Sehemu ya pili;
Maisha baada ya kumaliza kidato cha sita yalimfungua sana akili Leo.
Kipindi chote baada ya kuhitimu alikitumia kumsaidia mamake katika shughuli za uuzaji samaki maji chumvi, Biashara ambayo familia yao iliachiwa na marehemu baba yake alipofariki.
Kumsaidia mamake katika biashara hiyo kulimfanya Leo afahamu jinsi gani mamake alikuwa ni hodari katika shughuli zake hizo. Kumsaidia mamake katika shughuli hizo za uuzaji samaki wa maji chumvi katika soko kuu la mjini kwao kulimfanya aone ni jinsi gani mamake alikuwa ni mwanamke aliyejituma .
Biashara hiyo iliyokuwako katika soko kuu la mji huo wa Morogoro, ilikuwa katika duka kubwa lililokuwa na maneneo,”Kwa wapogoro Fisheries”. mlangoni mwake, duka hilo la samaki lilikuwa maarufu mji wotewote.
Akiwa dukani hapo akimsaida mamake shughuli za hapo dukani Leo alikumbuka jinsi miaka kumi iliyopita, baba yake alivyofariki katika ajali ya gari, na kutia simanzi sana familia yao, na kuwaacha Leo na dada yake wakiwa na mama yao.
Leo alikumbuka jinsi enzi hizo mama yake alijawa na hofu kama angeweza kuendesha biashara hiyo na kuwalea Leo na mdogo ake peke ake. Leo aliona ni jinsi gani mamake aliweza kusimama na kuiendesha biashara hiyo vyema kabisa, hata kufikia wakati huo akawa kaitanua na kuifanya kuwa ni biashara kubwa na yenye umaarufu kwa wakazi wengi wa mji wao, ambao walifunga safari toka kona zote zote za mji kufika hapo sokoni na kununua samaki kwenye duka hilo lao tu.
Leo alipenda sana uzoefu wa mamake wa kupatana bei na wauzaji wakubwa wa samaki wa Dar es Salaam, na jinsi alivyokuwa makini kuhifadhi mzigo wa samaki usiharibike, na mbinu zake za kibiashara kwa ujumla.
Wachuuzi wengi wadogowadogo wa samaki walinunua samaki hapo dukani kwa amake na migahawa kadha ya kuuza chakula ilipata samaki kwa kusambaziwa na duka hilo.
Hivyo moja kati ya mambo aliyokuwa akiyafanya Leo ilikuwa ni kupeleka samaki wabichi katika migahawa, iliyokuwa ikitoa oda ya mzigo dukani mwao.
Basi, moja kati ya migahawa aliyopelekea samaki ulikuwa ni mgahawa ulioitwa “Mahanjumati Restaurent”, uliokuwako katika mtaa maarufu ulioitwa Konga. Mgahawa wenyewe ulimilikiwa na mwanamama mmoja hivi. Basi, siku ya kwanza kufika mgahawani hapo, Leo alipenda sana mazingira ya mgahawa huo, alipenda usafi wa eneo hilo harufu za vyakula za mgahawani hapo hata akawa kasimama ndani ya mgahawa huo, akishangaashangaa uzuri wake wakati akisubiri malipo ya samaki alopeleka hapo, toka kwa mama mmiliki wa mgahawa huo.
Huku akiwa anaangaliaangalia uzuri wa mgahawa huo, mara akagutuliwa na sauti ya kike, sauti ya kuvutia ya kike, ikimwambia, “kaka pesa yako hii hapa”, Leo akamgeukia huyo dada aliyekuwa akimpa malipo ya kupeleka samaki dukani hapo siku hiyo.
Msichana huyo alivutia sana, hivi kwamba, macho yalimtoka Leo na kumrushia msichana huyo. Ndani ya muda mfupi tu akampitishia macho mwili mzima na kumfanyia uchambuzi yakinifu wa harakaharaka kichwani mwake.
Kabla hata hajapokea pesa alokuwa akipewa na mlibwende huyo, Leo akawa kesha toa tathmini kichwani mwake kuwa binti huyo alikuwa ni kifaa cha aina yake, Kwa haraka tu aliona uzuri wa macho ya binti huyo, macho makubwa madogo hivi ya kusinzia mithili ya macho ya mnyama mbuzi. Huku binti huyo aling’ara kwa ngozi yake ya weusi wa kupendeza, mfano wa rangi ya tunda chungwa. Mrembo huyo ambaye alikuwa kavalia tu mavazi ya kupikia katika mgahawa huo alipendeza sana, hivi kwamba. hata Leo akajiuliza harakaharaka, kuwa binti huo alionekanaje avaliapo nguo za kupendeza ikiwa ni mwenye kuvutia hata avaapo manguo ya kufanyia kazi ya kupika.
