Simulizi:The President and I(Mimi Na Rais)

The Boldly

JF-Expert Member
May 21, 2017
2,377
5,147
Imeandikwa na Lello Mmassy


UTANGULIZI
Naitwa Joseph Kaduma Ndani Ya Serikali Ya Nchi Ya STANZA Watu Hupenda Kuniita Joe.Nina Nusu Saa Tu Ya Kuamua Kati Ya Maisha Yangu,Familia Yangu Na Utajiri Wangu Ama Uhai Wa Rais. Rais Anaeongoza Zaidi Ya Watu Milioni 70,Mwenye Ulinzi Zaidi Ya Ma Rais Wengi Hapa Duniani Leo Hatma Ya Maisha Yangu Ipo Mikononi Mwake Na Yake Mikononi Mwangu.

Nimwache Animalize Au Nimmalize Nibaki Salama?.Siwezi Kurudia Kosa Nililolitenda Hapo Kabla.Ni Ama Mimi Ama Rais.

Inaendelea..
**************************
 
SEHEMU YA KWANZA

WITO WA RAIS
“Baba kuna wageni wanakuulizia”, Derick kijana wa kwanza wa Joseph alimwita baba yake aliekuwa bustanini akiweka mbolea kwenye mashina ya migomba nyuma ya nyumba yake.

“Kina nani Derick, mbona sina miadi na mtu leo?”, Joseph alimuuliza Derick huku akiendelea na shughuli na asionyeshe shauku ya taarifa ya wageni aliyopewa na mtoto wake.

“Sijawajua ila wamekuja na magari yenye namba za blue na hazieleweki”, Derick alimjibu Joseph. “Ok, tell them I am coming” (Sawa waambie nakuja), Joseph alimjibu kijana wake. Joseph alimalizia kuweka mbolea kwenye shina moja kisha akaelekea ndani kuonana na wageni.Kwa namna Derick alivyomwelezea baba yake juu ya wale wageni tayari Joseph alishawatambua ni kina nani.

“Meshack habari”, Joseph alimsalimia kiongozi wa msafara aliekuwa amesimama kibarazani. “Joe, habari mkuu?, Mh. Rais anakuhitaji sasa hivi lipo jambo anataka kuongea na wewe”, Meshack alimwambia Joseph huku akiwa ameweka tabasamu la bandia na akimkazia macho usoni huku amemshika mkono wa salamu.

Joseph alibaki kimya kwa dakika kadhaa huku akiwatupia macho maafisa wengine watatu wa idara ya usalama wa taifa waliokuwa wameambatana na Meshack. “Rais ana shida gani nami Meshack?, Nilishatoka huko, alishanifukuza kwa aibu na fedheha kubwa baada ya kulitumikia taifa kwa moyo mkunjufu kwa miaka yangu 15 ya utumishi. Ameninyanyasa vya kutosha, amenifilisi na sasa nina kesi ya uhujumu uchumi. Leo amenikumbuka? Namba yangu anayo angeweza kunipigia simu.” Joe alimjibu Meshack huku akiwa amemkazia macho.

Alikuwa akiongea kama mtu aliekuwa na uchungu mwingi moyoni. Machozi yalikuwa yakimlengalenga. Meshack alimwangalia Joe kisha “Joe, please accept his excellency’s call” (Joe, tafadhali kubali huu wito wa muheshimiwa). Meshack alimsihi Joe kwa sauti ya upole.

“Sawa naomba mmwambie nitafika Ikulu kesho saa nne asubuhi” Joe alimjibu Meshack na kisha waliagana wakaondoka.

Joe aliingia ndani na kumkuta kijana wake mkubwa Derick na mke wake wakiwa sebuleni kimya kama watu waliokuwa wakisubiri taarifa fulani. Alipoingia tu mke wake alimuuliza kulikoni, Joe alimweleza mke wake juu ya ule wito. “Joe, usikubali kuingia tena kwenye mtego huu. Mtu huyu ameshatunyanyasa vya kutosha. Tii wito wake lakini tafadhali usikubali kufanya nae kazi”, mke wake Joe alimsihi mumewe.

*********************************
Joseph Kaduma mwanadiplomasia mbobevu, balozi mstaafu wa Stanza nchini Urusi na mbobevu kwenye idara ya usalama wa taifa la Stanza ndio huyu leo anahitajika na Rais. Joseph ambae hujulikana kama Joe ni muhanga wa utawala dhalimu wa Rais Sylvester Costa, Rais aliepo madarakani kwa muhula wa tatu baada ya kuibadili katiba ili imruhusu kufanya hivyo.

Ni balozi pekee aliefukuzwa kazi na Rais Costa na kufutiwa hadhi ya ubalozi mara baada ya kupingana nae mara tu Rais Costa alipoanzisha vuguvugu la kutaka kubadili katiba ili aendelee kubaki madarakani. Joe hakumuunga mkono, hivyo mara tu baada ya Rais Costa kushinda uchaguzi uliojawa na utata mwingi alimteua ubalozi na baada ya miezi mitatu alimrudisha nchini Stanza kumvua ubalozi na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi akihusishwa na ununuzi uliokiuka taratibu wa jengo jipya la ubalozi kule Urusi.

Joe kwa wakati huo alishafilisiwa mali zake nyingi na nyingine nyingi kuwekwa chini ya uangalizi wa serikali huku yeye akiendelea na kesi. Watoto wake wawili waliokuwa wakisoma nchini Sweden walirudishwa nchini na yeye na familia yake wote walinyang’anywa haki ya kusafiri nje ya nchi.
Lakini wakati hayo yakimkuta ni Joseph huyu huyu kwa kutumia ujuzi wake katika masuala ya diplomasia na ushawishi aliwezesha ujenzi wa Chuo kikuu cha Kilimo nchini Stanza ambacho kinaongoza kwa bara la Africa na kilichosababisha mapinduzi makubwa ya kilimo nchini Stanza.

Ni yeye aliesababisha ujenzi wa Bandari kubwa ya kisasa inayoliingizia taifa la Stanza robo ya GDP hivyo kuifanya chanzo cha mapato namba mbili baada ya kilimo. Bandari hii ilijengwa kwa msaada wa China, Urusi na India.

Ni yeye aliesababisha Stanza kukubaliwa kuwa mwanachama mwalikwa wa umoja wa kiuchumi wa BRICS (Brazil, Russia, India, China na Afrika ya Kusini) .

Joe kama wengi serikalini walivyozoea kumwita alishiriki kwenye suluhisho la amani la Sudani ya Kusini. Isitoshe ni yeye alihusika sana kwenye kuweka mikakati iliyomwingiza Rais Sylvester Costa madarakani awamu ya kwanza na ya pili. Hakuna alieamini kama ni huyu Joe angekuja kugeukwa na Rais Costa na kuwekwa kwenye mateso makubwa na kurudishwa kwenye umaskini.
Joe alikuwa ni mbobevu wa mambo ya usalama. Hata Rais Costa alipotaka kupinduliwa na jeshi katika mwaka wa tatu wa utawala wake wa awamu ya pili ni yeye akishirikiana na mbobevu mwenzake Stanley Macha (ambae kwa sasa ndio mkuu wa Idara ya Usala wa Taifa) walihusika sana kurudisha hali ya usalama wa nchi katika hali ya kawaida na kulituliza jeshi.Ueledi na uzalendo wa Joe kwa taifa la Stanza haukupaswa kuhojiwa.

Joe alioana na Eliza mwaka 1995, mkewe Eliza akiwa mtaalam na mbobevu katika sekta ya mabenki alifanikiwa kujijenga sana kibiashara pia. Eliza akiwa mmiliki wa makampuni matatu moja ya uzalishaji bidhaa za mabomba ya plastiki na nyingine ya uchakataji madini na moja ya usafirishaji bidhaa za kilimo nje ya nchi aliingia kwenye rekodi za kuwa kati ya wanawake 10 wenye nguvu katika taifa la Stanza.

Mara baada ya Rais Costa kupishana na Joe kampuni zote zilifilisiwa na kutaifishwa. Joe alirudishwa kwenye umaskini ulioambatana na mateso ya kutofanya lolote la maendeleo. Alibaki kama mpweke na mtu mwenye uchungu mwingi asijue ni kwa nini Rais Costa ameamua kumfanyia yote hayo kwa yeye kuonyesha msimamo wake juu ya demokrasia.

Alijiuliza sana kama Rais Costa hakupenda msimamo wake ilikuwa ni suala la yeye kutomteua tena ubalozi na kumwacha aendelee na Maisha yake hakukuwa na haja ya kumfanyia yote hayo anayomfanyia. Joe, alikuwa akiishi kwa uchungu mwingi.

************************
Ilikuwa ni asubuhi tulivu sana kwenye viunga vya Ikulu ya Stanza iliyojengwa mwambaoni mwa bahari ya Hindi. “Ndg. Joseph karibu sana. This way Sir…”, Meshack alimkaribisha Joseph aliewasili ikulu kuitikia wito wa Rais Costa.

Alimwelekeza kuelekea chumba ambacho ndipo Rais anakuja kuongea nae. “Habibu anaendeleaje” Joseph alimuuliza Meshack wakiwa wanatembea kuelekea kwenye chumba cha mkutano. “Yupo vizuri sana, hana matata”, Meshack alijibu huku akicheka.

Habibu ni mmoja wa vijana matunda ya Joseph katika wigo wa diplomasia. Sasa Habibu ni balozi nchini India. Ni mmoja wa vijana ambao Joe anamkubali sana. “Habibu is genius” (Habibu ana akili sana), Joe alimjibu Meshack .“Sure” (Hakika), Meshack alijibu huku akimkaribisha Joe aketi na kumsubiri Rais.
“My friend Joseph Kaduma welcome home” (Rafiki yangu Joseph kaduma karibu nyumbani), Rais Sylvester Costa aliingia kwenye kile chumba ambacho Joe alikuwa akimsubiri huku akicheka na kumsalimia Joe kwa sauti kubwa. Alimkaribia Joe na kumpa mkono.

