Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,708
Alipoamua siku hiyo kuwa karibu na msichana anayehudumu katika klabu ya Tanga Raha, Jackson Malima ambaye pia alipachikwa jina la ‘Baba Mchungaji’ na wafanyakazi wenzake, hakujua kwamba hatua hiyo ilikuwa chanzo cha mlolongo wa matatizo lukuki; ndoa yake kutetereka, cheo cha ukurugenzi alichopaswa kupewa kuchukuliwa na mtu mwingine, na baya zaidi ni kujikuta akituhumiwa kwa mauaji ambayo hayajui…
Kutoka kwa mtunzi wa 'Gereza la Kifo'
Simu: 0758 143457
JACKSON Malima, alitoka bafuni na kuangalia saa yake iliyomwonesha kwamba inaelekea saa mbili usiku. Akiwa bado amejifunga taulo, aliamua kuangalia taarifa ya habari kabla ya kutoka kama alivyokuwa amepanga.
Kwa takribani siku sita alizokuwa Tanga, alikuwa hajaangalia taarifa ya habari ya usiku kama ilivyo kawaida yake anapokuwa nyumbani kwake Dar es Salaam kutokana na kubanwa na ratiba.
Alipokuwa akitoka kwenye semina jioni, alilazimika ama kuandaa kile atakachowasilisha kesho kwenye semina au kwenda kutafuta chakula cha usiku alikotumia muda huo kubadilishana mawazo na wenzake.
Alishagundua kwamba pale kwenye klabu alipokuwa akienda kupata chakula cha usiku, mbali na kukosa utulivu hata kama angeomba wahusika waweke taarifa ya habari wasingemwelewa kwani kilichokuwa kinapendelewa zaidi na wengi ni mpira wa miguu au muziki.
Aliwasha seti ya runinga katika chumba chake alimofikia katika nyumba ya kulala wageni ya Twiga Executive Lodge na kuketi kitandani.
Taarifa ya habari ilimkaliza chumbani humo hadi saa tatu kasorobo alipozima runinga. Alivaa suruali ya michezo, tisheti ya rangi ya maziwa na raba kisha akatoka baada ya kuhakikisha kwamba hajasahau kuchukua fedha kidogo kwa ajili ya matumizi ya usiku huo.
“Binti, natoka kidogo,” alisema akikabidhi funguo za chumba chake kilichokuwa kimepewa jina la Kigoma kwa binti aliyekuwa mapokezi. Akaondoka.
Nyumba ya kulala wageni aliyofikia, kama zilivyo nyingine nyingi mjini Tanga, ilikuwa haiandai chakula cha mchana wala usiku zaidi ya kifungua kinywa asubuhi. Wateja walikuwa wakielekezwa kwenda kutafuta chakula katika hoteli, klabu au migahawa ya karibu.
Chakula cha mchana, Jackson na wanasemina wenzake walikuwa wakikipata katika Hoteli ya Kitalii ya Mkonge walikokuwa wakifanyia semina yao ya wiki moja ambayo sasa ilikuwa inaelekea ukingoni, huku yeye na wenzake wakilazimika kujitafutia chakula cha usiku. Jackson alikuwa ameamua kukaa katika nyumba hiyo ya wageni kutokana na kuwa eneo tulivu huku wenzake wanne aliotoka nao ofisi moja wakiamua kukaa katika nyumba za wageni zilizoko katikati ya jiji la Tanga.
Hao wenzake walikuwa wanywaji wa pombe na wapenda wanawake lakini yeye alikuwa akijitahidi sana kujitenga na mambo hayo, hali iliyofanya apachikwe na baadhi ya wafanyakazi wenziye jina la Baba Mchungaji.
Hata hivyo, baada ya semina mara nyingi alikuwa anakutana na wenzake hao pamoja na wanasemina kutoka taasisi zingine zilizokuwa zinashiriki kwenye semina hiyo usiku katika klabu ya Tanga Raha ambayo haikuwa mbali sana na alikokuwa amefikia.
Klabu hiyo ilikuwa inachangamka sana, hasa nyakati za usiku kutokana na kuandaa vyakula vya aina mbalimbali pamoja na vinywaji. Lakini kitu kilichokuwa kinavutia wateja wengi hususani wanaume ni uwepo wa wasichana warembo, wengi wakiwa ni wale waliojaaliwa kuwa na maumbo halisi ya Kiafrika.
Wasichana vimbaumbau pia walikuwepo wachache lakini wengi walikuwa ni wale ambao utadhani meneja wa klabu hiyo alikuwa akipita nchi nzima akisaka mabinti warefu, wenye sura za kuvutia na makalio makubwa.
Ilikuwa wastani wa takribani dakika nane kutembea kwa miguu kutoka nyumba ya wageni alimofikia Jackson hadi Tanga Raha Club kama bango lake lilivyokuwa linasomeka.
