SEHEMU YA 240
Kwenye mida ya saa kumi jioni, James alimuita Erica na kumpa ruhusa ya kuondoka,
“Yani hata hukumbuki kuwa unatakiwa kwenda chuo?”
“Nilisahau”
“Hebu acha mawazo Erica, fikiria maendeleo yako tu kwasasa, acha mawazo ya kijinga hayo mdogo wangu”
Muda huu Erica alijisikia vizuri sana kuitwa mdogo wangu na James, basi akamuaga pale na kuondoka zake.
Alienda kupanda daladala, ila leo kuna wakaka walikaa pembeni yake na akasikia maongezi yao,
“Yani mademu hawa vimeo vimeo, kuna demu nimekutana nae, ukimuona ni staarabu kumbe ni mbwa tu”
“Yule wa siku ile? Nilikwambia lakini jomba hukunisikia, uliona kama nakuonea wivu ndugu yangu, Yule demu jau yani kimeo cha mwisho”
“Najuta hata kutokufuata ushauri wako, ila mimi nikija kupata demu mwenye upendo wa dhati hakika nitatulia”
“Upendo wa mademu upo kwenye hela, yani ukiwa na pesa utapendwa wewe balaa ila uwe kapuku sasa utajuta yani mademu kwa pesa huwawezi ndiomana mimi sina demu wa kudumu huwa natembea nao na kuwaacha”
Erica aliwasikiliza mpaka alipofika kwenye kituo chake na kushuka ila kwa maongezi yale aliyoyasikia aliona kuwa wanaume wanapenda kuchezea wanawake wakati hata wao walikuwa wanalalamika kuwa wanawake wana matatizo.
Alifika nyumbani kwao na kumsimulia mama yake kuwa Yule mtu alifika ofisini kwao, ila hakumwambia kilichomnfikisha pale Yule mtu,
“Kumbe ni rafiki wa shemeji bhana Yule mkaka”
“Kheee mwanangu ila nilikwambia, kuwa makini na majibu sio kila kitu ni kujibu vibaya”
“Ila mama kama mtu anakutongoza na humtaki?”
“Si nishakwambia, mjibu kiustaarabu kwani ukisema hapana sitaki kuna tatizo gani? Sio unaanza ooh wewe sijui dini nyingine, kimeenda kimerudi sasa ndio nini hapo? Unatakiwa kuwa na jibu moja linaloeleweka”
“Sawa mama nimekuelewa na sitorudia tena mama yangu”
“Ndio usirudie, unanidhalilisha mimi ukifanya ujinga”
Erica aliinuka na kwenda chumbani haraka haraka maana alijua pengine mama yake angemuuliza kuwa mbona kawahi kurudi.
Alikaa chumbani ila wazo la Erick lilimjia kichwani na wakati akimfikiria Erick alipigiwa simu muda huo huo na Erick, kwakweli Erica akatabasamu na kuona ni jinsi gani upendo kati yake na Erick ulivyo mkubwa kiasi kwamba hata Erick anamuwaza vile vile na yeye anavyomuwaza, Erica akapokea ile simu
“Mbona kimya mpenzi wangu hukunitafuta tena?”
“Siku hizi nimeanza kazi Erick, kwahiyo narudi nyumbani nikiwa nimechoka balaa ila nakukumbuka sana tu, yani hata muda huu nimetoka kukukumbuka”
“Vipi facebook siku hizi hutumii?”
“Natumia”
“Mbona huwa sikuoni?”
Erica akakumbuka kuwa alifuta urafiki na erick maana hakutaka kumkwaza Rahim, alimwambia Erick,
“Labda nilitoa urafiki kwa bahati mbaya, ngoja nikuombe tena urafiki ili tuwe tunawasiliana”
“Sawa”
Erica alikata simu na kwa mara hii akachukua ile simu yake na kuingia kwenye mtandao ingawa kwa siku hizo hakupenda kuingia kwani kila alipomuona Rahim alihisi kuumia sana, na leo alikuta Rahim yupo hewani vizuri kabisa ila hakutumiwa ujumbe wowote na Rahim, akamtumia Erick ombi la urafiki na Erick alilikubali muda ule ule na kuanza kuwasiliana nae kwenye mtandao sasa,
“Ila Erick, muda sio mrefu nitalala, maana nimechoka”
“Sawa Erica, ila nakumiss sana na ninatamani siku moja tuishi wote. Subiri tu nirudi kutoka Kusini, ila usinisaliti Erica”
Kidogo Erica alisita kujibu maana kama usaliti kashaufanya sana tu mpaka na mtoto kapata, ila akamjibu kuwa asijali hatomsaliti, bado hakuweza kumwambia Erick kuhusu mtoto aliyekuwa nae maana alihisi kama upendo juu yake utapungua.
Akamuaga Erick kuwa muda huo analala, ila kabla hajatoka hewani alishangaa ujumbe kuingia kutoka kwa Rahim, akaufungua na kuusoma,
“Kweli mwenye asili haachi asili, kwahiyo umemtafuta Erick hadi kuanza tena urafiki nae? Nashukuru Erica, hela zote nilizokuwa nakupa ni kazi bure”
Erica alisoma mara mbili mbili ujumbe wa Rahim bila hata kuelewa kuwa Rahim amejuaje kuwa yeye na Erick wameanza urafiki tena, ila akakumbuka kuwa facebook ina mtindo wa kuandika Fulani na Fulani wamekuwa marafiki, kwahiyo inamaana labda Rahim kaona ujumbe huo ndio kajua kuwa Erica na Erick wamekuwa marafiki tena. Erica hakujua ajibu nini kwahiyo alipotezea huo ujumbe na kulala tu.
ITAENDELEA