SEHEMU YA 179
Akachukua simu yake na kumpigia Rahim ila iliita sana tu kama jana yake na bila ya kupokelewa ila akakumbuka kuwa Rahim aliwahi kumwambia kuwa yupo hotelini kwa mwezi mzima, ikabidi aende pale hotelini.
Alifika chumba alichomkodiaga Rahim na kugonga ila alifunguliwa na mwanamke, akawa anamshangaa Yule mdada gafla akamuona Rahim akiwa amejifunga taulo yani ametoka kuoga.
Akili ilimruka kabisa Erica na kushindwa hata cha kufanya kwa muda huo huku akitamani hata kukimbia, wakati amegeuka nyuma ili aondoke, alishikwa mkono na Rahim na kuingizwa chumbani, kisha Yule mdada aliyekuwa mule chumbani kwa Rahim alitoka.
Erica alikuwa akilia sana, yani alilia hadi alihisi kuchanganyikiwa ila Rahim alimkalisha chini, kisha kumuacha akilia halafu yeye akivaa nguo. Alipomaliza alimsogelea na kumuangalia tu akilia hadi Erica aliona ni ujinga wa kuendelea kulia, akanyamaza na kumuangalia Rahim kwa hasira sana, ila kabla hajaongea chochote Rahim alimuuliza,
“Sasa kinachokuliza ni nini?”
Erica alimuangalia Rahim na kuongea kwa gadhabu sana,
“Yani bila hata aibu unaniuliza kinachoniliza ni nini!”
“Aibu gani sasa?”
“Hivi Rahim wewe ni mtu wa aina gani? Yani mimi nikutafutie hoteli halafu wewe ulale na wanawake wengine?”
“Kwahiyo hiyo hoteli uliyonitafutia unalipa wewe au nalipa mimi?”
Erica alizidi kupata hasira na kumwambia,
“Hata kama unalipa wewe ndio unifanyie mambo ya ajabu kweli? Ni haki hiyo?”
“Mambo ya ajabu yapi?”
“Hivi unaona ulichofanya ni sawa? Kulala na mwanamke mwingine unaona ni sawa?”
“Erica hebu acha masikhara, wewe ulichoka na nilikwambia kuwa nilirudi kwaajili yako ila ulidai umechoka kwahiyo ulitaka nifanyeje?”
“Yani Rahim ndio unaniambia hivyo kweli? Asante sana”
Erica akainuka, ila Rahim alimshika tena mkono na kumkalisha chini kisha akamwambia,
“Hebu acha mawazo ya kijinga, nilikuwa napima uelewa wako na wivu kama unao. Hivi kweli Yule anagekuwa mwanamke wangu angeondoka? Si angeanza kugombana na wewe? Halafu nianze tu kutafuta wanawake na kulala nao kwenye chumba kile kile ulichonikodia? Si nitakuwa sina akili, kwani hoteli hapa mjini zimeisha Erica? Kama ningekuwa na tabia hiyo basi hata hii hoteli nisingekaa sana, lazima ningetafuta hoteli nyingine ya kwenda kuwa na wanawake wengine”
“Kwahiyo Yule mwanamke ni nani?”
“Hilo ndio swali ulilotakiwa kuniuliza toka mwanzo sio kuanza kujiliza, Yule mwanamke nilimpa nguo zangu akanifulie na aliniletea leo, sasa nikamwambia aniwekee kitandani sababu naoga, nashangaa ndio wakati anatoka sijui wewe ndio umegonga na muda huo nimetoka bafuni. Yani una mawazo ya kijinga Erica jamani! Huamini mama, amini nakupenda sana”
Erica sasa akatabasamu kwani hakuamini kama Rahim angeongea nae kwa uzuri kiasi kile, kisha akamuangalia na kumuuliza,
“Kwahiyo Rahim wewe sio muhuni?”
