Simulizi: Msichana Ndotoni Mwangu

Simulizi: Msichana Ndotoni Mwangu

SEHEMU YA 09



KWA hakika nilichanganyikiwa macho yangu yaliganda kwa muda ndani ya gari nikimwangalia Tyra kwa macho ya matamanio kisha nikayarudisha tena kwa Monalisa ambaye taratibu alikuwa akitembea kuja upande wetu.

Mwili ulinitetemeka lakini nilijitahidi sana kuficha hali hiyo. Sikutaka kuonekana dhaifu lakini lazima nikiri kwamba wanawake hao wawili waliuchanganya sana moyo wangu.
“Phillip get in the car, please!” (Phillip ingia kwenye gari tafadhali!)Tyra aliniambia kwa sauti yenye ukali kidogo.

Kwa mara ya kwanza nilimshuhudia Tyra akizungumza kwa sauti ya ukali. Nilitulia kwa muda nikitafakari cha kufanya, kabla sijapata majibu tayari Monalisa naye alikuwa anaongea.
“Come with me, please, baby!” (Tafadhali njoo huku, mpenzi.)

Kwa kweli nilichanganyikiwa nikapoteza mwelekeo, nikashindwa kuelewa kitu cha kufanya. Sekunde chache baadaye Monalisa alikuwa ameshafika nilipokuwa nimesimama, akanipigapiga begani kisha akaanza kuzungumza tena:
“Phillip why can’t you here my voice, please. Let’s go!” (Philip mbona husikii sauti yangu tafadhali. Twen’zetu!)

“Excuse me, Monalisa. I am going somewhere with Tyra, I had an appointment with her.” (Samahani Monalisa. Ninakwenda sehemu fulani na Tyra, nilikuwa na ahadi naye.)
Hata hivyo, moyoni nilijua kabisa kwamba nilimjibu kwa kumridhisha maana sikuwa na ahadi naye. Isitoshe hakuna yeyote kati yao niliyekuwa na uhusiano naye wa kimapenzi, hivyo nilikuwa na uhuru wa kufanya chochote bila ruhusa ya yeyote.

“Where to?” (Wapi huko?)
“Bagamoyo.”
“Who is this girl?” (Huyu msichana ni nani?)
“She is just my friend.” (Ni rafiki yangu tu.)


“If it is so, can’t you postpone it as I have very important talks with you?” (Kama ndiyo hivyo, huwezi kuahirisha maana nina mazungumzo muhimu nawe?”
Nilishangazwa na jinsi Monalisa anavyojiamini, isingekuwa rahisi kwa mwanamke mwingine kujiamini na kuongea na mwanaume maneno yale mbele ya mwenzake ambaye hajajua uhusiano wao.

Sikuwa mwepesi kujibu swali lake, nilichokifanya ni kusoma kupitia macho ya Tyra. Nilichokifanya ni kuinama kidogo kisha kuchungulia kwenye kioo cha gari nikakutana na macho ya Tyra yakizungumza; alikuwa analia.
Moyo wangu ukaenda mbio, Tyra hakujua kitu kimoja machozi yake yalimfanya azidi kuonekana mrembo zaidi. Nikahisi huruma moyoni mwangu. Ni kweli kwamba Tyra alitaka kutoka na mimi, tena ni yeye aliyenipigia simu kuniomba, nami kwa moyo mkunjufu nikamkubalia.

Kwa vile hakuna yeyote kati yao niliyekuwa na uhusiano naye wa kimapenzi ilikuwa rahisi sana kufanya uamuzi. Kitu pekee nilichotakiwa kukifanya ni kuondoka na Tyra kama nilivyokuwa nimekubaliana naye mwanzoni.

Nikainua kichwa changu kisha nikayatuliza macho yangu juu ya uso wa Monalisa. Midomo yangu ikaanza kucheza, nilikuwa natafakari maneno ya kumwambia ili aridhike.
“Excuse me, Monalisa. I cannot go out with you today as I already have an appointment with Tyra. I am sorry for inconveniencing you, but I believe you will understand me.” (Samahani Monalisa. Siwezi kutoka na wewe leo kwa sababu tayari nilikuwa na ahadi na Tyra. Samahani kama nitakuwa nimekuudhi, lakini naamini umenielewa.)

Baada ya hapo sikuongea neno jingine lolote zaidi ya kufungua mlango na kuketi upande wa abiria, nikageuza shingo yangu kumwangalia Tyra, alikuwa akijifuta machozi kwa kitambaa cheupe.
“Excuse me, Tyra. I did not like this to happen. Let’s go,” (Samahani sana Tyra, sikupenda haya yatokee, washa gari twende), nilimwambia Tyra nikiwa nimeyatuliza macho yangu usoni mwake.

Kitu cha ajabu, hakusema neno lolote zaidi ya kuwasha gari kisha akageuza na kuliondoa kwa kasi. Monalisa akabaki anatusindikiza kwa macho hadi tulipotokomea. Nilikuwa kimya kwenye gari, nikitafakari mambo yaliyotokea.
Kwa kweli sikuwa na la kuzungumza na Trya ambaye alionekana kuvimba kwa hasira. Kimsingi hakuwa na sababu ya kukasirika maana ni kweli kwamba hakuwa na uhusiano na mimi. Ukimya wangu ulimfanya naye awe kimya!

Mpaka tunafika Mwenge, hakuna aliyezungumza na mwenzake, gari likakata kushoto kuifuata barabara ya Bagamoyo na kwenda kwa kasi ile ile. Kwa bahati nzuri hapakuwa na foleni kabisa siku hiyo, hivyo alikuwa na uwezo wa kuendesha kwa kasi aliyoipenda.
Nilijitahidi kukaa kimya, lakini tulipofika Mapinga, nilishindwa kuvumilia. Nikaamua kufungua kinywa changu na kuanzisha mazungumzo.

“Mbona umenyamaza muda wote? Bado una hasira Tyra?” Niliongea kwa sauti ya taratibu kabisa.
“Tutaongea Bagamoyo!”
“Ok!”

Ni kama Tyra alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mimi maana tukio la Monalisa lilimchanganya sana kichwa chake. Ni kweli hakufungua tena kinywa chake kuongea na mimi hadi tulipoingia Bagamoyo katika Hoteli ya Paradise, tukashuka na kwenda kukaa kwenye moja ya meza zilizokuwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi.

Punde mhudumu alifika kutusikiliza, tukaagiza vinywaji na vyakula. Muda mfupi baadaye alituletea vinywaji kisha akatuambia kwamba vyakula vilikuwa vikitayarishwa jikoni na vingeletwa mezani baada ya dakika thelathini na tano.
Tukaanza kunywa pamoja lakini usoni Tyra alionekana kama anatunga sheria. Uso wake ulionesha kuwa ana mambo mengi sana yanayomchanganya.

“Ndiyo umefanya nini Phillip?”
“Kwa nini? Kivipi?”
“Hujui ulichokifanya?”
“Niambie basi!”

“Sikutegemea kama uliniita ili uniumize. Kwa nini unanitesa kiasi hicho?”
“Unajua mpaka sasa hivi sijakuelewa Tyra, bila shaka unazungumza kuhusu Monalisa.”
“Ndiyo huyo huyo Monalisa wako ambaye nilikwambia mchana kwamba chuo kizima kinajua uhusiano wenu ukakataa, sasa nimeshuhudia kwa macho yangu.”

“Tyra kwani sitakiwi kuwa na marafiki?”
“Simaanishi hivyo lakini kwa nini unautesa moyo wangu kwa kiwango hicho?”
“Inabidi uwe muwazi zaidi ya hapo!”

“BABY I LOVE YOU SO MUCH I HAVE ALWAYS SHOWED YOU VARIOUS SIGNS AND DONE MANY THINGS TO SHOW YOU MY LOVE. DO YOU WANT TO TELL ME THAT YOU DO NOT SEE THEM? WHY DO YOU WANT TO TORTURE ME IN THIS WAY? PLEASE, I ASK YOU TO OPEN YOUR HEART FOR ME. I LOVE YOU PHILLIP!” (Mpenzi nakupenda sana, kila mara nimekuwa nikikuonesha ishara kadhaa za mapenzi yangu kwako. Unataka kuniambia huzioni? Kwa nini unataka kunitesa kiasi hiki? Tafadhali naomba uufungue moyo wako unikaribishe. Nakupenda Phillip!) Tyra alitamka maneno haya akionesha hisia kali za mapenzi.

Nilisisimka mwili, aliongea maneno mazito ambayo yalinichoma. Kwa hakika nilimwonea huruma, nikatamani kuwa naye lakini tatizo lilikuwa ni Zamaradi. Kwa mbali nilianza kuhisi harufu ya manukato ya Zamaradi wangu. Woga uliongezeka baada ya kugundua kwamba tulikuwa tumekaa ufukweni mwa bahari, eneo ambalo ndani yake ndiyo makazi ya Zamaradi.
HAKIKA Tyra alikuwa akinieleza maneno mazito sana, siwezi kumlaumu maana zilikuwa ni hisia kutoka ndani ya moyo wake. Alikuwa na haki ya msingi ya kueleza kila alichojisikia moyoni mwake.

Nilitegemea kusikia maneno hayo, maana siku zote niligundua kwamba Tyra alikuwa akinipenda sana. Si yeye peke yake bali wanawake wengi kila wanaponitazama walivutiwa na mimi. Haikuwa kosa lake bali moyo wake.

Ni kweli hata mimi nilimpenda sana, hilo napenda nikiri mbele yenu, lakini nisingeweza kuwa na mwanamke mwingine tofauti na Zamaradi. Natamani sana jambo hilo litokee lakini niliogopa kutokana na maneno ya Zamaradi aliyokuwa akijiapiza mara kwa mara anaponitokea usiku.

Ukimya wangu ukamfanya Tyra apate wasiwasi, alitamani kusikia sauti yangu nikisema chochote kuhusu ombi lake. Akayatuliza macho yake usoni mwangu, nami pia. Hata hivyo, sikuwa na jibu la kumpa.
“Phillip!” Tyra aliita kwa sauti ya taratibu sana.
“Nakusikia.”

“Nasubiri jibu lako.”
“Samahani, hatuwezi kubaki kuwa marafiki?”
“Hapana, acha utani wako bwana. Kumbuka hizi ni hisia za ndani ya moyo wangu. Naomba usizidhihaki, nipokee tafadhali. Nakupenda!”
“Najua lakini kwa nionavyo mimi, tunapendeza tukibaki hivi tulivyo kuliko kuanza uhusiano mwingine mpya!”

“Hapana sikia kilio changu, mimi nakupenda.”
“Najua hata mimi nakupenda tena nakupenda zaidi ya unavyonipenda, lakini kwa sababu ya mapenzi hayo ndiyo maana sitaki tuanzishe kitu kingine tofauti.”
“Mbona sikuelewi?”

“Hautanielewa kirahisi lakini unachotakiwa kufahamu ni kwamba ni hatari sana mimi kuwa na uhusiano na wewe. Tafadhali naomba uelewe.”
“Mbona sikuelewi? Unanichanganya kabisa!”

Kufikia hapo nikazidi kuchanganyikiwa maana Tyra alikuwa king’ang’anizi kweli kweli. Akanisogelea nilipokuwa nimekaa kisha akanikalia, hapo woga ukanizidi, nikamwona kabisa Zamaradi akija mbele yangu, kitu ambacho sikutaka kabisa kitokee.

Kwa mara nyingine nikaanza kumchukia tena Zamaradi, ni kweli alikuwa mwanamke mzuri lakini alininyima uhuru wa kufanya mambo yangu. Mbaya zaidi hatokei katika hali ya kawaida, ananinyanyasa na kuninyima uhuru.

Lakini sikutaka matatizo na Zamaradi, hivyo nikamsukuma Tyra aliyeanguka pembeni. Akaanza kulia kwa uchungu huku akilaumu kitendo nilichomfanyia.
“Kwa nini unanifanyia hivi, kwa sababu nimekupenda?”

“Hapana napenda sana maisha yako, utapata matatizo, usitake kuwa na mimi. Tafadhali niondoe kichwani mwako, nifanye kama rafiki tu,” nikamwambia kwa uchungu moyoni.
Maneno hayo ni kama hayakumwingia kabisa Tyra ambaye aliinuka pale chini na kunifuata kisha kunikumbatia kwa nguvu akiuleta mdomo wake kinywani mwangu, nilijua kilichotaka kutokea, sikuwa tayari.

Nikamsukuma kwa nguvu, akaanguka pembeni. Nikatumia nafasi hiyo kukimbia. Nilipofanya hivyo alinikimbiza kwa nyuma huku akiita jina langu lakini sikugeuka. Hakuweza kunikimbiza umbali mrefu nikafanikiwa kutoka nje ya geti la Hoteli ya Paradise kisha nikasimamisha pikipiki iliyonipeleka hadi kituo cha mabasi.

Hapo nikapanda basi linaloelekea Mwenge, Dar es Salaam. Moyoni nilikuwa na maumivu makali. Sikutaka kumuumiza kiasi kile Tyra lakini sikuwa na jinsi ya kufanya. Ilikuwa ni lazima niondoke maana maisha yake na yangu yalikuwa muhimu sana.

Nilimfahamu vyema Zamaradi, siku zote huwa na hasira sana juu yangu, nilijua kama ningeendelea kuwa na Tyra katika hali ile, lazima angemdhuru. Lakini pia nilisubiri adhabu yangu usiku ambapo nilitegemea lazima angenijia.

Nikiwa kituoni nilifanikiwa kupanda basi lililonifikisha mpaka Mwenge ambapo nilipanda daladala inayoelekea chuo. Niliposhuka katika kituo cha Utawala, macho yangu yaligongana na Monalisa aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Cresta. Akapiga honi kisha akafinya mkono kuashiria kuniita.

“Nakuja!” nilisema nikivuka upande wa pili.
“Ingia kwenye gari tafadhali,” alisema Monalisa kwa mtindo wa kuamrisha.
Nami nikaingia. Hakusema neno lolote zaidi ya kuwasha gari kisha akakata kulia akiifuata barabara ya chuo kuelekea kwenye geti la kwenda Ubungo.
“Vipi usharudi Bagamoyo?” aliuliza Monalisa akinitizama usoni.
“Ndiyo!” Nikamjibu kwa kifupi.

“Ok! Naona uliamua kuniacha sababu ya Tyra, lakini ni vile tu hujajua ni kiasi gani nakupenda. Ungenipa nafasi hiyo ningekuonyesha mapenzi motomoto.”
Hakujua ni kiasi gani maneno yake yalinichoma maana nilimkimbia Tyra huko Bagamoyo kutokana na mambo kama aliyoniambia. Nilimshangaa lakini pia nilimwonea huruma.
“Hatuwezi kubadilisha stori?”

“Tunaweza, naona unachukia sana tukizungumza kuhusu huyo mwanamke wako.”
“Halafu tunaelekea wapi?”
“Hapa Mlimani City, hutaki kukaa na mimi japo tupate maji ya matunda?”
“Ok!”

Monalisa akaendelea kuendesha gari hadi Mlimani City ambapo tulitafuta sehemu tukakaa na kuanza kula na kunywa. Tuliongea mambo mengi sana, kitu kilichonifurahisha zaidi ni kwamba Monalisa alinielewa maana hakuzungumza tena mambo ya mapenzi.

Tukaendelea kunywa kwa furaha hadi usiku sana. Monalisa akaniambia tuondoke, mimi nilikuwa nimeshika boksi lenye juisi na Monalisa alikuwa na boksi lenye mvinyo mweupe. Tulipoingia kwenye gari nikaanza kuhisi kuchangamka ghafla, ni hali ambayo sikuielewa, maana ilifikia mahali Monalisa alikuwa akinibusu nami nikamrudishia. Baada ya hapo sikukumbuka kitu chochote.

***
Utulivu ule ulinishitusha kidogo, lakini joto la mwanamke akiwa pembani yangu lilinizidishia woga, nilipofungua macho yangu na kujiangalia vizuri nikagundua kwamba nilikuwa mtupu na Monalisa.

Haikunichukua muda mrefu kugundua kwamba nilikuwa nimefanya mapenzi na Monalisa tena pembeni mwa barabara, ndani ya gari. Nikashituka sana.
“Umenifanya nini Monalisa?”

“Usiogope kwani hujui tulichokifanya? Naomba unisamehe lakini sikuwa na njia nyingine yoyote ya kukufanya uelewe kwamba nakupenda.”
“Utapata matatizo, nakuonea huruma sana, hatupaswi kufanya hivi.”

“I DON’T CARE PROVIDED I LOVE YOU, I’M READY FOR ANY EVENTUALITY!” (Sijali, maadam nakupenda nipo tayari kwa lolote.) Monalisa aliniambia akionesha kujiamini sana.
Nilimuonea huruma, maana hakujua kama kuna Zamaradi, mwanamke wa ndotoni mwangu ambaye ni hatari sana.
 
SEHEMU YA 10


KIAPO alichoapa Monalisa baada ya mimi na Tyra kuondoka na kumwacha akiwa amesimama nje ya bweni letu kilikuwa ni kulipiza kisasi. Alijihakikishia kwamba adhabu pekee ambayo iliyomfaa Tyra ni kutoka na mimi kimapenzi.

Katika hilo hakujali njia ambayo angetumia, iwe kwa ridhaa yangu mwenyewe au kwa kutumia nguvu za ziada lakini kikubwa alichotaka kilikuwa ni kulala na mimi kimapenzi.

Siku yake iliharibika lakini kwa sababu alishajua bweni nililokuwa ninaishi aliahidi kuniwinda hadi anipate tena siku ile ile. Wakati nilipokuwa nashuka kwenye daladala nikitokea Mwenge, yeye alikuwa kwenye mawindo. Alikuwa akiniwinda.

Nilimkubalia ombi lake la kutoka naye usiku huo nikiwa sielewi kilichokuwa ndani ya moyo wake. Kwa bahati mbaya sana Monalisa alikuwa ameshakula kiapo kwamba lazima anipate.

Mbaya zaidi hakujua matatizo ambayo angeweza kuyapata. Hakujua kwamba mimi ni mwanaume hatari ambaye sikutakiwa kutoka kimapenzi na mwanamke yeyote tofauti na Zamaradi.
Nikiwa sina hili wala lile, nilimwomba niende uani kujisaidia.

Cha kushangaza alitabasamu na kwa hakika niligundua kwamba alifurahishwa na safari yangu ya kwenda msalani, ingawa sikujua sababu.
“Mbona unatabasamu?” nilimuuliza.
“Basi tu!”

“Haya bwana ngoja narudi muda si mrefu!”
“Hata kama ukilala huko huko,” akasema kimizaha huku akicheka.
Nikaondoka nikiwa na mawazo tele kichwani bila kujua sababu ya Monalisa kucheka. Muda mfupi baadaye nikarudi na kujumuika naye mezani. Kitu ambacho kilinishangaza ni uchangamfu wangu wa ghafla.

“Mbona umechangamka sana?” Monalisa aliniuliza kwa sauti tamu huku akinitazama usoni.
“Nimefurahi tu, kwani wewe hujafurahi?” Nilimjibu huku nikiwa sijielewi.
“Nimefurahia pia, napenda siku zote uwe hivi.”
“Nakuahidi.”

Kwa hakika sikuelewa kilichoendelea lakini nilijishangaa sana uchangamfu ule wa ghafla. Kitu cha ajabu, kadiri muda ulivyozidi kwenda ndivyo nilivyozidi kuchangamka, baadaye nikahisi kizunguzungu kabisa.
Hadi tunapanda kwenye gari lake nilikuwa sijielewi, kitu cha mwisho kukumbuka ni kwamba nilihisi usingizi mzito. Nikapotelea usingizini.

***
“Lakini nakuonea sana huruma, hukupaswa kufanya hivi Monalisa. Ni hatari!” nilimwambia Monalisa.
“Nimeshasema kilichonifanya nifanye yote haya ni mapenzi yangu ya dhati si kitu kingine.”
“Monalisa naomba uelewe, pamoja na kwamba umesema ni mapenzi yako ya dhati lakini yanaweza kukusababishia matatizo.”
“Nipo tayari kwa lolote.”

“Lakini umenifanyia nini?”
“Naomba unisamehe, ukweli ni kwamba nilichanganya juisi yako na pombe kali. Naomba unisamehe.”
“Sawa yameisha lakini ninakusikitikia sana.”
“Kwani una nini wewe, mbona umesisitiza sana hilo?”

“Huo ndiyo ukweli Monalisa, umefanya jambo baya na hatari sana.”
“Sasa?”
“Naomba unirudishe bwenini!”
“Hatuwezi kuendelea kidogo?”
“Jambo hili kamwe halitatokea tena, hujanifurahisha Monalisa.”
“Nilishakuomba msamaha nadhani tuondoke.”

Hatukuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuvaa nguo zetu kisha Monalisa akawasha gari na kunirudisha bwenini. Akasimama nje ya jengo la bweni letu tukiwa tunaagana.
“Samahani sana kwa yaliyotokea, usiku mwema,” Monalisa aliniambia.
“Usijali, usiku mwema na wewe pia.”

Nikashuka garini na kupanda ngazi fupi za kuelekea kwenye mlango mkubwa, Monalisa akawasha gari na kuondoka. Nilikuta mlango uko wazi, nikaingia bila kumwamsha Lameck, nikaenda bafuni kuoga kisha nikarudi kitandani kulala. Hofu yangu kubwa ilikuwa ni Zamaradi.

***
Nilishituka sana kumwona Zamaradi akija katika hali aliyokuja nayo. Hakuchana nywele, hakujiremba kama ilivyo kawaida yake, bali uso wake ulikunjamana na ulisoma hasira na kisasi. Ni dhahiri Zamaradi alikuja kwa ajili ya kutoa taarifa mbaya. Nikashituka sana.
“Umefanya nini?” aliuliza Zamaradi kwa sauti ya ukali.
“Nisamehe sikujua.”

“Hukujua nini?”
“Zamaradi hata wewe uliona kwamba alifanya kitendo hicho bila hiari yangu.”
“Najua na ninakuhakikishia lazima nimuadhibu, lazima.”
“Hapana naomba umsamehe Zamaradi, naomba umsamehe mpenzi wangu.”
“Siwezi kufanya hivyo lazima nimshikishe adabu, ili liwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia inayofanana na ya kwake.”

Niliendelea kumshawishi Zamaradi asimdhuru Monalisa lakini alinihakikishia kwamba ni lazima angemfundisha adabu. Niliogopa sana lakini nilikuwa sina uwezo wa kumshawishi zaidi ya pale maana kuna wakati alinitishia kwamba angeweza kunidhuru hata mimi.
“Samahani kwa yote, vipi mbona hujaja na mtoto? Nina hamu sana ya kumwona Mina wangu!” nilisema nikitegemea ningepunguza hasira zake.
Kumbe nilikuwa najidanganya, muda huo huo Zamaradi alitoweka.

***
Siku nzima iliyofuata nilishinda nikiwa mnyonge, kwa kujikongoja jioni nilikwenda mazoezini. Sikumwona Monalisa kama kawaida yake. Nilicheza chini ya kiwango, baada ya mazoezi ambayo kwa hakika sikuyapenda kutokana na taswira ya Zamaradi kuniandama siku hiyo, nilitoka na kwenda bwenini.

Nikiwa naelekea bwenini, nikashangaa kukuta watu wamesimama vikundi vikundi wakiongea. Moyoni nikashituka ingawa sikujua kilichowafanya wajikusanye katika vikundi. Nikasogelea kikundi kimojawapo kisha nikatega sikio kujua kilichokuwa kinazungumzwa.
“Nasikia ameumia sana,” nilimsikia mmoja wa wanafunzi akizungumza.
“Ndiyo ilikuwa ajali mbaya sana.”

“Kwa hiyo amelazwa wapi?”
“Yuko Muhimbili hajitambui kabisa, kwa kweli sijui kama atapona,” mwingine alidakia na kunifanya nishikwe na shauku ya kutaka kujua waliyekuwa wanamzungumzia.
“Mnamzungumzia nani?” nikauliza nikionesha wasiwasi mwingi.
“Usiniambie hujui, Monalisa amepata ajali mbaya sana jioni hii katika Barabara ya Sam Nujoma!”

“Monalisa? Monalisa Malisa?” niliuliza nikitaka kupata uhakika zaidi.
“Ndiye huyo huyo!”
Moyo wangu ukaingiwa ubaridi mkali, nikaogopa. Mimi ndiye chanzo cha yote, nikajihukumu ndani ya nafsi yangu. Sikupata tabu kugundua kwamba ilikuwa ni kazi ya Zamaradi.

NILIPATA mshtuko mkubwa sana, nilimfahamu vyema Zamaradi wangu, asingeweza kuvumilia tukio lile. Moyo wangu uliniuma maana sikuwa tayari kwa kitendo alichonifanyia Monalisa bila idhini yangu.

Uso wangu ulibadilika, nikaonesha wasiwasi mwingi, hivyo ili kukwepa maswali ya watu waliokuwa eneo lile, nikaamua kuondoka haraka. Kwa bahati nzuri kwenye chumba chetu Lameck hakuwepo, hivyo nilijifungia na kuanza kulia mwenyewe.

Niliumia sana, sikulipenda kabisa tukio lile lakini nilijua kabisa Zamaradi aliamua kulipiza kisasi. Nilimaliza siku vibaya, ingawa tangu kulipokucha nilikuwa sina amani kabisa baada ya Zamaradi kunitokea ndotoni na kunihakikishia kwamba angelipa kisasi.

Hata Lameck alipokuja aligundua tofauti niliyokuwa nayo, nilikuwa sina furaha kabisa, haikuwa rahisi kwake kunyamaza wakati aliniona nikiwa katika hali tofauti, hivyo alitaka kujua kilichokuwa kinanitatiza.

“Kaka vipi mbona haupo sawa?” Aliniuliza Lameck.
“Acha tu ndugu yangu, yaani nimechanganyikiwa kabisa.”
“Nini kimetokea?”
“Hujapata taarifa?”

“Ya nini?”
“Monalisa amepata ajali!”
“Monalisa?”
“Ndiyo. Nimepata taarifa nikiwa natoka uwanjani, yaani nimechanganyikiwa kabisa.”
“Ana hali mbaya sana?”

“Yupo Muhimbili, nasikia haongei mpaka jioni hii!”
“Aisee, pole sana rafiki yangu, Mungu atamsaidia, atapona!”
Tulizungumza mengi, usiku nikajilazimisha kulala ingawa ilikuwa shida sana kupata usingizi.

***
Tofauti na matarajio yangu, niliamka asubuhi bila Zamaradi kunitokea usiku wake. Jambo hilo lilinishangaza sana maana nilikuwa nina mashaka kwamba yeye ndiye aliyehusika na ajali ya Monalisa.

Hata hivyo, mwenye ukweli alikuwa ni Monalisa, hivyo mara moja nikajiandaa na kuelekea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa ili niweze kumuona na kuzungumza naye. Niliamini kupitia mazungumzo, ningegundua kama Zamaradi alihusika.
Kwa bahati nzuri nilifika wodini kwake, nikamkuta ameshazinduka. Mwili ulisisimka sana, nikamuonea huruma.

“Pole sana Monalisa!”
“Ahsante Phillip mpenzi wangu!”
“Nini hasa kilitokea?”

“Yaani nashindwa kuelewa kabisa, nilikuwa kwenye mwendo wa kasi, nikashangaa namuona mwanamke mchafu akiwa amebeba mtoto anakatiza mbele yangu akiwa ametoa macho, ghafla nikapata ajali. Sikujua kilichoendelea, nilipozinduka nilijikuta hapa.”

Hapo moyo wangu ukapiga kwa nguvu, nikajua wazi kwamba alikuwa ni Zamaradi akiwa na mtoto wetu Mina. Niliumia sana lakini kwa upande mwingine nilimlaumu Monalisa, maana nilimuonya mapema.

“Ukikutana tena na huyo mwanamke utamkumbuka?”
“Hapana, mpaka sasa nashindwa kuelewa, maana aliponitokea macho yalikuwa mazito na kuona giza. Sitamkumbuka hata kidogo. Eee Mungu wangu nisaidie!” Alitamka maneno hayo Monalisa huku akilia.

Nilijitahidi kumtuliza lakini moyoni nikiujua ukweli. Sikuweza kuvumilia kukaa pale kwa muda mrefu, nilikuwa na uchungu mwingi moyoni, hivyo baada ya muda mfupi nilirudi chuoni huku nikiwa na uhakika kabisa aliyesababisha ajali hiyo ni Zamaradi.

***

Uso wake ulikuwa umekunjamana, ni wazi alikuwa na hasira kali sana na mimi. Kama ilivyokuwa safari iliyopita, alikuja akiwa na nguo chafu huku nywele zikiwa timutimu lakini alikuja na mwanetu Mina.

Zamaradi alikuwa amekasirika sana, alionekana kuwa na maneno mazito aliyotaka kuniambia. Woga ukanizidi na wasiwasi tele moyoni. Nikiwa katika mshangao mkubwa, Zamaradi akanipa mtoto, nami nikampokea kisha nikaanza kucheza naye.
“Naomba unisamehe Zamaradi, najua nimekukosea lakini si kwa kupenda mpenzi wangu.”
“Sitaki kusikia upumbavu wako hapa.”

“Tafadhali nipo chini ya miguu yako, naomba umsaidie Monalisa apone, najua unaweza kufanya kitu chochote ukitaka, lakini naomba umsamehe.”
“Siwezi, tena nataka kukuhakikishia kwamba inawezekana nikamuua kabisa. Siwezi kuvumilia upumbavu kama huu. Kwani wewe huelewi kama mimi nakupenda? Nataka kukuhakikishia kwamba nitamuua Monalisa wako, mpumbavu kabisa!”

“Usifanye hivyo tafadhali mpenzi, hata wewe unafahamu kwamba nakupenda na sina uhusiano wowote mbaya na Monalisa, tafadhali msamehe.”
“Siwezi, siwezi nimesema siwezi, sasa atakula jeuri yake kitandani.”
“Anateseka sana!”

“Ndiyo lengo langu, acha ateseke, tena akicheza nitamuua.”
Nilizungumza mengi sana kumshawishi Zamaradi abadilishe uamuzi wake, lakini hakuonekana kunisikiliza kabisa. Jazba ilikuwa imempanda sana, kwa ilivyoonekana alikerwa sana na kitendo cha Monalisa kutembea na mimi kwani siku zote hakupenda kuchangia mwanaume.

Kila nilipojitahidi kumuomba amsamehe Monalisa, hakuonekana kunielewa kabisa, bado alikuwa na kisasi kikubwa moyoni mwake.
“Nipe mwanangu niondoke,” baadaye alisema kwa ukali akinitazama usoni kwa macho yaleyale mekundu yanayotisha.

“Bado nina hamu naye, huwezi kusubiri kidogo nicheze na mtoto?”
“Phillip nipe mwanangu niondoke, mbona hunielewi?” Alisema Zamaradi kwa ukali zaidi.
Ni sauti hiyo ndiyo iliyonifanya niamini kwamba hakuwa anatania. Nikampa mtoto, kisha muda huo huo akaondoka na kuniacha peke yangu. Hakika nilikuwa na mawazo sana, nilimuonea huruma Monalisa, sikutaka afe lakini hilo halikuwa ndani ya uwezo wangu, mwamuzi alikuwa ni Zamaradi.

***
Asubuhi nilipoamka nilikwenda Muhimbili kumuona Monalisa, vitisho vya Zamaradi viliniogopesha sana. Sikuwa na uhakika wa kumkuta akiwa mzima. Njia nzima nilikuwa mwenye mawazo mengi, nikiwa na mawazo mengi juu ya Monalisa.
Nilipofika Muhimbili, moja kwa moja nilikwenda katika wodi aliyolazwa na kupiga hatua za taratibu hadi kitandani mwake. Nikamkuta Monalisa akiwa amelala, uso wake ukionesha uchungu mwingi.

“Pole sana Monalisa, utapona tu. Mungu atakusaidia!” Nilimwambia Monalisa kwa sauti ya taratibu.
Hakujibu kitu, badala yake mvua ya machozi ikaanza kutiririka machoni mwake. Nikazidi kupatwa na uchungu moyoni
je nini kitaendelea
 
SEHEMU YA 11


NILISISIMKA mwili mzima nikiwa na hofu sana na Monalisa, sikujua ni kwa nini alikuwa akilia, lakini ndani ya moyo wangu nilianza kuhisi kwamba alikuwa na ujumbe mzito aliotaka kunipa.

Nilianza kuhisi kwamba, Zamaradi aliamua kumtokea mwenyewe na kumuonya. Sikutaka jambo hilo litokee hakika, mapigo ya moyo wangu yakaenda kwa kasi ajabu, taratibu nikatoa kitambaa mfukoni mwangu kisha nikaanza kumfuta machozi yake.
“Pole sana Monalisa, najua maumivu unayoyapata, lakini hakuna jinsi, vumilia Mungu atakusaidia.”

“Hapana Phillip, mimi siwezi kupona.”
“Kwa nini Monalisa?”
“Naumwa sana, hali yangu inazidi kubadilika siku hadi siku, yaani sijisikii vizuri. Nitakufa nikikuacha mwanaume ambaye nakupenda kwa moyo wangu wote!”
“Usiseme hivyo tafadhali, ukisema hivyo unaniumiza na mimi. Tafadhali nakuomba sana unyamaze!”

Niliumizwa sana na maneno yake ambayo yalikuwa makali kuliko kawaida, aliposema ananipenda, ndiyo nikazidi kuchanganyikiwa, maana sababu ya yeye kuwa kitandani ni kunipenda!
Sikutaka kukaa muda mrefu pale wodini, maana nilihisi kama nautesa moyo wangu. Nikatafakari kwa muda, nikitamani Zamaradi atokee ili niendelee kumsisitiza amsamehe Monalisa, lakini hilo halikutokea.

“Monalisa hayo ni majaribu tu, tafadhali jikaze, utapona.”
“Lakini ni vigumu kuzoea hii hali, sijui ni kwa nini balaa hili limenipata mimi.”
“Hapo sasa utakuwa unakufuru, ni lazima ukubaliane na kilichotokea. Mwachie Mungu kila kitu, yeye ndiye mwenye uweza na atajua cha kufanya kwa ajili yako.”
“Ahsante kwa kunipa moyo Phillip.”

“Sawa, ugua pole, mimi nakwenda zangu.”
“Ok! Phillip.”
Nikaondoka pale wodini, nikiwa na msongo wa mawazo kichwani, moyo wangu ulikuwa kama umepigwa shoti ya umeme. Niliumia zaidi, maana nilikuwa nafahamu wazi kuwa sababu ya matatizo yale yote ni mimi.

Niliporudi chuoni, sikufanya chochote kwa siku nzima zaidi ya kulala. Hata jioni sikuweza kwenda mazoezini, mwili wangu ulikuwa mzito sana. Nisingeweza kufanya chochote wakati Monalisa alikuwa akiteseka kwa ajili yangu.
Rafiki yangu Lameck alishangazwa sana na mabadiliko yangu ya siku hiyo, sikuwa nimechangamka kama kawaida yangu.
“Phillip una tatizo gani?”
“Nipo sawa, rafiki yangu!”

“Hapana, haupo sawa, lazima kuna tatizo. Kwanza hujaingia kwenye kipindi tangu asubuhi, halafu mazoezini hujaenda. Umebaki chumbani tu siku nzima. Lazima kuna kitu. Hebu niambie una nini rafiki yangu?”
“Niamini mimi Lameck, hakuna tatizo, zaidi ya mambo ya kawaida tu kichwani mwangu!”

“Mficha maradhi, kifo humuumbua, mimi ni kama ndugu yako sasa hivi. Tunaishi pamoja kwa muda mrefu sana, lazima unieleze kama una tatizo!”
“Sina,” nikamjibu kwa kifupi na kugeukia upande mwingine kisha nikajifunika shuka gubigubi.
Sikutaka kuzungumza zaidi, isingekuwa rahisi kumwambia kilichotokea, hiyo ilikuwa siri ya moyo wangu. Nikaamua kulala.

***
Kutokana na kuguswa sana na ajali ya Monalisa, kila siku asubuhi baada ya kuamka ilikuwa lazima niende kwanza Muhimbili kumjulia hali kisha niendelee na ratiba nyigine. Ndivyo nilivyofanya pia asubuhi hiyo.
Nilijiandaa vyema kisha nikatoka na kwenda Muhimbili. Nilimkuta Monalisa akiwa katika hali mbaya sana, sikuweza kuendelea kumwangalia akipumua kwa shida huku machozi yakimtoka.

Nilichokifanya ilikuwa ni kusimama mara moja na kwenda ofisini kwa Dk. Mang’ola ambaye ndiye aliyekuwa akimuhudumia tangu alipofikishwa hospitalini hapo.
“Pole sana kijana,” Dk. Mang’ola aliniambia, nami nikiketi kitini.

“Ahsante sana dokta, hali ya mgonjwa naona si nzuri kabisa, vipi kuna matumaini?”
“Kwa kweli hali yake kwa sasa si nzuri. Unajua mgonjwa amevunjika uti wa mgongo, kwa hiyo amepooza mwili mzima isipokuwa kichwa tu! Jana jioni nilikuwa na mkutano na wazazi wake na ndugu zake wengine tukijadiliana kuhusu hali yake. Wameamua kumpeleka Uingereza kwa matibabu, kama mambo yataenda sawa, huenda kesho wakasafiri.”

“Mungu wangu, Uingereza? Inamaana hapa mmejaribu kila njia mmeshindwa?”
“Kwa kweli haiwezekani kabisa, lazima waende nje kujaribu, ingawa uwezekano wa kupona ni mdogo sana na hata akipona, maisha yake yote yaliyobakia atakuwa kitandani!” Dk. Mang’ola aliniambia.

Moyo wangu uliingiwa na ubaridi mkali, sikuwa na uwezo wa kuendelea kumsikiliza daktari, nilisimama mara moja na kumuaga kisha nikaondoka zangu. Iliniuma sana kuona Monalisa anateseka, huku mimi nikiwa naijua sababu ya mateso yake.

***
Sauti kubwa ya mwanamke akicheka ndiyo iliyonishtua, baadaye nikaona mwanga mkali mbele yangu, ghafla nikaona cheche za moto zikiwaka kwa kasi sehemu niliyokuwa nimekaa.
Kitambo kidogo, kicheko kikapungua na kuisha kabisa. cheche ziliendelea kutoka, kisha nikasikia sauti ya mtoto akilia. Hapo nikajua kila kitu; ni Zamaradi alikuwa amekuja kunitembelea.

“Phillip mpenzi wangu, sikubahatisha kukupenda, nakupenda kwa dhati ya moyo wangu, hivyo siwezi kumruhusu mtu yeyote aniingilie. Sikia...kifupi najua kila kinachoendelea. Huyo mpumbavu wako watahangaika naye sana, lakini hatapona.

“Najua kwamba wanataka kumpeleka Uingereza kwa kuwa wana fedha. Fedha zao si kitu katika mapenzi yangu kwako, Phillip nakuahidi lazima nitamuua Monalisa. Ngoja kwanza ateseke kidogo mpaka siku hasira zangu zitakapotulia kidogo nitamuua akapumzike!”

“Usifanye hivyo Zamaradi tafadhali, nakuomba sana...najua amekosea, lakini ukumbuke kwamba si kwa makusudi, maana hajui yote haya. Msamehe tafadhali,” nikamwambia Zamaradi nikiamini angesikia maneno yangu, lakini ilikuwa kinyume chake.

“Sina cha kuongeza, nakuhakikishia lazima nimfundishe adabu. Tena nakuambia, uwe makini na hao wanawake zako, akitokea mwingine akafanya ujinga kama wa Monalisa, dawa itaendelea kuwa ile ile, kuwaua tu!” Akasema Zamaradi kwa sauti iliyojaa hasira.
“Tafadhali naomba usikilize sauti yangu, nipo chini yako Zamaradi, msamehe...nakuomba sana!”

“Sina msamaha na msaliti, kifo ndiyo adhabu inayomstahili. Jiandae kuona maiti yake, tamaa ndiyo imemponza!” Akasema Zamaradi kwa hasira kisha akatoweka.
Nikabaki natetemeka, huku machozi yakimwagika machoni mwangu.
“Kwa nini Zamaradi hataki kunisikiliza?” Nikajisemea, lakini haikusaidia kitu.
Tayari Zamaradi alishatoweka.
ZAMARADI tafadhali naomba ubadilishe mawazo!” Nilitamka kwa sauti kubwa.
Ghafla nilishtuka. Nilikuwa peke yangu nikiwa natokwa na jasho mwili mzima. Zamaradi alikuwa ameshaondoka, akiniacha na mateso makali. Nilikuwa natetemeka kwa woga, nikihofia kifo cha Monalisa ambaye kama angekufa ni wazi kuwa mimi ndiye chanzo.

“Phillip!” Ilikuwa ni sauti ya Lameck ikiniita.
Sauti yake ilinishtua sana, sikutegemea kama angekuwa macho mpaka muda ule. Nilihofia kwamba inawezekana alinisikia wakati nikibishana na Zamaradi kuhusu Monalisa. Sikutaka kabisa agundue jambo hilo.

“Phillip vipi, una tatizo gani?” Lameck akauliza, baada ya kuona simuitikii.
“Niache tu kaka!”
“Kwani vipi?”
“Nilikuwa kwenye ndoto mbaya.”
“Pole sana.”
“Ahsante.”

Nilipoangalia saa ya ukutani tayari ilikuwa imeshatimia saa 9:30 usiku. Bado kulikuwa na saa mbili na nusu mbele kabla ya kupambazuka. Kwa hakika sikutaka kabisa kifo cha Monalisa.

Sikuwa na kitu kingine zaidi ya kuanza kulia. Nilianza kulia kwa sauti ndogo lakini muda ulivyozidi kwenda ndivyo sauti ya kilio changu ilivyozidi. Lameck akanisikia...
“Phillip nahisi kuna kitu kingine zaidi unanificha.”
“Nini hicho?” Nikamuuliza.

“Kwa nini unalia?”
“Mimeota ndoto mbaya sana, inanitisha na kunifanya niweweseke.”
“Ndoto ni ndoto Phillip, haina uhusiano wowote na matukio ya kweli.”
“Unaweza kusema hivyo kwa sababu haijakutokea wewe, lakini mimi inanitesa sana.”
“Pole, jitahidi ulale. Puuza ndoto mbaya!”
“Ahsante Lameck, sasa nitalala!”

“Ok! Usiku mwema.”
“Ahsante, nawe pia!”
Hapo kidogo nikajitahidi kujikaza na kuishilia usingizini. Hofu yangu kubwa ilikuwa ni Zamaradi kunitokea tena baada ya kupitiwa na usingizi.

***
Nilikuwa wa kwanza kuamka asubuhi hiyo, nikaingia bafuni kuoga kisha nikajiandaa na kwenda kituoni kupanda daladala iliyonifikisha Mwenge ambapo nilipanda daladala ya kwenda Muhimbili.

Niliposhuka katika kituo cha daladala cha Muhimbili nikatembea kwa kasi sana hadi katika wodi aliyokuwa amelazwa Monalisa. Kitu cha kushangaza sikumuona kitandani mwake.

Nikapatwa na wasiwasi, kitu kilichovamia akilini mwangu kwa kasi, ni kwamba huenda alikuwa amekufa. Nikatoka mbio hadi ofisini kwa daktari. Hofu kubwa ilikuwa imetanda mbele yangu. Sikutaka kukutana na taarifa za kifo cha Monalisa.

“Pole sana kijana, Monalisa amesafirishwa alfajiri ya leo kwenda Uingereza, hali yake ilibadilika na kuwa mbaya zaidi, hivyo wazazi wake wakaamua kufanya mpango wa kumuwahisha zaidi!” Dk. Mang’ola aliniambia baada ya kumuuliza alipo Monalisa.
“Ameshapelekwa?”

“Ndiyo!”
“Mungu atamsaidia,” nikajikuta nikitamka maneno hayo.
“Uingereza wana vifaa vizuri zaidi, inawezekana wakajitahidi kuokoa maisha yake. Tuombe Mungu!” Akasema Dk. Mang’ola.

