NTAGAMBI.......15
Mtunzi; Lovi Pius Kijogoo.
0757 238 304.( WHATSAP )
0622 738 310.
0713 417 189.
Tanga.
SEHEMU YA KUMI NA
TANO.
( 15 )
ILIPOISHIA...
"Wahhhhhh.! Wahhhhh" mtoto alilia tena kwa sauti ya maumivu. Lakini awamu hii tumbo lilikuwa likivimba, pamoja na miguu. "Uchungu wa mwana aujuaye mzazi" Chidumu alishindwa kuvumilia, nae akaanza kulia. Ntagambi akawa na jukumu la kuwabembeleza wote wawili.
ENDELEA NAYO......
"Kuna majani kama yale, mama aliwahi nipaka. Nikiwa nimeugua ugonjwa wa ajabu usioeleweka" kumbukumbu hiyo ilimuijia ghafla Ntagambi, akakimbia na kuyachuma majani hayo. Akampaka mwanaye kwa utulivu. Dakika thelathini tu zilitosha kumrejesha mwanaye katika hali ya kawaida.
Kwa mara nyingine tena, Chidumu anatabasamu. "Hii misukosuko itakwisha lini?" Chidumu aliuliza. "Haya ni mapito tusikate tamaa!" alijibu Ntagambi. "Lakini kwa yale tuliyoshuhudia usiku, hapa pia si mahali salama!" alieleza Chidumu. "Ni kweli, usemalo. Nipo hapa naumiza kichwa ni wapi tuelekee. Tupo katika nyakati ngumu, uvumilivu ndio silaha pekee itakayotukomboa" alizidi kusisitiza Ntagambi.,
Upepo mkali ulikuwa ukivuma. Vumbi nalo lilizidi kutimka na kuzunguka kwa kasi ya ajabu huku likiikusanya kila aina ya taka. Tufani! Miti iliinama na kuinuka. Shwiii shwaaa zikisikika kule na huko. Ndege angani wenye rangi za kutamanisha na kuliwaza kwa pumbazo la kibakunja, hawakuachwa nyuma. Waliruka huku wakiziachia mbawa zao kwa madoido. Ni dhahiri walikuwa wakiikaribisha siku ya kipekee. Siku ambayo iliaminika vuli zingeungana na kuleta mvua kubwa ya masika....
Hiyo ndiyo hali ya hewa iliyokuwepo porini hapo. Ilikuwa ni siku ambayo Ntagambi aliamini ilishiba matumaini, na uzao upya wa maisha ya familia yake.
Himaya ya ardhi ya Omulenga.
Huzuni ilitanda, vilio visivyo na mwisho vikalipamba anga hilo. Malkia alikuwa katika mateso mapya. Kila alipokuwa anamkumbuka mwanaye, alilia sana, na kupoteza fahamu.
"Yuko wapi mwanangu jamani? damu yangu! kipenzi changu!. Ukute anateseka huko alipo! moyo wangu unaumia. Nateseka mimi, masikini ya Mungu. Sijui mwanangu kauawa au laa" alilamika Malkia. Machozi yakiwa yanambubujika bila simile.
Mfalme Bunini nae alikuwa hoi. Usiku na mchana askari walizunguka, kumsaka Chidumu. Walitamani ni bora wakaupata hata mwili wake akiwa mfu. Kuliko kuendelea kumtafuta pasi mafanikio.
"Natoa siku tatu za mwisho. Binti yangu apatikane!" alifoka kwa hasira mfalme. "Na yule kijana, tuliyemtoa gerezani akamtafute binti yangu. Kisha hajaonekana mpaka leo, mleteni hapa akiwa mfu!" alimalizia kuzungumza mfalme.
Ni wakati mgumu tena kwa askari. Njia na wao, wao na njia. Awamu hii walidhamiria kweli, kwamba liwalo na liwe. Walitumia farasi, wakiibeba mishale ya sumu. Mbwa wa kunusa harusu walitangulizwa mbele.
"Kwa taarifa tulizopata, alikimbilia katika pori hili!" alizungumza mkuu wa msafara huo.
"Huyu mbona tutampata tu!" alidakia askari wa pili.
"Twendeni tukakague pale, unaona mbwa wamekatali papo huku wakibweka" alizungumza askari wa tatu. Walipofika hapo wakakuta ni kama kijumba kimejengwa. Naam! ni kile kijumba cha awali alichokijenga Ntagambi, kisha akaondoka.
"Inavyoonekana huyu mtu aliishi hapa. Kasikia tunakuja kakimbia, najua hayupo mbali na hapa, tusonge mbele" ilikuwa ni sauti ya mkuu wa msafara akitoa amri.
Waliendelea na safari. Mishale ikiwa tayari kufyatuliwa kwa adui yeyote yule, ambaye angelikatiza mbele yao. Hii ya sasa ilikuwa ni kufa na kupona. Walijiapiza ni lazima Ntagambi apatikane, na binti mfalme pia.
