Simulizi: Nafsi Iliyoonja Mauti

Chilojnr

JF-Expert Member
Jul 5, 2012
302
1,306
Mawasiliano namba: 0718069269

Sehemu ya 01

Watu walishika vichwa vyao, vinywa wazi kuonyesha mshtuko walioupata, kila mmoja alikuwa haamini alichokuwa akikiona mbele ya macho yake. Ajali mbaya ya gari ilitokea Mwenge katika makutano ya Barabara ya Ally Hassan Mwinyi na Sam Nujoma.

Gari ndogo aina ya Subaru iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyekuwa na asili ya Kiarabu ilirushwa juu, zilisikika sauti za watu wawili wakilia ndani ya gari hilo lililokuwa limeendeshwa kwa kasi ambalo liligongana uso kwa uso na lori la mchanga.

Ilikuwa ni ajali mbaya hata kwa kuiangalia kwa macho tu, gari hilo ambalo ilionyesha uzembe mkubwa wa dereva ama kugoma kwa breki lilipokuwa juu sauti za watu hao zilikuwa zikisikika lakini baada ya kutua chini, hapakuwa na sauti yoyote ile.

Watu waliogopa, wanawake wasiokuwa na mioyo migumu wakafumba macho yao na wengine kuondoka mahali hapo. Waliogopa, picha iliyokuwa imeonekana mbele yao ilitisha na kusisimua mno.

Wanaume kadhaa wakaanza kukimbia kulifuata gari lile ambalo baada ya kutua chini, lilibingirika kwa umbali fulani na kukaa mataili yakiwa juu. Walipofika hapo, kitu cha kwanza kukiona kilikuwa ni damu zilizokuwa zikitiririka barabarani katika vipande vya vioo vilivyokuwa vimevunjika.

“Jamani kuna mtu amepona humu?” lilikuwa swali la kwanza aliloliuliza jamaa ambaye alifika hapo huku akionekana kuwa na hofu kama wenzake.

Hapakuwa na mtu aliyemjibu, lilikuwa swali ambalo hakutakiwa kujibiwa kwa haraka mpaka pale ambapo watu wangewaona watu waliopata ajali hiyo ambao bado walikuwa ndani ya gari hiyo.

Watu wakavunja vioo vya dirishani na kuchungulia ndani. Waliwaona watu wawili, mmoja alikuwa mwanaume wa Kiarabu aliyenyoa kwa mbwembwe kabisa, alikuwa kimya, mdomo wake, pua vilipasuka kwa kiasi kikubwa, ni kama taya lilianza kuachia huku kichwani mwake akiwa amechomwa na kioo ambacho kiliingia ndani kabisa. Alikuwa amefariki dunia hapohapo.

Upande wake mwingine kulikuwa na msichana aliyekuwa kimya kabisa. Huyu hakuwa na majeraha makubwa zaidi ya damu ambayo ilikuwa ikimtoka puani tu, aliyafumba macho yake kama mtu ambaye alikuwa amekwishakata roho ndani ya gari hilo.

“Mungu wangu!” alisema jamaa mmoja alipomwangalia msichana huyo.
Haraka sana watu hawakutaka kupoteza muda, wakaanza kuwatoa watu hao ndani ya gari hilo. Maiti ya mwanaume huyo ikatolewa na kuwekwa barabarani na kisha msichana huyo kufuata.

Watu walijazana mahali hapo, walihitaji kushuhudia hao waliopata ajali kwenye gari hilo, walihitaji kujua walikuwa kwenye hali gani kwani kwa jinsi ajali ilivyotokea, kila mmoja alikuwa na uhakika hapakuwa na mtu aliyenusurika.

“Wazima hao?” aliuliza mwanaume mwingine huku akiwaangalia watu hao.
“Mwanaume amekufa ila sijajua kuhusu huyu msichana! Mh! Lakini mzuri kishenzi!” alijibu jamaa mwingine.

Alichokisema kilikuwa kweli kabisa. Msichana aliyekuwa akionekana mbele yao alikuwa mrembo mno, alivutia, alichanganyikana rangi, inawezekana kabisa mmoja kati ya wazazi wake alikuwa Mwarabu na mwingine Mswahili kama wengine.

Moja ya magari yaliyokuwa yakipita mahali hapo likasimishwa, haraka sana watu hao wakaingizwa humo na safari ya kuelekea katika Hospitali ya Lugalo kuanza mara moja.

Ndani ya gari hilo mbali na watu waliopata ajali na dereva kulikuwa na wanaume watatu ambao walikuwa wakiizungumzia ajali hiyo lakini kubwa zaidi walikuwa wakimzungumzia msichana yule ambaye sura yake ‘iliita’, alikuwa na umbo matata huku kifua chake kikiwa cha saa sita kabisa.

“Mh!” jamaa mmoja, wenzake walijua kwa nini aliguna, wote wakatabasamu, walitamani kucheka lakini hawakufanya hivyo kutokana na kile kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.

Baada ya dakika kadhaa wakafika katika hospitali hiyo, machela ikaletwa, watu hao wakateremshwa na kuingizwa ndani. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwapima, mwanaume wa Kiarabu ambaye ndiye alikuwa dereva ilithibitishwa kufariki lakini msichana aliyekuwa pembeni yake alikuwa mzima japokuwa mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa mbali sana.

Akapelekwa katika chumba cha upasuaji ambacho kwa nje juu ya mlango kiliandikwa Theatre na kuanza kupata matibabu, madaktari walikuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha msichana huyo anapata nafuu, muonekano wake ulionekana kuwaridhisha kidogo kwa sababu hakuwa na majeraha makubwa ila wasiwasi wao mkubwa ulikuwa ndani ya mwili wake.

“Miguu yake?” aliuliza daktari mmoja, haraka sana akashikwa miguu.
“Ipo safi!” alijibu daktari mwingine.
“Na mikono?”
Ilikuwa ni kazi ya kumwangalia kwa kumgusa kabla ya kumuingiza kwenye mashine ya MRI (Magnetic Resonance Imaging) na kuangalia sehemu zingine za mwili.

Kwa kila sehemu ambayo walimgusa alionekana kuwa safi, yaani hakuwa na mvunjiko wowote ule kitu kilichomfanya kila mmoja kuona alikuwa na bahati sana.

Walimtibu kwa saa moja katika sehemu ambazo walikuwa na hofu nazo na baada ya hapo walihitaji kujua zaidi kuhusu ndani ya mwili wake kama alikuwa na tatizo lolote lile.

Akachukuliwa, mlango ukafunguliwa na kupelekwa katika chumba kingine kilichokuwa na mashine ya MRI kwa lengo la kumwangalia kwa ndani zaidi ili wajue ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mwilini mwake. Akaingizwa kwenye mashine hiyo na kupigwa picha.
Kilichotoka, madaktari wote hawakuamini macho yao, msichana huyo mrembo alivunjika mgongo wake mara mbili, yaani pingili za uti wa mgongo zilivunjika juu na chini.

“Ni hatari!” alisema daktari mmoja kwa sauti ndogo.

Wanaume wale waliokuwa wamempeleka hospitalini pale walikuwa nje ya chumba kile wakisubiri, waliambiwa na madaktari kwamba hawakutakiwa kuondoka mpaka pale ambapo wangepewa majibu ya kile kilichokuwa kikiendelea, hivyo wakasubiri.

Mikononi mwao walikuwa na simu za watu hao, walitaka kuwasiliana na ndugu zao lakini kwanza wakasita, hawakutaka kufanya haraka mpaka pale ambapo wangepewa majibu ya kilichokuwa kikiendelea.

Baada ya saa moja na nusu daktari mmoja akawafuata watu hao na kuongea nao kirafiki, hakutaka kuwaficha, aliwaambia wazi kwamba yule mwanaume alifariki dunia hata kabla ya kupelekwa ndani ya hospitali ile kwa ajili ya matibabu.

“Hilo tulilijua! Na yule msichana?” aliuliza jamaa mmoja.
“Yupo mahututi! Hali yake ni mbaya sana!”
“Mbaya sana?”
“Ndiyo!”
Wakatamani kuwapigia simu watu wao wa karibu kwa lengo la kuwapa taarifa lakini simu zote zilifungwa, yaani ilikuwa ni lazima uingize namba ya siri na ndipo ufungue, hivyo wakashindwa kufanya hivyo.

Walichokifanya ni kumkabidhi daktari simu hizo na wao kuondoka mahali hapo kwani kama ni wema, waliufanya pasipo kuangalia ni nani.

Dokta alikaa na simu hizo kwa dakika kadhaa tu, marafiki na ndugu wa watu hao wakaanza kupiga simu ndipo dokta akapokea na kuwapa taarifa juu ya kilichotokea.

“Hospitali gani?” lilikuwa swali lililoulizwa na kila mtu aliyepiga simu.
“Lugalo!” alijibu daktari.

Je, nini kitaendelea?

Hii itakuwa inatoka kila Jumatano na Jumapili. Itakuwa inapishana na ile ya Ulimwengu Ndotoni Mwangu inayotoka kila Jumanne na Ijumaa.

