwambao ni ule ule. Tofauti kubwa ni wingi wa misikiti iliyopo Moroni. Karibu kila baada ya nyumba tano au kumi kuna msikiti, ikiwa ni pamoja na msikiti mkubwa wa kihistoria wa Badjanani ulio mji mkongwe wa Medina, na ambao ulijengwa mwaka 1427. Kutokana na volkano na mawe, mji wa Moroni na viunga vyake hauna mwalo mkubwa wenye mchanga mchanga.

[https://2]Msikiti Mkuu wa Badjanani, Moroni. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

Comoro, kama nchi, ni muungano wa visiwa vya Ngazidja, Nzuani, Mwali, na Maoré, au kama alivyotufahamisha mfanyakazi wa Hoteli ya Florida mjini Mutsamudu, mji mkuu wa Nzuani majina ya kibeberu ni Grande Comore, Anjouan, Mayotte, na Moheli, sawia. Maelezo mafupi yanatosha kuuelezea Muungano au Umoja huu wa Visiwa vya Comoro.

Bendera ya Visiwa vya Comoro ina mistari yenye rangi nne. Rangi nyeupe ni kielelezo cha Maore, rangi ya manjano inawakilisha Mwali, rangi ya bluu ni Ngazidja na rangi nyekundu ni kielelezo cha Nzuwani. Bendera pia ina mwezi mpevu wenye nyota 4 zikiwa ni kielelezo cha dini ya kiislam na umoja wa visiwa, au masiwa kingazidja.

Wananchi wa Comoro ni mchanganyiko wa watu wenye asili nyingi. Wapo wenye asili ya kibantu, kishirazi (Iran), kiarabu (hususan Yemen na Oman), Zanzibar, na Madagascar. Kila kisiwa kina lugha yake lakini zinafanana, zikihitalafiana kwa lafidhi. Lugha hizo hutumika katika mawasiliano sambamba na kifaransa, kiswahili na kiarabu. Mbali na kusheheni kibantu, istlahi ya lugha hizo ina maneno lukuki ya kiswahili. Kwa mfano tu maneno; mkoba, jirani, mume au mme, upepo, pumzi, dirisha, bahari yana maana ileile kingazija na kizuani. Wao husema mushe wangu wakimaanisha mke wangu; mwana mtiti maana yake mtoto mdogo; mlongo hutumika vilevile kwa maana ya mlango; shibaka kumaanisha dirisha pia; djambo djema kingazija ni jambo jema kiswahili; na mwenzani wangu hutumika pia kumaanisha rafiki yangu.

Nimevutiwa sana na Methali za Mwali na ambazo zinafanana sana na zile za kiswahili, kama zilivyo katika kitabu kiitwacho Mahadisi ya Shihale ambacho kimechapishwa naKomEdit wa Moroni. Watu wa Mwali husema: Ulimi kauna shiba; Mali kaina hisabu uhibu bila habari; Kapvuma djahazi ya maha mia; Taabu ya baharini, mlozi de aidjuao; Subira udja na hairi; Dalili ya mvua: maingu; Baharia kana hasara; Msafiri kafiri; Mwidzi, suku arba arbaini; Kula suku tdi djumwa; Madjitso, mdjuhu; Haraka haraka kaina baraka; na Mtsaha sha vuvuni, unyama. Kuna mfanya biashara mmoja kutoka Tanzania ambaye katika majadiliano aliteteza ulimi na kuwasema vibaya wafanyabiashara wa kiComoro ambao walikuwa wakitumia kifaransa bila kujua kwamba wanasikia kiswahili.

Hivyo basi wageni wanaozungumza kiswahili wanashauriwa kuzingatia kwamba waComoro wengi huzungumza kiswahili na wale ambao hawazungumzi kiswahili wanaweza kusikia mazungumzo ya kiswahili kutokana na maneno mengi yanayofanana na lugha zao.

[https://2]

Magofu ya Kaviri Djohe, Ikoni, Moroni. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

[https://3]

Mwanamke wa kingazija katika vazi la kitamaduni akiwa amepaka Msindani (Liwa), aina ya urembo unaofanya ngovi kuwa nyororo nay a kuvutia. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

NZUWANI (NZUANI au ANDJOUAN)

Safari ya kwenda kisiwa cha Nzuani (au Nzuwani) ni kwa njia ya meli au ndege. Ukiamua kusafiri kwa meli mahali pa kuanzia ni kwa wakala wa meli inayoondoka Moroni siku hiyo. Baada ya kukata tiketi, kituo cha pili ni ofisi za forodha na uhamiaji. Hapo hati za kusafiri hukaguliwa na inabidi kueleza sababu za kwenda Nzuwani. Tulifikiri kwa kuwa tumepata visa ya mwezi mmoja ya kuwepo nchini, hiyo tu ingetosha. Lakini sivyo.

