STORY: KARATA YA MAUAJI
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WhatsApp: +255621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE 18+
SEHEMU YA KWANZA
MALI
JANGWA LA MALI
Mali ni moja ya mataifa ambayo yana joto zaidi duniani lakini pia ni miongoni mwa mataifa makavu zaidi baadhi ya maeneo kwa sababu ya kutokuwa na hali ya mvua za kutosha lakini pia ni moja ya maeneo ambayo yana historia kubwa zaidi duniani hasa kutokana na umaarufu wake wa biashara tangu enzi na enzi.
Bamako ndiyo mji mkuu wa mali na jiji ambalo lina mzunguko mkubwa zaidi wa biashara ndani ya taifa hilo ambalo linadaiwa kwamba aliwahi kuishi moja ya watu matajiri zaidi kuwahi kuishi kwenye uso wa Dunia, Mansa Musa. Kaskazini mwa Mali ndiko ambako kuna hali ya ujangwa kwa sababu ya uhaba wa mvua, jamii ambayo inaishi huko ni jamii ya kabila la Tuareg ambao huwa wanalazimika kutumia ngamia kama njia ya usafari ambayo ndiyo rafiki kwa maeneo hayo kwa sababu wanasafiri umbali mrefu kuweza kupata huduma ya maji pamoja na mizunguko ya kibiashara.
Kwenye moja ya nyumba kuu kuu kwenye jangwa hilo alikuwa ameketi mwanaume mmoja ambaye kwa mwonekano ni kama alitoka kufanya mazoezi kwa sababu mwili ulikuwa unatoka jasho. Alikuwa anatumia taa za sola ya jua kwa ajili ya kuhakikisha anapata mwanga ndani ya eneo hilo hivyo alikuwa yupo huru kwenye nyumba hiyo akiwa anamenya tunda na kisu mkononi huku akiwa anazunguka ndani na kupiga mlunzi mpaka pale ambapo mluzi huo ulikwama. Haukukwama kwa sababu alipata shida ya koo bali ni kutokana na kitu ambacho alihisi kinatokea. Alisita baada ya kusikia kama kuna muungurumo kwa mbali, alivuta hisia za masikio yake akatambua kwamba huenda kulikuwa na ugeni eneo hilo ndiyo sababu aliamua kusimamisha alichokuwa anakifanya na kuamua kusogea dirishani ili kuweza kuona kama masikio yake yalikuwa sahihi.
Alifungua pazia kidogo na kuacha waya na nondo ambazo zilishonwa kwenye dirisha hilo zimpe nafasi ya kuweza kuona nje kwa usahihi. Masikio yake yalikuwa sahihi kwa sababu yalimpatia taarifa ya kweli. Mita kama mia mbili kutoka ambapo alikuwepo yeye kulikuwa na gari mbili ambazo zilisimama na sio kusimama tu bali aliona watu wanashuka tena wakiwa na silaha nzito. Hakuwa na muda wa kujiuliza kuhusu jambo lile kwa sababu eneo lile halikuwa na nyumba nyingine na watu wale uelekeo wao ulikuwa ni kule ambako yeye alikuwepo na hapo ndipo alitambua kwamba ni yeye ambaye alivamiwa na kwa aina ya watu ambao walikuwa wanakuja na uzito wa silaha ambazo zilikuwa kwenye mikono yao ni lazima walikuwa wanaenda kumuua yeye.
Alisonya na kutukana kwa wakati mmoja kwa sababu hazikuwa habari njema kwa wakati wake. Mwilini alivaa vesti nyeusi huku akiwa amevaa suruali ya kuvutika na buti moja zito mguuni, kichwani alikuwa amejifunga skafu moja ambayo ilizungushiwa vizuri kama mtu ambaye alikuwa akiswali haswa. Alizima taa zote ndani kukawa na giza bila shaka alikuwa anatuma ni taarifa kwa watu wake kwamba alikuwa akitambua uwepo wao hilo eneo. Alifungua stoo moja ambayo haikuonekana kutumika mara nyingi akaingia huko kisha akatoka akiwa na bastola mbili ambazo alizipachika kiunoni huku mkononi akiwa na kisu kile ambacho alitumia kukatia tunda.
