SEHEMU YA 299
Basi Yule mama akampa ruhusa ya kuondoka tu bila kinyongo, wakati Erica anatoka kwenye ile hoteli alimuona Sia mlangoni, alishtuka sana akaamua kujibanza ili Sia asimuone basi Sia akapita pale na Erica akaanza kumfatilia nyuma kuwa Sia anaenda wapi, akamuona akienda alipo Yule mama na alipofika alikumbatiana na Yule mama, ndipo akili ikamjia kuwa Yule ni mama Erick.
Kwakweli Erica aliishiwa raha muda ule, hata furaha hakuwa nayo tena, akaondoka na kuelekea nyumbani kwao.
Alipotoka tu nje ya ile hoteli wakati anatembea akielekea kituoni, hakuangalia mbele, kuna mmama aligongana nae na kujikuta akiangusha vitabu vya Yule mama ambavyo alikuwa amevibeba, aliinama kuviokota huku akimuomba msamaha sana Yule mama, ila Yule mama alimwambia,
“Usijali binti, ila unaonyesha una mawazo sana”
Erica alicheka tu ili kujigelesha swala la kuwa na mawazo, basi Yule mama alimuomba Erica namba ya simu na kusema,
“Mimi ni mwanamaombi, nimeomba namba yako ili niwe nakualika kwenye maombi kanisani kwetu. Hivi nawahi kanisani”
Kwavile Yule mama alijitambulisha kuwa mwanamaombi basi Erica hakusita kutoa namba yake kwa Yule mama kisha alimuaga na kuendelea na safari ya kuelekea kituoni.
Wakati yupo njiani akielekea kupanda daladala, alikutana na Moses njiani ambaye alisimamisha gari na kutaka kumpa lifti,
“Hapana usijali, naenda tu mwenyewe”
“Hapana Erica, yani nikuone hapa njiani nikuache kweli! Unataka nionekanaje mimi, naomba nikupeleke tu, si unaenda kwenu?”
“Ndio”
“Basi, naomba nikupeleke”
Basi Erica hakuona kama ni vyema kuendelea kubishana na Moses pale kwahiyo alipanda ile gari ya Moses na safari ya kuelekea kwao ikaanza.
Ila Moses alimuona Erica kama anainesha hana furaha ilibidi amuulize,
“Mbona unaonekana huna furaha?”
“Hamna nipo kawaida tu”
“Ni muda mfupi nimekuzoea Erica, hapana hivi ulivyo sio kawaida, inaonyesha una tatizo. Haya bhana kama hutaki nilijue”
Erica aliamua kubadilisha mada na kumuuliza,
“Kwani ulikuwa unaenda wapi?”
“Aaah leo niliwahi kutoka ili nimuwahi mke wangu, nimemmiss sana, wiki yote hii nipo busy sina siku ya kupumzika yani kila siku nipo kazini, kwakweli leo nimewahi kutoka na kesho nimemuomba udhuru Erick maana sitafungua duka nahitaji kuwa karibu na mke wangu”
“Sasa kumbe unawahi kwa mkeo, mbona umejitolea kunipeleka mimi nyumbani?”
“Erica, hivi naanzaje kumwambia Erick nilikutana na Erica njiani akielekea nyumbani ila sikumpeleka, naanzaje kusema? Unajua sielewi kipi kipo katikati yenu wewe na Erick ila nahisi mnajuana, mi nikikupeleka ndio nitaenda kwa mke wangu najua hata Erick nikimwambia hivyo atafurahi sana”
Erica akatabasamu tu na kumuuliza tena Moses,
“Inaonyesha unampenda sana mke wako”
“Yani nahisi nampenda kuliko hilo neno na sana, yani nampenda balaa”
“Hukuwahi kuwaza kumsaliti?”
Moses akacheka,
“Erica, huwa nakutana na wasichana warembo kama wewe hivyo ila kwakweli sababu mke wangu nimempa nafasi ya kwanza basi anakuwa ni mrembo kuwazidi wote. Na kwanini umeniuliza hilo swali?”