Nafsii.jpg
 
Sehemu ya 02

Ni baada ya nusu saa ndugu za watu hao wakafika mahali hapo. Kila mmoja alionekana kuumizwa na kilichotokea, sura zao zilikuwa kwenye majonzi mazito, hiyo ajali waliyoambiwa na daktari waliisikia kabla lakini hawakujua kama walikuwa watu hao.
Wazazi wa dereva wakafika na kupewa taarifa ya kifo cha kijana wao, mwili wake ulikuwa mochwari, wakaenda huko na kuonyeshwa, walihuzunika kupita kawaida.
Wazazi wa msichana walipofika mahali hapo nao wakaambiwa kuhusu binti yao, alikuwa na bahati, ajali hiyo haikuyakatisha maisha yake, alinusurika kufa japokuwa naye alikuwa mbele ya gari hilo.
“Ahsante Mungu!” alisema baba yake na msichana huyo, akanyanyua mikono yake juu kama ishara ya kumshukuru Mungu.
“Ila kuna tatizo!” alisema daktari.
“Tatizo gani?” akaingilia mke wake.
Hakutaka kuwaambia hapo, alichokifanya ni kuwaambia wamfuate ofisini kwake. Alikuwa akitembea mbele na wao kuwa nyuma, sura zao tayari zilionyesha hofu kubwa, walichokifikiria ni binti yao kuvunjika miguu, mikono, kiuno ama shingo.
Walipofika humo, wakakaa kwenye viti na daktari kuanza kuwaambia kilichotokea. Jasho ziliwatoka, walikuwa na hofu ya kusikia kile walichotaka kuambiwa mahali hapo. Mapigo yao ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida.
Walitamani kumwambia daktari asiwaambie lakini hawakutaka kufanya hivyo, ilikuwa ni lazima wajue binti yao alikuwa na tatizo gani, kama hakufa, basi hata kama angekuwa mgonjwa kwa kiasi gani, mwisho wa siku angepona kabisa.
“Dokta tuambie kuna nini!” alisema baba wa msichana huyo, aliitwa mzee Jackson Chavala.
“Binti yenu amevunjika uti wa mgongo mara mbili!” aliwajibu huku akiwaangalia, hakuwaambia tu bali aliwapa na picha ya X ray iliyokuwa imepigwa.
Wakaichukua na kuanza kuiangalia, hawakuamini macho yao, macho yao yakaanza kukusanya machoni na hatimaye kuanza kutiririka mashavuni mwao. Waliumia, hawakuamini kama kweli kile walichoambiwa ndicho kilichotokea kwa binti yao wa pekee, waliyekuwa wakimpenda kupita kawaida.
“Binti yangu amevun....” alisema mama yake, aliitwa Bi. Najrat, mwanamke aliyekuwa na asili ya Kiarabu, kile alichokiona kiliufanya mwili wake kusisimka. Hata kabla hajamalizia sentensi yake akaanza kulia. Dokta na mumewe wakapata kazi ya kumbembeleza.
“Ndiyo! Naomba niwahakikishie atapona! Tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha anarejewa na hali yake kama kawaida,” alisema daktari, ilikuwa ni ngumu, aliligundua hilo lakini yeye kama daktari ilikuwa ni lazima awape moyo kwani watu hao walihitaji kusikia maneno ya faraja kutoka kwake na ndiyo maana aliwaambia hivyo.
Wazazi hao walisikitika na kulia. Kuvunjika kwa uti wa mgongo kulimaanisha binti yao angepooza, asingeweza kutembea wala kufanya kitu chochote kile, hicho ndicho kitu ambacho walikiogopa sana.
Kwa kuwa msichana huyo aliyeitwa kwa jina la Sylivia alihitaji matibabu makubwa zaidi ya wataalamu wakubwa, akahamishwa kutoka hapo Lugalo na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
Alipofikishwa huko, madaktari wakaweka kikao kwa lengo la kuanza kuijadili ripoti ambayo ilitoka huko Lugalo ili wajue ni mahali gani walitakiwa kuanzia na mgonjwa alikuwa na tatizo gani kubwa.
Kila daktari aliyeona ripoti ile alishtuka, hakukuwa na aliyeamini kama kungekuwa na mtu aliyepata majeraha makubwa ya uti wa mgongo kama ilivyokuwa kwa Sylivia.
Uti wa mgongo ulivunjika hali iliyoonyesha ni lazima apooze kitandani pale alipokuwa. Kila mmoja alimsikitikia lakini hawakuwa na jinsi kwani kama uti wa mgongo ulivunjika vibaya namna ile, wasingeweza kuurudisha katika hali yake kwa kipindi kifupi, ingeweza kuchukua hata miaka hamsini mpaka kuwa sawa.
Uti wake wa mgongo ukagawanywa kwa sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ya juu ilikuwa ikianzia C1 hadi C4, sehemu hii waliiweka alama ya bluu na iliitwa High-Cervical Nerves iliyokuwa na pingili nne.
Mgonjwa anapokuwa amevunjika katika sehemu hii ya kuanzia C1 hadi C4 inamaana mwili wake angepooza miguu, mikono, asingekuwa na uwezo wa kula au kuoga yeye mwenyewe na ilikuwa ni lazima atafutiwe mtu wa kumfanyia mambo hayo yote, asingekuwa na uwezo wa kuendesha gari, kwa kifupi alitakiwa kuwa chini ya uangalizi kwa saa ishirini na nne.
Mbali na hicho, pia kulikuwa na pingili nyingine walizoziwekea rangi ya kijani. Hizo ziliitwa Low-Cervical Nerves ambazo zilianzia C5 hadi C8.
Mgonjwa anapovunjika pingili hizo, kwake isingekuwa vigumu sana kufanya mambo mengine kwani angeweza kunyanyua mkono, kutembea na wakati mwingine hata kuzungumza kama kawaida lakini tatizo kubwa ambalo angekutana nalo ni kwenye mfumo wote wa upumuaji, asingeweza kupumua kwa kawaida, ilikuwa ni lazima kutumia mashine maalumu kupumua.
Kulikuwa na pingili nyingine walizozipa rangi nyekundu, hizi ziliitwa Thoracic Nerves walizozipa T1 hadi T5. Hizi nazo kama zingevunjika basi mgonjwa angepata matatizo katika kifua chake, miguu na mikono ingepooza ambapo kwa kitaalamu hujulikana kama Paraplegia.
Walipitia kila kitu kwa umakini mkubwa na tatizo kubwa lililotokea kwa Sylivia ni kwamba pingili zake mbili zilikuwa zimevunjika hali iliyoonyesha hatari kubwa katika maisha yake.
“Nimefanya kazi kwa miaka mingi lakini sijawahi kukutana na mgonjwa mweye tatizo kubwa kama hili! Mungu nisaidie na wenzangu tuweze kumrudisha kwenye hali ya kawaida, japo mfumo wake wa upumuaji urudi na kuwa sawa,” alijisemea daktari mmoja aliyeitwa Innocent Nambuo, alikata tamaa lakini bado alijipa moyo kwamba kila kitu kingekwenda salama kabisa.
***
“Unadhani nakudanganya Nandy! Sisi madaktari tuna kazi kubwa sana, sio kama nyie watu wa mahesabu,” alisikika kijana mmoja akimwambia rafiki wake wa kike aliyekuwa naye katika duka moja la simu za mkononi katika moja ya maduka ya Mlimani City.
“Sisi tuna kazi kubwa mno! Unajua hesabu ndiyo baba lenu! Yaani watu kama sisi tunaweza kuipeleka nchi tunavyotaka sie, nyie kazi zenu madaktari ni ndogo sana, mtu akiumwa maralia hata majani ya mti wa mwarobaini anakunywa, ugumu upo wapi sasa?” aliuliza Nandy huku akimwangalia mwanaume aliyezungumza hilo.
“Nandy bwana! Hivi unafikiri mchezo mchezo! Udaktari noma sana! Hivi wewe tangu umezaliwa si unajua kuhesabu pesa, sasa kuna ugumu gani hapo?” aliuliza jamaa huyo.
Walikuwa wakipiga stori huku wakitaniana. Watu hawa walikuwa marafiki wakubwa kutoka huko nyumbani kwao, Kinondoni walipokuwa wakiishi. Walikua na kusoma pamoja mpaka walipokutenganishwa baada ya kuingia chuo.
Msichana huyo alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea mambo ya biashara na kumaliza huku kijana huyo aliyeitwa kwa jina la Samuel ama Sam akijiunga na Chuo Kikuu cha Udaktari kiitwacho Muhimbili University Of Health and Allied Sciences (MUHAS) kilichokuwa jijini Dar es Salaam.
Alisoma chuoni hapo kwa miaka minne, hakuwa amemaliza, alitakiwa kusoma zaidi na zaidi ambapo hapo baadaye angekuwa na uwezo wa kuamua kama angekwenda nje ya nchi kumalizia mwaka mmoja ama kusoma hapahapa Tanzania.
Alipenda utabibu, katika maisha yake tangu alipokuwa kijana mdogo alipenda sana kujiita kwa jina la dokta. Wazazi wake ambao nao walikuwa na uwezo walimtengenezea mazingira mazuri, walimnunulia koti la kidaktari akiwa mdogo, mashine nyingine za kawaida na kila alipokuwa nyumbani, alivalishwa na kupewa vifaa hivyo.
Vilimchanganya, akajikuta akipenda zaidi kuwa daktari. Wazazi wake walimtia moyo kwa kumwambia hakuna kitu kigumu chini ya jua, kile ambacho unasema hiki ni kigumu, kuna mtu fulani aliwahi kukifanya hapo kabla.
Wakampa mfano wa madaktari, kulikuwa na madaktari wengi duniani, hao waliwezaje mpaka yeye ashindwe? Kama watu hao waliweza basi hata na yeye angeweza, alichotakiwa kufanya ni kusoma sana.
Na kweli akasoma, alisoma na kusoma huku akiwa na ndoto yake hiyo kichwani mwake, moyo wake ulijipa moyo kama alivyoambiwa na wazazi wake angekuwa daktari kama alivyopenda.
“I know I can...” (Najua ninaweza) alijisemea.

Je, nini kitaendelea?
SImulizi hii nayo inapatikana WhatsApp ikiwa kamili kwa namba 0718069269. Kwa walio chini kiuchumi, tuendelee kuifuatilia hapahapa mpaka mwisho.

Tuendelee kushare kwa lengo la kuitangaza page.
 