“Mh. Rais”, Joe alinyanyuka na kumpa mkono wa salamu Rais Costa.

“Unaendeleaje, kesi inatajwa lini tena?” Rais Costa alimwambia Joe huku akiketi kwenye kiti.

“Siku utakayosema itajwe itatajwa” Joe alimjibu Rais Costa kwa ghadhabu kidogo huku akiketi.

“Give us space gentlemen and Meshack switch them off” (Vijana tupeni nafasi kidogo na wewe Meshack zizime) Rais Costa aliwaamrisha walinzi wawili walioambatana nae watoke nje ya chumba ili azungumze na Joe na kumwambia Meshack azime vifaa vyote vinavyorekodi sauti kwenye kile chumba.
“Joe, sahau yanayoendelea sasa kwenye familia yako Taifa linakuhitaji hasa mimi ninakuhitaji. Lipo jambo ninataka unisaidie nimejaribu watu wangu wote limekwama umebaki wewe” .Rais Costa alianza kuongea na Joe huku akimmimina Joe kahawa iliyokuwa kwenye meza kati kati yao.

Joe akiwa amekaa kwa utulivu huku akimwangalia Rais Costa kwa macho yaliyojaa uchungu mkubwa alinyanyuka na kukaa vizuri kisha “Sylvester, sidhani kama nina la kukusaidia ama kulisaidia taifa hili mara baada ya yote niliyokwisha kufanya na kuishia kuishi maisha ninayoishi sasa. Bila kusikia hata unachotaka nikusaidie naomba niseme wazi sitaweza”. Joe alimwambia Rais Costa kwa kumwita kwa jina.

Alikuwa akiongea kwa ghadhabu na kwa wakati ule alisahau kama Costa ni Rais bali alimwona kama mtu wa kawaida, mporaji, mnyanyasaji na asiestahili hadhi ya Urais. Hakuwa na chochote cha kupoteza zaidi ya alivyopoteza, alishapoteza kila kitu na labda kilichobaki ni yeye kupewa hukumu ya kuishia jela.

“Joe, naweza kufuta kesi zako zote na kurudisha hadhi yako na heshima yako na vyote ulivyopoteza kwa kunisaidia hili suala langu” Rais Costa alimwambia Joe huku akikunja nne kwenye lile kochi alilokuwa amekalia.

“Tofauti zetu tunahitaji tuzimalize leo na tuangalie mbele” Rais Costa alimalizia. Joe alimwangalia Rais Costa kwa macho yaliyojaa wekundu uliosababishwa na machozi. Aliwaza na kupata uhakika kuwa yote yaliyomtokea ni kwa sababu Rais Costa aliamua iwe hivyo.

Aliwaza jinsi hali ile ilivyomsababishia matatizo ya kisukari na presha ya kushuka. Aliwaza jinsi alivyonyimwa kumsafirisha mama yake kwenda matibabu India kwa sababu ya amri ya Rais Costa ya kutoruhusu mtu yeyote wa familia ya Joe kutoka nje ya nchi na hivyo mama yake kufariki dunia. Joe alipatwa hasira sana.

*********************
“With all due respect Mr. president there is nothing to resolve between me and you. I can’t help” (Kwa heshima mheshimiwa Rais hakuna kitu cha kutatuliwa kati yetu. Siwezi kusaidia). Joe alimjibu Rais Costa huku machozi yakiwa yamechirizika mashavuni huku akinyanyuka kwenye lile kochi alilokalia tayari kwa kuondoka.

“Bahati Mbaya sana huwezi kutoka humu ndani mpaka tumeelewana na kukubaliana. Utakapokuwa tayari kuongea na mimi mwambie Meshack aniite” .Rais Costa alimjibu Joe huku akitoka kwenye kile chumba.

Wakati Rais Costa amefika mlangoni haraka Joe akamsimamisha “Unataka nifanye nini?” Joe alimuuliza Rais Costa.

“Nataka nikutume Korea Kaskazini”

“Nini!!”

“Ndiyo” Joe na Rais Costa walijibizana. Wote walirudi kwenye makochi na kukaa.
Joseph alikuwa tayari kumsikiliza Rais Costa, hakuona sababu ya kuendelea kupambana nae alikumbuka mafundisho waliyopewa wakiwa mafunzo ya usalama wa taifa nchini Israel kuwa unaweza kupambana na mtu yeyote lakini si aliekalia kiti cha u Rais, kupambana nae ni kujiumiza mwenyewe. Alikuwa mpole na kuwa tayari kumsikiliza.

“Joe, nashukuru sasa tunaweza kuongea” Rais Costa alimwambia Joseph huku akiketi. “Nakusikiliza” Joe alijibu.

“Ninahitaji nikutume Korea ya Kaskazini” Rais Costa alianza maongezi. Joe alibaki kimya akimsikiliza kisha “Mkuu kutokana na makubaliano ya umoja wa mataifa tulisaini wenyewe kutoshirikiana na taifa hili suala unalotaka kufanya litatuletea vikwazo na nchi nyingine. Lakini kwanza nijue ninahitajika kwenda kufanya nini” Joe alishauri na kuuliza.

“Joe ninaelewa ndio maana nilitaka kutafuta mtu mahiri katika hili na hii inakuwa ni misheni nyeti na yenye usiri mkubwa. Kwa hali ilivyo tunamuhitaji Korea Kaskazini kama mshirika.

Ninajua tuna historia na taifa hili lakini ushirikiano wetu umeyumba sana hasa baada ya kuzifutia usajili zile hospitali zao tatu walizozifunguaga hapa nchini. Ulikuwa ni uamuzi uliokosa busara lakini wenye umuhimu kwa wakati ule.

Kwa sasa ninahitaji kuimarisha jeshi na vifaa vya vita ikiwepo rada. Ninahitaji mfumo mpya wa mawasiliano wa Ikulu na idara ya usalama wa taifa kwani tupo kwenye hatari kubwa sasa hivi hasa baada ya kukataa kuunga mkono baadhi ya sera za nchi za Magharibi hasa Ushoga.

Unajua pia badiliko la katiba nililolifanya lililoniruhusu kugombea tena halikuwafurahisha. Usisahau tumepingwa sana kwenye huu mradi wa ufuaji madini ya Uranium mradi ambao mimi naona unatija kwetu.

Lakini pia tulipowabana hawa wawekezaji wa sekta ya gesi tumejiongezea maadui sana, sijioni kuwa salama hata kidogo tunahitaji kupanua wigo wa marafiki.

Mifumo yetu ya mawasiliano tunayotumia sasa ni ya kwao, jeshi letu silioni kutosha kupambana na aina za uvamizi wa kisasa. Nahitaji Korea ya kaskazini sasa kuliko kawaida”. Rais Costa alimweleza Joe kwa kituo. Joe alionekana kutulia akisikiliza na kisha alivuta pumzi kwa nguvu.
“Mheshimiwa Rais nadhani bado tuna nafasi kubwa ya kuwatumia China, Urusi na Japan kufanikisha yote hayo uliyosema. China wana mifumo mizuri ya mawasiliano. Urusi na Japan tunaweza kuwatumia kwenye kuimarisha jeshi na kama una shaka na Israel kwa mafunzo ya kiusalama Urusi wanaweza kutusaidia hata Cuba.

Tukiwatumia hawa hatutaleta hamaki kama tukiwatumia Korea Kaskazini.Hawa tuna mashirikiano nao mazuri sana na wapo kwenye ushindani wa kawaida na hayo mataifa mengine. Nina uzoefu nao kuliko huko Korea. Na hawa hawana shurti ya kufuata sera zao kama wa magharibi isipokuwa tu wataangalia watafaidika vipi. Nilikuwa nashauri tuwatumie hawa”. Joe alishauri.
“Hapana. Hivi karibuni mahusiano yangu na Rais wa China sio mazuri hasa baada ya kumkatalia raia wake zaidi ya laki moja waliotaka kuingia nchini kufanya biashara ndogo ndogo.

Sikukubali maana hawa machinga wangu ningewapeleka wapi niliahidi kuwainua kiuchumi sasa haiwezekani mpaka machinga niwaletee wachina, nilikataa.

Urusi nae anataka amiliki asilimia 80 ya fedha zitakazotokana na uchimbaji wa mafuta kule jimbo la Kindori na sisi tubakiwe na 20%, hilo nimekataa pia na inaonekana Vijisky hajafurahia ndio maana naona kwa sasa tuende na Korea Kaskazini”, Rais Costa alimjibu Joe.

“Lakini mheshimwa nadhani kutokukubaliana ni Sehemu ya mazungumzo na tuna nafasi ya kurudi tena mezani kuzungumza na kufikia muafaka wa sisi wote kufaidika kuliko kuwaacha na kuhamia Korea, twajuaje kama huko nako hatutakubaliana?.

China mfano, badala ya kumkatalia ungempa nafasi ya yeye kutujengea soko kubwa la kisasa la matunda na mazao halafu umwambie unampa 60% ya umiliki na watu wake wakati 40% ichukuliwe na sisi na vijana wetu. Hapa tungekuwa tumeinua uchumi wa wakulima wa matunda na mazao lakini pia ajira na soko la nje.

Urusi suala la mafuta pia linajadilika, lakini vipi Japan, India na Cuba?”. Joe alionekana kuzidi kusisitiza kutoungana na Korea Kaskazini.

“Joe nimekuita hapa unisaidie kufanya ninalokuomba na sio kunishauri. Siku nikihitaji ushauri nitakwambia unishauri, kwa sasa nahitaji unisaidie maongezi na Korea.” Rais Costa alionekana kukerwa na ushauri wa Joe.

