Simulizi; Nitamlea

NITAMLEA
Mtunzi, Robert Heriel
Chungu Cha 09

Usiku uliofuata Johari hakulala. Alikuwa analala huku macho yakiwa wazi, moyo wake ukiwa kama mtu aliyedondoka baharini bila kujua kuogelea. Ndani alimuangalia Neema aliyekuwa amejifunika kwa kitenge kilichokuwa kimetoboka huku akikoroma kwa uchovu wa mtoto mdogo asiye na makosa. Machozi ya Johari yalitiririka kimyakimya. Alihisi dunia imemchoka. Kila njia aliyojaribu haikufika popote. Alijitahidi, alihangaika, aliomba dua, alifanya kazi lakini bado mwisho wa siku anabaki mtu wa kudharauliwa na watu wa mtaani. Mtu wa kukosa hata chakula Cha yeye na bintiye.

Kesho yake hakwenda kuuza uji, hakuwa na mtaji tena. Hakuwa na hata mia moja. Alikaa ndani, akimwangalia Neema akichezea kijiti akisema anapika chakula. Wakati mchana unaingia, mwenye nyumba aligonga mlango kwa nguvu. “Johari, toka kabla sijaita mgambo! Siku zako tatu zimeisha!” alikoroma kama mbwa aliyekosa mfupa.

Johari alifungua mlango polepole, macho yakiwa yamevimba kwa kulia. “Baba mwenye nyumba… nisaidie wiki moja tu, wiki moja nipate pa kuhamia.”
Mwenye nyumba alicheka kwa dharau, “Hayo siyo maisha yangu dada, nachotaka ni kodi yangu! Ukishindwa… toka!”

Johari alifunga mlango huku akitetemeka. Hakuweza kula siku hiyo, wala hakumwandalia Neema kitu cha maana. Alimwekea maji tu na kipande cha maandazi kilichobaki kwenye chakula cha jana.
Wakati wa jioni, akaamua kutembea mtaani angalau apate mawazo ya Nini afanye. Wakati anakatiza mtaa wa pili, akamuona mzee mmoja amekaa chini karibu na duka la dawa, suruali yake ilikuwa imechanika, lakini uso wake ulikuwa na amani ya ajabu. Mzee alimwangalia Johari na akasema kwa sauti ya taratibu lakini yenye uzito: “Binti, hata mtu akizama baharini, ilimradi haujafa bado ana nafasi ya kuona pwani.”


Johari alisimama, akageuka. “Umesema nini mzee?”
Mzee akajibu kwa tabasamu, “Tumaini lipo. Jua linawaka hata kama mawingu yametanda. Ukiona kivuli, jua kuna jua nyuma ya giza.”

Johari hakujua kwa nini machozi yalibubujika. Alijikuta amekaa karibu na huyo mzee na kuanza kusimulia maisha yake yote, kuachwa na baba wa mtoto wake, kufukuzwa kazi, kufilisiwa mirathi, kupoteza kila kitu. Alimsimulia kwa machozi matupu. Baada ya dakika thelathini mzee akanyanyuka, “Binti nakuomba… kama bado unayo miguu ya kutembea na mdomo wa kusema… usikate tamaa. Nenda pale Kariakoo kona ya msikiti wa Manyema, kuna dada mmoja anatafuta mtu wa kufanya kazi ya usafi wa hoteli yake ndogo. Ni kazi ya jioni na asubuhi, unalala ndani na unapata posho ndogo lakini inasaidia.”

Johari hakuamini. “Una uhakika mzee?”
“Si lazima niwe na uhakika,” mzee akajibu kwa busara, “lakini tumaini halina gharama, jaribu.”
Johari alirudi nyumbani na Neema akiwa amebeba matumaini mapya. Hata kama yalikuwa madogo kama punje ya chumvi, moyo wake ulihisi joto jipya.

Alipoamka alfajiri, alienda Kariakoo kama mzee alivyomwelekeza. Alifika kona ya msikiti wa Manyema, akatafuta hoteli ndogo iliyoandikwa “Amani Lodge”. Alipofika, alimkuta mama mmoja mwenye umbo kubwa akiwa anapanga vyombo.
“Asalaam aleykum mama,” Johari alisalimia kwa unyenyekevu.
“Wa aleykum salaam, unahitaji nini?” yule mama akauliza kwa sauti ya amri.
“Nimesikia kuna kazi ya usafi hapa… natafuta kazi,” Johari alijibu kwa unyenyekevu mkubwa.
Mama wa hoteli alimkagua juu mpaka chini. “Una mtoto?” aliuliza.
“Ndiyo, lakini atabaki kwa jirani, sitaleta shida,” Johari alijitetea.
Baada ya ukimya mfupi, mama wa hoteli alitikisa kichwa, “Njoo kesho saa kumi na mbili asubuhi. Utaanza kazi ya kupiga deki na kusafisha vyumba vya wageni. Siyo kazi rahisi, lakini bora kuliko kukaa njaa.”

Johari hakuamini. Hakukumbuka mara ya mwisho aliambiwa ‘karibu’ kwenye kazi. Alimshukuru mama wa hoteli, akaondoka akiwa na mwanga mdogo wa matumaini.
Lakini aliporudi nyumbani, alikuta mwenye nyumba akiwa na watu wawili, mgambo. “Nimechoka na huyu mwanamke, leo anatoka kwa lazima!” Johari alilia, akaomba lakini hakuwa na msaada. Akapewa dakika ishirini kuchukua virago vyake. Alimfunga Neema mgongoni na kubeba godoro lake chakavu.

Wakiwa hawana pa kwenda, walilala kwenye kituo cha daladala ya Kinyerezi, kwenye benchi la mbao. Usiku ulikuwa na baridi, mbu walikuwa kama wanamla moyo wake. Lakini angalau alikuwa na matumaini kuwa kesho ana kazi.

Johari akajifunika na kitenge alichokuwa nacho, akamkumbatia Neema kwa nguvu huku machozi yakitiririka kimyakimya usiku kucha.
Asubuhi alijikaza, akasali kimyakimya, kisha akaelekea kwenye kazi mpya Amani Lodge akiwa na matumaini mepesi kama jani linalopeperushwa na upepo, lakini moyo wake ukiwa mgumu kama jiwe la kusaga.
*****
Siku ya kwanza ya kazi ilimkuta Johari na Neema wakiwa wamebanana kwenye viti vya lodge, wamekaa kama wageni wanaosubiri huduma. Johari alikosa pa kumwacha Neema. Alihangaika kutafuta jirani wa kumwachia lakini hakuna mtu aliyetaka kujitwisha mzigo wa mtoto wa mtu. Alijua kabisa kazi ya hoteli siyo mchezo, lakini hakuwa na namna. Kuliko kumwacha Neema apotelee mitaani, bora amchukue kazini.

Dakika chache baadaye mama mwenye lodge, Mama Halima, alitokea akiwa amevalia dera la rangi ya kijani kibichi, kitambaa kichwani na buti ndefu miguuni. Alimkazia Johari macho, macho ya mtu mwenye miaka mingi kwenye mtaa, anayejua kuchuja watu kwa sekunde tano tu.

"Johari! Ulisikia nilichokuambia jana eeh? Kazi ya lodge siyo sehemu ya kuleta watoto! Hapa watu wanashinda wakiwa na stress, wengine wakiwa na wanawake wa mtaani… Unaleta mtoto hapa atasikia maneno mabaya. Sitaki stress za watoto hapa," alifoka kwa sauti ya kutisha.
Johari alitetemeka, mikono ikatetema vibaya. Alimshikilia Neema kwa nguvu, machozi yakianza kutiririka. “Mama Halima… tafadhali… sina pa kumwacha mwanangu. Nimehangaika… hakuna wa kumchukua. Nitafanya kazi vizuri, hata kama ni kuosha vyoo nitafanya. Huyu ni damu yangu… sitaki kuachana naye. Tafadhali… tafadhali sana.”

Mama Halima alinyamaza. Akamwangalia Neema ambaye alikuwa kakaa kimya, macho yakiwa yametulia. Mtoto huyo hakulia, hakuwa na vurugu, alikuwa mpole. Hali hiyo ilimgusa mama Halima kwa namna ambayo hata yeye hakuelewa. Akakunja sura, akahema kwa nguvu.