Muda huo wote Leo akiwa anafanya tathmini zake kichwani, binti wa watu alikuwa akimsubiri apokee pesa ya malipo ya samaki alowaleta, hata mtoto wa watu akawa akimshangaa Leo, na kujiuliza kijana huyo kapigwa na bumbuwazi gani hata hapokei hela yake ya samaki bali kabaki kumkodelea yeye macho.
“Samahani kaka pokea hela yako, unanisimamisha”, alilalama msichana huyo kwa sauti yake ya kuvutia na kumgutua Leo,
“hebu rudia tena, nikusikie vizuri tena”, kwa tabasamu Leo aliomba msichana huyo aongee tena ili mradi tu asikiie tena sauti ya kuvutia ya msichana huyo, ambaye sasa alianza kutia na nyodo za hasira, kumbe hivyo alivyofanya ndio kama alikuwa akizidisha uzri wa sauti yake.
“Nakwambia beba hela yako ya samaki ulo leta nashangaa unanitumbulia macho”, aliongea huyo binti huku akibinua binua midomo yake na sasa akawa mkono mmoja kashika kiuno badili ya ule mwengine aloushika hela alizokuwa akimpa Leo kama malipo ya kuleta samaki mgahawani hapo.
Lakini Leo akazidisha tabasamu lake na akafikicha macho yake kana kwamba amuone vizuri binti hiyo utadhani hakumuona vizuri hadi wakati huo.
Basi, akaipokea hela yake na kumtazama binti huyo na kumtolea maneno, “dada hongera sana, mimi nakwambia sijawahi sikia sauti nzuri kama hii ilotoka kinywani mwako”, hata binti wa watu akaogopa
“Hee we vipi, hiyo sauti yangu vipi iwe hivyo, wakaka wengine sijui mkoje”, safari hii mtoto wa watu alijikaza na kuongea kwa hasira kidogo ila Leo akawa akiyasikilizia kwa maneno yakemakali kwa kufumba macho kabisa, tena kwa hisia, hakika hakuwahi sikia sauti nzuri kama hiyo, kwa mara ya kwanza aliisikia sauti iliyoweza kumtoa nyoka pangoni. Basi huku kafumba macho yake na huku katabasamu na kumshangaza mtotot wa watu alokuwa kamsimamisha tu hapo, Leo akajiongelesha kwa kujiapiza kwa mungu eti, “hakika mungu wangu nashuhudia zile sauti za kutoa nyoka pangoni ni kweli umeziumba na wala si simulizi za kufikirika”
Kufumbua macho yake, akajikuta katupia macho yake kwenye midomo ya binti huyo, midomo minene minene ya kikike iliyovutia saaana.
“Hivi wewe ni malaika?”, Leo aliuliza, na binti wa watu akatoa macho kwa kushangaa, kichwani mwake alihisi, labda huyo mleta samaki mahala hapo siku hiyo alikuwa hayuko sawa kiakili.
Ila mara, wote wawili wakagutuliwa kwa sauti ya ukali ya mama mwenye mgahawa huo, ikitokea toka jiko la mgahawa huo,“we Zuena hebu harakisha kusafisha samaki waloletwa, unafanya nini huko”. Na binti huyo akaitikia na kugeuka haraka kumuacha Leo na matabasamu yake kasimama hapo mgahawani. Leo akabaki kamkodolea macho binti huyo ambaye alielekea mlango wa jiko la mgahawa huo,
ila mara kabla Leo hajageuka kuondoka mahala hapo alimuona binti huyo akigeuka na kumchungulia toka mlango wa huko jikoni, na wakagongana macho na kutazamana, huku Leo akimtazama kwa tabasamu na binti huyo akimtazama Leo kwa mshangao. Kisha binti huyo akatokomea humo jikoni.
Leo, akawa kama asiyejielewa akatoka mgahawani humo huku kafurahi na kutabasamu na kuelekea pikipiki yake alokuja nayo hapo na kuipanda kurejea dukani kwa mamake.
