SEHEMU YA 43
Ilikuwa siku ya kuzaliwa ya George na aliamua kwenda kwenye matembezi na mpenzi wake Erica,
“Utanipa zawadi gani kwenye siku yangu hii muhimu?”
Erica alicheka tu,
“Tafadhali Erica usiishie kucheka ujue nakupenda, na ninatamani kuwa na wewe”
Erica alijikuta amemkubalia George kuwa yupo tayari kutembea naye kwa siku hiyo, kwakweli George alifurahi sana na kutafuta chumba maeneo yale haraka iwezekanavyo.
Wakiwa ndani baada ya tendo, George alionekana kuchukizwa sana kisha kuchukua nguo zake na kuvaa halafu alimuangalia kwa chuki sana Erica, mpaka Erica aliogopa na kumuuliza,
“Vipi George imekuwaje?”
“Vaa nguo twende”
“Imekuwaje tena George?”
Safari hii George aliongea kwa ukali,
“Nimesema vaa nguo twende”
Kisha George alitoka nje, ikabidi Erica nae achukue nguo zake na kuvaa upesi upesi huku akijiuliza kuwa ni kitu gani amefanya.
Kisha George alitoka nje, ikabidi Erica nae achukue nguo zake na kuvaa upesi upesi huku akijiuliza kuwa ni kitu gani amefanya.
Lakini alikosa jibu kabisa maana yeye aliona kuwa ni kawaida sasa swala la George kuchukia kiasi kile lilimshangaza sana, akatoka nje ila hakumkuta George kwa maana kwamba alishaondoka muda tu, akachukua simu na kumpigia ila George hakupokea simu ile. Akajiangalia mfukoni, hakubeba hela yoyote maana George alimfanyia safari ya kumshtukiza, akawaza sana kuwa atafanyaje. Akampigia simu rafiki yake Dora,
“Best nimekwama huku, una hela kidogo unitumie nirudi, nikifika nitakupa hela yako”
“Umekwama wapi na kipi kilichokukwamisha?”
“Nitakwambia nikifika ila kwasasa nahitaji msaada wa pesa kidogo niweze kufanya nauli”
“Sina sh kumi shoga yangu, pole weee. Mpigie George”
“Hadi nimekupigia wewe jua nimekosa msaada kote huko, naomba nisaidie rafiki yangu”
“Sina hela”
“Niazimie hata kwa mtu nikirudi nitampa”
Simu ikakatika maana salio liliisha na kumfanya Erica achanganyikiwe zaidi ukizingatia kosa alilolifanya kwa George mpaka muda huo hakulijua na pia hakujua kuwa anarudi vipi hosteli, yani hapo kichwa kilikosa uelekeo kabisa.
Alienda kukaa mahali akilia maana hakujua hata aanzie wapi na aishie wapi, kuna mmama wa makamo alimuona na kumsogelea karibu na kumuuliza,
“Mwanangu vipi una tatizo gani? Mbona umejiinamia hapo? Unajua ni usiku huu?”
Erica aliinuka na kumuangalia Yule mama kwa uchungu sana, kisha akamwambia,
“Nimeibiwa mkoba wangu ndio ulikuwa na nauli hata sijui narudi vipi nyumbani”
“Pole sana, inuka mwanangu twende nyumbani kwangu maana huku nilikuwa nafanya mazoezi tu. Twende nyumbani nikakupe nauli naamini itakusaidia na utafika kwenu”
Erica aliinuka na Yule mama kisha kuanza kuondoka nae taratibu kuelekea anapoelekea Yule mama, kumbe alikuwa haishi mbali na maeneo yale maana walifika kwenye nyumba moja na kumkaribisha Erica,
“Karibu, hapa ni nyumbani kwangu. Karibu ndani nikutolee nauli binti yangu”
“Usijali mama, nitasubiria hapa hapa”
Erica hakutaka kukaribia ndani maana mambo ya mjini hayaelewekagi, unaweza kujikuta umekaribia kumbe unaenda kuchinjwa ila Yule mama nae hakutaka kumlazimisha sana Erica, alienda ndani na kumtolea nauli.
Alirudi na noti ya elfu kumi na kumkabidhi, kisha kujitambulisha
“Naitwa Mrs.Peter unaweza tu kuniita mama. Sijui wewe binti yangu unaitwa nani?”
“naitwa Erica”
“Karibu sana nyumbani kwangu, hapa ni kwangu hata usiwe na mashaka yoyote yale yani wewe ujisikie upo nyumbani. Sinaga mtoto wa kike, nina watoto wawili tu wa kiume na wote wapo masomoni nje ya nchi, karibu sana mwanangu”
“Asante sana”
“Unaweza ukawa unakuja kunitembeleaga, na vizuri ukinipa na namba zako za simu”
Basi Erica alimpa Yule mama namba zake za simu na kumshukuru sana kwa ukarimu wake kisha akamuaga na kuondoka zake.