“Usinililie hapa! Mimi sipendi drama za wanawake. Leo kazi ni ya majaribio. Ukifanya kazi vizuri bila malalamiko ya wateja, utanisihi mwenyewe nikuache umlete huyu mtoto. Lakini nikisikia shida… nakutoa hapa papohapo.”
Johari alijikuta akipiga magoti kwa shukrani, akambusu mkono mama Halima. “Asante mama, Mungu akuzidishie riziki,” alisema kwa sauti ya unyonge.

Siku ya kazi ilianza. Johari alipiga deki hadi sakafu ikang’aa kama kioo. Alisafisha vyoo mpaka hata mende walishangaa. Wateja waliridhika. Mama Halima alikuwa anapita mara kwa mara kuangalia, lakini hakusikia lawama yoyote. Neema alikuwa akikaa pembeni kwenye kona ya mapokezi, mara nyingine akisaidia kufuta meza kwa kitambaa kidogo.

Mwisho wa siku, Mama Halima alimuita Johari na kumpa noti kumi za elfu kumi, akasema, “Hiyo ni advance ya mshahara wako wa mwezi… ninaona unajitahidi. Ukiendelea hivi utakuwa mtu wangu wa nguvu”
Johari alishindwa kujizuia, alilia kama mtoto mdogo. Alimwambia Neema, “Unaona mwanangu… mwanga umeanza kutokea.”
Baada ya kazi ya siku tatu mfululizo, Johari aliamua kutumia sehemu ya hela ile kupanga chumba cha kawaida kule Manzese. Alienda akakodi chumba kidogo cha giza kisicho na umeme. Chumba kilikuwa kimepinda ukuta, hakikuwa na umeme lakini kilikuwa salama. Walikula mihogo ya kukaanga wakashukuru Mungu kwa hatua ya kwanza.

Wiki mbili zikasogea, Johari alianza kuona maisha yanabadilika. Akawa anaweza kununua unga wa sembe, maharage, hata sabuni ya kufulia. Alikuwa anatoka kazini na kurudi akiwa na tabasamu dogo usoni. Alianza kufahamiana na wafanyakazi wenzake akawa mtu wa kupendwa lodge nzima.

Siku moja wakati wa kazi ya usiku, alikuja mteja mmoja kwenye lodge, kijana mwembamba, wa miaka ya kati, mwenye suti safi na perfume ya kuvutia. Aliomba chumba, akapewa namba 9, akakaa siku mbili mfululizo. Johari alikuwa ndiye wa kufua nguo zake, kusafisha chumba chake na kumletea kahawa ya asubuhi. .Kijana huyo alikuwa anaitwa Lucas Lakini sio mwashambwa. Alikuwa ni fundi wa magari, mwenye gereji kubwa pale Buguruni. Lakini alikuwa pia mtu mwenye roho nzuri. Siku ya tatu alimwambia Johari, “Mrembo, sijawahi kuona dada anayefanya kazi kwa roho ya dhati kama wewe. Kila nikikuangalia unaweka moyo wako kwenye kazi.”Johari alishusha macho, kwa sababu hakuwa na mazoea ya maneno ya wanaume. Aliamua kuwa mkweli. “Nina binti, ndio kila kitu kwangu. Sifanyi kazi kwa kujipendezesha, nafanya kwa kutafuta chakula cha mwanangu.”

Lucas alishangaa. “Una mtoto?”
“Ndiyo, Neema. Ana miaka miwili na miezi saba,” Johari alijibu kwa unyenyekevu.
Lucas alimtazama Johari kwa macho yenye huruma. Akasema, “Nitakuwa nakuja hapa mara kwa mara. Najua mateso ya maisha yanavyotafuna watu wa aina Yako, single mother. Nikija sitaki upige deki kwenye chumba changu, utakuja kukaa tupige stori.”

Johari alicheka, akasema, “Sawa bosi. Tuko pamoja.”
Lucas alianza kuja mara kwa mara. Kila akija alikuwa na zawadi ndogo kwa Neema, aidha pipi, aidha uji mzuri wa watoto au mchele kidogo kwa ajili ya nyumbani. Polepole moyo wa Johari ukaanza kubadilika. Aliyewahi kusema hatapenda tena, akaanza kuona kuna watu bado wana moyo wa ubinadamu.
Mwezi mmoja na nusu ulipofika, Lucas aliamua kusema kilichokuwa moyoni mwake. Siku hiyo alikuwa amekuja lodge akiwa na zawadi ya gauni jipya la mtoto na kilo mbili za mchele.
“Johari, sina maneno mengi. Najua maisha yamekupiga sana. Sijakuona kwenye mavazi ya fahari lakini nimeona tabia yako. Sikujali kwa sura yako, nimependa moyo wako. Kama uko tayari, nataka nikuoe.”

Johari alitetemeka. Alishindwa kujizuia. Aliangalia maisha yake jinsi yalivyomfinya, jinsi alivyoishi kwenye mto wa machozi bila msaada. Huyu kijana mzuri alikuwa anaona thamani kwenye moyo wake, sio mwili wake. Ilikuwa ndoto iliyokuwa haipo kichwani mwake.

Lakini alikaa kimya. Alijua ni mapema. Alijua bado kuna mengi ya kujua kuhusu Lucas. Lakini kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu… moyo wake uliona mwanga. Neema alimkumbatia mamake, akasema kwa maneno yasiyoeleweka vizuri, “Mama atacheka sasa?”

Johari alicheka, macho yakiwa na machozi.

Ndani ya chumba chake cha giza Manzese, kwenye godoro lililochoka, Johari alijua safari mpya inaanza. Safari ya matumaini, safari ya upendo, safari ya maisha mapya.
**********

Siku zilianza kusonga, hazikuwa zimeganda kama awali, maisha ya Johari na Neema yakaanza kuwa na ladha mpya. Ingawa chumba cha Manzese kilikuwa cha giza, kilianza kupata mwanga wa matumaini. Johari alikuwa akiamka kila asubuhi na kwenda kazini akiwa na tabasamu, siyo kama mwanzo alipokuwa anakwenda kwa kulia na kuomboleza moyoni. Neema naye alizoea maisha mapya, alijua mama anarudi mchana na jioni akiwa na kitu angalau, hata kama ni mandazi au kipande cha sabuni, alikuwa na hakika kuna kitu kutoka kwa mama.
Lucas naye hakuacha kuonekana. Kwa wiki mbili mfululizo, alikuja lodge mara tatu, akizungumza na Johari kama rafiki, akimsikiliza, akimwelewa. Hakutaka kulazimisha penzi wala kumpa presha Johari. Aliamua kuwa mwanamume wa tofauti.

Siku moja Johari aliporudi kazini mchana wa Jumapili, Lucas alikuwa pale mapokezi, tayari ameketi akisubiri. Alimwambia Johari, “Leo huna haja ya kupiga deki wala kufagia. Leo ni siku yako ya mapumziko. Nimeshaongea na mama Halima. Kuna sehemu nataka twende.”
Johari alijaribu kupinga kwa heshima lakini Lucas alimsihi. Mama Halima naye alitabasamu na kusema, “Leo nenda kapate hewa, si kila siku kupiga deki hadi mikono igeuke.”

Johari alichukua khanga yake ya zamani, akamchukua Neema, wakaelekea Kariakoo walipokutana na Lucas kwenye gari lake dogo aina ya Passo. Johari hakuamini macho yake, ilikuwa mara ya kwanza kupanda gari binafsi baada ya muda mrefu. Lucas aliwapeleka kwenye mgahawa mdogo lakini safi, walikula wali na kuku, Neema akapata juice na keki. Walikaa hadi jioni wakizungumza mambo ya maisha. Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, Johari alicheka kutoka ndani ya moyo. Alihisi kama mwanamke, si mtumwa wa maisha.

Lakini baada ya siku kadhaa kurudi kazini, maisha yakamgonga tena kwa namna nyingine. Aliitwa na mama Halima na kuambiwa kuna mabadiliko kwenye lodge, baadhi ya wafanyakazi wapya wameshaajiriwa. Johari atahitaji kupunguza siku zake za kazi, atafanya shift moja tu kwa wiki tatu. Hii ilimaanisha mshahara wake mdogo utapungua zaidi.

Johari hakutaka kumuambia Lucas mara moja. Alijua asingeweza kuendelea kulipia chumba chake Manzese kwa kipato kidogo alichobakiwa nacho. Aliumia moyo wake ukavunjika tena, lakini hakutaka kurudi nyuma. Aliamua kurudi kwenye biashara yake ya uji kwa upande mmoja na kufanya kazi ya lodge upande mwingine.