Moyoni mwake alifurahi sana kufahamu jina la binti huyo, Zuena, jina ambalo lilimkumbusha wimbo moja hivi aliousikia utotoni mwake wenye mashairi yaliyomsifu binti mrembo wa kuvutia na tabia za kupendeza aliyeitwa Zuena.
Basi ikawa siku zilizofuata Leo alipeleka tena samaki katika mgahawa huo ambao Zuena alikuwako, na kila siku alifurahia tu kumuona huyo Zuena. Na kila siku aliyopeleka samaki hapo alizidi kumuona Zuena kuwa ni binti aliyevutia na kupendeza.
Huo ukawa ndo mwanzo wa mazoea ya wao wawili. Urafiki wao ukakua zaidi, baada ya Leo kuchukua namba ya simu ya Zuena na kuanzisha mawasiliano ya simu baina yao. Wakawa ni watu wenye maongezi mareefu kwenye simu kila siku, ama kuchati na kutumiana jumbe fupifupi. Na kwa vile wote walikuwa waongeaji, hakuna aliyemchoka mwezie.
…………………
Leo hakuweka wazi uhusiano wake na Zuena, kwa watu wake wa karibu ikiwamo, Nema, binti ambae walikua wote toka wako watoto.
Lakini kila mtu aliyekuwa karibu nae alihisi kuwa Leo kabadilika, kwa maana hakuwa akionekana onekana sana mtaani na hakuwa na muda wa kupiga porojo mtaani na washkaji zake kama zamani, kumbe mwezao muda wake ulikuwa ni yeye na Zuena, Zuena na yeye.
Huyo Nema mwenyewe ambaye alikuwa akimtaka sana Leo, ila Leo hakumtaka, alikuwa na hamu sana ya kufahamu ni kipi hasa kilichokuwa kikimfanya Leo awe biiize zaidi ya kumsaidia mamake kuuza samaki, hivi kwamba alikuwa hana muda wa kuwepo mtaani kupiga stori.
Ila wala haikuchukua muda picha ikaanza kujichora yenyewe, mana mdogo wa kike wa Leo, alikuwa ni mropokaji. Siku moja Nema alikuwa akipiga stori, barazani kwao na rafiki zake, huko nyumbani kwao katika barabara moja ya mitaa ya Kwarara, mmoja wa hao rafiki zake alikuwa ni huyo mdogo wa Leo, Sanura.
Kwenye maongezi yao wakawa wakizungumzia watu wasioonekana mtaani kutokana na kuwa bize, sasa mmoja wa watu hao akatajwa Leo, na wakamzungumzia sana kuwa yuko biize haonekani. Ndipo mdogo wake akaanza kuropoka kuwa kakake lazima atakuwa yuko bize na demu fulani mjini hapo ila tu yeye hamfahamu.
Sanura akropoka zaidi kuwa Leo siku hizo alikuwa ni mtu wa kuongea kwenye simu kwa suti ya chini kwa muda mrefu, kuchati huku akicheka mwenyewe, mida mingine kuchelewa kurudi hom, mdogo wake huyo akaapia kuwa wallahi tena Leo alikuwa na kila dalili alikuwa na demu mahala ambaye alikuwa akimfanya awe biize.
Wakati huo, Nema ambaye aliwahi kufunguka kwa Leo kuwa anampenda sana akabaki akisikiliza jinsi Sanura alivyofunguka juu ya ukweli wa mambo.
Basi ikawa wazi kwake kuwa Leo alimpenda msichana mwengine mbali kabisa na yeye, kwenye moyo ilimuuma na alitaka amfahamu huyo msichana, ili tu kujua huyo msichana alikuwa na vigezo gani vya ajabu hasa hata Leo ampotezee yeye na awe na huyo msichana mwengine.
…………………
“namba unayopiga haipatikani kwa sasa tafadhali jaribu tena baadae”, hiyo ndiyo ilikuwa sauti ya ujumbe aliyopewa Leo kila alipojaribu kumpigia simu mpenzi wake mpya, Zuena, toka asubuhi ya siku hiyo, alishamtumia meseji kibao ila wala hazikujibiwa na Zuena.
Sasa hata alianza kupata wasiwasi, hiyo ilikuwa ni saa sita mchana siku hiyo ya jumapili, na haikuwa kawaida Zuena kutopatikana kwenye simu kwa muda mrefu.
Na kwa kawaida Leo alizoea siku kama hiyo ya jumapili, Zuena alikuwa free hakwenda kufanya kazi mgahawani.
Hivyo kwa vyovyote kulikuwa na jambo lilimfanya Zuena asipatikane kwenye simu, muda wote alokuwa akimtafuta toka asubuhi.
Huku akiwa anaendelea kuchezea simu yake aina ya motorola bapa ya kubofyabofya mara akashangaa mlango wa hapo sebuleni kwao ukifunguliwa na mara akamuona Nema akiingia sebuleni humo. Nema alikuwa usoni machozi yakimtiririka na akionekana mwenye uchungu mwingi sana.
Leo alipomuona Nema tu akajikuta anakunja uso. Kwa maana alifahamu nini kimemleta Nema sebuleni kwao hapo, mana toka jana ya siku hiyo Nema alikuwa haeshi kumsumbua kwenye simu, akimlalamikia Leo kwanini alikuwa na mahusiano na msichana mwengine zaidi yake yeye, wakati yeye Nema alimpenda sana,
Tena Nema alimlalamikia kwa kilio kwanini hakumwambia hapo kabla kuwa ana mahusiano na msichana mwengine hadi akaja kujua kupitia kwa watu mtaani, wakati yeye Nema alimfungukia Leo ukweli wake wote wa jinsi gani alimpenda sana.
Basi huku michozi ikimtiririka sana machoni huku akionekana kuwa na mauchungu mengi Nema akaingia sebuleni humo na kusimama katikati ya sebule hiyo huku akimtazama Leo ambaye sasa alijawa na hasira kwa kumuona Nema hapo, nae Leo akasimama basi, wakawa wakitazamana na Nema, Nema na michozi yake ya uchungu na Leo na hasira zake nyingi.
Huko kujilliza kwa Nema ndiko kulimfanya Leo akasirike hata zaidi, sasa akawa kama anataka kulia kwa hasira, na akaanza kufoka kwa hasira.
“Nema nilishakwambia sikuwahi kuwa na mahusiano na wewe, sijawahi kukutaka, wala sistahili kuona machozi yako ya uchungu kwangu, mimi sikupendi japo unanipenda, lakini dada unaanza kuwa kero, tangu jana unanitumia meseji zako za kunilaumu kwanino niko na msichana mwengine kana kwamba hivi tuna mahusiano wakati hatuna kitu kati yetu”, alifoka Leo.
Kufokewa huko kulimtoa machozi Nema hata zaidi nayo hayo machozi yakamkarahisha Leo hata zaidi,
“Leo, mimi ninakupenda sana, hata nilishakuambia ya moyoni mwangu kwako,”
Wakati huo Leo alimkata Nema bonge la jicho, yani jicho lingekuwa linauwa Nema angeanguka kufa mahala hapo, naye Nema akawa akiendelea kufunguka,
“kweli nimependa nisipopendwa”, aliongea Nema huku akijiliza zaidi, kitu kilichozidi kumtia hasira Leo hata akawa kama anataka kulia kwa hasira, basi wakawa wote kama wanalia sebuleni hapo.
“Umenionesha kwa kila hali kuwa hunipendi hata kidogo, wakati moyoni mwangu nakupenda kwa hakika”alijiliza Nema hata zaidi.
“Nimekuja hapa kukuonesha chozi langu kwa kwa mara ya mwisho, nisingeweza kuongea nawe tu kwenye simu, nimekuja hapa kukuonesha chozi langu la mara ya mwisho, ulione chozi langu labda utanifikiria Leo”,
Leo alishtuka kidogo, “Nikufirie vipi, wewe hebu toa kilio chako sebuleni kwetu nisimfikirie mpenzi wangu nimpendae kwa dhati Zuena nikufikirie wewe, unayetaka mapenzi kimabavu, mtu hakutaki we unamtaka”, alijibu Leo kwa hasira, na Nema akaangua kilio hata zaidi na Leo sasa akawa kamchoka binti huyo, ambaye walikua wote toka wako wadogo na kusoma wote na kuhitimu wote kidato cha sita hata mama zao walikuwa marafiki wakubwa., ila sasa ilionekana mapenzi yalimliza huyo mmoja wa kike tena peke ake.
“Leo, mimi nakutakia kheri katika mahusiano yako na huyo unayemuita Zuena, mimi ukweli wangu unaufahamu jinsi ninavokupenda ila kweli siwezi lazimisha penzi”, aliongea Nema na kuanza kujikaza kutotoa machozi, “Namuomba mungu nami aninyooshee nipate mtu mwengine nitakaye mpenda naye akanipenda kama nionavyo wewe umpendavyo huyo Zuena, hakika huyo Zuena ni binti mwenye bahati sana”, alimaliza kuongea Nema.
Basi, sasa Nema akawa kanyamaza na akaondoka sebuleni humo na kumuacha Leo kabaki mwenyewe sebuleni mwao katibuka akili.
Nema alipotoka tu Leo kwa hasira akauendea mlango wa sebuleni kwao na kuufunga kwa kufuli kana kwamba binti huyo asiingie tena ndani mwao.
Basi akaelekea chumbani kwake na kujitupa kitandani na kufikiria kilio alichokileta Nema sebuleni mwao na kukasirika zaidi, ndipo mara akasikia simu yake ikiita na kukata huko sebuleni, akajiinua na kurejea huko sebuleni na kuona kuwa simu yake ilikuwa na “missed call”toka kwa Zuena.
Haraka sana akampigia, na mara baa ya simu hiyo kupokelewa akasikia sauti ya kilio upande wa pili,
“Zuena vipi mbona kama una kilio mpenzi wangu, halafu mbona hupokei simu yangu mchana wote toka asubuhi?”, aliuliza Leo, na mara Zuena akajibu kuwa alikuwa kafiwa na mama yake na habari ndio alikuwa kapata asubuhi ya siku hiyo, hata simu yake akasahau kuichaji hivyo hata hakupatikana katika simu toka asubuhi.
Leo alishtuka sana na kumwambia Zuena kuwa muda huo huo atafanya haraka afike huko kwao, kisha wakakata simu. Mbiombio Leo akafunga safari kwenda huko kwa kina Zuena alikokuwa akikaa.
Zuena mwenyewe alikuwa akiishi kwa dadake mitaa fulani iliyokuwa ikiitwa mtoni Street, na hapakuwa mbali toka mitaa ya Kwarara kwa akina Leo, hivi kwamba nusu saa tu baade Leo akawa kafika huko mitaa ya mtoni na kuonana na huyo Zuena wake.
Zuena alimuambia Leo kuwa mamake aliyekuwa akiishi huko Babati, alikuwa amefariki kwa mshtuko wa moyo usiku wa kuamkia siku hiyo, na kwamba wao taarifa waliambiwa kwenye simu asubuhi ya siku hiyo. Ilikuwa ni huzuni sana, Zuena alikuwa kajawa na machozi na kulia kwa uchungu.
Basi, huo msiba ulimfanya Zuena aondoke kwenda huko Babati kwa mazishi.
Safari ya huko Babati ambayo Leo alitegemea Zuena angerejea Morogoro ilikuwa ndio kimoja, mana baada ya mazishi Zuena aliombwa na ndugu zake abakie hapo Babati kusaidia kulea wadogo zake ambao mamake aliwaacha.
Hiyo ikawa ndo changamoto ya mwanzo na mwisho ya mahusiano yao hayo ya mwezi mmoja na nusu, Zuena akawa yuko huko Babati, Leo yuko Morogoro, mapenzi yao yakabaki kuwa ya kwenye simu.
…………………
Na muda nao haukuganda kama mwezi mmoja hivi tangu Zuena kuondoka kwenda kwao Babati, matokeo ya kidato cha sita ya mwaka huo wa 2007 yakatoka.
Shule ya sekondari Eastsides ambayo Leo ndiyo alikuwa akisoma ilifanya vizuri sana mwaka huo mana wanafunzi wake wote walifaulu, wengi wakiopoa divisheni wani za pointi za juu kabisa wengine wakipata divisheni ya pili na kadhaa tu wakipata divisheni ya tatu, huku ikitia fora mji mzima wa Morogoro kwa kukosa divisheni nne hata moja, na kupiku shule kadhaa za binafsi na serikali katika ufaulu mwaka huo wa 2007.
Na kama kawaida vichwa vitatu vya hapo Eastsides sekondari, Amina, Gibson na Leo walikuwa ni vinara kila mmoja akipata daraja la kwanza kabisa na kuongoza katika manispaa na mkoa kwa ujumla.
Siku yenyewe ya kupokea hayo matokeo, wakazi wa mitaa hiyo ya Kwarara wote walijua kuwa Leo alikuwa ni miongoni mwa wanfunzi walioongoza katika mitihani hiyo ya kidato cha sita katika ngazi ya mkoa, siku hiyo mtaa mzima uliripuka kwa shangwe na kila aliyemfahamu Leo alimshangalia humo mitaani kila alipoonekana.
Ambaye hakika alifurahi kuliko wote kuwa Leo kafaulu kwa kiwango cha juu kabisa alikuwa ni mamake, bi. Sofia.
“Kila kona ya mitaa ya Kwarara nikipita najua watu wananiangalia, na kunizungumzia kwa kitu cha kujivunia, ‘ona yule anakatiza mamake Leo, yule kijana aliyeongoza mkoa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita”, mamake alimuambia Leo kwa furaha na kujivuna huku akimkumbatia mwanae na huku wote wakicheka kwa furaha.
“Haya mama ni madogo sana sasa nakwambia, ninaenda chuo kikuu, kubeba na shahada na huko naapia nitaongoza nawe utapata hata sababu nyingi zaidi za kujivunia”, Leo alimuambia mama yake kuendelea kumfurahisha,
“Utazunguka mtaani, huku ukisikia tena watu wakikuzungumzia ‘ona yule Bi. Sofia Mpogoro akipita yule ndo mama wa mwanazuoni maarufu nchini yule kijana Leo Chande’na wakimuona mdogo wangu pia watamzungumzia kuwa yeye ndiye Sanura Chande, dadake ake Leo, aliyebobea”aliendelea kumuambia mamake na wote wakawa wenye furaha humo ndani mwao.
…………………………
Mwaka huo wa 2007, Leo alibahatika kuchaguliwa kujiunga na chuo kikuu kikongwe nchini, chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Alifurahia sana kupata nafasi ya kwenda kusoma chuo hicho ambacho alisikia sana juu ya ukongwe na heshima yake alisikia mengi kuhusu chuo hicho.
Chuo chenyewe kilikuwapo huko jijini Dar es Salaam, nacho kilikuwa chuo kikubwa hasa,kilichokuwa kimejengwa katika mandhari eneo la kilima, la juu kidogo penye muinuko hata matokeo yake jina lengine maarufu la chuo hiko likawa ni Mlimani.
Chuo kilikuwa na mandhari ya kuvutia, chenye hewa na maeneo mengi ya kusomea pia miti mingi, na kutoka katika moja ya kona za mlimani hapo chuoni, mtu angeweza kuona mandhari ya majengo ya kuvutia ya Dar es Salaam kutokea kwa mbali.
Leo alifika chuoni hapo kusomea masula ya benki na usimamizi wa fedha. Kitu ambacho alikuwa na ndoto nacho kusomea toka alipokuwa kidato cha sita.
Chuo hicho kikubwa kilikuwa chenye wanafunzi wengi, toka maeneo yoteyote nchini, mabinti waliosoma chuoni hapo walivutia sana na walionekana wa kisasa.
Kila binti aliyesoma hapo alikuwa na mambo ya kizungu,kastaarabika, ana nywele ndefu na rangi ya kuvutia.
Basi huko kwenye hosteli Leo alikofikia, wanafunzi wa mwaka wa pili walikuwa haweshi kuwatisha wao wanafunzi wa mwaka wa kwanza, “ Madogo kuweni makini, UDSM kuna mengi hapa, mademu wetu wa hapa wako wa aina nyingi”, alianza kutoa vitisho, roommate mmoja wa Leo.
“Wapo, walibwende wenye hadhi kubwa na majina katu hamuwezi kuwapata wanatoka na watu wa maana, madogo mkiwatokea hao mtaumia, kuna wala bata, madogo hamna hela za kuwalisha bata hao muwaache, kuna wake za watu hao watasababisha mfe, halafu UDSM hakuna mapenzi hapa ukiwa na demu wako jua ni demu wa chama lote, washkaji zako tu wanaweza kubeba sa usiulize wadau wengine, wanapakua tu, ukipakuliwa demu wako hapa usilielie ”, roommate huyo alisababisha wezie wote wacheke.
Ndipo, mwengine akadakia, “Kuna mademu wengine wana moto, wanavutia, wana akili, wana tokea kwenye pesa na kila kidume hakika angetamani kuwa na mademu kama hao,”chumba kizima kilimgeukia huyo jamaa aliyeongea maneno hayo hapo kitandani mwake alipolala nae akawageukia, na kuendelea kuongea,
“Demu kama Sunaina, ndio kwanza kaingia chuo mwaka huu lakini ni kama vile chuo chote tunamjua, demu huyo ni pini,mtoto kaumbika, kila pande anasifiwa, halafu toto nasikia kichwa noma na pesa hashangai kwao zimejaa”
Basi kila mmoja aliyelala chumba hicho, Leo akiwa mmojawapo alipata hamu hasa ya kumuona huyo asiwaye Sunaina.
……………………
Sunaina mwenyewe alikuwa ni habari nyengine, alikuwa ni binti toka familia ya kitajiri. Aliyevutia sana, japo hapo chuoni alikuwa ndo kwanza kajiunga first year alikuwa tayari kashakuwa maarufu kutokana na ukweli kuwa yeye alikuwa na marafiki wenye majina makubwa makubwa kama vile waigizaji maarufu na wanamziki, pia aliwahi kuonekana katika video ya mwanamziki machachari wa enzi hizo aliyeitwa Jeey Master, na moja kati ya rafiki zke alikuwa ni Wema Wolper ambaye aliwahi kushiriki shindano la ulibwende la taifa, na kuibuka kuwa Miss Tanzania namba mbili mwaka wa 2006.
Sunaina pia alikuwa ni binti mwenye akili sana na aliyesomea katika shule internationale, kama vile Feza girls, pia alisoma sana nje ya nchi, ambapo alisomea nchini uingereza ambako baadhi ya ndugu zake walikuwa wakiishi.
Na ilisemekana chanzo cha kuamua kusomea chuo cha UDSM, ilikuwa ni kukataa kwake kusoma nje ya nchi kwa kuwa alichoka kuzunguka ughaibuni, kitu kilichokuwa tofauti kabisa na watoto wengi wa kitanzania ambao hupendelea kusoma ughaibuni pale uwezo wa familia zao unaporuhusu, yeye ulaya alipachoka hakutaka kusomea huko.
Na tena kutokana na uzuri wake Sunaina aliitwa a.k.a nyingi sana ikiwamo,‘toto Suna’, pia kutokana na rangi yake ya chungwa watu walipenda kumuita ‘orange Suna’, huku mashoga zake walimuita ‘shostito Suu’, huku jina mbadala alilovuma nalo saana lilikuwa ni ‘Miss California’hii ilitokana na ukweli kuwa aliishi mtaa wa matajiri ulioitwa California ambao ulikuwako huko mitaa ya fahari kubwa jijini Dar es Salaam, mitaa ya Oysterbay.
Ila mwenyewe hasa alipenda kuitwa jina lake halisi la Sunaina, na alipenda zaidi kujidhihirisha uwezo wake wa akili kuliko urembo wake, ila tu kwa majaaliwa yake mungu, uzuri wake uling’ara hivi kwamba hangeweza kujizuia watu kumuita majina mengine ya kumuadmire.
Kwanza hapo chuoni alikuwa na jopo lake lake la marafiki wawili ambao muda woote walikuwa wamemzunguka na kumfuata kwa nyuma, alikuwa ndio role model wao, kiongozi kundi lao na ndo staa wao.
Basi bwana, kwa misifa yoote ya Sunaina hakika hakuna mtu ambaye angeweza kuacha kuwa ‘amaized’na binti huyo, hata Leo nae hakujizuia akafuatilia sana habari za binti huyo.
Na siku aliyomuona hakika akakiri moyoni mwake kuwa sifa zimuendee mwenyezi mungu mwingi wa rehema kwa kuijaza dunia kwa kheri nyingi nyingi ikiwamo kheri ya dunia kuwa na kifaa kama huyo Sunaina. Mana haikuwahi tokea, yeye Leo kuona binti mrembo kama Sunaina.
……………………….
Basi bwana, Siku moja Leo alikuwa kenda kufuata kitambulisho chake cha chuo. Basi alisimama kwa muda mrefu katika foleni ili apate kitambulisho hadi akawa akifikia fikia dirisha la mgawa vitambulisho hivyo vya chuo, huku akishukuru kuwa hatimaye kafikia karibu na kupata hicho kitambulisho.
Ila mara mrembo Sunaina nae akafika eneo hilo kufuata kitambulisho chake, na akakuta foleni kuubwa, basi akaitazamaa hiyo foleni na kuona jinsi ilivyo ndefu.
Woote waliokuwa kwenye foleni hiyo walikuwa ni boys na wasichana wachache, na wote walipogundua Sunaina kafika hapo wakamgeukia kumtazama na kumfurahia kama vile waliopigwa bumbuwazi.
Basi Sunaina kuona watu wote wanamchekeachekea akawasogelea karibu na kujilizaliza kikike, “jamani guys, nachelewa kipindi naombeni mnisaidie, guys, nichukue kitambulisho changu please guys, just once”, alilalama mtoto wa kike hapoo nayo majitu katika foleni kama yamechanganyikiwa wakamruhusu awaruke woote akaenda mbele kabisa pale dirishani kuchukua kitambulisho chake.
Leo hakuamini, haikumuingia akilini, yani muda wooote alopoteza kusubiria foleni apate kitambulisho halafu anatokea mtoto wa mtu kisa eti ana shavu zuri kama dodo bivu akubaliwe tu kuiruka foleni,
Basi na yeye Leo akaona haiwezekani akaenda moja kwa moja dirishani pembeni kabisa ya Sunaina na kudai pia apewe kitambulisho, mara kundi la watu wote waliokuwa katika foleni wakamjia juu, akwende zake pale mbele arudi kwenye foleni yake, Leo hakuelewa akapayuka, “mbona huyu Sunaina mna mruhusu kuruka foleni, kwani ana nini kimstahilicho sana kuruka foleni?”, aliuliza Leo, mara wezie wakaanza kumrushia karatasi, “acha ufala toka hapo”, “kaa foleni mbuzi we”, walio kwenye foleni walimtusi na kumzomea hadi akarudi kwenye foleni yake.
Naye Sunaina alipomaliza kuchukua kitambulisho chake dirishani akapita karibu na Leo na kumtizama huku akimtabasamia kisha akarusha nywele zake ndefu za wigi na kuziweka mgongoni, kisha akaaga watu walioko kwenye foleni na kuwashukuru na kusepa. Leo hakuamini kabisa kilichotokea, aliona ni ubaguzi wa hali ya juu.
Ila kilichotokea kilimfanya aone Sunaina alikuwa ni demu matawi kiasi gani, hii ikamtia shauku kumjua Sunaina kiundani zaidi
, basi wala haikumchukua muda akamuelewa vizuri.
Mana, Leo alipoingia chuoni hapo alikuwa na lengo la kujiunga na kundi la vijana lililojiita , National Youth For Change Alliance (NYCA), kundi ambalo Leo alishauriwa ajiunge na mfanyabiashara maarufu aliyehudhuria mahafali yao, kwa kile mfanyabiashara huyo aliona kuwa Leo alistahili kuwa katika umoja kama huo ili kuendeleza uelewa wake wa mambo mbalimbali.
Basi siku ya kwanza tu kwa Leo kuhudhuria kikao cha kundi hilo la wana NYCA, Sunaina naye alikuwapo huko, tena akawa kapewa kiti cha mbele, Leo alistaajabu sana juu ya hadhi zote kubwakubwa anazopewa binti huyo, aliona watu wanamnyenyekea sana binti huyo, eti kisa mzuri na ana jina lenye kaumaarufu.
Basi katika kikao hicho Sunaina alisimama kuongea kama mwanamemba wa kundi hilo la NYCA na kwamba yeye alikuwa ni mwanachama wa NYCA toka zamani, na akajitambulisha kwamajina yake kuwa aliitwa Sunaina Habib Nasri, kisha watu wakampigia makofi naye akakaa chini.
Leo mara moja akagundua kitu, kumbe Sunaina ni binti ake na Mzee Habib Nasri, mzee mfanyabiashara maarufu wa maduka makubwa ya Habib malls. Na mmliki wa mashamba ya miwa na matunda. Mzee ambaye ndiye alidhamini zawadi ya mwanafunzi bora shuleni mwao, zawadi ambayo yeye Leo aliishindania ila hakuipata.
Leo akabaki akimtazama Sunaina aliyekaa meza kuu alimtazama kwa makini binti huyo. Ila akajikuta alitabasamu kwa maana ilikuwa ndio kwa mara ya kwanza kwake kukutana na msichana wa aina ya Sunaina, alifurahia sasa kuonana na mtu wa aina hiyo chuoni, na hakika, aliona atafurahia chuo chake hicho cha UDSM, kama kutakuwepo na watu wa aina hiyo.
Itaendelea……………………….