Dakika moja tu ilitosha kufanya zile hatua za wale wanaume kuanza kusikika vizuri, walikuwa wameizingira nyumba hiyo kwani walionekana kuwa na taarifa juu ya uwepo wa mhusika ambaye walikuwa wanamtafuta ndani ya hiyo nyumba. Wengine walizungukia nyuma na baadhi walipita kwa mbele ili kupata urahisi wa kutekeleza jukumu lao kama wahusika walivyokuwa wamelipanga kwa usahihi. Mlango wa mbele ulivunjwa wakaingia na silaha zao ila kutokana na kile kiza totoro iliwalazimu kutumia tochi zao kwa ajili ya kumulikia. Mmoja wao alikuwa mbele, aliona kuna korido fupi hivyo akawa anatembea kwa mahesabu kuweza kuwahi eneo lile ambalo alihisi kwamba huenda mbele yake kulikuwa na mtu ambaye walimfuata.
Alifika pale na kukunja kushoto kwake akiwa makini ila wakati anaikunja tu silaha yake alisikika akiwa anaguna, wenzake walianza kumuita kwa jina lake lakini hakuitikia kwani alikuwa akienda sakafuni. Walianza kushambulia kwa risasi lakini waligundua kwamba risasi zao zilikuwa zinaishia ukutani tu hawakufanikiwa kumpata mtu ambaye alikuwa amemshambulia mwenzao, walijitahidi kumpatia huduma ya kwanza bwana yule ila kwa bahati mbaya hakumaliza hata sekunde ishirini akawa amekufa kwakuwa alikatwa sehemu mbaya ya shingo yake. Walisimama na kukonyezana kisha wakaanza kutembea kwa tahadhari kuelekea ndani zaidi ila hawakujua kama mwenyeji wao alikuwa juu ya paa akiwa anawaangalia kwa umakini wakati wanamnyatia.
Alishuka na kutua nyuma yao, mwanaume aliyekuwa nyuma aligeuka kwa pupa akakutana na kisu ambacho kilitenganisha kifua chake eneo la moyo akatupwa pembeni. Wa nyuma alikuwa anajiandaa kupiga risasi baada ya kushtukia jambo hilo lakini mwenyeji wake alivuta bastola yake akaibamiza kwenye buti lake ili kuikoki akampiga bwana huyo risasi kwenye shingo akashuka akiwa amejishikilia eneo hilo huku silaha akiitupa mbali. Wakati anaitupa silaha yake alikuwa ameruhusu risasi zitoke hivyo zilienda kupiga kwenye paa la eneo hilo na ile milio ikawashtua na wengine. Wakati hayo yote yanatokea wale wanaume ambao walikuwa karibu pale hawakuwa wakishambulia kwa silaha maana kulikuwa na kiza na taa zao zilikuwa zikiyumba na mhusika aliutumia ule mwanya kuweza kujitetea.
Aliteleza kwa magoti yake kwa nguvu akajinyanyua kwa sarakasi ambayo ilimfanya kutua nyuma ya mwanume mmoja, alimkunja shingo yake na kuinyonga akamtupia pembeni. Ni mmoja tu alikuwa amesimama mbele yake wakati akiwa anamtafuta mtu huyo alitambua kwamba alikuwa nyuma yake, aligeuka kwa pupa akiwa anaruhusu risasi ambazo zilipiga pembeni kwa sababu hakufanikiwa kugeuka vizuri, kisu kilichomekwa katikati ya paji lake la uso kikashushwa mpaka kwenye pua hadi eneo hilo likabaki wazi. Bwana yule ambaye alikuwa mwenyeji wa lile eneo hakuendelea kusubiri kwa sababu alitambua kuna watu wengine ambao walikuwa wamepitia mlango wa nyuma bado walikuwepo hivyo alielewa kwamba kulikuwa na kazi ya kuweza kuifanya bado kwa wakati huo.
Aliamua kutokea mlango wa mbele ili aweze kuwazungukia kwa nyuma kwa sababu alielewa watu hao walikuwa wametokea nyuma wanakuja mbele. Baada ya kuzunguka mpaka kule nyuma ilionekana kama watu wale walitumia muda mwingi kujaribu kuufungua mlango ule na wakati ule ndipo walikuwa wakiingia ndani hivyo aliwafuata kwa nyuma. Walikuwa ni watatu watu hao kwa sababu aliwaona vizuri kupitia zile taa zao ambazo walikuwa nazo, hawakuonekana kuwa wepesi kama wale wa mwanzo ambao aliwaua muda mfupi ambao ulipita na alielewa kwamba huenda ndiyo ilikuwa sababu watu hao walikuwa wamejitenga wenyewe. Alitembea kwa tahadhari kubwa akiwa anaenda hatua sawa na zao ambazo walikuwa wanapiga, aliyekuwa nyuma alisimama baada ya kuhisi kama nyuma yake kulikuwa na mtu mwingine mbali na yeye, aligeuka kwa kasi akiwa anahema kwa mbali lakini hakuona kitu hivyo akaendelea na safari yake.