Mwenyeji wetu alichukua muda mrefu kuwapa maelezo, lakini hawakuridhika. Ilibidi ampigie simu Mheshimiwa Balozi kumwomba aingilie kati. Baada ya Balozi kuzungumza na wahusika ruhusa ya kusafiri ikapatikana. Baadaye tukafahamishwa kwamba maofisa wa usalama wa Comoro walihofu kuwa tulitaka kwenda kisiwa cha Nzuani ili tupate urahisi wa kwenda kisiwa cha Maore, ambacho kwa sasa ni sehemu ya Ufaransa, na hatimaye kuzamia Ufaransa kama wakimbizi. Kwa taarifa tu, mke wangu na mimi kwa umri tumezidi miaka 65 kila mmoja. Hatujui hili suala la kuwa wakimbizi watarajiwa ili kuzamia Ufaransa lilitoka wapi. Hakika kuishi kwingi, kuona mengi na kusikia mengi, walisema wahenga.

Ilipangwa meli iondoke bandari ya Moroni kuelekea Mutsamudu saa 4 asubuhi lakini tukaondoka saa 6. Kwamba tulichelewa kuondoka kwa saa mbili haikutupa shida. Kwani muda huku kwetu Afrika una mnyambuliko wa aina fulani. Tulipomueleza rafiki yetu Mcomoro kuhusu suala hili akatukumbusha kirefu cha Kampuni yetu ya ndege ATC kuwa maana yake ni Any Time Changed au Any Time Cancelled, au Safari inaweza kuahirishwa au kufutwa wakati wowote! Nami nikakumbuka tulivyolibatiza jina Shirika la ndege ka Italia, ALITALIA, kuwa Arrive Late in Tokyo and Luggage (left) in Amsterdam, maana yake unachelewa kufika Tokyo na unakuta mzigo wako uliachwa Amsterdam.

[https://4](Picha: Emmanual Mwandosya)

[https://3]

Meli ya Abiria El Jaanfari ikiwa bandarini Moroni. (Picha:Emmanuel Mwandosya)

Tulipanda Meli EL DJAANFARI yenye usajili wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Meli Duniani (International Maritime Organisation-IMO) IMO:8843903, yenye uwezo wa kubeba abiria mia tatu hivi. Tumesafiri mara nyingi majini hivyo tulitegemea maelezo ya usalama yangepewa kipaumbele. Ilibidi, wa taratibu za usalama pia tupate maboya ya kutuokoa wakati wa dharura. Haikuwa hivyo. Hakika Mamlaka ya Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) hapa kwetu isingewaruhusu kutoa huduma bila kuzingatia usalama wa abiria. Tulichojifunza pia katika safari hiyo ni kwamba hakuna aliye mzoefu katika safari ya majini.

Safari ya Moroni mpaka Mutsamudu kwa meli hiyo huchukua saa 5. Saa mbili za kwanza bahari ilikuwa shwari. Baada ya hapo, kwa muda wa saa mbili, bahari ilichafuka sana. Mawimbi makubwa yaliifanya meli iende chini na juu kwa kasi. Ndipo abiria wengi na wafanyakazi wa meli walipopata ugonjwa wa bahari (sea sickness). Ugonjwa huu haubagui kwa cheo, umri, umasikini, au utajiri. Karibu kila mtu alitapika tena kwa muda mrefu kufuataia kuwepo kwa mawimbi.

Kijana mmoja wa kinzuwani alitufurahisha. Ni mwanafunzi Nairobi na alikuwa anarudi nyumbani kwao ili kukwepa uwezekano wa kuzuka vurugu baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 8 Agosti, 2017. “Sijawahi kutapika nikiwa safarini majini”. Kwa kuwa yeye ni mwenyeji wa Nzuwani basi tukamuamini. Akalalamika kuwa ametoka Moroni bila kula chochote. Haukupita muda mrefu akaenda nje, akashililia reli na kuanza kutapika. Aliporudi tukamuuliza “vipi tena?”. Akajibu “Najisikia vibaya kutokana na marashi niliyopaka mwilini asubuhi”. Sijawahi kusafiri kutoka Unguja kwenda Pemba kwa meli. Naambiwa hali ya wasafiri kupata ugonjwa wa bahari hutokea na inakuwa mbaya meli inapopita sehemu za Nungwi. Tuliwasili Mutsamudu saa 11 jioni na kupokelewa na mwenyeji wetu Ibrahim, mfanyabiashara maarufu Nzuwani. Mutsamudu maana yake Musa Mweusi. Ndiye aliyekuwa mkaazi wa kwanza mahali hapo.

[https://2]

Kisiwa cha Nzuani na Mji wa Mutsamudu unavyoonekana kwa mbali kutoka melini. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

Wenyeji wetu walitushauri tusiishie Ngazija tu bali tufike Nzuani na Mwali. Tulidhamiria kufika Nzuani ili kukiona kisiwa ambacho mwaka 2008, askari wa jeshi letu, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kwa kusaidiana na Afrika ya Kusini liliongoza vikosi vya Umoja wa Afrika pale Rais Mohamed Bakari wa Nzuwani alipokataa kuachia ngazi baada ya kumaliza muhula wake na hivyo kuhatarisha amani ya Comoro. Bakari alisaidiwa na wafaransa kukimbia uhamishoni Ufaransa. Mapatano ya WaComoro ya Mwali ya mwaka 2001 ni kwamba kila Rais wa Kisiwa apewe muhula mmoja na kila kisiwa kitoe Rais wa Muungano kwa mzunguko wa miaka mitano.