Kwa msaada wa Lucas aliyemkopesha elfu themanini, Johari alinunua chupa za chai tano, ndoo moja, na sukari ya kuanzia biashara ndogo ya uji. Alianza kupika alfajiri kabisa na kwenda kuuza uji maeneo ya Magomeni kabla ya kwenda kazini jioni. Muda mwingi alikuwa amechoka sana lakini moyo wake haukukubali kukata tamaa.

Neema alizidi kukua, sasa alikuwa anaelewa dunia ilivyokuwa na magumu. Alimuangalia mama yake anavyohangaika kila siku, akisema, “Mama naweza kusaidia kusambaza uji?”

Johari alimkumbatia bintiye na machozi yakimtoka. “Mwanangu, sitaki maisha haya yakukondoe moyo. Sitaki maisha haya yakufundishe kukata tamaa. Utasoma, utakuwa mtu mkubwa, mama atapambana hadi tone la mwisho la damu.”

Lucas aliendelea kuwa karibu, alikuja mara kwa mara kusaidia hata biashara ya uji, alikuwa anampelekea Johari mchele au sabuni bila ya kujisifu. Alikuwa mtu wa vitendo, siyo maneno matupu. Johari aliona mabadiliko makubwa. Alijifunza kuwa upendo siyo maneno matamu bali ni vitendo vya msaada wa kweli.

Baada ya miezi miwili, Lucas alimwambia, “Johari, nimeanza mipango ya kuanzisha gereji yangu nyingine pale Gongo la Mboto, nataka unisaidie kuwa msimamizi wa ofisi. Wewe ni mtu mchapakazi, siogopi kukupa nafasi hii. Na pia… nataka tujenge maisha pamoja kama familia, si kwa huruma, bali kwa heshima.”
Johari alilia. Aliyapitia mengi, aliumizwa, alichekwa, alisahaulika, lakini hatimaye akaona kuna mtu aliye tayari kumpa nafasi mpya si kwa kumhurumia bali kwa kutambua thamani yake. Alimwangalia Neema na kumuambia, “Tumaini ni kweli halifi, hata maisha yakupige vipigo kiasi gani… mwisho wa siku kuna mtu atakutambua kwa thamani yako ya kweli.”

Johari akajua… safari ilikuwa bado ndefu, lakini hakukuwa na sababu ya
kuogopa tena.

ITAENDELEA…

Tunaingia Chungu Cha 10.
Twende tusiende,
Twedreee

Chuma kinakuja,..
Mtanisamehe Kwa arosto
 
NITAMLEA
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu Cha 10

Lucas alipompa Johari taarifa ya kusimamia gereji mpya pale Gongo la Mboto, Johari aliona kama ndoto ambayo hakutarajia kuiona katika maisha yake. Alienda kuikagua gereji ikiwa bado iko kwenye matengenezo, mafundi wakiweka mabati mapya. Lucas alimsindikiza huku akimshika mkono, walitembea wakizungumza kuhusu mipango ya biashara, jinsi watakavyojenga maisha yao kidogokidogo bila kuangalia nyuma.

Baada ya wiki mbili, Lucas alikuja usiku akiwa na uso wa kutabasamu tofauti na siku zingine, akaweka mkono begani mwa Johari, akasema, “Johari, sipendi michezo ya muda mrefu. Sipendi mwanamke wa maisha yangu kubaki kuwa ‘girlfriend’ miaka yote. Nataka nikuheshimu mbele ya dunia, nataka uwe mke wangu.”

Johari alinyamaza, macho yakijaa machozi. Aliamini hakutakuwa na mtu wa kumpenda tena kwa moyo wake wa dhati. Aliamini stigma ya kuwa single mother ni kifungo cha maisha. Lakini Lucas alikuwa amevunja ukuta huo kwa maneno machache, yenye heshima, yenye thamani.
Alichukua pumzi ndefu, akasema, “Lucas… ungeniambia hivi mwaka mmoja uliopita ningecheka, lakini leo… nataka niseme ndiyo. Lakini pia nataka ujue mbele yetu hakutakuwa rahisi. Najua uko na familia kubwa, najua historia yangu haijawahi kunisaidia, lakini moyo wangu uko tayari.”

Lucas alimkumbatia kwa nguvu, akasema, “Usijali… tutapigana kwa ajili ya upendo huu.”
Harakati za posa zilianza. Lucas alizungumza na familia yake, akawapa taarifa rasmi kuwa amepata mwanamke wa maisha yake na anataka kwenda hatua ya mbele. Mama yake Lucas, Mama Sada, mwanamama mwenye asili ya Kizaramo, mwenye maduka matano Kariakoo, mashamba Morogoro na apartment tatu Sinza, hakuamini masikio yake. Alikasirika, akaita kikao cha familia usiku huo huo.

“Lucas… wewe ni mjinga au umerogwa?” mama aliuliza kwa sauti ya matusi. “Umetoka kwenye familia ya heshima, tumehangaika kukusomesha, tumekutafutia mchumba wa maana… msomi, binti wa Daktari Katunzi wa Mikocheni, halafu unatuletea single mother kutoka vumbi la Manzese? Mtoto wa uji? Lodge?”

Lucas alinyamaza, alijua vita inaanza. Alipojaribu kujitetea, dada yake mkubwa, Husna, alisimama kwa dharau, “Una akili kweli wewe Lucas? Johari ni nani? Mtoto wa nani? Baba yake alikuwa nani? Msichana wa mtaani, aliyekuwa chuo kwa mwaka mmoja, baadaye akaishia kumaliza maisha kwenye vyoo vya lodge! Unataka aingie kwenye familia yetu na huyo mtoto wake wa ajabu ajabu?”
Lucas alijaribu kujitetea, “Alikuwa chuoni… maisha yalimpiga, kama wengine wanavyopigwa. Alihangaika kulea mtoto wake mwenyewe…”

Lakini mama yake alimkarisha kwa sauti ya amri, “Kwa sababu ya umalaya wake ndio maana akashindwa chuo! Huyo mtoto wake ni ushahidi wa kuwa yeye alikuwa msichana wa kukimbizana na wanaume… halafu leo unakuja kuharibu familia yetu na huo uchafu?”
Siku ya utambulisho ikafika. Lucas alimwambia Johari, “Sitaki uogope, twende kwetu… usiogope chochote, mimi niko nyuma yako.”

Johari alijitahidi kuvaa vizuri, alikopa gauni kwa rafiki yake anayefanya saloon pale Buguruni. Neema alibaki kwa dada mmoja jirani aliyemzoea. Johari akiwa amebana roho yake, aliingia kwenye nyumba ya kifahari ya familia ya Lucas pale Mikocheni. Sakafu ilikuwa ya marumaru ya shiny white tiles, mapazia yenye mishono ya Ulaya, kila kona ilikuwa na harufu ya pesa.

Mama yake Lucas hakuvaa hata tabasamu, aliwakaribisha bila hata kupeana mikono. Dada zake walikaa kwenye sofa wakimkodolea macho kama mbwa anayeingia kwenye mgahawa wa watu. Walikuwa wanamuangalia toka juu mpaka chini, kutoka nywele zake zilizonyooka kwa pasi ya mtaani, hadi viatu vyake vya kuazima vilivyokaribia kufumuka nyuzi.

“Lucas… huyu ndio Mwanamke wako? Huyu ndio Bibi harusi wetu?” Husna alibeza huku akiangalia simu yake.
“Mimi ndio mwanamke wake. Sitaki kudanganya mtu hapa,” Johari alijibu kwa sauti ya heshima lakini ya kujiheshimu.
Mama yake Lucas alicheka kwa dharau, akasema, “Sasa hivi mna guts kabisa kusema mbele yetu? Eti sitaki kudanganya mtu hapa? Hatuongei na mtu kama wewe… una roho ngumu kuliko magogo ya msitu wa Pugu.”

