STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 4
Calvinjr aliendesha gari lake kuelekea nje kidogo ya mji, Mbezi Temboni ndiko alikokuwa anaelekea majira hayo ya jioni kwenda kuonana na mama yake mzazi ambaye alikuwa akiishi huko.
Gari yake ilikuwa inaenda kwa spidi kali sana, baada ya kufika sehemu ambayo ilikuwa na mgawanyiko wa barabara nyingi, alichepuka na kuishika njia ambayo ilikuwa na mabonde bonde mengi sana, hakuwa akipenda kabisa mama yake aweze kuishi eneo kama hilo lakini mwanamke huyo yeye aliona ni sahihi kuishi huko na hakutaka kabisa mtu yeyote apingane na hayo maamuzi yake.
Calvin aliendesha gari kwa nusu saa nzima kwenye hiyo njia mbovu mpaka alipo kutana na tambalale, hapo aliendesha gari kwa kasi kwa dakika zipatazo kumi akawa analiangalia geti la blue ambalo lilikuwa mbele yake. Lilikuwa ni jumba la kifahari mno ambalo lilijengwa nje ya mji huko na hapo ndipo palikuwa nyumbani kwao, geti lilifunguliwa baada ya kipiga honi mara tatu, aliliingiza ndani na kushuka ili aelekee ndani.
"Waooo mziwanda wangu, naona leo umekuja bila hata taarifa bila shaka umeniletea taarifa za kuniletea mkwe hapa" mama huyo aliongea kwa furaha huku akimkumbatia mwanae wa kiume na kumbusu kwenye baji lake la uso, huyo ndiye alikuwa mtoto wa mwisho kwenye familia hiyo.
"Aaah! mama wewe unawaza kuoa tu"
"Ebu kelele na wewe, ujue wewe na dada yako siwaelewi. Umri wangu unazidi kwenda lakini cha ajabu sioni hata dalili ya kuletewa wajukuu humu ndani, mnajifanya mko busy na kazi ambazo hata sijui mnamfanyia nani kama hamtaki familia. Naye dada yako anajifanya yuko busy na masomo ambayo hata sijui anasomea nini, sitaki huo ujinga kwenye nyumba yangu" mama huyo aliongea huku akiwa anampa kijana wake maziwa.
Alikuwa anawapenda sana wanae ila alikuwa anaumia umri unaenda na hawamletei wajukuu wa kucheza nao, Calvinjr alitabasamu tu huku akikaa kwenye sofa, kwa maana alikuwa na mazungumzo marefu kidogo na mama yake.
"Sawa mama nimekuelewa kwa hilo lakini kwa leo nimekuja kuongea na wewe jambo la mhimu sana tena zaidi ya sana. Naomba usinidanganye tafadhali, mimi nakuamini sana hivyo nategemea utakacho niambia utakuwa ni ukweli na nitakuamini mama yangu" maneno ya Calvinjr yalimshtua mama yake, kiasi kwamba akaacha alichokuwa anakifanya na kusogea kwenye kiti ili amsikilize mwanae wa mwisho alihitaji kujua kuna nini mpaka akamuomba asimdanganye.
"Mama yako nipo hapa, nambie ni kipi hicho kinacho kusibu mwanangu" mama aliongea kwa upole na kumpa nafasi mwanae huyo kuweza kuyasema yale ambayo yalionekana kuutesa mtima wake.
"Mama nataka kuujua ukweli kuhusu baba yangu, kwani mimi ni nani mama? Nafanana na nani, je kuna maisha yangu mengine ambayo huenda siyajui mama yangu unanificha labda?" Maswali aliyo ulizwa yalimuacha mama huyo mdomo wazi, hakutarajia ama kutegemea kama angeulizwa kwa namna kama hiyo.
Alibaki ameganda kama sanamu ambalo linasubili kuhamishwa kutoka lilipo ili kwenda mahali pengine, machozi yakikuwa yanamshuka kwenye macho yake akiwa haelewi afanye nini kwa maana maneno ambayo yalitoka kwa mwanae ilikuwa ni haki yake kujijua yeye ni nani lakini kwake ulikuwa ni mwiba mkali sana kwenye nafsi yake.
"Mwanangu kuna mtu amekwambia kwamba wewe unafanana na mtu?" Mama huyo ambaye jina lake alifahamika kama Dainesi Mtandu aliuliza akiwa anajifuta machozi taratibu kwenye macho yake. Calvinjr hakumficha kitu kwa sababu alidhamiria kumwelekeza kila kitu ambacho alikisikia wale wafanyakazi wake wakiongea kule ofisini hususani kwa mzee Bakezi (alifanya kosa kubwa sana kumtaja huyo mzee).
Mama huyo alimsogelea mwanae na kumbusu kwenye shavu lake kisha akatoka na kwenda chumbani ambako alirudi na kitabu kimoja kikiwa kwenye mkono wake.
"Hii ndiyo zawadi pekee ambayo baba yako aliniachia kabla ya kupotea siku ya mwisho kwenye macho yangu" alikuwa anaongea huku anampatia mwanae kitabu hicho.