Tukiongozwa na mwenyeji wetu Ibrahim Badrane tulizuru kisiwa cha Nzuwani kutoka Mutsamudu na kupitia maeneo yafuatayo: Chiconi; Bandrane; Mjamaoue; Sima; Vuani; Vassi; Maraharare, Marontroni; Bandrani ya Pomoni; na Moya; sehemu za mwambao. Kutoka Moya, ukipanda milimani unapitia maeneo ya Nyumakele; Hadda dueni; na kurudi pwani kupitia Domoni; Gege; Bambao mtanga; Chuo Kikuu cha Umoja wa Comoro, Patsy; Koki; Bazamini; Barakani; Nyantragua; Quani, na kurudi tena Mutsamudu.

Tulilobaini katika ziara hii ni jinsi kila jamii ya watu wa Anzwanu ilivyojitenga kutokana na asili yake. Kwa mfano: Eneo la ukanda wa juu, Nyoumakele na Hadda daueni, wakaazi wake ni asili ya kibantu; eneo la ukanda wa kati la Domoni wenyeji wake ni asili ya washirazi; Wahabeshi na wasomali huishi eneo linaitwa Gege; Bamba mtanga wenyeji wake ni asili ya wazambara(wasambaa?); wakaazi wa Moya asili yao ni Zanzibar, Yemen na Oman; na waishio katika maeneo mengine yaliyobaki ni mchanganyiko wa watu.

Kisiwa cha Nzuwani kinavutia sana. Mazingira yake ni mazuri na uoto wa asili ni mkubwa. Kisiwa kimesheni mazao ya karafuu au karafu kama wanavyoita wao, minazi, vanila, mirangi rangi au langi langi, miwa, na matunda. Haieleweki kwa nini utalii usiwe pato kubwa la kisiwa hiki kutokana na mandhari yake, milipa, pwani, bahari.

[https://2](Picha: Emmanuel Mwandosya)

[https://4](Picha: Emmanuel Mwandosya)

[https://2]Mandhari ya maeneo mbalimbali ya Kisiwa cha Nzuwani (Picha: Emmanuel Mwandosya)

Kurudi Moroni unaweza ukatumia usafiri wa anga. Ndege ndogo aina ya Cessna ya kampuni ya Inter-Air, yenye uwezo wa kuchukua abiria 13 hutumika. Kuhusu usafiri wa ndege kati ya Moroni na visiwa vya Nzuwani na Mwali, taarifa tuliyopata tukiwa huko ni kwamba kampuni ya ndege, ATCL, wamepata ruhusa ya kufanya biashara ya usafiri wa abiria katika visiwa vya Comoro. Mashirika mengi duniani hutafuta nafasi ya namna hiyo ya nchi kuweka kando kizuizi kinachotokana na kile kinachoitwa mhimili wa tano. Ni matumaini yetu kwamba ATCL wataitumia fursa hii mapema. Vinginevyo nchi nyingine, hasa Kenya, wakipata nafasi hii wataitumia vilivyo.

[https://1]

Kiwanja cha Ndege cha Douni, Mutsamudu, Nzuwani. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

Wananchi wa Comoro wanaunganishwa na dini ya kiislamu ya madhehebu ya Sunni, lugha, na utamaduni. Moja ya nguzo muhimu ya utamaduni wao ni sherehe za harusi. Sherehe muhimu ni lie inayoitwa Ada, sherehe ambayo ni kubwa, ya gharama, na inabidi ifanyike hata kama ndoa ni ya zamani. Mwanaume ukifanikisha sherehe hii basi unapanda daraja katika ngazi ya jamii. Unaheshimika na unaweza ukakaa na wenzako na kujadili na kuamua kuhusu masuala ya jamii. Vilevile unaweza ukavaa joho maalum katika sherehe, joho linalokutambulisha kwamba umetimiza wajibu wako. Unapewa nafasi ya mbele kukaa, kiitifaki.

