SEHEMU YA 77
Erica alikuwa na mawazo sana siku hiyo, akikumbuka kuwa Erick alimuona na Bahati wakikumbatiana ila Erick aliondoka kwa hasira na mpaka muda huo hakumtafuta, Erica akiwaza kuwa amtafute yeye na kujaribu kumuelewesha ila kila alipokumbuka aliyoambiwa na Tumaini hakutaka tena kuwasiliana na Erick,
“Sijui kwanini nimetembea nae, itabidi kesho nikapime ukimwi. Kumbe Erick kawa muhuni vile, najuta mimi Erica”
Aliwaza sana na kumfanya aumie sana moyoni mwake, ila jumbe alizozipata toka kwa Bahati zilimpa faraja sana.
Kesho yake hakuweza kufanikisha lile swala lake la kwenda kupima maana masomo yalikuwa mengi sana, kwahiyo akajikuta akiwa yupo makinisana na masomo yake, na alishtukia kuwa mwezi huo ni mwezi wa mitihani kwahiyo alijishughulisha sana na masomo hata hakutaka kuwasiliana sana, hata dadake alipompigia simu na kumwambia kuhusu kuongea nae alimwambia kuwa kipindi hiko ana mitihani kwahiyo aongee nae kwa kipindi kingine.
Kwahiyo karibia mwezi mzima alikuwa busy sana na masomo yake hadi pale walipomaliza mitihani na kufunga chuo kwaajili ya kuingia mwaka mwingine, mtu pekee aliyekuwa akiwasiliana nae mara moja moja kwa kipindi hiko alikuwa ni Bahati tu.
Erica alirudi kwao likizo ila alijiona kuwa yupo tofauti sana na siku zote, kwanza alikuwa akichoka sana na muda mwingi alijisikia usingizi na kujiuliza kuwa atakuwa na tatizo gani, akawaza kuwa kesho yake aende hospitali ili akaangalie hali yake vizuri.
Kesho yake ilivyofika, kabla hajajiandaa kuondoka, walifika nyumbani dada zake wawili, dada yake Bite akiwa ameongozana na dada yake Mage, aliwasalimia na kuwakaribisha.
“Mama yupo?”
“Ametoka ameenda kwenye kikoba”
“Haya, kilichotuleta sio mama ila tuna shida na wewe”
“Shida gani?”
“Erica, inabidi tukakupime ujauzito”
“Mkanipime ujauzito kwanini?”
“Erica usije ukatutia aibu, hebu nenda kajiandae huko twende hospitali, tulikuwa tunangoja tu ufunge chuo mjinga wewe”
Erica aliwashangaa sana dada zake hawa ila hakuweza kuwabishia maana walikuwa wakimfatilia vilivyo, basi akajiandaa ili aende nao huko hospitali, ila Mage akawakatisha
“Bite, kwanini tujisumbue kwenda mpaka hospitali wakati kuna vile vipimo vya mimba!”
“Vinapatikana wapi sasa”
“Maduka yote ya madawa, nenda kanunue basi”
Mage akamuelekeza Bite kisha Bite akaondoka na kwenda kununua, kwahiyo Erica alibaki na dada yao mkubwa Mage ambaye alimuita Erica karibu,
“Mdogo wangu kwanini umekuwa na tabia za ajabu?”
“Hapana dada sina tabia za ajabu”
“Yani kweli wanaume wanakufata hadi nyumbani unasema huna tabia za ajabu kweli?”
“Sasa dada mnavyonifanyia hivi mnaona ni sahihi? Mimi ni msichana mkubwa sasa”
“Hatukatai ni mkubwa ila bado hujaolewa, upo kwenye uangalizi wetu. Unafikiri leo na kesho ukileta matatizo hapa aibu kwa nani? Sisi ndio tutaaibika Erica. Katika watoto wote wa mama sikufikiria kama wewe unaweza kuwa na tabia za ajabu kiasi nilichoambiwa”
“Hapana dada, sina tabia za ajabu mimi”
“Sasa mdogo wangu huwa unahangaika na nini, si utulie tu ukimaliza chuo utaolewa”
“Dada, aliyewaambia mimi nahangaika nani? Mbona mimi ni mpole tu”
Mage alitumia muda mwingi sana kumshauri mdogo wake huyu na kumwambia kuwa kwanini wameamua kuja kumpima ujauzito maana wamekuwa na mashaka nae halafu habari zake wamezisikia.
“Mmezisikia wapi dada?”
“Jua kwamba habari zako tunazijua”
Erica alijiuliza sana kuwa wanajua habari zake zipi na wanazijua jua vipi ila hakupata jibu.
Bite alirudi na kipima mimba, kisha wakamtaka Erica kukinga mkojo wake ambapo alifanya hivyo na wakapima pale nay eye akiwa anaangalia,
“Mungu wangu Erica una mimba? Aibu gani hii umetupa jamani Erica?”
“Nilijua tu dada, ndiomana nikakuzania tuje tumpime ujauzito, aliyeniambia anamjua sana huyu mdogo wetu, kipindi hiki alikuwa na mitihani ila alikuwa analala sana badala ya kujisomea, kumbe ana mimba loh!”
Erica alikuwa kimya tu akiwaza maana ni swala la aibu kweli ila hakujua afanye nini, dada zake nao waliongea kwa ukali sana na gadhabu kubwa.
“Bite mdogo wangu twende kwanza tukajadiliane cha kufanya, tukikaa hapa na huyu mtoto tutampasua bure”
Wakaondoka na kumuacha Erica pale, muda kidogo mama yao alirudi ila Erica hakumwambia ukweli mama yake kuwa dada zake walifika maana aliona ni swala la aibu sana na hakujua hata ataanzia wapi kumwambia mama yao, kwani hata yeye swala lile lilimchanganya vilivyo.