SEHEMU YA 220
Nyumbani kwakina Erica walianza kumsema Erica, haswa mama yake,
“Hivi Erica, angalia aibu uliyonitia mama yako jamani! Hivi ulishindwa kupanga na huyu muuza samaki wako, kwani hukuelewa kuwa ndugu zake wangefika wangeshtushwa na mtoto? Wangapi wanaolewa wakiwa na watoto tayari? Ni wengi tu lakini wanakuwa na makubaliano na wenza wao yani hilo linajulikana wazi, bora hata mtoto angekuwa wa Kiswahili, tatizo mtoto ni wa kiarabu Erica yani hapo ndio kuna shida mwanangu dah hata sijui inakuwaje”
Erica aliinuka na kwenda chumbani kwake maana yeye alipata aibu kushinda ile aliyoipata Tony kwa kumleta Dora.
Alifika chumbani na kumuweka mwanae pembeni ila machozi yalimtoka, kitendo hiko kilionekana kinamuumiza pia mtoto wake kiasi kwamba hata mtoto wake alianza kulia, ikabidi Erica anyamaze na kuanza kumbembeleza mtoto.
Alitulia kimya sasa ila baada ya muda kidogo dada zake yani Bite na Mage walienda chumbani kwa Erica kuzungumza nae,
“Erica, usisononeke kwa hili lililotokea ila sisi tunaelewa mdogo wetu ulikuwa tu ukitaka kutuliza haja ya moyo wa mama ila ukweli upo wazi kuwa Yule mwanaume si muhusika wa huyu mtoto, si ndio?”
“Ndio”
“Basi kama ni hivyo, inamaana yote haya uliyategemea mdogo wetu. Sidhani kama ni jambo jema kwako kuendelea kuwa na mawazo”
“Sawa dada zangu nimewaelewa”
“Ila hebu leo tuongee kirafiki, baba wa Angel yuko wapi? Na huwa anasema nini kuhusu swala la ndoa wewe na yeye? Na huwa anasemaje kuhusu kumuona mtoto? Kuwa muwazi mdogo wetu”
“Dada zangu ngojeni tu niongee, baba wa mwanangu nadhani nilifanya makosa sana kumuamini mwanaume kiasi hiki ila kiukweli kanitamkia wazi kuwa hana mpango wa kunioa mpaka nibadili dini”
Erica akainama na kulia, ila dada zake wakamtuliza,
“Eeeh swala la kutokukuoa bado sio tatizo, unaweza kuolewa na mtu mwingine. Vipi kuhusu kumuona mtoto?”
“Yani siku zote huwa ananiambia nitakuja na hataki kusema atakuja lini?”
“Na vipi kuhusu kumuhudumia mtoto?”
“Huwa anamuhudumia”
“Basi sio tatizo”
“Ni tatizo dada, yani kiukweli Rahim kabadilika sana siku hizi. Zamani kabla sijawa na mtoto alikuwa akinitumia hela nyingi sana, hata wakati naenda kujifungua alinitumia hela nyingi ila siku hizi kabadilika kwanza shida ya hela hadi nimwambie halafu hanitumii kwa kiwango kile alichokuwa ananitumia mwanzoni. Yani siku hizi naweza nisimpate hewani hata mwezi na nusu halafu akiibuka nikimwambia nashida na hela basi anatuma laki mbili, na hapo nikimtumia ujumbe mwingine wa kumuomba hela hajibu ujumbe wangu. Ndiomana namuuliza mara kwa mara atanioa lini? Pengine nikiishi nae atamuhudumia vizuri mtoto wake”
“Mmmh ila Erica, hebu tuambie ukweli unajua wewe hata mtu akikusikiliza kuhusu swala la mwanaume kutokukutumia pesa hatokuamini kabisa, kwanza toka mtoto kazaliwa huyu hujawahi kupanda nae daladala, unaendaga kliniki ya mbali kabisa na unaenda na tax na kurudi na tax. Hufanyi kazi wala biashara Erica, nina uhakika hata mama hajawahi kukupa hela ya tax ila ni hela zako. Kama huyo mwanaume kabadilika siku hizi basi mwanzoni alikuwa anakutumia hela nyingi sana si ndio? (Erica akatingisha kichwa kumuitikia dada yake) Haya sasa, alikuwa akikutumia kama kiasi gani?”
“Mara nyingine milioni moja, mbili au tatu na akituma laki tano basi ndio ametuma hela ndogo”
“Mmmh kwa aina hiyo ya mwanaume mdogo wetu ulikuwa na haki ya kubabaika ila ungetushirikisha dada zako na tungekufundisha mbinu za kula na kipofu, haya sasa hizo hela nyingi umefanyia nini?”
“Nifanyie nini dada? Nilikuwa natumia tu”
“Unatumia milioni tatu, sijui mbili kwa matumizi gani hayo? Erica mdogo wangu hata hukuwaza kuanzisha biashara!”
“Dada, kipindi kile nilikuwa nasoma wala wazo la biashara sikuwa nalo. Kwanza nilijua nikimaliza chuo basi nitaanza kazi, kwahiyo sikuwa na wazo la biashara kabisa kichwani”
“Sasa hizo hela ziko wapi? Inamaana zote umekula?”
“Dada, hela niliweka benki ila kwa matumizi yangu na mtoto zimebaki kidogo sana na nikimwambia yeye ananitumia hela za mawazo hadi kichwa change kimevurugika na sijui cha kufanya”
“Watu huwa wanafurahia mapenzi kabla ya ndoa na kabla ya kuzaa, ungetuuliza kwanza dada zako. Yani kabla hujachukua uamuzi wa kubeba mimba, ungetuuliza kwanza, huyo kaka inaonyesha ana hela, mwanaume afikie hatua ya kukutumia milioni tatu ya matumizi tu! Huyo ni tajiri, sasa mdogo wangu ungeuliza ila cha ajabu hizo hela hata dada zako hatujawahi kuziona. Kumbe ndiomana ulikuwa huoni shida kukodi gari kutoka nyumbani hadi chuoni, kumbe ulikuwa na hela!”
“Nisameheni dada zangu, ila mnanishauri nifanyeje kwasasa?”
“Cha kukushauri maana ulishakosea tena ulikosea kabisa ila unatakiwa tu kuwa mpole, yani huyo mwanaume wasiliana nae kwa upole kabisa, ila kwavile kasema hatokuoa hadi ubadili dini ujue hapo ndoa hakuna”
Bite akatoa ushauri mwingine,
“Sasa dada, mdogo wetu akitaka apate tena hela za Yule mwanaume ajifanye anakubali kubadili dini ndio atamchota vizuri”
“Bite mdogo wangu, unafikiri kuna muowaji kweli hapo? Yani kuhusu dini ni kisingizio tu, yani hapo hamna cha ndoa wala nini ila Erica shukuru Mungu umeshaujua ukweli halafu usonge mbele. Saivi angalia jinsi ya kutunza mtoto wako tu, usihofu kuhusu mume utapata tu”
Erica alianza kuwaelewa dada zake na kuishiwa maumivu kidogo yale aliyokuwa anayawaza moyoni.
ITAENDELEA