“Sawa dokta, acha mimi nikuache, nakutakia kazi njema.”
“Nawe pia siku njema.”
Nikatoka ofisini kwa dokta na moja kwa moja nikaenda kituoni nilipopanda daladala, safari ya kwenda chuoni ikaanza.

***
Kwa wiki nzima, sikuingia kwenye vipindi, nililala kila siku bwenini nikisingizia ugonjwa, ingawa ukweli niliokuwa nao moyoni ulikuwa mwingine kabisa. Nilikuwa na maumivu juu ya Monalisa.

Baada ya muda huo nikaanza kujizoesha ratiba zangu kama kawaida. Nikawa naingia darasani na kwenda mazoezini jioni kama kawaida. Taratibu kumbukumbu za Monalisa zikaanza kupungua.

Siku moja nikiwa naendelea na mazoezi uwanjani, nilikuwa nikishangazwa sana na jinsi wasichana walivyokuwa wakinishangilia kila ninapochoma mpira kwenye kikapu. Nikawa nawaangalia kwa kuibia, mara macho yangu yakagongana na msichana mmoja mrembo sana.

Moyo wangu ukapasuka, alikuwa mwanamke mrembo kuliko kawaida. Muda wote uliobakia sikuweza kucheza vizuri, akili yangu ilikuwa kwa yule msichana. Baada ya kumaliza mazoezi, nilipotoka nje ya uwanja yule msichana alinifuata mbio.

“Hongera sana Phillip!” Akasema akiachia tabasamu pana.
Moyo wangu ukawa kama umepigwa ganzi. Tabasamu lake likanitetemesha na kuamsha hisia kali za mapenzi ndani ya mwili wangu. Alikuwa mwanamke mzuri kuliko kawaida, sikamsahau kabisa Zamaradi.

“Phillip hongera...” akasema tena, baada ya kuniona nimekaa kimya badala ya kumjibu.
“Nashukuru sana...vipi nimecheza vizuri?”
“Sana.”
“Ahsante kwa pongezi zako, sura yako ni ngeni sana machoni mwangu, bado mgeni au?”
“Nipo muda mrefu na tangu nimesikia sifa zako, kila siku nimekuwa nikihudhuria hapa mazoezini kukuangalia ukicheza.”

“Sifa gani hizo?”
“Wewe hujui? Zaidi ya kucheza pia unavutia sana. Hukupata taarifa kwamba siku ambazo ulikuwa huji uwanjani mashabiki walipungua?”
“Hivyo eeeeh! Sikujua hilo!”
“Ndiyo hivyo sasa.”

“Samahani napenda kujua jina lako!”
“Naitwa Linna.”
“Jina zuri sana, unachukua nini?”
“Computer Science.”
“Mh!”

“Mbona unaguna?”
“Wewe mkali sana, unasoma kozi ngumu namna hiyo, inaonekana ulipasua sana A Level!”
“Kawaida tu!”
“Sasa nataka kwenda, kama vipi tuongozane!”
“Haina shida mimi nimekuja na gari. Unakaa bweni gani?”
“Hall 5.”

“Twende.”
Nikachukua mfuko wangu wenye nguo, kisha nikaingia garini, tukaondoka uwanjani. Nilijitahidi sana kuficha hisia zangu, lakini ukweli ni kwamba hata Linna naye alionesha kunipenda. Alinipeleka mpaka bwenini kwangu.
Tayari giza totoro lilishaanza kuingia. Akaegesha gari pembeni karibu na ngazi za kupandia kwenye lango kuu la kuingia bwenini. Linna akaniomba anibusu wakati wa kuniaga, nikakataa maana nilijua madhara yake.

“Kwani una wasiwasi gani? Si tumeshakubaliana kuwa sisi ni marafiki?”
“Ndiyo, sasa ndiyo unibusu?”
“Mambo ya kizungu hayo!”
“Hapana!”
Nilikataa kwa nguvu zote, lakini ghafla Linna akanivuta na kunibusu kwa nguvu. Nikafungua mlango kwa hasira na kuondoka.

***
“Najua kilichotokea, siwezi kuvumilia, lazima nimfundishe adabu,” alikuwa ni Zamaradi akiniambia kwa ukali.
“Lakini hatujafanya kitu Zamaradi.”
“Kukubusu ni kosa kubwa sana kwangu, halafu mbaya zaidi alifanya ukaidi maana niliona wakati ukimzuia, sasa nitamfanya kinyago!”

Nikashtuka sana, nikaanza kumuonea huruma Linna. Siku zote Zamaradi huwa hana utani katika kauli zake, ni wazi kuwa ilikuwa lazima amfanyie jambo baya. Nikaendelea kumsihi Zamaradi apunguze hasira na abadili mawazo lakini hakunielewa.
Nikajiandaa kupokea taarifa mbaya juu ya Linna.
JE NINI KILIENDELEA
 
SEHEMU YA 12


KILA nilipokumbuka tukio la Monalisa la kupata ajali mbaya na kupooza mwili, tena akiwa amesafirishwa na wazazi wake kupelekwa nchini Uingereza kwa matibabu niliumia sana.

Niliumia kwa sababu nilikuwa najua kila kitu kuhusu ajali yake. Mimi ndiye chanzo, jambo ambalo lilinitesa sana moyoni wangu. Mbaya zaidi ni Zamaradi ambaye kila wakati alinitokea usiku kwenye ndoto na kunieleza ukweli kwamba kamwe hawezi kumsamehe!

Zamaradi alinitisha sana kunieleza kwamba hata kama alikuwa amesafirishwa kwenda nje ya nchi, ni kazi bure maana hawatafanikiwa kumtibu na kupona. Alinihakikishia kuwa lazima atamtoa uhai.

Nikiwa bado sijapona maumivu hayo ambayo yalinisumbua sana, Linna naye akafanya tukio ambalo halikumfurahisha Zamaradi, akanieleza wazi wazi kuwa atamkomesha.
Ilikuwa lazima nichanganyikiwe sana. Usiku huo ukawa mgumu sana kwangu, sikufanikiwa kupata usingizi hata kidogo. Niliona maluweluwe huku matukio ya ajabu yakizunguka kichwani mwangu juu ya Linna.

Namfahamu vizuri sana Zamaradi, huwa haahidi uongo hata mara moja na katika siku zote za maisha yangu na yeye ya kimapenzi, hajawahi kuniahidi ahadi ya uongo. Hilo liliniumiza sana, nilijua lazima kuna jambo baya lilikuwa njiani kumkuta Linna.

Nilichanganyikiwa sana, nikatamani Zamaradi anitokee tena ili niendelee kumuomba msamaha, lakini hilo halikutokea. Niliamka asubuhi nikiwa sijaonana tena na Zamaradi, taa za hatari zikawa zinawaka ubongoni mwangu.

***
Ilikuwa Jumapili, nilipoamka sikutaka kwenda kanisani, kumbukumbu za Zamaradi zikaendelea kunitesa. Nilijihisi kama muuaji wa watu wasio na hatia. Nafsi yangu ilinisuta na hakika sikutaka Linna afe kwa kosa ambalo alilifanya bila kujua.
“Lazima nifanye kitu fulani hapa, Linna anaweza kupata matatizo,” nikawaza kichwani mwangu.

Hata hivyo kwa hakika sikujua ni jambo gani hasa ambalo nilipaswa kulifanya kwa ajili ya kumuokoa Linna. Kichwa changu kikawa kama kimejaa mambo mengi ambayo yalikuwa nje ya uwezo wangu.

“Sijajua...lakini lazima nikutane naye,” nikaendelea kuwaza kichwani mwangu.
Nilichokifanya ni kutoa simu yangu ya mkononi na kubonyeza namba zake. Simu iliita kwa muda mfupi sana, Linna akawa amepokea, akizungumza kwa furaha sana.
“Hello Phillip!”
“Vipi Linna?”

“Poa.”
“Kwa nini jana ulifanya vile?”
“Nilifanyaje?”
“Umesahau mara hii?”
“Ni kuhusu kukubusu?”
“Ndiyo!”

“Mh! Yaani mpaka leo bado unakumbuka kitu hicho hicho jamani? Basi samahani kama nitakuwa nimekuudhi, lakini halikuwa lengo langu kukuchukiza.”
“Unachukulia rahisi sana tatizo hili.”
“Kwa nini?”
“Unavyoongea tu!”

“Kwani ni jambo kubwa kiasi hicho?”
“Sikiliza Linna, hili ni jambo kubwa, nahitaji kuongea na wewe leo jioni. Utakuwa na nafasi tukutane?”
“Hata sasa hivi nipo tayari.”

“Hapana, iwe jioni tafadhali, maana sina muda kwa sasa.”
“Saa ngapi?”
“Tukutane saa 10.00.”
“Unapenda wapi?”
“Udasa Bar.”
“Poa.”

“Usipuuze ni lazima tuongee.”
“Hamna shida Phillip, mtanashati wa chuo, nitakuja.”
“We’ endelea kuchukulia utani, lakini ni kwa faida yako Linna!”
“Faida yangu?”

“Ndiyo!”
“Kivipi?”
“Utajua jioni.”
“Haya tutaonana.”

Tukakata simu zetu nikiwa na mawazo mengi sana, lakini ukweli ni kwamba sikupenda jinsi Linna alivyochukulia utani katika mambo muhimu kwa maisha yake kama yale. Hata hivyo isingekuwa rahisi kumlaumu kwa sababu hakujua alichokuwa akikifanya.

***
Nilifika katika Baa ya Udasa iliyokuwa ndani ya chuo chetu mapema sana. Cha ajabu wakati naingia tu, niliona gari lake limeegeshwa nje. Nikajua wazi kuwa alikuwa amenitangulia kufika.

Nikampigia simu, akanielekeza mahali alipokuwa amekaa. Nikajongea taratibu na kumfuata. Alikuwa amekaa kimya akiendelea kunywa maji ya matunda.
“Karibu Phillip,” akanikaribisha.
“Ahsante, umefika muda mrefu?”
“Tangu nusu saa iliyopita nilikuwa hapa. Ilikuwa lazima niwahi kabla yako.”

“Vizuri.”
Nilitulia kwa muda nikimwangalia na kujiridhisha kweli alikuwa mwanamke mrembo sana. Kwa hakika hakustahili kabisa kufa. Moyo wangu ukaenda mbio, nikashindwa kujua mahali pa kuanzia.

Kwa jinsi ilivyoonekana, Linna alikuwa na shauku sana ya kutaka kujua nilikuwa nataka kumwambia nini. Alikuwa kimya kuliko kawaida, akionesha utayari wa kusikia chochote kutoka kwangu.
Kinywa changu kilikuwa kizito kuongea, nilimwangalia kwa nukta kadhaa bila kutamka chochote. Naye alionekana kuanza kuingiwa na wasiwasi kidogo.

“Linna, kwa nini jana ulifanya vile?” Nilimwuliza nikimwangalia usoni.
“Samahani kwa kukuudhi, najua hukupenda lakini lazima niwe mkweli kwamba, nilifanya vile kwa hisia zangu za ndani kabisa kutoka moyoni.”
“Hisia zipi?”

“Phillip tambua kwamba wewe ni mwanaume mtanashati sana, hakuna mwanamke ambaye atakubali kupata nafasi ya kukaa na wewe sehemu ya peke yenu, akaacha kutamani angalau kupata busu lako. Ndivyo ilivyokuwa kwangu, nilitamani unibusu. Kama nilikukosea naomba unisamehe.”
“Kwa hiyo unataka kusema kwamba unanipenda?”
“Ndiyo!”

“Acha kabisa Linna, mimi sitakiwi kuwa katika uhusiano wa aina hiyo kabisa.”
“Hutakiwi kivipi, kwani wewe hunipendi?” akaniuliza.
Lilikuwa swali gumu sana, nilichukua muda kidogo kumjibu. Ni kweli ndani ya nafsi yangu nilijihisi kumpenda sana Linna, lakini isingewezekana kutokana na masharti magumu ya Zamaradi.

“Elewa tu hivyo.”
“Mh!”
“Usigune, ndiyo ukweli wenyewe ulivyo...halafu, vipi tangu hiyo jana hakuna tukio lolote lililotokea?” Nikamwuliza, lakini nikiogopa sana.
“Tukio, unamaanisha nini?”

“Basi, kama hakuna.”
“Sijakuelewa Phillip, unamaanisha nini?”
“Usijali,” nikamwambia na kubadilisha kabisa maongezi.

Nisingeweza kuongea zaidi ya pale, maana kama baadaye angepatwa na tukio lolote, ingekuwa rahisi kulihusisha na maelezo yangu. Tukaanza kuzungumza mambo tofauti kabisa na yale.
Saa tatu na dakika zake, usiku nikarudi zangu bwenini, lakini bado moyoni mwangu nilikuwa na wasiwasi mwingi. Zamaradi aliendelea kunitesa mawazoni.

***
Ndani ya gari alikuwa msichana mrembo sana, akiendesha gari kwa mwendo wa kasi. Alikuwa akitumia Barabara ya Sam Nujoma akitokea Ubungo. Muziki laini uliendelea kumsindikiza katika safari yake huku kiyoyozi kikimpuliza!

Alipita eneo la Mlimani City kwa kasi sana, mbele kidogo ya kituo hicho akiwa anakaribia kufika katika mzunguko zinapokutana Barabara za Ardhi na Sam Nujoma, akashangaa kumuona mwanamke akiwa amesimama barabarani, mikononi mwake amebeba mtoto.

Akashtuka sana na kupunguza mwendo, akiwa anajaribu kumkwepa akashangaa yule mwanamke anabadilika, wakaonekana wanawake wengi wanaofanana na yule aliyemuona awali, wote walikuwa wanalia, machozi yao yakitoka damu.

Akakata kushoto ili aingie kwenye sheli ya Bonjour, lakini cha kushangaza akiwa anajaribu kukanyaga breki, gari ndiyo likaongeza kasi, kama amekanyaga mafuta! Akaenda kuvaa pampu moja ya mafuta aina ya petroli.

“Puuuuuu....” mlio ukasikika na hapo hapo, moto mkali ukaanza kulipuka.
Gari likaanza kushika moto, msichana huyo akiwa ndani yake. Alipiga kelele bila msaada wowote, magari mengine yaliyokuwa karibu yakatolewa, yeye akiendelea kuteketekea ndani ya gari.

Akajitahidi kufungua mlango na kutoka ili kuinusuru roho yake, akiwa ndiyo anamalizia mguu wa mwisho, akahisi kama kuna mtu anamvuta. Akarudishwa ndani kwa kasi! Akaendelea kuungua!
Sasa hakupiga tena kelele, alikuwa kimya! Msichana huyo mrembo alikuwa ni Linna.

Sauti ya msichana iliendelea kusikika kutoka katikati ya moto kuomba msaada lakini hakuwepo mtu mwenye uwezo wa kumsaidia, kila aliyekuwa karibu alijaribu kuokoa maisha yake. Lilikuwa ni tukio la kusikitisha, wote walimhurumia lakini hawakuwa na cha kufanya zaidi ya kushuhudia akifa.

“Nakufa! Nisaidieni. Nateketea, niokoeni!” alizidi kupiga kelele msichana huyo akiomba msaada.
“Tufanyeje?” mmoja wa wafanyakazi wa kituo alimuuliza mwenzake.
“Tuwapigie simu Zimamoto.”

“Hawa ambao wakifika eneo la tukio wanakuwa hawana maji?”
“Sasa tufanyeje?”
“Mimi nashauri tuwapigie Knight Support au Ultimate Security, hao kidogo ni wepesi na huwa wanaegesha magari yao karibu kabisa na maeneo ya viwanda huku Mwenge.”
“Uamuzi wa busara.”

Wakati wanafikia uamuzi huo bado kituo kilikuwa kikiendelea kuteketea, Linna akiwa tayari amekwishanyamaza kuashiria kabisa kuwa roho yake ilishatoka. Kitendo cha mguu wake kubanwa na moja ya vyuma vya bodi ya gari ndicho kilichosababisha akumbwe na mkasa huo, laiti mguu wake ungeachwa huru angefanikiwa kutoka ndani ya gari lake kabla moto haujawa mkubwa na kuokoa maisha.

“Ultimate Security hapa.”
“Ndiyo, kuna kituo cha mafuta kinateketea.”
“Wapi?”
“Hapa Mwenge karibu kabisa na Mlimani City.”
“Hicho cha kwenye kona ya Chuo Kikuu?”
“Ndiyo.”

“Wewe ni nani?”
“Mfanyakazi wa kituo.”
“Nani atalipia gharama ya kuzima?”
“Nyinyi njooni tu mzime, bosi wetu atalipa.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo.”
“Basi tunawasiliana na wenzetu walioko Mwenge, Coca Cola.”

***
Bahati nzuri dereva wa gari la Zimamoto lililomilikiwa na Kampuni ya Ultimate Security alikuwa njiani kuelekea maeneo ya Ubungo, simu yake ilipoita aliipokea na kupewa maelekezo ya kwenda haraka eneo la tukio ili kujaribu kuokoa mali na maisha ya watu. Akabadilisha gia na kuwasha king’ora kilichokuwa kimezimwa na kuongeza kasi.

“Nilishauona huo moto, moshi wake ni mkubwa mno, niko umbali wa kama mita mia mbili tu kufika eneo la tukio.”
“Uzimeni haraka, watatulipa baada ya kazi.”
“Sawa.”

Dakika moja na nusu baadaye kwa sababu hapakuwa na msongamano wa magari barabarani, gari la Zimamoto lilifika na watu waliokuwa wamesimama mbali kuanza kushuhudia maji yakiruka na moto kuzimwa ndani ya dakika kumi. Gari la Linna lilikuwa limeteketea kabisa, yeye mwenye akiwa amelala nje ya gari hilo mguu mmoja ukiwa umebanwa.

Alilala kifudifudi juu ya ardhi, hakuna sehemu ya mwili wake mgongoni kuanzia kichwani hadi miguuni iliyobaki bila kuungua, walichokifanya askari wa Zimamoto ni kumbeba haraka na kumpakia ndani ya gari lao kisha kuondoka kwa kasi kuelekea hospitali wakiwa hawajui ni ipi iliyokuwa karibu na kama mtu waliyekuwa wakijaribu kuokoa maisha yake alikuwa hai au la.

“Wapi?” Dereva aliuliza.
“Tutawahi Muhimbili kweli?”
“Siyo rahisi.”
“Sasa tutaelekea wapi?”

“Tujaribu hospitali ya jeshi Lugalo.”
“Ni mzima huyu kweli?”
“Hakuna mwenye uhakika, wewe twende tu madaktari watajua baada ya kumpima.”
Gari lilizidi kuendeshwa kwa kasi huku king’ora kikilia na kufanya magari mengine yaliyokuwa barabarani yapishe, dakika tano baadaye gari hilo liliegeshwa Idara ya Mapokezi Hospitali ya Lugalo na wauguzi wakafika na machela yao.

“Mungu wangu.” Mmoja wa wauguzi alisahau maadili ya kazi yake na kujikuta akitamka neno hilo baada ya kuushuhudia mwili wa Linna.
Haraka wauguzi wakavaa mipira mikononi mwao na kuushusha mwili huo ambao kila sehemu waliyogusa ilibanduka ngozi, hakika Linna alikuwa ameungua vya kutosha, hakuna sijui ni maneno gani yangetamkwa kuelezea vizuri hali hiyo zaidi ya mtu kushuhudia mwenyewe. Akashushwa na kulazwa juu ya machela kisha kukimbizwa chumba cha daktari.

“She is still breathing, but this is a severe case of third degree burn!” (Bado anapumua, lakini ni mgonjwa aliyeungua vibaya kabisa, kiwango cha daraja la tatu..) Aliongea daktari wa kike akiwa amezungukwa na vijana walioonekana kuwa wanafunzi wa udaktari.

“What is the prognosis in cases like this one?” (Nafasi ya kupona ikoje kwa wagonjwa kama huyu?) Mmoja wa wanafunzi madaktari aliuliza.
“To be honest the prognosis is very poor, may be until a miracle happens!” (Kusema ukweli nafasi ya kupona ni ndogo, labda utokee muujiza.) Daktari aliongea na kuwaamuru wauguzi wamkimbize haraka sana mgonjwa chumba cha wagonjwa mahututi.

Linna akabebwa na kupandishwa juu ya machela akiwa bado hajitambui.
Kilichofanyika chumba cha wagonjwa mahututi ni kasi ya kumuongezea maji mfululizo ili kuziba pengo la maji yaliyopotea kwa kuungua, mashine ya hewa ya oksijeni ilifungwa puani na mdomoni kwake.

Yote haya yalifanyika kujaribu kuokoa maisha ya msichana huyu ambaye mpaka wakati huo alikuwa hajatambulika, kwani sura yake ilikuwa imeharibika vibaya na hata gari lake pia liliteketea kiasi cha namba zake kutoonekana. Madaktari hawakujali hilo, cha muhimu kwao ilikuwa ni kumponyesha mgonjwa, mengine yangefuata baadaye.

“Will she survive?” (Atanusurika?) Dk. Mafuru, bingwa wa upasuaji kwenye Hospitali ya Lugalo aliwauliza wenzake kwenye kikao cha kumjadili mgonjwa huyo.

“Not possible, even if she does, she will never be the same again, the deformities caused by the scars will be too bad.” (Siyo rahisi, hata akinusurika, hatakuwa yule yule tena, vilema vitakavyosababishwa na makovu vitakuwa vibaya mno.)
“Kama wazazi wake ni matajiri, wanaweza kumpeleka kwenye hospitali kubwa nje ya nchi ambako atafanyiwa upasuaji wa marekebisho, si chini ya operesheni hamsini au sitini hivi ndiyo zinaweza zikamsaidia, tofauti na hapo atakuwa na maisha magumu sana.

Sijui kama anaweza kuona tena.” Dk. Matilda aliyempokea Linna kwa mara ya kwanza aliongea.
“Nawashauri kwanza tushughulikie kuokoa maisha yake mengine yatafuata, ila kwa kweli ameungua, sijawahi kuona mtu aliyeungua kiwango hiki tangu nianze kazi hii miaka thelathini iliyopita.”

“Tunaendelea na matibabu gani sasa?”
“Drip za Normal saline kwa kasi na prophylactic anti-biotics, kuzuia maambukizi.”
“Kama ipi hiyo anti-biotic?”
“Urgumentin.”
“Haya jamani tuwasiliane baadaye.”
Kikao kikamalizika na madaktari wakasambaa kwenda kuendelea na kazi nyingine za kuhudumia wagonjwa.

***
“Mh!”
“Mbona unaguna?”
“Sijamsikia Linna akirudi.”
“Hata mimi au tulipitiwa na usingizi?”
“Hebu ngoja nikaangalie chumbani kwake, haiwezekani awe hajarudi mpaka saa hizi na hata kutupigia simu kutoa taarifa kwamba yuko na rafiki zake mahali fulani.” Mama yake Linna alisema na kukurupuka kitandani kisha kutembea moja kwa moja na kushusha ngazi hadi chini kilikokuwa chumba cha Linna, mlango ulikuwa wazi akaufungua na kuingia ndani.

“Mh!” Akaguna tena baada ya kukuta binti yake hayupo, saa ya mezani ilisomeka saa 6:20. Haikuwa kawaida ya Linna kukaa nje mpaka muda huo bila kutoa taarifa kwa mama yake ambaye pia alikuwa rafiki yake mkubwa, mama akapandisha ngazi moyo wake ukiwa umejawa na hofu, hisia zilimtuma kuanza kuamini kulikuwa na tatizo lililompata mwanaye baada ya kuusikia kabisa mwili wake hauko sawa.

“Hayupo.” Alimwambia mume wake.
“Mh! Hebu piga simu yake.” Mzee alisema pia akianza kuingiwa na wasiwasi moyoni mwake.
Simu ya Linna ilipopigwa ilionekana imezimwa, wakajaribu kupigwa kwa rafiki zake ambao mara nyingi alikuwa nao usiku jibu likawa wote walikuwa nyumbani kwao wamelala na hawakujua mahali Linna alikokuwa. Wasiwasi ukazidi kuongezeka.
“Sasa atakuwa wapi?”
“Hata sijui.”

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 13



Phillip alikuwa akimuota msichana mrembo na baadaye yeye na msichana huyo walifunga ndoa ndotoni na kuzaa mtoto mmoja. Kwenye ulimwengu halisi, hivi sasa Phillip ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako wasichana wanahangaika kumpata bila mafanikio.

Msichana wa ndotoni (Zamaradi) alishamuonya kwamba kila mwanamke atakayekuwa na uhusiano naye atamdhuru. Jambo hili ni siri yake, kamwe asidiriki kuwaeleza wasichana waliomtaka kimapenzi kuwa yeye ni mume wa jini mkali na mwenye wivu.

Wasichana wakidhani Phillip alikuwa mvulana mwoga, wakamfanyia njama na kumfanya ashiriki mambo ya mapenzi bila ridhaa yake. Kilichowapata wasichana hao ni ajali za gari; wa kwanza alikuwa ni Monalisa ambaye akiendesha gari kwa kasi, alishitukia mwanamke mwenye mtoto akisimama mbele yake.

Wakati akijaribu kumkwepa gari lake lilipinduka, akaumia ubongo na uti wa mgongo hivi sasa amepooza na wazazi wake wanahangaika kutafuta matibabu sehemu mbalimbali duniani.
Linna msichana wa pili naye akamshawishi Phillip na kumbusu kwa nguvu, muda mfupi tu baadaye akiendesha gari lake kuelekea nyumbani, mwanamke akaonekana katikati ya barabara, wakati akimkwepa gari liliacha njia na kuingia kwenye kituo cha mafuta na kugonga pampu ya mafuta ya petroli, moto mkubwa ukalipuka na kumuunguza vibaya.

Zimamoto walifanikiwa kuuzima moto na kumtoa Linna akiwa katika hali mbaya, wakampeleka hospitali ambako madaktari wamempokea wakiwa na uhakika kabisa asingepona. Wazazi wake walipogundua usiku kwamba Linna hayuko ndani ya nyumba, walipiga simu yake bila mafanikio, wasiwasi mwingi ukawaingia zaidi hasa baada ya kuwapigia hata rafiki zake ambao pia walithibitisha kutomuona. Hivi sasa wamechanganyikiwa, hawajui cha kufanya.
Je, nini kinaendelea? SONGA NAYO…

Wazazi walikuwa wamechanganyikiwa kabisa, Linna ndiye mtoto pekee aliyebaki, tegemeo lao na mrithi wa utajiri wao baada ya kaka yake kufariki miaka michache iliyopita. Hawakuwa tayari kumpoteza, kulifikiria jambo hilo tu peke yake kulimfanya mama yake Linna aanze kulia na mume wake kumpigapiga mgongoni akimfariji na kumwambia asiwe na wasiwasi Linna angerejea.

“Kweli?”
“Usiwe na shaka.”
“Moyo wangu unaniambia mwanangu yupo katika matatizo.”
“Hizo ni hisia tu mke wangu.”
Waliendelea kumsubiri bila mafanikio, kila walipoisikia muungurumo wa gari nje ya nyumba yao, walisimama na kuchungulia wakiamini Linna alikuwa amerejea, haikuwa hivyo, magari mengi yaliyopita yalikuwa ni ya majirani. Walishangaa siku hiyo jinsi masikio yao yalivyokuwa na uwezo mkubwa wa kusikia kuliko siku nyingine.

Mpaka saa kumi na mbili asubuhi Linna alikuwa hajarejea, walishapiga simu yake bila kufanikiwa kumpata na walikuwa hawajasinzia kabisa. Baba akainuka kitandani na kuchukua rimoti ya televisheni iliyokuwa juu ya meza ndogo kando mwa kitanda, akaibonyeza akiwa ameilenga runinga na kuiwasha.

“Hii ni taarifa ya habari kutoka Shirika la Utangazaji la Taifa, msomaji wako ni mimi Leodgar Masome, …
Dar es Salaam; Ajali mbaya ya moto imetokea jijini Dar es Salaam baada ya gari dogo kuacha njia na kugonga kituo cha mafuta cha Bonjour, dereva wa gari hilo ambaye amejeruhiwa vibaya kwa moto na hali yake ni mbaya amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili… tuungane na mwandishi wetu Brighton Masalu aliyefika eneo la tukio…

Mama yake Linna aliyekuwa amejilaza kitandani, aliposikia maneno hayo alikurupuka na kuisogelea runinga, yeye na mume wake wakaanza kuangalia namna moto ulivyokuwa ukiwaka huku gari la zimamoto likiendelea kuzima na baadaye majeruhi alivyotolewa ndani ya gari ambalo lilikuwa limebadilika kabisa na kuwa na rangi nyeusi.

“Anaweza kuwa Linna huyu?” Mama yake aliuliza.
“Hapana!”
“Hata kama ni yeye, naomba hii isiwe ukweli, iwe ndoto!”
“Hawezi kuwa yeye, gari lile si lake.”
“Ile inaonekana kama Peugeot, siyo BMW!”
“Kabisa.”

“Afadhali, angekuwa yeye sijui ingekuwaje.”
“Lakini atakuwa wapi, hata kama yuko kwa mpenzi wake ni bora arudi nyumbani, anatutesa sisi wazazi wake.”
“Ni kweli kabisa.” Mama alijibu akihema kwa nguvu, mapigo yake ya moyo yalikuwa yamebadilika kabisa.

Waliendelea kusubiri huku wakiwasiliana na ndugu, jamaa na marafiki ili kuona kama Linna alikuwa amefika kwao lakini kote hawakufanikiwa. Hii iliendelea kuwajaza wasiwasi, hatimaye ilipofika saa sita mchana wakafikia uamuzi wa kuondoka nyumbani kwenda kituo cha kati cha polisi ambako waliulizia kama kuna ajali yoyote ilikuwa imetokea, wakaelezwa ni ya moto peke yake iliyohusisha gari kwenye kituo cha mafuta.
“Huyo majeruhi yuko hospitali gani?”

“Muhimbili wodi ya wagonjwa mahututi.”
“Ni vyema twende tukamuone, huwezi kujua anaweza kuwa ni mtoto wetu.”
“Ushindwe katika jina la Yesu!” Mama yake Linna aliongea akimuangalia mume wake.
“Nisamehe mpenzi wangu, ni mawazo tu.”

Wakaingia ndani ya gari na kwenda moja kwa moja hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako gari liliegeshwa na wakashuka kisha kutembea kwa haraka hadi chumba cha wagonjwa mahututi, ingawa muda wa kuona wagonjwa ulikuwa umeisha, baba yake Linna alitumia kufahamika kwake kumshawishi muuguzi angalau awaruhusu waingie kumuona majeruhi wa moto.

“Baba nawapa dakika mbili tu!”
“Zinatosha sana mwanangu.”
“Asante binti.” Mama alisema na wote wakaingia haraka na kupelekwa mpaka kwenye kitanda alicholazwa Linna, wakaanza kumwangalia kuanzia kichwani hadi miguuni, nywele zote zilikuwa zimeungua na ngozi ya mwili ilikuwa imebabuka na kuufanya uwe nyama iliyo wazi.

“Ni yeye?” Baba yake aliuliza.
“Hapana, huyu siye, afadhali!” Mama aliongea akitabasamu, kitendo cha kukuta mtu aliyeteketea ndani ya gari si Linna kilimfurahisha na kumfanya atamani Linna arejee nyumbani.
“Lakini urefu ni sawa.”
“Hata kama ni sawa, huyu si Linna.”

Walipotoka hapo walirejea nyumbani, mioyoni wakidhani wangeweza kumkuta Linna amekwisharejea lakini haikuwa hivyo, mpaka saa moja jioni. Wakazidi kuchanganyikiwa, usiku wa siku hiyo pia hawakulala mpaka asubuhi ambapo walifikia uamuzi wa kwenda kituo cha polisi wakitaka kujua kama kweli gari lililoungua halikuwa la Linna.

Walipofika kituoni walijitambulisha, bahati nzuri baba yake Linna alifahamika na watu wengi, hivyo haikuwa kazi ngumu kumuona mkuu wa kituo na kumweleza tatizo lake. Yeye ndiye aliyewachukua na kuwapeleka nyuma ya kituo ambako gari lilikuwa limeegeshwa, kwa jinsi lilivyokuwa limeteketea haikuwa rahisi hata kidogo kulitambua.
“Ni lenyewe?” Mkuu wa kituo aliwauliza.

“Siyo.” Mama yake Linna aliitikia.
“Lakini mimi nina wasiwasi kidogo, muundo ndiyo wenyewe, nashauri nikimbie nyumbani mara moja nikachukue faili la gari la Linna ili tupate namba za chesisi yake, hiyo ndiyo itatupa uhakika kama kweli gari hii siyo ya mtoto wetu.”
“Baba Linna, ya nini yote hayo? Au unataka mwanangu ndiyo awe ameteketea kwenye gari hii?”

“Siyo hivyo mke wangu, moyo wangu umeingiwa wasiwasi, twende!” Aliongea mzee huyo na kwa pamoja wakamuaga mkuu wa kituo na kuingia ndani ya gari lao, safari kuelekea nyumbani iliwachukua dakika kumi na tano wakawa wameshafika, kuegesha na kupandisha juu kwenye chumba cha Linna ambako walifungua kabati na kulipata faili, haraka wakashuka hadi kwenye gari na kuondoka tena kuelekea kituoni.

Mkuu wa kituo aliomba msaada wa maaskari ambao walifungua sehemu ya mbele ya gari na kukuta injini ikiwa imeungua lakini si kiasi cha maandishi ya kuchimbwa kwenye injini kushindwa kusomeka, haikuchukua muda mrefu namba za chesisi zikapatikana, wote wakasogeza vichwa vyao karibu na kuanza kusoma namba moja baada ya nyingine.

“Uuuuwi! Maskini mwanangu Linna! Uuuuuwi!” Ilikuwa ni sauti ya mama yake akilia baada ya kugundua namba ya chesisi iliyoonekana ni ya gari la Linna, ilimaanisha mtoto wao ndiye alikuwa ameteketea ndani ya moto, yalikuwa ni maumivu makali yasiyopimika, kama mkuki wa moto kuuchoma moyo wa mtu akiwa hai.

Mama akaanguka chini na kuanza kugalagala akilia, kazi ya mume wake ikawa ni kumbembeleza mpaka alipotulia ndipo kwa msaada wa polisi akasaidiwa kutembea mpaka kwenye gari, wakaondoka pamoja mpaka hospitali na kupelekwa tena kwenye kitanda cha mgonjwa.

“Linna! Linna! Linna!” Mama aliita lakini Linna hakuitika, bado hakuwa na fahamu, alipumua kwa kutumia mashine ya oksijeni iliyokuwa kando ya kitanda huku dripu nyingi zikiingia mwilini mwake kupitia mirija.
“Mama hawezi kukusikia, tangu amekuja hapa hana fahamu, ni ajali mbaya sana ya moto kuliko zote ambazo nimewahi kushuhudia.”

“Mwanangu atapona daktari?” Baba yake Linna aliuliza, naye akijifuta machozi, haikuwa rahisi kujizuia kwa jinsi hali ilivyokuwa.
“Ni kazi ya Mungu, tunajitahidi sana kufanya kazi yetu ambayo ni kutibu, lakini mponyaji ni Mungu.” Daktari huyo aliongea.
“Bila shaka wewe ni Dk. Mafuru?”
“Ni kweli.”

“Nakufahamu sana.”
“Hata mimi nawafahamu sana wazee wangu, sikujua tu kwamba huyu ni Linna, si rahisi kumtambua.”
“Tusaidie daktari, angalau mtoto wetu apone.”
“Mungu atasaidia, ila hata kama akipona, ukweli ni kwamba hawezi kuwa Linna yule yule tena, roho inaniuma sana, lakini sina jinsi. Sijui ni kwa nini Mungu huwa anaruhusu matukio kama haya?”

“Sisi tunamshukuru Mungu, najua ni kwa nini ameruhusu jambo hili litokee.” Baba yake Linna aliongea kwa huzuni.
Mama yake Linna alipiga magoti kando ya kitanda na kuendelea kulia huku akimuomba Mungu amsaidie mwanaye apone, muda huo baba yake Linna alikuwa akiwasiliana na uongozi wa Chuo Kikuu kuwapa taarifa za kupatikana kwa mtoto wao akiwa katika hali mbaya. Taarifa hizo zikabandikwa kwenye ubao wa matangazo na kuwataka wanafunzi wenye nafasi wafike haraka Hospitali ya Muhimbili kumuona mgonjwa, tayari ilikuwa saa tisa na nusu alasiri.

***
Baada ya chakula cha mchana, Phillip alikuwa katikati ya mawazo mengi chumbani kwake, akiyapitia mambo yaliyokuwa yakitokea maishani mwake, kuanzia kwa Monalisa aliyekuwa amepooza na sasa alikuwa hajui ni wapi alipokuwa Linna baada ya kumlazimisha busu mara ya mwisho walipoonana. Hisia zilimtuma kufikiri lazima kuna jambo lililokuwa limetokea, Zamaradi alikuwa amemtenda jambo, pengine kumuua na maiti yake kupotea.

“Acha niende chuoni labda nitakuta amerejea, namuomba Mungu asaidie ili asije akawa ameingia kwenye matatizo.” Aliwaza Phillip na kunyanyuka kitandani kisha kuchukua begi lenye kompyuta yake na kuanza kutembea taratibu kuelekea darasani.
Alishangazwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika mbele ya jengo la utawala, wakiwa katika vikundi vidogo vidogo wakijadili jambo huku wengine wakiwa kwenye ubao wa matangazo, wote wakisoma jambo.

Akawahi hapo na kupenya katikati ya watu mpaka akaufikia ubao na kuanza kusoma, muda wote alipokuwa akisoma machozi yalikuwa yakimbubujika kwani alielewa kilichotendeka, hasira dhidi ya Zamaradi zikampanda akiamini kabisa alikuwa akiwadhuru watu wasio na hatia.

“No! Something has to be done! I can’t let her continue tormenting innocent being.” (Hapana! Jambo fulani linahijika kufanyika, siwezi kumwacha aendelee kutesa viumbe wasio na hatia.) Alijisemea moyoni mwake Phillip na kwenda kando ambako alianza kulia kama jinsi wanafunzi wengine wengi walivyokuwa wakibubujikwa na machozi.

Haukupita muda mrefu sana mabasi matatu yakafika na wanafunzi wakapanda, wote walikuwa wakielekea Hospitali ya Muhimbili kumuona mwanafunzi mwenzao, Phillip akawa miongoni mwao ili akamuone Linna. Moyoni alikuwa na maumivu makali mno, sababu alielewa kila kitu kilichokuwa kikiendelea na alihisi kuwajibika.


Aliketi kiti cha nyuma kabisa dirishani, akiendelea kububujikwa na machozi, kando yake akiwepo Tyra, msichana mrembo ambaye pia alikuwa katika ligi ya kumpata. Mkono wa Tyra ulikuwa begani kwa Phillip akijaribu kumbembeleza asilie, kwake nafasi hiyo ilikuwa muhimu na alitaka kuitumia vyema kumuonyesha Phillip kwamba ni kiasi gani alimjali.

“Tyra.”
“Bee!”
“Toa mkono begani, usinipapase, utapata matatizo!”

“Matatizo gani? Kama ni mapaparazi wa chuo mimi siwaogopi, siwezi kukuacha uendelee kulia, najua matukio ya Monalisa na Linna yamekuumiza sana. Usisikitike, Mungu hakuwapangia wao, pengine hii ilikuwa ni riziki yangu…”
“Tyra!” Phillip aliita akimuangalia kwa jicho la huruma, alielewa ambacho kingefuata kama msichana huyo angeendelea na mpango wake, yeye pia angekutwa na matatizo kama yaliyowapata wenzake.

“Bee!”
“Nisikilize mimi, ninajua ninachokisema, tafadhali usinilazimishe nizungumze mambo mengine ambayo mimi sipendi kuyaongea.”
“Mambo gani Phillip?”
“Basi tu, wewe toa tu mkono.” Phillip aliongea akiutoa mkono wa Tyra begani kwake, wanafunzi wengine waliokuwa jirani waliangaliana, Tyra msichana mzuri na mwenye maringo kuliko mwingine yeyote katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alijisikia vibaya mno.

“Haya bwana, sitakufuatilia tena, hii ni mara ya mwisho.”
“Nashukuru.”
Tayari basi walilopanda likawa linakata kona kutoka Barabara ya Umoja wa Mataifa na kuingia Barabara ya Malik kuelekea Muhimbili, hawakuongea tena kitu chochote mpaka wanashuka Idara ya Mapokezi. Walishangazwa na umati wa wanafunzi waliowakuta, kumbe wengi walitangulia hospitalini kutoka mabwenini, zaidi ya wanafunzi elfu nne walikuwa wamejaa mbele ya jengo la mapokezi, walikuwa wamezuiliwa kwenda chumba cha wagonjwa mahututi kumuona Linna, baadhi walikuwa wakilia.

Aliposhuka ndani ya basi, Phillip hakutaka kuongea na mtu tena, alichagua eneo la pembeni karibu kabisa na Idara ya Maabara na kuketi kwenye msingi wa nyumba , akainamisha kichwa chake chini na kuendelea kulia, huku mkononi akiwa ameshikilia kijiti na kuandika juu ya ardhi; I love you, don’t die! maneno ya Kiingereza yaliyomaanisha; Nakupenda, usife.

Akayasoma maneno hayo mara nyingi na kuzama ndani yake, kwa mara ya kwanza akaamini moyoni mwake alikuwa akimpenda sana Linna, bila Zamaradi kuwepo maishani mwake na akapewa nafasi ya kuchagua mwanamke wa kuoa, asingemchagua mwingine yeyote isipokuwa yeye, sasa alikuwa ameungua na moto, Zamaradi alikuwa amemteketeza, kwa hali aliyokuwa nayo lazima angekufa, moyo ukamuuma.

“Haya tukusanyikeni! Wanafunzi wote tukusanyikeni, daktari anataka kuongea na sisi” Ilikuwa ni sauti ya Jason Mbwambo, rais wa serikali ya wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Sauti hiyo ndiyo iliyomgutua Phillip na kumuondoa katika dimbwi la mawazo alilokuwa amezama ndani yake, akanyanyuka taratibu na kujikongoja mpaka mahali ambako wanafunzi wote walikuwa wakijikusanya, minong’ono ikaanza kusambaa kwamba Linna alikuwa amefariki dunia, taarifa hizo zilimuumiza sana, akabaki kimya katikati ya wanafunzi wenzake akimsubiri daktari aje atangaze. Dakika ishirini baadaye daktari alifika na kusimama mbele ya wanafunzi.

“Habari zenu!”
“Nzuri shikamoo daktari.”
“Marahaba, naitwa Dk. Mafuru, mimi ndiye ninashughulika na tatizo la mwanafunzi mwenzenu, rafiki yenu Linna, nimejitokeza hapa kuwapeni habari kwamba, hali yake si nzuri, ameungua sehemu kubwa sana ya mwili wake. Tunajitahidi kadiri ya uwezo wetu kuokoa maisha yake, hatuwezi kusema atapona kwa sasa, ila tuendeleeni kumuombea! Hizo ndiyo habari nilizotaka kuwapatia. Kama kuna swali mnaweza kuniuliza.” Alimaliza daktari na kuanza kuwaangalia wanafunzi, mkono mmoja ulikuwa hewani.

“Naitwa Phillip, sina swali ila nilikuwa naomba nikamuone mgonjwa.”
“Suala la kumuona nyinyi nyote ni gumu, mgonjwa anahitaji utulivu, hivi sasa hana uwezo wa kuzungumza, hivyo kuwaruhusu kwa wingi wenu muingie itakuwa ni sawa na kumsumbua mgonjwa, lakini tunaweza kuruhusu viongozi wenu wawawakilishe.”
“Sawa daktari!” Wanafunzi wengi waliitikia.

Phillip hakuwa miongoni mwa viongozi wa serikali ya wanafunzi, lakini alishinikiza mpaka kujikuta yuko kati ya wanafunzi saba walioruhusiwa kuongozana na daktari hadi ndani ya chumba cha wagonjwa mahututi, hakuamini alichokiona Linna alipoondolewa kifaa kilichomfunika juu yake kukiwa na mashuka na kubaki wazi, Phillip alilia, hakuwa Linna bali kiumbe kingine tu kilichochunwa ngozi na moto.