Lakini Ada ni sherehe inayogharimu sana. Kawaida inabidi mwanaume umpe mkeo dhahabu wastani wa kilo mbili hivi. Matumizi ya wastani wa euro elfu hamsini au shilingi za kitanzania milioni 70 ni kawaida. Msimu wa sherehe hizi ni kuanzia Juni mpaka Septemba. Ni katika kipindi hiki wanapokuja nyumbani kwa likizo waComoro wanaoishi nje ya nchi kwa ajili ya likizo. Wengi wao huishi na kufanya kazi Ufaransa. Fedha ambazo wanadiaspora hawa hungiza nchini mwao ni sehemu kubwa ya uchumi wa Comoro. Hali hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kutambuliwa kwa uraia pacha katika Katiba ya nchi. Karibu kila familia ina ndugu aliye Ufaransa. Ukipita maeneo mengi mbalimbali ya Moroni na vijijini utaona nyumba nyingi ni kubwa lakini hazijamalizika. Nyumba za ghorofa zimeishia chini na zinakaliwa, sakafu ya pili ina vyuma vikijitokeza kwenye nguzo, kuonesha kazi itaendelea baadaye. Ukiuliza kwa nini nyumba ziko hivi, unaambiwa sehemu ya juu watajenga watoto walio diaspora. Kuhusu ukubwa wa nyumba, maelezo ni kwamba iwapo familia ina wasichana basi wanapo olewa waume zao wanahamia kwa wake na wakwe zao.

Tulikuta misururu au foleni ndefu kwenye vituo vya mafuta mjini Moroni. Tulidhani kuna upungufu wa mafuta. Tukaambiwa hali hiyo hujitokeza kila mwaka waComoro walio diaspora wanaporudi nyumbani. Magari yanakuwa mengi barabarani kuliko kawaida. Ajali nyingi hutokea kutokana na vijana kutoka nje ya nchi kuendesha magari kwa kasi kama vile wako ufaransa Wanadiaspora wa Comoro wanajulikana kwa utani kama mashevdje, maana yake walionacho, wenye fedha.

[https://3]

Kituo cha Petroli, Moroni wakati wa uwepo wa Wacomoro walio Ughaibuni. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

[https://2]

Mabaki ya Kaviri Djohe,Makazi ya Masultan Wakuu wa Ngazidja, Ikoni, Moroni. (Picha: Emmanuel Mwandosya)

SIASA ZA UMOJA WA VISIWA VYA COMORO

Mahali pa kuanzia ili kupata uelewa wa siasa za Comoro ni kutembelea na kupata maelezo yanayohusu magofu ya lililokuwa jumba la wafalme wa Comoro au makaazi ya Sultan Tibe, kama ambavyo Sultan Mkuu wa Ngazidja alivyojulikana. Jengo hilo au lilijulikana kama “Kaviri Djohe”, maana yake kichaa au mwendawazimu haruhusiwi kupita. Sultan Tibe wa mwisho kuishi hapo alikuwa Said Ali bin Sultan Said Omar. Baada ya kukorofishana, mwaka 1892 Wafaransa walimpeleka uhamishoni Reunion, na baadaye Tamatave, Madagascar ambako alifariki na kuzikwa mwaka 1916. Hapo kwenye magofu, Ikoni, kuna makaburi mawili, moja la Said Ibrahim bin Sultan Said Ali, mwana wa mfalme Said Ali, na lingine ni la mke wake. Tulipomuuliza Mzee aliyetupa maelezo ya eneo hilo, akatujibu, “ Tunalojua ni jina la Sultan. Jina la mkewe sio muhimu”. Said Ibrahim alizaliwa Antananarivo mwaka 1911. Alirudi Ngazidja na baadaye akachaguliwa kuwa Mbunge katika Bunge la Ufaransa, na mwaka 1970-1972 akawa Waziri Mkuu wa kwanza wa Comoro. Kwa heshima yake na kumbukumbu, kiwanja cha ndege cha Hahaya, Moroni, kimepewa jina la Prince Said Ibrahim.Said Ali Kamal ni mwana wa Said Ibrahim. Ni kiongozi wa Chama la Umoja wa Masiwa (CHUMA). Amewahi kuwa Balozi wa Comoro Ufaransa, Waziri wa Fedha, na Mbunge wa Ikoni, Bashile, Mde, Mwanzaza, Nduani na Serehine. Mtoto mwingine wa Said Ibrahim ni Fahmy Said Ibrahim, mwanasheria ambaye mpaka wiki chache zilizopita alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba. Mheshimiwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro alitutambulisha na tukasafiri naye kutoka Moroni kuja Dar es Salaam.