SEHEMU YA 03

Kwenye simu yake kulikuwa na nyimbo nyingi lakini wimbo ambao alikuwa akiupenda mno kuusikiliza ulikuwa ni wa Mwana HipHop Nas, I Can ambao kila alipokuwa akifanya hivyo, alisikia nguvu mpya ya kusonga mbele.
Masomo yalikuwa magumu, kuna wakati alionekana kukata tamaa lakini kila alipokumbuka kulikuwa na madaktari wakubwa duniani, aliamini nao walisoma masomo hayohayo aliyokuwa akiyasoma yeye kipindi hicho, hivyo alitakiwa kujua kila kitu kilikuwa kinawezekana kabisa.
Siku zikakatika huku ukaribu wake na msichana Nandy ukiwa mkubwa, alimchukulia kama rafiki yake lakini msichana huyo ilikuwa ni tofauti kabisa.
Alimpenda mno Sam, alitamani kumwambia jinsi moyo wake ulivyojisikia lakini aliogopa kufanya hivyo. Aliteseka moyoni mwake, alikuwa na msongo wa mawazo, penzi juu ya Sam lilimchanganya kupita kawaida.
Kila siku kazi yake ilikuwa ni kupanga, nitamwambia kesho, ikifika hamwambii, nitamwambia wiki ijayo lakini kila siku mambo yalikuwa yaleyale, hakutaka kumwambia ukweli.
Wanaume walikuwa wakimsumbua alipokuwa akifanya kazi lakini hakutaka kukubali, moyo wake ulimwambia Sam ndiye alikuwa mwanaume wake wa pekee, wa kufa na kuzikana lakini si hao wengine ambao walikuja na kuondoka.
Kila msichana ambaye alijisogeza karibu na Sam, aliweka vizingiti vyake, hakutaka aguswe na msichana yeyote yule mpaka siku ambayo angemwambia ukweli jinsi alivyompenda, ambavyo hakuwa akilala kwa ajili yake.
“Ila nitamwambia tu! Halafu kwa nini namuogopa sana?” alijiuliza.
Hilo swali lilikuwa ni mara ya elfu moja kujiuliza lakini mara zote hizo hakuwa na majibu kabisa. Alizungumza na Sam, alikuwa na uhuru naye lakini maneno ya mapenzi tu ndiyo aliyokuwa akiogopa kumwambia.
Ilimuumiza mno lakini hakuwa na jinsi, wakati mwingine alijidanganya muda bado, alipanga kumwambia mwanaume huyo pindi atakapomaliza kusoma na kupata kazi, alitamani siku hiyo ifike lakini aliona siku zikienda tararibu sana.
“Na ikitokea nikamwambia, hivi hawezi kuniambia mimi ni dada yake? Mh! Halafu ikitokea akampata mwanamke mwingine nitafanya nini? Hapana! Kwa jinsi ninavyombana na kuweka vizingiti, hakuna mwanamke atakayetokea na kuwa naye zaidi yangu,” alijisemea.
Siku ambayo Sylivia alifikishwa hospitalini hapo Sam alikuwa mahali hapo akifanya field yake ya mambo ya mifupa aliyokuwa akisomea. Aliposikia king’ora cha gari la wagonjwa, haraka sana akatoka ndani na kuelekea huko, alihitaji kuona ni mgonjwa wa aina gani alikuwa akiteremshwa.
Baada ya dakika kadhaa, gari likasimama na mlango kufunguliwa, machela ikateremshwa na kuanza kusukumwa. Mgonjwa aliyekuwa juu ya kitanda hicho hakuwa akimfahamu, na mbaya zaidi hakumuona vizuri mahali hapo kutokana na damu zilizokuwa zimemtoka, alibahatika kuona nywele tu, machela ikasukubwa na kuondoka mahali hapo.
“Huyo mgonjwa anasumbuliwa na nini?” alimuuliza daktari mmoja aliyeonekana kuwa na haraka mno.
“Amepata ajali mbaya ya gari!” alijibiwa.
Akawa na hamu ya kusikia zaidi, kama alipata ajali inamaana na yeye angekuwa ndani ya chumba cha upasuaji na kuangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, alitakiwa kujifunza zaidi na zaidi.
Akawa na hamu ya kuingia humo, aliwahi kufanya hivyo kipindi kilichopita na muda huo alikuwa na hamu ya kufanya hivyo kwa mara nyingine.
Baada ya madaktari kumaliza kuijadili ripoti ya Sylivia, haraka sana baadhi yao wakaenda ndani ya chumba kile kwa lengo la kuanza kazi mara moja.
“Leo hamtoweza kuingia wote, huyu mgonjwa hali yake si nzuri kabisa, ningependa waingie vijana watatu tu,” alisema daktari huku akiwaangalia wanafunzi kumi na mbili ambao wote hao walitaka kuingia na kujifunza kila kitu kilichokuwa kikiendelea humo.
Haraka sana Sam akapiga hatua na kusimama mbele kabisa, alikuwa na hamu ya kuingia humo, hao watu waliokuwa wamepata ajali kubwa ndiyo ambao alitaka zaidi kuwaona, hivyo walipofika watatu, wakachukuliwa na kuingizwa humo.
Kabla ya kuanza kumfanyia upasuaji, madaktari wakashikana mikono na kuanza kusali kila mmoja na dini yake. Walipenda kufanya hivyo kwa kuwa hawakutaka kuamini wao ndiyo waliokuwa wakileta uponyaji, mponyaji alikuwa mmoja tu, Mungu muumba mbingu na nchi, wao walikuwa wakitumiwa tu.
“Amen!” kila mmoja aliitikia kwa nafasi yake baada ya kumaliza.
Upasuaji ukaanza kufanyika, kila mtu alikuwa makini kabisa. Sylivia alikuwa kimya kitandani pale, Sam alikuwa akiangalia kwa makini kabisa, alifuatilia kila hatua iliyokuwa ikiendelea.
Kazi zao nyingine zilikuwa ni kuagizwa vifaa, kama kulikuwa na kifaa fulani kilihitajika, waliambiwa wao, walikuwa wakifundishwa mambo mengi yaliyokuwa yakiendelea humo.
Upasuaji ulichukua saa kumi na mbili, walipomaliza, wakamuacha apumzike huku kila mmoja akiwa hoi kabisa, wakatoka na kuhitaji msichana huyo apelekwe katika chumba cha wagonjwa mahututi ambacho kwa nje kiliandikwa ICU.
Sam na wenzake wakaanza kusukuma machela ile kuelekea katika chumba hicho. Alimwangalia msichana huyo, hakuwa akimuona vizuri, uzuri wake ni kama ulijificha hivi, puani alikuwa na mashine ya oksijeni iliyomsaidia kupumua na pia kulikuwa na dripu iliyokuwa ikining’inia ambayo iliendelea kumuingizia maji mwilini mwake.
Wakamfikisha ndani ya chumba hicho na kumuacha, wakatoka na kuendelea na mambo yao. Kwa picha aliyokuwa ameiona ndani ya chumba kile, moyo wa ushujaa ambao ulimuingia akaamini angekuja kuwa dokta mkubwa mno, atakayeaminika kuliko madaktari wengine wote nchini Tanzania.
Alikaa huko kwa saa nyingine chake kisha kurudi nyumbani kwao. Njiani kichwa chake kilikuwa na mawazo juu ya yule mgonjwa, hakujua ni kwa sababu gani lakini kila alipofanya hili na lile, picha ya mgonjwa yule ilimjia kichwani mwake.
Hakuwa vizuri na hata alipokutana na Nandy msichana huyo aligundua hakuwa kama alivyokuwa siku nyingine, siku hiyo alionekana kuwa tofauti sana.
“Kuna nini?” aliuliza msichana huyo.
“Hakuna kitu! Kuchoka tu!” alijibu.
“Kweli?”
“Kabisa!”
“Au kuna mwanamke ameanza kukuchanganya?” aliuliza Nandy, hakutaka kusikia jibu la ‘ndiyo’ kutoka kwa Sam lakini akajikuta tu ameuliza japokuwa alihisi kama jibu lake lingekuwa hivyo lingemuumiza mno.
“Hapana! Siwezi kupelekeshwa na mapenzi! Madaktari tunapelekeshwa na vitu vingine vikubwa vikubwa lakini si mapenzi,” alijibu huku akiachia tabasamu, moyo wa Nandy ukajisikia furaha mno.
Usiku hakulala vizuri, alikuwa akimfikiria mgonjwa yule, akawa na hamu ya kesho ifike ili arudi tena hospitalini na kumjulia hali. Siku hiyo alichelewa kulala kwa ajili ya mawazo, alilala majira ya saa saba usiku.
Asubuhi ilipofika, akaamka, akajiandaa na kuelekea chuoni. Bado kichwa chake kilikuwa kwa msichana huyo, hakujua kulikuwa na nini kilichokuwa kikiendelea lakini akajikuta akiwa na hamu ya kumuona na kuona alikuwa akiendeleaje.
Alikwenda chuo, akasoma na alipomaliza, akaelekea hospitalini ambapo alipofika nje tu, macho yake yakatua kwa wazazi wa msichana yule mgonjwa ambao walionekana kuwa na majonzi tele, akawasogelea na kuanza kuwafariji kwa kuwapa pole kwa hali ngumu aliyokuwa akipitia binti yao kitandani.
“Poleni sana...” alisema Sam kwa sauti ndogo huku akiwaangalia.
“Tumekwishapoa...hali yake inaendeleaje?” aliuliza baba yake kwa sauti ya chini pia.
“Inaendelea vizuri japokuwa daktari anayemshughulikia atawapa majibu zaidi. Ninaingia kwa ajili ya kumjulia hali, ila mategemeo ya kuwa mzima yanaonekana, cha msingi endeleeni kumuomba Mungu,” alisema maneno hayo huku akionekana kuumia moyoni mwake.
Baada ya kuongea nao kwa sekunde kadhaa, akaingia ndani ya chumba kile. Hapakuwa na mtu aliyekuwa akiruhusiwa lakini kwa kuwa naye alionekana kama daktari, akaingia ndani.
Akakifuata kitanda alicholazwa Sylvia na kusimama pembeni. Akaanza kumwangalia, alitaka kuona ni kwa sababu gani msichana huyo siku hizo mbili alimpa sana mawazo.
Hapo ndipo akagundua kitu kingine, msichana aliyelala mbele yake hakuwa wa kawaida, alikuwa na uzuri wa kipekee mno, sura nzuri, nyembamba, pua kama ya Kisomali na lipsi nene kidogo.
“Ni binti mzuri mno!” alijisemea huku akianza kutoa tabasamu, Sylivia alikuwa kimya kitandani pale, yaani hakutingishika wala kuyafumbua macho yake. Ni kama angekuwa kimya milele.

Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 04.

Ndugu, jamaa na marafiki wa Sylivia walifika hospitalini hapo kwa lengo la kumuona msichana huyo aliyekuwa akiendelea kuteseka kitandani.
Hawakuruhusiwa, kwa kipindi hicho haikuwa sahihi kwa mtu yeyote yule kuingia humo na kumuona. Alikuwa kwenye hali mbaya, hakuwa amerudiwa na fahamu na hakujua chochote kile kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
Kila mmoja alikuwa na huzuni, waliwapa pole wazazi wao waliokuwa wakilia kila wakati. Walijiona kupitia kwenye maisha ya uchungu, yaliyokuwa na maumivu kupita kawaida.
Mzee Chavala alikuwa tajiri mkubwa, alikuwa na biashara nyingi Tanzania, kwa kipindi hicho aliacha kila kitu na kuanza kufuatilia hali ya mtoto wake wa kwanza, Sylivia aliyekuwa akimpenda mno.
Madaktari walikuwa wakiingia na kutoka ndani ya chumba kile, kila aliyetoka humo aliwaambia walitakiwa kusubiri kwani bado msichana huyo alikuwa akipambania uhai katika kitanda ndani ya chumba kile.
Maneno hayo yaliwachoma, hawakuona kama binti yao angepona na kuwa kama alivyokuwa zamani. Walitamani kufanya zaidi ya hayo, kama inawezekana wamuhamishe hospitali, wampeleke hata India ambapo huko angepatiwa matibabu zaidi.
Hilo lilishindikana kwanza, kwa kawaida hata kama mgonjwa alikuwa na hali mbaya, hospitali kama Muhimbili haikutakiwa kumuhamisha ghafla na kumpeleka huko hata kabla ya kuandika ripoti kuhusu ugonjwa wake, walitakiwa kufanya hivyo ili baada ya kufika huko India, wangeipitia ripoti hiyo na kujua wenzao waliishia wapi.
Siku zilikuwa zinakatika tu, msichana mrembo aliendelea kubaki kitandani hapo, aliyafumba macho yake, kula kwenyewe alipitishiwa mipira mdomoni ambayo ilikuwa ikipeleka chakula moja kwa moja.
“Binti yangu atafumbua macho lini?” lilikuwa swali ambalo mzee Chavala alikuwa akimuuliza kila daktari aliyekuwa akimuona.
Hawakuwa na majibu ya kuridhisha, hawakuwa na uhakika kwani aliumia sana, uti wake wa mgongo ulivunjika, walitegemea angechukua kipindi kirefu mno.
“Labda miezi kadhaa!”
“Miezi kadhaa?”
“Ndiyo! Mzee! Binti yako ameumia vibaya, yaani hapa tunatakiwa tumshughulikie kwa kiasi kikubwa sana. Msijali! Watalaamu wa mifupa wapo na kila siku wanaendelea kufuatilia hali yake,” alisema daktari huku akimwangalia mzee huyo.
Wakati huo wote Sam alikuwa akiingia ndani ya chumba kile na kumwangalia msichana yule, pale ilipohitajika kufanya kitu fulani cha kidaktari, alikuwa akimfanyia, kama kumbadilishia dripu na mambo mengine.
Alikuwa karibu na mgonjwa huyo, alikuwa akimfuatilia na kila siku alipokuwa akimwangalia, moyo wake ulimpenda kupita kawaida.
Sylivia hakuzoeleka machoni mwake, kila alipomwangalia alionekana kuwa msichana wa ajabu, uzuri wake ulikuwa kitu kingine kabisa, alimpenda kupita maelezo.
Mwezi ukakatika ndipo Sylivia alirudiwa na fahamu, aliyafumbua macho yake kwa mara ya kwanza. Asubuhi ya siku hiyo aliporudiwa na fahamu ni Sam pekee ndiye aliyekuwa ndani ya chumba kile, aliyagandisha macho yake kwa msichana huyo, ghafla akamuona akiwa ameyafumbua.
Akashtuka, hakuamini alichokuwa akikiona, ilikuwa ni kama ndoto, baada ya kusubiri kwa mwezi mzima, hatimaye msichana huyo alirudiwa na fahamu.
Akamsogelea zaidi, hakutaka kwenda kumuita daktari, mtu wa kwanza ambaye alitakiwa kuona na msichana huyo alikuwa yeye, na ndicho kitu alichokifanya, alitaka kuwa mtu muhimu, hakutaka kujua historia yake, alikuwa mpenzi wa nani, alichokuwa akihitaji ni kuwa naye tu.
“Sylivia...” aliita huku akimwangalia msichana huyo.
Sylivia alirudiwa na fahamu lakini alionekana kutokuwa sawa kabisa. Alimwangalia Sam, hakujua mwanaume huyo alikuwa nani, alikuwa wapi na alikuwa akifanya nini, akabaki akimshangaa tu.
Hakuwa na nguvu za kuongea, asingeweza kufanya hivyo kutokana na mipira iliyokuwa imepitishwa mdomoni mwake, alichokifanya Sam ni kutoka na kwenda kumuita daktari.
“Kuna nini?”
“Yule binti amerudiwa na fahamu!”
“Nani?”
“Sylivia!” alijibu.
Dokta aliposikia hivyo tu, haraka sana akatoka ofisini kwake na kwenda ndani ya chumba kile, alichoambiwa ndicho alichokutana nacho. Sylivia alirudiwa na fahamu huku akiangalia kila kona ndani ya chumba hicho.
Akaanza kumshughulikia na kumuweka sawa, moyo wake ulikuwa na furaha mno na hakuamini wazazi wake wangejisikiaje baada ya kugundua binti yao alirudiwa na fahamu japokuwa hakuweza kutingisha kitu chochote kile.
Zilipita saa mbili ndipo mzee Chavala, mkewe na watoto wao wawili waliingia hospitalini hapo. Kwa kuwaangalia tu walionekana kukata tamaa, walijua siku hiyo ingekuwa kama siku nyingine tu.
Kidogo wakaonekana kuwa na matarajio makubwa baada ya kumwangalia daktari ambaye alionyesha tabasamu pana, wakamuuliza siri ya tabasamu lile, hakuwajibu, alichowaambia ni kwenda nao ofisini.
“Binti yenu amerudiwa na fahamu!” alisema daktari huku akiwaangalia, sura yake ilikuwa na tabasamu pana.
“Kweli?”
“Ndiyo! Tunamuandaa! Nitawaruhusu kwenda kumuona japo kwa dakika tano!” alisema daktari.
Mzee Chavala akashindwa kuvumilia, machozi ya furaha yakaanza kumtoka machoni na kutiririka mashavuni mwake. Hapohapo akatoka kwenye kiti na kupiga magoti, akainyoosha mikono yake juu na kumshukuru Mungu.
Alimpa sifa, alimtukuza kwani kwa kazi aliyokuwa ameifanya haikuwa ndogo hata kidogo, aliamini kwa rehema zake ndiyo maana binti yake aliyafumbua macho na si utaalamu mkubwa wa madaktari.
Walizungumza kwa dakika kadhaa kisha kwenda ndani ya chumba kile kumuona binti yao. Walipofika, wakasimama pembeni yake na kumwangalia. Alikuwa kimya, aliwaangalia, hakufanya kitu chochote kile, hata kutabasamu alishindwa.
Wakiwa humo, mlango ukafunguliwa na Sam kuingia, alipowaona watu hao, naye akatoa tabasamu na kuwaambia hatimaye Mungu alifanya kazi yake na kwa jinsi inavyoonekana Sylivia angekuwa mzima wa afya hapo baadaye.
“Tunashukuru sana kwa msaada wako!” alisema mama yake Sylivia, alimfahamu Sam, alikuwa kijana aliyeongoza kuingia ndani ya chumba hicho, yaani alionekana kumuhudumia binti yake kupita kawaida, hawakujua kama tayari mwenzao moyo wake ulianza kuzama kwa binti yao.
“Haina shida. Nitakuwa namsaidia kila siku. Nitajitoa kwa ajili yake,” alisema Sam huku naye akitoa tabasamu, ili kuwaonyesha alikuwa makini na alichokisema, akajifanya kuanza kumuandaa vizuri pale alipokuwa.
Hayo ndiyo yalikuwa maendeleo makubwa ya Sylivia kitandani alipokuwa. Aliendelea kula na kunywa kwa kutumia mipira na kila siku Sam alikuwa akiingia humo na kumuhudumia kama kawaida.
Baada ya wiki mbili, hatimaye akatolewa mipira ile na kuanza kula kama kawaida huku akilishwa na mama yake. Sylivia alitamani sana kuzungumza lakini alishindwa na mbaya zaidi hata kuinua viungo vyake hakuweza.
Hilo lilimshangaza, hakupewa taarifa kwamba alipooza, hawakutaka kufanya hivyo mpaka pale ambapo angeanza kuongea kitandani pale.
Siku ziliendelea kukatika kama kawaida. Hatimaye mdomo wake ukaanza kupata nguvu, taya zake zilikuwa tayari kunyanyuka lakini si kwa matumaini makubwa.
Kila siku macho yake yalikuwa yakimuona Sam akiingia ndani ya chumba kile na kumuhudumia, alikuwa daktari ila alikuwa na umri mdogo mno. Alikuwa na maswali mengi kuhusu mwanaume huyo, jinsi alivyokuwa akijitoa kwa namna ile lakini akakosa jibu.
Kila alipokuwa akiyakutanisha macho yake naye, Sam aliachia tabasamu pana, tabasamu lililokuwa likielezea kile kilichokuwa moyoni mwake.
Hisia zake zilimwambia inawezekana moyoni mwa mwanaume huyo kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, hakutaka kujipa uhakika juu ya hilo, hisia hizo hazikuwa nzuri kwani alichokikumbuka ni kwamba alikuwa na mpenzi wake, Cassim aliyekuwa akimpenda mno.
Katika siku zote hizo alizokuwa pale hospitalini hakuweza kumuona mwanaume huyo, alishangaa, haikuwa kawaida, kwenye kila tatizo alilokuwanalo mtu wa kwanza kufika alikuwa mwanaume huyo.
Alifariki dunia kwenye ajali lakini hakulijua hilo. Lilimuumiza, akahisi kama alibadilika na hakutaka kuwa naye tena na ndiyo maana hakufika kabisa hospitalini hapo.
Moyo wake ulimuuma, ukachoma lakini hakuwa na jinsi, aliendelea kupata matibabu mpaka siku ambayo mdomo wake ukawa na nguvu na kuanza kuzungumza mbele ya wazazi wake lakini kwa sauti ya chini kabisa.
“Kwa n..ini.. nipo h...ap..a..?” lilikuwa swali la kwanza kabisa alilouliza.
Wazazi wake hawakuwa wamesikia, walichokifanya ni kusogeza masikio yao na kusikiliza tena, akawauliza swali lilelile kwa nini alikuwa mahali hapo.
“Ulipata ajali ya gari?” alijibu baba yake.
“Aj..al..i ya g..ar..i..?” aliuliza.
“Ndiyo! Tunasubiri Mungu akupe nguvu binti yetu!” alisema baba yake.
Sylivia hakuzungumza tena, machozi yalikuwa yakimtoka, moyo wake ulimuuma, kitendo cha kuambiwa alipata ajali akaanza kukumbuka tena mara ya mwisho alipokuwa ndani ya gari lile ambalo lilipinduka baada ya kugongana na lori, hapo akawa na majibu kwamba inawezekana hakumuona mpenzi wake mahali hapo kwa kuwa alifariki dunia.
Moyo ukachoma zaidi, machozi yakaongezeka, alitamani kuyafuta lakini mkono wake haukunyanyuka. Hilo lilimshangaza, akawauliza wazazi wake, walichomjibu ni kwamba alikuwa amepooza.
“Nimep...oo...za..?” aliuliza kwa mshtuko, wazazi wake hawakujibu, wakaanza kutokwa na machozi.
Hilo lilimuumiza, katika maisha yake hakuwahi kufikiria siku moja angepooza na kutoweza kunyanyua kiungo chochote kile mwilini mwake.
Aliwakumbuka wagonjwa waliopooza jinsi walivyokuwa wakipata tabu vitandani mwao, aliumia kuona hata na yeye alikuwa akienda kuishi maisha kama ya watu hao ambao kila siku aliwaonea huruma.
Wazazi wake wakaanza kumfariji kitandani pale kwamba kupooza mwili mzima haikumaanisha alikuwa akienda kufa kulikuwa na watu wengi waliokuwa kwenye hali hiyo lakini bado walikuwa wakipumua na kuendelea kuishi kama kawaida.
Japokuwa alitiwa moyo sana lakini bado hakuwa na furaha, kwake aliona kila kitu kilikuwa kinakwenda kuisha, yaani kuishi bila kufanya kitu chochote kile, hakika yalikuwa maumivu ambayo hakuhisi kama ingetokea siku moja yangepona na kuwa kwenye hali ya kawaida.
Muda mwingi Sam alikuwa akimwangalia Sylivia, alihisi yale mapenzi yake ya kipindi cha nyuma yakiendelea kuchanua moyoni mwake, kuna kipindi alitamani kumwambia ukweli, auweke moyo wake huru lakini kwa sababu ya hali aliyokuwanayo, akaamua kupotezea hilo, akajipa muda wa kusubiri.
“Sylivia...” alimuita siku moja alipokuwa akimuhudumia kama kawaida yake.
“Abeee!”
“Ipo siku Mungu atakuponya na kurudi kwenye hali yako ya kawaida,” alimwambia huku akimwangalia.
“Una uhakika nitapona?”
“Asilimia mia moja, huwa hakuna tatizo linalomshinda Mungu muumba wa Mbingu na nchi,” alimwambia.
“Kabisa.”
“Basi unatakiwa kuamini kwenye hilo pia, imani yako itakuponya,” alimwambia kwa sauti ya upole kabisa.
Walikuwa wakizungumza kama kawaida yao, moyo wa Sam ulijisikia furaha mno, hakuwahi kuwa kwenye kipindi cha furaha kama kipindi hicho, aliusikia moyo wake ukiwa huru kabisa.
Kila alipomwangalia Sylvia aliisikia sauti moyoni mwake ikimwambia kwamba huyo ndiye mwanamke aliyetakiwa kuwa naye na si mwingine, alitaka kumuoa, hakuja hali aliyokuwanayo, lile penzi alilokuwanalo moyoni mwake lilitosha kabisa.
Akatamani kumbusu, kumwambia alivyokuwa akimpenda, yaani kwa kipindi hicho alitamani mambo mengi kwa pamoja lakini alitakiwa kuwa mvumilivu, asubiri kwanza.
“Ila muda unakwenda tu,” alijisemea, sauti yake ilisikika kwa Sylvia.
“Unasemaje?”
“Ooh! Hamna kitu! Naomba nikuache upumzike,” alisema Sam huku akimwangalia msichana huyo.
“Haina shida! Nashukuru!” alisema Sylvia.
“Sawa.”