Wakati Jackson anafika kwenye klabu hiyo usiku huo, nje kulikuwa na magari mengi kiasi kwamba yeyote aliyekuwa akija kwa gari muda huo alilazimika kwenda mbali kidogo kuegesha gari lake. Ndani pia palikuwa tayari pamejaa watu kiasi kwamba upatikanaji wa viti ulianza kuwa wa shida.
Jackson alisimama pembeni karibu na mlango mkubwa akiangaza mahala ambapo anaweza kuona kiti aende kukaa. Kwa kawaida mwanga wa ndani ya klabu hiyo ambayo mchana ukipita unaweza kudhani ni godauni au gereji, ulikuwa si mkubwa sana. Wakati mwingine mpaka umkaribie mtu ndipo unamtambua.
Aliangaza huku na kule akitafuta pia kuwaona wanasemina au wafanyakazi wenzake katika Tume ya Teknolojia na Mawasiliano (TTM) ili kuungana nao lakini hakuona yeyote, labda kutokana na mwanga hafifu wa mahala pale. Alikuwa hana hakika pia kama mfanyakazi mwenziye na rafiki yake wa karibu, Andrew Mambo, alikuwa ameshawasili. Alisogea pembeni na kupiga simu yake lakini hakupokea.
Mara aliona wanasemina wawili wakiongozana na walipofika pale alipokuwa amesimama karibu na mlango, wakamsalimia. Wakasema wanahamia kwingine. Alipoangalia mahala walipotokea, akaona watu wengine wakiwahi viti walivyoviacha. Ilikuwa ni sehemu ambayo wapenzi wa mpira wakikaa wanaona vizuri kutokana na skrini kubwa iliyokuwa mahala hapo.
Wakati bado anaangaza macho huku na kule, msichana mmoja, mhudumu wa klabu hiyo, alimfuata na kumshika mkono.
“Habari kaka… Twende nikuoneshe mahala pa kukaa.”
Jackson aliandamana naye, hiyo ikiwa ni mara ya tatu au zaidi kuhudumiwa naye na sasa bila shaka kila mmoja wao alikuwa ameshamkariri sura mwenzake. Ni msichana ambaye kwa mtazamo wake alikuwa mrembo kupita wote katika klabu hiyo. Hata siku ya kwanza alipomwita amhudumie, binti huyo maji ya kunde ‘alimtikisa’ vilivyo Jackson lakini akaheshimu maadili aliyojiwekea.
Ukiwa ni mwaka wa 15 tangu afunge ndoa, Jackson alikuwa hajawahi kwenda nje ya ndoa yake. Mbali ya kumwogopa Mwenyezi Mungu anayewakataza viumbe wake kuzini katika vitabu vyake vyote, Biblia na Kurani, Jackson alikuwa hafikirii kwamba kuna siku atamsaliti mkewe mpenzi, Salome Bakunda. Ni mwanamke aliyempenda na kumridhisha kwa kila hali na hivyo hakuona sababu ya kuchepuka kama alivyokuwa akiona kwa wenzake akiwemo rafiki yake, Andrew.
Isitoshe, yeye alikuwa mshauri mkubwa wa wafanyakazi wenzake, hususani vijana waliokuwa wakianza kazi katika ofisi yao kuhusu kuzingatia maadili bora ya kazi, kujiheshimu, kuacha zinaa na kufanya yanayompendeza Mwenyezi Mungu.
“Kaka, inaonekana wewe hunywi lakini nadhani leo utanipa offer ya bia moja tu, yaani nina kiu sana kaka yangu… Nakuomba,” alisema yule binti baada ya kumpeleka kwenye meza moja iliyokuwa kwenye kona, upande wa kulia wa klabu hiyo kutoka lango kuu la kuingilia. Katika meza hiyo kulikuwa na viti vingine viwili vitupu lakini kule eneo la kuingilia alikokuwa amesimama awali alikuwa hawezi kupaona.
“Bia moja tu mdogo wangu, haya, nitakununulia...”
“Asante sana kaka… Enhe, nikuletee nini?”
“Nitapata kuku nusu wa kienyeji wa kuchoma na ndizi mzuzu mbili za kuchoma pamoja na mbogamboga?”
“Bila shaka kaka,” alijibu yule msichana akiachia tabasamu pana lililoanza kumgusa Jackson. Alitoa Sh 20,000 na kumuuliza kama kiasi hicho cha fedha kinatosha chakula alichoagiza na bia aliyoomba. Alijibu kwa bashasha kwamba kinatosha sana.
“Je, nikitaka soda pia ili niwe navutia muda wakati nasubiri kuku wangu, pesa inatosha?”
“Bado inatosha na chenji inarudi.”
“Basi niletee soda ya moto,” alisema kisha msichana yule ambaye muda wote alikuwa amesimama, akageuka na kuondoka.
Sasa Jackson, Mwanasheria Mkuu wa Tume ya Teknolojia na Mawasiliano (TTM), alipata wasaa mzuri wa kumtazama kwa nyuma na kung’amua kwamba uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu ulikuwa umekamilika vilivyo kwa kiumbe wake huyo.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia riwaya hii ya kusisimua...