“No! Huyu siyo Linna, nionyesheni mwingine.” Aliongea akijiunga na wanafunzi wenzake wote kulia, ilikuwa picha mbaya mno kuishuhudia.
Haikuwezekana kabisa kubaki ndani ya chumba hicho, wote baada ya kupiga magoti pembeni mwa kitanda na kusali walinyanyuka, wakawapa pole wazazi kisha kutoka hadi nje ambako walishindwa hata kuwasilimulia wenzao walichokishuhudia. Dakika ishirini baadaye walipanda kwenye mabasi na safari kurejea chuo kikuu ikaanza, huko Phillip hakuwa na la kufanya zaidi ya kushuka na kwenda moja kwa moja bwenini kwake, akajifungia na kuanza kulia.

Baadaye fahamu zilimpotea, ulikuwa ni usingizi mzito uliomchukua, akamshuhudia Zamaradi pamoja na mwanaye akimwijia, uso wake ukiwa na tabasamu, mkononi akiwa ameshikilia boksi na kuliweka juu ya meza. Phillip alikurupuka kitandani na kuanza kumfokea akilalamika ni kwanini alikuwa akitesa watu bila huruma kiasi hicho, Zamaradi hakuwa na la kusema zaidi ya sentensi “Samahani, nakupenda mno, niko tayari kufanya lolote kukulinda mume wangu.”

Aliposema maneno hayo Zamaradi alipotea, Phillip akafumbua macho yake na kushuhudia juu ya meza kukiwa na boksi kama alivyoona ndotoni. Taratibu akajinyanyua kitandani kulisogelea boksi hilo, alipofungua ndani yake alikuta kuna mkufu, saa ya dhahabu na bulungutu la dola za Kimarekani.

Pia kulikuwa na karatasi ndogo ambayo juu yake iliandikwa maneno “I am sorry!” kwa kutumia damu ambayo Phillip hakuelewa ilikuwa ni ya binadamu au mnyama gani. Taratibu akaanza kuhesabu noti za dola mia alizozikuta, zikatimia elfu kumi! Moyo wake ukaanza kushuka, hasira aliyokuwa nayo ikaanza kupungua hasa baada ya kuivaa saa mkononi pamoja na mkufu shingoni, tabasamu likarejea.

***
Hali ya Monalisa ilikuwa mbaya kupita kiasi, juhudi zote za madaktari zilionekana kugonga mwamba lakini wazazi wake hawakuwa tayari kukata tamaa. Ni kweli alikuwa amepooza na asingenyanyuka kitandani siku zote za maisha yake kwa maelezo ambayo madaktari waliyatoa lakini bado wazazi hao walitaka kujaribu njia nyingine, fahamu zilishamrejea binti huyo na alikuwa akilia akiwaomba wazazi wake wasihangaike sana.

“Baba!”
“Naam!”
“Msihangaike, mliyoyafanya yanatosha, bila shaka huu ndiyo ulitakiwa kuwa mwisho wangu. Jambo moja tu naomba mnifanyie, nitafurahi sana.”
“Jambo gani mwanangu?”
“Nahitaji kuongea na mwanafunzi mmoja chuo kikuu anaitwa Phillip.”

JE NINI KITAENDELEA
 
SEHEMU YA 14




“I think this is beyond our control, we cant save the life of this victim, she has severe bruises and burns which penetrated into her body. She must be referred,”
(Nafikiri hii ni nje ya uwezo wetu, hatuwezi kuokoa maisha ya mwathirika huyu, ana malengelenge na majeraha ya moto yaliyopenya hadi ndani ya mwili wake. Lazima tumtafutie rufaa) aliongea Daktari Mafuru wakati akijadiliana na Bodi ya Madaktari wa Muhimbili juu ya hali ya mgonjwa yule.

Hospitali ya Muhimbili ndiyo iliyokuwa kubwa zaidi nchini Tanzania, hivyo kumtafutia rufaa kulimaanisha kumpeleka nje ya nchi kwenye hospitali bora zaidi. Wakati madaktari wakijadiliana, baba na mama yake Linna nao walikuwa wakifikiria suala hilo hilo.
“Tangu tumlete mwanangu hapa hospitali sioni mabadiliko yoyote, mume wangu tusipochukua uamuzi wa haraka tutampoteza mtoto huku tunashuhudia.”

“Ni kweli mke wangu, lazima tufanye jambo haraka. Hata kama tutalazimika kuuza kila tulichonacho ilimradi mtoto wetu akatibiwe mimi niko tayari,” aliongea baba yake Linna huku akijifuta machozi. Japokuwa alikuwa ni mwanaume na baba wa familia, hali ya mwanaye ilimfanya ashindwe kuyazuia machozi. Ikawa kila mmoja anajifuta machozi kutokana na hali aliyokuwa nayo Linna.

Muda mfupi baadaye waliitwa kwenye chumba cha Daktari Mafuru na kuelezwa kile madaktari walichoona kinafaa.
“Tumependekeza mkajaribu kwenye Hospitali ya Johannesburg Trauma Centre, pale huduma zao ni za hali ya juu hasa kwa wagonjwa waliopatwa na majanga kama hili lililomkumba binti yenu. Mungu atawasaidia na naamini atapona ingawa hataweza kuwa kama alivyokuwa kabla ya kupatwa na matatizo.

Bila kupoteza muda, madaktari wa Muhimbili wakiongozwa na Dokta Mafuru walianza kufanya mawasiliano na wenzao wa Johannesburg Trauma Centre. Baba yake Linna alishughulikia taratibu za uhamiaji, akafuatilia vibali ubalozini na hatimaye kila kitu kikawa tayari.

Kwa kutumia ndege maalum iliyokodiwa, Linna akasafirishwa hadi jijini Johannesburg sambamba na wazazi wake. Ndege iliyowabeba ilipotua nchini humo, tayari gari la wagonjwa (ambulance) kutoka kwenye hospitali ile lilikuwa likiwasubiri uwanja wa ndege. Linna akashushwa kwenye ndege na kuingizwa moja kwa moja kwenye ambulance, safari ya hospitalini ikaanza.

Alipofikishwa Johannesburg Trauma Center, alipitishwa mpaka chumba cha wagonjwa mahututi ambapo alianza kutibiwa haraka. Kitu cha kwanza ilikuwa ni kumuunganisha na mashine ya kusukuma hewa ya Oksijeni iliyomsaidia kupumua.

“She has been dehydrated! Her body is running a severe shortage of water and mineral salt. We need to hydrate her first before we proceed.”
(Amepungukiwa na maji mwilini. Mwili wake una upungufu mkubwa wa maji na madini ya chumvi. Tunapaswa kumuongezea kwanza kabla ya kuendelea) Daktari Amstrong Reymann, mkuu wa kitengo cha majanga ya moto hospitalini pale alikuwa akitoa maelekezo kwa madaktari wenzake. Muda mfupi baadaye Linna akatundikiwa dripu ya maji na chumvi, huku akipakwa dawa za kuua wadudu (Antibiotics) mwili mzima.

Kwa kipindi hicho chote, Linna alikuwa amelala usingizi wa kifo, akiwa haelewi chochote kilichokuwa kinaendelea kwenye ulimwengu wa kawaida.
Baada ya dripu karibu sita kutiririka kwa kasi mishipani mwa Linna, mapigo yake ya moyo yalianza kuongezeka taratibu. Madaktari wakawa wanapishana kwenye kitanda chake kuhakikisha mgonjwa huyo anapona.

Huduma bora za kiwango cha juu ilikuwa ni miongoni mwa sifa zilizoitangaza hospitali ile dunia nzima. Kila aliyewahi kutibiwa pale, hakuacha kusifia huduma bora kabisa za afya. Hali ile iliwapa matumaini wazazi wa Linna, wakapata moyo kuwa mtoto wao anaweza kupona ingawa hawakujua kama atarudia hali yake kama ya zamani.

Baada ya mapigo ya moyo, kiwango cha maji na chumvi mwilini kuanza kuridhisha, Dokta Amstrong Reymann alishauriana na madaktari wenzake namna ya kuifanyia marekebisho ngozi ya Linna iliyokuwa imeharibika vibaya mwili mzima.
“We need to implant her body with the modern skin grafting method, at least we can minimize the damage.”

(Tunatakiwa kupandikiza ngozi mpya juu ya mwili wake kwa kutumia mbinu ya kisasa ya upandikizwaji wa ngozi, angalau tutapunguza madhara mwilini mwake)
Kilichofuatia ilikuwa ni utekelezaji lakini kilichowakwamisha ikawa ni mahali pa kuipata ngozi ambayo ingetumika kwa zoezi lile.

Mwili wote wa Linna ulikuwa hautamaniki na hakukuwa na sehemu ambayo ngozi yake haikuungua. Baada ya madaktari kukwama, waliwaita wazazi wake na kuwaeleza hali halisi. Suluhisho pekee lililoonekana kufaa ilikuwa ni wazazi wake kukubali kupimwa ngozi zao na kama zingeendana na mtoto wao, wangekatwa ili kumsaidia Linna.

Waliingizwa maabara ambapo vipimo kadhaa vya ngozi vilichukuliwa. Majibu yalipotoka, wote walionekana kuendana na mtoto wao, hivyo zoezi ambalo lilifuatia lilikuwa ni kukata sehemu ya ngozi miilini mwao na kumpandikiza Linna. Wakaambiwa wakasubiri maelekezo nje.
“Mmh! Unajua mke wangu mi naogopa sana. Niliwahi kusikia kuwa wakitaka kukutoa ngozi wanakata makalio.”

“Baba Linna nawe, huachi woga wako wa kitoto. Hata kama ingekuwa usoni, si unamtolea mwanao? Au unataka afe?”
“Basi mke wangu, nilitaka kukuchangamsha kidogo kwani ulikuwa umepooza sana,” aliongea Baba Linna wakati wakisubiri maelekezo ya daktari.

Alichokizungumza baba yake Linna kilikuwa kweli kwani daktari Amstrong alipowaita ofisini kwake aliwaeleza kuwa kama watakubali, ngozi ya kwenye makalio yao ndiyo itakayokatwa kwa ajili ya kuipandikiza kwenye mwili wa Linna. Waliangaliana machoni kwa muda kisha wakatabasamu, kwa pamoja wakatingisha vichwa vyao kuonesha kuwa wako tayari.

Kilichofuatia ikawa ni kuingizwa chumba cha upasuaji, mmoja baada ya mwingine. Wakakatwa ngozi kisha Linna akaanza kufanyiwa ‘skin grafting’. Baada ya baba yake kumaliza kufanyiwa zoezi lile, mama yake naye aliingizwa maabara. Matibabu kwa Linna yaliendelea na angalau akaanza kuonesha matumaini ya kupona ingawa bado alikuwa hajarejewa na fahamu zake.

Licha ya wote kujitolea ngozi kwa ajili ya mtoto wao, bado haikutosha kuufunika mwili wote wa Linna. Ikabidi taratibu zifanyike za kuwaita ndugu zao wengine waliokuwa Tanzania kwa ajili ya kwenda kujitolea kuokoa maisha ya Linna.

Ndugu saba wa ukoo wa akina Linna wakasafirishwa mpaka Afrika Kusini. Walipoenda kupimwa damu na ngozi zao, watano kati yao walionekana kuendana na Linna. Wakaingizwa maabara na kufanyiwa kama wenzao. Angalau ngozi ikatosha kufunika maeneo yote muhimu.
Madaktari walihakikisha kuwa ngozi waliyoibandika mwilini mwa Linna inajishikiza vizuri na kuungana na mwili wake. Wakawa wanampa dawa nyingi za kuua wadudu na kulainisha ngozi.

Hilo lilifanikiwa kwani mwezi mmoja tangu zoezi lile lifanyike, hatimaye Linna alirejewa na fahamu zake na kufumbua macho kwa mara ya kwanza. Tofauti na alivyokuwa awali kabla hajapatwa na ajali ile mbaya, upasuaji wa kupandikiza ngozi ulimfanya abadilike kwa kila kitu. Hakuwa Linna yule wa zamani, binti mrembo mwenye tabasamu pana muda wote. Alikuwa mtu mwingine tofauti kabisa, hali iliyomliza mno mama yake.

Uso ulikuwa na alama nyingi za mishono, kichwa hakikuwa na nywele hata moja. Mwili mzima ulikuwa na viraka kama nguo iliyopelekwa kwa fundi mara nyingi. Hata hivyo wote walimshukuru Mungu kwa miujiza aliyoifanya kwani hakuna ambaye alikuwa na matumaini ya Linna kufumbua macho yake tena.
Siku ya kwanza tangu Linna arejewe na fahamu ilipita, wazazi wake wakawa bado hawajamwambia nini hasa kilichomsibu. Kumbukumbu zake zilikuwa zikirejea taratibu sana, kiasi kwamba hakukumbuka nini kilichomtokea mpaka akawa pale.

“Lakini kwani hapa ni wapi? Mbona hamtaki kuniambia ukweli?”
Baba na mama yake walitazamana kwa muda kama wanaoulizana wamwambie au la. Wakapeana ishara ambayo waliielewa wenyewe kisha mama yake akaanza kumweleza.
“Hapa ni hospitali mwanangu, pole kwa yote yaliyokupata. Tunamshukuru Mungu kwa kukulinda mpaka leo.”

“Kwani nini kilinipata mpaka nikaletwa hapa?” Alizidi kuhoji Linna lakini hakuna aliyemjibu.
“Nataka kwenda ‘toilet’!”
“Utaweza kusimama kweli, ngoja tumwambie nesi aje atusaidie kukuinua.”
“Mbona naweza kuinuka mwenyewe,” Linna aliongea huku akijivuta pale kitandani na kusimama.

Kwa kuwa alishatolewa dripu na ile mashine ya kusukuma Oksijeni aliyokuwa amefungiwa, haikumuwia vigumu kusimama. Mama yake akamsaidia kushuka kitandani na wakamshikilia huku na huku, wakampeleka chooni.

Wakati wanaelekea chooni, walipofika sehemu iliyokuwa na vioo vikubwa ukutani, Linna alisimama kwa muda. Akawa ni kama anajishangaa kupitia vile vioo kwani tangu alipopatwa na masaibu yale, hakuwahi kujiangalia jinsi alivyo.

“Yule ni nani?” Alinyoosha kidole kujionesha mwenyewe kwenye kioo. Baba na mama yake walitazamana tena, machozi yakawa yanawalengalenga. Mama yake alimkumbatia na kumwambia kuwa yule aliyekuwa anamuulizia ni yeye mwenyewe.

“Mbona nimebadilika hivi? Noo! Siyo mimi, labda ni mtu mwingine,” aliongea Linna huku akianza kulia. Alikuwa amebadilika mno. Ilibidi wazazi wake wafanye kazi ya ziada mpaka akatulia na kukubaliana na matokeo.

Walimfikisha msalani, akamaliza haja zake kisha wakamrudisha wodini. Alipofika tena eneo lile lenye vioo vikubwa, alizidi kujishangaa huku safari hii akishindwa kujizuia kulia.
“Mi nafikiri tukamuite daktari kwa ajili ya kumjenga upya kisaikolojia ili akubaliane na hali halisi, vinginevyo atapata shida sana kuyakubali mabadiliko makubwa aliyonayo.”

“Ni sawa, lakini kabla ya kumuita daktari hata sisi wenyewe tunaweza kumsaidia. Nafikiri huu ni muda muafaka wa kumueleza nini kilichompata mpaka akawa hivi.”
“Unafikiri itasaidia?”
“Yaah! Itasaidia sana.”

Baada ya kuteta pembeni kwa muda mfupi, baba na mama Linna walirejea kwenye kitanda alichokuwa amelala mtoto wao aliyekuwa anaendelea kulia kwa uchungu, wakaanza kumbembeleza na kumweleza kila kitu kilichomtokea. Ni hapo ndipo kumbukumbu zake zilipomrudia vizuri. Alikumbuka siku aliyopata ajali mbaya kisha gari lake kulipuka baada ya kugonga pampu ya mafuta.

“Mamaa nakufa! Niokoeee!” Alipiga kelele Linna kumbukumbu za jinsi ajali ilivyotokea zilipomrudia.
“Tulia Linna, mshukuru Mungu kwamba mpaka muda huu uko hai,” aliongea mama yake huku akimshika mwanaye na kumtuliza pale kitandani.

“Mamaa, nilimuona mwanamke akivuka barabara akiwa amembeba mtoto, nilipojaribu kumkwepa ndiyo gari likanishinda,” aliongea Linna huku akitetemeka mwili mzima. Zilikuwa ni kumbukumbu mbaya ambazo ama kwa hakika zilimfanya atie huruma.
Maneno yale aliyoyasema kuwa alimuona mwanamke akivuka barabara akiwa amembeba mtoto, yaliwafanya wazazi wa Linna kuanza kuhusinisha ajali ya mtoto wao na ya mwanafunzi mwenzake, Monalisa.

“Mbona Monalisa na yeye alipopata ajali alisema aliona mwanamke akivuka barabara akiwa amembeba mtoto?”
“Lazima kuna jambo hapa! Siyo bure.”
“Inawezekana kuna siri nzito iliyojificha nyuma ya pazia. Mimi si mwepesi wa kuamini nguvu za kishirikina, lakini katika hili nahisi zinahusika.”

“Tumwachie Mungu, cha msingi mtoto wetu ameanza kupona.”
Daktari Amstrong aliingia wodini na kukuta mama na baba Linna wanambembeleza mtoto wao. Alitambua matatizo ya kisaikolojia yanayoambatana na tatizo kama lile lililokuwa limemsibu Linna. Aliwaomba wazazi wake wamfuate ofisini kwa ajili ya maelekezo zaidi juu ya tiba ya Linna.

“Japokuwa mgonjwa amerejewa na fahamu, bado tuna kazi kubwa ya kuurekebisha mwili wake. Hii ni hatua ya awali tu kwani kuna zaidi ya oparesheni nyingine 50 ambazo inabidi tumfanyie ili angalau kurejesha mwonekano wake wa awali.”
“Oparesheni hamsini? Zote hizo za nini?”
“Bado tunahitaji kurekebisha viungo kama macho, pua, midomo, masikio na vingine vingi, ajali ya moto ilimharibu kabisa.

***
Hali ya Monalisa ilizidi kuwa mbaya licha ya kusafirishwa hadi nchini Uingereza. Kauli ya mwisho aliyoitoa ilikuwa ni kuwaomba wazazi wake wamkutanishe na Phillip kabla hajafa.
Wazazi wake walimhakikishia kuwa watatimiza ombi lake. Kilichofuatia baada ya hapo ikawa ni baba yake Monalisa kusafiri hadi jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumfuata Phillip.

Alipowasili, alienda mpaka kwenye uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuomba kuonana na Phillip.
“Mimi ni baba yake Monalisa! Amenituma nije kuonana na wewe na kukufikishia ujumbe kuwa anahitaji kuonana na wewe.”
“Sasa atanionaje wakati yuko hospitali, tena Uingereza?”
“Usiwe na wasiwasi, familia yangu itakugharamia usafiri na malazi, cha msingi ni utayari wako.”

“Mimi niko tayari mzee wangu, hata sasa hivi!””Ok, safi kijana! Sasa jiandae, ngoja mimi nifuatilie taratibu zote za vibali vya usafiri. Naomba ukapige ‘passport’ na unipe kitambulisho chako, kesho mambo yote yatakuwa tayari,” aliongea baba Monalisa kisha akaagana na Phillip.

Baada ya kuachana naye, alitamani Zamaradi amtokee na kumuombea tena msamaha Monalisa kwani kwa hali ilivyokuwa, uwezekano wa kupona ulikuwa mdogo. Phillip alibaki na msongo mkubwa wa mawazo juu ya hali ya Monalisa. Aliumia kuona mtu asiye na hatia akiangamia kwa sababu ya wivu wa Zamaradi.

Alimuomba Mungu wake ampe ujasiri kwenye safari ile ngumu ya kwenda kuonana na Monalisa. Alijikuta machozi yakimlengalenga.
Ndege ya Shirika la British Airways ilikuwa ikiiacha ardhi ya Tanzania na kupaa kuelekea jijini London, Uingereza. Phillip na baba yake Monalisa walikuwa ni miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya ndege ile. Hakuna aliyemsemesha mwenzake japo walikaa siti zilizokaribiana.

Masaa machache baadaye, ndege ile ilikuwa ikitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heathrow jijini London. Abiria wote waliteremka, Phillip akiwa miongoni mwao sambamba na baba yake Monalisa.
Hawakuwa na muda wa kupoteza. Waliunganisha moja kwa moja mpaka hospitali. Walipofika, baba yake Monalisa alimuomba Phillip amsubiri sehemu ya mapokezi kwa ajili ya kwenda kumuandaa mgonjwa.

Katika hali ambayo hakuitegemea, Phillip alishtuka kumuona baba yake Monalisa akitoka wodini huku amejiziba uso wake kwa kitambaa. Alipomchunguza vizuri aligundua kuwa alikuwa akilia.
“Mungu wangu! Nini tena?” aliongea Phillip na kuinuka kwa kasi kumfuata baba Monalisa.
“Mzee kwani vipi?”

“Hatunaye tena! Monalisa ametangulia mbele za haki?”
“Niniii?” Phillip akiwa katika hali ya kutoamini kile alichokisikia, alishangaa mwanamke wa makamo akitoka wodi ile ile huku akilia na kuja kumkumbatia baba yake Monalisa. Alimtambua kuwa ni mama yake Monalisa.

“Pigo kubwa kiasi gani? Yaani safari yote kutoka Dar es Salaam kumbe nakuja kuiona maiti yako? Kwa nini usingesubiri japo nikuone mara ya mwisho Monalisa! Eeeh Mungu, mpumzishe kwa amani!” aliongea Phillip huku akilia kilio cha kwikwi. Hakuna aliyekuwa na uwezo wa kumtuliza mwenzake, ikawa ni maombolezo wakati mwili wa Monalisa ukitolewa wodini na kupelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

je nini kiliendelea
 
SEHEMU YA 15


Lilikuwa ni tukio la kusikitisha mno, Phillip alilia kuzidi hata wazazi wa Monalisa. Moyoni mwake aligundua wazi kuwa hata yeye alimpenda msichana huyo kupita kiasi. Lakini sasa alikuwa amekufa kabla hawajaongea chochote, safari yake kuja Uingereza haikuwa na matunda. Alimlilia Monalisa kwa nguvu zake zote, hasa alipokumbuka namna walivyoishi vizuri chuoni.

Hasira zake zote zilielekezwa kwa Zamaradi, alimchukia, tena sana. Hakutaka tena kuwa naye kwa sababu alikuwa muuaji, aliyemuua Monalisa bila hatia na kumjeruhi Linna kwa moto ambaye pia Phillip aliamini, kwa hali aliyokuwa nayo, asingeweza kupona. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kufikiria namna ambayo angeweza kujinasua kwa mwanamke huyo hatari.

“Nataka kuishi maisha ya ukweli, nataka kuishi maisha halisi, sitaki tena maisha ya chini ya maji, lakini nitajitenganisha nayo vipi? Zamaradi ataniua,” Phillip alijiuliza bila kupata jibu.

Taratibu za kuusafirisha mwili wa Monalisa kutoka Uingereza zilishughulikiwa na Watanzania waishio nchini humo kwa kushirikiana na ubalozi wao, wakati huo Phillip akiwa amechukuliwa chumba kwenye Hoteli ya Conrad ambako pia wazazi wa Monalisa waliishi.

Hakuwa na jingine la kufanya akiwa chumbani isipokuwa kulia, hakulala wala kula chochote mpaka siku iliyofuata ambapo walipanda ndege na kusafiri watatu na mwili wa Monalisa hadi uwanja wa ndege, Dar es Salaam.

Maelfu ya watu walikuwepo uwanjani, wengi wakiwa ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, marafiki na majirani wa familia ya kina Monalisa maeneo ya Upanga. Vilio vilisikika kwa mbali, wanafunzi wakimlilia Monalisa. Alipotoka nje ya uwanja, Phillip alikumbatiwa na Tyra ambaye alimchukua hadi kwenye maegesho ya magari, akafungua mlango na kumpakia.

Baadaye msafara mrefu wa magari uliondoka uwanjani kuelekea Upanga, Phillip na Tyra wakiwa peke yao ndani ya gari, muda wote Tyra akimfariji na kumwambia asijali kwa yaliyotokea. Kwake kifo cha Monalisa kilimuumiza lakini pia ilikuwa nafasi ya yeye kumpata Phillip kwa urahisi hasa baada ya Linna kuungua vibaya kwa moto, alihisi Phillip alikuwa amemaanishwa kwa ajili yake.

“Usilie Phillip.”
“Sawa lakini inaniuma.”
“Najua, ulikuwa unampenda sana Monalisa na pia Linna.”
“Siyo hivyo, ananiuma kwa sababu amekufa akiwa bado kijana sana. Isitoshe ninajua kilichosababisha kifo chake.”

“Si ni ajali au kuna kitu kingine?”
“Siwezi kukuambia, niache tu nilie.”
“Usiumie sana, mimi nipo, nitakufariji.”
“Sawa. Una habari gani za Linna?”

“Hali yake bado ni mbaya, amefanyiwa tena oparesheni nyingine jana. Ameharibika sana sura, havutii tena, sidhani kama kuna mtu atakuja kumpenda Linna kabisa.”
“Hayo anayajua Mungu, hujafa hujaumbika. Pia yeye halikuwa kosa lake, najua kilichosababisha akaungua kwa moto.”

“Ni nini? Maana nasikia maneno yanasambaa kwamba kuna mkono wa mtu, eti walimuona mwanamke mwenye mtoto katikati ya barabara kabla ya ajali kutokea.”
Phillip hakujibu kitu tena, hakuwa tayari kujadiliana juu ya Zamaradi.

Gari likazidi kusonga mbele mpaka wakafika nyumbani kwa kina Monalisa maeneo ya Upanga, ambako pia kulikuwa na mamia ya watu wakisubiri. Ulikuwa ni msiba mkubwa tena wa kifahari uliojaza watu wote maarufu na matajiri sababu baba yake Monalisa alikuwa miongoni mwao.

“Naweza kubaki humu humu ndani ya gari?” Phillip alimuuliza Tyra.
“Hakuna tatizo, tunaweza kubaki tu humu humu ndani mpaka baadaye.”
“Hauna safari yoyote?”
“Sina.”

Phillip alilaza kiti naye kujilaza akiwa amefumba macho. Mawazoni aliendelea kumfikiria Monalisa, akahamia kwa Linna na baadaye kuendelea na Zamaradi. Roho ilimuuma sana hasa alipogundua kwamba hata Tyra pia kama angediriki kumshawishi au kumlazimisha kufanya tendo la mapenzi, pia angepatwa na ajali mbaya na hata kufa. Hapo Phillip akafumbua macho na kumuangalia Tyra.

“Mbona unaniangalia kwa jicho hilo?”
“Nakusikitikia.”
“Kwa nini?”
“Tyra!”
“Bee!”

“Naomba tu uniache, usije ukajaribu kunilazimisha kuwa mpenzi wako, utapata matatizo.”
“Matatizo gani?”
“Huoni yaliyowakuta wenzako?”
“Toka hapa… Unataka kunitia woga? Hakuna chochote, hizi ni ajali za kawaida, usitake kujichukulia umaarufu kwamba wewe ndiye umezisababisha.”

“Sijazisababisha mimi lakini yupo aliyezisababisha.”
“Nani?”
“Siwezi kukutajia ila fuata maneno yangu.”
“Sitaki.”
“Shauri yako.”

Hivyo ndivyo ilivyokuwa, wote wawili walilala ndani ya gari, saa kumi na moja alfajiri, Phillip akiwa katikati ya usingizi alishitukia mwili wake unapapaswa, mwanzoni alidhani ni ndoto kwani hakutambua mahali alipokuwa lakini akili yake ilipokaa sawa, tayari Tyra alishamfungua zipu ya suruali yake na kuzitoa sehemu zake za siri nje.

“Tyra! Utakufa,” alisema Phillip kwa sauti huku akinyanyuka.
“Nakupenda Phillip, wewe ni haki yangu ndiyo maana akina Monalisa na Linna wamenipisha. Tafadhali nipe haki yangu,” aliongea Tyra kwa sauti ya upole uso wake ukiwa umejawa na aibu.

“Haiwezekani, nakupenda mno ndiyo maana nakataa.”
Tyra hakukubali, akaanza kulia huku Phillip akimuangalia kwa jicho la huruma, kwani alielewa ambacho kingefuata kama angeruhusu jambo hilo litendeke. Walishinda msibani Phillip akihuzunika kwa kifo cha Monalisa, huku Tyra akihuzunikia kitendo cha Phillip kumnyima penzi.

“Unaweza kunipeleka bwenini nikabadili nguo?” Phillip alimwambia Tyra ilipotimia saa kumi jioni.
“Hakuna shida.”
“Twende basi.”

Wakaondoka mpaka chuo kikuu ambako Phillip alishuka na wote wawili wakapandisha hadi ghorofa ya tatu kilipokuwa chumba chake, katika hali ambayo hakuitarajia, Phillip alibadilisha mawazo na kuamua Tyra aondoke ili yeye apumzike sababu alisikia usingizi, tena alikuwa mkali wakati akiongea maneno hayo.
“Nikufuate baadaye?”
“Nitakuja mwenyewe.”

Tyra hakuwa na la kufanya isipokuwa kushusha ngazi hadi kwenye gari lake ambako alipanda, kuwasha na kuondoka kwa kasi kuelekea Upanga, akiwa amepanga kupitia njia ya Ubungo, Manzese, Magomeni, Faya na baadaye kuingia Upanga msibani kuungana na wanafunzi wenzake.

***
Zamaradi aliyashuhudia yote yaliyotokea ndani ya gari na hasira kali kumpanda, ilikuwa ni zamu ya Tyra kufa, tena alidhamiria kumuua pale pale ambapo ajali ingetokea. Baada ya hapo wabaya wake wote wangekuwa wamekwisha. Phillip akiwa usingizini alimtokea na kumpa taarifa ya jambo alilokuwa anakwenda kulifanya, akamsihi asifanye hivyo badala yake amsamehe Tyra.

“Tena ukizidi kunizuia hata wewe nitakuua.”
“Usifanye hivyo, hawana hatia, ni hisia za kimapenzi zinawasumbua, cha muhimu ni kwamba mimi nina msimamo.”
“Haiwezekani. Lazima Tyra afe.”

Tyra aliendesha gari lake kwa kasi akiwa hajui Zamaradi alikuwa akimsubiri kwa hamu kubwa kwenye taa za kuongozea magari za Faya. Kabla hajakata kona kuelekea Upanga, alipanga kuzipasua tairi zake zote za mbele na kisha kulipindua gari mara tano na hatimaye ligongane na gari jingine, huo ndio uwe mwisho wa Tyra.
Alishuhudia gari likishuka maeneo ya Magomeni kuelekea Jangwani, akajiandaa kwa ajili ya kazi.
Jini Zamaradi, mke wa Phillip katika ulimwengu usioonekana amedhamiria kuwaua wasichana watatu (Tyra, Monalisa na Linna) ambao ni wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako pia Phillip anasoma. Hakuna anayejua siri ya Phillip kuwa ni mume wa mtu kwenye ulimwengu usiooonekana, wasichana hao wanamuona ni mvulana mzuri na wanapanga kila mbinu ili waweze kumpata kimapenzi, hapo ndipo wakakutana na hasira ya Zamaradi.

Kwanza alikuwa ni Monalisa, akamsababishia ajali mbaya ya gari iliyosababisha msichana huyo kupooza baada ya kuumia ubongo. Hivi sasa ameaga dunia na kurejeshwa nchini kutoka Uingereza kwa mazishi.

Wa pili alikuwa Linna ambaye pia Zamaradi alimsababishia ajali mbaya ya gari iliyomfanya msichana huyo kuungua vibaya ndani ya gari lake alipogonga pampu ya mafuta ya petroli kwenye kituo cha Bonjour kilichoko njia panda ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam karibu na eneo liitwalo Mlimani City.

Hivi sasa msichana huyu aliyeungua vibaya mwili wake yupo nchini Afrika Kusini akifanyiwa upasuaji kurekebisha mwili wake, sura imebadilika kabisa kwa sababu ya moto na Zamaradi anafurahia jambo hilo lakini Phillip anaumizwa sana kwani anajua kinachoendelea.

Hawa wakiwa na hali hizo, Tyra pamoja na maonyo yote aliyopewa na Phillip anamfungua kijana huyo zipu ya suruali yake kwa lengo la kufanya naye mapenzi ndani ya gari lake, jambo hili lilimuudhi Zamaradi ambaye yupo kwenye taa za kuendeshea magari za Faya akimsubiri Tyra afike, apasue tairi za mbele za gari lake kisha kulipindua, huo ndiyo uwe mwisho wa msichana huyo mrembo.

Tyra yupo maeneo ya Jangwani kwenye Barabara ya Morogoro, amebakiza mita chache tu afike Faya ambako jini Zamaradi anamsubiri kwa hamu kubwa akiwa amedhamiria kuing’oa roho yake bila huruma.
Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

“He is so handsome, I can’t resist him.” (Ni mzuri mno siwezi kujizuia nisimpende.) Tyra aliwaza akiwa ndani ya gari lake dogo aina ya Volkswagen New Model, muziki laini ukiporomoshwa na Celine Dion kupitia kwenye spika zilizoko kwenye mlango.

Hakika msichana huyu alikuwa na kila kitu maishani mwake, kuanzia sura, umbile na utajiri wa wazazi wake. Simu yake haikutulia, wanaume wakimpigia simu kumtaka mapenzi na wote aliwakatalia, hakuwa na mpenzi kabisa ndani na nje ya Tanzania baada ya kuachana na mpenzi wake wa kwanza miaka mitano kabla, sasa alimtaka Phillip kwa gharama yoyote.

Kwa kuwatazama watu hawa wawili na historia za maisha yao, utajiri wa familia zao, Basi msichana kama Tyra hakutakiwa kabisa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Phillip hata kama alikuwa na sura nzuri kiasi gani, lakini sasa alikuwa amenasa, akili yake haikufanya kazi sawasawa, taswira ya Phillip ilionekana kichwani mwake kila alikokwenda, hakuwa na nafuu yoyote hata alipolala usingizi, Phillip alionekana katika ndoto.

Alishangazwa na umati mkubwa wa watu waliokusanyika kwenye viwanja vya Jangwani huku wengine wengi wakizidi kumiminika kuelekea kwenye viwanja hivyo, bila kutarajia akajikuta akishusha kioo cha gari lake na kuanza kusikiliza spika zikitangaza kwa sauti ya juu kutoka kwenye viwanja hivyo, mguu wake wa kulia ukahama kulia na kuja katikati, gari likapunguza mwendo.

Najua mnayo masumbuko mengi maishani mwenu, wengine mna kila kitu lakini bado mnateseka, Yesu anawaita ili aje awatue mizigo yenu. Imetosha kusumbuka, iwe kwa magonjwa au maumivu ya moyo sababu kuna watu wamekutenda vibaya, Mungu wetu analijua hilo na sasa anataka kukuweka huru… Njoo kwake leo, hutajuta…

Tyra aliyasikia maneno hayo kupitia masikio yake yote mawili, bila kupanga akakata kona kuelekea kwenye viwanja hivyo, hata siku moja hakuwahi kufika hapo kusikiliza neno. Hakuwa mtu wa kanisa sana, ni kweli alimwamini Mungu na alikuwa Mkristo lakini si mhudhuriaji wa ibada, siku zote alikuwa mtu wa starehe na kuhudhuria kumbi za starehe huku akiwacheka wanafunzi wenzake walioonekana wacha Mungu, akiwaita wanafiki.

Aliegesha gari lake kando, akashuka na kujichanganya katikati ya maelfu ya watu waliokuwa wamekusanyika kwenye viwanja hivyo kumsikiliza Mhubiri wa Neno la Mungu, Mchungaji Moses Lubala kutoka Kanisa la Word Alive la jijini Dar es Salaam aliyekuwa akiendesha mkutano katika viwanja hivyo.

Tyra alisimama na kuendelea kusikiliza mafundisho ya Mchungaji huyo, akiwataka watu wote kugeuka na kuacha njia zao mbaya, kwamba Yesu alikuwa amekaribia kurudi kuja kutoa hukumu ya kutupwa katika ziwa la moto, maneno hayo yakaingia moyoni mwa Tyra moja kwa moja, akiwa amefumba macho akaanza kuyapitia upya maisha yake, akajiona mwenye dhambi aliyestahili msamaha wa Mungu. Machozi yakambubujika, kwa mara ya kwanza maishani mwake akajikuta akitamani kumfahamu Mungu zaidi ya alivyokuwa akisikia kutoka kwa wazazi wake.

“Wangapi wako tayari kukabidhi maisha yao kwa Yesu jioni ya leo ili aweze kuwabadilisha na kuwafanya wapya, ili hatimaye waweze kuurithi ufalme wa Mungu na pia kulindwa na mwovu Shetani ambaye kazi yake ni kuharibu… Kama wapo naomba wapite mbele.”

Mtu wa kwanza kufika mbele ya jukwaa alikuwa ni Tyra, machozi yakimbubujika na mwili wake kutetemeka. Alikuwa amejisikia mwilini mwake hali ambayo hata siku moja haikuwahi kumtokea, akapiga magoti na kusujudu mbele ya jukwaa huku watu wengine wakizidi kumiminika.

Mchungaji akawaongoza watu hao sala ya toba ili Mungu apate kuwasamehe dhambi zao, alipomaliza aliwaruhusu kuondoka lakini Tyra hakufanya hivyo, akaomba kuongea na Mchungaji baada ya mkutano kumalizika. Hicho ndicho kilichotokea, akamweleza mtumishi huyo wa Mungu kila kitu kuhusu maisha yake na hasa alivyoteswa na mapenzi ya Phillip, Mchungaji hakuwa na cha kufanya zaidi ya kumwombea ili roho hiyo imtoke.

“Mchungaji naomba twende nyumbani ukawaone wazazi wangu!”
“Unaishi wapi binti?”
“Upanga.”
“Nisubiri basi tumalize shughuli zote tutaongozana.”
“Asante mtumishi.”

Saa moja na nusu ndipo Tyra alimuongoza Mchungaji hadi kwenye gari lake, wote wawili wakapanda na kuondoka. Walipoingia tu barabarani, Zamaradi ambaye bado alikuwa hajaondoka eneo hilo alijiweka tayari kwa mashambulizi, hasira yake ilikuwa palepale na alitamani kumuondoa Tyra duniani ndipo kazi yake ikamilike. Gari lilipofika, alinyosha mkono wake ambao ulitoa kitu kama moto uliokwenda moja kwa moka kwenye gari kwa lengo la kupasua tairi, cha kushangaza tofauti na siku nyingine zote moto huo uligeuka na kuanza kumrudia yeye, ukampiga pamoja na mwanaye wote wakaanguka chini.

“Mh!” Tyra aliguna.
“Vipi binti?”
“Gari imetingishika.”
“Twende, nimekwishaelewa kilichokuwa kinaendelea, roho wa kifo alikuwa hapa akikusubiri wewe lakini Mungu amekunusuru.”
“Kweli?”
“Ndiyo.”

“Kwani imekuwaje?”
“Nimemwona mwanamke mmoja ana mtoto, akanyosha mkono wake ambao ulitoa nguvu za giza lakini nikaziamuru zimrudie yeye.”
“Mh! Mwanamke na mtoto tena, inawezekana akawa ni yuleyule aliyewatokea rafiki zangu wawili, Monalisa na Linna, magari yao yakapinduka. Hivi sasa ninavyoongea na wewe Mchungaji Monalisa ni marehemu, Linna ni majeruhi wa moto aliyeungulia ndani ya gari lake…”

Waliongea mengi Mchungaji akimsimulia Tyra juu ya mapepo na namna yanavyofanya kazi na kwamba kinga pekee ilikuwa ndani ya Mungu, ambako watu wote wamchao hawakuwa na hofu ya mapepo hata kidogo. Tyra akamuahidi Mchungaji kumcha Mungu kwa uwezo wake wote tangu siku hiyo.

Kilichofanyika nyumbani kilikuwa ni utambulisho wa Mchungaji kwa wazazi wa Tyra ambao kwanza walishangaa sana kusikia mtoto wao aliyewahangaisha kwa muda mrefu amempokea Yesu, wakamtaka awe anakwenda kuabudu kanisani kwa Mchungaji Moses Lubala ili azidi kukomaa kiroho.

Hivyo ndivyo ilivyotokea, kwani baada tu ya mazishi ya Monalisa, Tyra alianza kuhudhuria mafundisho na ibada kwenye kanisa hilo. Chuoni wanafunzi walimshangaa sana kwani tabia yake ilibadilika kabisa, hakuwa na makundi tena na hata hakudiriki usiku kutoka kwenda disko kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Kitu pekee kilichomsumbua akili ni Phillip, pamoja na kuokoka lakini bado alijisikia kumpenda kijana huyo, hiyo ndiyo vita aliyokuwa amebakiza na ilikuwa ngumu sana kupata ushindi. Hata hivyo, aliuahidi moyo wake kupambana mpaka hatua ya mwisho asirejee dhambini, baadhi ya wanafunzi Chuo Kikuu walimcheka na kudai alikuwa akiigiza ulokole, kwamba muda si mrefu angeanguka na kurejea tena kwenye dhambi zake.

“Umebadilika sana siku hizi, nini siri ya mafanikio yako? Kifo cha Monalisa kimekuumiza sana labda?” Ilikuwa ni sauti ya Phillip alipomfuata kuzungumza naye.
“Hapana. Ni Mungu, ameamua kubadili maisha yangu, nakukaribisha sana kanisani kwetu pale Sinza Mori.”
“Ningependa kufika hapo kanisani ili nione kitu gani kimefanyika, wewe? Wewe Tyra? Ndiyo umekuwa hivi, siyo rahisi kuamini.”
“Karibu.”

Mazungumzo hayo ndiyo yaliwaunganisha zaidi, tangu siku hiyo wakawa karibu kuliko ilivyotokea baada ya tukio lililotokea ndani ya gari nyumbani kwao na Monalisa wakati wa msiba. Phillip akahudhuria kanisani ambako mafundisho yalimgusa, akakabidhi maisha yake kwa Yesu pia na kusimulia mkasa mzima uliomtokea wa kuoa jini ambaye alizaa naye mtoto na alikuwa na wivu mkubwa uliosababisha kuwashambulia wanawake wote waliompenda, Tyra hakuamini alichokisikia ndani ya ofisi ya Mchungaji, akalia machozi mbele ya Mchungaji.

“Ndiyo maana nilikuwa nakwambia uniache.Wenzako niliwakataza hawakunielewa, roho inaniuma sana kwa yaliyowapata,” akamwambia Tyra akimpapasa mgongoni.
“Usiwe na wasiwasi Phillip, Zamaradi hutamuona tena akikusumbua, wala mwanao ambaye pia ni jini, tulikutana nao njiani wakimsubiri Tyra, nguvu ya Mungu ikawashughulikia.”
Phillip alilia kwa uchungu, akajisikia huru moyoni mwake. Taratibu akamnyanyua Tyra na kumkumbatia kisha kunong’ona sikioni mwake “I LOVE YOU TYRA, CAN YOU MARRY ME?” (Nakupenda Tyra, unaweza kukubali nikuoe?)

“Oh, my God! I can’t believe this, are you sure?” (Oh, Mungu wangu! Siwezi kuamini hivi, una uhakika?) Tyra aliuliza maswali mfululizo akilia kwa furaha.
“Absolutely! Our Pastor is my witness.” (Kabisa. Mchungaji ni shahidi wangu.)
“Yes, I can marry you Phillip, I love you too.” (Ndiyo, niko tayari unioe, nakupenda pia.)