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumapili mahali hapa.
 
Sehemu ya 04

Kwa kumwangalia mara moja tu tayari Nandy aligundua Sam hakuwa kwenye hali ya kawaida, kila siku alimuuliza kisa nini kilichomfanya kuwa vile lakini hakutaka kumwambia, hilo lilimuumiza mno moyoni mwake na kila alipomuuliza hakumwambia ukweli.
Moyo wake ulikufa na kuoza, alitamani kumwambia Sylivia jinsi alivyojisikia lakini alishindwa kufanya hivyo, hivyo aliendelea kuugulia moyoni mwake.
Siku zilikatika huku naye Nandy akijipanga, tayari alimuona Sam kuwa wake na kusingekuwa na mwanamke yeyote ambaye angemchukua, yaani alihisi mwanaume huyo aliumbwa na kuletwa kwenye dunia hii kwa ajili ya kuishi naye tu.
Kwenye kujipanga huko, siku moja akainuia kwamba ndiyo ilikuwa ya kumwambia Sam ukweli, yaani siku hiyo asiogope kwa lolote lile. Alifanya kazi zake vizuri kabisa na alipomaliza akampigia simu mwanaume huyo na kumuomba kuonana naye.
“Nitakuwa hospitalini!” alimwambia.
“Lakini leo ni Jumapili!”
“Najua! Kuna mtu nakwenda kumuona!”
“Nani?”
Hakujibu swali hilo, ni kama alijishtukia. Nandy alipoona kuna ugumu wa kujibu, akaleta stori nyingine na wakapiga stori nyinginezo lakini kichwani mwake alitaka kujua ni nani hasa Sam alikuwa akienda kuonana naye huko Muhimbili.
Ilipofika majira ya saa sita, haraka sana akaelekea huko, hakumpigia simu Sam, alitaka kumshtukiza kama mwanamke anapoamua kwenda kumfumania mume wake, alipofika huko, akaka sehemu iliyokuwa na kanisa pembeni ndani ya eneo la hospitali hiyo ya taifa.
Alitulia hapo kwa dakika kadhaa na kwa mbali akabahatika kumuona Sam, akainuka na kuanza kumfuatilia. Kwa muda kama huo ilikuwa vigumu kumgundua kwa kuwa kulikuwa na watu wengi mahali hapo, huku akiwa na koti lake jeupe Sam akaanza kuelekea katika wodi ya mifupa, MOI kwa lengo la kumuona Sylvia.
Mpaka kufika hapo, Nandy akatulia kwenye benchi moja, alihitaji kufuatila kila kitu, alifuatilia na kufuatilia lakini hakuona lolote lile kama huyo Sam alikuwa na mwanamke mwingine kwani ilikuwa ni lazima kumuona akiongea naye, alipoona hali shwari, akaamua kumfuata.
“Sam...” alimuita huku akimsogelea.
Sam akageuka, akaanza kumwangalia Nandy, kwa jinsi alivyoonekana, macho yake yalikuwa yakilengwa na machozi.
“Kuna nini tena?” aliuliza Nandy huku akiwa amemsogelea.
“Moyo wangu unaniuma!”
“Kwa sababu gani?”
“Nitakwambia!” alimjibu.
Nandy hakujua Sam alimaanisha nini kumwambia hivyo, moyo wake uliuma kwa sababu gani? Kulikuwa na mwanamke aliyekuwa akimuumiza ama kulikuwa na mgonjwa ambaye alimuonea huruma na hakutaka kuona akifa?
Akamuuliza zaidi na zaidi mwanaume huyo hakujibu lolote lile. Kwa kuwa yeye alikuwa rafiki yake akaona si jambo baya kama angemchukua na kwenda naye kwenye mgahawa mmoja kwa ajili ya kula na kuelekea nyumbani.
Wakaenda huko na kutulia. Bado Sam hakuonekana kuwa sawa, kwa jinsi alivyoonekana kulikuwa na kitu kilichokuwa kikimsumbua na Nandy alitamani kufahamu kilikuwa kitu gani lakini alikuwa mgumu kumwambia.
Sasa hapo akabaki akijiuliza kama ilikuwa sahihi kwake kumwambia jinsi alivyokuwa akimpenda ama alitakiwa kumuacha mpaka siku nyingine. Akajiuliza sana mwisho wa siku akasema angemwambia watakapofika nyumbani, hivyo akatulia.
Walikaa mgahawani kwa dakika arobaini na baada ya kumaliza wakaondoka zao. Ndani ya gari kidogo Sam akaanza kurudi kwenye hali yake ya kawaida, aliongea huku akionekana kama alivyokuwa siku nyingine. Nandy akapelekwa mpaka kwao, alipofikishwa, kwanza hakutaka kutoka ndani ya gari.
“Sam...” alimuita.
“Niambie!”
“Kuna jambo linaniumiza miaka na miaka, naomba tu nkwambie niwe huru,” alisema Nandy, wakati huo mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa nguvu, sasa akaamua kujilipua.
“Kitu gani?” alimuuliza.
Nandy hakutaka kujibu kwanza, akatulia na kuanza kujiuliza kama ulikuwa muda sahihi kumwambia mwanaume huyo ama alitakiwa kwanza atulie mpaka siku nyingine.
Alipofikiria hilo, akaona lingekuwa jambo la kipumbavu sana endapo angenyamaza na kuondoka bila kumwambia lolote lile.
Aliteseka sana moyoni mwake, alijisikia wivu alipomuona akiwa na wanawake wengine wakiongea, aliyapata yote hayo kwa sababu ya ujinga wake wa kuamua kuwa kimya na wakati alikuwa na uwezo wa kumwambia ukweli kuhusu moyo wake.
“Ninakupenda Sam,” alimwambia huku akijisikia aibu.
“Nashukuru sana Nandy! Umekuwa rafiki yangu mkubwa, nakupenda pia,” alimwambia.
“Sam! Listen! I don’t mean that kind of love!” (Sam. Nisikilize! Simaanishi aina hiyo ya upendo) alimwambia.
“What kind of love do I seem to mean?” (Aina gani ya upendo naonekana kumaanisha?) alimuuliza.
“A Philia love,” (Upendo baina ya marafiki) alimjibu.
“And what kind of love do you mean?” (Na wewe unamaanisha upendo wa namna gani?)
“Eros love,” (Upendo wa chumbani) alimjibu.
Sam akanyamaza kwanza, alimwangalia Nandy huku akiwa haamini kile alichokisikia kutoka kwake. Siku zote msichana huyo alimchukulia kama rafiki yake mkubwa, urafiki uliokuwa ukikomaa na kuwa kama ndugu lakini leo hii alimwambia kuhusu aina hiyo ya upendo.
Aliduwaa tu! Hakutegemea kusikia kitu kama hicho kutoka kwa msichana kama huyo, hakujua alitakiwa aseme nini, ilikuwa ni rahisi kumwambia alikuwa rafiki yake mkubwa lakini hilo halikuwazuia watu hao kupendana.
Kumkubalia halikuwa tatizo lakini tayari msichana huyo alichelewa kumwambia kwani tayari moyo wake ulikuwa kwa mtu mwingine, msichana aliyekuwa mgonjwa ambaye alikuwa akipambania uhai wake kitandani.
“Nandy!” alimuita kwa sauti ya chini.
“Don’t hurt my heart, pleaseee...” (Tafadhali usiuumize moyo wangu) alimwambia.
“Why didn’t you tell me before?” (Kwa nini hukuniambia kabla?) alimuuliza.
“I was scared!” (Nilikuwa naogopa)
“Damn!”
“Kuna nini?”
“Umechelewa kuniambia hili,” alimwambia.
“Kivipi?”
“Tayari moyo wangu umeangukia kwenye penzi la msichana mwingine,” alimjibu.
“Moyo wako umeangukia kwa msichana mwingine?”
“Ndiyo!”
“Nani? Sam! Kama hunitaki niambie tu,” alimwambia.