Kitabu ambacho alikishika kwenye mkono wake kiliandikwa, INNOCENT KILLER (THE REVENGE), kikiwa na maana ya MUUAJI ASIYE NA HATIA (KISASI). Calvinjr alikipokea kwa mara kwanza kabisa kwani hakuwahi kujua kama kuna kitabu ambacho baba yake aliwahi kukipenda sana kukisoma.
"Kitabu hicho mimi nimekisoma baada ya yeye kutoweka, sikuwahi kukigusa, aliwahi kunikataza kabisa kukisoma kwani alisisitiza kwanza kama nitataka kukisoma kitabu hicho basi inanibidi nisome kwanza kitabu ambacho kinaitwa ULIMWENGU WA WATU WABAYA ila kwa bahati mbaya sana niliwahi kukitafuta sana kitabu hicho bila mafanikio na hakipo sehemu yoyote ile ndani ya maktaba zote kubwa zilizopo hapa nchini"
"Baada ya muda mrefu kupita niliamua kukisoma hivyo hivyo na nilicho kutana nacho ndani, ni kwamba kilikuwa kinamhusu mwanaume mmoja ambaye alikuwa anaishi maisha ya kawaida sana na alikuwa ni ndugu wa jaji mkuu wa nchi ila aligeuka kuwa mnyama wa kutisha sana baada ya baadhi ya watu kumuua ndugu yake na familia yake nzima"
"Mwanangu, sijui kitabu hicho mpaka leo kinahusu nini hasa ila nadhani kuna ujumbe ambao una maana fulani humo ndani japo ukikisoma unaweza usijue lolote kama ambavyo mimi sina nilijualo mpaka leo hii. Sina mengi juu ya hicho kitabu ila tu nitakujibu swali lako kama ifuatavyo"
"Mimi na baba yenu tuliwahi kupendana sana isivyokuwa kawaida, mapenzi yetu mazito ndiyo yaliyo pelekea nyie kuzaliwa. Licha ya sisi kupendana sana na kuwa tayari kuishi kwenye mazingira magumu pamoja kwa hali yoyote ila ila tulikuwa ndani ya umaskini mkubwa sana, tulikuwa na maisha ambayo hayakuridhisha kabisa hasa kwa sisi ambao tulikuwa tumepata familia kubwa hasa baada ya wewe kuongezeka ukiacha dada yako ambaye alizaliwa miaka miwili kabla yako"
"Ukubwa wa familia uliongeza mzigo mkubwa ambao ulimfanya baba yenu kuchukua maamuzi magumu sana, maamuzi ambayo mimi binafsi sikuyaridhia ila sikuwa na namna zaidi ya kuheshimu kile ambacho alikiamua. Baba yenu aliamua kwenye kuitafuta bahati yake kwenye machimbo ya madini huko Shinyanga, kwa wakati huo alipata taarifa kwamba mashimo ya madini yanatema sana"
"Ila kama ningejua basi huenda ningelazimisha tu abaki, tangu alipo ondoka siku ile, ule ndio ulikuwa mwisho wa kumuona mume wangu, sikuwahi hata kuisikia japo sauti yake kwa mara nyingine na ni miaka ishirini na mitano imepita kwa sasa."
"Baada ya muda mrefu sana kupita nililazimika kuanza kufuatilia ili nijue tatizo lilikuwa nini? Niliamini hata kama angekuwa amezidiwa sana na kazi, bado asingekosa muda wa kunitafuta na kunijulia hali ikiwa nina mtoto mchanga kabisa ambaye ulikuwa ni wewe hapo."
"Baada ya kufuatilia kwa wiki nzima bila kupata majibu, ilitolewa taarifa kwenye mitandao na vyombo vya habari kwamba zaidi ya machimbaji wadogo hamsini walikuwa wamefukiwa na vifusi vya mgodi na kupoteza maisha.
Jitihada za kuwatafuta zilifanyika lakini walifanikiwa kuipata miili ishirini tu, hiyo mingine thelathini walitafuta bila mafanikio wakaamua kutangaza kwamba watu hao wamefia huko ndani na hivyo kuliko kuendelea kupoteza pesa ambazo zingesaidia kusomesha wanafunzi, basi mgodi huo unafungwa kwa heshima ya watu waliofukiwa na hilo eneo linatengwa kama kaburi maalumu kama heshima kwa nchi kwa kuwapoteza wapambanaji hao"
"Nilichanganyikiwa kiasi kwamba nikawa natamani niyachukue hata maisha yangu baada ya watu wote ambao walipona kuruhusiwa kurudi nyumbani lakini cha ajabu baba yenu hakurudi kabisa, kwa maana hiyo ni kwamba baba yenu alikuwa moja ya watu ambao walifukiwa na vifusi hivyo huko kwenye machimbo. Kwangu mimi sikutaka kuamini kwamba mume wangu amekufa kwa sababu sikuona hata mwili wake nikathibitisha mwenyewe ila kwa asilimia sabini ni kwamba hakuwa hai"
"Kama mume wangu angekuwa mtu aliye changanyikiwa na dunia ningeamini kwamba alipata madini na akaamua kuitelekeza familia yake kwenda kuishi maisha mazuri mbali na sisi, lakini baba yenu aliipenda familia yake kuliko kitu chochote kile hivyo asingeweza kabisa kufanya jambo la hovyo kama hilo"
"Kilicho nifanye nighairi yale maamuzi ya kujiua, ni nyie hapo wewe na dada yako, niliwaza nitamuachia nani watoto wangu mwenyewe? Hakuwepo. Nikawaza kwa namna dunia ilivyo na watu wabaya nani atawalea wanangu kwa mapenzi ya dhati? Sikuona. Ndipo nikagundua kwamba mzigo ulikuwa ni wangu, tena wangu pekeangu!"