Joseph alikaa kimya kwa dakika chache kisha “Sawa nitafanya kama utakavyoona inafaa lakini kwanza nijue nitapata nini kwa kulifanya hili” Joe alitaka kujua.
“Kwanza kesi yako itafutwa. Nitatoa maagizo vikwazo vyote vilivyowekwa dhidi yako viondolewe. Biashara zote za mke wako na mali zilizoshikiliwa na serikali utarudishiwa.

Mke wako nitamtafutia nafasi benki kuu na Watoto wako watasoma nchi utakayoipendekeza. Joe sidhani kama kuna lingine nimelibakiza” .Rais Costa alimalizia huku akimwangalia Joe usoni. Joseph alihema kwa nguvu kisha alimshukuru Rais.

“Nadhani Joe tusahau yaliyopita na tusaidiane kuijenga nchi. Utaniambia unahitaji nini ndani ya siku tatu ili tuanze mikakati ya namna ya kulienenda hili suala. Thank you for coming my old friend”. Rais Costa alimalizia kuongea huku akifungua mlango na kutoka huku akisindikizwa na wasaidizi wake waliokuwa wakimsubiri.

Joe alibaki pale kwenye kochi akiwa ameinamisha kichwa chini. Alikumbuka maneno ya mke wake kuwa asikubali atakachoombwa na Rais na alikuwa hajui atakwenda kumweleza vipi Eliza. Alijipa moyo na kusimama.
Haraka Meshack akiwa ameambatana na kijana mwingine mmoja walikuja kumwomba watoke na kwa mshangao Joe alipotoka nje alielekezwa aingine kwenye Land Cruiser V8 toleo jipya. Hakuelewa kinachoendelea.

Alikuwa akiwaza sana nini maana ya hayo yote, kuwa Rais Costa anamuhitaji kwa ajili ya hayo tu? kuimarisha jeshi na mfumo wa mawasiliano? Kuwa ni hilo tu?hakuelewa. Wakati akiwaza hilo alijikuta tayari yupo mbele ya nyumba yake na kumkuta mkewe Eliza na Watoto wake wawili wakiwa nje huku vijana zaidi ya watano wakiwa wanatoa mabegi ya nguo nje huku askari zaidi ya sita wakiwa wameizunguka nyumba.

“Mheshimiwa karibu, tunahitaji kuwahamisha kwa maelekezo ya Rais. Tunaelekea nyumba uliyopangiwa Endokasi Estate”. Meshack alimwambia Joe.

Endokasi Estate ni mahali penye nyumba za serikali ni eneo analoishi Waziri mkuu na Spika wa bunge. Joe na familia yake walikuwa wanahamia huko. Joe alikuta pia Land Cruiser ingine ikiwa pale aliyoambiwa ile ni ya mke wake.

Eliza alipomuona Joe alimfuata na kumuuliza kwa upole “Nini kinaendelea mume wangu?”. Joe kwa utaratibu alimjibu mke wake kuwa atamweleza baadae ila Rais amemtuma kazi.

“Joe, umekuwa mume wangu kwa miaka 23 sasa sikuwahi kuacha kukubaliana nawe katika maamuzi yako. Tumepoteza vingi kwa sababu ya Rais huyu dhalimu. Tumempoteza mama, tumejichumia magonjwa tumeishi kwa dhihaka kubwa leo unaniambia Rais amekutuma?” Eliza alianza kumrushia Joe maswali mfululizo.

“Eliza tutazungumza utaelewa” Joe alimsihi Eliza.

“Hapana Joe ninasikitika kukwambia kuwa nimemwita mwanasheria, ninafungua jalada la talaka. Mimi si mke wako tena. Utaishi na Rais Costa” Eliza alimwambia Joe huku akiondoka kuelekea ndani ya nyumba. Joe alisimama pale asijue afanye nini.
************************
Nini kitaendela katika simulizi hii ambayo ndio kwanza inaanza?.Anza kufuatana nami sasa katika mtiririko huu mzima wa kisasi,ghiliba,Kushinda na Kushindwa
 