Ilikuwa ni vigumu kuamini kile alichoambiwa, kwake hakikumuingia akilini hata kidogo, kila siku alikuwa na kijana huyo, walikuwa wakifanya mambo mengi pamoja, hakumpa nafasi ya kuwa na mwanamke mwingine, hakuwa amezoeana nao zaidi yake tu, sasa iweje amwambie kulikuwa na mwanamke mwingine? Alikuwa nani na aliishi wapi? Watu hao walikuwa wakionana muda gani? Hayo maswali yote hayakuwa na majibu hata kidogo.
“Nandy! Najua ni vigumu kuniamini!”
“Niambie chochote tu nitakuamini!”
“Nimetokea kumpenda sana Sylvia!” alimwambia.
“Ndiye nani?”
“Yule mgonjwa aliyeletwa kwenye matibabu na kupooza,” alimjibu.
Kama ni maumivu aliyoyasikia yalifanana na yale ya kuchomwa na kitu chenya ncha kali moyoni mwake, hakutegemea kusikia maneno kama hayo kwamba mwanaume aliyekuwa akimpenda alimpenda mwanamke mwingine na si yeye.
Akapoa! Alimwangalia Sam machoni kwa mtazamo uliyoyaonyesha maumivu makali katika uvungu wa moyo wake, alitamani kuhuzunika, akatamani kulia, yaani kila hatua mbaya kwa muda huo alikuwa akiitamani.
“Sam!”
“Nandy! Kwa nini hukuniambia mapema?” alimuuliza.
“Nilikuwa naogopa!”
“Basi pole sana. Moyo wangu upo kwa mtu mwingine,” alimwambia kwa sauti ya chini.
Nandy hakuwa na jinsi, akateremka ndani ya gari na kuanza kuelekea ndani kwao, kwa jinsi alivyokuwa akitembea tu alionekana kuvurugwa mno na kile kilichotokea.
Alipofika chumbani kwake, akajifungia chumbani na kuanza kulia. Alilia kwa maumivu makali, alilia kwa kumaanisha, alilia kwa kulikosa penzi la mwanaume aliyekuwa akimpenda kutoka moyoni kabisa.
Moyo wake ulimlaumu, alikaa na Sam kwa miaka na miaka, kumpenda hakukuanza leo, kulianza miaka mingi tu lakini ujinga wake hakutaka kumwambia, kila siku alisema kesho, kesho, kesho na mwisho akaambiwa alichelewa.
“Hapana! Sikubali!”
Hayo ndiyo maneno pekee aliyoyatamka mahali hapo, ni kweli hakutaka kukubali kumuacha Sam, ilikuwa ni lazima apambane kuhakikisha analipata penzi la mwanaume huyo ambaye kwake tayari alimuona kama mpenzi wake.
Baada ya kufikiria kulipambania penzi hilo, sasa akaamua kunyamaza, akayafuta machozi yake na hivyo kuingia kwenye ulingo wa vita, kupambana na Sylvia aliyekuwa kitandani.
Asubuhi ilipofika, akaondoka na kuelekea Posta, huko akaenda kununua saa nzuri, miwani na baadhi ya vitu na kisha kuvifunga vizuri kwa lengo la kwenda kumgawia Sam kama zawadi.
Hakuwa na kingine cha kufanya zaidi ya hicho, ilikuwa ni lazima kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha anauteka moyo wake. Alikaa chuo huku akiwa na mawazo tele, kwa siku hiyo kila mmoja alihisi Nandy alikuwa na tatizo kwani hakuwa kama alivyokuwa siku za nyuma.
“Nandy!” aliita rafiki yake.
Kimyaaa!
“Nandy!”
Kimyaaa!
“We’ Nandy!”
“Abee Cecilia!”
“Mbona upo hivyo?”
“Nipoje?”
“Haupo sawa. Kuna tatizo?”
“Hamna! Kawaida tu!”
“Haiwezekani! Haupo sawa shoga yangu, hebu niambie tatizo nini,” alimwambia.
Nandy hakutaka kujibu kwa haraka, kwanza akaanza kujiuliza kama lilikuwa jambo jema kumwambia Cecilia kilichokuwa kikiendelea ama alitakiwa kunyamaza.
Huyo alikuwa rafiki yake kipenzi, mwandani wake, aliyekuwa akifahamu siri zake nyingi lakini kitu cha ajabu kuhusu suala la Sam hakuwa amemwambia, sasa naye akatakiwa kujua.
“Kuna nini Nandy?” alimuuliza tena baada ya kuona ukimya wa sekunde kadhaa.
“Mapenzi!”
“Ooh! Kama kawaida yetu! Nayo yamekufanyaje tena? Yuleyule Antony ama?” aliuliza Cecilia.
“Hapana!”
“Sasa nani?”
“Sam!”
“Sam! Kaka yako?” aliuliza Cecilia huku akionekana kushtuka.
“Cecilia nisikilize kwanza!”
“Aya niambie!”
“Sam si kaka yangu kama nilivyowaambia!”
“Siyo kaka yako?”
“Ndiyo! Ni family friend tu, tumekua pamoja na familia zetu zinajuana sana, ila si ndugu kabisa,” alimjibu.
“Ooh! Kwa hiyo umempenda?”
“Ndiyo!”
“Kwa nini usimwambie?”
“Nimemwambia!”
“Akasemaje?”
“Ana mtu!”
“Sasa wewe hukujua kama ana mtu?”
“Sikujua!”
“Kwa nini na wakati ulikuwa karibu naye kila siku?”
“Yaani acha tu!”
“Kwa nini?”
“Huyo mtu amemuona mwezi uliopita, ni mgonjwa aliyelazwa pale Muhimbili, yaani kumuona tu, amempenda!” alijibu Nandy.
“Eeh! Wanaume jamaniiiiiiiiiiiii!”
“Yaani wewe acha. Ameniambia nimechelewa kwa sababu ya mgonjwa ambaye hajui hata historia yake, hajui kama ana mpenzi ama mume, yaani hanitaki kwa ajili ya msichana huyo,” alimwambia.
“Mh! Ndiyo kwanza nasikia leo!”
“Yaani acha! Ila sitaki kukata tamaa, nampenda sana Sam, lazima nifanye juu chini nihakikishe nampata!”
“Utampataje?”
“Nimejaribu kumnunulia zawadi! Ninazo hapa! Ila naogopa sana kumpa,” alimwambia.
“Basi niachie mimi kazi ya kumpa!”
“Utaweza?”
“Sasa nishindwe nini?”
“Sawa. Nadhani sasa hivi atakuwa hospitalini!”
“Nitamfuata hukohuko! Namba yake si ileile?”
“Yeah! Mwisho 22!”
“Sawa!”
Sasa kazi akapewa Cecilia kwa lengo la kwenda kumfikishia Sam zawadi hizo, akachukua mzigo ule na kumpigia simu mwanaume huyo na kumwambia anataka kuonana naye.
Hilo halikuwa na shida, akaambiwa aende huko hospitalini na angemkuta, akaelekea huko, alipofika, akaulizia na kuambiwa mahali alipokuwa, kwenye wodi ya mifupa, MOI ambapo akaenda huko huku akiwa na mfuko.
Alipokuwa kwa mbali na kuangalia, akamuona akiwa amesimama na watu kadhaa, kama wanne kwenye kitanda alichokuwa mgonjwa mmoja, kichwa chake kikamwambia inawezekana mgonjwa huyo ndiye huyo mwanamke aliyeambiwa na Nandy, sasa naye akataka kumuona.
Akapiga hatua mpaka mahali walipokuwa, alipofika akamshika Sam bega kwa nyuma, alipogeuka akamsalimia huku akiachia tabasamu, akawasalimia na watu wengine huku akiwaangalia, mtu wa mwisho kabisa kumwangalia alikuwa yule mgonjwa aliyelala kutandani.
Hakuamini macho yake.
Hakujua kama alikuwa akimwangalia binadamu ama malaika.
Aliwahi kusikia maneno mengi kuhusu uzuri.
Yule aliyelala kitandani alikuwa ndiyo mwenye huo uzuri.
Alivutia!
Alikuwa maana halisi ya uzuri!
Akajisahau na kujikuta akibaki akimkodolea macho tu, yeye mwenyewe uso wake ukashindwa kuvumilia, akajikuta akitoa tabasamu pana, akatamani hata kumsogelea huyo Sylvia na kumkumbatia kitandani pale.
“Ni mzuriiiiiiiii...” alijikuta akijisemea moyoni mwake.
Hata alichotumwa akakisahau kwa muda.

Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya

“Cecilia...” aliita Sam huku akimwangalia msichana huyo ambaye baada ya kuitwa, akashtuka kwa mbali.
“Abeee!”
“Upo kimya sana! Tunaweza kuzungumza?” alimwambia na kumuuliza.
“Haina shida!”
Wakaenda pembeni, kwa kumwangalia tu usoni Cecilia alionekana kama mtu fulani aliyekuwa amevurugwa na kitu fulani, kwa jinsi alivyomuona Syliva machoni mwake akakiri kabisa alikuwa na mtihani mgumu wa kumshawishi Sam kuwa na rafiki yake.
Hapo pembeni msichana huyo akamwambia Sam kuwa aliagizwa na Nandy kwa lengo la kupewa zawadi zilizokuwa kwenye mfuko lakini pia alitakiwa kumwambia ni kwa namna gani alikuwa akipendwa na msichana huyo.
“Amesemaje?” alimuuliza.
“Anakupenda sana!”
“Mwambie nashukuru!”
“Hilo tu?”
“Yaaap!”
Baada ya kuzungumza maneno hayo, hakutaka kuendelea kusimama na Cecilia, akaondoka zake kuelekea chumba kingine na kuweka mfuko ule wa zawadi huko na kurudi pale alipokuwa Sylvia ambapo akamkuta tena Cecilia akiwa anamwangalia tu msichana huyo.
Walikaa na kuzungumza kidogo na baada ya hapo akamsindikiza kuelekea nyumbani kwao. Walitoka mpaka nje ya hospitali hiyo ambapo akamuitia bodaboda kwa lengo la kumrudisha alipotoka.
Cecilia alikuwa na mambo mengi ya kumwambia Sam, alitumwa kwa lengo la kumlaghai mwanaume huyo awe na rafiki yake lakini kwa kile alichokikuta ndani ya hospitali ile, hata mdomo wake ukawa mgumu zaidi kufumbuka.
Alimfahamu rafiki yake, Nandy, ni kweli alikuwa msichana mrembo mno, wanaume walitamani kuwa naye lakini kila alipomkumbuka Sylvia, yule msichana alikuwa wa tofauti kabisa, yaani alikuwa mrembo kupita kawaida.
“Tutaonana!” alimwambia na kuondoka.
Safari hiyo ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa akina Nandy kwa lengo la kuongea nye, alitaka kumwambia ukweli wa kile alichokutana nacho kule alipokwenda, alikuwa na hofu kwamba rafiki yake angemuona kuwa mnafiki na msaliti lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kumwambia kile alichokiona.
Huku akiwa njiani, Nandy akaanza kumpigia simu mfululizo, alihitaji kufahamu kile kilichotokea huko, hakutaka kupokea simu zake, alihitaji kwenda mpaka nyumbani kwao na kumwambia ana kwa ana kile alichokiona huko.
Hakuchukua dakika nyingi sana akafika nyumbani kwa akina Nandy na kuingia ndani, rafiki yake huyo baada ya kumuona, akaonyesha tabasamu huku akimsogelea, kwanza akamkumbatia kwa kuwa aliamini kulikuwa na taarifa nzuri aliyotaka kumpa.
“Imekuwaje?” alimuuliza huku akimwangalia.
“Ni kweli nilikwenda!”
“Ukakutana naye?”
“Ndiyo!”
“Ukampa?” aliuliza Nandy kwa shauku.
“Ndiyo!”
“Akasemaje?”
“Akashukuru!”
“Hilo tu?”
“Ndiyo!”
“Hajaonyesha hata hali fulani hivi?”
“Hapana! Aliniambia nikwambie anashukuru sana!” alimjibu, kidogo Nandy akapoa.
“Na huyo msichana ulimuona?”
“Ndiyo!”
“Yupoje?”
Cecilia hakutaka kujibu swali hilo kwa haraka kwa kuwa aliamini jibu ambalo angelitoa kwa rafiki yake huyo ilikuwa ni lazima kumchanganya na kumnyima furaha kabisa.
Alikipa kichwa chake kazi ya kufikiria ni kwa namna gani alitakiwa kumwambia kile alichokutana nacho huko. Ukimya huo kidogo ukamfanya Nandy kuhisi kulikuwa na jambo ambalo rafiki yake huyo hakutaka kumwambia muda huo.
“Imekuwaje?” alimuuliza baada ya ukimya wa sekunde kadhaa.
“Ulishawahi kumuona huyo msichana?” alimuuliza.
“Hapana! Yupoje?” alimuuliza.
“Aiseee!”
“Kwani yupoje?”
“Ni mzuri sana! Yule msichana ni mzuri mnooo!” alimjibu, ilibidi iwe hivyo ingawa hakutaka kumwambia kabisa juu ya ule uzuri aliokuwa amekutana nao huko.
Ni kweli alivyofikiria ndicho kilichotokea, Nandy akapoa, moyo wake ni kama uliingiwa na ubaridi fulani, alibaki akiwa amesimama, wakati mwingine alitamani kuona kile kilichokuwa kikiendelea kuwa kama ndoto fulani ambapo baada ya muda angeamka na kujikuta akiwa kitandani.
Kama rafiki yake alimwambia huyo msichana kwamba ni mzuri sana, ni kweli inawezekana alikuwa mzuri na hiyo ilimaanisha ingekuwa ni vigumu sana kwake kumpata Sam kwa kuwa tu alikutana na msichana aliyekuwa mrembo mno.
“Nandy! Najua ni kwa namna gani unaumia, naomba uachane tu na Sam, tafuta mwingine, wanaume wapo wengi sana,” alimwambia kwa sauti ndogo, Nandy akayainua macho yake, machozi yalianza kutiririka mashavuni mwake.
“Siwezi....siweziiiiiii....” alisema Nandy na kuanza kulia kwa sauti.
Aliwahi kuwa na maumivu ya kila aina kwenye maisha yake lakini yale ambayo aliyasikia kipindi hicho yalikuwa ni zaidi ya mauamivu. Hakuwahi kufikiria hata siku moja kwamba ingetokea siku ambayo angekuja kumpenda mwanaume ambaye hakuwa na mpango naye.
Hakutaka tena kuongea na Cecilia, alichomwambia amuache na yeye kujifungia chumbani, sasa akaendelea kulia zaidi na zaidi huku akitamani sana kuwa na Sam kitu ambacho hakikuwezekana kabisa.
***
Sam alimaanisha kuhusu upendo wake mkubwa kwa Sylvia, kila alipomwangalia msichana huyo kitandani pale aliyasikia kabisa mapenzi mazito moyoni mwake.
Hakutaka kufanya siri na hivyo kumwambia Sylvia jinsi alivyokuwa akimpenda mno kutoka moyoni mwake. Kwa msichana huyo ilikuwa ni vigumu kukubaliana naye, hakutaka kuamini kama Sam alimpenda kweli kutokana na jinsi alivyokuwa.
Hakuwa kama alivyokuwa kipindi cha nyuma, asingeweza kutembea tena, alikuwa mtu wa kulala kitandani na kubwa zaidi asingeweza hata kumzalia mtoto kitu ambacho kilikuwa ni ndoto ya kila mwanaume katika dunia hii.
Pamoja na kuambiwa hayo yote lakini bado Sam alimwambia alimpenda, kwenye dunia hii hapakuwa na msichana yeyote aliyemuingia moyoni mwake kama yeye, hivyo alihitaji sana awe mpenzi wake.
“Sam! Ni vigumu sana,” alimwambia huku akimwangalia.
“Nimekwishasema Sylvia, hakuna kitu kitakachoweza kunitenganisha nawe. Ninakupenda sana,” alimwambia.
“Hivi unajua kama nimepooza?”
“Najua!”
“Unajua kama sitoweza kutembea tena?”
“Najua!”
“Unajua kwamba sitoweza kukupatia hata mtoto?”
“Najua! Hayo yote najua mama!”
“Sasa why me?”
“Ni kwa sababu nakupenda. Ninakupenda sana Sylvia na nimekuwa nikijilaumu kwa sababu gani sikuwahi kukuona hapo kabla. Nadhani sijachelewa, naomba kuwa nawe,” alimwambia msichana huyo.
Mapenzi mazito yakaonekana machoni mwake, kwa Sylvia alitamani kumkataa lakini kila alipomwangalia, mwanaume huyo alionekana kumaanisha kwa asilimia mia moja.