Lucas akasimama akasema, “Mama, dada… tafuteni sababu nyingine lakini sio kumtukana Johari. Kama ni kuwa na mtoto, ni maisha, na huyu mtoto siyo laana bali baraka. Mimi ndio niliamua kumpenda mama mwenye mtoto. Na mimi ndio nachukua jukumu la malezi. Kama hamtamkubali… msinilazimishe kuishi maisha yenu.”
“Mimi niliwahi kuwa lodge, lakini siwezi kuwa na roho ya lodge. Niliwahi kuwa mtaani kama muuza wa uji, lakini siwezi kuishi kama mtu wa uswahilini, wa uji milele,” Johari aliongeza taratibu huku akivuta pumzi.

Mama mkwe alisimama kwa hasira, akasema, “Lucas… natangaza hapa, ukimuoa huyo binti wa uji, sahau mali za familia hii. Tutasahau jina lako kwenye mirathi yetu. Tutakupeleka kwa bibi yako Kijijini… tunataka mke mwenye hadhi, siyo kutuletea kinyaa mezani.”
Lucas alikosa nguvu, akaketi kwenye sofa kwa huzuni. Johari aliinuka, akamwangalia Lucas machoni akasema kwa upole, “Lucas… sina la kukwambia. Familia ni kitu cha maana. Sitaki kuwa mtu wa kuharibu utulivu wenu. Nilikupenda si kwa sababu ya pesa zenu wala maisha yenu, nilikupenda kwa sababu niliona heshima kwenye macho yako.”

Akashika begi lake la kitenge, akasema, “Kama kweli unanipenda, hutaniacha, lakini kama familia ni bora kuliko utu wa mtu… niko tayari kurudi kule nilikotoka.”

Lucas alitazama macho ya Johari, akashika kichwa chake kwa maumivu. Moyoni alipigwa vita kali. Johari alijua safari yake ilikuwa imeingia kwenye giza nene… lakini moyo wake
ulikuwa bado umesimama wima.
********

Johari alifuta machozi kimya kimya aliponyanyuka kwenye kochi lile la kifahari, machozi yakiwa yamejaa machoni lakini akijizuia yasiteremke mbele ya watu waliomwangalia kama uchafu wa mtaani. Aliikota pochi yake kwa nguvu, akavaa vile viatu vya mkopo miguuni na kuanza kutembea kwaa! Kwaa! bila hata kujali , Alitoka nje, mlangoni nyuma yake akaacha sauti za dharau zikimfuata.

“Kasoro ya kinyaa imeondoka, tunashukuru!” Husna alipaza sauti kwa dharau.
Mama Sada naye hakuchelewa, “Haya ndio maisha ya lodge, mtu hawezi hata kukaa kwenye kochi ya watu wenye heshima. Arudi kwenye matope yake.”
Dada mwingine akamchomekea, “Kwa sura na mwili huo, hata mbwa wa mtaa wetu ameshiba kuliko yeye.”

Zomea, kejeli, maneno ya kashfa vilimfuata hadi nje. Johari alihema, moyo wake ukimwangukia miguuni. Aliwahi kutukanwa sokoni, alijua mateso ya mtaani, lakini namna familia ya Lucas walivyomdhalilisha ilikuwa kiwango kingine, kilichomuumiza mpaka kwenye mifupa. Alitembea haraka, machozi yakimtiririka bila kujali.

Lucas alimkimbiliia kutoka kwenye kikao, akamkuta Johari anatembea mbele mtaa wa pili akipepesa macho huku akijizuia kulia kwa sauti. Lucas alimkimbilia akamshika mkono.

“Johari, tusizungumzie maneno yao tafadhali, njoo nikupitishe hata uende nyumbani…”
Lakini Johari alimuangalia Lucas kwa macho yaliyojaa maumivu. Sauti yake ilitoka kwa uzito, “Lucas… leo sio siku yangu ya kwanza kudharauliwa, lakini sijawahi kufanyiwa hivi na watu waliompa nafasi mwanaume kunipenda. Leo umenipeleka katikati ya mapanga, nikakatwa bila huruma. Hujui inauma kiasi gani.”
Lucas alihema, akatoa pesa mfukoni, laki moja akaishika mkononi, “Chukua hii… tafadhali, panda bajaji, rudi nyumbani. Nitakufuata kesho… nitazungumza na familia yangu vizuri.”

Johari hakuwa na nguvu ya kugoma, alichukua pesa na kuondoka kimya kimya.

Lucas akarudi ndani akiwa na hasira usoni, macho yakiwaka moto. Akavuta kiti akapiga meza kwa hasira. “Husna, na wewe mama… si mnajifanya watu wa heshima sana? Si mnaniambia eti msichana wa lodge hafai? Huyu dada yangu Husna… mtoto wake yuko wapi? Hivi mnaweza kuniambia yule mtoto wake wa pili baba yake ni nani? Husna si ni single mother hapa nyumbani?”

Husna alisimama akimfokea, “Lucas! Wewe unalinganisha nini sasa? Mtoto wangu hata kama sijaolewa, baba yake ana pesa na anahudumia… sio kama huyo chawa wenu wa uswahilini”

Lucas alipiga meza kwa nguvu, “Uniseme mimi lakini usimseme Johari! Yeye ni mwanamke jasiri kuliko wewe, analea mtoto wake peke yake, amepambana hadi ameanza kusimama… siyo kama wengine mnapata mimba mnazaa kisha mnawarudishia wazazi kulea.”

Mama yao aliingilia kwa hasira, “Lucas! Umelogwa? Au unaumwa kichaa? Huyu mwanamke amekuroga! Wewe unatuonyesha meno sisi? Unataka tukufute? Mali yetu usisahau, weka sahihi kabisa, ukimwoa huyo malaya, tunafuta jina lako kwenye familia!”

Lucas alikosa nguvu, moyo wake ukiuma, alijikalia kimya huku jasho likimtoka.
Baada ya saa moja kikao kilivunjika na kila mtu akaenda zake huku mamake na dada zake wakizidi kuporomosha maneno.

Siku mbili baadaye habari zilimfikia Yvonne, mchumba aliyepangwa na familia ya Lucas. Msichana wa kitajiri mwenye degree mbili, kutoka familia yenye msimamo. Yvonne aliposikia Lucas alimpeleka msichana kwao, aliwaka. “Johari? Huyo ndio nani tena?”
Yvonne aliwasha gari yake ndogo aina ya IST nyeupe, akafuatilia habari akagundua Johari anafanya kazi gereji mpya maeneo ya Gongo la Mboto.

Jumatatu ya asubuhi Yvonne alienda gereji hiyo. Alifika akiwa amevalia magauni ya kisasa, hereni za dhahabu, na viatu vya thamani vilivyoshonewa Ulaya. Johari alikuwa amevaa kombati yake ya kazi na fulana yake ya bluu iliyochakaa, akifuta engine ya canter iliyokuwa imeshiba mafuta ya mzee mmoja.
“Johari?” Yvonne aliita kwa sauti yenye tabasamu la dharau.
Johari aligeuka, akamwangalia yule msichana mrembo, asiyemjua.

“Ni mimi… naitwa Yvonne,” Yvonne alitabasamu huku macho yake yakiwa na sumu ya maneno. “Rafiki wa karibu sana wa familia ya Lucas. Niliskia umekuwa gumzo mtaani.”

Johari hakuelewa, akasema, “Habari yako dada.”
Yvonne alicheka kwa kejeli, “Hujui hata mimi ni nani… lakini leo nimekuja kukuambia kitu kimoja tu. Maisha ni uchaguzi. Ukiyachagua maisha ya kujituma, unaweza kufika mbali… lakini ukichagua kuingia kwenye familia ambazo hukubaliani nazo, maisha yatakumaliza mapema.”

Johari alinyamaza.

Yvonne aliendelea kwa lafudhi ya kicheko cha dharau, “Una uhuru wa kuamua, utachagua maisha huru, ya mwanamke wa kujitegemea, au utaamua kuwa mwanamke wa kuvutia mapigo ya moyo kwa kila mtu, kuharibu familia ya watu, kuharibu mafanikio ya mwanaume mwenye hadhi?”

Johari alimsikiliza bila kuelewa kwa haraka, lakini moyo wake ulianza kujaa maswali.

“Kwa hiyo ni wewe?” Johari aliuliza kwa sauti ya kutetemeka.

Yvonne alitabasamu, akasema kwa utulivu wa mtu anayeficha kisu nyuma ya mgongo, “Mimi ni mke mwenza unayepambana naye… ila bado hujui vita gani umeingia.”
Yvonne aligeuka, akapanda gari yake, akamuachia Johari maswali mawili, aendelee na mapambano yake, au atafute njia
ya kuponya moyo wake kabla haujasambaratika.