Siasa za Comoro ni ngumu. Wenyeji wetu walituelewesha wingi wa viongozi wa nchi kama mfano wa hali hiyo. Comoro ilipata uhuru wake toka kwa Wafaransa tarehe 6 Julai 1975. Uhuru ulikuwa ni matokeo ya kura ya maoni iliyofanywa 21 Desemba 1974 ambapo Ngazidja, Mwali na Nzuwani zilipiga kura ya kujitenga na Ufaransa. Maore ilipiga kura ya kupinga uhuru, ikitaka kubakia sehemu ya Ufaransa. Baada ya uhuru, Maore ilipiga tena kura ya maoni mwezi Februari 1976 na kuthuibitisha tena nia ya kubakia sehemu ya ufaransa. Moja ya simulizi tulizopata kutoka Jumba la Makumbusho, Moroni, inahusu jinsi Maore ilivyochukuliwa na wafaransa. Tsi Levalou alikuwa mmoja wa wafalme wa sehemu inaitwa Boina, Madagascar. Baada ya kushindwa vita na mfalme jirani akakimbia na mwishowe kukaribishwa na Sultan Mwana Madi wa Mayotte kama mkimbizi. Tsi, aliyebadili jina lake kuwa Andriansoly, akawa kamanda katika jeshi la Sultan, na kutokana na ushujaa wake akapewa sehemu ya kisiwa. Hatimaye mwaka 1832 akampindua Bwana Kombo, mwana wa Mwana Madi, aliyerithi usultan wa Mayotte na kujitangaza Sultan wa kisiwa chote. Hata hivyo kutokana na vita dhidi yake na hofu ya kupinduliwa, mwaka 1841 akakubali kuuza Kisiwa cha Mayotte kwa wafaransa kwa faranga za kifaransa 5000 za wakati ule, sawa na euro tano za sasa.

Ahmed Abdallah alikuwa Rais kwa kwanza wa Comoro huru kwa muda wa wiki tatu tu 6 Julai 1975-3 Agosti 1975. Akapinduliwa na jeshi, na Ahmed Mohamed Jaffar akawa Rais 3 Agosti 1975 mpaka 3 Januari 1976. Aliyemfuata ni Ali Soilih kuanzia 3 Januari 1976 hadi 13 Mei 1978 alipopinduliwa na jeshi na kuuawa. Akaja Said Athoumani 13-23 Mei 1978, akifuatiwa na Ahmed Abdallah na Mohamed Ahmed wakiwa viongozi wenza Mei mpaka Oktoba 1978. Uongozi huo ukafuatiwa na na Ahmed Abdallah kama Rais kuanzia 25 Oktoba 1978 mpaka alipouawa tarehe 26 Novemba 1989. Haribon Chebani akachukua uongozi wa muda wa siku mbili tu 26-27 Novemba 1989. Alifuatia Said Mohamed Djohar, Novemba 1989 mpaka Septemba 1995 alipopinduliwa na jeshi. Aliyemfuata alikuwa Combo Ayouba, Septemba-Oktoba 1995, akifuatiwa na Mohamed Taki Abdoulkarim na Said Ali Kamal kama uongozi wa mpito 2-5 Oktoba 1995. Caabi El-Yachroutu Mohamed akachukua uongozi wa mpito 5 Oktoba 1995-26 Januari 1996 aliyefuatiwa na Said Mohamed Johar 26 Januari-25 Machi 1996. Baada ya hapo Mohamed Taki Abdoukarim akawa Rais 25 Machi 1996 mpaka alipofariki akiwa kazini tarehe 6 Novemba 1998 katika mazingira ya kutatanisha. Tadjidine Ben Said Massounde akawa Rais wa mpito 6 Novemba 1998-30 Aprili 1999 alipopinduliwa na Azzari Assoumani ambaye aliongoza nchi 30 Apirli 1999 mpaka 21 Januari 2001. Hamada Bolero akawa Rais wa mpito 21 Januari-26 Mei 2001. Baada ya hapo uongozi ukatokana na makubaliano ya kuzunguka kisiwa hadi kisiwa. Akachaguliwa Azzari Assoumani, wa Ngazija, 26 Mei 200-26 Mei 2006; Ahmed Abdallah Sambi, wa Nzuani, 26 Mei 2006-26 Mei 2011; Ikililou Dhoinine, wa Mwali, 26 Mei 2011-26 Mei 2016; na sasa ni Azzari Assoumani, wa Ngazija, 26 Mei 2016 kwa kipindi kinachoisha 26 Mei 2021.

Huwezi ukakamilisha safari yako Visiwa vya Comoro bila kuuliza na kupata maelezo kuhusu kupindi kigumu na kipindi cha giaza kinachomhusu askari wa kukodi au askari mamluki mfaransa aitwaye Robert “Bob” Denard. Ni kipindi cha aibu kwa mwafrika na kwa Afrika. Alizaliwa ufaransa mwaka 1929. Aliajiriwa kama Askari wa Jeshi la Ufaransa. Alipigana vita vya Algeria dhidi ya wapigania uhuru wazalendo. Baadaye akawa askari wa polisi Morocco kabla hajaanza vituko kama askari wa kukodi akitumiwa na wafaransa, nchi za magharibi, na baadhi ya viongozi wa kiafrika dhidi ya wapigania uhuru wazalendo, pamoja na sehemu nyingine, Benin,Nigeria, Gabon, Congo, Angola, Afrika ya Kusini, Seychelles, Msumbiji, na Comoro.

