SEHEMU YA 96
Rahim akapumua kidogo, kisha akaendelea kumwambia Erica
“Je upo tayari kuwa mchumba angu na badae kuwa mke wangu? Tafadhali kubali Erica nakupenda sana”
Kabla Erica hajamjibu Rahim, alifika Bahati kwenye maongezi yao na kusema,
“Nimekuja mbele yako Erica unikane kwa macho yangu kuwa mimi si mchumba wako”
Kwanza ni kitu ambacho Erica hakukitegemea kwahiyo alipigwa na bumbuwazi hivi kwa muda na kujikuta akiwa hana cha kujibu kwa muda kidogo, ila akakumbuka kuwa simu yake ipo kwa Rahim, akamuangalia na kumpa simu yake kisha akamwambia,
“Na mimi nipe simu yangu”
Rahim alimshangaa kwa muda kidogo Erica na kumuuliza kwa mshangao,
“Kwani imekuwaje? Huyu kijana ni nani?”
“Simjui”
Bahati akaongea kwa mshangao,
“Leo hii hunijui mimi Erica sababu ya huyu kijana wa kitajiri? Unanidharau sababu sina uwezo wa kukupeleka sehemu za aina hii Erica? Nilihisi yote haya maana huyu kijana simsahau kabisa toka siku ile beach”
Rahim akashangaa,
“Mlikuwa wote beach?”
“Ndio, huyu Erica ni mpenzi wangu”
Rahim akamuangalia Erica na kumwambia,
“Erica kwanini unakuwa muongo hivyo? Hupendezi kuwa muongo msichana mzuri kama wewe, kumbuka umeniambia hapa muda sio mrefu kuwa huna mchumba, kumbe unaye. Basi sema hapa ni yupi unayempenda kati yetu!”
Bahati akadakia,
“Ukweli ni kuwa Erica ananipenda mimi, ila wewe kakudanganya sababu kakuona ni tajiri”
Erica alichukizwa sana na maneno ya Bahati na kujikuta akiongea kwa jazba,
“Tena wewe Bahati unikome, nikome kabisa. Sijawahi kukupenda maisha yangu yote, nilikuwa na wewe sababu ya kukuonea huruma tu. Katika maisha yangu nampenda kijana mmoja tu anayeitwa Erick, na kwa ujinga wako huu huu umefanya nimkose Erick wangu”
Kisha akachukua mkoba wake na kuondoka, halafu akawaacha pale Rahim na Bahati wakiwa wanashangaa tu. Na wao hawakuweza kuendelea kuongea kwani muhusika alishaondoka na walimuona akipanda bodaboda na kutokomea, kwahiyo waliangaliana kisha Rahim akamwambia Bahati,
“Hakuna haja ya kugombana mimi na wewe ikiwa muhusika ameondoka, hata angekuwepo bado yeye ndio angekuwa na muafaka, sio mimi na wewe”
“Sawa lete simu yake”
“Hukunikabidhi wewe, nitairudisha mwenyewe”
“Usiwe mbishi, jua mimi ni mpenzi wake”
“Ila amekukana mbele yangu kuwa hajawahi kukupenda. Yani tusibishane bure hapa, si wewe wala si mimi anayependwa na Erica bali ni Erick. Kwaheri”
Rahim aliondoka zake, ikabidi Bahati nae aondoke zake ila bado alikuwa hajaridhika na moyo wake.