ITAENDELEA…

Twende tusiendeleeee?

Chungu Cha 11 kije kisije,
Nasikiliza maoni yenu....
 
Aisee mateso yamezidi
Kuna wakati nilifatilia hadithi yako hukumaliza nikakucheki inbox kama unatoa kitabu ukawa upo kimya.naomba nieleweshe kama umetoa vitabu na vinapatikana wapi.kwenye page nyingine za,makala uko vizuri huku unapwaya sana sasa sijui unakwama wapi.jina lako kubwa kijana wangu.
 
NITAMLEA
Mtunzi; Robert Heriel
Chungu 11

Johari aliishi wiki chache za kuchanganyikiwa, akihangaika na mawazo yenye utata usio na majibu. Alikaa usiku mwingi akimwangalia Neema aliyekuwa amelala, akajiuliza maswali yasiyo na majibu. “Naenda wapi? Nitamleaje huyu mtoto? Na mapenzi yangu ni ya kweli au njaa ya faraja tu? Vipi kama namtesa?”

Sasa alikuwa kwenye njiapanda. Amchague Lucas Mwanaume aliyempenda vile alivyo lakini maisha yake yatawindwa. Au aendelee na Maisha yake ya ufukara akimlea Neema, ambaye Baba yake hatulii kama mgunduzi wa kijerumani. Akawa kila siku anasita, mara moyo wake umuite Lucas, mwanaume aliyemsaidia kujiona mwanamke wa thamani, mara kumbukumbu zimrudishe kwa Denis, baba wa mtoto wake ambaye kwa kipindi cha nyuma alimpa mgongo, lakini bado alihisi kuna chembe za upendo za zamani kwenye moyo wake. Ingawaje ni ndugu yake wa Damu, Kwa Baba.

Lucas alikuwa mwepesi kwenye moyo wake, mtanashati, alikuwa anamuonyeshea heshima hata mbele ya watu. Alikuwa na kazi nzuri, gereji kubwa na sasa alimwahidi ndoa. Yeye ndiye aliyemtoa kwenye nyumba ya giza ya Manzese, akamtoa kwenye maisha ya kula ugali kwa chumvi na kumleta sehemu ambapo aliona tena nuru ya kuishi kama mwanamke. Lucas alimnunulia simu ya kisasa, smartphone ya kisasa yenye memory kubwa na kamera kali. Johari alipokuwa akikodolea macho ile simu mpyaa, moyo wake ulipata furaha isiyoelezeka. maisha yanabadilika.

“Baby wangu… usisahau, huu ni mwanzo tu, sitaki uendelee kuficha uzuri wako. Sitaki uishi kinyonge. Nitakulinda,” Lucas alimwambia siku aliyompa ile simu. Johari alijisikia kama msichana mdogo wa chuo tena, akafungua akaunti mpya Instagram na Facebook, akaanza kupost picha mpya, mapozi yake ya furaha na caption zenye matumaini. Neema naye alianza kung’aa, alipendeza, alipata viatu vizuri vya shule na hata begi jipya la shule.

Kila mtu aliyezoea kumuona Johari akiwa amechoka kwenye viunga vya Manzese alishtuka alipomwona akiwa kwenye mitandao, akicheka, akijivinjari, akienda kula bata na Lucas. Aliandika kwenye post moja: “ Mtu sio nyani… tunasonga mbele, maisha ni vita lakini tumeumbwa kwa ushindi.”

Kumbe mbali kabisa, kule Mwanza, Denis alipokuwa kijiweni anakunywa kahawa kwenye kibanda cha mgahawa wa kawaida, marafiki zake walikuwa wakimdhihaki wakimwonyesha picha za Instagram. “Broo! Mbona mama mtoto wako yuko na mwanaume wa gereji huko Dar? Alafu kesho ndo engagement yao.”

Denis aliduwaa, akaichukua simu ya mwenzake akawa anakodolea macho picha za Johari na Lucas. Macho yake yalibinuka na moyo wake kama sindano za moto ukachoma. Alijiona mpumbavu, miaka yote kabla haijajulikana wao ni ndugu angeweza kumwoa. Alikuwa alimpenda sana Johari. Sasa kuona anachukuliwa na mwanaume mwingine kilimuumiza vibaya, kilimkaba koo.

Alifunga safari ya haraka kurudi Dar es Salaam, akapanda basi, akiwa na shilingi elfu kumi tu mfukoni na matumaini ya kurudisha penzi lake. Hakutaka kusikia habari za undugu. Hilo alilikataa. Alipofika, hakuwa na sehemu ya kwenda moja kwa moja zaidi ya Manzese, alipofikia kwa rafiki yake anayeishi chumba cha kupanga. Huko alijua angekutana na Johari lakini Johari alikuwa ameshahama Manzese na kuhamia Goba.

Siku ya engagement ilipowadia, Johari alipendeza. Gauni lake la bluu iliyometameta lilionyesha mabadiliko yake waziwazi. Saluni walimuweka vizuri, nywele zikasukwa kisasa, Lucas aliandaa sherehe ya kawaida lakini ya heshima, watu wachache wa familia ya upande wake walioamua kumkubalia ombi lake, marafiki wachache wa kazini na watu wa gereji walikuwepo.

Johari alipiga picha nyingi sana, akazitupia Instagram. “Leo ni mwanzo mpya, #engaged, #lovewins,” aliandika.

Dakika chache baadaye, simu yake ilianza kulia mfululizo. Ilikuwa namba ya Denis. Aliikata mara ya kwanza, ya pili, ya tatu. Kisha ikaja sms moja: “Tafadhali nipe dakika tano tu, nipo nje ya mlango wa ukumbi.”

Johari alishangaa, moyo wake ukaanza kwenda kasi. Akajipa nguvu, akatoka nje. Alimkuta Denis amesimama pembeni ya ukumbi, kapauka, macho yake yamevimba kama bondia aliyetoka kukamuliwa, nguo zake zimechoka. Alimtazama Johari bila kusema Chochote kwa sekunde kadhaa.

“Johari… sitaki kuharibu furaha yako… lakini naomba unisikilize, siwezi kukubali mtoto wangu alelewe na mwanaume mwingine bila hata mimi kujua,” Denis alianza kwa sauti ya ukali.

Johari alitetemeka. Denis hakuwa na kitu, lakini alikuwa mzazi mwenza, damu ya Neema. Mapenzi yao ya zamani yalicheza wimbo wa huzuni kichwani mwake. “Nimehangaika… nimepotea… lakini bado ninapigana. Ninahangaika kwaajili yenu,” Denis aliongeza.

“Nilikudharau Denis… uliniacha… uliniacha nikiwa mimba yangu, hukufikiri kuhusu mateso yangu,” Johari alisema kwa sauti ya huzuni.

Denis alitikisa kichwa, machozi yakimtiririka, “Najua… lakini bado nina nafasi? Siyo kwako, bali kwa mtoto wetu… nisikatwe mzizi wake.. nahitaji kumlea"

Johari akashindwa kujibu, moyo wake ulipasuka vipande viwili. Lucas alimpa upendo mpya na maisha yenye heshima, Denis alimkumbusha kiini chake, damu ya mtoto wake. Alijiuliza vipi kama Lucas atakataa Denis kujihusisha na Neema. Au akitaka Neema achukuliwe na Denis jambo ambalo aliapa asingekubali. Alisimama, machozi yakimtiririka, akasikia sauti za watu wakimuita kwenye sherehe.


Alikuwa Njiapanda, upande mmoja kuna mapenzi yenye mwanga wa maisha mapya, upande wa pili kuna damu, asili, mzazi mwenzake.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yake Johari alijikuta hana jibu la haraka. Alibaki katikati ya njia, akishindwa kupiga hatua…
*******
Johari alikuwa bado amesimama pale, moyo wake ukimdunda kwa kasi ya ajabu, midomo yake ikitetemeka, akili yake ikigawanyika vipande vipande. Hakuwa amemwona Denis kwa muda mrefu, na sasa ghafla kaibukia kwenye siku yake ya furaha. Kabla hajapata hata nguvu ya kuamua la kufanya, sauti ya kebehi ilichoma masikio yake kutoka upande wa kushoto.