Anajulikana zaidi kwa jinsi alivyotumika na Shirika la Kijasusi la Kifaransa kuitikisa Comoro na kuifanya kituo cha mashambulizi ghidi ya wapigania uhuru wa Msumbiji na Angola, na kuhakikisha Comoro inatumika kama kituo cha Ufaransa, Israeli na nchi za Magharibi kupitisha silaha na bidhaa nyingine kukwepa vizuizi vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa kibaguzi na dhalimu wa makaburu wa Afrika ya Kusini. Ili kukwepa kujulikana na Balozi zilizokuwa Moroni, kisiwa cha Njuwani kilitumika katika kutekeleza mkakati huo. Bob Denard ambaye alijulikana kwa jina lingine kama “Gilbert Bourgeaud” alitumia muda mrefu, zaidi ya miaka 20, Comoro ambako alikuwa akijiita “Saïd Mustapha Mahdjoub”.

Baada ya Ahmed Abdallah Abderemane kutangaza uhuru wa Comoro, kwa maelekezo ya serikali ya Ufaransa, Denard akapindua serikali ya Comoro na kumweka Ali Soilih kuwa kiongozi. Sera za Ali Soilih za mrengo wa kushoto hazikuifurahisha Ufaransa na hivyo Denard akatumika tena kumpindua Ali Soilih na kumrudisha madarakani Ahmed Abdallah Abderemane. Wakati huo Denard alikuwa ndiye mkuu wa kikosi cha walinzi wa Rais. Ahmed Abdallah Abderemane alipojaribu kubadili mfumo wa ulinzi kwa kumwondoa Denard kama mkuu wa kikosi cha ulinzi wa Rais, Denard akaipindua serikali na kumuua Ahmed Abdallah. Kwa msaada wa ufaransa na Afrika ya Kusini Denard aliondolewa Comoro na kurudishwa Ufaransa. Kwa kipindi alichoishi Comoro ni dhahiri kwamba Bob Denard alikuwa ndiye “kiongozi” wa nchi, akipata maelekezo kutoka kwa Jaques Foccart, aliyekuwa mshauri mkuu wa masuala ya Afrika wa Rais Charles de Gaulle na Rais Georges Pompidou. Amehusika na mapinduzi mara tatu na jaribio moja la mapinduzi nchini Comoro. Ni vema vijana wetu wakaifahamu historia hii ili kujua unyonge wa mwafrika na kuazimia “katika historia tumeteseka vya kutosha, tumenyanyaswa vya kutosha. Wakati umefika wa mwafrika kujikomboa kiuelewa, kielimu, na kisayansi na kiteknolojia, na kifikra.

Yaliyotangulia hapo juu ni elimu tosha kuhusu siasa za Comoro. Kwani kuanzia ulipopatikana uhuru mwaka 1975, kumekuwa na vipindi 28 vya uongozi wa nchi. Katika kipindi hicho kumekuwa na Wakuu wa Nchi 17, baadhi wakiwa wanarudia rudia. Baadhi ya Wakuu wa Nchi wameitwa Rais, wengine Wenyeviti wa Baraza la Mapinduzi na wengine Wenyeviti au Wenyeviti wenza wa Kamati za pamoja za Kijeshi na Kiraia. Ili mradi wote ni viongozi wa nchi. Kati yao 8 wamekuwa marais wa mpito; mmoja ameuawa akiwa Rais, na mmoja amefariki akiwa kazini. Tangu uhuru wa Comoro yametokea mapinduzi ya kijeshi 7 na majaribio ya mapinduzi 12. Hali ya utulivu wa kisiasa imekuwepo kuanzia mwaka 2001 mpaka sasa kutokana na makubaliano ya kuwa na mzunguko wa urais kila baada ya miaka mitano, baina ya visiwa hivyo vitatu.

Mjadala unaoendelea Comoro ni ule unaohusu kile kinachoweza kuitwa “Maradhi ya Uongozi, Afrika (African Leadership Malaise)”, uongozi ulio madarakani kutaka kubadili katiba kwa madhumunu, pamoja na mengineyo, kujiongezea muda wa uongozi. Mjadala huo ni mkali. Wanaounga mkono wanasema wakati umefika wa kuitazama Comoro kama nchi moja bila kujali nani anatoka wapi. Wanaopinga hutoa hoja kuwa suala hili lina mtazamo wa kibinafsi zaidi wa kutaka Rais aliyepo madarakani aendelee muhula wake utakapokwisha. Wanatoa hoja kwamba kwa sababu Ngazidja ina watu wengi basi kuna uwezekano wa uongozi wa nchi kutoka huko muda wote. Wanakumbusha kuwa kwa miaka 16 sasa kumekuwa na utulivu wa kisiasa kutokana na makubaliano ya kubadilishana uongozi.