"Twendeeee, twendeni, tupambane mpaka mwisho. Twendeeeni, tusichoke nasema twendeeee. Twendeeeni. Tuipiganie ardhi ya Omulenga, twendeni." askari walikuwa wakiimba njiani. Wakatamani angepatikana mtu kama marehemu mzee Moris mwenye uwezo wa kupiga ngoma kumi, ingependeza sana. Nyimbo hizo ziliwaongezea morali ya kuzidi kusonga mbele bila ya kuchoka. Yalibaki masaa kadhaa waweze kuikanyaga ardhi ya pori jipya lenye mandhari ya kipekee kabisa.
"Kwa hapa tuongeze umakini zaidi. Huyu mtu hayuko mbali!" alizungumza mkuu wa msafara. Wakapeana majukumu, wakajigawa katika makundi matatu. Kisha wakatawanyika kila kundi na upande wake. Anga lilikuwa limetulia tuli. Likawapa wepesi wakupanga mipango yao. Waliuchagua mwendo wa kunyata, ili adui yao asipate kushtuka na kujipanga zaidi yao.
Askari walianza kufyatua mishale ovyo. Wakawa wanafunga mitego katikati ya miti. Wakatengeneza na mabomu ya kienyeji ya kurusha. Lakini katika pori hilo. Walikuwa wakisikia kama watu wanalia, wengine wanaimba na kushangilia. Wakatafuta zinapotokea sauti hizo, lakini hawakufanikiwa.
"Mnasikia hizo kelele! zinatokea wapi?" alinong'ona kwa sauti ya chini kabisa askari mmoja. Wakiwa bado wanatafakari hilo. Awamu hii wakasikia kama mtu anachapwa fimbo na kulia kwa sauti ya juu. "Mniacheee!! mniacheee" sauti hiyo ilisikika hivyo.
"Mishale juu, tembea chini. Tumbo kwa nyasi, kidevu kwa ardhi. Tambaa kwa utayari, kaza mkono. Elekeza mshale kila Kona, haya tusonge" alitoa amri kiongozi wa msafara. Ikaanza kufyatuliwa mishale ya sumu. Sauti hizo za watu wasioonekana ziliwachanga Sana.
"Kipenzi changu! hapa si mahali salama kwetu" alizungumza Ntagambi.
"Ngoja tukae hizi siku mbili, kisha tuone tunaelekea wapi!" alijibu Chidumu.
"Huoni kama itakuwa hatari kwetu?" alihoji Ntagambi.
"Kikubwa tuwe makini sana!" alijibu Chidumu.
"Basi haina neno, andaa chakula, tuweze kula mapema!" alizungumza Ntagambi.
Chidumu aliamka na kwenda nje kuandaa chakula. Wakati huo Ntagambi aliutumia kunoa panga lake. Mapigo ya moyo yalimuenda mbio, akahisi hali ya usalama si shwari. Akaamua kujipanga mapema kwaajili ya usalama wa familia yake pendwa.
Chidumu aliingia ndani kuchukua kibakuli. Aliporudi anakuta kivuli cha mtu kimesisima lilipo jiko. Alipotokeza tu kivuli kile kilikimbia. Alishtuka ila akajua labda hajaona vizuri. Basi akaendelea na upishi. Alipika mboga za majani za porini na ugali kidogo. Walianza kula huku walikumbushana siku ya kwanza kuonana. Wakacheka sana huku wakigonga mikono yao kwa pamoja.
Walivyomaliza kula, zikapita dakika thelathini. Matumbo yaliwavuruga, si Chidumu wala Ntagambi. Walianza kutapika ovyo.
"Hiki chakula umeweka nini?" aliuliza Ntagambi, akiwa ameuweka mkono wake kinywani kuyakabili matapishi.
"Sijaweka kitu chochote!" alijibu Chidumu. Nguvu zilikuwa zimemuishia sababu ya kutapika. Maumivu makali ya tumbo yaliwakabili. Ntagambi akawa anajikaza huku anaumia. Chidumu alipoa akajikunja akiwa amelishika tumbo lake.
"Mwanangu nakuacha peke yako! naondoka mwanangu! tumbo, tumboooo, mama ayiiiiii. Aaah! nitunzie mwanangu, naumiaaaa, nipeleke kwa mama kabla sijafa" alilamika Chidumu akiwa analia, maumivu yalikuwa makali, akashindwa kuvumilia akapoteza fahamu.
Mtoto nae alianza kulia, Ntagambi mkono mmoja akilishika tumbo lake lililojawa na maumivu. Mkono mwingine akimpepea mkewe. Mwanamke kazimia, atamnyonyesha vipi mtoto apate kunyamza. Ulikuwa ni mtihani kwa Ntagambi.
Ntagambi nae hali ilizidi kuwa mbaya, tumbo likawa litatowa ngurumo kama za radi, akawa anamuangalia tu mtoto akilia. Nguvu za kumbeba hakuwa nazo tena.
"Uzito wa kudra za mateso umenipiga dafrau, kama tamviri. Nimeyumbishwa, sina wa kunisitiri, nayaona maisha kama laana. Naishia kusema laiti ningelikufa mapema." aliongea kwa uchungu mkubwa sana Ntagambi. Huku akiwa analia.....
********* ITAENDELEA ********