Wiki moja baadaye walivalishana pete ya uchumba kanisani mbele ya waumini, ndugu na jamaa na kubatizwa, Tyra akabadilisha jina na kuitwa Genevieve, huku Phillip akiendelea na jina lile lile. Ndoa ilipangwa kufungwa baada ya kumaliza masomo yao, muda wote wakiwa chuoni wangeendelea kuwa wachumba. Mioyo yao ilijaa furaha.

Je, nini kitamtokea Tyra?
 
SEHEMU YA 16


ILIPOISHIA

“Oh, my God! I can’t believe this, are you sure?” (Oh, Mungu wangu! Siwezi kuamini hivi, una uhakika?) Tyra aliuliza maswali mfululizo akilia kwa furaha.
“Absolutely! Our Pastor is my witness.” (Kabisa. Mchungaji ni shahidi wangu.)
“Yes, I can marry you Phillip, I love you too.” (Ndiyo, niko tayari unioe, nakupenda pia.)

Wiki moja baadaye walivalishana pete ya uchumba kanisani mbele ya waumini, ndugu na jamaa na kubatizwa, Tyra akabadilisha jina na kuitwa Genevieve, huku Phillip akiendelea na jina lile lile. Ndoa ilipangwa kufungwa baada ya kumaliza masomo yao, muda wote wakiwa chuoni wangeendelea kuwa wachumba. Mioyo yao ilijaa furaha.

SASA ENDELEA

Phillip na Tyra ambaye sasa alikuwa akiitwa Genevieve waliendelea na masomo huku kila mtu chuoni pale akiwashangaa. Wengi walikuwa wakimshangaa Genevieve kwani ndani ya muda mfupi tangu alipotangaza kumpokea Mungu, maisha yake yalibadilika sana. Hakuwa tena Genevieve wa kwenda kwenye kumbi za starehe na kuvaa mavazi ya kidunia.

Kila jambo alilifanya kwa upole huku jina la muumba wake likitawala mdomoni mwake. Hali kadhalika, Phillip naye alibadilika sana na sasa akawa mtakatifu kwa kila alichokuwa anakifanya. Japokuwa haikuwa rahisi kwake kuwasahau Zamaradi na mwanaye, alimshukuru Mungu kwa kumfungua kwenye kifungo kilichomtesa siku nyingi maishani mwake. Mawazo, akili na moyo wake alivielekeza kwa Genevieve na aliamini hakuna kitakachowatenganisha zaidi ya kifo.

Siku zilizidi kusonga huku mapenzi yao yakiwa gumzo kila walikopita. Wapo waliowabeza na kuwaona kama watu waliokuwa wakiigiza ingawa pia wapo waliokuwa wanawaombea mema kwenye maisha yao.
“Hivi mapenzi ya kilokole yanakuwaje?”
“Yanakuwa kama mapenzi mengine, kwa nini unauliza hivyo?”

“Nauliza kwa sababu nawashangaa sana Phillip na Genevieve, eti wanaigiza mapenzi ya kilokole, ina maana hawajawahi kuduu?”
“Wewe nawe, maswali gani hayo unauliza, kwani hujui amri kumi za Mungu zinavyosema?”
“Sawa najua kuwa Mungu amekataza watu kuvunja amri ya sita, lakini ukiwaangalia Phillip na Genevieve watakuwa hawajahi kukutana kimwili kweli?”

“Bwana eeeh, hayo maswali kawaulize wenyewe, mi ninachojua ni kuwa haitakiwi wachumba kufanya tendo la ndoa mpaka watakapohalalishwa madhabahuni,” wanafunzi waliokuwa wakifanya ‘discussion ‘chini ya mti mkubwa kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliacha kujadili masomo na sasa wakawa wanawajadili Genevieve na Phillip.

Kila mmoja alikuwa akiongea lake lakini ukweli walikuwa nao wenyewe. Kwa kutambua kuwa wanafuatiliwa sana na wenzao, Phillip na Genevieve hawakutaka kuingia kwenye skendo yoyote, wakawa wanajitahidi kuishi kwa kufuata maagizo yote ya Mungu. Hawakuacha kusali kila asubuhi, mchana na jioni bila kujali kama ilikuwa Jumapili au la.
Siku zilizidi kuyoyoma na hatimaye wakamaliza chuo na kutimiza ahadi waliyokuwa wamewekeana, wakafunga ndoa na kuwa mume na mke halali.
***
MWAKA MMOJA BAADAYE
“Haya ndiyo maisha niliyokuwa nayaota siku zote za uhai wangu,” aliongea Phillip wakiwa wamepumzika kwenye bustani nzuri za maua na mkewe, Genevieve.
“Unamaanisha nini mume wangu?”

“Siku zote nilikuwa nikiota kumpata mke mwema ambaye nitaishi naye maisha ya raha mustarehe, unajua mi nimekulia kwenye shida na dhiki sana,” aliongea Phillip huku akijaribu kuvuta kumbukumbu za maisha yake ya utotoni.

“Jamani mume wangu, Mungu ndiyo anapaswa kushukuriwa kwa yote, najua umepitia mambo mengi magumu tofauti na mimi mkeo, lakini hatimaye ndoa imetuunganisha na sasa tumekuwa mwili mmoja,” aliongea Genevieve na kumbusu mumewe shavuni. Alishatambua kuwa kumbukumbu za maisha ya zamani ya mumewe zilikuwa zikimuumiza, jambo ambalo hakuwa akipenda litokee. Akawa mfariji mkubwa kwake.

“Nakupenda sana mume wangu, mimi pia nilikuwa naota kumpata mwanaume kama wewe, una kila kitu nilichokuwa nakihitaji,” aliongea Genevieve huku akijilaza kifuani kwa mumewe. Hawakuitana tena majina yao waliyokuwa wanayatumia tangu wakiwa chuoni.
Licha ya maisha ya kifahari waliyokuwa wakiishi, nyumba nzuri ya kifahari waliyoijenga baada ya kuunganisha mishahara yao na magari ya kisasa ya kutembelea, bado walikosa kitu cha muhimu, watoto.

Mwaka mzima waliokaa ndani ya ndoa haukuwa na mafanikio yoyote, wakaanza kuandamwa tena na walimwengu ambao walikuwa wanawatania kuwa wanamaliza magodoro na kujaza choo.
“Unajua mume wangu mi’ najisikia vibaya sana majirani na ndugu wanavyotudharau na kutunanga eti kwa sababu hatuna mtoto,” aliongea Genevieve huku akilengwa lengwa na machozi.

“Usiwajali mke wangu, kuzaa ni majaliwa ya Mungu, mara ngapi tumefunga na kusali tukimuomba Mungu atupe mtoto? Naamini ameshasikia maombi yetu, hatupaswi kutilia mashaka ahadi za Mungu wetu,” aliongea Phillip kwa hisia.
“Sawa mume wangu, lakini wakati tunasubiri majibu ya Mungu, kwa nini na sisi tusijaribu kwenda hospitalini?”

“Wazo zuri mke wangu, lakini kama ikibainika mmoja wetu ana matatizo huoni ndiyo itakuwa sababu ya mapenzi yetu kupungua?”
“Hapana mume wangu, nakuahidi kuwa hata kama ni wewe ndiyo mwenye tatizo, kamwe upendo wangu kwako hautapungua, nitazidi kukupenda daima.”

“Hata mimi mke wangu nakuahidi kuwa kama mimi nikiwa mzima na tatizo likionekana lipo kwako, sitakutenga bali nitazidi kukupenda kwa siku zote za maisha yangu,” aliongea Phillip, wakakumbatiana kwa furaha. Walikubaliana kuwa siku inayofuata waende pamoja mpaka hospitalini kwenda kuonana na daktari anayeshughulikia masuala ya uzazi.
Kesho yake waliongozana mpaka hospitalini, wakaonana na daktari ambaye aliwafanyia vipimo kwa kina.

Majibu yalipotoka, Genevieve hakuwa na tatizo bali Phillip ilibainika kuwa mbegu zake za kiume hazina uwezo wa kurutubisha yai la mwanamke na kusababisha ujauzito.
“Uliwahi kupata mtoto enzi za ujana wako kabla hujaoana na huyu mkeo wa sasa?” aliuliza daktari, swali ambalo lilimfanya Phillip azame kwenye dimbwi la mawazo.
“Mume wangu daktari si anakuuliza?”

Phillip alishindwa kujibu kwani ni kweli aliwahi kuwa na mtoto lakini siyo katika ulimwengu huu unaoonekana. Alishindwa kujua daktari atamuelewaje atakapompa ukweli huo wa maisha yake.

“Sijawahi daktari, huyu ndiyo mke wangu wa kwanza na sina mtoto yeyote nje ya ndoa,” alijibu Phillip huku mkewe akimuangalia kwa huruma. Alipomueleza vile, daktari aliandika kitu kwenye cheti na kuwaomba wakasubiri nje kwa muda wakati anatafuta ufumbuzi wa tatizo lao.

Aliwaita madaktari wenzake wawili na kujadiliana nao nini cha kufanya ili kumsaidia Phillip apate mtoto.
“Her wife is physically fit, her uterus can conceive and the fallopian tubes are in good condition,” ( Mke wake yuko fiti, mji wake wa uzazi una uwezo wa kutunga mimba na hata mirija yake ya uzazi ipo kwenye hali nzuri)
“How about him?” ( Vipi kuhusu yeye)

“His sperms are not viable. They lack motility ability and they can’t swim to the uterus,” (Mbegu zake za kiume hazina rutuba. Zinakosa uwezo wa kujongea na haziwezi kuogelea kwenda kwenye mji wa mimba)
Madaktari waliendelea kujadiliana juu ya tatizo la Phillip. Mwisho walifikia hitimisho la kumpa dawa ambazo zingeenda kuongeza nguvu na rutuba kwenye mbegu zake. Daktari aliyewapima akawaita Phillip na Genevieve ofisini na kuanza kuwapa ushauri nasaha kabla ya kumpa Phillip dawa za kutumia.

“Mama jitahidi kumpikia mumeo vyakula vyenye wanga na mafuta ya asili kwa wingi. Pia inashauriwa mjizuie kukutana kimwili mara kwa mara ili kuzipa muda mbegu zake zikomae, mkizingatia haya naamini mwezi huu hautaisha bila majibu kuonekana,” aliongea daktari na kuwapa maelekezo mengine ya ziada.

Alipomaliza waliaga na kuondoka, njiani wakawa wanamshukuru Mungu wao kwa kuwasaidia. Waliamini kwake hakuna linaloshindikana. Hakuna kitu walichokuwa wanakisubiri kwa hamu kama mtoto kwenye ndoa yao.

Hata baada ya mwezi mmoja kupita, bado hawakuona dalili yoyote, Genevieve hakuwa amenasa ujauzito. Hali ile ikaanza kusababisha huzuni miongoni mwao. Ni kweli walikuwa wakipendana kwa dhati lakini walihitaji kitu kuurutubisha upendo wao.
Genevieve alikuwa na kazi ya ziada ya kumfariji mumewe kwani majibu yale yalionekana kumsononesha zaidi, hasa baada ya kuambiwa tatizo lilikuwa kwake.

“Au bado Zamaradi analipa kisasi kwenye maisha yangu? Lakini mbona tangu niokoke na kuoana na Genevieve hajawahi kunitokea tena? Na kama kweli sina uwezo wa kumzalisha mwanamke, mbona yeye alibeba ujauzito wangu na kunizalia mtoto?” Maswali mengi yaliyokosa majibu yalikuwa yakipishana kichwani mwa Phillip na kumfanya awe kama mwendawazimu.

Licha ya hali ile, Genevieve aliendelea kumpenda huku akijitahidi kuwa karibu naye kwa kila jambo.
“Mke wangu!”
“Abee mume wangu?”
“Kwa nini tusiende kujaribu kwa waganga wa kienyeji? Nasikia wengi wamefanikiwa.”
“Haaa! Yaani mume wangu unaweza kukosa imani kiasi hicho hadi kuamua kutumia njia hiyo badala ya kumwamini Mungu?”

“Kwani waganga wanaotibu si wanatumia miti iliyoumbwa na Mungu kututibu? Kibaya ni kupiga ramli mke wangu, sioni kama kuna tatizo kwenda kujaribu, hatuwezi kundelea kuishi maisha kama haya.”

“Hapana mume wangu, niko radhi nisizae kabisa maishani mwangu, lakini kamwe siwezi kuabudu miungu wengine zaidi ya Mungu aliye juu.”
Phillip na Genevieve walikuwa kwenye mjadala mzito juu ya hali ile yakutopata mtoto iliyowatokea. Phillip alionekana kuanza kukata tamaa kiasi cha kujaribu mbinu mbadala lakini mkewe hakuwa tayari.

“Sasa tutafanya kitu gani mke wangu, mimi ndiyo mwenye tatizo na ninahitaji tiba ili niwe na uwezo wa kukupa ujauzito.”
“Si kwa kwenda kwa waganga Phillip, tuendelee kumwamini Mungu, sisi tumeokoka hatuwezi kufanya jambo hilo. Tatizo ni kwamba umepoteza imani kabisa, hata maombi yako hayamfikii Mungu.”

“Siyo rahisi kuendelea kuwa na imani, swala hili limeniumiza sana, nataka mtoto, nataka mtoto Tyra.”
“Kuwa na imani, Mungu atajibu kwa wakati wake, Sara alisubiri miaka mingi kabla Isaka hajazaliwa, wewe umeshindwa nini?”

Phillip akamuelewa mkewe, imani yake ikarejea tena. Tangu siku hiyo akawa ni mtu wa kuhudhuria maombi, aliposikia mhubiri mpya ameingia jijini Dar es Salaam alihudhuria na kueleza shida yake, maombi yakafanyika lakini bado hakuwa na uwezo wa kumfanya Tyra mjamzito, imani yake ikazidi kuporomoka tena.

Kwa siri kubwa akaanza kuwa anamdanganya mke wake kwa safari za kikazi, kumbe alikwenda kwa waganga na waganguzi ambako alipewa dawa za mitishamba na kuzitumia kwa siri lakini nazo pia hazikumsaidia mpaka mwaka mmoja mwingine baadaye ukaisha wakiwa hawana mtoto, jamii nzima kuwateta kwa sababu tu hawakuwa na mtoto, jambo hili lilimuumiza sana Phillip na kumfanya wakati mwingine ajifungie chumbani na kulia.

Hata kazi ilimshinda, ikabidi achukue likizo bila malipo.
“Hakuna sababu ya kulia, kitu cha muhimu tutafute jibu la tatizo letu na usiwe na wasiwasi Phillip, nakupenda mno, tuwe na mtoto, tusiwe na mtoto, mimi nitaendelea kukupenda tu.”

“Najua Tyra, lakini roho inaniuma sana, naamini anayenifanya hivi ni huyo huyo Zamaradi, kwa kweli simpendi.”
“Usijali, yote yatapita.”

Alikuwa ni Tyra, mwezi mmoja baadaye akipitia mtandaoni kujaribu kufuata suluhisho la tatizo lao aliposoma juu ya Dk. Zim Kohrer, Mjerumani bingwa wa masuala ya urutubishaji wa mayai ya uzazi na masuala ya viumbe vidogo ambaye kwa Kiingereza walimwita Consultant Embryologist.

Daktari huyu maarufu nchini Ujerumani alikuwa amewasaidia watu wengi ambao hawakuwa na tegemeo la kupata mtoto, hatimaye kufanikiwa, nguli wengi kutoka Hollywood huko Marekani walimiminika katika Jiji la Berlin kupata huduma yake iliyowafanya baadhi kuzaa mpaka watoto pacha.

“Nina habari njema!” Tyra alimwambia Phillip aliporejea kutoka kazini na kumkuta ameketi sebuleni akiwa mwenye mawazo mengi, Phillip akanyanyua kichwa na kumwangalia.
“Habari gani?”
“NImepata daktari wa kutusaidia tatizo letu.”
“Wapi?”

“Ujerumani.”
“Ujerumani? Umempataje?”
“Mtandaoni.”
“Kweli?”
“Ndiyo, ningependa tumjaribu naye.”

“Siyo gharama kubwa?”
“Ni kubwa lakini tutamwambia baba atusaidie…” Tyra hakumalizia sentensi yake simu ya mkononi ikaita, mara moja akabonyeza kitufe cha kupokea na kuiweka sikioni, akaanza kuongea.
“Halo! Halo! Nini? Mama mbona unalia?...Nakuja.” Aliuliza maswali kwa mshituko.
“Kimetokea nini tena?” Phillip aliuliza.
“Baba ameanguka bafuni…. Twende haraka”

Ilikuwa imetimu saa kumi na nusu jioni wakati wanaingia ndani ya gari, Phillip akiwa kwenye usukani na kuendesha moja kwa moja kuelekea nyumbani kwa wazazi wake Upanga wakitokea Mikocheni. Walipofika walipewa taarifa kuwa mzee alikimbizwa Hospitali ya Muhimbili, hawakutaka kupoteza muda wao hapo, gari ikageuzwa na kunyoosha hadi Muhimbili Idara ya Wagonjwa Mahututi ambako walikuta mama yake Tyra akilia, huku wauguzi na majirani wakiwa wamemzunguka.

“Mama nini?”
“Baba yako katutoka.”
Tyra alianguka chini na kuanza kugalagala huku akilia kwa uchungu, Phillip akawepo kumnyanyua hadi kwenye gari ambako alianza kumbembeleza na kumpa maneno ya kumtia moyo. Ukweli haukubadilika, taarifa ilipotolewa baadaye na daktari ilithibitisha kuwa mzee huyo alikuwa amefariki kwa shambulio la moyo, Tyra alilia kupindukia kwa siku zote mpaka walipomzika huko Machame mkoani Kilimanjaro mamia ya watu wakiwa wamehudhuria kumzika mtu tajiri.

Mpaka mwezi mmoja baadaye, Tyra na Phillip walikuwa bado wako kijijini Machame wakiomboleza msiba, tatizo lao la kukosa mtoto lilishapotea kabisa ubongoni, kilichokuwa kikifikiriwa wakati huo ni msiba mzito ulioipata familia.
Kikao cha ndugu kilipokaa, mwanzoni mwa mwezi wa pili Tyra alisimikwa kuwa mrithi wa utajiri wote wa baba yake uliokadiriwa kuwa mamilioni ya dola yakiwa katika viwanda na biashara mbalimbali, kufumba na kufumbua jina la Tyra likabadilika, akaanza kuitwa Mkurugenzi.

Kutajirika kwa Tyra, kulikuwa pia kutajirika kwa Phillip, watu hawa wawili walikuwa mtu na mke wake, hivyo kila alichokuwa nacho Tyra kilimstahili Phillip na alichokuwa nacho Phillip pia kilimstahili Tyra. Wote wakaacha kazi ili wasimamie mali za familia, pamoja na utajiri wote huo suala la mtoto liliwasumbua, walihitaji mtoto, hiyo ilikuwa furaha yao.

“Kwanini tusisafiri kwenda Ujerumani kumuona Dk. Kohrer? Tuna fedha ya kutosha sasa kulifanya jambo hili.” Ilikuwa ni sauti ya Tyra siku moja wakiwa wamelala ndani ya chumba chao kikubwa chenye kila kitu.

“Sina tatizo. Nahitaji sana mtoto mke wangu, inaniumiza sana mimi kuwa chanzo cha tatizo hili”
“Usijali, hatuhitaji mtoto tu, tunahitaji watoto pacha kwa mara ya kwanza ili tufidie muda uliopotea, niko tayari kulipa chochote kwa daktari huyo ili awezeshe mimi kupata watoto wawili kwa wakati mmoja.”

“Nitafurahi mno.”
Kama utani, mwezi mmoja baadaye walikuwa ndani ya ndege ya shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa, shirika la gharama kubwa pengine kuliko mengine yote duniani, wakiwa wameketi kwenye daraja la watu maarufu. Hii ilikuwa safari ya kwenda kwenye Jiji la Berlin kuonana na daktari aliyewasaidia watu wengi kupata watoto.

Ilikuwa ni safari ya saa kumi na mbili, kwanza waliruka mpaka Amsterdam, Uholanzi, ambako waliunganisha na ndege nyingine ya shirika hilo hilo hadi Berlin, wakapokelewa na wafanyakazi wa Hospitali ya Freiburg ambao waliwapeleka kwanza hotelini ili wapumzike na siku iliyofuata waweze kumwona Dk. Kohrer.

Mioyoni mwao walijawa na furaha kubwa kama vile tayari walishapata watoto waliowatarajia, hakuna walichokihitaji zaidi ya watoto wawili kwa wakati mmoja tena wote wawe ni wa kike.
 
SEHEMU YA 17


PHILLIP alikuwa akikoroma huku mkewe akiwa amemkumbatia, walionekana kuufaidi usingizi lakini ghafla Genevieve aligutuka na kujikuta akitoka jasho jingi ingawa chumba chao cha kulala kilikuwa na kiyoyozi.
“Vipi?” Phillip aliuliza baada ya kuzinduka usingizini na kumkuta mke wake ameketi kando ya kitanda akitetemeka.
“Sidhani kama ni ndoto.”

“Kwani vipi?”
“Nimeota ndoto ya kutisha.”
“Ndoto gani?”
“Eti Mzee Mpangala amefariki kwa shambulio la moyo, halafu mimi na wewe tumesafiri kwenda Ujerumani kumuona daktari uliyekuwa unamzungumzia.”
“Ni ndoto tu, Mzee Mpangala hajafa ingawa ni kweli Dk. Zim Kohrer tumempata.”
“Inawezekana ni kwa sababu ya mazungumzo yetu ya jana.”

“Kweli kabisa.”
“Acha nimpigie baba angalau niongee naye.”
“Ni usiku sana atakuwa amepumzika.”
“Phillip! Ni ndoto tu hii, yaani nimeona kila kitu mpaka tukiwa Machame kwenye mazishi.”
“Ni ndoto tu mke wangu.”

“Acha niongee na baba.”
“Haya mpigie.”
Huku Genevieve akitetemeka, moyo wake ukiwa bado hauamini kama kilichotokea ni ndoto alimpigia baba yake na kuzungumza naye, ingawa hakumweleza chochote juu ya ndoto aliyoota. Baada ya maongezi hayo ndipo alirejea kitandani na kujilaza kando ya mume wake, hawakupata usingizi tena muda wote walizungumzia habari ya watoto na safari ya Ujerumani.

Wiki moja baadaye walisafiri mpaka Berlin na kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Schonefeld ambako walipokelewa na wafanyakazi wa hospitali ya Freiburg ambao waliwapeleka moja kwa moja hospitalini kuonana na Dk. Zim Kohrer, mzee mfupi na mwenye mvi nyingi na aliyevaa miwani muda wote, uso wake ukiwa umejawa na tabasamu.
“Mnahitaji kupumzika ili tuanze matibabu kesho?” Aliwauliza baada ya salamu ofisini kwake.

“Hakuna sababu, hatujachoka kiasi hicho, karibu safari yote tulikuwa tumelala vitandani.”
“Aha! Mmesafiri kwenye daraja la watu wazito bila shaka.”
“Ni kweli.”
“Basi tuanze.”

Dk. Kohrer akafungua kompyuta yake na kuanza kuandika maelezo yao yote tangu walipooana, madaktari waliowaona na namna walivyofanya tendo la ndoa, mwisho akamuuliza Genevieve maswali mengi kuhusiana na mzunguko wake wa hedhi. Alipomaliza maswali hayo aliwaeleza juu ya vipimo ambavyo vingefanyika katika kulitafuta tatizo.
“ Kwanza tutaupiga picha mfuko wa uzazi, mirija ya viwanda vya mayai ya Genevieve.

Pia tutapata manii yako kwa ajili ya kuzichunguza ili tuone kama mbegu zako zina tatizo lolote, lazima tujue idadi yake na kama zina uwezo wa kurutubisha yai au la, yote haya ni muhimu tuyafahamu kabla ya kuchukua hatua yoyote.”
“Hakuna tatizo lolote daktari, tumeacha shughuli zote kuja kukuona na tunaamini utakuwa na jibu la tatizo letu.”

“Hakuna kisichowezekana, wengi wamepata furaha yao hapa hapa kwenye chumba hiki.” Dk. Kohrer aliongea akitabasamu.
Kilichofuata siku hiyo ni kuchukuliwa vipimo, zoezi lilipokamilika waliondoka kwenda Hoteli ya Berlin Hilton ambako walifikia. Ilikuwa ni ya nyota tano, chumba kimoja kililipiwa dola elfu moja mia tano kwa usiku mmoja. Hapo ndipo Genevieve na Phillip waliamua kuishi mpaka wapate suluhisho la tatizo lao, gharama zote zikilipwa na Mzee Mpangala.

Siku tatu baadaye wakiwa hotelini walipigiwa simu na Dk. Kohrer akiwataka wafike ofisini kwake mara moja kujadiliana juu ya majibu yaliyopatikana, mioyo yao ikiwa imejawa hofu na furaha waliondoka hadi ofisini kwake na kumkuta akiwasubiri kwa hamu kubwa. Tofauti na nyuso zao kuwa na wasiwasi, Dk. Kohrer alikuwa na uso wenye furaha na matumaini.
“Tumekuja daktari.”

“Imebidi niwaite maana majibu yote yamekamilika.”
“Sawasawa.”
“Itabidi niwe mkweli maana lengo ni kusaidia.”
“Hakuna tatizo.”
“Uchunguzi unaonyesha kwamba Genevieve huna tatizo lolote kabisa, tatizo liko kwa mumeo, Phillip…” Dk. Kohrer alimalizia kwa kuita.
“Naam.”

“Mbegu zako hazitoshi, ni chache na zaidi ya kuwa chache pia hazina mbio, zinashindwa kulifikia yai la mwanamke ili mimba itungwe. Nilipozichunguza zaidi nikagundua hata kama zikilifikia yai hazina uwezo wa kutungisha mimba, nimekuja kwenu na jibu lifuatalo, kama kweli mnahitaji mtoto hamna jinsi zaidi ya kutafuta mbegu za kiume za mtu mwingine ili tufanye kitu kiitwacho IVF.”
“IVF ni nini daktari?”

“Kirefu chake ni In Vitro Fertilization, kitakachofanyika hapo ni kuchukua mbegu za Genevieve na kuziunganisha na mbegu za mwanaume mwingine ili mimba itungwe kisha nitaipandikiza ndani ya tumbo la mkeo na itakua vizuri mpaka mpate mtoto au watoto mapacha kama mnataka.”
“Inawezekana daktari?” Phillip aliuliza.

“Kwanini isiwezekane, hizo ndizo kazi zangu, huwa nazifanya kila wiki.”
“Mtu wa kutoa mbegu za kiume tutampata wapi?”
“Tutatanganza mtandaoni, atajitokeza mtu na kulipwa si chini ya dola elfu kumi ili atoe mbegu zake. Kama mko tayari mnaweza mkaniambia niendelee na utaratibu wa kumtafuta mtoa mbegu, gharama zangu mimi zitakuwa dola elfu ishirini na mbili kwa mtoto mmoja na mara mbili yake kwa watoto pacha.”

“Tuko tayari daktari, tunachohitaji sisi ni watoto.” Phillip aliongea uso wake ukiwa umeinamishwa chini ni kweli alikuwa hajisikii vizuri kuwa na watoto ambao si damu yake lakini hakuwa na jinsi zaidi ya kukubali.

“Basi kesho fanyeni malipo ili mambo yafanyike haraka.”
“Tutalipa daktari, wewe tafuta tu mtu wa kutoa mbegu.”
“Hii hapa ndiyo namba ya akaunti yangu, mnaweza kuniingizia fedha hizo moja kwa moja pale NedBank.”
“Hakuna shida.”

***
Novotroitsk, Urusi.
Kilikuwa ni kipindi cha majira ya baridi nchini Urusi, watu wengi walijifungia ndani ya nyumba zao ambao waliwasha mitambo ya kuongeza joto. Watu kidogo sana kwenye mitaa ya mji wa Novotroitsk, maarufu kwa viwanda vya vyuma duniani, walikuwa nje sababu ya baridi. Barafu zilikuwa zimeganda juu ya ardhi, kiasi cha kuyafanya hata magari yashindwe kutembea kwa mwendo wa kasi.

Katika hali hii mtu mmoja aitwaye Victor Fedorov, alikuwa nje akipigwa na baridi, hakuwa na mahali pa kuishi, alikuwa maskini kama walivyo maskini wengine wengi barani Afrika ingawa aliishi katika taifa lenye utajiri mkubwa. Moyoni alijawa uchungu, akitamani siku moja kuwa na mafanikio ndiyo maana alikimbia jijini Moscow alikozaliwa kuja kutafuta maisha kwenye mji huu mdogo wenye idadi ya watu wasiozidi laki moja kwenye mpaka wa Urusi na Kazakhstan.

“Siku moja nitafanikiwa tu, sina sababu ya kuendelea kuishi Moscow wakati sina hata familia, mke na watoto wangu walishanikimbia sababu ya umaskini..” Aliwaza Victor.
Kila alipotaka kupata joto aliingia kwenye vyumba ambavyo vilitoa huduma kwenye mtandao wa Intaneti kwa malipo, akalipa fedha kidogo na kupata joto huku akitafuta taarifa mbalimbali mtandaoni. Mchana wa siku hiyo baridi ilipomzidi alielekea kwenye chumba kimoja cha huduma hiyo na kuingia ndani ambako alilipia na kuonyeshwa kompyuta, akakaa na kufungua kisha kuanza kupita kwenye mitandao mbalimbali.

“Sperm donor needed urgently! Ten thousand dollars will be paid.” (Mtu wa kutoa mbegu za kiume anahitajika haraka, dola elfu kumi zitalipwa.) Aliyasoma maneno hayo kwenye mtandao na moyo wake kushituka, alihitaji fedha kuliko kitu kingine chochote wakati huo na aliamini dola elfu kumi zingetosha kabisa kuanzisha biashara ya kununua vyuma na kuuza, kwa muda mrefu sana alikuwa ametamani kufanya hivyo lakini kikwacho kilikuwa ni mtaji.

Haraka akajaza fomu iliyokuwepo akielezea utambulisho wake na mahali alipokuwa nchini Urusi ikiwa ni pamoja na kuweka anwani ya barua pepe na namba yake ya simu, baada ya kumaliza akaendelea na kupitia mitandao mingine. Masaa mawili kabla hajatoka ndani ya chumba hicho, simu yake iliita, namba iliyoonekana kwenye kioo haikuwa ya Urusi.
“Halo!”
“Halo! Victor?”

“Ndiyo.”
“Naitwa Dk. Kohrer, napiga simu kutoka Ujerumani nimeiona fomu yako sasa hivi mtandaoni kwamba uko tayari kutoa mbegu kwa gharama ya dola elfu kumi.”
“Ndiyo.”
“Unaweza kunielezea jinsi ulivyo?”
“Ni Mrusi, mweupe, mrefu na nina nywele nyeusi.”

“Unaweza kupiga picha na kunitumia sasa hivi?”
“Niko kwenye chumba cha Intaneti, hivyo ndani ya dakika kumi nitakuwa nimeishatuma.”
“Nasubiri, nikishaipokea mara moja nitakupigia.”

Dakika kumi na tano baadaye walikuwa kwenye simu tena, Dk. Kohrer akiongea na Victor kumthibitishia kuwa alikuwa amekubalika na angesafirishwa hadi Ujerumani kwa ajili ya kutoa mbegu ingawa kwa sharti moja tu kwamba hakutakiwa kukutana na watu ambao walihitaji mbegu yake, kazi yake ingekuwa ni kutoa mbegu, kulipwa na kuondoka.

“Hilo si tatizo kwangu, cha muhimu ni malipo.”
“Hakuna shida, nitakutumia sasa hivi namba ya tiketi na fedha ya matumizi njiani ili kesho usafiri kuja hapa Berlin.”
“Hakuna shida.”

BAADA ya Phillip na Genevieve kukubaliana na Dk. Kohrer juu ya gharama zinazohitajika kwa ajii ya kufanya IVF, njia ya kupandikiza mbegu za mwanaume mwingine ndani ya mji wa uzazi wa Genevieve kwa lengo la kupata mtoto, wawili hao walikamilisha malipo kupitia Benki ya NedBank kama walivyokubaliana na kilichofuatia ikawa ni kumtafuta mwanaume ambaye atakubali kutoa mbegu zake kwa malipo ya dola elfu kumi.

Baada ya kutangaza mtandaoni, Victor Fedorov, mwanaume fukara anayeishi kwenye Mji wa Novotroisk, Urusi alijaza taarifa zake mtandaoni kuonesha kuwa yupo tayari kuchangia mbegu zake za kiume kwa malipo ya dola elfu kumi. Baada ya kujaza taarifa zake, Dk. Kohrer alimpigia simu na wakakubaliana kufanya kazi hiyo haraka kwa sharti moja la kutokutana na watu waliokuwa wakihitaji mbegu zake.

Baada ya makubaliano,Victor alitumiwa tiketi ya ndege mpaka Ujerumani na siku iliyofuatia akawa tayari amewasili kwenye Hospitali ya Freiburg aliyokuwa akifanyia kazi Dk Kohrer.

“Karibu bwana Victor, naitwa Zim Kohrer, mtaalamu wa embryology, kama tulivyozungumza kupitia mtandao, kuna biashara hapa ya kuuza mbegu zako za kiume kwa ajili ya kuwasaidia wanandoa wenye matatizo ya kupata mtoto.

Hundi yako ya dola elfu kumi hii hapa, cha msingi twende maabara ukafanyiwe vipimo kuona kama huna matatizo yoyote kisha mambo mengine yatafuatia,” Dk. Kohler alikuwa akizungumza na mwanaume mrefu, mweupe mwenye nywele nyeusi, Victor kutoka Urusi.

Hakuwa na kipingamizi chochote, kwake fedha ndiyo kitu alichokuwa anakihitaji kuliko vitu vyote. Baada ya kuingizwa maabara na kufanyiwa vipimo vya kina kuchunguza kama hakuwa na tatizo lolote, majibu yalipotoka alionekana kuwa na afya njema.

Kilichofuatia ikawa ni kuingizwa tena kwa mara nyingine maabara ambapo alitolewa mbegu zake za kiume kwa kutumia utaalamu wa hali ya juu. Alipomaliza alikabidhiwa hundi yake kisha akaaga na kuondoka. Kwake ile ilikuwa ni zaidi ya bahati ya mtende kuota jangwani. Ufukara uliomtesa kwa kipindi kirefu hadi kusababisha mkewe na wanaye wamtoroke, sasa ulikuwa umefikia mwisho.

Kwa kutumia dola elfu kumi alizozipata, alipanga kuanzisha biashara ya kununua vyuma na kwenda kuviuza, kazi ambayo aliitamani kwa siku nyingi lakini akawa anakwama kutokana na kukosa mtaji.
Hakutaka kupoteza muda, jioni ya siku ile ile kwa kutumia tiketi aliyokuwa amekatiwa na Dk. Kohrer, alisafiri hadi Novotroisk, mji aliokuwa akiishi na kuanzisha biashara ya kununua vyuma kama alivyopanga.

*******
Phillip na Genevieve walikuwa chumbani kwao ndani ya hoteli wakiendelea kufarijiana, mara simu ya mezani ikaita. Kwa haraka, Phillip aliinua mkonga na kuongea na upande wa pili. Alikuwa ni Dk. Kohrer akiwataarifu kuwa kazi ya kupata mwanaume wa kutoa mbegu za uzazi tayari imekamilika na aliwataka wafike haraka hospitalini kwa ajili ya Genevieve kuchukuliwa mbegu zake tayari kwa kuunganishwa na mbegu ya mwanaume aliyepatikana, ambaye wote hawakutakiwa kukutana naye.

“Mke wangu, kila kitu kipo tayari, daktari amesema tujiandae kwenda hospitali sasa hivi,” aliongea Phillip kwa furaha huku akimkumbatia mkewe. Kwa pamoja walimshukuru Mungu kwani hawakudhani kuwa kazi ya kumpata mtoa mbegu ingekuwa rahisi kiasi kile.
Baada ya kujiandaa, Phillip na mkewe walishuka ngazi hadi kwenye maegesho ambako dereva wa hoteli alikuwa akiwasubiri, wakaondoka wakimhimiza aendeshe kasi hadi Hospitalini, gari likaegeshwa na wakashuka na kwenda moja kwa moja hadi ofisini kwa Dk. Kohrer aliyekuwa akiwasubiri.

Bila kupoteza muda aliwaeleza mafanikio ya mpango wao huku akiwaonesha picha ya mwanaume aliyetoa mbegu zake na kila mmoja akaridhika na mwonekano wake.
“Hamtakiwi kukutana naye kabisa, wala yeye hapaswi kukutana nanyi ili mradi amekwishatoa mbegu, kazi yake imekwisha!” Aliongea kwa msisitizo Dk. Kohrer.

Kilichofuata kikawa ni Genevieve kuchukuliwa hadi chumba cha upasuaji mdogo ambapo zoezi la kuzinyonya mbegu kwenye viwanda vyake vya mayai lilifanyika, bahati nzuri alikuwa katika kipindi ambacho mayai yake yalikuwa tayari kwa kurutubishwa.

Ilikuwa ni operesheni ndogo lakini ilichukua muda wa masaa matatu, ndipo mayai yakapatikana na Dk. Kohrer kuyachukua kwenye chombo maalum kiitwacho Incubator hadi maabara ambako alishirikiana na wataalamu wengine kuliunganisha moja ya mayai hayo na mbegu ya Bwana Victor Fedorov iliyogandishwa, ambaye tayari alikuwa ndani ya ndege akirejea Urusi.

Zoezi la kurutubisha na kupandikiza kiumbe hicho ndani ya mfuko wa uzazi wa Genevieve na uchunguzi kama hakikuwa na matatizo yoyote lilipokamilika masaa arobaini na nane baadaye, alipewa muda wa mwezi mmoja kupumzika wodini ili kuhakikisha kiumbe hicho kinapata muda wa kuzamisha mizizi yake kwenye mfuko.

Mambo yote yalipokamilika ikiwa ni pamoja na kulipa gharama zote zilizokuwa zinahitajika, Phillip na Genevieve waliruhusiwa kurejea Tanzania kwa makubaliano ya kuendelea kuwasiliana na Dk. Kohrer katika hatua zote za ukuaji wa ujauzito ule.
Saa kadhaa baadaye wakawa ndani ya ndege ya shirika la usafiri wa anga la Ujerumani, Lufthansa. Mioyo yao ikiwa imejawa na furaha, hakika safari yao ilikuwa ya mafanikio makubwa.

Walipowasili Dar es Salaam, waliendelea na maisha yao kama kawaida na baada ya wiki kadhaa kupita, Genevieve akaanza kuonesha dalili zilizoamsha matumaini mapya kwao. Alianza kusikia kichefuchefu na kuanza kuchagua aina ya vyakula.

“Kaniletee ndimu mume wangu, halafu samaki wabichi siwatamani hata kuwaona, wananifanya nijisike kichefuchefu,” aliongea Genevieve kwa kudeka akiwa amejilaza kwenye kifua cha mumewe. Dalili zile zilimfurahisha zaidi Phillip kwani aliamini sasa na yeye atapata heshima kama wanaume wengine wenye familia.

Mwezi wa nne wa ujauzito huo ulipoingia, afya ya Genevieve ikiwa nzuri, walikwenda hospitali kupima ili wapate uhakika wa jinsi mtoto alivyokuwa akiendelea kukua. Wakati wa kuwapa majibu, sura ya daktari ilikuwa imejawa na tabasamu.
“Mimba inaendelea vizuri sana, tena nina habari nzuri za kuwapa... Genevieve una mimba ya watoto pacha!”

“Asante Mungu, furaha yangu itakuwa mara mbili!”
Hakuna aliyekuwa anaelewa namna walivyofanikisha suala lile la Genevieve kupata ujauzito, wakaendelea kuifanya siri kama walivyokuwa wamekubaliana. Kwa kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kwenda mbele, ujauzito wa Genevieve ulizidi kuongezeka, tumbo lake likawa kubwa, hali iliyowafanya wote wawili kujisikia fahari kubwa mioyoni mwao.

Ujauzito wake ulipofikisha miezi sita, Genevieve alilazimika kupumzika nyumbani na kuacha shughuli zote alizokuwa akizifanya, kama walivyokuwa wameshauriwa na Dk. Kohrer, lengo la kufanya hivyo likiwa ni kuzuia ujauzito ule kuharibika katika hatua za mwisho. Phillip akawa na kazi ya kumtunza mkewe kwa uangalifu, huku wakizidi kumuomba Mungu wao kila uchao.

Hatimaye miezi tisa ilitimia, Genevieve akashikwa na uchungu wa kujifungua. Kwa kuwa Phillip alikuwa amemuandalia mkewe kila kitu, alipoanza kuonesha dalili za uchungu tu, alimkimbiza haraka hospitali.

Alipofika mapokezi akiwa anaendesha gari mwenyewe, Phillip aliwasiliana na manesi wakunga ambao kwa haraka walisogeza kitanda cha magurudumu karibu na gari lake, Genevieve akateremshwa na kuwekwa juu yake, akawa anakimbizwa kuelekea kwenye wodi za wazazi huku akijinyonganyonga kutokana na maumivu makali aliyokuwa akiyahisi.

Aliwekwa kitandani, Phillip akawa kando yake akishuhudia hatua kwa hatua namna mke wake alivyokuwa akifanya kazi ya kuwaleta watoto hao duniani! Jukumu lake lilikuwa ni kumfariji na kumtia moyo.
je nini kiliendelea
 
SEHEMU YA 18


Hospitali ya Aga Khan ilikuwa umbali wa kama mita mia mbili na hamsini tu kutoka walipoishi Phillip na Genevieve, ilikuwa hospitali kubwa ya gharama pale ambapo mtu alihitaji huduma kutoka kwa madaktari wake. Kwenye chumba ambacho mlangoni kilikuwa na kibao kilichoandikwa “Labour Room” ndimo alimokuwa amelala Genevieve akihangaika na maumivu, Phillip akiwa kando yake, akimpapasa tumbo na kiuno kama njia ya kumpunguzia maumivu.

“So painful!” (Inauma sana.) aliongea machozi yakimtoka.
“I know, just be strong because soon you are going to be happy. Our dream is going to be realized and you are the dream bearer” (Najua, kuwa imara tu, sababu muda si mrefu utafurahi, ndoto yetu itatimia na wewe ndiye uliyeibeba ndoto.) Phillip alimwambia mke wake.

Wauguzi walikuwepo muda wote kutoa kila aina ya msaada uliohitajika lakini kwa saa zote kumi na mbili lakini bado Genevieve hakuweza kujifungua, daktari akafikia uamuzi wa kumchoma sindano ya kuongeza uchungu, Oxytocin, ambayo ilipochomwa tu, muda wa kama masaa matatu baadaye, mtoto wa kwanza wa kike alitoka na akafuatiwa na mwingine wa pili ambaye pia alikuwa wa kike.

Genevieve akainua kichwa chake na kuwaangalia watoto wake, machozi ya furaha yakamtoka, Phillip akasogea karibu na kumkumbatia. Hakika ndoto ilikuwa imetimia, haikujalisha kabisa mbegu za watoto hao zilitoka wapi, walikuwa ni watoto wao, Mungu alikuwa amewapa ili wawalee na kuwatunza.
“Mwaaa!” Phillip alimbusu mke wake usoni.

“Thank you, finally we are going to be the happiest couple on earth.” (Asante, hatimaye tutakuwa wanandoa wenye furaha kuliko mwingine yeyote duniani.)
“Yeah!” (Ndiyo.)
Watoto waliondolewa na kupelekwa kwenye chumba maalum ambako walivalishwa nguo na kufanyiwa huduma zote, Genevieve akatundikiwa dripu ya maji ya Glucose ili kumuongezea nguvu mwilini maana alikuwa amedhoofika sababu ya kusukuma watoto kwa muda mrefu. Masaa mawili baadaye, Phillip akiwa bado na mke wake wazazi wa Genevieve waliingia, wakiongozwa na mzee Mpangala, wote nyuso zao zilikuwa zimejawa na furaha.

“Hongera mwanangu.”
“Asante baba, nimekuletea wake wazuri wawili, kama ndoto yangu ya kwamba umekufa niliyoota ingekuwa kweli, basi ungewakosa.” Genevieve aliongea akiikumbuka ndoto mbaya aliyoota kabla hawajasafiri kwenda Ujerumani kuonana na Dk. Kohrer.