“Naona mtaa mzima umehamia hapa, mapenzi ya kihuni yanatafuta nafasi kwenye familia za heshima,” ilisikika sauti ya Yvonne, akivinjari kwa maringo huku akitikisa pochi lake la gharama. Alikuwa amevaa gauni refu lililombana, miguu iking’aa kwa mafuta ya bei mbaya, kucha zikiwa zimepambwa kwa rangi nyekundu za kung'aa, na macho yaliyopambwa kama kasuku wa Comoro.

Denis aligeuka, macho yake yakatua kwa Yvonne. Kwa mara ya kwanza akajiona kama kibogoyo kimekalia shibe ya nyama. Johari alipiga hatua moja nyuma, akijua kelele za Yvonne hazikuwa za bure.

“Wewe Yvonne, unataka nini hapa?” Johari alijitahidi kujizuia kuanguka machozi, lakini mwili wake ulikuwa hauna nguvu.

Yvonne akakenua meno yake meupe, “Wewe Johari, unafikiri utachukua mwanaume wa familia ya heshima kama Lucas kirahisi tu? Ulishindikana huko Manzese sasa unataka kuingia kwetu? Huna hata aibu… mwanaume wa maana yupo ukumbini wewe uko nje na mwanaume mwingine, ni sifa hiyo?”

Denis akajikaza, akamshika Johari mkono kwa upole, “Heshima inakuja kwa moyo, siyo kwa pesa au ukoo. Kama kuna mtu anapaswa kumheshimu Johari hapa ni wewe Yvonne. Yeye ni mama wa mtoto wangu.”
Yvonne akacheka kwa dharau, “Hii familia kweli imekufa, Denis mzururaji wa Mwanza na mwanamke wa mtaani wameshikana mkono, mkitafuta huruma ya kuokoteza mikate kama panya kwenye jalala.”

Mara ghafla milango ya ukumbi ikafunguliwa kwa nguvu, Lucas akatoka akitazama huku na kule. Alikuwa ameshindwa kustahimili kuona Johari haonekani ukumbini. Macho yake yalipambana moja kwa moja na taswira ya Johari akishikana mkono na Denis.
Uso wa Lucas ulipauka sekunde ileile, kifua chake kikiwa kimejaa moto wa wivu na maumivu yasiyoelezeka. Mapigo ya moyo wake yalibadilika, akasogea taratibu kama simba anayenyemelea windo lake.

Yvonne hakuwa amekaa kimya, alipomuona Lucas akitembea akaongeza moto kwenye maneno yake, “Sasa umeyaona Kwa macho yako? Huyu ni mwanamke unaepanga kumwoa… engagement ya kichekesho wakati mwanamke wako yupo nje akishikana mikono na mwanaume mwingine tena mzururaji?”
Lucas alihisi dunia inamgeuka, machozi yakitaka kumtoka, lakini alijikaza kisabuni. Akafika na kusimama mbele ya Johari, Denis na Yvonne. Akamwangalia Johari machoni, akajitahidi kutabasamu lakini misuli ya uso wake ilikuwa inakataa.

Johari alinyamaza, Denis akavuta pumzi ya nguvu, akamuachia mkono Johari na kusogea pembeni. Lucas akachukua nafasi, akamshika Johari mkono kwa nguvu ya upendo, macho yakiwa mekundu kwa kuungua ndani kwa ndani.
“Johari siyo mchepuko… Johari siyo malaya wa mtaa kama unavyomwita,” Lucas alimgeukia Yvonne kwa sauti ya upole lakini iliyobeba uzito wa maumivu na hasira. “Ni mwanamke aliyepambana na maisha, mwanamke aliyebeba mateso peke yake… na bado akasimama. Kwa heshima yoyote, yeye ana thamani kuliko ulimi wako wa chuki.”

Yvonne akashindwa kujizuia, akacheka kwa dharau, “Huyu mwanamke anacheza michezo miwili mbele yako Lucas… mwanaume mwingine tayari kashamshika mkono, halafu wewe bado unamfanya malkia.”
Lucas akapumua kwa nguvu, lakini kabla hajajibu mlango wa pili ukafunguliwa, Neema akatokea akiwa na harusi boys mmoja aliyekuwa amemsindikiza kumtafuta mama yake. Lucas alikuwa amemshika mkono Neema alipokuwa akielekea kumtafuta Johari.

Lakini Neema alipomuona baba yake Denis, macho yake yalifunguka kama taa za gari, akamkimbilia kwa nguvu huku akilia, “Baba, baba… nimekuzimia sana!”
Denis akainama, akamkumbatia Neema, machozi yakimtiririka kama mvua ya masika. Lucas akabaki amesimama, ameshika mkono wa Johari huku moyo wake ukipasuka vipande vipande. Alikuwa anajua ni lazima amtunze Neema, lakini kumwona akimkimbilia baba yake halisi, wakati yeye yupo hapo, kulimchoma vibaya.

Johari naye akabaki kama kinyago cha mpapai, macho yake yakizunguka huku na kule, moyo wake ukipasuka pande tatu. Upande mmoja ni Lucas, mtu aliyemtoa shimoni, upande wa pili ni Denis, mzazi mwenza, upande wa tatu ni mtoto wake Neema anayemwita baba mwingine kwa furaha ya kweli.
Lucas alimeza mate kwa taabu, akasema kwa sauti ya maumivu, “Johari, siwezi kupigana na damu… sitaki kumzuia Neema kumpenda baba yake, lakini usiniweke kwenye kona ya mateso.”

Johari akavuta pumzi ndefu, akainama kumwangalia Neema aliyekuwa kwenye mikono ya Denis, akicheka na kulia kwa furaha. Akamwangalia Lucas aliyekuwa akimshika mkono wake kwa moyo mzito, akatazama upande wa pili na kumuona Yvonne akimcheka kwa kejeli.

Kwa mara nyingine tena, Johari alihisi dunia inamzunguka, lakini safari hii si kwa hofu bali kwa uzito wa maamuzi makubwa.

ITAENDELEA…

Mnisamehe Kwa kuwaacha juujuu kama kishada.

Chungu Cha 12 Kiko hapahapa, usitoke
 
NITAMLEA
Mtunzi, Robert Heriel
Chungu 12

Asubuhi ya kesho yake Johari aliianza akiwa hana usingizi wa kutosha. Usiku mzima alikuwa amelala usingizi wa mang’amung’amu, akijizungusha kitandani na kuamka kila baada ya dakika kumi. Kila alipofumba macho alikumbuka tukio la jana, maneno ya Yvonne yalimchoma kama sindano ya moto, machozi ya Denis na mshiko wa upendo kutoka kwa Lucas. Lakini zaidi ya yote, picha ya Neema akimkimbilia Denis ilimchanganya akili kuliko kitu chochote. Johari alipenda kumwona Neema akiwa na furaha. Hii ilimuweka njiapanda.

Aliamka mapema, akamuandalia Neema maji ya kuoga, akampikia chai na chapati aliyonunua jana kwa mshahara wake wa wiki. Akatazama simu yake ya smartphone aliyozawadiwa na Lucas, notifikesheni za Instagram zikiwa zimejaa comment za pongezi na wengine wakimrushia kejeli kwa “kutafuta faraja kupitia mwanaume wa gereji”. Alishusha pumzi ndefu, akaitupilia mbali ile simu kwenye kitanda na kujishughulisha na maandalizi ya Neema kwenda shule.

Baada ya kumpeleka shule, Johari alienda kazini kwenye gereji. Alikaa kwenye ofisi ndogo aliyokabidhiwa, akijitahidi kupunguza mawazo kwa kusoma mafaili ya manunuzi na kurekodi maelezo ya wateja. Lakini kila baada ya dakika tano akili yake ilimrudisha kwa Denis na Lucas, kama mkanda wa sinema unaojirudia bila kikomo.

Saa nne asubuhi simu yake ililia, ilikuwa Lucas.

“Baby uko kazini tayari?” Sauti ya Lucas ilikuwa na upole lakini kulikuwa na tone la maumivu ndani yake.
“Ndio baby,” Johari alijibu kwa sauti ya kutojiamini.
“Leo tunaenda Goba kwa mama yangu. Nimeamua nisikubali mama yangu akubebee mikosi. Kuna mipaka ya wazazi. Nitakutambulisha rasmi mbele yake kwa heshima kama mke mtarajiwa,” Lucas alisema kwa msisitizo.

Johari alinyamaza kidogo kabla hajajibu, “Lucas… siwezi kupinga heshima unayonipa, lakini moyo wangu umeshika kamba mbili. Naogopa.”