Bwana yule alipaswa kuziamini zaidi hisia zake kwa sababu zilikuwa zinampatia taarifa ya mhimu ambayo aliamua kuipotezea. Alihisi tena kama kuna mtu anamjia nyuma hivyo akaamua kupotezea kwa sababu mara ya kwanza alihisi kwamba hakuwa sahihi lakini hali ile ya kusita kufanya maamuzi ilienda na maisha yake. Alipigwa ngumi nzito kwenye mgongo wake mpaka mifupa ikaitikia, aligeuka kwa buti lake zito ambalo lilidakwa kwa mkono na yule bwana ambaye aliuvunja ule mguu hali iliyopelekea yule mtu kuanza kupiga kelele za maumivu ambazo ziliisha baada tu ya kisu kuchimbua eneo lake la koromeo na hapo ndipo risasi zilipoanza kulindima kwa nguvu.
Ni wanaume wawili ambao walikuwa wamebaki ndio walikuwa wakizirusha zile risasi ambazo zilielekea kwenye ukuta ambao bwana yule alijirushia. Walirusha risasi nyingi kiasi kwamba zile silaha zao nzito ziliishiwa risasi hivyo ikawalazimu kutoa bastola zao wakiwa wanasogea eneo lile kuhakiki kama bwana yule alikuwa amekufa tayari. Walisogea mpaka karibu lakini walipigwa na butwaa baada ya kutambua kwamba eneo lile halikuwa na mtu hata mmoja yaani walikuwa wao wawili tu hapo ndipo wakatambua mwenyeji wao aliwapoteza. Waligeuka kwa pamoja ila muda haukuwa rafiki kwa upande wao, zilikuwa zinapigwa risasi nyingi hali iliyofanya mwanaume mmoja kumtumia mwenzake kama ngao ya kujikingia risasi kwani hata hivyo alikuwa amepigwa risasi nyingi hivyo hakuona shida kumtoa sadaka.
Mpiga risasi alikuwa anashambulia huku akiwa anasogea kwa kasi hali ambayo ilimnyima bwana yule nafasi ya yeye pia kushambulia. Akiwa amemtanguliza mwenzake mbele ambaye ndiye alikuwa anapokea risasi zote hizo alishtuka kukutana na mgandamizo mkubwa ambao ulimsukumia mbali ukutani akajibamiza hata ile bastola ikaenda mbali, wakati huo nyumba ilikuwa na mwanga wa taa na bila shaka ni mwenye hiyo nyumba aliziwasha. Walikuwa wakionana vizuri wanaume hao wawili ambapo yule mmoja alikuwa hana silaha ila mwenyeji wake alikuwa na bastola lakini nazo ziliisha risasi huku kwenye kiuno kikiwa kinaonekana kile kisu.
Wawili wale walibaki wanaongea kwa ishara, nyuso zao zilikuwa zinapeana taarifa kwamba kulikuwa na namna moja tu ya kufanya mle ndani, ni mabavu yao ndiyo yalitakiwa kuongea kwa wakati ule lakini yule ambaye alikuwa sakafuni alionekana kuwa na akili ya ziada. Muda wote alikuwa akiangalia kule ambapo bastola ilikuwa imedondokea, bila shaka alihitaji kuiwahi ili imrahisishie kazi hivyo akajirusha ili aidake lakini alijivutia pembeni baada ya kuona kisu kinaenda kule kwa kasi, kama angechelewa basi kingemkata kiganja hivyo kujivuta kwake kulifanya bastola ile ndiyo ikutane na kisu ambapo ilimeguka na kurushiwa mbali hivyo bwana yule akaruka kwa sarakasi moja safi na kusimama wakiwa wanaangaliana, hakukuwa na namna ya mmoja wao kukimbia eneo hilo.
Alimuendea mwenyeji wake kwa nguvu akiwa anarusha mikono yake kwa kasi kubwa, mkono ulitua kwenye ukuta ukatoboa eneo hilo. Alijivuta na kuzungusha mguu wake ambao ulipanguliwa lakini mguu mmoja ambao ulikuwa umebaki ulifanikiwa kuzigusa mbavu za mwenyeji wa eneo lile ambapo aliuma meno lakini hata yeye alirusha mkono wake ukatua kwenye tumbo la bwana yule ambaye aliukunja uso wakati anarudi nyuma na kwenda kujikunja kunja kwa maumivu. Mara ya pili alienda kwa mahesabu, hakukurupuka kama ambavyo alifanya mara ya kwanza kwa sababu alitambua ingekuwa ni hatari kubwa kwa upande wake kufanya jambo kama hilo.