“Ilikuwa ni ndoto tu mwanangu, hongera sana, ukoo unazidi kuongezeka.”
“Kweli baba.”
Ilikuwa ni siku ya furaha mno kwa kila mmoja wao, kitu kilichomsumbua Phillip moyoni ni historia ya watoto hao, bado alielewa kabisa uwazi kwamba hakuwa baba yao halisi. Kwa mbali hili lilimuumiza, kwani hakujua nini kingetokea iwapo yeye na Genevieve siku moja wangeshindwa kuelewana na hatimaye kutengana, hiyo ilimaamnisha angeweza kuambiwa watoto wale hawakuwa wake. Akajipa moyo kwamba Genevieve asingeweza kumfanyia kitendo hicho.

Muda mfupi baadaye watoto walitolewa chumbani walikopelekwa na kuletwa kitandani kwa Genevieve, wakalazwa kando yake, kwa furaha akawafunua na kuanza kuwabusu.
Mzee Mpangala na watu wote waliokuwa chumbani walionyesha mshituko kwa rangi za watoto hao hazikuwa za Waafrika halisi lakini hakuna aliyediriki kufungua mdomo wake kuulizia jambo hilo.
“Wanafanana sana na marehemu bibi yetu mzaa mama, yeye alikuwa na asili ya Kibeligji,” Phillip aliongea baada ya kuzisoma kwa makini nyuso za watu waliokuwemo chumbani na kuugundua wasiwasi wao, hakutaka mtu yeyote aelewe siri ya kupatikana kwa watoto hao.

“Duh! Tulitaka kushangaa, imekuwaje nyinyi Waafrika mzae watoto wa aina hiyo.” Mzee Mpangala aliongea.
Hawakukaa sana baada ya hapo, ndugu na marafiki wakaondoka na kuwaacha Phillip na Genevieve peke yao wakiendelea kuweka msimamo wa kuificha siri ya watoto hao. Siku mbili baadaye waliruhusiwa kuondoka hospitali na kurejea nyumbani Upanga ambako furaha iliendelea mtindo mmoja, ndugu na jamaa wakiendelea kumiminika kuwaona watoto pacha wa Genevieve na Phillip.
“Naomba nipewe nafasi ya kuwapa watoto wangu majina.” Genevieve aliongea mbele ya ndugu na jamaa.
“Endelea.” Watu wote wakaitikia.

“Hawa watoto wataitwa Dorice na Dorica!”
“Yupi Dorice, yupi Dorica?” Phillip akauliza.
“Wa kwanza kutoka ni Dorica na wa pili ni Dorice!”

Makofi yakapigwa watu wakishangilia, majina yalikuwa yamewafanana kabisa watoto kwa jinsi sura zao zilivyokuwa nzuri. Miezi mitatu baadaye watoto wakiendelea kukua vizuri, Phillip alirejea kazini kwake kwenye kampuni ya simu za mikononi iliyoitwa T-Mobile ambako alifanya kazi kama mwanasheria na Genevieve akaendelea kufanya kazi kwenye kampuni ya baba yake ambako alitumia elimu yake ya uchumi akiwa Mkurugenzi Msaidizi, lengo la Mzee Mpangala lilikuwa ni kumrithisha kila kitu ili aendeleze mambo aliyoyafanya, muda wa kustaafu ukifika.

Miezi tisa baadaye watoto walitimiza mwaka mmoja, sherehe kubwa ya kuzaliwa kwao ikafanyika, mpaka wakati huo hakuna mtu hata mmoja aliyejua siri ya namna walivyopatikana. Dk. Kohrer alialikwa siku hiyo kusherehehea mafanikio lakini aliombwa kutoongea chochote juu ya namna mimba ilivyotungwa, hiyo ilitakiwa kubaki siri mpaka mwisho wa dunia.

***
Victor Fedorov alipoingia nchini Urusi, taarifa ya kwanza aliyoipokea ni juu ya kifo cha mke na watoto wake kwenye milima ya barafu walikokwenda kushiriki mchezo wa kuteleza kwenye barafu. Ingawa siku zote alimchukia mke wake, Fedorov aliwapenda mno watoto wake Misha na Kunin, alilia na kuomboleza, kilichomsikitisha zaidi ni kwamba hakuweza kuziona maiti zao.

Kilichofanyika baada ya hapo maishani mwake, hakikuwa kufanya biashara ya vyuma kama alivyokuwa amepanga baada ya kupokea dola elfu kumi kutoka kwa Dk. Kohrer, akaamua kuingia kwenye ulevi. Kazi yake kubwa ikawa kunywa na kulewa, lengo likiwa ni kupoteza mawazo ya kupoteza mke na watoto, maisha yakaharibika, akawa mtu wa kulala baa na mtaani.
“Sina sababu ya kufanya kazi au biashara tena, acha ninywe tu.” Aliwaza na kila siku hilo ndilo jambo alilofanya; kunywa.

Miezi mitatu baadaye, fedha zote ilikuwa imekwisha, akaanza kuteseka tena. Mwisho akiwa amebakiza dola tano mfukoni aliamua kuitumia kununua tiketi ya bahati nasibu kubwa iliyokuwa ikifanyika nchini Urusi, zawadi yake ikiwa dola milioni moja kwa ambaye angeshinda. Alifanya hivyo kama jaribio la bahati yake, ingawa hakuwa na uhakika wa kushinda.
Be the next Millionaire, ulikuwa ni mchezo mkubwa sana nchini Urusi, maelfu ya watu walishiriki wakijaribu bahati yao. Kila mwaka alipatikana mshindi mmoja tu katika nchi hiyo kubwa yenye idadi ya watu wasiopungua milioni 141, ushindani ulikuwa mgumu, hata Victor aliponunua tiketi yake alijua angeshindwa, hata hivyo alitaka kujaribu kwa sababu hakuwa na jambo jingine la kufanya.

“Huwezi jua pengine naweza kushinda, hakyanani nikipata fedha tena safari hii sitafanya mchezo, namuahidi Mungu kwamba nitabadilika kabisa, sitakunywa pombe tena na nitatoa sehemu ya kumi kwake kama Zaka…Ee Mungu nisaidie”
Aliitunza tiketi yake kwenye karatasi la nailoni ili isiweze kuharibika kwa unyevunyevu uliosababishwa na umande, kila siku jioni akiwa mtaani kwenye veranda alilolala ilikuwa ni lazima aifungue na kuanza kuzisoma namba zake.

“18243004!” alitamani siku ya kutangazwa mshindi namba hiyo ndiyo isomwe, akiteseka kwa ubaridi aliendelea kusubiri mtaani kwa hamu kubwa, akipata msaada wa fedha ya chakula kwa kuombaomba kwa wapita njia, moyoni akijilaumu kwa kuchezea fedha aliyopata baada ya kuuza mbegu.
“Siku itafika tu! Matangazo yatoke kwamba mimi ndiye mshindi wa Bahati Nasibu…ni Machi 16, siyo mbali, itafika tu!” aliwaza Victor akiwa mtaani.

***
Dorice na Dorica walikuwa wazuri mno, kila mtu aliwapenda, tena walikuwa ni wapole waliobebwa na kila mtu. Watu hawakusita kusema wangesumbua sana vijana wa kiume kama wangefikisha umri wa miaka kumi na sita, sura zao zilikuwa ni mchanganyiko wa baba na mama yao ambao kwa hakika walikuwa na mvuto wa kutosha.

Wakaendelea kukua vizuri, siri ya walivyopatikana ikaendelea kufichwa, watu wote mpaka familia waliamini mbegu za Phillip ndizo zilizotumika jambo ambalo halikuwa kweli. Jambo hilo halikutakiwa kabisa kuvuja, hata wao wenyewe waliliongelea mara chache na hawakupenda kabisa lijitokeze, Genevieve alimheshimu Phillip kama baba wa watoto wake.

“Hivi itakuwaje kama itakatokea siku moja siri ikavuja na aliyetoa mbegu zake akajitokeza na kudai Dorice na Dorica ni watoto wake?” Phillip alimuuliza mke wake siku moja akicheza na watoto wake sebuleni.
“Haiwezekani, atajuaje?”
“Huwezi kuelewa, lakini ikitokea hivyo, nakuhakikishia mke wangu kwamba nitakufa au nitaua mtu, hawa ni watoto wangu kabisa, ndivyo ninavyojisikia ingawa sikutoa mbegu, nawapenda kuliko kitu kingine chochote maishani mwangu, najua ndiyo watarithi kila kitu nitakachokipata!”

“Ina maana unawapenda kuliko hata mimi mama yao?”
“Siyo hivyo mke wangu, nyote nawapenda kwa upendo mmoja, teh! teh! teh!” Phillip alimaliza kwa kucheka.
Miaka miwili na nusu baadaye Genevieve akiendelea kuendesha kampuni za baba yake kama Mkurugenzi Mkuu na Phillip akipandishwa cheo kuwa Mwanasheria Mkuu wa T-Mobile, Dorice na Dorica waliandikishwa chekechea katika shule ya Awali iitwayo Upanga Maranatha Kindergaten school.

Ilikuwa ni siku ya furaha mno kwa watoto na hata wazazi wao, huko walijifunza kuandika, kuimba, kusoma na hata kuhesabu na uwezo wao ulikuwa mkubwa sana kuliko watoto wengine kituoni hapo, jambo hili liliwapa Phillip na Genevieve tumaini kubwa.
“Wanaendelea vizuri sana, tumaini letu ni kwamba hata wakianza darasa la kwanza watakuwa na akili hivi hivi!” Ilikuwa ni sauti ya mwalimu akiwaeleza Phillip na mke wake siku ya mkutano wa wazazi na walimu shuleni.

“Tutafurahi mno, ahsanteni sana kwa jinsi mnavyowafundisha watoto wetu”
“Pia ninyi, kwa ushirikiano mnaotupa na malezi bora kwa watoto, hiyo inafanya kazi ya kuwafundisha iwe rahisi, ni wasikivu sana na wana adabu”
Miaka miwili baadaye na nusu baadaye, Dorica na Dorice wakiwa na umri wa miaka mitano taratibu za kuwatafutia shule ya kuanza darasa la kwanza zilianza kufanyika, walikuwa wamekuwa kiasi cha kutosha, kiasi kwamba haikuonekana sababu yoyote ya kusubiri mpaka watimize umri wa miaka saba ambao watoto wengi walianza nao darasa la kwanza.

“Mom I am so happy, tomorrow am going to be a big girl!” (Mama nina furaha mno, kuanzia kesho nitakuwa msichana mkubwa) ilikuwa ni sauti ya Dorica akimwambia mama yake huku uso wake ukiwa umejawa na tabasamu lililomfanya azidi kuvutia na kufanana kabisa na mama yake.
“Me too mom!” (Mimi pia mama) Ilikuwa ni sauti ya Dorice.
“Why?” (Kwanini?)
“We are going to start Primary School!” (Tutaanza darasa la kwanza) wote wawili wakaitikia wakimkumbatia mama yao.

Siku hiyo walilala usingizi wa mang’amung’amu, wakiifikiria siku iliyofuata, ya kwanza kuanza darasa la kwanza. Ilibaki kidogo tu walale wamevalia sare za shule kwa furaha waliyokuwa nayo. Phillip na mke wake walicheka sana, wao pia walilazimika kuingia kitandani saa nane usiku sababu wasingeweza kuwaacha watoto wakiwa macho peke yao.

Kulipokucha Phillip na mke wake walishirikiana kuwaandaa, baadaye Phillip aliondoka akimwacha Genevieve ili muda ukifika awapeleke kwenye kituo ambako basi la Shule ya Holy Ghost lingepita na kuwachukua, baada ya hapo ndiyo yeye angerejea nyumbani kuendelea na shughuli nyingine.

***
Mamilioni ya watu nchini Urusi walikuwa nyuma ya runinga zao, ilikuwa ni siku ya Machi 16, kila mtu mkononi akiwa ameshika kipande cha karatasi, kilikuwa ni tiketi ya Bahati Nasibu ya Be the next Millionaire, kila mmoja aliamini yeye ndiye angekuwa mshindi na maisha yake yangebadilika kuanzia siku hiyo.

Victor Fedorov, alikuwa nje ya baa iitwayo Zona, ambako watu wengi maarufu walikwenda kuburudika siku za mwisho wa wiki. Alikuwa hapo akiomba kwa watu waliokuwa wakiomba kuingia na kutoka ndani ya baa hiyo maarufu, yeye pia alikuwa na kipande chake cha tiketi mkononi, akichungulia ndani kwenye runinga kubwa iliyokuwa ukutani, ambayo ililengwa na macho ya watu wote wakitaka kushuhudia nani angeibuka Milionea.

“Na mshindi ni mwenye tiketi namba…!” Mtangazaji, msichana mwembamba mrefu mwenye sura ya kuvutia aliyejaa sawasawa kwenye kikoo cha runinga alisema, watu wote wakawa kimya, mapigo ya moyo yakisikika namna yalivyogonga kifua, huku macho yao yakiwa yameelekea kwenye kipande cha karatasi na masikio yakiwa yameongezewa uwezo wa kusikia. Victor alikuwa kimya, yeye pia akiisoma tiketi yake.
“Narudia tena mshindi ni mwenye namba 1824300…!”

“Mungu wangu! Mungu wangu! Mungu wangu!” Victor alisema kwa sauti ya chini chini, mwili wote ukitetemeka na machozi yakimtoka, alikuwa amebakiza hatua moja tu maishani mwake awe milionea!
Kilichofuata baada ya hapo, sekunde chache tu baadaye ni kelele nyingi nje ya ukumbi, mtu akipiga kelele na kushangilia, watu wote wakatoka mbio kwenda kuona nini kilichotokea lakini hawakumwona, alishapotelea gizani. Wakarudi ndani kuendelea na vinywaji, kila mmoja wao akisonya na kujisikia ni mwenye bahati mbaya.
JE NINI KITAENDELEA
 
SEHEMU YA 19


ILIPOISHIA
“Na mshindi ni mwenye tiketi namba…!” Mtangazaji, msichana mwembamba mrefu mwenye sura ya kuvutia aliyejaa sawasawa kwenye kikoo cha runinga alisema, watu wote wakawa kimya, mapigo ya moyo yakisikika namna yalivyogonga kifua, huku macho yao yakiwa yameelekea kwenye kipande cha karatasi na masikio yakiwa yameongezewa uwezo wa kusikia. Victor alikuwa kimya, yeye pia akiisoma tiketi yake.
“Narudia tena mshindi ni mwenye namba 1824300…!”

“Mungu wangu! Mungu wangu! Mungu wangu!” Victor alisema kwa sauti ya chini chini, mwili wote ukitetemeka na machozi yakimtoka, alikuwa amebakiza hatua moja tu maishani mwake awe milionea!
Kilichofuata baada ya hapo, sekunde chache tu baadaye ni kelele nyingi nje ya ukumbi, mtu akipiga kelele na kushangilia, watu wote wakatoka mbio kwenda kuona nini kilichotokea lakini hawakumwona, alishapotelea gizani. Wakarudi ndani kuendelea na vinywaji, kila mmoja wao akisonya na kujisikia ni mwenye bahati mbaya.
SASA ENDELEA
…4!” ndivyo alivyomalizia mtangazaji.
Victor hakuamini alichokisikia, hisia zake zilimtuma kuwa huenda masikio yake yalikuwa yamemdanganya au alikuwa akiota ndoto. Mshindi wa bahati nasibu wa dola milioni moja awe yeye? Lilikuwa ni jambo lisilowezekana kwa maskini ambaye hakuwa hata na mahali pa kulaza ubavu wake kuibuka na kitita hicho.

Kwa hofu kubwa aliyokuwa nayo ya kuuawa na pengine kunyang’anywa tiketi yake, Victor alikimbia umbali wa kama mita mia tano hivi na kuingia chini ya daraja ambako alizama huku akihema kwa nguvu katikati ya mapipa mawili ya takataka.

“Siamini! Ahsante Mungu,” alijisemea moyoni mwake huku akiendelea kububujikwa na machozi ya furaha.
Hakutoka hapo, wadudu waliendelea kumuuma lakini alijikaza mpaka kulipokucha. Saa kumi na mbili kasorobo ndipo alipoondoka katikati ya mapipa na kuanza kutembea kuelekea mjini ambako alianza kuzitafuta ofisi za Be a Billionaire mpaka akazipata na kuketi mbele ya mlango wake.

Tayari mwanga wa siku ulishajitokeza na kulikuwa na baridi kali iliyomfanya atetemeke kiasi cha meno kugongana kama vile alikuwa na homa kali. Hakujali, mawazo yake yote yalikuwa kwenye dola milioni moja, tayari alikuwa tajiri. Kwa fedha hizo asingelala nje tena, angenunua nyumba nzuri yenye mitambo ya kuongeza joto.

“Pombe basi tena! Sitafanya makosa ya mwanzo. Mungu amenipa nafasi nyingine,” aliwaza Victor.
Saa mbili kamili mfanyakazi wa kwanza wa ofisi hiyo alifika na kumkuta Victor ameketi mbele ya mlango, haraka akamuamuru aondoke akidhani ni watu wasiokuwa na makazi, Victor aligoma kuondoka na kumwambia alikuwa na shida kwenye ofisi hiyo.

“Hakuna msaada hapa.”
“Sijaja kutafuta msaada, kwa fedha niliyonayo naweza kukuajiri wewe uwe unafua nguo zangu za ndani tu! Wala si suruali na mashati”
“Kaka usinitukane, nahisi wewe ni punguani.”
“Baada ya muda si mrefu utaanza kuniamkia.”
“Akuamkie nani?” aliuliza mwanaume huyo huku akifungua mlango kisha kuingia ndani, Victor alimfuata kwa nyuma.

“Kaka nimekwambia subiri nje.”
“Soma hii…” Victor aliongea akimwonyesha tiketi.
“Mungu wangu! Ni wewe? Shikamoo kaka, karibu kiti, utatumia kinywaji gani?”
“Sihitaji chochote, hivi sasa ndiyo unaanza kuniamkia?”
“Samahani sana, sikufahamu.”

“Naomba fedha yangu niondoke.”
“Kaka subiri, meneja anakuja muda si mrefu, atawaita waandishi wa habari na kukutangaza, hongera sana.”
Victor hakujibu, alibaki kimya akionekana mwenye chuki sababu ya dharau alizofanyiwa. Nusu saa baadaye mwanaume mfupi mnene mwenye kitambi chenye uzito usiopungua kilo hamsini aliingia, mfanyakazi aliyetangulia akasimama kwa heshima na kumwamkia kisha kumtambulisha kwa Victor, yeye pia alionesha hali ya kutoamini.

“Ni wewe?”
“Ndiyo”
“Unaishi wapi?”
“Sina makazi, naishi mtaani.”

Mchana wa siku hiyo, Victor alinunuliwa suti nzuri ya vipande vitatu, akanyolewa nywele zake vizuri, akavaa pamoja na viatu vyeusi vya ngozi vipya tayari kwa mkutano na waandishi wa habari akitangazwa kama mshindi wa dola milioni moja. Uso wake ulikuwa umejawa na tabasamu, hakuwahi katika maisha yake kupigwa picha nyingi kiasi hicho. Gazeti la jioni lilipotoka lilikuwa na kichwa cha habari kisemacho A homeless become a millionaire (Asiye na makazi aibuka milionea). Ilikuwa ni furaha isiyo na kifani.

Urusi na dunia nzima ilisoma habari za Victor Fedorov, siku hiyo hakulala nje, alipangishiwa chumba kwenye hoteli ya nyota tano ya Hilton akifanyiwa kila kitu kama mfalme. Siku iliyofuata asubuhi taratibu za kufungua akaunti na kuhamisha fedha zake zilifanyika, dola milioni moja zikaingizwa kwenye akaunti yake.

Kitu cha kwanza alichokifanya ilikuwa ni kuchukua moja ya kumi ya fedha hizo zote na kuzipeleka kanisani kama alivyomuahidi Mungu, kisha kuwakusanya watu wote wasio na makazi walioishi katika Mji wa Novotroitsk na kuwafanyia sherehe kisha kuwapatia mitaji wa biashara. Baada ya hayo hakutaka kuchezea fedha kama alivyofanya awali, alikimbia haraka kwenye soko la hisa ambako alionana na madalali na kuambiwa kampuni ya vyuma iitwayo Novic Metals, ilikuwa ikiuza hisa zake kwenye mnada.

“Kwa dola laki tisa naweza kununua asilimia ngapi ya hisa?”
“Asilimia themanini.”
“Niko tayari.”
“Unazo fedha?”
“Ninazo.”

“Wapi?”
“Kwenye akaunti yangu.”
“Benki gani?”
“Russian Commercial Bank.”
“Unaweza kuniruhusu nimpigie meneja wa Benki?”
“Hakuna shida.”

Hilo lilifanyika, dalali mkuu wa soko la hisa la Urusi akapata uhakika na biashara ikafanyika. Bila kutarajia wala kupanga, kampuni hiyo kubwa ya uchimbaji wa chuma ikawa mali ya Victor Fedorov. Wanahisa wote wakatangaziwa na kukutana naye kwenye mkutano wa wanahisa siku tatu baadaye. Hakuna aliyekuwa tayari kuamini kwamba mtu ambaye hakuwa na makazi, waliyempita mtaani akipigwa na baridi ndiye sasa alikuwa mmiliki wa kampuni hiyo.

Victor akaanza kuchapa kazi akiwa na uchungu mkubwa wa maisha, alitaka kufanikiwa na alitamani kuwa tajiri. Hivyo alifanya kazi usiku na mchana, akiwa na chumba cha kuishi ndani ya kiwanda chake. Hii iliwafanya wafanyakazi wote wafanye kazi kwa kujituma, huku akitoa motisha kwa wale waliofanya kazi kwa bidii kuliko wengine.

Miezi michache baadaye aligundua kuwa kilichoifanya kampuni hiyo isipate faida kilikuwa ni uvivu na kutojituma kwa wafanyakazi. Aliporekebisha tatizo, faida kubwa ilipatikana ndani ya miezi sita tu, kampuni ikaanza kukua na ndoto ya Victor kuwa tajiri ikaanza kuonesha njia. Akanunua nyumba kubwa na gari la kifahari kisha kumuoa binti mrembo aitwaye Maria Nosh kwenye harusi iliyokusanya matajiri na wanasiasa wengi kwenye mji huo. Tayari alishakuwa miongoni mwao.

Wakati kampuni ikiendelea kukua, Victor ambaye aliwauzia Phillip na Genevieve mbegu zake za kiume, hakuweza kupata mtoto katika mwaka wa kwanza wa ndoa yake. Moyo wake uliumia kwani alihitaji mtoto kuliko kitu kingine chochote, alitaka mrithi wa utajiri wake baada ya watoto wake kufa mwaka mmoja kabla.

Haraka yake ya kupata mtoto ilimfanya aachane na Maria Nosh mwaka mmoja na nusu tu baada ya ndoa yao, akamuoa mrembo mwingine aitwaye Milka Vashnic ambaye pia mpaka mwaka mmoja baadaye alikuwa hajapata mtoto, Victor akamuacha bila kujiuliza mara mbili.

“Nahitaji mtoto, haraka iwezekanavyo,” alijisemea moyoni mwake, ghafla akazikumbuka mbegu zake alizouza kwa Dk. Kohrer. Akachukua simu na kuipiga namba yake akitaka kufahamu nini kilitokea baada ya yeye kuondoka Ujerumani.

“Aaa! Yalikuwa mafanikio makubwa, walizaliwa watoto wawili.”
“Wako wapi?”
“Siwezi kusema, ni kinyume na taratibu za kazi yangu.”
“Daktari, nawahitaji hao watoto, ni wa kwangu.”
“Victor umechanganyikiwa?”

“Sijachanganyikiwa, nahitaji watoto wangu kwa gharama yoyote.”
“Utajuaje mahali walipo?”
“Nitajua. Fedha haishindwi, mimi si maskini mlala nje tena.”
“Siyo rahisi.”

“Naapa kwa Mungu kuwa lazima watoto wangu nitawapata. Kama ni dola elfu kumi niliyopewa niko tayari kuirejesha hata kama ni mara kumi au mia moja zaidi lakini nipewe wanangu.”
Tayari simu ilishakatwa upande wa Dk. Kohrer.
ILIKUWA ni ofisi kubwa iliyopambwa kwa vioo kila upande na kulikuwa na meza kubwa pamoja na kabati iliyotengenezwa kwa fomaika, kando kulikuwa na mashine ya kuongeza joto chumbani kwa sababu baridi ilikuwa chini ya nyuzi sifuri kwa wakati huo kwenye mji wa Novotroitsk, nyuma ya meza hiyo aliketi mwanaume aliyevalia suti nyeusi ya vipande vitatu, tai nyekundu na shati jeupe, uso wake haukuonekana wenye furaha hata kidogo.

Alikuwa Victor Fedorov, ambaye miezi michache tu kabla alikuwa akiishi nje sababu ya kukosa makazi huku akipigwa na baridi. Sasa alikuwa mkurugenzi wa kampuni ya Novic Metals yenye wafanyakazi zaidi ya elfu mbili na mia tano, yeye akiwa mwajiri wao.

Kichwani mwake alikuwa na wazo moja tu; watoto. Aliwataka watoto waliotokana na mbegu zake wapatikane na kusafirishwa kuja Urusi mara moja, uwezo wa kufanya hivyo alikuwa nao sababu ya utajiri mkubwa alioumiliki akiendesha kampuni ya kuchimba na kufua vyuma iliyoshika namba mbili kwa ukubwa nchini Urusi.

“Nahitaji watoto wangu!” alisema Victor kwa Kirusi huku akipiga meza kwa nguvu.
Moyoni mwake aliamini kuna jambo lingemwezesha kuwapata watoto hao zaidi ya kutafuta mpelelezi au kampuni ya upelelezi ambayo angeilipa ili ifanye kazi hiyo dunia nzima mpaka watoto watakapopatikana. Alizungusha akili yake huku na kule akitafakari na kufikiria kampuni yoyote ambayo ingeweza kumsaidia kulifanya jambo hilo hata kama malipo yangekuwa makubwa kiasi gani.

“Niitie Ditrov,” alimwambia katibu muhtasi wake kupitia katika simu.
“Sawa bosi!”
Dakika tano baadaye mlango wa ofisi yake ulifunguliwa, akaingia mwanaume mfupi mwenye misuli aliyevalia suti ya rangi nyeusi pia, kwa kumtazama tu mtu yeyote angeamini lazima sehemu kubwa ya maisha yake ilitumika kubeba vyuma. Huyu ndiye alikuwa Ditrov mlinzi wa Victor Fedorov, ambaye historia yake ilihusisha mapambano katika vita vya Chechnya, kufanya kazi katika Shirika la Kijasusi la Urusi na kazi nyingi za hatari.

“Ndiyo bosi.”
“Nataka unisaidie.”
“Niko tayari.”
Victor alikwenda mbele na kumsimulia sehemu ya mkasa uliokuwa ukimkabili na kumwomba amsaidie kama alifahamu mtu yeyote nchini Urusi ambaye angeweza kufanya kazi ya kupeleleza mahali watoto wake walikokuwa, akamhakikishia kwamba angekuwa tayari kulipa kiasi chochote cha fedha ili mradi amweleze ni wapi watoto walipokuwa na ikiwezekana watekwe na kusafirishwa moja kwa moja hadi Urusi.

“Inawezekana!”
“Nani anaweza?”
“Mimi.”
“Kweli?”
“Kabisa.”

Baada ya mazungumzo ya muda wa karibu saa nzima, walikubaliana malipo ya dola laki moja na elfu hamsini ili kuhakikisha kwamba watoto hao wanapatikana, Victor alikubali na akaahidi kulipa kiasi cha dola elfu hamsini kama malipo ya utangulizi na baada ya hapo angeendelea kulipa dola elfu hamsini-hamsini mpaka fedha zote zikamilike lakini watoto wapatikane.

Siku tatu baadaye kila kitu kilikamilika, malipo yakafanyika na Ditrov akapanda ndege na kuruka moja kwa moja hadi Ujerumani kwenye Jiji la Berlin kwenye kadi yake ya benki kukiwa na dola elfu hamsini, kwa fedha hiyo alikuwa na uhakika wa kupata kila taarifa muhimu juu ya watoto waliozaliwa kutoka kwenye kliniki ya Dk. Kohrer hata kama daktari huyo alikuwa hataki.

Alitua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Schonefeld saa kumi na mbili jioni kwa majira ya Ujerumani, hakuwa na mtu wa kumpokea, akachukua teksi na kumwamuru dereva ampeleke kwenye hoteli ya nyota tano na dereva huyo akampeleka katikati ya jiji ambako alipanga chumba ghorofa ya tano kwenye hoteli iitwayo Metropolitan, iliyoaminika kuwa ni ya gharama kubwa kuliko nyingine yoyote nchini humo.

Baada ya chakula cha usiku na vinywaji kidogo kwenye baa ya hoteli hiyo, alipandisha hadi chumbani kwake ambako alitumia muda wa kama nusu saa kwenye mtandao akichunguza kliniki ya Dk. Kohrer, akagundua msichana wa mapokezi ambaye picha yake ilikuwa miongoni mwa picha za wafanyakazi wa kliniki hiyo aliitwa Nasha, kwa muonekana alionekana kama Msomali.

“Huyu ndiye atanisaidia kujua ukweli ninaoutafuta,” alisema moyoni mwake na hakutaka kuendelea kuwaza tena, akavuta shuka yake na kujifunika gubigubi, dakika arobaini na tano baadaye alikuwa akikoroma na hakuamka mpaka kulipokucha asubuhi siku iliyofuata.

Saa nne kamili alikuwa mapokezi ambako aliomba aelezwe utaratibu wa kukodisha gari ambalo angeendesha mwenyewe, akawashangaza wahudumu alipoulizia kama angeweza kupata Q7, gari la kifahari kupita kiasi, wakamwangalia kwa mshangao wakiwa hawaamini walichokisikia.

“Q7?”
“Ndiyo.”
“Kwa nini Q7?”
“Najua ni kwa nini.”
“Twende,” mmoja wa wahudumu alimwita na kumchukua moja kwa moja hadi kwenye chumba ambacho mlangoni kiliandikwa maandishi: Metropolitan Car Hire.

“Anataka gari la kukodi.”
“Aina gani?”
“Q7.”
“Q7?” msichana aliyekuwa nyuma ya kaunta aliuliza.
“Ndiyo.”
“Hatuna Q7.”

“Mna gari gani nzuri inayonifaa mimi na ya kifahari?”
“Ferrari!”
“Safi kabisa, inakodishwa kiasi gani kwa saa?”
“Dola mia tano.”
“Naitaka kwa saa ishirini na nne kazi yangu itakuwa imemalizika.”
“Hakuna shida, unaweza kulipia.”

Hawakuamini alipojaza fomu na baadaye kutoa kadi yake ambapo fedha zote za kulipia gari hiyo kwa saa ishirini na nne zilikatwa, akakabidhi hati yake ya kusafiria na kuonyesha leseni ya kimataifa ya udereva na hapo ndipo akapewa ufunguo wa gari na kuondoka moja kwa moja kuelekea ilikokuwa kliniki ya Dk. Kohrer, akiongozwa na kifaa maalum cha kuonyesha njia kilichokuwa ndani ya gari lake ambacho mtu aliandika jina la mahali alikokwenda kisha kilimwelekeza mitaa mpaka kumfikisha.

Akaegesha gari mbele ya jengo kubwa la hospitali ya Freiburg na kushuka, kisha kutembea akiingia ndani ya jengo hilo mpaka mapokezi, haikumsumbua hata kidogo kumtambua Nasha, moyoni mwake akakiri msichana huyo alikuwa mrembo kupindukia.
“How are you Nasha?”
“I am fine and you?” (Mimi mzima wewe?)
“I am fine too, do you remember me?” (Mimi mzima pia, unanikumbuka?)
“Nop!” (Hapana)

“I came here with my wife last year, you attended us very well, I am here to say thank you.” (Nilikuja hapa na mke wangu mwaka jana, ulituhudumia vizuri sana, nimekuja kukuambia ahsante.)
“You are welcome!” (Karibu!)
“Is doctor Kohrer in?” (Dk. Kohrer yupo?)
“Yes, very busy though!” (Ndiyo, lakini ana kazi nyingi sana.)

“Ok! Say hi to him! Can you come with me to my car? There is something I would like to hand you.” (Sawa, utamsalimia! Unaweza kunifuata kwenye gari? Kuna kitu ninataka kukupa.)

“No problem!” (Hakuna shida) Nasha aliitikia na kuanza kumfuata Ditrov kwenda nje ambapo alifika na kufungua mlango wa gari, sauti ya Nasha kwa nyuma ikasikika akisema: “Oh! My God! You are riding a Ferrari? You must be very rich, you didn’t tell me your name sir?” (Oh! Mungu wangu! Unaendesha Ferrari? Lazima utakuwa tajiri sana, hukuniambia jina lako) Nasha aliongea akipokea bahasha kutoka kwa Ditrov, ndani yake kukiwa na dola elfu moja.

“I am staying at the Metropolitan Hotel, please pass by for a cup of tea in the evening if you have time!” (Nimefikia Metropolitan Hotel, tafadhali ukipata nafasi jioni unaweza ukapita angalau tupate kikombe cha kahawa.)
“No problem I will at 7:00!” (Hakuna tatizo nitapita saa moja.)
“JOB DONE!” (Kazi imekamilika) Ditrov alijisemea moyoni mwake, akimkumbatia Nasha, wakaagana na akaondoka akimwacha amesimama mwenye mshangao.
JE NINI KILIENDELA
 
SEHEMU YA 20


DITROV aliondoka akiendesha kwa mikogo Ferrari yake ya kukodi huku Nasha akimwangalia kwa mshangao, kwa tamaa zake msichana huyo alihisi hiyo ilikuwa ni bahati ya mtende iliyomwijia bila kutarajia. Hakuhisi kabisa kilichokuwa kikiendelea, kwake saa moja ya jioni ikaonekana ni kama mwaka kesho, alitaka muda huo ufike upesi ili achukue teksi na kwenda moja kwa moja hotelini kwa Ditrov, hakika alimtaka kwa udi na uvumba.

“Warum hast du glucklich warden so plotzlisch”(Kwa nini umepata furaha hivyo ghafla?) msichana mwingine wa mapokezi alimuuliza Nasha.
“Eine reiche person hat mich fur kafee eingeladen am Abend” (Mtu tajiri amenikaribisha kahawa jioni)
“Vorsichtig sein.”(Uwe mwangalifu)
“Ich beginne, ihn zu lieben” (Nahisi nimeanza kumpenda).

Saa zilitembea taratibu mno siku hiyo, hatimaye saa 12:30, muda wa kutoka kazini ukawadia, Nasha akasaini kitabu na kubeba mkoba wake kwapani na kutembea hadi nje, kichwani mwake akimfikiria Ditrov tu, alihisi ndiye mwanaume wa ndoto yake ambaye kwa kipindi kirefu alikuwa akimsubiri na alitamani awe hajaoa ili baadaye amtamkie kwamba alitaka kuwa mume wake.

Nje alipanda ndani ya teksi na kumwelekeza dereva ampeleke Metropolitan Hoteli ambayo ilikuwepo umbali wa nusu kilometa kutoka ilipokuwa kliniki ya Dk. Kohrer, dakika kumi baadaye waliegesha mbele ya jengo la hoteli hiyo, Nasha akalipa kisha kushuka na kunyoosha moja kwa moja hadi mapokezi.

“Ich hier, um zu treffen Herr Ditrov” (Niko hapa kumuona bwana Ditrov)
“Fur einem Moment zu warten”( Subiri muda kidogo) aliongea msichana huyo wa mapokezi na kupiga namba ya simu, akasikika akiongea na mtu upande wa pili, alipoweka simu chini alimwita kijana aliyekuwa kando yake ambaye alivalia suti nyeusi ya vipande vitatu na kumwomba ampeleke Nasha chumbani kwa Ditrov.

kwa msaada wa lifti walipandisha hadi ghorofani ambako kengele iligongwa mlangoni, Ditrov akiwa kwenye taulo tu akafungua, moyo ukamwenda mbio Nasha alipomtazama jinsi mwili wake ulivyojazia sababu ya mazoezi, hakuonekana kama mzee, kifupi alimvutia kimapenzi. Mlango ulipofungwa nyuma yao, Ditrov alimshika mkono na kuanza kumvuta kumpeleka kitandani, akamsukuma na kumlaza chali.

“You know what?”(Unajua nini?)
“No!”(Hapana)
“I love you and I want us to have sex”(Nakupenda na nitaka tufanye ngono)
“Just like that?”(Hivyo tu?)
“Yeah!” (Ndiyo)
“No! Lets talk first!”(Hapana! Tuongee kwanza)

Ditrov ambaye tayari alishavua taulo na kulitupa pembeni alisitisha zoezi na kuketi kando ya Nasha kisha kuanza kumwambia maneno ya mapenzi akieleza jinsi alivyompenda baada ya kumwona tu pale kliniki na hakuwa tayari kumpoteza msichana mrembo kama yeye.
“I am ready to do anything but have you!”(Niko tayari kufanya lolote niwe na wewe!)
“Are still married?”(Bado umeoa?)

“No! I divorce my wife last year, right now I am looking for a woman with lucky, I think you’re the one”(Hapana! Nilimtaliki mke wangu mwaka jana, sasa hivi natafuta mwanamke mwenye bahati, nafikiri ni wewe) aliongea Ditrov akitabasamu.
“Sure?”(Hakika?)
“Yeah!”(Ndiyo)

Maneno hayo yalimlainisha kabisa Nasha, akahisi kuishiwa nguvu mwilini mwake, ghafla akajiona mwenye bahati kuliko wanawake wengine wote chini ya jua ambayo hakutaka ipotee. Akamruhusu Ditrov azungushe mkono wake begani na kuanza kumpapasa taratibu nyuma ya shingo. Kitu kama umeme wenye nguvu kali, ukapita mwilini mwake na kumpiga shoti, akazidi kulegea, mhemo wake ukabadilika na taratibu akalazwa kitandani na kuanza kuvulishwa nguo alizokuwa nazo mpaka akabaki mtupu.

Kilichofuata baada ya tukio hilo, hakielezeki, hakuwahi tangu azaliwe kukutana na mwanaume kama Ditrov, alihisi ni kwa sababu ya mazoezi aliyoyafanya. Ni kweli alikuwa na mchumba aliyetarajia kuolewa naye lakini kama Ditrov angetaka kumuoa na kuondoka naye kwenda Urusi, alihisi alikuwa tayari kwa hilo bila kuogopa lawama.
“Ditrov!”
“Yes” (Ndiyo)

“Can I tell you something?”(Naweza kukueleza kitu?)
“Go ahead”(Endelea)
“You are good!” (Wewe ni mtaalam)
“In?”(Katika?)
“Love making!”(Kufanya mapenzi)

“Thank you, that is just a beginning, lets take a fifteen minutes break and then I will show you who I am!”(Ahsante, huo ni mwanzo, tupumzike kwa dakika kumi na tano halafu nitakuonyesha mimi ni nani?)
“Oh! My God! That’s just a beginning? You gonna kill me”(Oh! Mungu wangu! Huo ni mwanzo tu? Utaniua.)
“No! You will enjoy it!”(Hapana! Utafaidi)
Nusu saa iliyofuata ndani ya chumba hicho ilikuwa ni vilio na kelele zilizowasumbua mpaka watu wa vyumba vingine, Nasha alikuwa katika hali ambayo hakuwahi kukutana nayo, Ditrov akiwajibika ipasavyo, ghafla akasitisha huduma na kumwangalia Nasha machoni ambaye tayari alikuwa taaban akielekea mwisho wa safari yake.

“Usiache!” Nasha alipiga kelele.
“Listen, I want you to do me one favour!”(Sikiliza, nataka unifanyie upendeleo mmoja)
“What is that favour baby? I can do anything for you, I love you so much Ditrov, you name it, I do it!”(Kitu gani hicho mpenzi? Naweza kufanya chochote kwa ajili yako, nakupenda mno Ditrov, ukikitaja tu nakifanya)

“ I need one file from Dr. Kohrer’s Clinic!”(Nahitaji faili moja kutoka kwenye kliniki ya Dk. Kohrer)
“Whose file is that?”(Faili la nani?)
“A guy named Victor Federov, who donated sperms to a certain couple few years ago!”(La mtu aitwaye Victor Federov ambaye alitoa mbegu zake za kiume kwa wanandoa fulani miaka michache iliyopita)
“When do you need it?”(Unalihitaji lini?)
“Tomorrow!”(Kesho)

“I will do that in the morning!”(Nitafanya hivyo asubuhi)
“Thank you!” (Ahsante)
Ditrov hakumwachia Nasha, usiku mzima alimfanyia mambo ambayo msichana huyo hakuwahi kukutana nayo, kifupi hawakulala na wala Nasha hakukumbuka kwenda nyumbani kwake. Saa mbili asubuhi ndiyo aliamka na kuanza kujiandaa, sababu hakutaka kwenda kazini na nguo zile zile, Ditrov alishuka hadi ghorofa ya chini ambako alimnunulia nguo nyingine mpya na kumletea, akavaa na kumbeba kwa gari hadi kliniki ambako alimwacha na kurejea hotelini.

Saa nne kamili, simu chumbani kwa Ditrov iliita, akaikimbilia haraka na kuipokea. Ilikuwa ni sauti ya Nasha akipiga simu kutoka kliniki na kumtaarifu kwamba alishalipata faili hilo, Ditrov akamwomba alitoe kopi ili akienda hotelini ampelekee nakala.
“It is an electronic file!”(Ni faili la kielekroniki) alijibu Nasha akimaanisha faili hilo lilikuwa kwenye kompyuta.

“That is even better, send to my email now”(Hiyo ni nzuri zaidi, nitumie kwa barua pepe sasa hivi)
“Five minutes!”(Dakika tano)
Hivyo ndivyo ilivyotokea, dakika tano baadaye Ditrov alipofungua sanduku lake la barua pepe alikuta faili limetumwa, akafungua na kuanza kulisoma, hakuamini alichokishuhudia, kazi ilikuwa imekuwa rahisi kuliko alivyofikiria. Akafunga kompyuta yake na kulisogelea begi lake, haraka akalifungua na kuanza kukusanya kitu kimoja baada ya kingine akikiweka ndani ya begi.

***
Saa tano kamili Nasha alitoroka kazini kwake na kwenda moja kwa moja hotelini Metropolitan, lengo likiwa ni kwenda kumwona Ditrov, akili yake ilishachanganyikiwa kabisa, kazi zilikuwa hazifanyiki. Taswira ya mwanaume huyo ilikuwepo kila mahali, alitaka amwone tena kabla hajaendelea na kazi.
Mapokezi hakuongea na mtu, akapitiliza moja kwa moja kwenye lifti na kwenda hadi chumbani ambako alikuta mlango umefungwa, akagonga kwa muda bila kufunguliwa. Alipohakikisha Ditrov hakuwemo chumbani ndipo akaamua kwenda mapokezi kuulizia.

“Ameondoka!”
“Ameondoka?”
“Ndiyo”
“Siyo kweli”
“Amesaini hapa”
KITU cha kwanza alichokifanya Ditrov bila kupoteza muda baada ya kulipata faili ni kumpigia simu Victor Fedorov kumtaarifu juu ya ushindi alioupata ndani ya muda mfupi, Victor alifurahi mno akiwa haamini alichokuwa akiambiwa. Mara moja akamtaka Ditrov apande ndege na kuruka hadi Moscow ambako angeunganisha ndege nyingine na kusafiri hadi Novotroisk, safari ambayo ingemchukua saa kumi na mbili.

“Hakikisha unafika hapa ndani ya muda huo, kweli umepata faili?”
“Ndiyo bosi, utakuja kuona.”
“Tafadhali njoo, umenifurahisha mno, lazima nikupe motisha.”
“Hakuna shida, nakuja.”