Lucas alichukua muda kabla ya kujibu, “Sawa… tutakutana baada ya kazi, tutaongea.”
Ilipofika saa kumi na moja jioni, Johari alichukua route ya Goba. Lucas alikuja kwa gari, wakampakia Johari na Neema na kuingia njia ya vumbi kuelekea nyumbani kwa mama yake Lucas. Njiani walikuwa kimya sana, hata Neema alikaa kwa nidhamu isiyokuwa ya kawaida. Johari alikuwa akiwaza, je ni busara kuendelea na mipango ya ndoa wakati moyo wake bado umefunguliwa katika pande mbili?

Walipofika Goba, nyumba ya mama Lucas ilikuwa ya kifahari. Kiwanja kikubwa kilichojengwa nyumba ya kisasa yenye vyumba vingi na bustani ya maua yaliyopendeza. Lakini Johari hakujisikia amani hata kidogo. Mama Lucas alitoka akiwa na tabasamu la bandia.

“Karibuni nyumbani,” alisema huku macho yake yakimchoma Johari kama sindano.
Walikaa sebuleni, mazungumzo yakaanza, lakini hayakuchukua muda mama Lucas alianza kutuma maneno ya kejeli.

“Lucas, nilifikiri baada ya kikao kile ungefanya maamuzi ya maana. Lakini ptuu! Sio kutuletea mwanamke wa mitaani.”

Johari alishika pua yake kwa tabu, alikazana kuwa mtulivu lakini moyo wake ulikuwa unavunjika.
Lucas alimtazama mama yake kwa hasira isiyofichika, “Mama, nataka kukwambia leo, Johari ana heshima yangu. Alipambana kule Manzese akiwa na mtoto wake, ameishi maisha magumu kuliko hata ninavyoweza kueleza. Na sasa, mimi ndiye nitakayekuwa naye.”

Mama Lucas alikunja mdomo wa dharau, “Na mtoto wake? Utalea mtoto wa mwanaume mwingine, halafu useme ni familia ya heshima? Na huyu binti anayekimbilia mwanaume mwingine mbele yako? Ulishamwona jana alivyoikimbilia damu yake? Aliachaje kukukimbilia wewe Lucas? Wewe unajidhalilisha kwa mapenzi!”

Lucas alipumua kwa nguvu, akamshika Johari mkono kwa heshima, “Nitamlea Neema kama mwanangu. Mambo ya damu yanapaswa kutengwa na mapenzi ya watu wawili.”
Mazungumzo hayo yaliendelea kwa maneno ya kuudhi mpaka saa mbili usiku. Johari aliondoka hapo akiwa amechoka, Lucas alikuwa amemkasirikia mama yake lakini bado alitaka kusimama na Johari.

Walipokuwa njiani kurudi nyumbani, simu ya Denis iliita. Lucas aliona jina ‘Denis’ liking’aa kwenye kioo cha simu ya Johari. Hakuwa na maneno, moyo wake ulivimba Kwa hasira lakini alinyamaza.

Johari aliitazama simu kwa muda, akakata.

“Baby unakata simu ya baba wa mtoto wako?” Lucas alimuuliza kwa sauti ya kicheko cha kukata tamaa.
“Nimekata kwa sababu sitaki drama nyingine usiku huu,” Johari akajibu.
“Usimkatae! Pokea simu. Huwezi kumpotezea damu ya mtoto wake. Lakini nataka unitazame usoni… mimi ndiye ninayekupenda sasa hivi, si Denis wala mtu mwingine. Naomba uniheshimu, unijenge. Usiruhusu ya jana yaniharibu moyo wangu.”

Johari hakujibu, akashusha pumzi ndefu.

Siku zilizofuata Johari alijitahidi kutulia na Lucas, aliendelea kujenga heshima yake kwenye kazi na maisha, lakini Denis hakuwa kimya. Alimfuata shule Neema alipokuwa akiingia darasani, akamnunulia zawadi za shule, viatu na hata kulipia trip ya shule. Denis hakutoa presha kwa Johari bali alijitahidi kumuonyesha Neema kuwa yeye ni baba wa damu, mwenye moyo wa kweli.

Baada ya wiki mbili, Johari alipata taarifa za Denis kuanza kazi mpya kwenye kampuni ya kusambaza bidhaa za viwandani kama dereva. Taarifa hizi zilimchanganya zaidi.

Siku moja akiwa kazini, Denis alimtembelea Johari gerejini akiwa amevaa sare mpya za kazi. Alimuita pembeni.
“Johari sikudai mahaba wala heshima kwangu. Lakini nataka uwe na uhuru wa kuchagua maisha yako bila kutishwa na maisha ya leo au kesho. Sitaki kukuambia uachane na Lucas… lakini nataka uhakikishe Neema anajua mzazi wake wa damu.”

Johari alibabaika, akabaki akimwangalia Denis machoni.
“Denis… maisha yangu sasa hivi yamejengwa na Lucas. Kila mtu alinipa mgongo lakini Lucas alinipa mkono wa upendo.”
Denis alitabasamu, “Na sitaki uache kupendwa. Lakini nataka usinipe kisogo kwenye haki yangu ya kumsimulia Neema historia yake.”

Johari alikubali, “Hilo siwezi kupinga.”

Wiki ikafuata, Lucas akaja na zawadi ya gauni jekundu, “Kesho tunafanya engagement ya pili rasmi kwenye ukumbi. Nataka watu wajue nipo na wewe.”

Siku ya engagement ilifika. Johari alipendeza sana, ukumbi ukanoga. Picha zikasambaa mtandaoni.

Siku hiyohiyo Denis alifunga safari kwenda kwao Simiyu kwa familia yake ya ukoo wa Mama. Aliamua kufuta mawazo ya Johari na kurudi kujijenga upya kwa ajili ya Neema.
Lakini mambo hayakuishia hapo. Kesho yake, Johari alipokuwa amejipumzisha, Lucas alipokea ujumbe kutoka kwa mdogo wake. Ilikuwa picha ya Denis akiwa anasherekea na familia yake Simiyu huku caption ikisema: “Kuhakikisha familia haifutwi na historia.”

Lucas akamgeukia Johari, “Uliniahidi jambo moja… moyo wako unapaswa kuwa wa mtu mmoja. Denis anasherekea huko kama mtu anayetaka kurudi kwenye maisha yako.”

Johari alikaa kimya.

Lucas akasema, “Chagua mara moja… sitaki moyo nusunusu. Kama una hisia za Denis, niache kabla hatujasonga mbele.”

Macho ya Johari yalitoka machozi, akiwa kati ya mapenzi ya sasa na kumbukumbu za zamani… upande mmoja ni mwanaume anayempigania Neema na upande mwingine ni mwanaume aliyemtoa kwenye maisha ya mateso.
******

Miaka miwili ilipita kama ndoto, Johari aliingia kwenye maisha mapya ya ndoa. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, akaonja ladha ya mapenzi yenye utulivu. Lucas alimpenda bila masharti. Akampatia heshima na hadhi kama mke. Alikaa kwenye nyumba nzuri ya kupanga Goba, akawa na uhuru wa kuvaa na kujiremba, alimpeleka mtoto wake Neema shule nzuri ya binafsi. Akatembea na Lucas sehemu mbalimbali; Zanzibar, Bagamoyo, hata mbuga za wanyama. Sasa Alikuwa mama wa kisasa, mke mwenye hadhi. Maisha yalimtoa kwenye machungu aliyoyazoea ya kunyanyaswa na kudharauliwa. Na sasa Alijiona malkia.

Kwa upande mwingine, Yvonne aliamua kuachana na drama ya Lucas na Johari. Alijipanga upya, akajikita kazini na kupambana na maisha yake. Miaka miwili baadaye naye alipata mume wake, aliolewa na kijana wa familia aliyempenda pasipo kumbukumba za mabishano ya zamani. Akajipanga na maisha yake, furaha yake ikaonekana kwenye mitandao ya kijamii. Hakuwa tena na muda wa kutupiana maneno na Johari, aliamua kuweka maisha yake mbele.

Neema kwa upande wake alisonga mbele, akaendelea na masomo. Alikuwa darasa la tatu, mrembo wa kufanana na baba yake Denis. Johari alijivunia binti yake. Alimlea kwa mapenzi na malezi bora, alimpa kila alichokimudu, ingawa Neema muda mwingi alikua akimkumbuka baba yake Denis, japokuwa hakumwona kwa muda mrefu.