"Ningefanya kosa kubwa saba kama ningeamua kuwaacha pekeenu bila msaada wowote, hapo ndipo yale mawazo yalipo toweka kabisa kwenye kichwa changu ya kujiua"
"Maisha yalikuwa magumu sana pekeangu bila msaada wowote ule, nilizunguka kila sehemu huku nikiwa nimekubeba mgongoni na dada yako anatembea taratibu nikitafuta vibarua. Kuna watu walinisaidia na kuna watu walikuwa wakinitukana, yote ilikuwa kheri kwangu na nilishukuru kwa uzima"
"Nilibahatika kupata kazi ya kuuza kwenye mgahawa ambayo ndiyo ilibadilisha maisha yangu, nilifanya kazi kwa bidii sana maana kila nikiwaangalia nyie nilikuwa napata uchungu mkubwa sana moyoni mwangu.
Nilijitahidi kuhifadhi mpaka nilipo pata mtaji wa kuuza maji, niliuza maji na bidhaa za nyumbani ambazo zilileta tumaini jipya mpaka nikafanikiwa kuinunua kampuni yangu ambayo ndiyo unaisimamia mpaka leo na imebadilisha maisha yetu yote mpaka leo" mama huyo alimaliza kusimulia akiwa anamuangalia mwanae usoni.
Calvinjr alimsogelea mama yake na kumfuta machozi, hakutakiwa kuuliza hayo yote kwa maana ni kama alikitonesha kidonda kwenye moyo wa mama yake.
"Nimekuelewa mama na naomba sana unisamehe. Mimi nakuamini sana wewe mama kuliko mtu yeyote yule kwenye maisha yangu" Calvinjr alimbusu mama yake kwenye paji la uso huku akitoka nje na kuondoka. Hicho ndicho kitu pekee kilicho mpeleka kwa mama yake hivyo kukaa naye karibu huenda angeendelea kuiharibu furaha ya mwanamke huyo wa zamani kidogo.
Dainesi Mtandu baada ya mwanae kuondoka, alijibeba hapo na kuelekea chumbani kwake ambapo baada tu ya kuingia aliufunga mlango wa chumba hicho. Aliusogelea ukuta, sehemu ambayo usinge idhania palikuwa na mlango wa siri ambapo alisogeza jicho lake kwenye sehemu ya ukuta ambayo ilikuwa na nukta ndogo sana.
Sehemu hiyo ilifunguka, akaingia huko ndani. Kwenye ukuta zilikuwa zimebandikwa picha nyingi sana kubwa za mwanaume ambaye alikuwa ndani ya suti ya bei lakini kwenye picha zote mtu huyo alikatwa upande wa kwenye kichwa.
"Sitaruhusu huyu mtoto aje kujua lolote kuhusu wewe kamwe, hatakiwi kuijua historia ya maisha ya asili yake wala hatakiwi kukufahamu wewe. Acha aishi maisha ya kawaida kama waishivyo watoto wengine, nipo tayari kuibeba dhambi ya kumdanganya huyu mtoto mpaka naingia kaburini ila sio kumwambia ukweli wowote kuhusu wewe. Hata wewe huko uliko naomba unisamehe sana kuhusu hili maana sina namna." Mama huyo alitamka maneno hayo huku akiwa anatoa chozi.
Aliinama kwenye droo moja humo ndani na kuitoa simu. Aliiwasha simu hiyo na kupiga namba ambayo ndiye pekee ilikuwa imehifadhiwa kwenye simu nzima. Simu iliita upande wa pili na kupokelewa.
"Uko wapi?"
"Nakuja hapo sasa hivi mambo yameaanza kuharibika" mama huyo aliongea mfululizo baada ya mtu wa upande wa pili kumwelekeza alipokuwepo.
Hakuonekana kuwa na amani kabisa maana hofu ilimtawala moyoni, alifunga hiyo sehemu haraka sana na kujifunga mtandio usoni kisha akatoka ndani kwake. Nje aliwakuta walinzi wake wanamsubiri lakini cha ajabu aliwaambia kwamba gari ataendesha mwenyewe na asifuatwe na mtu yeyote.
Unahisi huyu mama ana siri gani moyoni? Anajaribu kumficha nini mwanae? Yule mwanaume kwenye kile chumba ni nani? Anaenda kukutana na nani na kwa sababu zipi?
Bado ni mapema sana, episode ya 4 inafika tamati.
Wasalaam.
Febiani Babuya.
Sent from my SM-A107F using
JamiiForums mobile app