SEHEMU YA PILI

RAIS COSTA ATIKISA MUHIMILI WA MAHAKAMA.JOE AFUTIWA MASHTAKA
“Sizya wataarifu Jaji Mkuu, Mwendesha Mashtaka wa Serikali na Mwanasheria Mkuu kuwa nitawahitaji kesho saa tatu asubuhi. Waziri wa Fedha na Msajili Mkuu wa Hazina nitakuwa na kikao nao kuanzia saa saba mchana na kisha nitataka kukutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Viwanda na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa jioni saa kumi”, Rais Costa akiwa ofisini kwake alitoa maagizo kwa msaidizi wake bwana Sizya Kagonda. Nae alitii.
Siku iliyofuata saa tatu kamili, Rais Costa aliingia kwenye chumba cha mkutano ili kukutana na Mwanasheria mkuu, Jaji mkuu na Mwendesha Mashtaka waSerikali. Aliwaeleza nia yake ya kutaka mashtaka yanayomkabili Joseph Kaduma yafutwe na hivyo alitaka ushauri namna ya kulitekeleza jambo hilo mara moja.
“Mheshimiwa Rais, kutokana na mwenendo wa kesi ilionekana kuna matumizi mabaya ya ofisi yaliyofanywa na Joe kuifuta kesi hii itatuweka kwenye wakati mgumu kwenye kesi nyingine mbili za uhujumu uchumi zinazoendelea sasa”, Jaji mkuu Dr. Charles Kaseja alishauri. Alishauri kuwa ni vyema kesi ikaachwa iishe halafu Joe apewe nafasi ya kukata rufaa halafu ndio ikamalizikie kwenye rufaa lakini alitoa angalizo kuwa itachukua muda kidogo tofauti na ombi la Rais.
“Kaseja kuna Ushahidi gani uliopata? Huna Ushahidi wewe zaidi ya huu mwendesha mashtaka anaojitahidi kuutengeneza. Joe hana kosa, kila jambo niliagiza mimi. Ninahitaji hii kesi isitishwe haraka iwezekanavyo”, Rais Costa alisisitiza.
“Mheshimiwa Rais, mahakama na utaratibu wa sheria hauendi hivyo, ni vyema tungeheshimu misingi ili kutopoteza imani ya wananchi na muhimili huu”, Dr. Kaseja alisisitiza kwa nidhamu kubwa. “Yeyote mwenye kuwaza sawa na Dr. Kaseja aseme”, Rais alihoji na mwanasheria mkuu pamoja na mwendesha mashtaka wa serikali walibaki kimya, hakuna aliyethubutu kumuunga mkono Jaji Mkuu kwasababu kumuunga mkono Dr. Kaseja ni kusema unapingana na Rais. Rais Costa aliwashukuru na kuwaruhusu waondoke.
Kama ilivyopangwa, saa saba kamili Rais Costa alikutana na Waziri wa Fedha na Msajili Mkuu wa Hazina. Aliwapa maelekezo kuwa mali za Joseph zilizotaifishwa zirudishwe mara tu kesi yake itakapofutwa. Pia, alimpa maelekezo Waziri wa Fedha kuwa Eliza, mke wa Joe aanze kutafutiwa nafasi Benki Kuu, cheo cha Mkurugenzi.
Waziri wa Fedha alishauri kwa kuwa nafasi ya mkurugenzi wa Benki ya Kilimo ipo wazi, ni vyema Eliza akapewa nafasi hiyo kuliko kupelekwa Benki Kuu kwani ana uzoefu na biashara za kilimo hasa usafirishaji wa mazao ya Korosho, Pamba na Kahawa. Kikao cha Rais na Waziri wa Fedha hakikuwa na changamoto nyingi.
Rais Costa ni mtu wa kwenda na muda. Ilipotimia jioni saa kumi na mbili, alikutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Viwanda na wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kama ilivyopangwa kwenye ratiba. Alitoa maagizo kuwa vikwazo vyote alivyowekewa Joseph vitolewe, pia alimuagiza Waziri aangalie namna ya kuanza kuviwezesha na kuvirudisha kwenye uendeshwaji viwanda vyote alivyokuwa anaendesha Eliza. Maagizo ya Rais Costa yaliafikiwa bila kuhojiwa.
Rais alimaliza siku kwa mafanikio kwa kuonana na watu wote wanaohusika katika kutekeleza yale waliyoafikiana na Joseph isipokuwa yote yangeweza kuendelea kama tu mahakama itatoa hukumu kuwa Joe hakuhusika na uhujumu uchumi na hivyo kufutiwa mashitaka jambo ambalo Jaji Mkuu alipingana na Rais Costa na lilionekana kutofikiwa muafaka.
***************************************
“Kwa mamlaka aliyopewa Mh. Rais na katiba chini ya ibara ya 57(ii)b, leo ametengua uteuzi wa aliekuwa Jaji Mkuu Dr. Charles Kaseja na kumteua ndugu Dastan Kibwana kushika wadhifa huo. Hapo kabla, Jaji Dastan Kibwana alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa. Aliyekuwa Jaji Mkuu Dr. Charles Kaseja atapangiwa kazi nyingine”, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, ndugu Alpha Wauwau alimalizia kutangaza kwa waandishi wa habari.
Rais Costa si mtu aliyependa kupingwa mawazo yake. Suala la kazi aliyomtuma Joe alitaka lifanyike kwa kasi aliyoihitaji na hakutaka mtu yeyote atokee wa kukwamisha azma yake. Dr. Kaseja aliyekuwa Jaji Mkuu alionekana kutoelewa hilo na sasa aliondolewa kazini ili awekwe mtu ambaye angeweza kwenda na kasi ya Rais Costa.
Dastan Kibwana, Jaji wa Mahakama ya Rufaa mbobezi wa sheria za biashara za kimataifa sasa alipewa dhamana ya kuwa Jaji Mkuu kwa maelezo ya kazi yake ya kwanza iwe kuhakikisha Joe anafutiwa mashtaka.
************************************
“Shemeji naomba umuelewe mume wako. Ni kweli mmeshapoteza vingi, lakini je, mtavirudisha kwa kuzidi kupingana nae? Mimi naona ni muda wa kuvirudisha mlivyopoteza kwa sababu ukisema mnamkomoa nani ajuaye muda atakaokaa madarakani? Lakini huoni hali hii inawaumiza na watoto ambao hawahusiki na ugomvi wenu na Rais?
Nadhani mume wako amefanya uamuzi wa busara kuafiki kufanya kazi na Rais. Sahau yaliyopita, msaidieni Rais kuijenga nchi” alikuwa ni Stanley Macha, Mkurugrnzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na rafiki mkubwa wa Joe akiwa anamsihi Eliza aelewe ni kwanini Joe amekubali ombi la Rais Costa.
“Hivi shemeji kama wewe unatambua hili na kwa nafasi yako na kama kweli Joe ni rafiki yako ulishindwa nini kuongea na Costa mpaka sisi tukaingia kwenye mateso namna hii kwa muda wote huo?”, Eliza alihoji.
“Eliza, Joe anaelewa hata hili suala la Rais kumtafuta yeye ni mimi”, Stanley alijibu kwa ufupi.
Ilikuwa ni baada ya wiki moja tangu siku ya kwanza Joe kukutana na Rais ambapo hakuwa kwenye maelewano mazuri na mke wake Eliza. Joe ilibidi amwombe Rafiki yake Stanley aje amsaidie kumwelekeza mkewe.
Tayari Joe alikuwa nje ya muda wa kupeleka mkakati kwa Rais Costa kama walivyokubaliana maana alitakiwa amrudie baada ya siku tatu. Joe alimwambia Rais angerudi kwake baada ya kujihakikishia mashtaka yake kufutwa. Baada ya siku mbili tangu Stanley kuongea na Eliza alionekana kuelewa. Alitulia, na sasa alikubaliana na hali kuwa ni ngumu kupambana na Rais akiwa madarakani.
****************************************
Haikupita wiki Mahakama ilitoa hukumu ya kutomkuta Joseph Kaduma na hatia zozote za uhujumu uchumi. Wachambuzi wengi na magazeti ya uchambuzi waliweka mijadala kila mahali kuelezea hatua hiyo wakichambua hatua ile kuwa na msigano wa kimaslahi na kutoeleweka ukizingatia maendeleo ya kesi ilivyokuwa hapo nyuma kufutwa imekuwa ni ghafla sana.
“Serikali imeshindwa kuleta Ushahidi pasi shaka na hivyo mahakama imemkuta Joe bila hatia. Tumeiagiza serikali na vyombo vyake kuachilia mali zote za familia ya Joseph na kumtolea vikwazo vyote iliyokuwa imeviweka dhidi yake hapo kabla”, alikuwa ni Jaji Kunambi akiongea na vyombo vya habari mara baada ya kutoka kutoa hukumu ya mashtaka yaliyokuwa yakimkabili Joe.
“Naishukuru mahakama kwa kunitendea haki. Hilo tu ndilo ninaloweza kusema” Joe aliwajibu waandishi kwa ufupi nje ya mahakama.
“Vipi serikali ikikuhitaji uitumikie maana tunajua wewe ni mwanadiplomasia mbobevu na ni serikali hii hii ilikutia hatiani”, Seif, mwandishi kutoka gazeti la NIJUZE alimuuliza Joe.
“Sijachoka kuitumikia serikali. Kesi yangu ni ishara kuwa serikali chini ya Rais Costa inapingana na vitendo vyovyote vya uhujumu uchumi na haibagui, yeyote anaweza kushtakiwa kama ikihisiwa anajihusisha na vitendo hivyo. Hivyo serikali ikinihitaji nitaitumikia sina ugomvi nayo”, Joe alimjibu mwandishi huku moyoni akiwa amejawa na hasira nyingi.
Kwa siku zile tatu vyombo vya habari vyote vilijaa habari ya mwanadiplomasia Joseph Kaduma kuishinda serikali juu ya mashtaka yake ya kuhujumu uchumi.
“Watu wanaisifia mahakama kwa kutenda haki, ni wazi wengi walikuwa wanamuhurumia Joseph” Gideon mshauri wa karibu wa Rais Costa alimwambia Rais mchana mmoja wakiwa wanakula chakula Ikulu. “I see, we have made the right move” (Naona, tumefanya jambo sahihi), Rais Costa alijibu kisha akanywa funda la mvinyo kushushia chakula.
***************************************
Ilikuwa ni siku ya Alhamisi yenye mchanganyiko wa hasira na furaha baada ya hukumu. Usiku wake Joe alikuwa ametulia chumbani na mke wake Eliza maeneo ya Endokasi Estate, mahali walipopewa nyumba na serikali. Walikuwa katika hali ya utulivu na tayari baadhi ya mali zao zilianza kurudishwa na vikwazo kuondolewa.
Hakuna aliyekuwa akiongea na mwenzake bali kila mmoja alikuwa akibubujikwa na machozi. Hawakuamini kilichotokea baada ya miaka mitatu ya kuishi kifungoni na maisha duni na ya manyanyaso makubwa, leo wanarudishwa tena.
Eliza alianza kuelewa nguvu ya Rais na alikuwa akijuta kimoyomoyo alivyokuwa anamkatalia Joe kukubali maagizo ya Rais Costa. Alianza kuelewa kuwa njia moja tu ya kupambana na mtawala ni labda kupambana nae kinyume na sheria yaani nje ya mfumo wa vyombo vya haki vilivyopo chini ya serikali au kupambana nae ukiwa sehemu ya serikali yake ila tu omba Mungu asikugundue kitu ambacho kwa mifumo ilivyo ni ngumu sana. Angalau hali ndiyo ipo hivyo katika nchi nyingi zinazoendelea.
Mawazo ya Eliza kutaka Joe apambane na Rais Costa yalikuwa si sahihi na yasingewafikisha popote, yangewamaliza. Alinyanyuka na kumkumbatia mume wake. “Joe, ya kale yamepita na tazama sasa yamekuwa mapya”, Eliza aliongea kwa sauti ya upole akiwa kifuani mwa Joe pale kitandani.
“Ni kweli mke wangu. Kila jambo lina wakati wake. Kadiri niishivyo nakuahidi kila mmoja aliesababisha tukaingia kwenye hali tuliyokuwa nayo ATALIPA. Kesho nakwenda kuonana na Rais Costa tayari kuanza kutimiza majukumu aliyonituma.
Najua Rais Costa hakunitafuta kwa ajili ya hiki alichonituma kuna kubwa nyuma ya hili, mimi ninaelewa ila ngoja nijifanye sielewi”, Joe aliongea kwa utaratibu na kumwacha Eliza akiwa na maswali mengi hasa aliposikia kuna suala la malipizi. Aliwaza mumewe anataka kufanya nini, amlipize nani, lini, kwa njia gani? Aliwaza hilo lililo nyuma ya pazia ni nini haswa? Mengi yalikuwa akilini mwake ila hakutaka kuuliza alibaki kimya.
Asubuhi ya kesho yake mishale ya saa mbili hivi Joe alikuwa tayari kuelekea Ikulu kuonana na Rais Costa ili kumpa mpango mkakati wake wa jinsi ya kulitekeleza suala la kurudisha mahusiano na Korea Kaskazini na kisha kufanya yale Rais anayoyataka wasaidiwe.
Alivaa suti nyeusi na tai nyekundu. Alibeba kalamu yake aina ya Vintage rare carandash AK-45 moja ya kalamu ghali zaidi alizopewa zawadi na Rais Vijisky wa Urusi siku chache kabla ya kufutiwa hadhi ya ubalozi na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi na Rais Costa.
Alijipachika na nembo ya bendera ya taifa pembeni mwa kola ya koti lake la suti. Hakika Joe alijua kuonekana nadhifu na kidiplomasia haswa. Nje ya nyumba yake, Land Cruiser V8 toleo jipya ilikuwa ikiunguruma na dereva akiwa nje ya mlango akimsubiri atoke.
Joe alisimama mbele ya kioo akajiangalia kwa muda wa dakika kama tatu hivi. Juu ya ile meza yenye kioo kulikuwa na biblia akafungua Zaburi ya 23 akaisoma yote. “Mungu nisaidie”, Joe alimalizia na kubeba mkoba wake na kutoka tayari kwenda Ikulu kukutana na Rais.
***********************************
Joe Yupo Tayari Kumsaidia Rais Costa Lakini Akiwa Na Mipango Yake Kichwani. Mipango Gani Hiyo?Atafanikiwa? ....
 
SEHEMU YA TATU

Joe Achagua Kikosi Kazi Chake Cha Misheni Ya Korea Kaskazini. Wakutana China. Rais Costa Atuma Kijana Wa Ki Vietinam Kuwafatilia Kwa Siri.
Korea ya Kaskazini ni taifa lililo na balozi 48 duniani kote lakini ni nchi 25 tu ndio zenye balozi zao jijini Pyongyang. Taifa hili hutegemea zaidi biashara kati yake na nchi za Uchina na India, ambapo asilimia 95 ya biashara zake za nje na uagizwaji wa ndani hufanywa baina ya nchi hizi mbili na asilimia iliyobaki kwingineko kama vile Ufilipino.
Tangu mtawala wa nchi hiyo Kim Jong Un atangaze majaribio ya makombora ya nyuklia ya masafa marefu, Marekani na Umoja wa mataifa iliiwekea vikwazo. Pia taifa la Marekani liliwataka washirika wake kutojihusisha kibiashara na Korea Kaskazini hata hapo itakapositisha majaribio yake. Hali hii ilifanya hali ya kiuchumi ya Korea Kaskazini kudorora na hata wananchi walipotaka kudai haki zao, ukatili uliongezeka dhidi yao na udikteta ukaota mizizi, ingawa katika utambulisho rasmi wa jina la nchi hiyo ni ‘Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea’.