Kwenda kwake kwa mahesabu na taratibu kulimpatia nafasi mpinzani wake ambaye alitoka kwa spidi mithili ya mtu ambaye alikoswa kuuawa akawa anajinasua, alishtukia wakati anapokea ngumi kwenye shingo, aliyumbia upande mmoja akazolewa miguu yake ambayo haikuwa na nguvu ya kutosha kuweza kusimama akabaki anaelea hewani, alikutanishwa na ngumi mbili ambazo zilishiba kwenye tumbo na kifua akatapika damu na kwenda kujibamiza ukutani huku akimwaga damu zaidi. Bwana yule aligeuka haraka na kumrukia mwanaume yule ambapo alimkutanisha na mguu wake kama mtu ambaye anaupiga mpira. Bwana yule alijibamiza tena ukutani na kumfanya hali yake kuwa mbaya zaidi, mwenyeji alimsogelea zaidi ili kumhoji maswali kadhaa maana hawakuwa wametambuana tangu mwanzo.
‘‘Nimeishi kwenye hili taifa kwa miaka miwili sasa, nawajua wazawa wa hili eneo na tabia zao zote hivyo hakuna mtu anaweza kuwa mzawa akawa kama wewe. Tunaweza tusikubaliane ila mimi na wewe wote tunajua kwamba wewe ni mtanzania kama nilivyo mimi, kwahiyo tusipotezeane muda unaweza kuniambia mmejuaje kama nipo hapa na ni nani ambaye amewatuma kuniua?’’
‘‘Wanajua mahali ulipo kwa sasa nadhani wataanza kukutafuta kwa sababu hiyo miaka miwili imetumika kukutafuta bila mafanikio’’
‘‘Nani ambaye ananitafuta kwa sasa?’’
‘‘Nadhani hata wewe unajua ni nani ila kama haujui basi mimi sitakwambia’’
‘‘Mimi ndiye nitakuwa mwamuzi wa hilo’’
‘‘Hahahahaha hahaha unahisi unaweza kukaa miaka yote wasikupate? Watakukamata tu, kutuua sisi haimaanishi kwamba wewe utaishi’’
‘‘Aliyewapatia taarifa zangu za kuwa huku ni nani?’’
‘‘Hahaha hahaha utakufa, utakufa’’
‘‘Ni nani kawatuma na nani amewapa taarifa za mahali nilipo?’’ alimuuliza akiwa anamkwida bwana yule kwenye shingo yake lakini hakuna ambacho angekipata kwa wakati ule kwa sababu mwanaume yule alikuwa amekufa tayari. Akiwa anamkagua bwana yule ambaye alimfia wakati ambao hakuutaka yeye, simu yake ya mezani ilianza kuita kwa fujo hali ambayo ilimshtua kwa sababu haikuwa kawaida kupigiwa simu nyakati kama hizo kwa lile eneo, alitembea taratibu kuifuata simu hiyo na baada ya kuifikia aliiangalia kwa muda kidogo ndipo akaamua kuipokea akiwa hana imani.
‘‘Unatakiwa kuondoka huko uliko haraka kwa sababu kuna watu wanajua mahali ulipo na kwa sasa unatakiwa urudi Tanzania, kuna watu ambao wanatakiwa kufa akiwemo raisi’’
‘‘Wewe ni nani?’’ wakati anauliza lile swali alitambua kwamba ile simu ilikuwa imekatwa, alibaki kwenye mshangao asijue ni jambo gani ambalo alikuwa anatakiwa kulifanya kwa muda ule kwani siku yake ilikuwa imeharibika vibaya.
Ndiyo kwanza tunaufungua ukurasa wa kwanza kabisa ndani ya simulizi yetu bora sana ya KARATA YA MAUAJI…… Utamjua huyu mwanaume ni nani, kwanini alienda kuishi Mali, ni watu gani walimvamia, nani alimpigia simu na mambo mengi ambayo utajifunza humu ndani kuhusu mapenzi, siasa, udanganyifu, ujasusi, mapigano, usaliti na mambo mengine meeeengi mazuri.
Mwandishi ni mimi mwenyewe FEBIANI BABUYA……. Ungana nami mpaka mwisho wa simulizi hii bora.