Saa mbili baadaye Ditrov alikuwa ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Urusi akikatisha mawingu, fikra zake zilitawaliwa na kazi iliyokuwa mbele yake, ni kweli alikuwa amefanikiwa kujua mahali watoto wa Victor Federov walikokuwa lakini hakufahamu njia ambayo angeitumia kuwachukua na kuwasafirisha mpaka Urusi bila matatizo yoyote.

Kompyuta yake ndogo ikiwa imefunguliwa, akiendelea kulisoma taratibu faili alilotumiwa ili apate kulielewa vizuri; Dar es Salaam, Tanzania, Upanga, Ally Khan Street, House Number 122, Phillip and Genevieve Mpangala. Alisoma maelezo hayo mara kwa mara akijiridhisha kisha kuitafuta ramani ya Jiji la Dar es Salaam iliyopigwa kwa setelaiti, akauona mtaa wa Ally Khan na kuanza kuitafuta nyumba namba 122 mpaka akaipata.

“Lazima watakuwa matajiri pia, nyumba kubwa sana hii,” aliwaza Ditrov ndege ikizidi kusonga mbele.
Saa tano baadaye, ndege ilianza kushuka na hatimaye kutua kwenye uwanja wa ndege wa Domodedovo ambako alishuka na kufanya taratibu za kuunganisha na ndege nyingine ya shirika hilo hilo iliyompeleka mpaka Novotroisk,
Nje ya uwanja alipokelewa na Victor ambaye uso wake ulijawa na furaha. Wakaingia ndani ya gari aina ya Benz nyeusi na kuondoka hadi ofisini kwa Victor ambako kitu cha kwanza ambacho Victor alichotaka kukiona ni faili, Ditrov akafungua kompyuta yake na kuanza kumwonyesha kila kitu alichokipata.

“Una uhakika ni wenyewe?”
“Asilimia mia bosi.”
“Hebu twende kwenye mtandao wa Google, tuangalie kama wana maelezo yoyote yanayowahusu.”
“Hakuna shida,” alijibu Ditrov na kuutafuta mtandao huo mpaka akaupata na kuandika majina ya Phillip, Genevieve, Upanga Tanzania na kubonyeza kitufe kilichoandikwa Enter.

Taarifa za Phillip na Genevieve tangu wakisoma chuo kikuu na baadaye kufunga ndoa zikaonekana, upande wa picha ilionekana ile waliyopiga kama familia na watoto wao wawili pacha, chini yake ikiwa imeandikwa “A wonderful and happy family of Mr Phillip and Mrs Genevieve”. Moyo wa Victor uliruka mapigo kadhaa baada ya kuiona picha hiyo.

“Ndiyo, hawa ni watoto wangu.”
“Wanafanana nawe kupita kiasi!”
“Kabisa, ndiyo wenyewe kwa gharama yoyote ile nawataka hapa Urusi, unanisikia Ditrov?”
“Nakusikia bosi. Unawataka lini?”

“Nawataka jana!” alisema tajiri Victor akionesha ni kiasi gani aliwataka watoto wake, kiasi cha kufikiri wangekuwa hapo kuanzia jana yake.
“Hakuna shida.”
“Utafanyaje?”
“Kwa hivi sasa sina jibu, nipe muda mpaka kesho niwasiliane na watu wangu.”

“Hakuna shida, lakini naomba uelewe kwamba furaha yangu haiwezi kutimia kama watoto hawa sitawapata.”
“Nitakuja na jibu zuri bosi wangu,” Ditrov akajibu kisha kuaga na kuondoka zake.

Kufanya kazi ndani ya shirika la kijasusi la Urusi kwa miaka mingi kabla ya kuacha na kuajiriwa na Victor, kulimpa Ditrov nafasi ya kufahamiana na watu wengi waliojihusisha na ujasusi, miongoni mwao akiwemo Dimitri Coscov kiongozi wa kundi la uasi la Chechnya. Huyu ingawa alikuwa adui mkubwa wa Urusi, kwa upande wa Ditrov alikuwa rafiki yake mkubwa. Kitu cha kwanza alichokifanya baada ya kuondoka ofisini kwa Victor ni kumpigia simu.

“Nina tatizo, nahitaji utaalamu wako kulitatua.”
“Tatizo gani?”
“Sitaki kuongea kwenye simu, napanda ndege sasa hivi kuja Grozny.”
“Karibu.”

Kesho yake majira ya jioni tayari alisharejea Novotroisk na kumpigia simu Victor ili kujua mahali alipokuwa, alikuwa bado yuko ofisini kwake kitini akiwafikiria watoto wake. Taarifa kwamba Ditrov alisharejea zilimfurahisha akamtaka afike ofisini mara moja ili aeleze mpango aliokuwa nao.
“Tayari ninalo jibu.”
“Naomba unieleze.”

“Gharama yake ni kubwa lakini.”
“Gharama siyo muhimu, cha muhimu ni watoto wangu.”
“Tumegundua kwamba watoto hao wanaitwa Dorice na Dorica, wanategemewa kuanza darasa la kwanza wiki mbili zijazo. Ambacho tumepanga mimi na wenzangu tutakaofanya kazi hii ni kwenda huko Tanzania na kuthibitisha yote tuliyoyagundua, hatutaki kuamini mtandao moja kwa moja, tukishathibitisha kwamba ni kweli, watoto hao watatekwa siku watakayokuwa wanakwenda kuanza darasa la kwanza na wataletwa mpaka hapa Urusi.”

“Mtafanyaje ili isijulikane?”
“Watu ninaofanya nao kazi sitaki kukuficha ni waasi wa Chechnya ambao tumekubaliana kusafiri nao hadi Tanzania, ili kuudanganya ulimwengu, basi ambalo watoto hao watapanda litalipuliwa kwa bomu la kutengenezwa na waasi humo humo nchini Tanzania!”

“Kwa hiyo na watoto wangu watafia kwenye basi hilo?”
“Hapana wao watatolewa sekunde chache kabla basi halijalipuliwa kwa bomu, kitakuwa ni kitendo cha haraka, watu hawatakumbuka sababu ya hofu itakayowapata bomu likilipuka.”
“Watasafirishwaje hadi hapa?”

“Tulifanya utafiti na kugundua kuna ndege huwa zinasafirisha madini kutoka kwenye mgodi uitwao Deep Search Mining Company ambao uko katika mji mdogo uitwao Geita mkoani Mwanza. Ndege huwa zinaruka moja kwa moja kutoka mgodini hadi Canada, na tayari tumekwishafanya mazungumzo na mmoja wa marubani kwa malipo ya dola laki mbili ili baada ya kuwateka watoto hao wachukuliwe kwa ndege ya kukodi hadi mgodini na kupakiwa kwenye ndege itakayokuwa inaruka kwenda Canada. Huko tutakodisha ndege nyingine itakayoruka mpaka hapa, unauonaje mpango wetu?”

“Uko sawa, lakini swali moja najiuliza, kuna namna yoyote ile ya kuwafanya watoto hao wasiwe na kumbukumbu kabisa ya mahali walipotoka?”
“Tumelifikiria hilo bosi na uamuzi tulioufikia ni kwamba, baada tu ya kutekwa, watachomwa sindano ya dawa ya usingizi iitwayo Memory Eraser ambayo kazi yake ni kufuta kumbukumbu kwenye ubongo wa mwanadamu ili asikumbuke alikotoka fahamu zikimrejea.”
“Dawa hiyo ipo?”

“Ipo. Waasi wa Chechnya wanaitumia sana kupata wapiganaji, hiyo ndiyo tutatumia.”
“Oh! Ahsanteni sana, kwa utaratibu huo nimewapata watoto wangu.”
“Lakini gharama ya kazi yote hiyo ni dola milioni moja.”
“Nitawaongezea laki mbili juu yake kama mtafanikiwa kuwafikisha watoto hapa.”
Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 21


SIKU tatu baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati ya Ditrov na Victor, tayari kundi la vijana tisa lilikuwa likishuka ndani ya ndege ya shirika la ndege la Urusi kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, walionekana kama watu waungwana au wawekezaji waliokuja nchini Tanzania kuleta neema, jambo ambalo halikuwa kweli.

Walikuwa ni waasi wa kundi la Chechnya waliokodiwa na Ditrov kwa kazi moja tu; kuwateka Dorice na Dorica na kuwasafirisha hadi kwenye mji wa Novotroitsk na kuwakabidhi kwa Victor, kazi yao ingekuwa imekwisha na kukabidhiwa kitita kisha kurejea Grozny.

Mzungu mmoja ndiye aliyewapokea kwenye uwanja wa ndege, shati lake la khaki likiwa na nembo iliyoandikwa Deep Search Mining Limited. Alikuwa ni Meneja Mkuu wa mgodi huo uliokuweko katika mji wa Geita. Baada ya mazungumzo ya muda mrefu kwenye simu na kuingiziwa na Victor kiasi cha dola laki mbili kwenye akauti yake nchini Afrika Kusini, mzungu huyu alikuwa amekubali kuwasaidia Ditrov na vijana wake kukamilisha kazi iliyowaleta.

“My name is Mike Eaglewood. You are all welcome to Tanzania.” (Naitwa Mike Eaglewood. Wote mnakaribishwa Tanzania.)
“Thank you, a nice country.” (Asante, nchi nzuri.)
Wakatembea mpaka kwenye maegesho ya magari na kupanda ndani ya gari aina ya Combi, Mike akaketi kwenye usukani na kuendesha taratibu mpaka maeneo ya Masaki nyumbani kwake. Ilikuwa ni nyumba kubwa na aliishi peke yake, hiyo ilimfaa Ditrov na vijana wake sababu walihitaji usiri wa hali ya juu hasa katika kazi ya kutengeneza bomu ambalo lingelipua basi lililobeba watoto wa shule.

Kilichofanyika nusu saa baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo, hakikuwa kingine isipokuwa kikao cha kupanga mikakati ya utekelezaji, Mike akiwahakikishia kila kitu kingekwenda kama kilivyopangwa. Makubaliano yakafanyika kwamba yakodishwe magari mawili aina ya Benz ambayo yangetumiwa na kikosi hicho siku ya utekaji lakini pia kupeleleza mienendo ya familia ya Phillip.

Pia uamuzi ukafikiwa kwamba baada ya watoto kutekwa, wangesafirishwa kwa njia ya barabara ndani ya kontena lililofungwa viyoyozi wakiwa tayari wamechomwa sindano ya kupoteza kumbukumbu hadi Geita ambako ndege ingekuwa imeandaliwa kwa ajili ya kuwabeba na kuruka nao moja kwa moja hadi Canada.Victor akaamua kuongeza dola nyingine laki tano kwenye milioni moja aliyokwishatoa ili kufanya zoezi hilo lifanyike kwa urahisi.
“Zoezi la utekaji litafanyika siku gani?” Mike aliuliza.

“Siku watoto watakapokuwa wanapelekwa shuleni.” Ditrov akajibu.
“Mnaijua hiyo siku?”
“Ndiyo.”
“Mnaijuaje wakati nyie ndiyo mmewasili Tanzania?”
“Phillip na Genevieve wana blog yao, kila kitu wanachokifanya huwa wanaweka huko. Tumesoma mtandaoni.”

“Itakuwa siku gani?”
“Tarehe kumi na nne, kama siku kumi na mbili kuanzia sasa.”
“Tarehe tisa kuna kontena mbili zinaondoka hapa kwenda mgodini, tunaweza tukapakua mizigo kwenye moja ya kontena hizo na kupakia kwenye lori, halafu kontena hilo tukalifunga viyoyozi kisha tarehe kumi na nne kama mambo yatakwenda vizuri, tukaondoka na watoto hadi mgodini ambako tarehe kumi na tisa kuna ndege inaondoka kwenda Canada.”

Wote wakakubaliana juu ya mpango huo na Ditrov akajitolea kusafiri na watoto ndani ya kontena akiwalisha mpaka wafike Geita, kilichofuata baada ya hapo ni kazi ya kulitengeneza bomu, vijana wawili kati ya tisa kwenye kundi hilo walikuwa ni wataalam wa kutengeneza mabomu ya petroli yanayoweza kutegwa na kulipuka baada ya muda uliopangwa.

Kazi ya kutengeneza bomu kwa vifaa vilivyonunuliwa kwenye maduka na vituo vya mafuta jijini Dar es Salaam, ilikamilika siku ya tarehe kumi na tatu huku upelelezi juu ya shule ambayo watoto walitakiwa kupelekwa na gari asubuhi ya tarehe kumi na nne pia ukiwa mezani.

Kwa kutumia ushawishi wa fedha, Ditrov na kundi lake wakijifanya wafadhili walimzoea dereva wa gari hilo mpaka akawapa ratiba kamili ya kazi yake kwa siku na mahali alipoliegesha gari hilo baada ya kazi na kurejea nyumbani.

Ilikuwa ni kwenye ofisi ya CCM karibu kabisa na nyumbani kwake Magomeni Mapipa ambako pia walihakikisha wanaonekana kwa walinzi ili iwe rahisi kwao kurejea usiku na kutega bomu ndani ya gari bila kutiliwa mashaka wakijifanya walikuwa wakilirekebisha kabla dereva hajafika.

Kwa ushawishi huohuo wa fedha walimfanya mlinzi wa ofisi ya CCM asiwatilie mashaka, watano wakiwa wamemzubaisha kwa maongezi walipofika alfajiri kumwuulizia dereva, wanne walikuwa kwenye gari, wawili kati yao wakitega bomu chini ya gari hilo huku kifaa kiitwacho Ignitor ambacho waya wake uliounganishwa kwenye betri ya gari na kuanza kuzunguka kikihesabu saa tayari kwa bomu hili kulipuka mara tu Dorice na Dorica wakipakiwa ndani ya gari hilo.

Baada ya kazi hiyo waliingia ndani ya magari yao mawili aina ya Benz, wakimsubiri dereva ambaye kwa ratiba aliyowaeleza, gari lake lingeifika Upanga saa mbili asubuhi kwenye kituo ambacho Dorice na Dorica wangetakiwa kupanda.Walianza kulifuata taratibu kwa nyuma na kushuhudia likipakia watoto kituo kimoja baada ya kingine mpaka idadi ya watoto kumi na sita wakapanda, tayari likafika kwenye kituo cha Upanga ambako walimuona Genevieve amesimama na watoto wake, taratibu akatembea na kuwapakia gari liliposimama kisha kuanza kuwapungua mkono, jumla ya watoto kumi na nane wakawemo ndani ya gari hilo.

Benz moja likapita na kwenda mbele ambako lilisimama ghafla kulizuia gari la shule na Ditrov akiwa na mmoja kati ya vijana wake wa kazi alishuka akiwa na bastola mkononi na kwenda moja kwa moja kwenye dirisha la dereva na kumwekea shingoni huku kijana mwingine akifungua mlango na kuwatoa Dorice na Dorica kisha kuwakimbiza kwenye gari lao, kilikuwa ni kitendo cha haraka mno kilichochukua sekunde kadhaa kiasi kwamba watu wengi waliokuwa jirani hawakushuhudia.

Hazikupita hata dakika tatu, bomu likalipuka huku magari mawili aina ya Benz yakiondoka kwa kasi, ndani ya moja ya magari hayo Dorice na Dorica walikuwa wakipiga kelele huku wakichomwa sindano. Dakika chache baadaye walikuwa wakikoroma na safari iliendelea hadi Masaki, huko waliingizwa ndani ya kontena lenye viyoyozi, likafungwa na safari ikaanza.

Ulikuwa ni msafara wa makontena mawili mbele yakiwa yamebandikwa maandishi makubwa yaliyosomeka “POISON IN TRANSIT” kuonyesha kwamba ndani yake kulibebwa sumu, hii iliwafanya maaskari njiani washindwe kuyasimamisha. Dorice na Dorica walikuwa ndani wakisafirishwa huku watu wote wakiwemo wazazi wao wakidhani walikufa kwenye mlipuko wa bomu.

LILIKUWA ni tukio la kusikitisha, watu wengi walioona habari hiyo ya kulipuka kwa basi la wanafunzi na kuua watoto kumi na nane walilia machozi.

Tanzania ilikuwa imepatwa na msiba mkubwa ambao haukuwahi kutokea kabla, mpaka vyombo vikubwa vya habari duniani kama CNN, Sky News na BBC vilitangaza tukio hilo likidaiwa ni la kigaidi na kuhusishwa na Osama bin Laden, hakuna mtu hata mmoja aliyejua kilichotokea, kwamba mwenye watoto wake alikuwa ameamua kuwafuata.

Polisi walikuwa kazini usiku na mchana katika jiji la Dar es Salaam, mipaka yote ikiwa imefungwa, mamia ya vizuizi yakiwa yamewekwa barabarani, ukaguzi katika kiwanja cha ndege cha Mwalimu Nyerere ukiwa umeongezeka, upekuzi kwenye nyumba za wageni ukifanyika usiku na mchana kuwasaka watu waliohusika na tukio hilo ambalo kwa maelezo ya mashuhuda, walikuwa ni wazungu.

Juhudi zote hizi zikiendelea bila mafanikio, gari lililobeba kontena ambalo ndani yake walikuwemo Dorice na Dorica lilizidi kukata mbuga, likipita mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida hatimaye likafika Isaka mkoani Shinyanga na kukata kona kuelekea Kahama ambako lingenyoosha moja kwa moja hadi mgodini Geita.

Hakuna askari aliyediriki kunyosha mkono wake hewani kulisimamisha baada ya kuona maandishi ya POISON IN TRANSIT, wote waliamini ni sumu iliyokuwa ikisafirishwa kwenda pengine nchi za Rwanda, Burundi, Congo au migodini.
“Sumu hiyo.”

“Inawezekana inapelekwa migodini kwa ajili ya kulipulia miamba.”
“Ndiyo, hawa wazungu wanaleta tu sumu ambayo mwisho wa siku inaingia kwenye maji yetu ya kunywa na kutusababishia kansa.”
“Kwani unadhani wao wanajali sana afya zetu, cha muhimu kwao ni dhahabu, basi!”

“Inabidi serikali yetu ndiyo itulinde sisi wananchi.”
Hayo yalikuwa ni maongezi ya maaskari wa usalama barabarani na maafisa wa Mamlaka ya Mapato waliolishuhudia kontena likipita mbele yao,bila kuelewa kuwa kitambaa chenye maandishi kuonyesha ndani kulikuwa na sumu kilikuwa ni geresha, kwani kama wangelisimamisha na kuomba lifunguliwe wangemkuta Ditrov akipulizwa na kiyoyozi huku watoto wawili wakiwa wamelala bila fahamu kando yake.

Siku tatu baada ya kuondoka Dar es Salaam, gari hilo liliingia ndani ya ngome ya mgodi wa Deep Search Mining Limited usiku wa manane, wafanyakazi wengi wakiwa wamelala na Bwana Mike Eaglewood,

Mkurugenzi wa mgodi huo ambaye alielewa kila kitu kilichoendelea baada ya kupewa kitita cha fedha aliwaongoza mpaka kwenye uwanja wa ndege wa mgodi huo ambako ndege iliyokwishapakiwa shehena ya mchanga wa dhahabu kwa ajili ya kupelekwa Canada ilikuwa ikisubiri.

“Quickly!” (Haraka!) Bwana Eaglewood aliongea kwa sauti ya kuonyesha kwamba hapakuwa na muda wa kupoteza, kila kitu kilikuwa ni muhimu kifanyike kwa kasi ili ndege iruke kutoka kwenye uwanja huo akidai ilikuwa iimechelewa.
“Yes sir!” (Sawa mkuu.) alijibu Ditrov akimalizia kuwachoma Dorice na Dorica sindano ya kuharibu kumbukumbu.

Watoto hao wakashushwa wakiwa hawajui kinachoendelea na kupakiwa ndani ya ndege, kisha Ditrov na vijana wake pia wakaingia, cha kwanza alichokifanya ni kuwasiliana na Victor Fedorov na kumtaarifu juu ya mafanikio waliyoyapata na kumtaka aandae ndege ya kukodi kutoka Ottawa Canada kwenda Moscow ambako pia walitakiwa wakute ndege nyingine ya kukodi ambayo ingewapaleka moja kwa moja hadi kwenye mji wa Novostroitsk ambako Victor angewapokea.

Hayo ndiyo yakawa makubaliano na Victor akawahakikishia kwamba kila kitu kingekwenda kama walivyopanga, akiwaeleza kuwa alichohitaji si kingine isipokuwa watoto wake. Hivyo alikuwa tayari kutumia kiasi chochote cha fedha nje ya makubaliano ya awali ili mradi Dorice na Dorica waingie mikononi mwake, hicho ndicho kitu pekee alichoamini kingempa furaha.

Dakika kumi na tano baadaye injini za ndege ziliwashwa, mapanga yakaanza kuzunguka na ndege ikaanza kusogea mbele kisha kupaa na kuiacha ardhi ya Tanzania, Ditrov akatabasamu akiwaangalia wenzake.

“Give me five, mission accomplished.” (Nipe tano, mpango umekamilika.) akaongea Ditrov akiinua mkono wake wa kuume juu na kuanza kugonganisha na wenzake.

Ilikuwa ni safari ndefu yenye kuchosha lakini wao waliiona kuwa fupi sababu muda wote walikuwa wakinywa pombe, kuimba na kushangilia, fedha ambayo walikuwa wanakwenda kulipwa na Victor Fedorov ilikuwa kubwa mno, maisha yao yasingekuwa kama yalivyokuwa, wote waliamini tangu siku hiyo wangemiliki biashara kubwa na kujiepusha na mambo ya ugaidi.

Saa kumi na tatu baadaye walitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ottawa ambako muda mfupi tu baada tu ya ndege kutua na injini kuzimwa, mwanaume mrefu mwembamba aliingia kwenye ndege akiwa amevaa suti nyeusi na kuwaangalia watu wote walioketi vitini, kisha akamgusa Ditrov begani, ilivyoonekana alikuwa na maelezo ya kutosha kabisa ya mtu aliyekuwa akimtafuta.

“Carry the children and follow me!” (Bebeni watoto na mnifuate.) aliongea mwanamume huyo.

“Ok!” (Sawa.) Ditrov akaitikia na kunyanyuka alipokuwa ameketi na kuzunguka kiti cha kwanza, akambeba Dorice na kumuomba mmoja wa vijana wake ambebe Dorica, wakashuka hadi chini kulikokuwa na gari maalumu na kupanda,likaondoka na kutoka nje ya uwanja kupitia mlango wa nyuma na kuendeshwa hadi kwenye uwanja mwingine mdogo wa ndege ambako walipanda katika ndege ambayo nusu saa baadaye iliruka wakiwa pamoja na mwanaume aliyewaongoza.
“Where to?” (Tunaelekea wapi?) Ditrov aliuliza.
“Moscow.”

“Thank you.” (Asante.)
Watoto walikuwa bado wako usingizini, mpaka wakati huo walikuwa hawajaweka chakula chochote mdomoni, hata maji ya kunywa. Safari yao ilitegemewa kuwachukua muda wa masaa matano ndiyo watue kwenye uwanja wa ndege wa Sheremetyevo, jijini Moscow.

Kwa maelezo ya mtu aliyekuwa anawaongoza, ndege nyingine ya shirika hilo hilo la kukodisha ingewapeleka moja kwa moja hadi Novotroitsk na hapo ndio ungekuwa mwisho wa safari yao. Ditrov na watu wake walikuwa na furaha mno, walikuwa wakisubiri kitu kimoja tu mbele yao; kufika na kukabidhiwa kitita, kisha kusambaa.
***
Ilikuwa yapata majira ya saa tatu na nusu za usiku, mvua ilikuwa ikinyesha sana kwenye mji wa Novotroitsk, sababu ya baridi kali watu wachache sana walikuwa nje, wengi walijifungia ndani ya nyumba zao kuota moto.

Hali ilikuwa tofauti kwa Victor Fedorov, pamoja na utajiri wake wote, alikuwa uwanja wa ndege akiwa amebana kwenye moja ya kona, simu yake ikiwa kiganjani, subira yote hiyo ilikuwa ni kwa watoto wake, alitarajia wakati wowote kupokea simu kutoka kwa Ditrov ikimweleza kuwa tayari walishatua.

“Driiiii! Driiiii! Driiiii!” ulikuwa ni mlio wa simu yake, haraka akaipokea na kuiweka sikioni na kuanza kusikiliza.
“Ditrov?”
“Ndiyo.”
“Mmefika?”
“Ndiyo.”
“Subirini hapo hapo nakuja,” aliongea Victor na kuanza kutembea kwenda mahali alipoliacha gari lake na kuingia, kisha kuliwasha na kuondoka kuelekea kwenye lango la kuingilia uwanjani, askari akafika akitaka kujua ni nani alitaka kuingia uwanjani muda huo wa usiku.

“Ah! Mzee,” askari huyo alisema baada ya Victor kuvua kofia yake kichwani, aliheshimika mno kwenye mji huo na alikuwa na uwezo wa kufanya chochote serikalini hata kumuachisha au kumhamisha mtu kituo cha kazi kama tu angegombana naye, hii iliwafanya wafanyakazi wengi wa serikali wamwogope.
“Naomba nikampokee mgeni wangu.”
“Hakuna shida, pita tu”

Victor akaendesha gari lake mpaka ndani kabisa mwa uwanja mahali ilipoegeshwa ndege ya shirika la ndege la Cross Atlantic ambayo aliikodisha kuwasafirisha watu wake mpaka kwenye uwanja huo, mlango wa ndege ukafunguliwa, Ditrov na kundi lake akashuka wakiwa wamewabeba Dorice na Dorica ambao walikuwa bado wako usingizini, miili yao ikiwa imesinyaa sababu ya kukosa chakula na maji.

Wakapanda garini, kabla gari haijaondoka, Victor alishuka kwenye usukani na kuzunguka upande wa pili, akapanda na kuanza kuwabusu watoto mfululizo huku akilia kwa furaha na kukiri kwa mdomo wake kuwa hakuwahi kutarajia siku moja angewaona watoto waliotokana na mbegu zake ambazo aliziuza sababu ya umaskini.
“Huu ni ukombozi,” alisema maneno hayo akiliendesha gari lake kwa kasi kuelekea nyumbani, furaha aliyokuwa nayo ilikuwa ni kubwa mno, alitaka afike nyumbani haraka ili awachunguze vizuri watoto wake.

Je, nini kitaendelea watoto wakizinduka? Nini kinaendelea nchini Tanzania kwa sasa ambako inaaminika watoto hao wamelipukia ndani ya gari lililolipuliwa kwa bomu? Kitendawili cha mafuvu kumi na sita wakati watoto waliokuwemo ni kumi na nane kitateguliwaje?

je nini kiliendelea
 
SEHEMU YA 22


MVUA kubwa ilizidi kunyesha kwenye Mji wa Novotroitsk ikiambatana na baridi kali iliyofanya watu wengi wajifungie majumbani mwao. Gari aina ya Volga GAZ-24 (New Era) la kisasa lenye vioo vyeusi lilikuwa likikatiza kwenye ukungu mzito kutokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Novotroitsk kuelekea mahali yalipokuwa makazi ya Bilionea Federov. Ndani ya gari kulikuwa na wanaume wawili, Federov mwenyewe na mlinzi wake, Ditrov ambaye ndiye aliyekuwa kiongozi wa msafara ulioenda kuwateka Dorice na Dorica na kuwafikisha Urusi.

Kwenye siti ya nyuma walikuwa wamelala watoto wawili, Dorice na Dorica ambao hawakuwa wakijitambua kutokana na kuchomwa sindano ya dawa ya Memory Eraser iliyokuwa na kazi ya kufuta kumbukumbu kichwani. Miili yao ilikuwa imesinyaa kwani hawakula chochote tangu walipotekwa jijini Dar es Salaam wakati wakipelekwa shule hadi wakati ule.

Vijana wa kazi’ wa Kundi la Chechniya waliofanikisha kazi ile sambamba na Ditrov lilikuwa likiwafuata taratibu. Walikuwa wakielekea nyumbani kwa Federov kukabidhiwa mamilioni yao waliyoahidiwa baada ya kuikamilisha kazi ile.

Walipofika nyumbani kwa Federov, tafrija fupi ya kuwapongeza wote waliofanikisha zoezi lile ikafanyika na makabidhiano ya fedha walizoahidiwa yakakamilishwa. Kila kitu kilikuwa kikifanyika chini ya ulinzi mkali kuzuia siri ile isivuje na kutua mikononi mwa watu wasiohusika.

Siku ile ile daktari maalum akatafutwa na kupewa kazi ya kuhakikisha Dorice na Dorica wanarejea kwenye hali zao za kawaida lakini wakiwa hawakumbuki kitu chochote kuhusu maisha yao yaliyopita. Fedha ilitumika kisawasawa kwani waliongezwa dozi nyingine ya Memory Eraser, wakaachwa walale mpaka siku iliyofuatia.

Furaha aliyokuwa nayo Federov haikujificha. Hakuamini kuwa hatimaye kazi ile ya kuwarejesha mikononi mwake watoto wake imefanikiwa. Alikuwa na furaha kubwa ambayo ilimfanya amuongezee Ditrov mshahara mara tatu zaidi ya ule wa awali aliokuwa anaupata.

Siku iliyofuatia, Dorice na Dorica walirejewa na fahamu, kazi ya kuwalisha chakula bora ikaanza ili kufidia muda mrefu waliokaa bila kula chochote. Licha ya kuwa walikuwa wamerejewa na fahamu zao, hawakuonekana kukumbuka kitu chochote maishani mwao. Hata kula ilibidi waanze kufundishwa upya. Kila kitu kwenye vichwa vyao kilikuwa kimefutika kama kompyuta ‘iliyofomatiwa’.

“Hawa ni wanangu waliokuwa wanaishi barani Afrika, nimeamua kwenda kuwachukua baada ya kuona nimezidiwa na upweke,” alisema Federov wakati akiwatambulisha Dorice na Dorica mbele ya walimu watatu ambao aliwapa kazi ya kuhakikisha wanawafundisha kila kitu upya kwani hakuna walichokuwa wanakikumbuka.
Wakabadilishwa majina na kupewa ya Kirusi, Dorice akiitwa ‘Марина’ au Mahreenah (Marina) na Dorica akiitwa ‘Мария’ au Mahreeyah (Mariya).

Wakafundishwa lugha ya Kirusi na taratibu wakaanza kuzoea majina yao na mazingira mapya.
Walimu wale waliwafundisha kwa bidii kwani walikuwa wakilipwa mshahara mnono na ndani ya wiki moja wakawa na uwezo wa kutamka maneno machache ya Kirusi.

Wakaamini kuwa walizaliwa kwenye mazingira yale na Federov ndiyo baba yao kama walivyofundishwa na walimu wao. Walibadilika kwa kila kitu na hawakukumbuka chochote kuhusu Tanzania.

Siku zilizidi kusonga na watoto wale wakawa wanazidi kuzoea mazingira mapya. Waliendelea kufundishwa mambo mbalimbali ikiwemo tabia njema na maadili ya Kirusi, na taratibu wakaanza kufanana na watoto waliozaliwa eneo lile. Suala lile lilimpa faraja kubwa Federov, ule upweke uliomtesa kwa miaka mingi sasa ukabakia kuwa historia.

“Baba, kwani mama yetu yupo wapi?” Dorice ambaye sasa alikuwa akiitwa Марина (Marina) alimuuliza Federov jioni moja wakati wakitoka kwenye matembezi ya jioni.

“Mama yenu alifariki wakati mkiwa bado wadogo kwa ajali ya gari, lakini msiwe na wasiwasi kwani baba yenu nipo,” aliongea Federov na kuwafanya watoto wale waamini kile walichoambiwa.

Kwa jinsi alivyokuwa anawapenda, alihakikisha wanapata mahitaji yote muhimu yakiwemo chakula, mavazi mazito yasiyoruhusu baridi kupenya na kila kitu kilichokuwa muhimu kwao. Hakutaka wapate shida kabisa. Alipofikiria kuwaandikisha shule, walimu wao walishauri kuwa wanapaswa kuendelea kufundishwa nyumbani kwa angalau mwaka mzima mpaka watakapozoea kabisa mazingira.

***
Phillip alikuwa na kazi ya ziada baada ya tukio lile la ajali iliyohusisha gari la shule ambalo kila mtu alikuwa anaamini kuwa Dorice na Dorica nao walikuwa ndani yake mpaka wakati linalipuliwa na bomu. Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa mkewe, Genevieve ambaye alishindwa kukubaliana na ukweli kuwa hatawaona tena watoto wake, akapatwa na mshtuko mkubwa siku ile ya tukio na kupelekwa hospitalini kulazwa. Licha ya madaktari kujitahidi kwa kila namna kumsaidia, bado hakuweza kuzinduka.

“Amka mke wangu, kila kitu kinapangwa na Mungu. Tazama amewachukua watoto wetu na kuwatanguliza mbele za haki, na wewe unataka kuondoka? Nitabaki na nani kwenye hii dunia mimi?” Phillip alikuwa akilia pembeni ya kitanda alicholazwa Genevieve hospitalini na machozi yake yakawa yanamdondokea usoni.

Phillip akawa na kazi ya kuomboleza, kwanza kwa ‘kufiwa’ na wanaye, pili kwa hali aliyokuwa nayo mke wake kipenzi. Jitihada za kumrejesha Genevieve kwenye hali yake ya kawaida zilishindikana, akawa ni mtu wa kitandani saa zote.

Madaktari waliielezea hali ile iliyompata kuwa ni huzuni kali ambayo huumaliza nguvu na kuudhoofisha ubongo na kusababisha ushindwe kufanya kazi yake ipasavyo, hali ambayo husababisha mgonjwa kupoteza fahamu kwa kipindi kirefu.

“Inaonekana aliwapenda sana watoto wake, ubongo wake umeshambuliwa kwa kiwango kikubwa na uwezekano wa kurejea kwenye hali yake ya kawaida ni mdogo. Hata akizinduka atakuwa na tatizo la kuzimia mara kwa mara kwani ubongo wake utakuwa unazalisha chaji za umeme kila atakapokuwa anawakumbuka wanaye, hali ambayo ni hatari sana,” alisema daktari aliyekuwa akimhudumia wakati akimuelewesha Phillip hali ya mkewe.

Hilo lilikuwa ni pigo lingine kwenye maisha ya Phillip. Furaha yote aliyokuwa nayo wakati familia yake ikiwa imekamilika, ilipotea kama mshumaa uzimikavyo gizani, akawa ni mtu wa kuomboleza na kulia muda wote.

Hakuweza hata kuendelea na kazi yake kama awali, muda mwingi akawa anautumia hospitali kumuuguza mkewe ambaye kila siku hali yake ilikuwa inazidi kuwa mbaya.

“Eeeh Mungu, nimekukosea nini mimi mja wako mpaka kustahili mateso makali namna hii?” alisema Phillip akiwa pembeni ya kitanda cha mkewe wodini huku machozi yakimbubujika kama chemchemi ya maji.
PHILLIP alikuwa kwenye kipindi kigumu kuliko kingine chochote maishani mwake, kufiwa na watoto wawili pekee aliokuwa nao katika ajali pamoja na kuuguliwa na mkewe mpendwa ambaye alikuwa amepoteza fahamu baada ya kushuhudia mlipuko wa bomu ulioua watoto wake, hayakuwa matukio madogo, hakika yalivuruga kabisa akili yake na kutamani siku zirudi nyuma ile ya mlipuko wa bomu iondolewe katika historia ya maisha yake.

Kwa hali ilivyokuwa, akiwa amechanganyikiwa kabisa, baada ya kuzunguka huku na kule mikononi mwa matabibu wa kitaalam na kienyeji, akiongozana na baba mkwe wake, hatimaye aliamua kuandika barua ya kuacha kazi ili ajikite moja kwa moja kwenye tiba ya mkewe.

Maisha yalikuwa yamebadilika, kila siku alipobaki peke yake alilia. Genevieve alimuumiza sana moyo kwa alivyokuwa akiteseka, kichwani mwake hakuwa na kumbukumbu hata kidogo za yeye alikuwa nani, watoto wake walikuwa wapi, alionekana kama zezeta tu jambo lililomuumiza sana Phillip na kumfanya awe tayari kutumia kila alichokuwa nacho akitafuta tiba za mke wake mpendwa.

Pamoja na yote hayo, hakusahau jambo moja kubwa kuwaombea marehemu watoto wake na hata kutembelea kaburi lao kila siku ya Jumapili, huo ndio ulikuwa utaratibu wake wa maisha. Alimsikitikia sana mke wake kwa sababu hakuelewa chochote kilichokuwa kikiendelea na kila siku ya Jumatano ya kila wiki alilazimika kumpeleka hospitali.

“Hivi iko siku mke wangu atapona na kurejewa na kumbukumbu zake za nyuma?” alimuuliza Dk. John Lupimo, bingwa wa magonjwa ya akili katika hospitali ya Muhimbili.
“Ndio.”

“Tatizo lake ni nini?”
“Linaitwa kitaalam Amnesia.”
“Amnesia? Ndio nini? Na inasababishwa na nini?”

“Ni tatizo la ubongo pale hasa unaposhindwa kuyavuta mafaili ya kumbukumbu kutoka kwenye stoo zake au kushindwa kutunza kumbukumbu, husababishwa na magonjwa ya akili au wakati mwingine ajali kwenye kichwa.

Hii ndio iliyotokea kwa Genevieve baada ya kushuhudia gari lililowabeba watoto wake likilipuka, akaanguka chini na kupiga kichwa ardhini.”
“Sasa itakuwaje?”

“Tunampa dawa iitwayo Amytal, hii inasaidia kurekebisha kumbukumbu, ipo siku Genevieve atarejea kwenye hali ya kawaida, hutaamini!” Daktari aliongea na kumfanya Phillip atabasamu, kauli hiyo ikawa imempa matumaini makubwa kwamba siku moja mke wake atarejewa na fahamu zake ili wote wawili wachangie maumivu ya kufiwa na watoto wao ambayo Genevieve hakuwa na habari nayo sababu ya tatizo lake la akili.

Kadiri siku zilivyozidi kusonga wakiwa wodini, ndugu na jamaa wakifika kuwasalimu, hali ya Genevieve iliendelea kuwa mbaya siku hadi siku, akazidi kukonda sababu ya kutokula chakula, matumaini yake ya chakula yakawa ni kwenye mpira kupitia puani au dripu.

Yote hayo hayakuweza kusaidia, hatimaye mwezi mmoja baada ya bomu kulipuka, Genevieve akaaga dunia na kuzikwa kando ya kaburi la watoto wake, katika mazishi yaliyohudhuriwa na maelfu ya watu wengi waliomlilia, Phillip alilia kama mtoto mdogo na kuzimia mara kadhaa.

“Life has no meaning any more, I better die!” (Maisha hayana maana tena, bora nife!) Phillip aliongea akibubujikwa na machozi mbele za watu waliokusanyika kumfariji, wengi wakiwa ni wafanyakazi wenzake pamoja na familia ya Phillip.

Baada ya mazishi Phillip hakuongea tena, muda wote akawa kimya kuliko ilivyokuwa kawaida yake, alitambulika kama mtu mcheshi mwenye mazungumzo kwa ajili ya kila mtu lakini sasa akachagua kubaki kimya sababu ya simanzi

alilokuwa nalo. Kitu kingine kilichojitokeza ni wakati wa usiku, alipiga kelele na kudai mke na watoto wake walikuwa wakimtokea na kumwambia awafuate, jambo ambalo hakuna hata mmoja aliyelithibitisha ingawa yeye alidai kila siku dirisha la chumba chake liligongwa na akaitwa jina.

Habari hii iliwashtua watu wengi na kuwafanya waamue kuwa wanakesha usiku ili waone kama kweli kilichodaiwa na Phillip kilikuwa ni cha kweli, wiki nzima baadaye hakuna aliyewaona Genevieve na watoto wake wakipita, hiyo kathibitisha kabisa kwamba Phillip alikuwa akinyemelewa na tatizo la akili, hii ilifanya siku chache baadaye abembelezwe na kukubali kupelekwa kwa daktari ambako awali alikuwa hataki kwenda akidai yeye alikuwa mzima wa afya.

“Kila siku mke na watoto wangu wanakuja kunigongea wakitaka niongozane nao, mimi sitaki kwenda huko ambako wao wanaishi, kuna mateso sana, hivi njia ya kwenda Kigoma inapitia Kigamboni? Ng’ombe na mbuzi yupi ni paka?” aliongea sentensi nyingi zisizo na maana.

Tayari daktari akawa ameshaligundua tatizo lake, hapohapo hakupoteza wakati, akatoa maamuzi kwamba mgonjwa alazwe kwenye wodi ya wagonjwa wa akili kwa matibabu ili pia awe anakutana na mtoa nasaha ambaye angebadilisha maisha yake baada ya kufiwa na mke pamoja na watoto wake.

Akaanza kupewa dawa ambazo hazikumsaidia chochote, aliendelea kuwa kimya huku mara kwa mara akilia na kuwaita mke na watoto wake. Kibaya zaidi alianza tabia ya kutupa nguo na kutembea utupu bila kujali heshima yake, hii ilifanya madaktari wamwandikie dawa zilizomfanya alale kwa muda mrefu ili kusaidia akili ikae sawa.

Dawa hizo ziliposimamishwa wiki mbili baadaye, angalau aliweza kujisikia vizuri, madaktari wakaridhika kabisa na kuamua kumruhusu arejee nyumbani kuendelea na dawa taratibu.

Huzuni yake ilikuwa pale pale, kila alipoyaona makaburi ya mke na watoto wake alipokwenda kuyatembelea alilia mno. Hakika alitamani kufa, akazidi kukonda sababu ya mawazo na hakujijali tena, wengi walimchukulia kama mtu aliyechanganyikiwa na akili sababu ya matatizo yaliyomkuta, alitembea sehemu nyingi akiongea peke yake.

“Hallow!” ilikuwa ni sauti ya mwanamke nje ya duka kubwa la Imalaseko ambako Phillip alikuwa akipita, akageuka na kuangalia upande sauti ilikotokea.
“Ndio dada.”
“Wewe ni Phillip?”

“Ndio, wewe ni nani? Sauti yako sio ngeni.”
“Nini kilitokea mpaka ukawa hivi?”
“Maisha tu dada yangu. Dunia inazunguka kwenye mhimili wake, watu tunaingia na kutoka.”

“Nimesikitika sana.”
“Kila mtu anayeniona anasikitika. Wewe ni nani lakini?”
“Unataka kunifahamu?”
“Ndio.”
“Njoo ndani ya gari yangu tuongee, nitakukumbusha kila kitu.”
“Kweli?”
“Ndio.”

“Naogopa kuingia kwenye gari lako!”
“Hakuna sababu ya kuogopa, wewe njoo tu nataka kukuonyesha jambo.”

“Mh!” Phillip aliguna, taswira ya Zamaradi ikamwijia kichwani, akaanza kuhisi pengine mtu huyo aliyekutana naye alikuwa jini ambaye angeweza kumdhuruHata hivyo, baada ya kusisitiziwa sana alijikuta anakubali na kuingia ndani ya Land Cruiser mpya ya rangi ya fedha, akaketi kitini kando ya dereva ambaye alikuwa ni mwanamke aliyekutana naye.
“Unataka kufahamu mimi ni nani?”
“Ndio.”

“Subiri!” mwanamke huyo aliongea akijifunua wigi usoni mwake, akaiondoa pia sura ya bandia na yake halisi kuonekana. Macho yakamtoka Phillip kwa mshangao akiwa amejifunika kwa mikono yake yote miwili mdomoni, bila kusema chochote alianza kulia.
“Usilie ndio dunia.”

Je, mwanamke huyo ni nani? Nini kinaendelea kwa watoto Dorice na Dorica ambao tayari wapo nchini Urusi wakiwa wamepoteza kumbukumbu zote za Tanzania na
wazazi wao baada ya kuchomwa sindano ya dawa iitwayo Memory Eraser ambayo hutumika kufuta kumbukumbu kwenye ubongo wa mwanadamu ili aanze upya kujifunza? Majina yao hivi sasa si Dorice na Dorica tena bali ni Mariya na Merina.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 23


BASI la shule lililobeba watoto kumi na nane linalipuliwa kwa bomu, watoto wote wanakufa palepale lakini baadaye yanapatikana mabaki ya watoto kumi na sita tu! Hiki kinakuwa ni kitendawili kwani kila mtu alikuwa na uhakika watoto waliopanda ni kumi na nane.

