SEHEMU YA 114
Asubuhi kulipokucha alikuwa anapigiwa sana simu na kuamua kuipokea, mpigaji alikuwa ni Derick,
“Mbona unaongea hivyo Erica, unaumwa?”
“Hapana”
“Naomba kuonana na wewe, twende basi tukanywe chai pamoja”
“Basi ngoja nijiandae”
Erica aliinuka pale kitandani na kwenda kuoga, kisha kutoka nje ili ampigie simu Derick, ila alishtuliwa na Yule msichana wa siku ile aliyekuwa anamwambia Erica kuwa ampe ujuzi ili na yeye apiganiwe na wanaume,
“Erica mambo”
“Safi”
“Mbona macho yamekuvimba hivyo?”
Mbele kidogo akatokea Derick kumfata Erica kwahiyo alimuita ili waondoke, ikabidi Erica amuage Yule binti,
“Badae Fetty”
Aliondoka na kumuacha Fetty akimuangalia tu.
Derick alienda kwenye mgahawa na Erica, wakaagiza chakula, akamuangalia Erica usoni naye alimuuliza kwa mshangao,
“Mbona macho yamekuvimba hivyo”
“Aaah sijui, kwani yamevimba sana?”
“Sio sana, ila inaonyesha umelia sana. Nini kilikuwa kinakuliza Erica, kuwa muwazi kwangu. Mimi ni muelewa sana”
Erica aliinama na machozi kidogo yalimtoka, na kumfanya Derick amsogelee na kumuuliza kwa upole kuwa kipi kinamliza,
“Sikiliza Erica, kukaa na kitu moyoni sio suluhisho kwani kitaendelea kuumiza milele. Wote wanaojiua sio kwamba wamependa ila hutokea sababu waliweka vitu moyoni na kushindwa wa kumshirikisha mtu mwishowe wakaona bora wajiue wakati kama wangeeleza matatizo yao wala isingepelekea kujiua. Usiupo moyo wako mateso ya kubeba mizigo ambayo haibebeki, unaposema unaupa moyo wako mwangaza na uhuru yani utajikuta moyo umeachia kabisa. Usipende kitu kikutese moyoni, niambie Erica una tatizo gani?”
“Sikia Derick, kuna mwanaume mmoja nampenda sana tena sana, yupo nje ya nchi ila nimesikia ana mwanamke mwingine”
“Pole Erica? Najua mapenzi yanavyoumiza, ila mimi si nilikwambia, hakuna mwanaume mwenye mapenzi ya dhati anapokuwa mbali. Mimi nikija kuoa, kama natakiwa kusafiri kikazi basi nitasafiri na mke wangu, siwezi kumuacha mke wangu na upweke. Usijali Erica, ndio mapenzi yalivyo. Utamsahau kabisa huyo mtu”
“Hujui tu jinsi gani nampenda, nampenda sana Erick”
“Anaitwa nani?”
“Anaitwa Erick”
“Wow, ona sasa Mungu alivyo mwema huyo alikuwa anaitwa Erick, na mimi naitwa Derick yani jina langu na lake limetofautiana kwa herufi moja tu yani D. Ila Mungu ana makusudi yake kukuletea mimi, acha huyo aende sababu hakutakiwa kuwa na wewe ila mimi ndio mwenye sifa za kuwa na wewe Erica, yani mfute Erick kabisa katika maisha yako na sasa muwaze Derick tu. Nahitaji ufurahi, huwa unapenda kwenda wapi?”
“Napenda kwenda ufukweni”
“Basi tupange siku, twende tukapunge upepo. Erica, mtoe Erick kabisa katika akili yako, je kuna mwingine anayeisumbua akili yako zaidi ya Erick?”
“Hapana”
“Basi usijali, Derick nipo na nimeletwa kwako ili huyo mtu asikusumbue tena mawazo yako. Mimi ni mwanaume wa tofauti sana,najua kupenda, kujali na kumdekeza mwanamke yani kwangu utapata ambavyo huyo Erick hajawahi kukupatia. Elewa nakupenda sana Erica”
Maneno ya Derick yalikuwa yakimuingia kwenye akili yake vilivyo ingawa kiukweli hakudhania kama anaweza tokea mtu wa kumsahaulisha yeye kumpenda Erick, ukizingatia ni muda mrefu ameanza kumpenda toka wako shuleni na hajaweza kuacha kumpenda.
“Sasa naomba jioni, twende kwenye mgahawa moja tukale, ni mzuri sana yani utaupenda”
Erica alikubali kisha kuagana na Derick na kurudi hosteli, siku hii hakuwa na kipindi chuo kwahiyo alirudi tu hosteli na kukusanya nguo zake chafu na kwenda kufua.
Wakati anafua alienda Yule Fetty na kuanza kumuongelesha Erica huku akimwambia,
“Hongera sana, sijui una kismati gani wewe mdada, majuzi tu wamepigana wakaka kwaajili yako halafu leo nakuona unaondoka na Yule Derick”
“Kwani unamjua Yule”
“Namfahamu ndio”
“Unamfahamu vipi?”
“Namfahamu tu, ila anaonekana yupo romantic sana mmh hongera”
Erica alicheka tu maana hizi hongera alizokuwa anapewa wakati alikuwa akimuwaza Erick tu muda wote huo.
Alimaliza kufua na kuendelea kupiga stori tu na huyu Fetty, kwa siku hizo mbili hakuwa na habari kabisa ya kuingia kwenye mtandao wa kijamii wala hakutaka kujua kama Rahim alimtafuta au la, kwahiyo alikuwa tu akiongea na Yule Fetty pale na kufurahi ili kusogeza siku tu.
“Kumbe wewe Fetty ni mcheshi sana”
“Ndio, si wewe unajiweka peke yako pake yako ndiomana watu wanaogopa hata kukukaribia”
“Hapana bhana, marafiki walinitenda ndiomana sitaki hata kuwa na marafiki wa karibu”
“Ila unatakiwa kuwa na rafiki, kuna mambo yanakupata unaona umuhimu wa kuwa na marafiki sema cha msingi ni kuchagua marafiki wema kwako”
Wakati wanaongea ongea, Derick alifika eneo lile kwa lengo la kumfata Erica na kwenda nae alipomuahidi.
“Mmmh Derick, mbona mapema sana”
“Ndio vizuri mapema”
“Basi ngoja nikajiandae”
Erica aliinuka pale na kumuacha Derick akiwa na Fetty, na baada ya muda alikuwa tayari na kumuaga Fetty kisha akaondoka na Derick.