Nchi nyingi za kiAfrika ziliingia kwenye wakati mgumu wa namna gani kukubaliana na Marekani na Umoja wa mataifa juu ya vikwazo walivyoweka dhidi ya Korea na wakati huohuo kuendelea kuwa na mahusiano mema na taifa hilo lenye historia kubwa ya kikomunisti na mataifa mengi ya kiAfrika.
Mahusiano mengi kati ya Korea Kaskazini na nchi nyingi za kiAfrika hayapo kisiasa tu lakini pia kiuchumi kwani inakadiriwa kati ya mwaka 2007 na 2015 biashara iliyofanywa kati ya taifa hili na nchi za kiAfrika yafikia dola za kimarekani milioni 217.
Korea ikilitumia shirika lake la Mansudae wametekeleza miradi kadhaa ya ujenzi katika nchi baadhi za kiAfrika lakini hasa Namibia ambapo Ikulu na Makazi ya Rais yamejengwa na Korea Kaskazini. Nchi za Uganda, Tanzania na Mozambique mwaka 2017 zilishutumiwa kuiomba Korea iwasaidie katika Nyanja za jeshi, shutuma ambazo nchi kama Tanzania ilizikana lakini Uganda walikubali na kuahidi kusitisha.
Mbali na miradi ya ujenzi barani Afrika, Korea Kaskazini pia hufanya biashara kubwa ya silaha za kivita. Katika nchi za Eritrea, Jamuhuri ya Afrika ya Kati, Congo na nchi nyingine, Korea ni washirika wazuri katika biashara hiyo. Pia, ripoti ya kiuchunguzi ya Forbasi, taasisi inayoaminika kwa uchambuzi wa masuala ya usalama duniani yenye makao makuu Uskochi inasema kuwa taifa hili la Korea Kaskazini ndilo husaidia ulinzi binafsi wa Rais wa Congo kwa kutoa mafunzo, utaalamu na ufuatiliaji wa usalama wake. Taarifa ambazo serikali ya Congo inakanusha hata leo.
Mwezi Septemba, 2017 Rais wa Marekani Chriss Donald kupitia agizo lake namba 13810 aliomba nchi zote marafiki wa Marekani kuungana nae katika kusitisha aina yoyote ya biashara na mahusiano na Korea Kaskazini kama kuunga mkono jitihada za kuhakikisha taifa hilo haliendelei na majaribio yake ya makombora ambayo Marekani ilihofia yangeachwa kuendelea, hatimaye wangefikia uwezo wa kitaalamu wa kutengeneza makombora ya nyuklia yanayoweza kusafiri masafa marefu na kufikia ardhi ya Marekani.
Stanza, moja ya nchi barani Afrika na mshirika mkubwa wa Marekani leo inafanya jitihada wanazotaka ziwe za siri kujenga mahusiano na Korea Kaskazini. Wakati asilimia 50 ya bajeti ya Stanza ikiwa inatokana na mapato ya ndani na asilimia 50 iliyobaki ikitoka kwa nchi wahisani, Marekani pekee inachangia asilimia 20, achilia mbali fedha nyingine nyingi inazopokea kupitia mashirika ya maendeleo ya ki Marekani. Ni katika hali hiyo Rais Costa anataka kukiuka maagizo ya Marekani juu ya mashirikiano yake na Korea Kaskazini.
Rais Sylvester Costa anataka kwenda mbali kuwaingiza kabisa watoe mafunzo, vifaa na mfumo mzima wa mawasiliano wa Serikali, Jeshi na Idara ya Usalama wa taifa la Stanza.
********************************
“Mh. Rais kutokana na hayo niliyokwishaeleza, basi kwa kuwa sisi hatuna ubalozi Pyongyang wala Korea Kaskazini hawana ubalozi wao hapa kwetu ni vema tukautumia ubalozi wetu pale China kama Sehemu ya kufanyia mikakati mimi na timu yangu nitakayoipendekeza. China wana mahusiano ya karibu sana na Korea na hivyo ninaweza kuwatumia baadhi ya marafiki pale katika, kwanza kujenga mahusiano kisha ndio nitaendelea na mengine uliyoniagiza.
Lakini nikuombe Mh. Rais kuwa wakati haya yakiendelea ni vyema usiwe na makwazo mengi kwa nchi za magharibi kwani wanaweza wakaanza kutufatilia sana kwa ukaribu na kuharibu mikakati na pia kuwekewa vikwazo vitakavyofanya hali ya uchumi wetu iwe mbaya.
Lakini pia angalia namna ya kuzungumza na Rais wa Urusi, Kamaradi Vijisky na Rais wa China pia juu ya yale mlioshindwa kuelewana. Njia hiyo itanisaidia sana mimi kuwatumia kwenye misheni yangu hii na pindi wa magharibi watakapoanza kutuletea zengwe wao watasimama kidete nasi”, Joe aliwasilisha mapendekezo yake kwa umakini wakati akielezea mikakati yake kwa Rais Costa.
Meza ile ilikuwa na watu watano, Rais Sylvester Costa, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Ernest Nduta, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Chonge Kalumanzila, Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Stanley Macha, na Joseph Kaduma.
Mara baada ya Joe kumaliza kuongea, kila mtu alikuwa kimya na kuonekana kumuelewa vyema. Aliyekata ukimya ule alikuwa ni Rais Costa, “Joe, tutajitahidi kufanya uliyopendekeza lakini niseme mambo haya kwasasa ni siri kubwa na nimewaeleza wenzangu namna ya kuenenda. Ninajua suala hili likiwafikia Marekani na washirika wake tutakuwa kwenye wakati mgumu na ninajua watang’amua mapema sana ndio maana sitaki tushindwe”, Rais Costa alimsisitiza Joe.

Joe aliomba timu ya watu wawili wa kusaidiana nae alimtaja Habibu Chamchua Balozi wa Stanza nchini India ambae ni kijana mpendwa wa Joe na Luteni Jenerali Pius Kihaka Mnadhimu Mkuu wa Jeshi na Mkuu wa kitengo cha Idara ya usalama wa jeshi na mmoja kati ya vijana wadogo na wasomi sana katika jeshi la wananchi wa Stanza.
Pius Kihaka ni Rafiki mkubwa wa Joe, hawa wote; Habibu na Pius ni wanafunzi wa Joe katika chuo cha Diplomasia walipokuwa wanafanya Shahada zao za Uzamili. Joe anaamini hawa ni baadhi ya vijana wenye upeo mkubwa sana katika uwanda wa kidiplomasia, ushawishi na ushushushu. Ndio watu aliowataka kufanya nao kazi. Lakini pia alikuwa na ajenda nao nyingine nyuma ambayo hakuna mtu alieijua. Rais Costa alimkubalia na kutoa maagizo vijana hao wataarifiwe na kuwa sasa watafanya kazi kwa maelekezo ya Joe.
Kikao kile kiliisha vyema. Joe aliridhika kuwa sasa anaweza kuanza kutimiza majukumu yake. Alipatiwa kila aina ya mahitaji na nyaraka alizohitaji ili kutekeleza kazi aliyopewa. Rais Costa alipeleka salamu za kutaka mazungumzo na Rais Kim wa Korea na kuwa ujumbe wake utaelekea huko. Rais Kim aliridhia na kutaka kujua haswa ni nini taifa kutoka Afrika tena wenye ushirika mkubwa na Marekani linataka kuzungumza. Hakika kila nchi ilijitayarisha kwa mazungumzo hayo.
*******************************
Habibu Chamchua, kijana mahiri katika medani za kidiplomasia, machachari katika ushushushu na sasa balozi wa Stanza nchini India alifurahishwa na taarifa kuwa anahitajika kufanya kazi na Joe. Habibu alikuwa kijana makini na aliyefanya vyema kwenye chuo cha diplomasia, alishawishiwa na Joe aingie kwenye siasa ili kushika nafasi za uongozi wa nchi.
Ni Joe aliyempa moyo Habibu kwa kumwambia kuwa anamuona siku moja kama Rais wa Stanza. Mara baada ya Habibu kuingia kwenye siasa alifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kuteka nyoyo za vijana wengi wa chama tawala mpaka upinzani. Ni yeye aliewezesha kubadili hali ya kisiasa kwa wakati fulani kwa jinsi alivyoweza kujenga hoja na kujieleza.
Katika chama tawala alionekana sana tishio na ni hapo Rais Costa ili kumpunguza nguvu aliona yafaa amtoe nchini na kumpangia ubalozi ili apotee machoni na masikioni mwa wengi. Habibu sasa anapewa jukumu la kuhakikisha Korea Kaskazini inasaidia Stanza kijeshi lakini hususani kufanya kazi na Joe, ilikuwa ni heshima kubwa kwake.
*******************************
Zilipita wiki mbili tangu mashtaka ya Joe dhidi ya uhujumu uchumi kufutwa na mahakama ya uhujumu uchumi na ufisadi ya Stanza. Waziri wa Fedha alimteua Elizabeth Kidampa Kaduma kuwa Mkurugenzi wa benki ya Kilimo ya Stanza. Elizabeth, mke wa Joseph Kaduma aliwasili makao makuu ya benki na kupokelewa kwa heshima kubwa. Eliza alijaa haiba na tabasamu, ni mwanamke asiejikweza mwenye uwezo mkubwa wa kusikiliza na kung’amua mambo.
Mara baada ya kusomewa taarifa fupi ya maendeleo ya benki, alibainisha wazi kuwa vipaumbele vyake ni pamoja na kuhakikisha fedha zote zinazotengwa na serikali kwa ajili ya ruzuku zinawafikia wakulima kwa wakati na hilo hatakuwa na msamaha na mtendaji yeyote atakayezembea, lakini pili ataanzisha maghala yatakayosimamiwa na benki na kuwa mazao yote ya biashara yatapangiwa bei elekezi na mfanyabishara atapaswa kuyanunua kwa bei hiyo kutoka kwa wakulima, vinginevyo basi benki itayanunua na kuyatafutia masoko.