Ukweli wa tukio hili ni kwamba, watoto wawili (Dorice na Dorica) waliondolewa kwenye gari na watekaji kabla ya bomu kulipuliwa. Watekaji hao walitumwa na Victor Federov, Mrusi bilionea asiye na mtoto ambaye wakati wa umasikini wake aliwahi kuwauzia Phillip na Genevieve mbegu zake za kiume.

Phillip na mke wake Genevieve hawaelewi juu ya jambo hili, wanalia kwa kupoteza watoto wao wawili katika ajali hiyo mbaya iliyomfanya Genevieve aanguke chini na kupoteza fahamu, mshipa wa damu ukapasuka kwenye ubongo kwa sababu ya kupanda kwa shinikizo.

Maisha ya Phillip baada ya hapo yanabadilika, akawa na kazi moja tu ya kumuuguza mke wake mpaka alipofariki na kufanya jumla ya watu waliofariki kwenye familia yake kufikia watatu. Amechanganyikiwa na kuwa kama mwendawazimu, akitambea na kuongea peke yake njiani.

Kwa msaada wa ushauri wa kisaikolojia aliopewa hatimaye alirejea katika hali ya kawaida, ndipo akakutana na mwanamke nje ya duka kubwa la Imalaseko katikati ya jiji, wakapanda kwenye gari kwa ajili ya maongezi, mwanamke huyo alipovua wigi na kujifunua uso wake, Phillip alishtuka na kuanza kulia.
Je, nini kitaendelea? Mwanamke huyo ni nani? SONGA NAYO…

“NINI kilikupata dada yangu?”
“Hunikumbuki?”
“Kabisa.”
“Mbona umelia?”
“Nakuonea huruma.”

“Nikikusimulia historia ya maisha yangu utanikumbuka, umewahi kuwa na rafiki msichana aliyeungua vibaya ndani ya gari?”
“Wewe ni Lina?!” Phillip aliuliza tena mshangao macho yakiwa yamemtoka, hakuwa tayari kuamini kama kweli msichana aliyekuwa mbele yake ndiye Lina aliyewahi kuwa msichana mrembo ambaye sasa uso wake ulikuwa umejaa makovu.

“Ni mimi, habari za siku nyingi Phillip?”
Phillip hakujibu, akaendelea kububujikwa na machozi, kichwani mwake taswira ya Lina wa zamani ilikuwa ikionekana, hakika alikuwa ameharibika, uso wake ukiwa umejaa makovu makubwa, ilivyoonekana upasuaji wote wa kumrekebisha sura haukuwa na mafanikio makubwa kwani sura yake ya awali haikurejea. Hasira nyingi sana akazielekeza kwa Zamaradi.

“Nisamehe!” Phillip alisema neno hilo pekee kwikwi ya kulia ilipomwachia.
“Kwa kipi Phillip?”
“Nahusika sana na ajali yako.”
“Unamaanisha nini? Ulijua itatokea? Ilikuwa ya kupangwa?”
“Hapana, ni historia ndefu naomba tu unisamehe.”

“Hakuna shida, naweza kukusamehe lakini ni vizuri ukanieleza pia ni kwa nini unaniomba msamaha?”
Phillip akajifuta machozi kisha kuanza kumsimulia Lina kila kitu kuhusu maisha yake, namna alivyoishi katika dunia mbili tofauti, inayoonekana na isiyoonekana akiwa mume wa Zamaradi, jini mwenye hasira ambaye alimshambulia kila mwanamke aliyemtaka kimapenzi. Lina alikuwa kimya akisikiliza.

“Ndiyo maana nilikuwa sikubali uhusiano wa kimapenzi na msichana yeyote, lakini mabinti walinilazimisha na Zamaradi akawadhuru, ajali yako ilisababishwa na Zamaradi, yeye ndiye aliyemuua Monalisa pia katika ajali! Nisamehe sana kwa yaliyotokea, haikuwa nia yangu.”

“Mh! Hii ni habari mpya, sikuwahi kufahamu jambo hili.”
“Huo ndiyo ukweli.”
“Huyo Zamaradi yuko wapi sasa?”

“Nilipokutana na marehemu mke wangu na kuamua kuwa na uhusiano naye kimapenzi, Zamaradi alijaribu kutushambulia lakini kwa sababu tulikuwa tumekabidhi maisha yetu kwa Mungu na tulilindwa saa ishirini na nne alishindwa kutudhuru, tangu siku hizo sikuwasiliana tena na ulimwengu usioonekana, nikamuoa mke wangu na kuzaa watoto wawili mapacha ambao sasa wote wameniacha!”

“Pole sana, nimesikia kila kitu kilichotokea, tuyasahau ya zamani tuangalie ulimwengu unaofuata mbele yetu.”
“Umeolewa?”
“Hapana, bila shaka hakuna mwanaume ambaye anavutiwa na mimi kwa jinsi nilivyo.”

“Usiseme hivyo, mshukuru Mungu.”
“Ahsante kwa kunitia moyo lakini mimi pia nataka nikuambie hata kama umepoteza mke na watoto wako, simama imara, endelea na maisha, usivunjike moyo, unakumbuka sura yangu mimi?”
“Ndiyo”

“Ilikuwa ya kuvutia, nikaipoteza katika ajali ya moto lakini bado nilisonga mbele, baada ya upasuaji wa kurekebishwa kufanyika, angalau kuwa hivi nilivyo niliendelea na masomo kwa msaada wa Umoja wa Mataifa mpaka nikapata shahada mbili za Uchumi na kuajiriwa nchini Marekani, nimehamishiwa hapa mwezi uliopita kuwa Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP!”

“Kweli?”
“Ndiyo”
“Umenitia moyo.”
“Hivyo ndivyo maisha yalivyo Phillip, Wazungu wanasema life is a series of events, yaani maisha ni mfululizo wa matukio, linaondoka hili linaingia lile, hivyo unatakiwa kusimama imara.”

“Ahsante sana.”
“Unaelekea wapi hivi sasa Phillip?”
“Nazungukazunguka tu!”
“Karibu nyumbani basi.”
“Hakuna shida twende nikapafahamu.”

Lina akashuka na kuzunguka upande wa pili ambako alikaa kwenye usukani, akawasha gari na kuondoka moja kwa moja kupitia Barabara za Ohio, Ali Hassan Mwinyi na baadaye Haile Selasie kuelekea Masaki ambako Lina alipiga honi kwenye jumba lenye lango kubwa na likafunguliwa.
“Mh!” Mlinzi akaguna.

“Vipi?”
“Gari ni lenyewe, sauti ni ile ile akini bosi siye.”
“Mungu wangu…” Lina aliongea akijigusa kichwani na usoni, alikuwa amesahau kuvaa wigi na sura yake ya bandia ndiyo maana mlinzi wake akashtuka, kwa muda wote walioishi pamoja hakuwahi kumwonesha jinsi alivyokuwa.

“Wewe fungua lango, mambo mengine hayakuhusu.”
“Bosi haruhusu wageni kuingia bila miadi.”
“Nakuambia fungua, unataka kazi au?”
“Eebwana ee, usinizingue, rudi kinyumenyume egesha pale nje umsubiri mpaka aje.”

“Sawa, ngoja nikamlete.” alijibu Lina na kuanza kurudi kinyumenyume bila ubishi, akaligeuza gari kwa kasi na kuondoka hadi barabarani ambako alizunguka upande wa pili na kuvaa wigi pamoja na sura yake ya bandia, akarejea tena kwenye usukani na kuendesha kwenda nyumbani kwake ambako baada ya honi lango lilifunguliwa.

“Karibu bosi!”
“Ahsante sana.”
“Walikuwa wamekuacha barabarani?”
“Ndiyo, kazi nzuri sana, nilitaka kukujaribu ili nione kama watu wanaweza kuingia hapa kwangu kwa urahisi tu. Safi sana, chukua hii elfu kumi utakunywa soda”

“Teh! Teh! Teh! Ahsante bosi nitaendelea kufanya kazi kwa uaminifu mkubwa.”
Gari likaingizwa ndani ya kuegeshwa sehemu yake, Lina akashuka na kumfungulia Phillip mlango kisha kumwita mlinzi na kumtambulisha kwamba huyo alikuwa rafiki pekee aliyeruhusiwa kumtembelea wakati wowote usiku na mchana bila kizuizi, Phillip na mlinzi wakashikana mikono.

“Naitwa Phillip.”
“Mimi ni Marwa, kutoka Taa-rime!”
“Nafurahi kukufahamu.”
“Na mimi hibyo, hibyo!”

Phillip na Lina wakaanza kupandisha ngazi kuingia ndani ambako tofauti na watu wenye uhusiano wa kawaida, Lina akaanza kumtembeza Phillip kwenye nyumba yake kuanzia jikoni kisha kupandisha ngazi hadi kwenye chumba chake cha kulala ambako aliketi kitandani na kumwomba Phillip afanye hivyo hivyo.
“Kaa tu usiogope, hakuna tatizo, jisikie uko nyumbani.”

“Ahsante.”
Kwa mara ya kwanza tangu apoteze familia yake, Phillip alijisikia faraja ya kweli moyoni mwake, akaketi kitandani kando ya Lina na wakaanza kuongea mambo mbalimbali kuhusu maisha tangu walipoachana, Lina hakuficha ukweli wake kwamba tangu aungue kwa moto hakuwahi kukutana na mwanaume hata akamwambia neno “Nakupenda” ingawa alikuwa na mafanikio makubwa mno maishani mwake.

“Pole!”
“Ahsante Phillip.”
“Nakupenda.”
“Kha!”
“Mbona unashangaa?”
“Una uhakika?”

“Ndiyo.”
“Hausemi tu kwa sababu una mfadhaiko baada ya kupoteza mke na watoto?”
“Hapana, nakupenda Lina, nilivutiwa na wewe wakati ule ukiwa na sura ile, sidhani kama nahitaji kubadilika leo ukiwa na sura hii, upendo wangu ni wa kweli, naomba uniamini.”

“Ghafla mno…”
“Mapenzi ya kweli hayana maandalizi, isitoshe mimi ndiyo chanzo cha yote yaliyokukuta, naomba uamini nakupenda. Wewe ndiyo utakuwa faraja ya mtima wangu, utanipunguzia maumivu niliyonayo ndani, nikiwa na wewe nitakuwa mtu tena”

Lina akainamisha kichwa chake chini, machozi yakaanza kudondoka na kulowanisha sakafu. Phillip akamsogelea na kumnyanyua, kisha kumkumbatia, akamvua wigi na sura ya bandia, halafu akamlaza chali kitandani na kuanza kumpiga mabusu mfululizo. Hisia za Lina zikawa kama mtu aliyekuwa akipigwa na shoti ya umeme.
“Usinishangae Phillip, ni miaka mingi sijakutana na jambo hili.”
“Basi leo ndiyo leo.”


KILIKUWA chumba chenye ukubwa usiopungua mita za mraba hamsini, kilijazwa samani nyingi zenye thamani kubwa, ukutani kukiwa na picha kubwa ya mwanaume akiwa na watoto wawili mapacha. Mwanaume kwenye picha hiyo ndiye aliyekuwa ndani ya chumba hicho akiwa ameketi nyuma ya meza kubwa, akiiangalia picha kubwa iliyokuwa mbele yake kwa umakini, ghafla akatabasamu.
“Siwezi kuamini kama hawa watoto wako mikononi mwangu!” aliwaza Victor Federov.

Moyo wake ulikuwa umejaa furaha kubwa kupindukia, ujio wa Dorice na Dorica ambao hivi sasa waliitwa Mariya na Marina ulifanyika kwa wakati muafaka. Kitu pekee kilichomsumbua akilini mwake ni kwa namna gani angeweza kuificha siri hiyo isivuje, kwani aliwahusisha watu wengi katika zoezi la utekaji na alielewa duniani hapakuwa na siri ya watu wawili, lazima siku moja kama si Ditrov basi watu aliokuwa nao, mmoja lazima angefungua mdomo na kuueleza ulimwengu namna watoto wake walivyopatikana. Mawazo hayo yalimfanya auchukue mkono wa simu uliokuwa kando yake na kuanza kupiga namba ya Ditrov.

“Ndio mkuu.”
“Uko wapi?”
“Ofisini kwangu.”
“Naomba uje haraka.”
“Sawa.”
Simu ikakatika.

Dakika tano baadaye mlango wa ofisi yake ukagongwa na Ditrov akaingia na kuketi mbele ya meza ya Victor. Mwili wake ulikuwa umeongezeka zaidi sababu ya mazoezi, fedha nyingi aliyolipwa katika zoezi la kuwateka Dorice na Dorica ilikuwa imebadilisha kabisa maisha yake, sasa hakuhangaikia mambo madogo madogo tena, mara nyingi baada ya kazi alitumia muda mwingi kwenye jengo la mazoezi.

“Ndio bosi nimeitika wito.”
“Ahsante, suala langu sio kubwa, nataka kukuuliza kama watu wote ulioshirikiana nao kwenye operesheni hii unawafahamu!”
“Sana, ni rafiki zangu.”
“Wakati wowote unaweza kuwapata?”
“Bila shida.”

“Sasa sikiliza.”
“Ndiyo.”
“Duniani hakuna siri ya watu …?”
“Wawili.”
“Ningependa kuona watu hawa wote wanakufa.”
“Mh!”

“Mbona umeguna? Nitalipa dola laki tano.”
“Kweli?”
“Bila shaka.”
“Kama dola laki tano zipo, mimi naweza kufanya hivyo kazi bila matatizo. Ni kiasi cha kutafuta Blood Pressure Uplifter, ambayo wakishainywea kwenye chai au kinywaji chochote, shinikizo la damu litapanda na watakufa mmoja baada ya mwingine.”

“Unaweza kufanya hivyo?”
“Bila matatizo, ndiyo kazi yangu.”
“Hiyo dawa utaipata wapi?”
“Ninayo.”
“Kabisa?”

“Tangu enzi za KGB,” Ditrov aliongea akimaanisha Shirika la Ujasusi la Urusi ambalo aliwahi kulifanyia kazi miaka mingi kabla.
“Basi kama ni hivyo, tekeleza.”
“Fedha yangu?”
“Ukimaliza kazi njoo unione.”

“Ahsante.”
Ditrov akaondoka kichwani mwake akifikiria dola laki tano ambazo angelipwa akimaliza kazi ya kuwaua watu wote alioshirikiana nao kwenye zoezi la utekaji, alielewa ingekuwa kazi rahisi sababu wote walimwamini. Alichokifanya kuanzia siku hiyo ni kuwa anawaita mmoja baada ya mwingine na kumpakia ndani ya gari lake hadi ufukweni mwa bahari kwa ahadi kwamba walikuwa wanakwenda kupunga upepo, huko aliitoa dawa hiyo na kumchanganyia mlengwa kwenye kinywaji, dakika chache baada ya kunywa hali ilibadilika, Ditrov akambeba ndani ya gari, njiani alikufa.

Alichokifanya ni kutumia boti maalum aliyopewa na Victor Federov kuubeba mwili huo mpaka katikati ya bahari ambako aliufunga jiwe na kuuzamisha hadi kwenye kina cha maji, akiamini huko usingeonekana milele. Alifanya hivyo mpaka akawamaliza wote, akimpa taarifa Victor Federov juu ya maendeleo.
“Hongera sana, njoo ofisini leo usiku kama saa saba hivi uchukue hundi yako.”

“Nakuja bosi.”
Katika muda huo huo aliopangiwa, ofisi ikiwa haina mtu, Ditrov alipandisha ngazi mpaka ofisini kwa Victor Federov ambako alipokelewa kama shujaa, akaketi kusubiri hundi yake, Victor alipofungua droo, badala ya kutoka na kitabu cha hundi, mkono ulitoka ukiwa na bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti.

“Nilikuambia duniani hakuna siri ya watu wangapi?”
“Wawili.”
“Inabidi Ditrov ufe ili nibaki peke yangu.”
“Hapana mzee nisamehe.”
“Paa! Paa! Paa!”

***
Kitanda kilikuwa kinacheza kama vile ni cha spiringi, ingawa kilitengenezwa kwa mbao imara za mninga, Phillip alikuwa kazini akijituma impasavyo mwanaume aliyekuwa akitafuta sifa. Alitaka kumwonyesha Lina kwamba uzuri wake haukuwa umbile la sura tu, bali hata kwenye ukanda wa sita kwa sita alikuwa ni mtaalam haswa.

Lina alikuwa akilia, si kwa maumivu bali kwa raha aliyokuwa akiipata. Ilikuwa imepita miaka mingi tangu akutane mara ya mwisho na mwanaume kimwili, moto uliomteketeza uliondoka na uzuri wake wote, hivyo hakuna mwanaume aliyevutiwa naye labda kwa wale walioangalia maumbile, maana mtaji peke yake aliokuwa nao ulikuwa ni hips zilizochomoza kama vilele vya mlima Meru!

Miili yao ilikuwa imelowa kwa jasho ingawa kulikuwa na kiyoyozi chumbani kilichoonyesha joto lilikuwa sentigredi kumi na nane. Mashuka yote yalikuwa yamelowa, kijana Phillip akiwajibika, kwake kitendo cha ngono kilikuwa ni njia ya kumsahaulisha yaliyokuwa yakimsumbua akilini mwake, aliichukulia ni kama faraja.

“Ahsante!” Lina alitamka maneno hayo Phillip alipojitupa kando yake.
“Karibu.”
“Sijawahi.”
“Hujawahi nini?”
“Kukutana na mtu wa aina yako, umezidi kunitia uchizi.”
“Nakupenda Lina.”

“Nakupenda pia Phillip, miaka yote, kama uliyoyasema ni kweli, basi mapenzi yangu kwako ndiyo yalinisababishia hata huu ulemavu.”
“Ndio maana niko na wewe, ndio njia pekee ya kukulipa kwa kile ulichopoteza kwa ajili yangu.”

Wakakumbatiana, Lina akiwa tayari kuanza tena lakini Phillip alimshauri wapumzike. Nusu saa baadaye ndipo walipoendelea mpaka usiku wa manane, kiasi kwamba Phillip hakuweza kuondoka tena, huo ndio ukawa mwanzo wa kuishi ndani ya nyumba hiyo akifarijiana na Lina ambaye kwake Phillip alikuwa kila kitu. Miezi sita ikapita na taarifa za uhusiano wao zikaenea kila mahali, wazazi wa Genevieve wakafurahishwa na jambo hilo wakiamini Phillip angesahau maumivu aliyokuwa nayo.

“Kuna jambo nataka kukueleza.”
“Jambo gani?” Lina aliuliza.
“Nimefikia uamuzi wa kukuoa, wewe peke yako ndiye unaweza kunisahaulisha vifo vya mke na watoto wangu,” alisema Phillip.

Hakuwa na habari kabisa juu ya kilichotokea, kwamba watoto wake hawakuwa marehemu bali walitekwa na vijana wa Victor Federov.
“Unasema kweli Phillip?”
“Kweli kabisa.”
“Nipo tayari.”

JE NINI KILIENDELEA
 
SEHEMU YA 24


“Lakini kuna kitu kimoja tu nataka kukueleza, kama utakubaliana nacho basi tutafunga ndoa yetu ili tuishi kwa furaha, kikikushinda basi tena maana mimi sina la kufanya, ni maumbile na sitaki kurudia tena kufanya kitendo nilichokifanya huko nyuma.”

“Kitu gani hicho unachotaka kunieleza, usizunguke, niambie tu.”
“Bila shaka nimewahi kukueleza kwamba nina uwezo wa kutoa mbegu za kiume lakini hazina uwezo wa kurutubisha yai la mwanamke, hii ina maana kama tukioana hatutakuwa na uwezo wa kuwa na motto. Je, hilo ni kikwazo kwako?”
“Hapana hata kidogo, cha muhimu kwangu ni kuwa na mtu anayenipenda, watoto ni majaliwa ya Mungu.”

“Ahsante Lina,” Phillip aliongea akimvuta na kumkumbatia, kilichofuata baada ya hapo ni sauti zao kuendelea kushuka huku wakinong’ona, neno I love you, likisikika mara nyingi, ghafla ukimya ukasikika na milio ya “Jwig!Jwig!Jwig!” ikasikika! Kilikuwa ni kitanda kikipiga kelele. Phillip alikuwa kazini akifanya kila alichoamini alikuwa na utaalam nacho ingawa hakuwa na uwezo wa kupata mtoto.

Siku iliyofuata kazini Lina alikuwa na jambo moja tu, kuwataarifu rafiki na wafanyakazi wenzake juu ya kilichokuwa kikifuata maishani mwake. Kila mtu akawa na hamu ya kumwona Phillip, aliyejitolea kumuoa Lina. Siku ya siku ikafika, Phillip akatambulishwa kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam kwenye tafrija ndogo iliyofanyika katika Hoteli ya

Johannesburg, ambayo pia Phillip aliitumia kumvisha Lina pete ya uchumba.
Kamati ikaundwa na utaratibu wa michango kama ilivyozoeleka nchini Tanzania ukafuata. Kiasi kikubwa cha fedha kikakusanywa na hatimaye harusi kubwa tena ya kifahari iliyosimamiwa na familia ya Lina pamoja na familia ya Genevieve na ndugu wa Phillip ikafanyika, ndoto ya Lina kuolewa na Phillip ikatimia.

Wakaanza kuishi pamoja kama mke na mume, katika maisha yaliyojaa furaha, huzuni zote zilizokuwa zimewafunika zikaondoka ingawa Phillip hakuisahau familia yake. Kila Jumapili ilikuwa ni lazima asindikizwe na mke wake wakiwa njiani kuelekea kanisani hadi makaburini ambako alisali akimkumbuka mke wake Genevieve na watoto wao Dorice na Dorica.

Hakuwa hata na hisia kidogo kwamba watoto wake walikuwa upande wa pili wa dunia, nchini Urusi wakiishi na baba yao wa kuwazaa, pia wakiwa hawana kumbukumbu ya mahali walikotokea baada ya kumbukumbu zote kufutwa kichwani kwa sindano za dawa iitwayo Memory Eraser.
***
Ditrov alikuwa amelala sakafuni, risasi mbili zikiwa zimepenya mwilini. Kulikuwa na dalili zote kwamba alikuwa amekufa na Victor akiamini siri yake ya kuwatorosha Dorice na Dorica kutoka Tanzania isingevuja, alisogeza mfuko mkubwa wa nailoni aliokuwa ameuandaa kwa ajili ya kazi hiyo na kuanza kumwingiza ndani yake huku mwili wake wote ukitetemeka.

Alikuwa na uhakika asilimia mia moja hakuna mtu angegundua kilichokuwa kikiendelea, taratibu akausogeza mfuko kando na kuanza kuisafisha sakafu mpaka alipohakikisha imetakata bila doa lolote la damu, akaunyanyua tena mfuko na kuupeleka mpaka kwenye lifti. Alipoingia ndani akabonyeza alama iliyoandikwa G, ili kuiamuru lifti ishuke moja kwa moja mpaka chini kulikokuwa na maegesho ya magari.

“Afande! Afande! Afande!” aliita alipotoka kwenye lifti bila kuuchukua mwili wa Ditrov, alitaka kuhakikisha hakuna mtu eneo hilo, ukimya ulimthibitishia kwamba aidha askari alikuwa amelala au alikuwa amepandisha juu kwa walinzi wenzake.

Akarejea kwenye lifti na kufungua, akaubeba mwili mpaka kwenye gari na kufungua buti kisha kuuingiza ndani na kufunika. Kwa kasi akazunguka upande wa dereva na kufungua mlango, akawasha na kuondoka kwa kasi, sehemu ya kutokea askari walimsimamisha lakini walipogundua ni bosi wao hawakuwa na swali.

“Nahitaji jiwe, kamba ninayo,” aliwaza akiendesha gari kuelekea nyumbani kwake.

Nyumba yake ilijengwa ufukweni kabisa na alimiliki boti iendayo kasi, hiyo ndiyo alipanga kuitumia kwa ajili ya kazi iliyokuwa mbele yake. Bahati nzuri hakuwa na mlinzi, alitumia mbwa na nyaya za umeme, hivyo alichofanya baada ya kuingia ndani ya ngome yake kabla hajafungua buti na kuutoa mwili wa Ditrov ni kutafuta jiwe kubwa na kushuka nalo hadi ufukweni, akalifunga vizuri na kamba.

Bila kupoteza wakati akaja kwenye gari, akafungua buti na kuutoa mwili wa Ditrov ukiwa kwenye mfuko wa nailoni usiovujisha damu na kuubeba begani huku akikimbia nao ufukweni.

Akaangaza macho yake huku na kule bila kuona mtu yeyote zaidi ya mbwa wake waliokuwa wakibweka, kilichosikika dakika chache baadaye ni muungurumo wa boti ikikata maji kuelekea katikati ya bahari.

Dakika ishirini hivi baadaye, alizima injini na boti kusimama. Giza lilikuwa nene kila upande, hivyo hakumhofia mtu yeyote, haraka akalikamata jiwe na kulitupa majini kisha kuusukuma mfuko, taratibu ukaingia majini na kuanza kuzama.

Huo ukawa mwisho wa Ditrov. Badala ya kusikitika, Victor Federov alitabasamu na kuwasha boti yake kisha kuondoka kwa kasi kurejea nyumbani ambako aliegesha na kuingia ndani bila mtu yeyote kugundua.

Hakupata usingizi hata kidogo mpaka kulipopambazuka asubuhi,akajiandaa kwa ajili ya kwenda kazini ambako alifanya kazi kama kawaida, saa nne na nusu alimpigia simu katibu muhtasi wake na kumwomba amwitie Ditrov.
“Hajaonekana tangu asubuhi bosi.”

“Haiwezekani, mtafuteni haraka sana nina kazi ya kufanya naye.”
“Sawa bosi.”
***
“Jina lako unaitwa nani?”
“Marina!”
“Na mwenzako?”

“Mariya.”
“Ninyi ni mapacha?”
“Ndiyo.”
“Baba yenu ni nani?”
“Victor Federov.”

“Ahaaa! Kumbe ni ninyi?”
“Ndiyo.”
“Karibuni sana Moscow International School.”
“Ahsante.”

Victor Federov aliwapenda sana watoto wake, kuthibitisha jambo hilo alihakikisha wanapata elimu bora. Alikuwa na fedha nyingi, utajiri wake ulitisha hata kama angetumia fedha zake kwa fujo kiasi gani, haikuwa rahisi kuzimaliza hivyo aliona ni bora kusomesha watoto wake kwenye shule nzuri ili wapate elimu bora itakayowasaidia kuendesha miradi yake vizuri baada ya yeye kuondoka duniani.

Shule aliyoona inawafaa ni Moscow International School, ambayo kwa mwaka kila mtoto alilipiwa milioni ishirini na tano. Watoto walimfurahia baba yao, hawakuwa na kumbukumbu yoyote tena juu ya Tanzania wala Phillip na Genevieve.

VICTOR Fedorov alipohakikisha kwamba sasa alikuwa amemaliza zoezi zima la mauaji, alirejea nyumbani kwake na kuingia moja kwa moja chumbani kwake ambako alijitupa kitandani, hakika alijiona mshindi kwa kazi aliyokuwa ameifanya na sasa siri juu ya watoto ilikuwa imebaki kuwa yake peke yake.
Hakupata usingizi hata kidogo mpaka kulipopambazuka asubuhi, akajiandaa kwa ajili ya kwenda kazini ambako alifanya kazi kama kawaida, saa nne na nusu alimpigia katibu muhtasi wake na kumwomba amwitie Ditrov.

“Hajaonekana tangu asubuhi bosi.”
“Haiwezekani, mtafuteni haraka sana nina kazi ya kufanya naye.”
“Sawa bosi,” katibu muhtasi alijibu.
Kwa muda wa nusu saa katibu muhtasi aliendelea kumtafuta Ditrov kwa namba zote alizozifahamu lakini hakupatikana, yeye pia akaingiwa na hofu, kwani haikuwa kawaida ya Ditrov kutofika kazini bila sababu yoyote na hakuwahi hata mara moja kuzima simu zake za mkononi.

“Lazima atakuwa na matatizo huyu,” aliwaza katibu muhtasi akinyanyua simu ili amtaarifu bosi wake.
“Ngrii! Ngrii! Ngrii!” simu ilisikika upande wa pili ikiita.
“Ndiyo.”
“Bosi mpaka sasa sijafanikiwa kumpata Ditrov.”
“Umepiga simu yake ya mkononi?”

“Ndiyo, bosi, tena zote mbili.”
“Sasa atakuwa wapi huyu?”
“Kwa kweli hata mimi inanishangaza.”
“Jaribu kwa mara ya mwisho kumtafuta nitahitaji majibu kama bado atakuwa hapatikani basi taarifa itolewe polisi, sawa?”
“Nitafanya hivyo,” alijibu katibu muhtasi na kukata simu.

***
Wakaanza kuishi pamoja kama mke na mume, katika maisha yaliyojaa furaha, huzuni zote zilizokuwa zimewafunika zikaondoka ingawa Phillip hakuisahau familia yake, kila siku ya Jumapili ilikuwa ni lazima asindikizwe na mke wake wakiwa njiani kuelekea kanisani hadi makaburini ambako alisali akimkumbuka mke wake Genevieve na watoto wao Dorice na Dorica.

Wiki moja baada ya kufunga ndoa maisha yakiwa ya furaha Lina alitakiwa kurejea kazini, hivyo alilazimika kumpa Phillip taarifa juu ya habari hiyo.
“Mpenzi!”
“Ndiyo,” Phillip aliitika
“Kesho nitaanza kazi.”

“Vyema mke wangu mimi nitakuwepo tu hapa nyumbani.”
“Nyumbani?”
“Ndiyo.”
“Ok! Nahitaji kufahamu ulisomea nini?”
“Nilisomea mambo ya sheria.”
“Unao uzoefu wa kutosha?”

“Kabisa.”
“Basi nitakutafutia kazi nahitaji utoke nyumbani ili usiwe mpweke.”
“Mwaa! Mwaa!” Phillip alimbusu Lina mfululizo.
“Ahsante nakupenda Phillip, hakika nitakufanya kuwa mwanaume mwenye furaha siku zote.”

“Nitafurahi sana Lina, nakuwa mpweke zaidi pale ninapokumbuka familia yangu, hakika niliipenda lakini naona yalikuwa mapenzi ya Mungu wote wakaniacha, naamini ujio wako kwangu utanirejeshea furaha iliyopotea miaka mingi kabla.”

“Hakika nakupenda amini,” Lina aliongea huku akimkumbatia Phillip wote kwa pamoja wakajifunika shuka na kulala. Kwao usiku ulionekana kuwa mfupi, hakuna aliyekuwa akitamani kumwacha mwenzake kitandani lakini kwa Lina ilikuwa ni lazima afanye hivyo kutokana na kazi yake. Hivyo alijilazimisha na kuamka kitandani kisha kuingia bafuni kuoga na kujiandaa tayari kwa kwenda kazini.
“Nitarejea muda si mrefu, nikuletee nini mpenzi?”
“Mh! Mh!” Phillip aliguna.

“Sema basi nikuletee kitu gani?”
“Nakuhitaji wewe,” alisema Phillip akimvuta Lina na kumpiga busu huku akimtakia siku njema.
Taratibu akatoka chumbani na kufunga mlango nyuma yake huku akimwacha Phillip kitandani.

****
Kwa muda wa saa tatu katibu muhtasi aliendelea kujaribu simu ya Ditrov bila majibu yoyote na hata alipojaribu kutuma mtu nyumba kwake na sehemu mbalimbali ambazo alifahamu angeweza kuwepo, bado hakupatikana.
“Ni vyema nikamtaarifu bosi juu ya Ditrov kwamba hapatikani,” aliwaza akinyanyua simu na sekunde mbili tu baadaye sauti nzito ikasikika upande wa pili.

“Ndiyo.”
“Bosi sijafanikiwa kumpata.”
“Unasema?”
“Ditrov hapatikani tumejaribu kufuatilia sehemu mbalimbali ambazo mara nyingi hupenda kutembelea, majibu yanayotolewa ni yaleyale kwamba hajaonekana.”

“Mh! Piga simu polisi kisha utoe taarifa, inawezekana ametekwa au kuuawa na watu fulani, unanisikia?”
“Ndiyo.”
“Nahitaji kufahamu majibu ya polisi mara moja na kama inawezekana msako mkali ufanyike, nataka Ditrov apatikane haraka iwezekanavyo,” alisema Victor Fedorov kwa hasira kali na kukata simu.

“Haa! Haaa! Haaa!” Victor Fedorov alicheka huku akinyanyuka kitini taratibu akasogelea picha kubwa iliyokuwa ukutani kisha kuibusu.
“Merina! Mariya! Nitawapenda mpaka kufa siko tayari kuwapoteza kwa gharama yoyote ile, ndiyo maana nimeamua kumuua Ditrov ili kuficha siri hii. Mwaa! Mwaa!” Victor Fedorov aliongea akiikodolea macho picha hiyo.

Je, nini kitaendelea? Ditrov ndiyo huyo amezamishwa baharini.
 
SEHEMU YA 25


ILI asigundulike kwa mauaji ya Ditrov anampigia simu katibu muhtasi wake akimtaka amtaarifu Ditrov kwamba alikuwa akimhitaji ofisini kwake kwa kazi maalum. Ditrov anatafutwa kwa muda bila mafanikio.

Katibu muhtasi anamrejeshea majibu kwamba mpaka wakati huo bado Ditrov alikuwa hajapatikana sehemu yoyote ile.
Uamuzi pekee wa Victor Fedorov aliyekuwa akifahamu wazi mauaji aliyoyafanya, anaamuru taarifa hizo zitolewe kwa jeshi la polisi ili msako maalum ufanyike haraka na Ditrov apatikane.

Ili kuficha siri ya mauaji ya Ditrov, Victor Fedorov anaudanganya umma wa Urusi kwamba naye pia yuko tayari kufanya kila kinachowezekana ili mradi tu Ditrov apatikane, hivyo ameamua kwenda makao makuu ya polisi na kuzungumza na mkuu wao ili kama jeshi hilo lingehitaji msaada wowote kutoka kwake basi wasisite kumweleza.

Baada ya maongezi hayo wote wawili waliagana na Victor Fedorov akatoka nje ya ofisi moja kwa moja akaliendea gari lake na kupanda kisha kuwasha na kuondoka kwa kasi ya ajabu, kwa kumwangalia alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa kwa upotevu wa Ditrov lakini ukweli ni kwamba aliidanganya dunia, aliufahamu ukweli wote na mpaka wakati huo alishaamini kwamba Ditrov alikuwa marehemu hivyo isingekuwa rahisi kupatikana tena.
Je, nini kinaendelea? SONGA NAYO…

Jeshi la polisi nchini Urusi lilidhamiria kufanya kila kilichowezekana ambapo Ditrov alitafutwa kila pembe, Urusi ikabinuliwa nje ndani, vyombo vya habari, zikiwemo televisheni, vikirusha matangazo na kuonyesha picha ya Ditrov kwamba alikuwa amepotea katika njia ya kutatanisha na alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba na yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake awe mzima au marehemu basi angelipwa kiasi kikubwa cha fedha.

Watu nchini humo wakanyanyuka, wakaingia katika msako, Ditrov alikuwa akisakwa, kiasi kikubwa cha fedha alichokitangaza Victor Fedorov kiliwachanganya watu wengi.Wakati msako huo ukiendelea, Victor Fedorov alikuwa akifuatilia kila kitu kwa karibu, aliwaona watu wote kuwa wajinga kwake, kwani ukweli ni kwamba mpaka wakati huo Ditrov hakuwa tena hai, hicho ndicho alichoamini, hivyo hata zawadi aliyokuwa ameitangaza kwa umma alifahamu wazi kwamba isingekwenda kwa mtu yeyote yule.

“Hata kitokee nini hawawezi kumpata niko tayari kufanya kila kitu watakachohitaji ili mradi tu kuuficha ukweli huu, sipo tayari, duniani hakuna siri ya watu wawili, hivyo kifo cha Ditrov kimefanya siri kubaki kwangu peke yangu, Mungu atanisamehe,” aliwaza akiangalia tangazo lililomwonyesha Ditrov likipita kwenye televisheni kubwa iliyokuwa ofisini kwake.

Mpaka wakati huo jeshi la polisi lilishafanikiwa kukagua hospitali zote nchini Urusi na kupata kibali cha kuingia katika vyumba vya kuhifadhia maiti kumsaka mtu huyo lakini bado hakupatikana sehemu yoyote, nao pia wakaanza kupoteza matumaini kwani upotevu wa mtu huyo ulisababisha kusimamisha kazi zao nyingi sana kutokana na Victor Fedorov kuwa na nguvu na ushawishi mkubwa sana ndani ya nchi hiyo.

Wiki ya kwanza ikapita msako ukiendelea kwa nguvu zote, wiki ya pili nayo ikapita hatimaye mwezi bila Ditrov kupatikana sehemu yoyote. Jeshi likashindwa kuelewa ni wapi alikokuwa mtu huyo.
“Ngrii!Ngrii!Ngrii!” mlio simu ukasikika ndani ya ofisi ya Mkuu wa Polisi.
“Ndiyo.”

“Sawa mkuu, hakuna shida hata sisi wenyewe tumeona ni vyema tukapumzika ili tujipange tena upya kutafuta njia nyingine, zoezi hili limekuwa gumu sana kwetu,” aliongea Mkuu wa Polisi ofisini kwake.

Victor Fedorov aliyekuwa upande wa pili wa simu ndiye aliyekuwa akiongea na mkuu huyo wa polisi akimpa ushauri wa juu ya zoezi hilo kwamba sasa lilikuwa limeshindikana hivyo watafute mbinu nyingine zitakazowezesha kupatikana kwa Ditrov.

Mkuu wa polisi alikubaliana na Victor na kusitisha zoezi hilo akiwa haelewi kabisa upande wa pili wa myu huyo, akaunga mkono hoja na kukata simu.

“Sasa nina hakika Ditrov atakuwa amekufa, laiti kama angepona angeshajitokeza ninavyomfahamu mimi ni mtu hatari sana huyu, hawezi kuwa hai akaendelea kujificha ni lazima angetoka na kuuelezea umma kila kitu,” aliwaza Victor Fedorov akiwa ndani ya ofisi yake.

***
Kitendo cha Lina kuongea na bosi wake na kumweleza kwamba katika ofisi yao alihitajika mwanasheria anayefahamu vyema sheria, kilikuwa ni kama bahati ya mtende, akatembea taratibu na kurejea ndani ya ofisi yake, huku machozi ya furaha yakimtoka, alishindwa kuelewa ni bahati gani iliyokuwa ikimtokea, machozi ya furaha yakaendelea kumtoka.

“Ahsante baba, Mungu kweli unatenda, hatimaye Phillip naye amepata kazi?” alijiuliza.
Kwa siku nzima, muda kwa Lina ulikwenda taratibu, saa zilikuwa hazisogei hamu yake kubwa ikiwa ni kurejea nyumbani na kumweleza Phillip juu ya habari aliyokuwa ameipata.
“Phillip atafurahi sana kusikia habari hii,” aliwaza.

Akiwa ofisini kwake akakivuta kiti na kuketi, sauti nyingi zikimwijia kichwani mwake, tangu siku aliyokutana na Phillip jinsi alivyomweleza kwamba bado alikuwa akimpenda na hatimaye kufunga ndoa na sasa alikuwa mke wa mwanaume aliyempenda kwa moyo wake wote.

“Ni kweli Phillip amefiwa na mke na watoto wake, lakini ilikuwepo sababu jambo hilo litokee ili mimi niweze kumpata, masikini Genevieve watoto wake Dorice na Dorica nauahidi moyo wangu kumpa Phillip furaha yote mpaka mwisho wa maisha yetu, hakika ninampenda kwa dhati,” alijisemea Lina kwa sauti ya chini chini.

Muda wa kurejea nyumbani ulipofika, hakuwa na sababu ya kuendelea kukaa ofisini, haja ya moyo wake ilikuwa ni kufika nyumbani na kumkuta mume wake mpendwa Phillip ili amweleze habari njema aliyokuwa nayo.
Huku akitembea kwa madaha, mkononi akiwa amening’iniza funguo akalisogelea gari lake akaingia ndani na kisha kuondoka kwa mwendo wa kasi, mawazo yake yote yakiwa kwa Phillip.

“Ninampenda, nafahamu wazi hata yeye ananipenda hanidanganyi hata kidogo, nitafanya kila kitu kuhakikisha simpotezi, mwanaume niliyempenda akanifanya nikapata matatizo mengi maishani mwangu ndiye aliyeko ndani ya nyumba yangu sasa tena akiwa mume wangu!” aliongea Lina huku akizidi kukanyaga mafuta.

Kwa mwendo wa saa moja na dakika kadhaa tayari alikuwa nje ya lango la nyumba yake, bila kuchelewa akapiga honi na lango likafunguliwa, akapita moja kwa moja ndani bila kusema kitu chochote na mlinzi wake.

“Mh!” mlinzi aliguna akishuhudia gari likizidi kutokomea. Kilikuwa ni kitendo cha ajabu sana kwani mazoea aliyokwishajijengea ilikuwa ni lazima asimamishe gari na kumtania kidogo lakini siku hiyo haikuwa hivyo kwa Lina ilionekana kuwa tofauti.
“Pengine anaumwa au kuna nini kimempata? Si kawaida ya bosi wangu kuwa hivyo lazima takuwa na walakini. Ngoja nisogee karibu nione,” aliongea mlinzi akisogea kwa mwendo wa pole.

“Bosi!” aliita.
“Bee!” Lina akaitika akitembea kwa kasi kuelekea lango la kuingilia ndani ya nyumba yake.
“Nini tatizo si kawaida yako kuwa hivyo unaumwa?”
“Mh!” alijibu akiingia ndani.
Mlinzi huyo alibaki hapo akiwa haelewi ni kitu gani kilikuwa kimempata bosi wake huyo, haraka akapata wazo kichwani mwake akaamua kuzunguka upande wa pili wa nyumba ambako dirisha la chumba cha bosi lilikuwepo huko.

“Ngoja nisimame hapa kama kuna tatizo nitajua kupitia hapa,” aliongea mlinzi akisogea kwa kunyata dirishani.
“Darling! Darling! Uko wapi? Tafadhali njoo, nakuhitaji haraka sana!” sauti ya Lina ilisikika.
“Yes baby!” (Ndio mpenzi) sauti ya Phillip ikasikika kwa chini kutoka chumbani.
“Bado umelala?” Lina aliuliza.

“Ndiyo!” Phillip akajibu.
Kwa mwendo wa haraka h Lina akatembea kuelekea chumbani akafungua mlango na kuingia, Phillip bado alikuwa kitandani akiwa amelala na shuka likiwa limemfunika mpaka kichwani.
“No! Unaumwa?” Lina aliuliza.
“Mh!” Phillip alijibu akitingisha kichwa.

Bila kuchelewa Lina akalivuta shuka na kulitupa pembeni, Phillip akaonekana na alipomwangalia vyema usoni aligundua alikuwa akilia kwani macho yake yalivimba kupita kiasi.
“What happened?” (Nini tatizo?)
“Familia yangu, mke na watoto wangu wapendwa!” alijibu Phillip kwikwi ya kulia ikizidi kumkaba.

“Sikiliza mume wangu hebu niambie unachohitaji tufanye nini ili upate furaha iliyopotea, niambie niko tayari kutoka moyoni mimi siipendi hali hii!”
“Watoto! Nahitaji kupata mtoto angalau mmoja,” aliongea Phillip akilia kwa uchungu.

Maneno hayo pekee yalimfanya Lina aelewe ni kiasi gani Phillip alikuwa katika upweke bila kuchelewa akaanza kuvua nguo moja baada ya nyingine na kuzitupa pembeni kisha kukisogelea kitanda na kupanda juu yake akamvuta Phillip na kumkumbatia, mabusu mfululizo yakishuka juu ya mwili wa Phillip na neno I love you, likisikika.