Yanaitwa Maradhi ya Uongozi, Afrika kwa sababu si kawaida maradhi hayo kuwapata viongozi wa mabara mengine. Ni maradhi yanayoambukiza. Dalili zake zinafanana. Ataanza mtu au kikundi cha watu kujitokeza hadharani na kutangaza kwamba kiongozi aliyepo amefanya makubwa na hivyo aongezewe muda wa uongozi, hata kama aliyoyatanya ndio yaliyotegemewa kutoka kwake! Kikundi kitajitokeza, na mara nyingi watatokana na marafiki wa kiongozi aliye madarakani, kuunga mkono hoja hiyo na kusema kwamba kuwe na mjadala wa kitaifa. Wimbo huo utaimbwa kwa sauti na kutoka sehemu mbali mbali za nchi. Hatimaye uongozi utasema “kama wananchi wameamua, mimi ni nani kwenda kinyume cha matakwa yao? Sauti ya Watu ni Sauti ya Mwenyezi Mungu (Vox Populi, Vox Dei). Katika hali ya namna hii huwa nafikiria Mwalimu Nyerere angelikuwa hai, angelisema nini kuhusu mjadala unaoendelea Comoro hivi sasa. Bila shaka angerudia yale aliyoyatamka alipokuwa akiaga wakati anang’atuka mwaka 1985. Kama kumbukumbu yangu ni sahihi alisema maneno yanayofanana na yafuatayo (paraphrase): “..... Wanasema Mwalimu sasa ukiondoka nchi itakuwaje? Nchi itayumba. Wananchi wanataka uendelee….. Kwa kweli hao ni wenye masilahi yao binafsi yanayotokana na mimi kuwa kiongozi. Si kwamba wanazungumza kwa niaba ya wananchi, bali wana hofu kwamba Mwalimu akiondoka basi mambo yao yataharibika….” Basi ni matumaini yetu kwamba uongozi na wananchi wa Comoro watafanya uamuzi wa hekima na busara kwa faida ya Comoro na faida ya Afrika kwa ujumla.

FURSA ZA USHIRIKIANO

Tulichobaini katika safari ya Comoro ni ukaribu wa kila aina kati ya Comoro na Afrika ya Mashariki na zaidi kati ya Comoro na Tanzania. Sehemu kubwa ya watu wa Comoro wana asili ya Tanzania, bara na Zanzibar. Pale katika Jumba la Makumbusho mjini Moroni kuna maelezo kuhusu Juma Mnyamwezi, Jemadari wa Kinyamwezi aliyewahi kuwa mkuu wa vikosi vya Sultan Said Ali bin Sultan Said Omar,Sultan Mkuu wa mwisho wa Ngazija,karne ya 19. Mbali na kifaransa, kicomoro, na kiarabu, lugha nyingine inayozungumzwa ni kiswahili. Kicomoro pia mizizi yake ni kibantu na asilimia kubwa ya istilahi yake inatokana na kiswahili. Mila na desturi za Visiwa vya Comoro zinafanana sana na zile za mwambao wa Tanzania bara na Zanzibar. Vazi rasmi Comoro ni kanzu na koti na barghashia au tarabushi kwa wanaume, na kanga au vitenge nadhifu na vilivyovaliwa kwa heshima. Dini ya Kiislam inaunganisha nchi hizi mbili.

Baadhi ya wasomi maarufu wa dini wameishi Zanzibar na Comoro. Kwa mfano, Marehemu Said Omar bin Smeth aliwahi kuwa Kadhi na Mufti wa Zanzibar na Mufti Mkuu wa Comoro. Marehemu Said Omar Abdallah Mwinyi Baraka alikuwa msomi wa theolijia ya dini ya Kiislamu Zanzibar na Ngazija na aliiwakilisha Comoro katika Umoja wa Nchi za Kiislamu. Marehemu Sheikh Burhani Mkele alikuwa msomi na mshairi maarufu wa kiarabu na kingazija, na alihamia Zanzibar kutoka Comoro. Ukiwa visiwa vya Comoro unaweza ukafdhani uko Zanzibar, tofauti ikiwa ni milima na jinsi milima hiyo inavyobadili tabianchi, hali ya hewa, mandhari, na bioanwai ikiwa ni pamoja na mimea na viumbe vingine.

Kuhusu jadi na utamaduni, ukiwa Visiwa vya Comoro huwezi ukakosa kusikia umaarufu wa Kisiwa cha Pemba. Utamaduni wa baadhi ya Wacomoro ni kufanya ziara Pemba kwa ajili ya tiba asilia, kutolewa majini, na kuombewa kupata na kupanda vyeo. Pemba ni maarufu kiasi cha kwamba eti Mcomoro akikudhulumu, au akikutendea baya, ukimwambia unakwenda Pemba basi mambo yanarekebishwa mara moja. Lakini tunaambiwa vilevile kwamba huku kwetu baadhi ya wanasiasa hutegemea sana na kuwaamini zaidi waganga kutoka Comoro, na wengi huenda huko wakati uchaguzi unakaribia!

Nchi huanzisha taasisi maalum kwa minaajiri ya kukuza na kueneza lugha na tamaduni zao duniani. Taasisi hizo huwa pia na madhumuni ya kuendeleza mahusiano na biashara na uchumi. British Council, Alliance France, Goethe Institute na Confucius Institute, ni mifano ya taasisi kama hizo za kiingereza, kifaransa kijerumani, na kichina, sawia. Kiswahili sasa ni lugha kubwa. Wakati umefika wa kuanzisha taasisi ya namna hiyo kwa madhumuni kama hayo. Nchi za kwanza kufaidika zitakuwa nchi za jirani na mataifa mengi duniani ambako kiswahili kimeanza kutumika.

Ukaribu kati ya Comoro na Tanzania, ukitumika vizuri unaweza ukachochea maendeleo ya watu wa pande zote mbili. Tumebaini watu wa Comoro kutokana na historia wajiona wako karibu na Ufaransa na Tanzania. Si mara chache utasikia, “kwetu sisi Dar es Salaam ni Paris ya pili”, kwa maana ya kwamba kibiashara, huduma za kijamii na utalii, Dar es Salaam ni karibu kwao kuliko miji mingine mikuu ya nchi jirani. Ni jambo la kawaida siku hizi kwa Mzee wa ki ngazidja kumwambia kijana wake aliye Ufaransa amtumie fedha ili aende Dar es Salaam kwa matibabu na kupumzika. Mbali na bahari inayoizunguka, visiwa hivyo vina rasilimali asilia ya kila aina na uwezekano mkubwa wa kuwepo gesi asilia na mafuta ya petroli. Wenyeji wetu kule Nzuwani walitusisitizia, “kisiwa chetu ni tajiri sana kwa rasilimali asilia, ikiwa ni pamoja na madini. Tungependa wawekezaji na majiolojia wa kitanzania waje tushirikiane vinginevyo wachina watachukua kila eneo. Msichelewe”. Utalii ni eneo jingine ambalo wenyeji wetu wa Nzuwani walitushauri tuwashawishi wafanyabiashara wa kitanzania wawekeze; katika sehemu mbalimbali za mnyororo wa thamani katika sekta.

Mazungumzo yetu na Mheshimiwa Balozi na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro yalihusu kwa kiwango kikubwa fursa za kibiashara zilizopo kati ya Tanzania na Comoro, ikidhihirisha mrengo wa kisasa wa diplomasia ni uchumi. Lakini kama kawaida yetu, tumeisaidia sana Comoro kisiasa na kiulinzi, tuna” goodwill” kubwa, tuna uhusiano wa kitamaduni, kilugha, na kijirani, na kidini, lakini nchi nyingine za jirani ndizo zitakazowahi na kufaidika na ushirikiano wao na Visiwa vya Comoro.

Wakatabahu,

Mark Mwandosya

Moroni, Ngazija, Comoro

Agosti, 2017
 
Nimefurahi tu kujua hayo maneno mapya wanayotumia watu wa Comoro...na pia wame nishangaza walivyo kuwa wanawapindua Marais wao katika muda mfupi mpaka walipoweka utaratibu wa kila kisiwa kutoa Rais kwa miaka mitano

Asante Prof Mwandosya
 
Mheshimiwa Mwandosyo Mungu akuzidishie maarifa, nilikuwa mbali na welewa wa kisiwa hicho, lakini umeeleweka sana.
 
Mmmmh,
Basi tena nakuja nami nikiishafikisha umri huo wa kulitumikia Taifa langu kisha nitaleta simulizi.

Hongera sana na umefanya vizuri kutujuza wengine.
 
Nilikua najiona nipo Comoro toka mwanzo wa simulizi mpaka mwisho ndo nimestuka nipo kitandani...Hali hii picha hazijafunguka

Ama kweli profesa kautendea haki uprofesa wake
 
Prof..si kwamba Tanzania haina ushirikiano na Commoro.. Hivi wale ng'ombe tuliokuwa tunawauzia commoro wakiwa na ule unga hizi tetesi zimeishia wapi?
 
Hongera mzee kwa stori murua,nimefumbua macho vya kutosha na siku moja nitatembelea visiwa vya comoro.
 
Asante kwa maelezo mazuri na utashi mwema kwa nchi yetu. Professa umeonesha uzalendo kwa nchi yetu na pia najua umri umekwenda ila umetumia pia muda mwingi kuandika habari nzuri na ndefu na tena kwa mtiririko mzuri sana!

Nafahamu wewe ni Prof wa engineering lakini kipaji cha uadishi ulichonacho ni kikubwa utafikiri prof. wa Kiswahili Amandina Lihamba, nk

Nakutakia kudumu katika uzalendo

Emmanueli usimwangushe baba na wewe kaza mwendo ufike hata mbali zaidi najua material yote ya kuwa hivyo unayo tayari.
 
Ahsante mzee. Mungu akujalie uzee mwema wenye amani na furaha! Usiache kumshauri raisi wetu, ushauri wako ni muhimu ili kuliongoza vema taifa letu.
 
Hapo upi vzr

Kwa hali hii uchaguzi huru na haki haupo Tanzania labda nguvu ya umma itumike

Oyoo oyoo
Hayo ni mawazo yako na ndiyo mwisho wa uelewa wako

Sent using Jamii Forums mobile app

Back
Top Bottom