Alitanabaisha benki ile ni lazima iwe msaada kwa wakulima kwa kutoa mikopo nafuu na kuhakikisha wakulima wa Stanza wananufaika. Pia, alielezea mpango wa benki kwa kushirikiana na wizara kujenga mabwawa makubwa na ya kisasa kwa ajili ya umwagiliaji katika kanda tano zinazoongoza kwa kilimo cha mazao ya biashara na chakula kwa kuanzia ili nchi itoke kwenye kutegemea mvua pekee kwa ajili ya umwagiliaji. Ilikuwa ni taarifa njema.
*********************************
“Kaka shikamoo”, alikuwa ni Habibu akimsalimia Joe kwa bashasha na tabasamu kubwa huku akimkumbatia ndani ya ofisi za ubalozi wa Stanza jijini Beijing China zilizopo mtaa wa Liang Ma He, Nan Lu. Ilikuwa ni faraja kubwa kwa Habibu kukutana na Joe. “Luteni Jenerali” Habibu alimwita Pius huku akionyesha ishara ya kupiga saluti kisha kumkubatia kwa kicheko kikubwa.
Habibu alikuwa akiwalaki Joe na Luteni Jenerali Pius Kihaka waliokuwa wamewasili kutoka Stanza, yeye akiwa amewatangulia siku moja kabla akitokea India. Habibu ndio alikuwa mdogo kiumri kati ya Joe na Luteni Jenereli Pius Kihaka. Wote kwa pamoja walilakiwa na balozi Kimweri anaeiwakilisha Stanza huko China.
Walielekea kwenye chumba walichotengewa na ubalozi maalumu kwa ajili ya vikao vyao na Joe alikuwa tayari kutoa muhtasari na mwongozo wa namna kazi itakavyofanyika. “Ni jukumu letu kuleta matokeo yanayotegemewa na Mh. Rais. Tutaingia kwenye vitabu vya historia kwa kuanzisha mahusiano na Korea Kaskazini lakini pia kwa kufanikisha kazi hii Mh. Rais aliyotutuma”, Joe alimalizia. Habibu na Pius walionekana kutikisa vichwa ishara ya kuelewa na kuafiki. Wakati Joe akiongea walikuwa wakipitia baadhi ya nyaraka Joe alizowagawia waziangalie na kuzisoma. Tayari ubalozi wa Stanza pale China ulishaanda utaratibu mzima wa Joe na wenzake kuingia Korea Kaskazini.
Baada ya maongezi yale yaliyodumu kwa masaa mawili wakiweka mikakati na nini cha kuzungumza na nani azungumze nini. Joe alipendekeza jioni wakutane mgahawa wa Cheng Lee ulio jirani na Ubalozi kwa ajili ya kupata kahawa.
**********************************
Ilikuwa ni habari iliyowasisimua viongozi wa taifa la Korea Kaskazini kusikia kuwa kuna taifa kutoka Afrika linataka kuanzisha mahusiano nao ukizingatia tamko na maazimio ya Marekani na Umoja wa mataifa. Rais Kim alikuwa akisubiria ujumbe kutoka Stanza kwa shauku kubwa.

Kuonyesha shauku yake na kwa ajili ya usalama aliagiza ndege kutoka shirika la ndege la Korea Kaskazini, Air Koryo llyushin II-62M ndiyo iwabebe kwa kuwatengea siti maalum. Viongozi wa Korea walijipanga kusikia nini ujumbe kutoka Stanza utawaeleza na mashirikiano gani wanahitaji, watafaidika vipi na wamejipangaje kushindana na shinikizo kutoka nchi za Magharibi zisizowaunga mkono hasa Marekani.
********************************
“Kimweri niambie kinachoendelea”, alikuwa ni Rais Sylvester Costa akiongea na balozi Kimweri aliyeko China kupitia mfumo salama wa mawasiliano ya kiserikali. “Mpaka sasa hakuna tishio lolote walilojadili ila jioni wamekubaliana kukutana mgahawa wa Cheng Lee kwa ajili ya kupata kahawa”, balozi Kimweri alimjibu Rais Costa. “Kuna mtu kule tayari? Nahitaji ufuatiliaji kwao hatua kwa hatua hasa wakiwa hapo China”, Rais Costa alisisitiza. “Ndiyo mkuu”, balozi Kimweri alijibu.
Bila Joe na wenzake kujua Rais Costa alishaweka namna ya kufatilia kila wanaloongea Joe, Habibu na Pius. Alihakikisha vyumba vyote watakavyokuwa wanakutana vimewekewa vinasa sauti kwa siri vyenye uwezo mkubwa sana. Maongezi yao na simu zao zote zilikuwa zikirekodiwa.
Rais Costa alikuwa akipata kila kinachoendelea kwenye maongezi ya Joe na wenzake. Japo alimwita Joe amsaidie kazi lakini hakumwamini. Alianza kupata mashaka hasa Joe alipotaka kazi ile asaidiane na Habibu na Pius watu anaowajua ni watiifu kwa Joe. Rais Costa hakutaka kupitwa na kitu hivyo tayari balozi Kimweri alishatuma mtu mgahawani kuangalia namna atakavyoweza kurekodi maongezi ya kina Joe bila wao kujua.
Kimweri alifanya hivyo mara baada ya kuona Joe ametoka kwenye kikao na kwenda kupumzika lakini hakumualika kwenye kahawa jioni wakati yeye ndo mwenyeji wao. Aliwaza ni nini Joe alitaka kwenda kuongelea huko. Kati ya watu watiifu na vipenzi wa Rais Costa basi balozi Kimweri ni mmoja wapo.
***********************************
Jioni ilifika na Joe, Habibu na Pius walitoka kwenda mgahawani. Walipofika Joe alichagua meza iliyo mwishoni mwa mgahawa ili apate kuona kila anaeingia ndani ya mgahawa na alihakikisha upande aliokaa hakuna anaeweza kingia bila yeye kumuona. Kati ya Habibu na Pius hakuna aliyekuwa anajua kinachotaka kujadiliwa pale, walidhani ni maongezi ya kawaida tu.
Waliketi, na baada ya kumaliza kuagiza kahawa Joe alivunja ukimya. “Guys, ninyi ni vijana wangu na ninaelewa nguvu yenu. Mfano Habibu unaelewa jambo nililoongea nawe miaka mitano iliyopita lililokufanya ujiingize kwenye siasa kwa mara ya kwanza. Pius wewe pia unaelewa au sio? Huu ndio wakati wa kuanza utekelezaji, tunaenda na yote mawili ndani ya moja”, Joe alitulia na kunywa kahawa.
Habibu na Pius walionekana ni kama watu wasioelewa Joe anazungumza kitu gani, walibaki wameshangaa wakiangaliana. Joe alikuwa akizungusha macho mgahawani kuhakikisha hakuna yeyote anakaa meza karibu yao ama hata kuwasogelea.
Akiwa amemaliza kunywa tena kahawa kwa mara ya pili simu yake ilitoa sauti kuashiria kuna ujumbe umeingia. Alipoangalia vyema aligundua ujumbe umeingia kupitia App ya game uliosomeka “Hakikisha mdudu yeyote hakukaribii wakati wowote wa mazungumzo nje ya Ubalozi”, Joe aliposoma alivuta pumzi na kujikaza ili Habibu na Pius wasishtuke kisha akaanza kuzungusha macho kila kona hasa maeneo ya ukuta na dirisha lililo umbali mchache kutoka pale walipokaa. Alipokuwa akiangalia aliona mdudu kama nzi akiwa anawasogelea.
Akaja akatua juu ya kichwa cha Joe kwa ukutani. Joe alishtuka sana akajikaza. Pius akawa kama kuna jambo ameshtukia akamuuliza Joe kulikoni? Joe hakujibu akamwonyeshea Pius ishara ya kuwa anyamaze, kisha akaonyesha ishara kuwa waondoke. Waliposimama na kuanza kuondoka Joe aliwasogelea wenzake na kukaa katikati yao kisha akawaambia atawaambia kilichotokea ila wasiwe na wasiwasi.
******************************
Stanley Macha, mkuu wa Idara ya Usalama wa taifa Stanza na Rafiki mkubwa wa Joe alikuwa akifuatilia hatua kwa hatua safari na misheni aliyotumwa Joe nchini Korea Kaskazini. Ni ukweli usiopingika Macha na Joe walikuwa ni zaidi ya marafiki, ni yeye alietengeneza mazingira misheni ya kutafuta mahusiano na Korea Kaskazini isifanikishwe na mtu yeyote katika serikali ya Rais Costa mpaka Joe aitwe.
Ilikuwa ni ngumu kumuacha Joe peke yake hasa akijua mahusiano ya kutilia shaka aliyonayo Joe na Rais Costa. Mara baada ya Joe kukubali kutumika na Rais Costa katika misheni ya Korea Kaskazini Macha aliamua kutafuta njia ya siri ya kuwa wanawasiliana na Joe. Waliamua wote kuwekagame (mchezo wa kwenye simu) unaoitwa Clash Royale ambao wachezaji huweza kutumiana jumbe na kuwasiliana. Ili mtu mwingine kuweza kufatilia jumbe zinazotumwa humu ni lazima uwe na wewe umeweka huu mchezo kwenye simu yako ama uwaombe wamiliki wakupe.
Lakini pia majina yanayotumika huwa sio ya halisi hivyo pia ni ngumu kujua ujumbe huu unatoka na kwenda kwa nani. Macha na Joe hutumia njia hii kuwasiliana. Macha alichelewa sana kupata taarifa juu ya mpango unaondelea juu ya Joe na wenzake unaofanywa na Rais Costa na balozi Kimweri. Hakuna anaejua alipataje hasa ukizingatia maelekezo ya Rais kwa balozi Kimweri ni ufuatiliaji wa Joe ufanywe baina yake na Kijana ambae Rais Costa alimpelekea balozi Kimweri kutoka Vietnam.
Balozi Kimweri na yule kijana wa kiVietnam walitumia kinasa sauti mfano wa Nzi kinachoweza kuendeshwa kwa rimoti ya kwenye simu kutokea mbali. Hivyo kutokea meza ya mbele kabisa ya mgahawa kijana yule wa kiVietinam alikitoa kile kinasa sauti na kuanza kukiendesha kwa simu kama mtu aliekuwa akichat kuelekea mwisho wa mgahawa walipokuwa wamekaa Joe na wenzake.
Macha alipopata ile taarifa alimtumia ujumbe Joe kuwa awe mwangalifu na mdudu yeyote arukae atakaesogea karibu nao. Joe aliona yule mdudu kama nzi na aligundua kilichokuwa kikiendelea. Waliondoka.
***********************************
Joe Alitaka Kuwaambia Nini Wenzake? Je, Rais Costa Atafanikiwa Kumfuatilia Joe Au Ndio Joe Kashamtoka?Vipi Kuhusu Misheni Ya Korea?...
 
