SEHEMU YA 16
Jumatatu kama kawaida Erica alijiandaa na kwenda shuleni, ila nay eye hakuwa na furaha kabisa siku hiyo kutokana na vile alivyosemewa na Johari na jinsi alivyosemewa na mama yake kwa mchungaji wao.
Akiwa amekaa darasani mara alikuja kuitwa na mwalimu, na kuongozana nae kuelekea ofisini. Alipoingia tu moyo wake ulishtuka sana kwani alimkuta mama yake na mwalimu wa nidhamu. Kwakweli raha ilizidi kumuisha kabisa kwani hakujua kuwa mama yake ameenda kufanya nini,
“Haya sogea huku Erica”
Erica alisogea kwa mwalimu na kuanza kumsikiliza,
“Ni kijana gani aliyekutongoza?”
Erica alikaa kimya kwani aliogopa kusema kwa kuhofia ni aibu kwa Erick, ila mama yake alimuangalia kwa gadhabu sana, na kumsogelea mwenyewe halafu akamnasa tena kofi,
“Hebu mtaje huyo mwendawazimu mwenzako”
Mwalimu nae akashika bakora kuwa asipotaja atamuadhibu, mwalimu akataka kumchapa bakora. Erica aliamua kusema,
“Lakini hakuna mtu aliyenitongoza”
Mama yake akawaka kwa hasira,
“Kwahiyo mimi ni chizi? Nimekuja kuleta habari za uongo, hebu muiteni rafiki yake Johari aje kuthibitisha ujinga wa huyu”
Mwalimu alimuangalia Erica na kumuamuru apige magoti, kisha mwalimu mwingine alienda kumuita Johari.
Alipofika aliulizwa kuhusu mwanaume aliyemtongoza Erica,
“Ni Erick mwalimu, ila msinitaje”
“Hebu toa ujinga wako hapa, na umuite huyo Erick upesi”
Basi Johari akatoka na kwenda kumuita Erick ambaye alishangaa kufika ofisini na kukuta kuna mmama amekaa huku walimu wawili wakiwa wamesimama na viboko vyao halafu Erica kapigishwa magoti.
Alipofika nae aliamriwa kupigwa magoti na kuulizwa kama ni kweli amemtongoza Erica,
“Ni kweli mwalimu ila sijamwambia kwa lengo baya ni kweli nampenda”
“Nyamaza upesi, unajua kupenda wewe? Ndio nyie mnaoanzaga kuharibu maisha ya wenzenu bado mapema kabisa, unakubali kirahisi rahisi tu.”
Wale walimu walimuomba mama Erica aondoke maana walisema watamshughulikia huyo Erick, kisha wakamwambia Erica ainuke na kwenda darasani.
Kiukweli Erica alishikwa na moyo wa huruma sana, kwani walimu wale walianza kumuadhibu Erick kwa viboko pale pale, basi Erica akasema
“Mwalimu lakini Erick hajanitongoza”
“Nyamaza upesi na wewe, unataka adhabu tukupe wewe eeh! Haya Erick tongoza tongoza nenda darasani, adhabu yako apate huyu kipenda roho”
Erick aligoma na kuwaambia walimu,
“Mimi ndio naye stahili kuadhibiwa kwani ni kweli nilimwambia Erica kuwa nampenda, ingawa sikuwa na nia mbaya. Na ninampenda kweli”
“Nyamaza wewe kijana, Erica toka upesi nenda darasani. Na siku nyingine mtu akikutongoza shuleni uje useme kwa walimu na sio kwenda kusema nyumbani. Mnawapanikisha sana wazazi”
Erica alitoka mule ofisini ila alijawa na roho ya huruma sana, alirudi darasani ila roho ilikuwa inamuuma mno.