SEHEMU YA 225
Alifika kwao na kukutana na mama yake ametoka dukani kwahiyo waliingia wote getini, mama yake alimuuliza kwa mshangao,
“Kheee Erica, leo umekuja kwa mguu bila gari? Yani mtoto wako umemuacha wazi kabisa”
“Nimechoka mama, nitamficha mtoto huyu hadi lini?”
“Ukiwaza hayo, wazo na kuwa utawezaje kueleza watu kuwa mtoto hana baba?”
“Jamani mama, kwani kuna watoto wangapi baba zao wamekufa na wanaishi?”
“Weeee usitake kufananisha watoto ambao baba zao wamekufa na mwanao, kumbuka wale baba zao wapo ila wamekufa ila mwanao hana baba kabisa yani hiyo ndio tofauti yao”
“Mama, kwakweli humu ndani mnanichanganya jamani. Mimi nishajiamulia kuishi na aibu yangu, kama huyu mtoto simtaki basi nikamuuze huko ila sio kumficha”
“Yani Erica, unamjibu mamako majibu ya shombo kiasi hiko jamani. Wewe mtoto loh! Utajibu mwenyewe wajomba zako wakija, na Yule mjomba wako aliyekuwa akikulipia ada utamuonyesha shahada uliyoipata chuo ulipomaliza walikutunuku mtoto”
Erica akaona si vyema ajibishane na mama yake, kwahiyo aliamua kwenda ndani tu.
Alicheza cheza na mwanae na kumlisha, kiukweli mwanae hakuwa mtoto msumbufu na alikuwa na afya nzuri tu kwahiyo haikumpa shida sana kwenye kumlea.
Usiku wake akawaza jambo moja, akakumbuka jinsi Rahim alivyomwambia kuwa anaomba hela za matumizi badala aombe hela za biashara, akafikiria kumuomba Rahim hela ya biashara ila akafikiria ni biashara gani sasa atafanya,
“Mmmh nitaenda kwa yule kaka kuangalia biashara ya hivyo vitu vya watoto halafu niianze hiyo biashara”
Akamsikia dada yake amerudi maana dada yake alianza tena kwenda kazini, kwahiyo alimfata kuongea nae ili kumuuliza kama ameshawahi kusikia biashara ya vitu vya watoto, alimsalimia pale na kumpa pole ya kazi kisha akamuuliza kuhusu hiyo biashara,
“Ni biashara nzuri sana umewaza mdogo wangu, ila hiyo biashara ukitaka ufanye vizuri na uheshimike, unatakiwa uwe na mtaji wa kutosha”
“Kama kiasi gani dada?”
“Kwa kuanzia sio mbaya ukiwa na milioni kumi na tano”
“Mmmh dada, mbona hela nyingi hivyo?”
“Hahaha Erica, bado hujaijua hela wewe yani milioni kumi na tani ni nyingi? Ukiwa na hela hata sio nyingi, sema ni kwavile hela hamna ndiomana”
“Nataka nimuombe baba wa mwanangu”
“Ila kama huyo mwanaume alikuwa nankupa hadi milioni tatu, nne sidhani kama milioni kumi na tano itamshinda. Tena atafurahi sana ukiwa na wazo la kufanya hivyo”
“Sawa dada, kwahiyo nimuombe milioni kumi na tano eeeh! Si utanisaidia dada kwenye hiyo biashara?”
“Nitakusaidia ndio, mimi nina rafiki zangu wengi tu wanajishughulisha na maswala ya bishara. Hata usijali nitakusaidia maana kusubiri kazi ni ngumu kwa kipindi hiki”
Erica alimshukuru pale dada yake, kisha muda wa kwenda kulala alimtafuta Rahimhewani na alimkuta ila leo hakutaka kabisa kumuanzishia mada sijui amekutana na mama yake pamoja na Salma, sijui swala la kumdanganya kumbe Salma ni mjamzito. Hakutaka kuzungumza nae swala hilo, na moja kwa moja alimueleza swala lake la kutaka biashara,
“Biashara gani utaiweza wewe?”
“Nataka biashara ya kuuza nguo za watoto na vitu vyao vya kuchezea”
“Kwahiyo unataka mzigo ukachukue China na Dubai?”
“Aaah ikiwezekana kufanya hivyo nitafanya, ila kwasasa nahitaji kuanza hiyo biashara”
“Haya, mtaji kiasi gani?”