SEHEMU YA NNE

Mazungumzo Mazito.Yawaacha Njia Panda

“Mr. President, I respect the outstanding, long time bilateral relations our countries have enjoyed for the past 50 years. I, personally appreciate the two-way respect between you and I, but with all due respect, I will not allow your country to forcibly impose your culture on ours. We will not allow or legalize homosexuality in our country. It is against our normalcy, tradition, and culture as Africans. It is against our spiritual beliefs and the order of nature. If you have accepted it as your way of life, let it remain yours”
(Mh. Rais ninaheshimu mahusiano mazuri na ya muda mrefu baina ya nchi zetu mbili katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Na binafsi, ninaheshimu pia mahusiano tuliyo nayo sisi wawili, lakini kwa heshima kubwa niseme sintoruhusu taifa lako lilazimishe mapenzi ya jinsia moja kukubalika kwenye nchi yetu. Ni kinyume cha tamaduni na desturi zetu, kinyume na imani zetu, lakini zaidi na muhimu ni kinyume na asili ya mwanadamu. Kama mmekubaliana hayo kuwa Maisha yenu, basi ibaki kuwa hivyo huko kwenu.)
Rais Costa alikuwa akiongea na Rais wa Marekani, Chriss Donald masuala mbalimbali yanayohusu Stanza na hapo alikuwa akimjibu matakwa ya Marekani kutaka mataifa yanayopokea msaada kutoka kwao kuruhusu mahusiano ya jinsia moja (ushoga).
“Mr. President I understand your position, but I suggest that we talk about this in the next bilateral meeting. We will need to review most of our foreign relations policy with Stanza, if at all we do not come into a mutual understanding on the matter.
I can tell that after deliberations, your position will change, and Stanza will consider same-sex marriage as not only a private matter between two adult individuals who have chosen to love one another but also as a basic human right to associate and to form social relations. That I can guarantee”.
(Mh. Rais naelewa msimamo wako, ingawa nashauri kuwa tulizungumzie suala hili katika mkutano ujao kati ya nchi zetu. Tutalazimika kufanya mapitio ya sera yetu ya mambo ya kigeni na Stanza, ikiwa hatutofikia maelewano kuhusu suala hili.
Ninaweza kusema kuwa baada ya kukaa na kufikiria, msimamo wako utabadilika na Stanza itakubaliana na ndoa za jinsia moja si tu kuwa ni masuala ya faragha kati ya watu wazima wawili walioamua kupendana, bali pia kama haki ya msingi ya binadamu ya kuhusiana na kuanzisha mahusiano ya kijamii. Nakuhakikishia hilo). Rais Donald alimjibu Rais Costa kwa sauti ya kuamrisha kidogo. Rais Costa alighadhibika ila akakaa kimya.
“Again, it is interesting Mr. President to hear that your country is intending to amend the constitution that will change the legal age to run for presidency from 40 to 55 years.
(Nimepata taarifa kuwa Stanza inakusudia kufanya mabadiliko ya katiba yatakayofanya umri wa kisheria wa kugombea nafasi ya Urais kuwa miaka 55 tofauti na miaka 40 ya sasa). Rais Chriss Donald alimwambia Rais Costa kwa kebehi.
“I think you are crossing the line Mr. President, Stanza is a sovereign country. It is of best interest if each of our countries is let to freely define democracy according to their local context and choose what works best for them.
(Nafikiri unakwenda mbali Mh. Rais, Stanza ni taifa huru. Nibusara kuachia kila nchiijiamulie nini maana yademkorasia kwao kwa misingi yamuktadha na kile ambachokinafanya kazi katika nchihusika). Rais Joe nae alijibu kwakicheko cha kebehi lakinikilichojaa ghadhabu.
“No no no. It is not my intention, nor that of the United States to interfere with your internal affairs. I raised the matter so that we can both have the same understanding of the happenings. We shall see to that too”.
(Hapana! Hapana. Si lengo langu wala la Taifa la Marekani kuingilia masuala ya ndani ya nchi yenu. Nimelisemea suala hilo ili sote, mimi na wewe tuwe na uelewa unaofanana wa masuala yanayotokea. Tutaliangalia na hilo pia’’), Donald alimalizia.
“It was nice time speaking with you Mr. President” (Umekuwa muda mzuri kuongea nawe Mh. Rais) Rais Costa alimuaga Rais Donald kwa hasira kidogo.
“Pass my hello to Chairman, Mr. Kim”, (Salamu nyingi kwa Mr. Kim), Donald alimalizia na kukata simu akimwambia Rais Costa amsalimie Kim, Rais wa Korea Kaskazini.
Rais Costa alibaki na mshangao ulioonekana waziwazi usoni mwake. Alijiuliza maswali mengi, muhimu zaidi ikiwa imekuwaje Rais Donald akamtaja Kim muda ambao Joe na wenzake wanatekeleza misheni aliyowatuma ambayo kwa wakati huo alitambua ni siri.
“Macha wapigie simu kina Joe, nataka kufahamu wamefikia wapi. Haraka nitafutie nani amevujisha mpango huu kwa Marekani kabla hata ya Joe kukutana na Rais Kim”, Rais Costa alimwambia Stanley Macha kwa ghadhabu kisha alijiegamiza kwenye kochi na kupumua kwa nguvu. Alichanganyikiwa. Anafahamu mabavu ya Marekani katika siasa za kimataifa. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, mataifa yaliyotofautiana na Marekani yameingia katika misukosuko mikubwa ya kiuchumi na kijamii.
**************************************
Ndege waliyopanda Joe na wenzake iliondoka mishale ya saa moja asubuhi kwa saa za China kuelekea Pyongyang ikitokea uwanja wa Beijing Capital International Airport. Joe na wenzake waliwekewa nafasi kwenye daraja la watu muhimu, ulikuwa ni ujumbe maalum unaosubiriwa sana na uongozi wa Korea Kaskazini. Kutoka Beijing mpaka Pyongyang ni safari ya masaa mawili hivi, hivyo mara tu baada ya ndege kutulia juu ya anga Joe aliwapa alama Habibu na Pius wasogee kwenye nafasi yake karibu. Nafasi zao zilifuatana.
Joe aliwaambia kwa kifupi kwanini aliwaondosha pale mgahawani. Aliwaambia kuwa Rais Costa alikuwa akifatilia maongezi yao kwa kuwatumiadrone yenye umbo la Nzi ili inase maongezi yao. Pius na Habibu bado walikuwa hawajaelewa kwanini hayo yanatokea. Joe alitambua hilo na haraka alianza kuwaweka bayana, “Nadhani kati yenu hakuna anaefurahia namna Costa anaipeleka nchi, ni jukumu letu sasa kumpumzisha kwa amani na usalama”.
“Najua mnaweza kudhani ninataka kulipa kisasi lakini nayasema haya kwa nia njema ya kizazi kijacho na ustawi wa nchi yetu ya Stanza”, Joe alikuwa akiongea kwa kunong’ona sana huku akiwakazia macho Pius na Habibu. “Ninawaambia haya kwa sababu ni ninyi mnaoweza kutekeleza hili. Ninawategemea kama vijana wangu, lakini ikiwa mtaona haya si ya msingi, basi tunaweza kuachana na mpango huu kabla hata hatujauanza. Tafakarini na tutaamua kwa pamoja uelekeo ambao ninyi mnatamani taifa letu lichukue”. Joe alimalizia na kukaa kimya kuwasikiliza.
Baada ya sekunde kadhaa za ukimya, Habibu ndiye aliyekuwa wa kwanza kuuvunja ukimya. “Joe, unachomaanisha ni kututaka tushiriki kumpindua Rais aliyepo madarakani kihalali?”. Habibu alionekana kutoelewa anachoshauri Joe. Habibu ni mtiifu kwa Joe lakini katika hili aliona ukakasi.
“Hapana, hatumpindui, tunampumzisha kwa ustawi wa Stanza.” Joe alijibu kiufupi. “Unampumzishaje mtu kabla ya muda wake wa kukaa madarakani kihalali kuisha?”, Habibu alizidi kuuliza.
“Muda wake kihalali uliisha 2015, nini kilitokea baada ya pale? Costa hana uhalali na nilazima ataibadili katiba na sasa nadhani Pius anafahamu, labda wewe kwa sababu upo mbali na varanda za Ikulu hujui, anataka kuhakikisha uchaguzi ujao anapandisha umri wa mtu kugombea Urais ili abakie yeye. Costa hana muda wa uhalali”. Joe alijibu huku akiwatazama usoni Habibu na Pius.
“Joe, nimekula kiapo cha kumlinda Rais, unachoniambia hapa ni Uhaini, na ni lazima utambue nafasi yangu katika jeshi”. Luteni Jenerali Pius Kihaka alionekana kumjibu Joe huku akiwa amekunja ndita.
“Luteni ulikula kiapo kuilinda katiba na Rais anayeitii misingi ya katiba. Utamlinda Rais pale tu akiitii katiba na si vinginevyo. Rais asiyetaka kuitii katiba, misingi ya haki na utawala bora anageuka kuwa muhalifu kama wahalifu wengine. Sasa nikuulize kiapo chako kinakuelekeza kumtii na kumlinda muhalifu?” Joe alimjibu Pius.
“Nahitajika kumtii yeyote alieshikilia nafasi inayoitwa Rais bila kujali anafuata katiba ama vinginevyo. Hivyo ndivyo mafunzo na miiko yangu jeshini inavyoniongoza. Wananchi ndio wanatakiwa waseme huyu haifuati katiba na wamtoe kwa chaguzi za kidemokrasia lakini sio mimi. Lakini je, wewe ndio kipimo cha kuhalalisha kuwa huyu anavunja katiba ama la? Au wewe ndio wa kusema huyu hafuati haki na utawala bora ama la? Nijuavyo mimi mamlaka hayo imepewa Mahakama au angalau Bunge na sio hisia za mtu binafsi Joe” Pius alisisitiza kwa maswali mfululizo.
“Pius, nadharia ya mgawanyo wa kimamlaka kati ya Serikali kuu, Bunge na Mahakama kiuhalisia haupo kwenye nchi zetu nyingi za kiAfrika achilia mbali Stanza. Nadharia hizo zimewekwa kwenye katiba kwa mkono mmoja na kuporwa kwa mkono mwingine. Tuliyajadili haya kwa kina sana nilipokuwa nawafundisha pale chuo cha diplomasia. Pius ulionekana kukasirishwa sana na hali hii, Habibu uliniahidi siku ukipata nafasi ya uongozi ungerekebisha haya, lakini tazama leo baada ya kuzipata nafasi mbalimbali mmesahau mara moja hii? Leo ninyi nanyi mnaona hali hii ni sawa na kunihoji maswali kana kwamba hamfahamu ukweli huu?” Joe aliongea kwa hisia kubwa na kuanza kuwapa darasa.
Aliongea nao kwa kina na kuwapa mifano mingi ya uvunjifu wa haki za raia, unyanyasaji na uteswaji. Aliwaambia jinsi hali inavyokwenda kuwa Mbaya baada ya Rais Costa kuweka sera nyingi mbovu na kuharibu sana mahusiano na mataifa rafiki. Aliwaambia hata safari yao ile ni kwa sababu Stanza inakosa marafiki na sasa inatafuta marafiki wapya kwa nguvu.
Aliwaeleza kinagaubaga namna mihimili miwili ya Bunge na Mahakama jinsi ilivyo ghoshiwa na Rais Costa na kuwa hakuna chochote kinaweza kuendelea ndani ya mihimili hiyo kilicho kinyume na Rais Costa hata kama kina maslahi makubwa kiasi gani na nchi ya Stanza. Aliwashangaa ni kwanini wao kwa nafasi zao inawawia vigumu kuling’amua hilo vipi kwa mtu wa kawaida.
Aliwaambia, wao wanaweza kukataa kwa sababu wana nafasi serikalini lakini wajueakumulikaye mchana usiku atakuchoma hivyo wasishangae siku moja kugeukwa na kuingia kwenye mateso makubwa. Aliwauliza nani katika serikali ile alikuwa rafiki wa karibu na Rais Costa kuliko yeye? Na je wanajua kilichompata?