“Hivi Erica, ningekuwa muhuni ningehangaika nini kukutafuta wewe? Kwanza nani aliyekwambia kama mimi ni muhuni? Sina hizo tabia mimi, nadhani hata mama yangu ashakwambia mengi sana kuhusu mimi, sinaga mambo ya wanawake kabisa. Niambie kipenzi changu maana naona umekuja kunishtukiza leo”
Erica akafungua pochi yake na kutoa yale majibu kuwa yeye ni mjamzito, kwakweli Rahim alonyesha kufurahi sana,
“Wow Erica jamani, umeamua kunibebea mimba! Nimefurahi sana Erica, na mimi nitaitwa baba sasa”
“Ndio, na mimi nitaitwa mama”
“Sawa, nakuomba Erica usitoe mimba yangu. Mwanangu nitamlea”
“Siwezi kutoa, ila uje nyumbani basi ujitambulishe na tufanye maswala ya harusi”
“Sawa, usijali kuhusu hilo, ila kwasasa nataka tena kusafiri. Yani nilitaka nikupigie simu leo kuwa kesho narudi Marekani. Nitakuja safari nyingine na kuja kwenu kujitambulisha na kukamilisha kila kitu”
“Jamani Rahim, sasa itakuwaje? Mama akijua?”
“Usijali, mwambie mama, mume yupo yani sitakawia kurudi Erica si unajua hata kwetu sijafika”
“Sawa Rahim, ila mimba haina siri mama akijua litakuwa balaa, unadhani mama yangu ataelewa nikimwambia kuwa mume yupo? Hatonielewa kwakweli”
“Usijali Erica, baada ya miezi miwili tu narudi. Nitakuja kwenu kukamilisha kila kitu”
Erica hakuwa na namna zaidi ya kumkubalia Rahim tu kuwa kesho yake anasafiri na ataenda kujitambulisha kwao akirudi baada ya miezi miwili ila alijipa moyo kuwa tumbo litakuwa bado kujitokeza. Kisha Rahim akamwambia tena Erica,
“Nakuomba leo tulale wote mpenzi wangu ili kesho unisindikize”
“Mmmh jamani hata nyumbani sijaaga?”
“Kwani na wewe huna njia ya kuaga nyumbani kwenu jamani Erica, nahitaji kumuaga mwanangu, si unajua nasafiri naenda mbali. Naomba tulale wote jamani Erica”
Ilibidi Erica akubali na atafute namna ya kumwambia mamake kwenye simu ili asiwe na wasiwasi.
Kesho yake Erica aliamka na Rahim kwenye ile hoteli kisha kujiandaa kwaajili ya kwenda uwanja wa ndege maana Rahim alisema ndio safari yake imewadia, kisha Rahim alimpa hela Erica na kumwambia,
“Chukua hii milioni moja ikusaidie saidie maana mimba zina mambo mengi sana, unaweza kutamani hiki mara hiki, hii pesa itakusaidia”
“Asante sana Rahim”
Kisha Erica alichukua ile pesa na kuiweka kwenye pochi yake, kisha Rahim alimwambia,
“Erica napenda kukwambia tena uwe mbali na mama yangu, sio saivi una mimba ndio unaenda kumtafuta mama yangu sijui uwe nae karibu. Tafadhali kuwa mbali na mama yangu, atakupa mawazo mama Yule. Mimba hazitaki mawazo Erica, mimba inataka pumziko la moyo. Kuwa mbali na mama yangu, sitaki ndugu yangu yeyote awe karibu na wewe”
“Nimekuelewa Rahim ila kumbuka siku ile ulitaka kunitambulisha kwa ndugu yako”
“Yani Yule nilikutana nae kwa bahati mbaya, akaniuliza kuwa mbona sijasema ujio wangu ndio nikamwambia yupo na shemeji yake yani nikamgelesha tu ngoja nimtambulishe ila siku ile nilishukuru kweli alivyoitwa maana hata mimi nilitaka kumfanyia mchezo pale wa bila kumtambulisha. Ndugu zangu ni wambea wambea sana, ndiomana sipendi kuwa nao karibu. Ila nakusisitiza tena kuwa mbali na mama yangu”
“Nimekuelewa Rahim”
Kisha wakaondoka na kwenda uwanja wa ndege ambapo Erica alimuacha Rahim kaingia uwanjani kisha yeye akarudi nyumbani kwao.
Erica aliingia kwao ila kwa muda huo mama yake hakuwepo kwahiyo alienda kuoga na kulala, alikuwa akishangaa tu mimba ya kipindi hicho imeanza bila makeke ya kutapika au kujihisi kichefuchefu.