Alichomwambia ni kuwa ampe muda na angemjibu, katika suala hilo ilikuwa ni lazima kuzungumza na wazazi wake, haikuwa rahisi kufanya uamuzi kama huo kutokana na hali aliyokuwanayo.
“Haina shida,” alimwambia.
Hilo ndilo lililofanyika, mara baada ya wazazi wake kufika hospitalini hapo, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuwaambia kuhusu huyo Sam, maneno aliyomwambia alitamani sana kuwa naye.
Wazazi hao walishtuka, ni kweli walihisi Sam alikuwa akimpenda binti yao lakini hawakuamini kama angefikia hatua ya kumwambia kuhusu mapenzi hayo na kutaka kuwa naye maishani mwake.
“Inawezekanaje?” alimuuliza.
“Sijui mama! Ameniambia ananipenda sana,” alijibu.
“Oopss!” alisikika mzee Chavala akishusha pumzi ndefu.
“Wewe uamuzi wako ni nini?” aliuliza mama yake.
“Sijajua! Sina uamuzi wowote ule, maamuzi yangu yapo juu yenu kutokana na hii hali niliyokuwanayo,” alimjibu.
Wazazi hao wakaangaliana! Kwa kile alichokisema Sylvia ni kweli kabisa, kwa muda huo hakutaka kupanga uamuzi kwa kuwa alikuwa akiishi na wazazi wake na kubwa zaidi ilikuwa ni ile hali aliyokuwanayo.
“Acha nikazungumze naye!” alisema mzee Chavala.
“Unakwenda kumwambiaje?” aliuliza mama yake Sylvia.
“Niachieni mie, nitajua tu cha kumwambia kama baba,” alisema mzee huyo, hakutaka kupoteza hata dakika moja, akatoka na kumfuata Sam ambaye alikuwa nje ya wodi hiyo huku akitetemeka, hakujua kutetemeka huko kulisababishwa na hofu ama la! Ila alitamani mno kuona wazazi wa msichana huyo wakikubaliana naye kwa kuwa tu moyo wake ulikuwa kwenye mapenzi mazito na msichana huyo mrembo.
Na moyo wake haukutaka kumkosa hata kidogo.
“Njoo tuzungumze,” alisema mzee Chavala mara baada ya kumfikia Sam, akamuita kwa pembeni, kwa heshima zote, kijana huyo akamfuata mzee huyo, kwa kumwangalia tu machoni akashindwa kuelewa kama kulikuwa na habari mbaya ama nzuri.
Akajiweka vizuri kumsikiliza.
“Una uhakika unampenda binti yangu?’ lilikuwa swali la kwanza kuuliza mzee Chavala huku akimwangalia Sam.
“Ninampenda kutoka moyoni mwangu!” alimjibu.
“Una uhakika unampenda?”
“Ndiyo!”
“Una uhakika unampenda kwa dhati?”
“Ndiyo!”
Mzee Chavala kwanza akakaa kimya, kwa vile alivyoongea Sam ni kama alimaanisha kutoka moyoni mwake. Alimfahamu binti yake, alikuwa msichana mrembo mno kwa kila mtu ambaye angediriki kukutana naye ilikuwa ni lazima kumpenda na kutamani kuwa naye.
Kwa Sam hali ilionekana kuwa tofauti kabisa, alimpenda binti yake, alikuwa tayari kwa lolote lile hata kama hakuwa na haja ya kufanya naye mapenzi kutokana na hali aliyokuwanayo, alichokitaka ni kuwa naye tu.
Kwa mzee huyo hapakuwa na tatizo lolote lile, alichokitaka ni kupata uhakika wa kile alichokisema Sam kwamba alimpenda kwa dhati, tena ili kupata uhakika alimuuliza swali moja mara tatu, na mara zote kijana huyo alimwambia ni kweli alimpenda kwa mapenzi ya dhati.
Wakatoka kule walipokuwa wamesimama kuongea na kurudi kule kilipokuwa kitanda cha Sylvia, kila mmoja alionekana kuwa na furaha tu kitu kilichowapata majibu kila kitu kilikwenda vizuri kama kilivyopangwa.
Wazazi wakaruhusu Sam awe na binti yao, mepenzi yakafunguliwa rasmi na hatimaye kuanza kuzungumza na kupanga mambo mengi kama wapenzi.
Katika kipindi chote hicho Sylvia alikuwa na maswali mengi kichwani mwake, hakuamini kama kungetokea na mwanaume ambaye angempenda kama alivyokuwa. Alipooza, alikuwa kitandani, hakuweza kufanya jambo lolote lile lakini cha kushangaza huku akiwa kwenye hali hiyo, mwanaume huyo akaibuka na kumwambia alimpenda mno.
Sylvia hakukaa sana hospitalini baada ya kuonekana ana nafuu, hatimaye akaruhusiwa kwenda nyumbani huku akiwa kwenye kiti cha matairi, na mtu aliyekuwa akimuendesha alikuwa huyo Sam ambaye hakuwa akiambiwa lolote lile kwa msichana huyo, alikuwa radhi kupoteza kila kitu lakini si kumpoteza Sylvia.
Maisha yao yakawa hivyo, kila siku Sam alipotoka chuo, sehemu ya kwanza ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa akina Sylvia aliyekuwa akiishi Mikocheni B, huku alikuwa akikaa naye kwa saa kadhaa huku akimuhudumia kwa kila kitu na kisha kuondoka kurudi nyumbani.
Kwa kitendo cha kuwa karibu na Sylvia, akatokea kupoteza ukaribu kwa marafiki wengine akiwemo Nandy ambaye mara nyingi alitamani kuwa karibu na mwanaume huyo ili amfanyie mambo mengi kuonyesha ni kwa namna gani alikuwa akimpenda lakini ilishindikana kabisa.
Baada ya mwaka mmoja, hatimaye Sam akamaliza masomo yake chuoni ambayo alisoma kwa miaka sita na hivyo kuajiriwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenye kitengo cha wagonjwa wa misuli kama alivyokuwa amechagua.
Kwake yalikuwa ni mafanikio makubwa mno, kila siku alimuomba Mungu amuewezeshe kumaliza masomo yake na hatimaye kuanza kazi, Mungu alifanya muujiza na hatimaye akamaliza na kuanza kazi hiyo.
Japokuwa alikuwa bize sana lakini kila siku ilikuwa ni lazima kwenda kwa akina Sylivia na kumsalimia, hakutaka kuwa na mwanamke mwingine, kwake, kitu cha kwanza alichokuwa akikipenda kilikuwa ni msichana huyo mrembo na cha pili kilikuwa kazi yake.
“Sylvia...” alimuita msichana huyo!”
“Abeee!”
“Ninataka kukuoa!” alimwambia.
“Unasemaje?” aliuliza Sylvia huku akionekana kutokuamini alichokisikia.
“Ninataka kufunga ndoa nawe.”
“Sam....”
“Kwenye hili sitaki kupingwa mpenzi! Nimetoka nawe mbali sana, mwaka na nusu huu, acha nikuoe, kama ni muujiza, acha Mungu aufanye tukiwa ndani ya ndoa,” alimwambia kwa sauti ndogo.
“Lakini....”
“Kwenye hili hakuna cha lakini mpenzi!” alimwambia.
Sylivia alibaki kimya kwa sekunde kadhaa huku akionekana ujifikiria kile alichoambiwa na mwanaume huyo, kuolewa naye kwake hakuona kama kingekuwa kitu chepesi sana, kwa kijana mzuri kama Sam alitakiwa kupata mwanamke mwenye afya tele ambaye angemzalia mtoto na hatimaye kutengeneza familia pamoja naye.
Kwake, aliona kama jambo hilo lingekuwa ni kumtesa kijana wa watu, alijaribu kumwambia hilo lakini Sam hakutaka kukubali hata kidogo, aliendelea kumwambia kwamba kwenye mambo yote aliyokuwa akitaka maishani mwake, cha kwanza kilikuwa ni kufunga ndoa pamoja naye.
“Sawa. Haina shida” alisema Sylvia huku akimwangalia mwanaume huyo, wakaachia tabasamu na kubusiana.

Je, nini kitaendelea?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom