SEHEMU YA 27
Kulipokucha akakumbuka kuhusu simu yake aliyoiacha nyumbani kwao hapo, akajiuliza kuwa aliiacha sehemu gani na je bado itakuwa nzima au mbovu akaanza kutafuta mule chumbani, alitafuta sana ila hakuipata, muda kidogo mama yake akamuita, alitoka na kumsalimia
“Unaonekana upo busy sana, unatafuta nini?”
“Hamna kitu mama”
“Mmmh mpaka leo Erica bado unamficha mama yako jamani, najua unachotafuta ni simu”
Erica akashtuka kidogo maana hakudhania kuwa mama yake anajua kuhusu ile simu, alibaki anamtazama tu na mama yake aliendelea kuongea,
“Umekuwa msichana mkubwa sasa na karibia utaenda chuo kikuu, mwanangu nilikuwa nafanya yote kukulinda ila bado nikashangaa umepata ujasiri wa kuhongwa simu! Mwanangu mwanaume aliyekuhonga simu hakukutakia mema na maisha yako, na Mungu ni mkubwa sana ukaisahau, unajua uliisahau wapi?”
Erica aliangalia tu chini, na mama yake aliendelea kuongea
“Uliisahau hapo kwenye meza ya kula chakula. Nilijua tu ni wewe umeiacha maana humu ndani tunakaa san asana wawili, sasa unajua kilichotokea kwenye ile simu?”
“Sijui”
“Basi ile simu ilianza kuita na hukuweka mlio zaidi ya mtetemeko tu, nilisikia kitu kikiungurumisha mezani, nikakuta anapiga mtu aitwaye John maana uliandika jina hilo. Nikataka nipokee nijue mbivu na mbichi kama ujuavyo mama yako sipendi kinishinde chochote, ila kwa bahati mbaya muda huo nilikuwa nimeweka ndoo maji ili nideki na ile simu iliniponyoka na kuingia kwenye maji”
Erica alishangaa sana, huku akitamani kujua nini kiliendelea kwahiyo alimuuliza mama yake,
“Kwahiyo ndio ikafa hapo?”
“Hapana, niliitoa na kuifungua nilitaka niweke ile laini kwenye simu nyingine ila wakati natoa ile laini kwenye ile simu ilivunjika, yani laini ilivunjika kabisa, na simu nimeiacha ndani nadhani imekuwa kopo sasa. Haya mwanangu uliitoa wapi na John ni nani?”
Erica aliona sasa ni njia pekee ya kujitetea maana mama yake hajajua ukweli wowote wa ile simu,
“Ile simu haikuwa yangu mama, ila kuna rafiki yangu wakati tunarudi aliisahau kwenye begi langu na bahati mbaya alisafiri kabla yangu kwahiyo alisema nimpelekee shuleni, na mimi nikaisahau hata sikujua nimeiacha sehemu gani”
“Kheee kumbe ni ya rafiki yako? Na huyo John?”
“Hata simjui mama, huniaminigi tu mama ila mimi sina mambo hayo, unamuona Yule mwalimu aliyesingizia kuwa kaniona mimi na Erick, kiko wapi sasa ndio kamzalisha Johari, mama kuna watu hawapendi tu maendeleo yangu, hayo mambo sina”
“Jitunze mwanangu, jitunze nije kula mahali yako nzuri. Uwe mtoto mwema na mzuri, umalize shule uolewe, mama zenu tulijitunza ndiomana hadi leo tupo kwenye ndoa zetu”
“Sina mambo hayo mama hata usinifikirie vibaya, mimi mwenyewe nataka nisome na nipate kazi halafu ndio niolewe. Sitaki kuchezea maisha yangu mama”
“Sasa huyo mwenzio ulimalizana nae vipi?”
“Nilimueleza dada Bite, na alimlipa Yule mwenzangu, ndiomana akaninunulia na mimi simu”
“Kwasasa tumia tu simu ila wasiliana na wasichana wenzio sio wakina John, sijui Erick hapana utaharibu maisha yako”
“Jamani mama, sina mambo hayo”
Erica aliona sasa amefaulu ule mtihani wa kutokuaminiwa na mama yake ingawa alijua wazi hawezi kuwasiliana tena na John, pia hakujua kama ingetokea siku aneonana tena na Erick, watu hawa alishawatoa kwenye akili yake ingawa mara moja moja alipatwa na mawazo kuwahusu ila bado hakujua ni yupi amchague kati yao maana wote walimvutia.