“Milioni kumi na tano”
“Na wewe una kiasi gani?”
“Mimi sina hela ndiomana nimekwambia wewe Rahim, si unajua nimemaliza chuo nikawa kwenye uzazi, sasa hela nitatoa wapi mimi?”
“Usinitanie Erica, hela zote nilizokuwa nakupa ulizipeleka wapi?”
“Rahim jamani, hakuna hela uliyonipa bila sababu. Hel azote zilikuwa na sababu na zilienda kwenye matumizi ya hizo sababu, sasa ningekuwa nazo ningekuomba kweli?”
“Erica, kuna wanawake wangapi wanauza maandazi, vitumbua, kachori, visheti? Kuna wanawake wangapi?”
“Wengi sana”
“Na wewe kwanini usiwe katikati ya hao wanawake?”
“Jamani Rahim, kwanini lakini unanifanyia hivyo? Sijazoea kuuza vitumbua, sijui visheti, hizo biashara zinataka mazoea”
“Aliyekwambia wale wamezoea nani? Yani Erica unataka mimi nitoe milioni moja, mbili, tatu, nne hadi kumi na tano kweli? Wewe msichana una akili kichwani mwako? Kichwa chako kizima hiko? Yani nitoe milioni kumi na tano kweli? Yani unaitamka kama sijui ni hela ndogo. Erica, kweli kabisa milioni kumi na tano?”
“Jamani Rahim, unajua mimi nikifanya biashara sitakusumbua wewe kuhusu swala la mtoto maana nitakuwa najitosheleza kuliko hivi. Kumbuka ni wewe ulinishauri nifanye biashara, kweli saizi unanishangaa jamani?”
“Kama unataka kusaidia kwenye malezi ya mtoto, kwanini usitafute kazi? Au basi ungeniambia naomba hela nianze biashara ya sambusa, najua mtaji wake hata elfu hamsini haifiki, unaniambia kitu cha mtaji wa mamilioni ya pesa jamani Erica? Unahisi sina majukumu mengine ila nina majukumu ya wewe tu?”
“Rahim, sikuelewi yani sikuelewi kabisa. Kwani ni kitu gani unachotaka mimi niwe? Kwakweli Rahim hapana jamani, mtandaoni kwenyewe nikutafute mimi, kila kitu nikubembeleze kama mtoto mchanga. Na kutwa kunitoa akili yani kama duniani nipo peke yangu nisiyekuwa na akili. Nashukuru Rahim kwa hayo unayoniambia”
“Ila kwani nakwambia uongo? Erica kiukweli akili huna, hata mwanaume atakaye kuoa atajuta, wewe sio mwanamke wa kuolewa maana huna akili hata kidogo. Huwezi kuja kuniomba hela yote hiyo mimi, kwa kazi gani ninayofanya?”
“Kweli nimeamini, mwanaume akishakutumia anakuona huna thamani tena. Siku zote hukujua kama sina akili hadi umenizalisha? Na ulianzaje kuzaa na mwanamke asiye na akili? Rahim, kwasasa nimefika mwisho maana nishajibembeleza kwako hadi nimechoka”
“Kwahiyo unamaanisha nini?”
“Rahim, kuanzia leo sitakutafuta tena hewani, sitakuomba tena hela yoyote ya matumizi ya mtoto yani sitakusumbua kwa chochote kile. Mimi ni mwanamke ndio ila nitapambana na nitaishinda hii hali, nimepata aibu, nimedhalilika ila bado sijafika mwisho. Kwaheri”
Alituma ujumbe ule akitegemea kujibiwa kwa kuombwa msamaha na Rahim ila ule ujumbe haukujibiwa na ilipita saa nzima bila ujumbe kujibiwa huku Rahim akionekana hewani tu, kitendo hiko kilimuumiza sana Erica, alijikuta akimwaga machozi.
Alilia sana hadi alisikia jogoo zikiwika na kugundua kuwa kumekucha, akachukua simu yake kuangalia mida akakuta ni saa kumi alfajiri, alihisi kichwa kikimuuma kwa kulia sana ila muda huu alijifuta machozi na kusema,
“Leo ndio mwisho wa kulia, sitalia tena. Kwasasa natakiwa kuinuka na kuonyesha kuwa naweza, mtoto wangu nitamlea mwenyewe”
Erica alilala kwa muda huo huku kichwa kikimuuma sana.