Lakini siku moja taarifa zikamfikia Johari kwamba Denis sasa amepata kazi Tanesco. Waliomwona Denis walimwambia kavaa vizuri, anatoka asubuhi, anarudi jioni, maisha yameanza kumnyookea. Denis naye alifurahia nafasi yake mpya, aliamua kurejesha maisha yake mstari. Siku Moja Akampigia Johari simu, kwa sauti ya upole akasema; “Sasa nataka Neema akae na mimi… ni haki yangu kama baba.” Johari alikasirika, akakata simu. Lakini Denis hakukata tamaa, akaenda mahakamani, akafungua kesi ya haki ya kulea mtoto.

Mahakama ilipokuwa ikisikiliza kesi, Johari alihisi dunia imemgeuka. Aliamini kuwa maisha yake sasa yamekamilika akiwa na Lucas na Neema. Lakini kumbe Denis bado alikuwa na sauti kwenye maisha ya Neema. Wakili wa Denis alimwakilisha vizuri, alipeleka vielelezo kuwa Denis ana kazi nzuri, kipato cha uhakika na mazingira salama ya kulea mtoto. Wakati huo Johari na Lucas walikuwa wameingia katika changamoto mpya… tangu Johari aolewe, hakuwahi kupata ujauzito.

Ilianza polepole, Lucas akizungumza kwa utani. “Mama, Neema si wa kwangu… kwa nini mke wangu hanipatii wa kwangu?” Lucas alitupa maneno hayo akicheka kidogo, lakini baadaye akaanza kuchukia kweli kweli. Alienda hospitali kufanyiwa vipimo vyake na akakutwa hana matatizo. Johari alichunguzwa zaidi ya mara tatu, lakini kila mara majibu yalikuwa hayatoi sababu ya msingi. Mimba hazikuingia.

Mwanamume yule aliyekuwa na upendo na utulivu alianza kubadilika. Johari alianza kuiona sura ya pili ya ndoa. Vituko vilianza nyumbani. Maneno ya kejeli, dharau, hata usiku Lucas alianza kulala upande wa pili wa kitanda. Mahakamani Denis alikuwa anapambana ili apate haki ya kulea mtoto wake, nyumbani Lucas anapambana na wazo kuwa Johari hana uwezo wa kumpatia mtoto wake wa damu.

Mama mkwe wake Lucas hakuwa na mchezo. Mara kwa mara alimpigia simu mwanae; “Lucas, familia yetu inakuhitaji. Hatuna mrithi mwingine zaidi yako. Unachukuliwa mateka na mwanamke aliyezaa nje ya ndoa na hadi sasa hana dalili za kukuongezea familia.” Lucas alinyongwa na presha za familia yake, mama yake, dada zake walimtukana Johari kila walipopata nafasi. Ilifika hatua Lucas alikua anarudi usiku na kulala bila hata salamu.

Mbaya zaidi, Lucas siku moja alipokuwa akienda kazini akakutana na Yvonne mjamzito. Yvonne alicheka kwa kejeli, akampa maneno Lucas yaliyomuumiza; “Baba mtu mzima uko kwenye ndoa miaka miwili hakuna hata ujauzito wa homa? Mwanamke aliyetoka Manzese, umalaya wa mitaani unamuandama… watoto wake siyo rahisi kuwahesabu kama wako. Si unajua alitolewa mimba chuo mpaka akafukuzwa?” Lucas alibaki hana maneno. Jioni yake alirudi na fujo kali kwa Johari, akamnyoshea kidole usoni, akamwambia; “Wewe ni Malaya, ndio maana mimba hazishiki, ulitoa nyingi chuoni hadi ukafukuzwa.”

Johari alilia. Alilia kweli. Kwa mara ya kwanza alitamani hata Dunia immeze. Mwaka wa ndoa ulikua wa upweke na mateso. Alikuwa amefungwa kwenye ndoa lakini hana raha, hakuna mtoto, hakuna heshima. Lucas alipomwona Johari akilia hakuonyesha huruma, alitoka akapiga mlango kwa nguvu.

Mgogoro mkubwa ulizuka kwenye familia ya Lucas. Mama yake Lucas aliitisha kikao akisema lazima Lucas aoe mke mwingine atakayemletea mjukuu. “Huyu mwanamke wa kuokotwa hana jipya. Hivi leo sijapata mjukuu! Ujinga huo sikubali.”

Johari alihisi anajifia taratibu. Alihangaika, akaanza kuumwa kwa msongo wa mawazo, akaenda kuchukua vipimo, matibabu, madawa ya kienyeji lakini hakuna kilichobadilika. Lucas akazidi kuwa mjeuri, akawa hatulii nyumbani.

Siku moja alipopata habari kuwa Denis ana ndoa mpya, tena kamwoa Salma aliyekuwa rafiki yake wa karibu tangu chuoni, moyo wake ulipasuka. Alikumbuka jinsi alivyozoea kusimulia maisha yake kwa Salma, jinsi walivyolala kitanda kimoja, wakipanga maisha yao, wakizungumza kuhusu Denis na Lucas. Sasa yule yule Salma ndio anachukua nafasi yake.

Johari alimpigia simu Denis lakini namba haikupatikana. Akamtafuta Salma, wapi! Hakupatikana. Hata kwenye Instagram akaunti zao zilifutwa. Lakini aliweza kuipata anwani yao, walihamia Mbezi Beach. Neema alienda kuishi kwa Denis kwa maagizo ya mahakama, na alipokuwa akija mara chache kuwasalimia. Neema alimwona mama mpya anayempenda, anayembeba shuleni, anayempeleka mazoezi, maisha ya Neema yalikuwa yamebadilika. Salama alijua kuteka akili ya Neema ukizingatia Neema alikuwa anamjua Salma tangu alipozaliwa.

Siku moja Johari alienda Mbezi Beach bila taarifa, akaingia pale alipokuwa anaishi Denis na Salma. Neema alipomwona mama yake akafurahi lakini Salma alimwangalia kwa sura ya mshangao. “Karibu,” alisema Salma kwa sauti ya kutoelewa. Johari alianza kwa upole lakini alipomuona Salma akiwa amependeza, akiwa na pete ya ndoa na mimba ya miezi mitano, akili ilimchanganya.

“Bado unafanya umalaya na mwanaume wa watu?” Johari alimvaa Salma kwa maneno ya chuki. Salma alicheka, “Malaya ni wewe, mimi niliingia kwenye ndoa rasmi, si vibanda vya Manzese au Goba.”

Matusi yakazidi, Neema akashuhudia wazazi wakitupiana maneno ya matusi. Salma alichoka, akampasulia Johari bomu kubwa: “Kwanza mtoto huyo unayemuita wa Denis si wake. Umesahau kipindi cha chuo ulivyokuwa na James yule MC wa sherehe za hapa mjini? Alikuwa akilala kwako kila wikendi, hukumbuki ulipata mimba hukujua ni ya nani? Wewe mwenyewe ulimwambia Denis kwa sababu James aliikataa.”

Johari aliishiwa pumzi, akatetemeka. “Unaongea nini?” Alilia.

Salma alimkazia macho; “Tafuta ukweli… huwezi kuwatesa watu kwa maigizo ya uongo. Denis amepata mke sahihi. Usituchanganye.”

Johari alipoteza nguvu. Alihisi ulimwengu unamzunguka. Miguu ilitetemeka. Alitetemeka huku machozi yakitiririka. Kichwa kikawa kizito. Je, kweli Neema si mtoto wa Denis? Ingawaje walifanana. Akakumbuka enzi zile za chuo, wizi wa mapenzi, mihangaiko ya kula kwa James na Denis kwa pamoja. Alianguka sakafuni, akaanza kulia kwa uchungu uliovuka maelezo.

Mlango wa nyuma Denis alitokea akiwa na Neema mkononi, Neema alienda kumwita Babaake, Denis. Alipofika aliwashangaa wawili wale wakibishana. Neema alikimbia kumshika mama yake, “Mama usilie,” lakini Johari alishindwa kujizuia, alitaka ardhi immeze pale pale.

"Umesema Neema sio Mtoto wangu? Umesema James MC?" Denis alisema akiwa amechanganyikiwa

Itaendelea
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…