Alimalizia kwa kuwaambia kuwa ili kutoka katika hali ile inahitajika juhudi za mmoja mmoja na sio kutegemea wengi. Wao kwa nafasi zao wapo kwenye nafasi nzuri za kuhakikisha Rais Costa anapumzishwa nje ya madaraka na marekebisho makubwa ya kimfumo,kisera na kikatiba yanafanyika kwa maslahi mapana ya wana Stanza. Joe aliongea kwa hisia, na baada ya kumaliza Habibu na Pius walionekana kuanza kuelewa.
“Kwa hiyo kwenye mpango huu upo na nani?”, Pius alihoji. “Ni mapema sana kuwaambia. Kwanza nilitaka nipate nafasi hii kuwapa huu muhtasari na kutaka utayari wenu kisha nitawaambia wote waliopo kwenye mkakati huu” Joe alijibu.
“Kwa hiyo jambo hili linafanikishwaje”, Habibu alihoji. “Nitawaambia, but first, let’s focus on what brought us all the way here”. Joe alijibu akikusudia kufunga ule mjadala, na kabla hajamaliza muhudumu wa ndege aliwasogelea na kuwauliza kama kuna kitu wanahitaji. Waliagiza Chai. Joe na Habibu wakarudi kukaa kila mtu akionekana kujaa mawazo. Mawazo ya jinsi gani watampumzisha Rais Costa nje ya madaraka, nani ataongoza Stanza na nini kitafuata baada ya hayo?
*************************************
“Sikiliza Sylvester, haya sio makubaliano yetu. Ulinitoa Canada kwa ahadi kuwa unakuja kunipa Uwaziri, umeishia kunipa Ukatibu Tawala wa jimbo tena huku kijijini, kweli? Ungeniacha Canada kule kule bwana”. Alikuwa ni mrembo, Ketina, kimada wa Rais Costa akiongea nae kwa simu kutokea Jimbo la Kichumbi alikomteua kama Katibu tawala.
“Keti, mbona una haraka mpenzi? Hujakaa kwenye hiyo nafasi hata miezi sita unataka nikupe Uwaziri? Hatuendi hivyo mpenzi wangu. Subiri angalau umalize mwaka nitakupa Ubunge kwa kutumia nafasi zangu kwa mujibu wa katiba halafu utaanza na Unaibu Waziri”. Rais Costa alijibu kwa utaratibu na kubembeleza.
“Nani asubiri mwaka mzima Costa? Mimi Keti au nani? Wachezee hao hao watu wako wa Stanza sio mimi. Hakuna linaloshindikana ukiamua. Wewe ni mtu mwenye nguvu kuliko wote chini ya jua la Stanza. Katiba imekupa mamlaka ya kuamua uzima na kifo cha yeyote nchi hii sembuse kunipa uwaziri mimi? Ketina alichachamaa.
“Kwanza ndani ya siku mbili tatu hizi nitakuja Peron kuonana na wewe nimeku miss”, Ketina alimalizia kwa sauti ya upole. Alimtaarifu Rais Costa kuwa anakuja Peron mji mkuu wa Stanza ilipo Ikulu ya Rais Costa kwa ajili ya kuonana nae.
“No, no Keti, I have pressing issues that I am dealing with right now. I will tell you when to come” (Hapana Keti, nina masuala nyeti ninayoshughulikia sasa hivi. Nitakwambia lini uje), Rais Costa nae alijibu kwa upole.
“Midts of your pressing issues, you can always slot a time to hang on with your bae, aren’t you Mr. President?”. (Hata katikati ya masuala yako nyeti huwezi kukosa muda wa kukutana na mpenzi wako, au sio Mh. Rais?). Ketina aliongea kwa sauti ya kimahaba iliyomlainisha Rais Costa. “Aaa…. aaaa. Ok Keti just come”, (Aaaa…. aaaaa. Sawa Keti njoo basi). Rais Costa alijikuta anakosa kauli. “That’s my baby” (Huyo ndio mpenzi wangu), Ketina alimalizia na kukata simu.
***************************************
Kwa macho na mbele ya wananchi na watendaji wa Serikali, Rais Sylvester Costa alikuwa akionekana mkali na mtu asiesogeleka. Ilikuwa ni ngumu kumwangalia machoni mara mbili akiwa anaongea na wewe. Hata watendaji wa serikali ikiwemo na mawaziri wake huongea nae wakiwa wameinamisha kichwa. Alikuwa mkali na mbabe kwelikweli.
Ketina Nikodemas, msichana mdogo kiumri aliyekutana nae nchini Canada miaka mitatu iliyopita katika moja ya ziara zake, ndiye pekee aliyeweza kumuendesha Rais Costa jinsi alivyotaka. Ketina akiwa nchini Canada kumalizia masomo yake ya Uzamili alionana na Rais Costa na katika kumsalimia, Rais Costa alivutiwa nae na hivyo kuagiza kuonana nae Hoteli aliyofikia.
Rais Costa alianzisha mahusiano na binti Ketina na hakika binti huyu alijua kumteka Rais. Ni katika mapenzi hayo ambapo Ketina alitaka apewe Uwaziri na hivyo Rais Costa alimrudisha nchini Stanza na kuanza kwa kumpa Ukatibu Tawala wa jimbo.
Ketina hakufurahishwa na uteuzi huo na sasa alikuwa akimlazimisha Rais ampe Uwaziri kamili. Hakuna aliyekuwa akijua kinachoendelea nyuma ya pazia kati ya Rais Costa na Ketina isipokuwa kwa wafanyakazi wachache wa Ikulu hasa vijana wa Usalama wanaotumiwa na Rais kupanga na kuandaa mazingira ya kukutana kwao mara kwa mara sehemu mbalimbali.
**********************************
Je, Habibu Na Pius Wamemuelewa Joe?Vipi Kuhusu Rais Costa Na Chriss Donald Wa Marekani?Vipi Kimada Ketina?.....
 
Back
Top Bottom