“Nasikia wanaume hawajatulia na mwanaume hawezi kutulia na mwanamke mmoja yani lazima atatafuta wa pembeni”
“Tatizo watu hutoa jibu kwa mfano wa mtu mmoja tu. Mimi toka nimuoe mke wangu sijawahi kumsaliti hata mara moja na wala sifikirii kumsaliti nampenda sana. Sisi wanaume pia tunapenda, ukiona mwanaume anahangaika na huyu mara Yule ujue hajapata bado Yule wa kwenye roho yake ndiomana anashika huyu mara huyu ili kuangalia je anaweza akamteka akili yake, ila akishampata wa kwake lazima atatulia. Yani mara nyingine sio mambo ya kulaumu sana sijui wanaume hawajatulia sijui nini na nini, watu hawaelewi tu mtu anakuwa hajapata hitaji lake au anayempenda kwa dhati anazingua ndio utakuta anahangaika hangaika ila akimpata wake hadi utashangaa ndio huyu kweli wa kuruka ruka na wanawake”
Erica alitabasamu tu kwani hapo aliweza kuelewa kuwa kwa Erick basi ni yeye ndiye mwenye nafasi kubwa sana, Moses alimuona Erica akitabasamu tu na kumuuliza,
“Vipi mbona furaha tu”
“Nimefurahi, nimependa vile ulivyosema unampenda sana mkeo. Hakika ulimwengu ungekuwa kama unavyosema basi hata magonjwa ya zinaa yasingekuwepo. Tatizo ni moja tu huyo mwenye upendo wa dhati utamjuaje?”
“Inamaana wewe humjui unayempenda kwa dhati? Yani mtu ukimpenda jamani, hata ukisikia jina lake tu unajisikia furaha, unaweza ukakaa halafu labda likatokea jambo unajikuta ukiwaza angekuwepo Fulani hapa yani unajikuta unapenda tu uwepo wake. Ila kama mtu upon aye tu kupeleka siku mbele vyovyote vile unaona sawa, awepo asiwepo unaona sawa, apige simu, asipige unaona sawa yani hata hujali uwepo wake ila unaweza kujigelesha na kujifanya kuwa unamkumbukaga kumbe kiukweli hakuna kitu”
Walifika nyumbani kwakina Erica, kwakweli Erica alimshukuru Moses na alishukuru pia kwa mazungumzo aliyozungumza nae kwa siku hiyo, kisha akamuaga na kuingia ndani.
Aliingia ndani kwao na kumkuta dada yake Bite pamoja na James, inaonyesha walifika kama mama yao alivyosema kuomba msamaha, pia ilionyesha ni muda huo huo ndio wametoka kufika. Baada ya salamu Erica aliambiwa na mama yake akae pale kwani walihitaji wasikie wote msamaha anaouomba James kwa Erica, basi james alianza,
“Erica shemeji yangu, mdogo wangu naomba unisamehe maana nilichokuwa nafanya kwako sio sawa. Ni shetani tu huyu anataka kuharibu undugu wetu, naomba unisamehe sana. Mimi bado ni shemeji yako na mimi bado ni mwanafamilia wenu. Naomba unisamehe Erica”
“Hakuna tatizo, nishakusamehe ilimradi umegundua kosa lako basi nimekusamehe”
“Nashukuru sana, mama naomba nawe unisamehe sana mtoto wako. Nisamehe kwa yote niliyokuwa nasema kuhusu Erica, nisamehe kwa tukio lile, ni shetani tu alinipitia”
“Nilikuwa nakusikiliza kwa makini sana habari za kusema shetani kakupitia, James usisingizie shetani ila ni akili zako mbovu ndio zimekutuma kufanya vile. Mimi sina tatizo, kaa chini na mkeo mlee mtoto wenu, ujinga ujinga wa kuendekeza ngono utakuponza. Mbona mwanangu Bite mzuri tu jamani kwanini unashindwa kuridhika James? Hebu tulia na mwenzio, na kipindi ukimchoka niletee mwenyewe nikae nae.”
“Usifike mbali mama yangu, nisamehe mtoto wako”
“Nishakusamehe na sina tatizo tena. Ila naomba nikuombe jambo moja”
“Jambo gani mama?”
“James, ingawa tumekusamehe na hatuna tatizo na wewe ila tafadhali sana sitaki ukaribu wako tena na Erica maana huyo shetani wako akakupitia tena ukasababisha matatizo kwa wanangu bure. Sitaki tena ukaribu wako na Erica, una shida yoyote kwa Erica niambie mimi nitafikisha ujumbe”
“Sawa mama nimekuelewa”
“Sawa, najua na mkeo mlishaombana msamaha huko mpaka mmefika hapa”
Bite akajibu,
“Ndio mama, nimeshamsamehe”
“Ila sio unasema umeshamsamehe huku bado una kinyongo moyoni, mumeo kakiri mwenyewe hapa ana urafiki na shetani hadi huwa wanapitiana, kwahiyo elewa kabisa sio unaitikia halafu kesho na keshokutwa unaanza sijui mama kimeenda kimerudi sitaki”
“Sawa mama”
Kisha wakainuka na kushikana mikono, na muda ule ule Bite na mumewe waliaga kwani bado James aliona aibu kuendelea kuwa mahali hapo akizingatia mama yao na wakina Bite hajambakisha na kitu, amemwambia ukweli tu.
Walipoondoka, Erica nae alienda chumbani kwake.