SEHEMU YA 328
Zilipita siku tatu, ilikuwa ni jioni wakati mama Erica akifagia uwanja wake, akashangaa kumuona tena Sia, na leo alivalia nguo nyeusi huku macho yakiwa mekundu kweli kweli, kwakweli mama Erica alihisi kuna jipya linazuka tena muda sio mrefu, ikabidi amuulize kulikoni, ila Sia alimsogelea mama Erica akamkumbatia na kulia sana, Yule mama akamuuliza kuwa imekuwaje,
“Mama yangu amekufa kweli, sina mama mimi. Liwazo langu kaondoka”
Akaendelea tena kumkumbatia mama Erica akilia, ikabidi mama Erica amuulize,
“Tatizo ndio lile lile la Erick kutokuongea na mama yako ndio kasababisha kifo au nini?”
“Hapana mama, Erick alikuwa akiongea vizuri kabisa na mama yangu hata leo asubuhi kaongea nae ila hali ya mama imebadilika jioni hii wakati tunatafuta usafiri tumuwaishe hospitali mama alikuwa ameshakufa”
Akaendelea kulia, ikabidi mama Erica aanze biashara ya kumbembeleza, kisha akaenda ndani kwake na kujivika kanga vizuri na kumuaga Erica,
“kuna msiba wa gafla umetokea ndio naenda”
Hakumpa Erica maelezo ya kutosha ila aliyoka nje na kuongozana na Sia kwenda msibani.
Alifika pale msibani kisha sia kwenda kuungana na ndugu zake wengine wakiendeleza vilio, Mama Erica aliingia nae ndani na kutoa pole kisha akatoka nje ili kuungana na wanawake wengine katika shughuli za pale kama kuandaa chakula na kuweka sawa mazingira ya msiba maana msiba hauna ugeni, aliwakuta wanapika chakula cha watu kwa usiku wa siku hiyo, sema hapakuwa na wamama wengi sana sababu msiba ndio umetokea siku hiyo hiyo, hadi mama Erica akaauliza,
“Mbona watu si wengi?”
“Aaah kwani na wenyewe walikuwa na tabia ya kushtuka msiba ukitokea basi? Baba yao ndio alikuwa hodari na alipokufa basi tena ila wat wengi watakuja siku ya mazishi”
wakati wanapika pika na wanawake wa pale wakaanza kuongea wakiongea,
“Yani hawa watoto akili zao jamani ni mbovu tu, mama yao anaumwa siku nyingi badala wampeleke hospitali eti atapona tu”
Mwingine akadakia,
“Mimi nilikuwa nikimkuta kazidiwa, nikiwaambia habari za hospiatali wanasema wana dawa zao”
“Kwanza cahanzo cha ugonjwa wa mama yao ni nini?”
“Huyu mama tangu mumewe amekufa basi na yeye akaanza kuumwa, ila kipindi hiki ndio vikachachamaa ila watoto wanadai wana dawa zao”
“Dawa gani hizo? Mbona mama yao kafa sasa kama wana dawa zao?”
“Yani watoto wajinga wale, sijui dawa gani wenyewe. Nakumbuka miaka miwili iliyopita kulikuwa na kijana mmoja anabadilishaga magari Yule mvulana, kazuri zuri hivi, ndio alikuwa anakuja na kumpeleka Yule mama hospitali hadi akawa anaendelea vizuri ila nimeshangaa mwaka huu toka uanze ukimkuta kazidiwa unajibiwa kuwa kuna dawa zake”
“Unajua hospitali ni muhimu sana, hata kama unatumia dawa za kienyeji ila nenda hospitali kwanza ujue unaumwa na nini, hata waombeaji wenyewe huwa wanasema kapime kwanza, maana ugonjwa ukijulikana ni rahisi zaidi tofauti na ugonjwa usipojulikana”
Mama Erica alisikiliza kwa makini sana na kugundua kuwa pale kulikuwa na tatizo licha ya Yule mama kuugua hadi kufa ila kulikuwa na tatizo.
Basi mama Erica alishughulika pale kisha alipoona usiku umeingia sana akaamua kuondoka kidogo kurudi nyumbani kwake maana asingeweza kulala hapo msibani kwani hata kwake hakutoa maelezo ya kutosha.
Alimkuta Erica akiwa sebleni tu maana ilikuwa ni usiku tayari. Erica alimsalimia mama yake kisha kumuuliza kuwa alikuwa akiwahi kwenye msiba wa nani maana alimwambia tu kuwa anaenda msibani,
“Nilienda kwenye msiba wa mama wa mke mwenzio”
“Mama wa mke wmenzangu? Kivipi?”
“Mama yake na Sia amekufa”
“Kheee mamake amekufa, masikini jamani”
“Hiyo kusikitika ya leo mbona haikuwepo siku ile Erica eeeh!!”
“Jamani mama! Lazima nisikitike maana si kitu nilichokitarajia, mbona niliongea vizuri na Erick kuwa awe anampigia simu mara kwa mara mama yake Sia, jamani mama wa watu amekufa! Inamaana Erick alikuwa apigi simu?”
“Hebu wewe nawe nitolee ujinga mie, huyo Erick ni daktari kusema akipiga simu anasema watumie dawa Fulani au nini? Erick ndio malaika mtoa roho kusema huyu nimchukue sasa au nini, hebu nitoleeni balaa, sema uzuri hujawa chanzo tena cha kifo cha huyu mama. Nadhani kifo chake kilifika ila kama kawaida wanadamu hutafuta sababu tu, mwishowe wakuchukie bure.”
Erica alibaki kusikitika tu, kisha akaenda chumbani kwake na kumpigia simu Erick ila simu yake haikuwa na salio, yani pale alipata mawazo sana kwani alihitaji haswa kuongea na Erick, akawaza akaona ni vyema akanunue vocha ili ampigie na kuongea nae, akatoka chumbani kwake na kujifunika kanga, ila mama yake alikuwa sebleni na kumuuliza,
“Haya saa hizi unataka kwenda wapi?”
“Nataka kwenda dukani mama kununua vocha”
“Hapana, siwezi kukuruhusu uende dukani muda huu, Erica mwanangu kumekuwa na matukio kwako yasiyoeleweka kabisa, hivi naanzaje kukuruhusu kwenda dukani eeeh! Ngoja kesho utaenda”
“Jamani mama”
“Nimesema leo hutoki, umenisikia? Wewe jione ni mtu mzima ila mimi nakuona bado ni mdogo sana, leo hutoki kwenda popote muda huu”
kisha mamake akaenda kufunga mlango na kwenda na funguo chumbani kwake, kwahiyo Erica hakuwa na namna yoyote ile zaidi ya kurudi chumbani kwake, ila alikuwa na mawazo sana hadi hakuwa na raha sababu alitamani sana muda huo aongee na Erick na hakujua ni kwanini Erick hakumpigia simu siku hiyo.
Alipokuwa amekaa na mawazo chambani kwake muda kidogo akapigiwa simu na namba ngeni, Erica alipokea simu hiyo kwani alikuwa na mawazo sana na Erick, kwani alikuwa akidhani mtu akimpigia simu ni Erick ingawa alikuwa akiona kabisa ile namba si namba ya nchi aliyokuwepo Erick, alipokea na kuongea nayo na kugunduwa kuwa mpigaji ni mzee Jimmy,
“Kheee bado unanifatilia wee mzee?”
“Naachaje kukufatilia Erica eeeeh! Katika maisha yangu sijawahi kumpenda mwanamke yoyote kama ninavyokupenda wewe, usisikilize maneno ya mama yako, nikubali mimi na huyo mwanao ataishi maisha mazuri kama jina lake”
“Asante kwa hayo maisha mazuri ila mimi nimeridhika”
“Erica, nishaiambia familia yangu yote kuwa nataka kuoa na wote wamenikubalia, niruhusu nikuoe Erica”
“Unajua unanichosha yani unanichosha sana, huwa sipendi hata kukusikia ukiongea kwenye simu unanichosha balaa”
“Erica, pole kwa kukuchosha. Naomba unisamehe, nifanye nini ili unisamehe?”
Erica akakumbuka kuwa anahitaji vocha, alijikuta tu akimuambia,
“Nitumia vocha”
“Hilo tu Erica? Niambie kitu gani tena?”
“Nitumie vocha nina shida nayo”
“Nikutumie ya shilingi ngapi?”
“Ya elfu tatu”
“Sawa nakutumia Erica, nakupenda sana umechanganya akili za mtu mzima mimi”
Basi Erica akakata ile simu na baada ya muda mfupi vocha iliingia kwenye simu yake, kuangalia ilikuwa ni vocha ya elfu hamsini, akatabasamu kisha akabonyeza namba za Erick na kumpigia, ambapo simu iliita bila kupokelewa, alipiga kama mara tatu na sim haikupokelewa, alikuwa na mawazo sana maana sio kawaida kabisa, hakuwa na ugomvi mkubwa na Erick wa kusema ashindwe kupokea simu, akashangaa sana, alikaa kama lisaa lizima, yupo macho tu akajaribu tena kupiga simu muda huu Erick alipokea simu ya Erica, ila Erick aliongea katika hali ya ulevi sana, mpaka Erica akamshangaa,
“Erick umeanza tena kunywa pombe kiasi hiko kweli? Si ulisema ulevi ulianza sababu yangu, leo vipi upo na mimi na unakuwa mlevi?”
“Erica huelewi tu”
“Sielewi nini sasa”
Erick alikuwa hata kujibu hajibu vizuri sababu ya kulewa hadi Erica aliamua kukata simu kwa hasira, huku akichukia sana moyoni, alihisi Erick kuna mwanamke mwingine anamsumbua ndiomana kaamua kunywa pombe, alijikuta akiumia sana yani siku hiyo hakuweza kulala kabisa.
Kwa kukosa usingizi hadi aliamua kuingia tena kwenye mtandao wa kijamii baada ya kipindi kirefu sana tangu alipogombana na Rahim, na alivyoingia tu alikutana na jumbe kadhaa za Rahim zikimpa lawama tu, kisha muda huo huo Rahim alituma tena ujumbe,
“Erica, leo umeingia mtandaoni siamini”
“Nipo”
“Habari Erica, mtoto anaendeleaje?”
“Leo ndio umejua kuwa una mtoto na mimi? Wewe si ulijifanya kunijibu shombo wewe?”
“Erica, una matatizo wewe sio bure, kwani hujui kosa lako la mimi kuwa vile? Hivi unawezaje kumuomba mwanaume milioni kumi na tano? Kuna mwanaume kichaa anayeweza kufanya hivyo? Hakuna mwanaume wa kukupa hela hiyo hata awe na hela kiasi gani”
“Si kweli Rahim, ungekuwa na malengo na mimi ungenipa. Najua hiyo hela uwezo nayo unao, na hata kama ungekuwa huna ungeniambia kiustaarabu ila sio kwa majibu yal uliyonipa, sikufurahishwa nayo kwakweli”
“Sawa, hukufurahishwa nayo ila namtaka mwanangu Erica”
“Usinichanganye, unamtaka mwanao kivipi? Mama yako mwenyewe alikuja hapa na hata kurudi tena hajataka, na mtoto mwenyewe alikuwa na mashaka nae kuwa si wa kwako halafu wewe unamuhijtaji mwanao kwa kigezo kipi haswa?”
“Unajua fika Yule ni mwanangu, yani hata uongee vipi ila ukweli unaujua kuwa Yule ni mwanangu, sikukutuma uje kwangu ila umalaya wako ndio uliokuleta kwangu, hadi ukadanganya kwenu kuwa unasafiri wakati unakuja kulala na mimi sababu ya umalaya wako na mimba ukabeba ukijua nitakuoa, ulibugi kwakweli kwani siwezi kuoa mwanamke kama wewe”
“Yani leo hii Rahim ndio unaniita malaya? Kwahiyo mtoto umezaa na malaya?”
“Erica, unajua sipendi kuongea sana, namtaka mwanangu. Ndio wewe ni malaya, kwani nani hajui hilo? Wewe mwanamke hufai ndiomana hata wazo la kukuoa halikuwepo katika akili yangu”
“Ulivyokuwa unaniambia unanipenda?”
“Nilikuwa nawe ili kupoteza muda tu, nilikwambia vile ili uniamini ila kiukweli wala sikukupenda. Mwanamke gani wewe, nasikia ulitembea na familia yangu nzima, na atakayekuoa wewe atakuwa chizi, hakuna mwenye akili timamu atakayemuoa mwanamke wa dizaini yako, na hata huyo mtoto namtaka tu ila sijui kama naye hajanitia aibu maana mtoto wa nyoka ni nyoka”
“Kwahiyo ndicho ulichotaka kuongea na mimi hicho mtandaoni kuwa kila siku ingia mtandaoni kumbe ndio ujinga huo unataka kuniambia?”
“Sio ujinga ila nakwambia ukweli, kawaida wanaume kuwa na wanawake wengi ila mwanamke kuwa na wanaume wengi kwa hakika huyo mwanamke hafai kwenye jamii, Erica huwezi kuolewa wewe kamwe, maana mtu akijua tu tabia yako atakuacha”
Erica alichukia sana na kutoka kwenye mtandao wa kijamii huku akianza kutokwa na machozi na kuitathmini tabia yake, ila alihangaika kote kutafuta penzi la kweli, alijiona mjinga sana kuhangaika na wanaume waliomwambia kuwa wanampenda kwa kumsanifu tu.
“Hivi mtu unawezaje kujifanya unampenda mtu wakati humpendi? Kweli kabisa leo hii huyu Rahim ndio ananiambia maneno haya jamani? Kuna uwezekano mkubwa sana wa wote waliosema wananipenda kumbe hawanipendi wala nini? Ni nani anayenipenda kweli? Hivoi Erick ananipenda kweli au na yeye atanigeuka siku moja kama leo alivyolewa? Lakini hapana Erick ananipenda bhana, nayachukia mapenzi, sijui kwanini yapo.”
Kiukweli siku hiyo hakulala kabisa kwani alijikuta akiwa na mawazo mengi sana mpaka asubuhi.