Mlinzi akiwa amesimama nje ya dirisha bila kuelewa ni kitu gani kilikuwa kikitokea alisikia sauti nyingine.
“Jwig!Jwig!Jwig!” kitanda kikipiga kelele.
“Mh!” mlinzi aliguna akiondoka eneo hilo.

Kwa muda wa saa mbili mfululizo, Phillip na Lina walikuwa kitandani kila mmoja akimwonyesha mwenzake ufundi wake wote kuhakikisha anapata furaha aliyoitarajia. Si Phillip wala Lina wote wawili walikuwa katika ulimwengu mwingine wakisahau shida na matatizo yote yaliyokuwa yamepita katika maisha yao.

“Phillip” Lina aliita.
“Naam mke wangu”
“Leo nahitaji uniambie ni kitu gani nitakufanyia ili uwe na furaha, sihitaji kuona machozi yako kila wakati, yananisikitisha mno!”
“Unajua nini?”

“Mh!” Lina aliguna.
“Lina.” Phillip aliita huku macho yake yakimuangalia Lina.
“Bee.”
“Nahitaji mtoto hata mmoja tu”
“Hicho tu?”
“Hakika ndicho.”

“Phillip ni jambo la kuzungumza tu na si kuliweka kichwani mwako.”
“Nitazungumza nini Lina ili hali unafahamu wazi kwamba sina uwezo wa kuzaa!”
“Najua lakini kwangu hilo si tatizo.”
“Kwangu ni tatizo mpenzi, nahitaji mtoto hata mmoja tu ambaye ataniita baba nami nitamwita mwanangu.”

“Mh!” Lina akaguna tena huku akionyesha kusikitishwa na maneno ya Phillip.
Kwa muda wote wapenzi hao walikaa kimya kila mmoja akifikiri ni jinsi gani wangeweza kupata watoto, kwa Lina halikuwa swali gumu kwani yeye alikuwa ni mzima kwa kila kitu tatizo pekee lilikuwa kwa Phillip ambaye mbegu zake hazikuwa na uwezo wa kurutubisha yai la mwanamke hivyo hata kama wangefanya tendo la ndoa kwa muda wa zaidi ya miaka kumi bado uwezekano wa kupata mtoto usingekuwepo.

“Phillip!” Lina aliita akimgusa mumewe begani.
“Nakusikia.”
“Twende tukaoge kisha tujadiliane kuhusu jambo hili.”
“Sawa.” Alijibu Phillip wakinyanyuka kutoka kitandani wakajikongoja hadi bafuni na kuanza kuoga.

Kwa muda wa dakika kumi nzima waliutumia kuoga bafuni huko Lina akiongea mambo mengi kuhusu mapenzi, nia yake kubwa ikiwa ni kumfanya Phillip aondokane na msongo wa mawazo uliokuwepo kichwani mwake. Hatimaye wakamaliza na kurejea tena chumbani ambako Lina alimkaribisha Phillip kwenye kiti maalum kisha yeye akaelekea sebuleni ambako alifungua jokofu akatoa boksi la juisi, akachukuwa glasi mbili na kurejea chumbani.

Kwa mwendo wa madaha huku akiwa ndani ya taulo dogo la rangi nyeupe, Lina alitembea mpaka karibu kabisa na Phillip, akaweka vitu alivyokuwa navyo mezani kisha kumsogelea Phillip na kumbusu mfululizo.
“Mwaa!Mwaaa!Mwaaa!”
“Ahsante,” alijibu Phillip kwa sauti ya chini.

Akiwa hapo, Lina alifungua boksi na kuanza kumimina juisi kwenye glasi moja baada ya nyingine na kumkaribisha Phillip huku akinyanyua glasi na kuipeleka mdomoni mwake kisha kuirejesha tena kwa Phillip kama ishara ya kuonyesha pendo zito alilokuwa nalo juu yake.
“Nakupenda.”
“Mimi pia nakupenda Lina.”

“Ahsante, lakini pia nina habari njema sana kwako.”
“Kuhusu mtoto?” Phillip aliuliza.
“Mh! Hapana lakini ni njema.”
“Tafadhali nieleze usikawie.”
“Mh! Mh!” Lina aliguna mfululizo.

“Hebu shika mapigo ya moyo wangu yanasubiri habari hiyo kwa hamu kubwa, tafadhali nieleze kabla sija…” Phillip aliongea lakini kabla hajafika mwisho wa sentensi yake Lina akanyoosha mkono wake na kuziba mdomo wa Phillip.
“Kunywa juisi kwanza nitakueleza si habari mbaya ni njema sana wewe mwenyewe hakika utafurahi.”
“Kweli?”

“Kabisa.”
Taratibu wakaendelea kunywa juisi huku mikono ya Lina ikipita huku na kule mwilini mwa Phillip huku maongezi matamu kati yao yakiendelea.
Hakika wawili hao walipendana kwa dhati, hawakuwa tayari kukumbuka historia zao za nyuma na hata ilipotokea jambo hilo likajirudia vichwani mwao basi waliona ilikuwepo haja ya kupuuza mawazo hayo na kuendelea na starehe.

Muda ukazidi kusonga bila Lina kufungua mdomo wake kumweleza Phillip kitu chochote, moyoni akitafakari ni jinsi gani habari hiyo ingepokelewa kwani alifahamu wazi kwa Phillip kupata kazi ingekuwa njia moja wapo ya kumwondoa katika msongo wa mawazo aliokuwa nao na hilo lingekuwa limekwisha na jambo ambalo lingebaki kuwa kitendawili katika maisha yao, watoto ambao kwa Lina japo alikuwa mwanamke kamili hakuona umuhimu wowote alichohitaji yeye kwa wakati huo ni kuwa na mwanaume aliyempenda kwa dhati na si kingine.

“Tafadhali Lina hebu nitoe katika mateso haya, nahitaji kufahamu ni kitu gani unataka kunieleza.”
“Hakuna jambo baya mpenzi wangu ni habari juu ya kazi”
“Kazi?”
“Ndiyo.”
“Imefanya nini?”

“Amini tayari umepata kazi”
“Mungu wangu! Unasema kweli Lina?”
“Ni kweli na si ndoto, Phillip tayari umeishika kazi mikononi mwako.”
“Wapi na lini?”
“Hivi sasa ninavyozungumza na wewe kesho asubuhi na mapema tutaongozana, kitu cha muhimu ni vyeti vyako vyote.”

“Sehemu gani?”
“Ofisini kwetu, Phillip ni bahati iliyoje, leo nilipoingia tu ofisini bosi wangu akaniita na kunieleza kwamba shirika letu lilihitaji mtu anayefahamu vyema sheria, akili yangu ikakumbuka kwamba hata wewe ulisoma sheria na uliimudu vyema kazi hiyo.”

“Lina ahsante kwa mara nyingine, nimeamini unanipenda nami ninakupenda pia, moyoni mwangu naanza kuamini kabisa kwamba Mungu alikuwa nayo sababu ya mambo yaliyotokea nyuma ya kupoteza mke na watoto wangu wote akifahamu wazi kwamba nitakutana na mwanamke mwingine atakayenipenda kama Genevieve, Mungu azilaze roho za wapendwa wangu hawa mahali pema peponi amina,” alisema Phillip machozi yakimtiririka, wakati hayo yakiendelea Phillip alihisi ni ndoto lakini alipofungua macho vizuri na kumwona Lina mbele yake akiwa katika sura ya kutabasamu, akanyoosha mikono na kumwelekea ambapo bila kuchelewa Lina akajichomeka katikati ya mikono hiyo wakakumbatiana na kuanza kulia.

***
Wiki moja baadaye Victor Fedorov akiwa ofisini kwake akiamini kabisa kwamba kila kitu kilikuwa kimekwenda kama alivyotaka, anashtushwa na taarifa ya habari kwenye televisheni.
“Mh ni kitu gani hiki?” anajiuliza akisogea karibu kabisa ili kusikiliza kwa ukaribu.

Mamia ya watu nchini Urusi walikuwa wakiandamana kupiga hoja ya jeshi la polisi kuhusu msako wa Ditrov, kwa ilivyoonekana wengi walikuwa wameumizwa na jambo hilo na walichokihitaji kwa wakati huo ni kufahamu ukweli juu ya mauaji hayo, wakisisitiza na kulaani kwa nguvu zote uamuzi huo, wananchi wengi wakidai kwamba nyuma ya pazia kulikuwa na siri nzito kwani kabla Ditrov hajapotea tayari washirika wake wote alioshirikiana nao katika kazi waliaminika kufa tena vifo vya kutatanisha.

“Mh! Ni lazima niwafunge midomo, wataniletea matatizo hawa, sihitaji dunia ifahamu kwamba ninahusika na vifo hivi, nataka iendelee kubaki siri tena siri kubwa, sasa ni wakati wa kuonyesha jeuri ya fedha zaidi ili kulifanya jeshi la polisi likae kimya milele,” aliongea Victor akinyanyua mkono wa simu.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 26


ILIPOISHIA
“Mh! Ni lazima niwafunge midomo, wataniletea matatizo hawa, sihitaji dunia ifahamu kwamba ninahusika na vifo hivi, nataka iendelee kubaki siri tena siri kubwa, sasa ni wakati wa kuonyesha jeuri ya fedha zaidi ili kulifanya jeshi la polisi likae kimya milele,” aliongea Victor akinyanyua mkono wa simu.
SASA ENDELEA
“Hello!” akaita Victor Fedorov kwa sauti nzito.

“Ndiyo,” sauti upande wa pili ikajibu.

“Ah! Naweza kuongea na mkuu wenu, tafadhali?” aliuliza na ukimya wa ajabu ukatokea kwake akiwa bado ameshikilia mkono wa simu.

Akili yake yote ilisharuka, hakuelewa ni nini kingefuata baada ya hapo kwani kwa jinsi wananchi walivyokuwa wamekasirishwa na mauaji yaliyotokea, waliapa kufanya chochote ili mradi tu wapate ukweli juu ya vifo vya ndugu zao.

Walikuwa tayari kufa lakini jeshi la polisi litoe tamko ambalo lingewaridhisha wote.

Pamoja na kiyoyozi kikali kilichokuwa ndani ya ofisi yake asubuhi hiyo Victor Fedorov alikuwa akitiririkwa na jasho mwili mzima akifahamu wazi kwamba kama ingetokea siri yake ikagundulika basi angepoteza kila kitu alichokuwa nacho, si utajiri tu hata watoto wake na heshima aliyokuwa amejijengea kwa muda mrefu.

Akiwa hapo taswira za watoto wake pacha, Mariya na Marina zikamwijia kichwani mwake, ni watoto hao ndiyo walisababisha afanye mauaji yaliyotokea ili kuficha siri.

“Naitwa Victor Fedorov, nahitaji kuonana na wewe tena ikiwezekana leo hii, ni muhimu sana, kuna taarifa nimeiona ofisi kwangu sasa hivi juu ya wananchi wanavyoandamana imeniumiza sana napenda nami niungane nao kufanya msako huo kwani nimepoteza mtu muhimu sana katika kazi zangu,” alisema akipigapiga meza kuonyesha msisitizo.

“Karibu!” mkuu wa jeshi alijibu upande wa pili wa simu.

“Ok! Nitafika hapo ofisini kwako muda si mrefu, ni vyema tukapata muda wa faragha kwa mazungumzo yetu na ningeomba asiwepo mtu mwingine yeyote wakati wa maongezi hayo.”

“Sawa hilo litafanyika,” sauti upande wa pili ikajibu na hapohapo simu ikakatwa.

Mkuu wa jeshi la polisi hakuelewa siri iliyokuwa ikimsumbua Victor Fedorov, alimwamini kwa asilimia mia moja kwamba naye alikuwa ameumizwa na mauaji hayo ndiyo maana alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha msako unafanyika kwa namna yoyote ile.

Victor Fedorov akasimama kutoka kitini mwake na kutembea mpaka mbele ya kioo kikubwa kilichokuwa ndani ya ofisi yake, hapo akaweka tai yake vyema na kuangalia uso wake na kwa kutumia kitambaa kidogo alichokuwa nacho akajifuta uso wake kisha kuchukua miwani ya rangi nyeusi akaivaa.

Kwa alivyoonekana, alidhamiria kuficha siri ya mauaji lakini msaada mkubwa ungetoka kwa jeshi hilo la polisi na kitu pekee ambacho angefanya ni kutumia fedha tu ili mambo yaende kimya na hatimaye kupotea kabisa.

Akatoka nje ya ofisi yake na kumuaga katibu muhtasi wake kisha kutembea mpaka sehemu alipoegesha gari lake na kupanda, mwendo alioondoka nao eneo hilo ulimshangaza kila mmoja aliyemwona kwani haikuwa kawaida yake.

“Mh!” mmoja wa wafanyakazi wake akaguna.

“Leo kuna tatizo hapa si kawaida ya bosi, hata miwani ulishawahi kumwona ameivaa?” mwingine alidakia.

“Mimi naona kupotea kwa Ditrov kumesababisha matatizo makubwa sana, alikuwa ni mtu wake wa karibu sana.”

“Nakuunga mkono, hali hiyo imemchanganya kabisa bosi wetu,” yalikuwa ni maongezi ya wafanyakazi wawili waliokuwa nje ya ofisi wakimshuhudia Victor Fedorov akitokomea.

Dakika kumi baadaye alishafika makao makuu ya jeshi la polisi Urusi, akaegesha gari na kushuka na kuanza kutembea kuelekea ndani ya ofisi, huku akiwa mwenye wasiwasi mwingi.

Aliangaza huku na kule na kuingia ndani ambako alipokelewa na kukaribishwa moja kwa moja kwenye ofisi ya mkuu wa jeshi.
“Habari za muda?”

“Njema tu, pole na kazi.”

“Ah, tumeshazoea sisi, ndiyo kazi zetu.”

“Kuna jambo moja tu kwa sasa,” alisema Victor kwa kujiamini.

“Sawa kabisa.”
Mkuu wa jeshi akakaa vyema ili kumsikiliza Victor Fedorov.
“Kuna kitu gani kinaendelea mpaka sasa juu ya msako wa Ditrov?” Victor Fedorov aliuliza akivua miwani yake.

“Mh! Kama tulivyokubaliana, kwamba tusitishe zoezi mpaka tujipange upya halafu tuendelee lakini cha kushangaza wananchi wameanza kuingia mitaani kupinga uamuzi huo huku wakisisitiza msako uendelee tena kwa nguvu zote, wengi wakidai kwamba kabla ya kupotea kwa Ditrov washirika wake wote waliuawa tena vifo vya kutatanisha.

“Kwa hiyo ninyi kama jeshi mmeamua nini?”
“Tuendelee na msako…” alisema mkuu wa jeshi lakini kabla hajamaliza sentensi yake kelele za ajabu zikasika kutoka nje ya jengo.

“Ndiyo, tunataka uchunguzi uendelee, tunataka kufahamu ndugu zetu wako wapi, tunajua kuna mtu mkubwa anayefanya mauaji hayo, pengine kwa sababu zake binafsi au kuficha siri fulani…Tunamtaka huyo atafutwe na ahukumiwe!” sauti zilisikika zikizidi kusogelea karibu kabisa.

“Choma hiyo! Choma jengo bila kuogopa, hakuna kurudi nyuma tunahitaji kufahamu ukweli tumechoshwa na jeshi kila wakati kutudanganya tu, chomaaaaa!” sauti zilisikika zikisogea kuelekea makao makuu ya Jeshi la Polisi la Urusi.

“Mungu wangu!” mkuu wa jeshi alisema.

“Nini tena?”
“Wananchi hatimaye wameamua kuja mpaka huku, hili jambo siyo dogo hata kidogo ni lazima msako uendelee haraka sana,” alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi la Urusi huku akinyanyua simu. Lakini kabla hajabonyeza namba mlango wa chumba chake ukafunguliwa kwa nguvu na askari mmoja akaonekana.
“Mkuu kuna matatizo.”

“Kimetokea nini?”

“Wananchi!”

“Wanafanya nini?”

“Wameamua kujitokeza kupambana na polisi eti wanadai kwamba kuna siri kubwa tunayoifahamu kuhusu mauaji yanayotokea.”

“Kwahiyo?”

“Wanaonekana wana hasira sana, tena wameshachoma vituo vya polisi karibu mji mzima na sasa wameingia hapa makao makuu.”

“Hebu nitoke kuongea nao.”

“Mkuu hapana, hutaweza! Wanaonekana kuwa na hasira nyingi sana.”

“Ni lazima kifanyike kitu hapa kunusuru usalama wetu na mali za nchi.”

“Kipi?”


“Mabomu ya machozi kuwatanya kwa nguvu sehemu zote ambazo wameandamana, umesikia?”

“Ndiyo mkuu,” alijibu askari huyo akitoka mbio kuelekea nje ambako alishuhudia maelfu ya watu wakizidi kusonga mbele kulielekea lango kuu ili waingie ndani na kufanya walichokitarajia.

Askari huyo alipotupa macho mbele ili kuangalia vizuri, alishuhudia maaskari wengi wakiwa chini.

Lilionekana kuwa jambo la kutisha wananchi walikuwa wamedhamiria kwa nguvu zote kuingia mitaani si kufanya fujo bali kulitia hekaheka jeshi la polisi ili liweze kuendelea na msako wake badala ya kukaa kimya.

“Hatimaye mwisho wangu umekuwa mbaya!” Victor Fedorov aliongea kwa sauti huku akinyanyuka kitini.

“Unasema?” mkuu wa jeshi aliuliza.

“Mh!” Victor Fedorov aliguna, na tayari alishaukamata mlango wa chumba akaufungua na kutoka nje huku akikimbia.
Walikuwa ni watoto wazuri, hakuna mtu aliyewaona watoto hao na kusita kutoa sifa midomoni mwao, japo walikuwa wadogo lakini uzuri wao ulionekana waziwazi na watu wengi kusema kwamba wakikuwa wangekuwa tishio kwa wanaume wengi nchini Urusi.

Ni watoto hao Pacha Mariya na Merina ndiyo walikuwa wakileta machafuko nchini Urusi bila wao wenyewe kufahamu siri nzito ilikuwa imefichwa, wakilelewa vyema na kusoma katika shule ya gharama huku wakihudumiwa kwa kila kitu walichohitaji wakiandaliwa kuja kuwa warithi wa mali za baba yao.

Kila aliyewaona watoto hao hakusita kujiuliza maswali juu yao, kwani walimfahamu vyema Victor Fedorov na historia ya maisha yake alishawahi kuoa wanawake kadhaa na kuachana nao bila kuzaa nao watoto lakini ghafla watoto wawili wakaibuka na watu kuelezwa kwamba walikuwa ni watoto wake.
“Mh! watoto wazuri sana!”
“Ni kweli”
“Ni wa nani?”
“Victor Fedorov”
“Huyu tajiri hapa Urusi?”
“Haswa ndiye.”
“Amezaa lini na wapi?”
”Kwa kweli hilo swali hata mimi sifahamu ila wenyewe watoto ukiwauliza wanasema Victor Fedorov ndiye baba yao.”

“Mh! Haya ukiwaangalia wamefanana naye lakini walikuwa wapi na mama yao ni nani?”

“Mambo ya Ngoswe mwachie Ngoswe mwenyewe,” walikuwa ni walimu wawili wakiongea wakati watoto hao wakipita mbele yao.
***
Taarifa aliyokuwa ameipata Phillip kutoka kwa Lina ilimpa furaha ya ajabu mno, hakika hakuwaza wala kutegemea tena kwamba baada ya kifo cha mke na watoto wake wapendwa angerejea katika hali ya kawaida kwani alishapoteza matumaini na hakuwa na furaha tena lakini kukutana na Lina kulirejesha furaha iliyopotea miaka mingi huko nyuma.

“Ahsante mke wangu ninakupenda.”
“Nakupenda pia Phillip.” Lina alijibu macho yake yote yakimwangalia Phillip.

“Hakika sina cha kukuzawadia laiti kama ningeweza…”aliongea Phillip lakini sentensi yake ikakatishwa na busu la Lina ambalo lilitua moja kwa moja mdomoni mwake.

“Najua unachotaka kusema.”
“Mh! Nini?”
“Unataka kuzungumza juu ya mtoto.”
“Ni kweli kabisa mke wangu sina uwezo wa kuzaa.”
“Tutapata mtoto.”
“Kwa njia gani?”
“Hata kama tutalazimika kutumia fedha zote tulizonazo lakini tupate mtoto!”
“Kivipi Lina?”
“Nitakueleza siku nyingine leo tupumzike kwa ajili ya kesho nitahitaji utafute vyeti vyako vyote na kuviweka pamoja tayari kwa kazi kesho.”
“Kesho?”
“Ndiyo!”
“Mh!” Phillip aliguna.
“Kwa nini unaguna?”
“Kesho sijajiandaa kabisa mke wangu.”

“Nasema kesho ni lazima tuondoke wote hapa nyumbani kwenda ofisini.”

“Sawa tuombe uzima,” alijibu Phillip na wote wakajitupa kitandani taratibu wakiwa hapo waliongea hiki na kile hatimaye wakapitiwa na usingizi.

***
Baaada tu ya kutoka ofisini kwa mkuu wa jeshi la polisi, Victor Fedorov huku akipishana na watu wengi njiani alifanikiwa kulifikia gari lake na kuingia ndani, akaliwasha na kuondoka hapo kwa kasi ya ajabu kichwani mwake akiwaza kitu kimoja tu watoto wake.

Ni kweli alifahamu wazi kwamba wakati huo walikuwa shuleni lakini hakuelewa walikuwa katika hali gani kwani kwa jinsi hali ilivyoonekana mambo yalikuwa yameharibika kabisa.
“Watoto wangu,”alitamka Victor Fedorov.

Shule waliyosoma Mariya na Merina haikuwa umbali mrefu sana kutoka mahali Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Urusi yalipokuwa hivyo wasiwasi wake ukazidi kuongezeka maradufu.

“Kwa jinsi hali ilivyo lazima niwafuate watoto wangu,” aliwaza Victor Fedorov akiendesha gari kwa kasi kuelekea huko, kichwani akamkumbuka Ditrov na unyama aliomfanyia, akaziona pia taswira za watoto wake Mariya na Merina wakimfurahia machozi ya uchungu yakamtoka lakini akajipa moyo na kusonga mbele kuelekea shuleni kwa watoto wake.

Kwa mwendo wa dakika kumi nzima aliendesha gari hatimaye akafanikiwa kufika eneo la shule akiwa hapo akashangazwa na ukimya wa ajabu uliokuwepo, hapakuonekana dalili ya walimu wala wanafunzi.

Haraka bila kuchelewa Victor Fedorov akaegesha gari lake na kushuka huku akiangaza macho huku na kule.

“Kimetokea nini hapa?” akajiuliza mwenyewe akitembea kwa kasi kuelekea majengo ya ofisi za walimu huko nako hakukuta mtu.
“Mungu wangu watoto wangu, haiwezekani,” aliongea Victor Fedorov akiingia mlango mmoja baada ya mwingine kukagua.

Shule ilikuwa kimya kabisa, hapakuonekana mtu yeyote eneo hilo zaidi ya karatasi zilizokuwa zikipepea juu kutoka ndani ya majengo kwenda nje. Moyo wake ukamwenda mbio, jasho jingi likamtoka na alipojaribu kupaza sauti yake na kuita majina ya watoto wake halikupatikana jibu lolote.

“Nimekwisha!”alisema Victor Fedorov akiporomoka chini kama mzigo.

Je, nini kitaendelea?!
 
SEHEMU YA 27


Oleg Malenko alikuwa ni mwanaume wa Kirusi, alizaliwa na kukulia nchi Urusi miaka mingi iliyopita, alikuwa ni baba wa watoto wawili na mke mmoja, jina lake lilifahamika kwa wengi kutokana na kazi zake za uvuvi kwani aliendesha maisha yake kwa kazi hiyo.
Alikuwa ameifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka isiyopungua kumi na tano na bado, pamoja na umri wake mkubwa. aliendelea kuifanya kwani ndiyo kazi pekee iliyoendesha maisha yake na familia yake.
Alfajiri ya siku hiyo kama ilivyokuwa kawaida yake, alitoka nyumbani kwake mapema kuliko kawaida akimuaga mke na watoto wake kwamba alikuwa akielekea kazini kwake jambo ambalo liliishangaza sana familia yake lakini hawakutilia mashaka hali hiyo kwani walimfahamu vyema.
Hakuishi maeneo ya mbali sana kutoka ufukweni ambako ndiko aliegesha mtumbwi wake mdogo, hivyo kwa muda wa dakika kumi tu tayari alishafika eneo la ufukweni, huku akiwa na taa ndogo mkononi mwake aliangaza macho yake huku na kule akijaribu kuangalia kama kulikuwa na mtu mwingine eneo hilo lakini hakuona kitu.
Kwa ujasiri alitembea na kuusogelea mtumbwi wake kwa kutumia taa ndogo aliyokuwa nayo mkononi ambapo aliangaza ndani ya mtumbwi huo kuangalia kama kulikuwa salama. Bila kuchelewa akaiweka taa ndogo aliyokuwa nayo mikononi mwake na kuanza kuusukuma mtumbwi huo kuelekea majini, tayari kwa kuanza kazi.
Alfajiri ya siku hiyo bahari ilionekana kuwa kimya kabisa, hapakuwa na purukushani kama ilivyokuwa kila siku, hivyo kuwa na uhakika kabisa kwamba angevua samaki wengi kwa sababu hakukuwa na watu wengine.
Kwa mwendo wa dakika kumi nzima aliendelea kupiga kasia akisonga mbele zaidi, lengo lake likiwa ni kufika mahali ambako aliamini samaki wengi zaidi walipatikana lakini ghafla mbele yake aliona kitu cha ajabu ambacho hakukitarajia, moyo wake ukamwenda mbio pamoja na kwamba kwa wakati huo nchini Urusi kulikuwa na hali nzuri ya hewa, lakini Oleg alitiririkwa na jasho jingi si kwa sababu ya kazi aliyokuwa ameifanya bali kwa kitu kilichokuwa mbele yake.
“Mungu wangu ni papa!”alijiuliza akinyanyua taa yake ndogo na kumulika eneo hilo.
Akayatoa macho yake yote kuangalia mbele lakini kwa sababu ya mwanga mdogo uliokuwepo hakuweza kuona vyema, woga ukazidi kumwingia na wazo pekee lililomwijia kichwani mwake ni kugeuza mtumbwi wake haraka na kurejea alikotoka, jambo ambalo hakuwa na uhakika nalo kama angefanikiwa.
Akiwa hapo alishuhudia mtumbwi wake ukiyumbishwa huku na kule, tayari alijua alikuwa katika hatari.
“Leo ninakufa, sidhani kama nitasalimika, ” alijisemea Oleg huku machozi yakimbubujika.

***
Usiku ulionekana kuwa mrefu mno kwa Phillip, mawazo na akili zake zote zikiwa kwenye kazi ambayo Lina alikuwa amemuahidi. Moyoni akamshukuru Mungu kwa mara nyingi kwa kumwona na kumchagua yeye, ni kweli alikuwa katika majonzi mazito lakini alikuwa amepewa njia nyingine tena.
“Jambo moja tu sasa litakalonisumbua ni jinsi gani nitapata tena watoto? Nahitaji watoto ambao watakuwa warithi wa mali zangu hapo baadaye,”aliwaza kichwani mwake akivuta shuka na kujifunika.
Asubuhi ya siku hiyo yeye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuamka kitandani, taratibu bila kumwamsha Lina alitoka ndani ya chumba na kuelekea jikoni ambako aliandaa kila kitu kwa ajili ya kifungua kinywa na kurejea chumbani ambako alifungua kabati akatoa nguo na kunyoosha tayari kwa maandalizi ya kwenda kazini.
“Darling?” (Mpenzi)
“Yes baby.” (Ndiyo mpenzi)
“Amka! Amka ukaoge sasa,” akasema Phillip kwa sauti ya kunong’ona.
“Mh!” Lina aliguna akijinyosha kitandani.
“Muda umefika?”
“Zamani sana mke wangu.”
Taratibu akafunua shuka na kunyosha mkono kuchukua simu yake ambayo haikuwa mbali, akatupa macho yake hapo na kugundua kwamba muda ulikuwa umewadia na alitakiwa kufanya haraka ili wasichelewe.
Taratibu akashusha miguu yake kitandani huku akiwa katika hali ya usingizi, Phillip akamshika mkono na kumuongoza moja kwa moja mpaka bafuni ambako walioga na kutoka.
“Utavaa nini leo?”
“Mimi?”
“Ndiyo.”
“Nguo tayari nimeshanyoosha.”
“Unasema kweli?”
“Hakika, nimeamka kitambo kidogo.”
Lina akasogea na kumbusu Phillip usoni ikiwa ni ishara ya kumshukuru, hakika watu hawa walikuwa katika penzi motomoto, kila mmoja akifanya mambo mazuri kwa mwenzake kadiri alivyoweza.
Kwa pamoja wakavaa na kutoka chumbani kuelekea sebuleni ambako nako mambo yalizidi kumshangaza Lina kwani tayari chai ilishatengwa mezani, kazi yake ilikuwa ni kusogea na kunywa.
“Leo umenifanyia mchezo wa ajabu sana mume wangu.”
“Kwa sababu nakupenda kupita kawaida.”
“Najua, nami pia ninakupenda sana Phillip.”
Kwa pamoja wakasogea mezani na kuketi hapo, wakanywa chai na walipomaliza Lina akachukua ufunguo wa gari lake aina ya Land Cruiser na kumkabidhi Phillip.
“Wewe leo ndiye dereva.”
“Mh! Una uhakika?”
“Kabisa gari hilo ni lako sasa.”
“Na wewe je?”
“Nitapata lingine muda si mrefu.”
“Ahsante kwa kunipenda mke wangu.”
“Usijali.”
Huku mkono wa Phillip ukiwa kiunoni mwa Lina, taratibu wakitembea kuelekea eneo gari lilipoegeshwa, Phillip akabonyeza kitufe fulani kwenye ufunguo na milango ikafunguka kisha kushika mlango mmoja wa mbele akaufungua na taratibu akamkaribisha Lina ambaye aliingia na kuketi huku akitabasamu.
Phillip naye akaelekea upande wa pili kwa dereva na kuingia ndani yake, akawasha gari kisha kutoka nje ya lango huku akipunga mkono kwa mlinzi ambaye naye aliachia tabasamu.

***
Baada ya kutangaziwa hali ya machafuko nchini Urusi uamuzi pekee uliofikiwa na uongozi wa shule ni kufunga shule kwa muda, mkutano ukaitishiwa na wanafunzi kupewa taarifa kwamba uongozi wa shule ulikuwa umeamua kusitisha masomo kwa muda kutokana na hali ilivyokuwa na kuwataka wanafunzi warejee majumbani mwao mpaka hali itakapotulia.
Uamuzi huo pekee uliwafanya Mariya na Merina kutoa machozi, hawakuwa na uhakika kama wangeweza kufika nyumbani kwao salama bila matatizo yoyote, isitoshe walizoea kuletwa shuleni na kufuatwa na sasa walikuwa wakirejea nyumbani wenyewe bila dereva.
“Mariya!” Merina aliita.
“Bee!”
“Twende huku.”
“Mimi sitaki nitakaa hapahapa kungojea gari la nyumbani.”
“Haliji sasa hivi na hali inazidi kuwa mbaya twende!”alisema Merina akimvuta Mariya ambaye muda wote alikuwa akilia.
Kwa pamoja huku kukiwa na purukushani nyingi, wakafanikiwa kutoka nje ya lango la shule wakiwa hawaelewi ni wapi waelekee.
“Merina! Mariya!” wakasikia majina yao yakitajwa.
Wakatupa macho yao kugeuka ili waangalie ni wapi sauti hiyo ilitoka na alikuwa ni nani aliyewatamka kwa majina.
“Mh! Unamjua?” Merina aliuliza.
“Hapana!”
“Lakini anatufahamu mbona ametuita kwa majina?”
“Hebu twende tukamsikilize pengine ametumwa na baba aje kutuchukua!”
“Mimi naogopa!” Mariya alijibu huku akisita.
Mbele yao alionekana mwanaume mrefu, mwili wake ulikuwa umejazia, na kwa kumwangalia harakaharaka alionekana kuwa ni mtu wa mazoezi. Kichwani alivaa kofia kubwa, machoni alikuwa na miwani ya rangi nyeusi. Huku wakitetemeka kwa hofu, wakasogea karibu kabisa na mwanaume huyo.
“Mariya! Merina!” akaita tena.
“Bee!” wakaitika huku wakitetemeka kwa hofu.
“Safi dili limekamilika,”alijibu mwanaume huyo na kwa haraka akawakamata kwa nguvu na kuanza kuwavuta kuelekea sehemu ambayo hawakuifahamu.

Wakionekana wenye furaha mara kadhaa wakipigana mabusu bila kujali kwamba walikuwa barabarani, Phillip aliendesha gari na hatimaye kwa muda wa nusu saa wakafika ofisini.
Ni Phillip aliyekuwa wa kwanza kushuka garini na kuzunguka tena upande wa Lina kisha kufungua mlango na kumshika mkono akimkaribisha.

“Ahsante”
“Mwaaa!”Phillip aliachia busu.
Kitendo hicho kilishuhudiwa na watu wengi waliokuwa wamefika ofisini muda huo. Hakika mapenzi yao yalipendeza.
“Si Lina yule?”
“Ndiye.”

“Na yule?”
“Mume wake.”
“Mh! Makubwa haya.”
“Kwa nini?”
“Si umeona mwenyewe,” yalikuwa ni maongezi ya wasichana wawili waliofanya kazi ofisi moja na Lina.
Kwa pamoja wakatembea njiani wakipishana na watu kadhaa na kuwasalimia na Lina alifanya utambulisho kidogo na kuendelea mbele.

“Ngo!Ngo!Ngo!” Sauti ya mlango ukigongwa ilisikika.
“Ndiyo.” Sauti kutoka ndani ikajibu.
Taratibu Lina akashika kitasa na kusukuma mlango kuingia ndani. Macho yake yakagongana moja kwa moja na bosi wake aliyekuwa ameketi nyuma ya meza kubwa ofisini kwake asubuhi hiyo.
“Karibu sana Lina.”

“Ahsante,” alijibu Lina na alipofungua mlango vizuri alionekana kuongozana na mtu mwingine.
“Karibuni sana,” aliongea bosi huyo akijiweka vyema kitini huku macho yake yakimwangalia Phillip.
***
“Watoto hawa watanipa kile ninachokitafuta,” aliwaza mwanaume huyo akizidi kuwavuta watoto Mariya na Merina kuelekea sehemu ambayo hawakuifahamu.

Badru Divostroc alikuwa ni mwanaume katili aliyeogopwa na watu wengi nchini Urusi kwa vitendo vyake vya kimafia, kutokana na ukatili wake huo watu wengi nchini humo wakambandika jina la Kuntakinte.
Kwake yeye kupata alichokihitaji halikuwa tatizo, hakuogopa kumwaga damu za watu ili mradi tu atimize alichokikusudia.

Kwa muda mrefu alifuatilia kwa ukaribu habari za tajiri Fedorov alitaka kumfahamu lakini hakupata mwanya huo, hivyo taarifa za Mariya na Merina ambao walikuwa ni watoto wa Victor Fedorov kuingia nchini Urusi kulimpa furaha ya ajabu.
Baada ya kufuatilia kwa kina na kugundua kwamba Victor Fedorov aliwapenda watoto wake kuliko kitu kingine, aliamua kuwafuatilia kwa ukaribu akichunguza shule waliyosoma na ni gari lililowapeleka na kuwafuata kuwarudisha nyumbani.
Kwa muda wa mwezi mzima alifanya kazi hiyo hatimaye akafanikiwa kugundua njia zote na namna watoto hao walivyopelekwa shuleni na kufuatwa wakionekana kuwa katika ulinzi madhubuti.

Ni machafuko yaliyokuwa yakitokea nchini Urusi kwa wakati huo kwake yeye aliona ni kama bahati kwani nia yake ya kufanya utekaji nyara wa watoto wa tajiri kama Victor Fedorov kungempa alichokikusudia.
“Leo nitajaribu kufanya utekaji nitatumia akili zangu zote kuwapata watoto wa Fedorov halafu…,”aliwaza huku akinyanyuka kitandani.

Akiwa chumbani kwake akaisogelea televisheni yake na kuiwasha macho yake yakakutana moja kwa moja na habari za maandamano makubwa ya wananchi nchini Urusi waliokuwa wakipinga matokeo ya jeshi la polisi baada ya kusitisha msako wa kumsaka Ditrov, wananchi walikuwa wakiandamana mitaani wengi wakishinikiza msako uendelee.
“Hureee! Hureee utajiri huo mikononi mwangu,”alipiga kelele akirukaruka chumbani mwake.

Taarifa hiyo iliamsha vyema hisia zake, kwani kwa muda mrefu alikuwa amefanya kila alichoweza kupata utajiri aliokuwa nao Victor Fedorov lakini hakufanikiwa, sasa ulikuwa umekaribia kuingia mikononi mwake.
Haraka bila kuchelewa akavuta suruali yake aina ya jeans, fulana pamoja na koti kubwa akavaa, akageuka tena upande mwingine akavuta soksi za mikononi na kuzivaa kisha kofia kubwa pamoja na miwani ya rangi nyeusi akakisogelea kioo kilichokuwa chumbani kwake na kujiangalia na kutikisa kichwa kwa jinsi alivyobadilika.

Taratibu akanyanyua gorodo na kuchukua bastola yake ndogo na kuipachika kiunoni.
“Hakuna mtu atakayeweza kunitambua kwamba mimi ndiye Badru…,’aliongea akifungua mlango ili atoke nje.
Akitembea kwa kujiamini moja kwa moja akaliendea gari lake aina ya Noah akaingia na kuliwasha, mawazo yake yote yakiwa juu ya watoto wa Victor Fedorov, aliamini kama angefanikiwa kuwapata watoto hao na kuwateka hakika angepata malipo makubwa kutoka kwa tajiri huyo.

Kwa mwendo wa dakika kumi nzima aliendesha gari hatimaye akafanikiwa kufika shule waliyosoma watoto hao. Akaliegesha gari lake mbali kidogo na shule kisha kushuka na kutembea njiani akipishana na watu wengi wakikimbia huku na kule.

“Wale pale,”aliongea akisogea karibu kisha kuanza kuwaita kwa majina.
“Wewe ni nani?”

“Hakuna haja ya kunifahamu, twendeni huku.” Sauti ya mwanaume huyo ikajibu akiwavuta watoto hao.
“Mariya” Merina aliita huku akilia.
“Bee.”
“Huyu ni nani na tunakwenda wapi?” Merina aliuliza swali jingine tayari wote wawili walikuwa wakilia huku wakijaribu kujitoa mikononi mwa mwanaume huyo.

Kwa nguvu zake zote aliwavuta watoto hao mpaka wakalifikia gari ambalo lilikuwa limeegeshwa nje kidogo ya eneo la shule akafungua mlango na kuwatupia ndani yake, akaangaza macho huku na kule kuangalia kama kulikuwa na mtu yeyote karibu eneo hilo, wengi walionekana wakikimbia kunusuru maisha yao.

“Ninachohitaji hivi sasa ni fedha, Victor Fedorov ni lazima atoe fedha kuwaokoa watoto wake vinginevyo nitawaua,” Badru aliwaza kisha aliwasha gari na kuliondoa kwa kasi.
Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 28


Mshtuko aliokuwa ameupata hakika ulikuwa hauelezeki, kupotea kwa watoto wake wawili? Lilikuwa ni swali ambalo halikuwa na jibu kichwani mwake, kwa dakika tano nzima aliendelea kubaki chini akiwa haelewi ni kitu gani angefanya ili kuwapata watoto wake Mariya na Merina.

Machozi yakamtiririka, alipojaribu tena kupaza sauti yake akiwaita kwa majina bado hakusikia sauti yoyote zaidi ya mwangwi uliopenya moja kwa moja masikioni mwake. Victor Fedorov akajiona ni mwanaume mwenye mkosi maishani mwake.

Akiwa haelewi ni kitu gani afanye, alijikongoja na kunyanyuka chini bado akiendelea kuangaza macho yake huku na kule pengine kuona kama walikuwa wamejificha mahali na baada ya kumwona wangejitokeza awachukue na kwenda nao nyumbani. Haikuwa kama alivyowaza, bado Merina na Mariya hawakuonekana sehemu yoyote ile ndani ya shule. Jasho jingi likimtiririka, alijikongoja na kulifikia gari lake akafungua mlango na kuingia ndani kisha akaliwasha na kutoka eneo hilo la shule.

“Watakuwa wapi hawa? Nini kimewapata watoto wangu,” alijiuliza maswali mfululizo bila kupata majibu.
Nje ya lango la shule bado vurugu iliendelea kuongezeka, watu wengi wakionekana kukimbia huku na kule kuokoa maisha yao, akakodoa macho yake yote kuangaza kila upande akiwatafuta watoto wake lakini bado hakuwaona, lakini akiwa hapo akajipa moyo na kuamini kwamba huenda walimu waliamua kuwarudisha nyumbani kwa sababu ya machafuko yaliyokuwa yametokea siku hiyo.

“Nakwenda nyumbani watakuwa huko nina uhakika,” aliwaza akikanyaga mafuta kusonga mbele.
Victor Fedorov aliishi nje kidogo ya jiji, hivyo ilimchukua muda wa dakika arobaini kufika kwenye makazi yake, kichwani mwake akiwa na mawazo mengi juu ya usalama wa watoto wake ambao mpaka wakati huo hakufahamu kabisa ni wapi walipokuwa na kama walikuwa hai au wamekufa.

“Piii!Piiii!” ilikuwa ni honi nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake.
Mara moja bila kuchelewa mlinzi alilifungua lango, akaingia ndani ya ngome ambapo aliliegesha gari lake kisha akashuka haraka.

Akazungusha macho yake huku na kule ndani ya ngome yake lakini hakuona kitu, hata alipojaribu kuangalia gari ambalo mara kadhaa liliwapeleka shule watoto wake na kuwafuata, nalo pia halikuonekana sehemu yake.
“Watoto wamerudi?” aliuliza kwa sauti ya ukali.
“Hapana bosi.”

“Unasema kweli?”
“Nina hakika.”
“Zhukov naye yuko wapi?”
“Sijamwona.”

“Mungu wangu watoto wangu!” alisema Victor Fedorov akichomoa simu yake ya mkononi mfukoni, akaonekana akibonyeza namba kadhaa kisha kuiweka sikioni na kusikiliza. Akiwa hapo mlinzi akamshuhudia bosi wake akitoka mbio kuelekea ndani bila kusema chochote, alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa kabisa.

Aliingia ndani na dakika mbili baadaye alitoka nje mkononi akiwa na bastola, na bila kusema chochote akaamuru lango kuu lifunguliwe, akaingia ndani ya gari kisha kuliwasha na kutoka mbio kama vile alikuwa katika mashindano.
“Nitaua! Nasema nitaua sina mchezo mbele ya watoto wangu,” alisema peke yake ndani ya gari.

Huku akiwa katika mwendo wa kasi, Victor Fedorov aliendelea kuangaza macho yake huku na kule pembezoni mwa barabara lakini bado hakuwaona watoto wake. Alikuwa ameamua kuingia mwenyewe barabarani akiwasaka kwa udi na uvumba watoto wake Mariya na Merina ambao mpaka wakati huo hakujua walikuwa wapi na kitu gani kilikuwa kimewapata. Kwa saa saba mfululizo aliendelea kuwasaka huku akijaribu kuwasiliana na watu mbalimbali kwa msaada, lakini bado hawakupatikana sehemu yoyote.

Hatimaye akaamua kuingia katika hospitali moja baada ya nyingine akiuliza kama kulikuwa na majeruhi yeyote au watu waliofariki, lakini bado jibu liliendelea kubaki palepale; hakukuwa na kitu cha aina hiyo.

“Fyuuu!”akashusha pumzi kwa nguvu. Victor Fedorov hakuwa tayari kuwapoteza watoto wake alikuwa tayari kutumia kila kitu alichokuwa nacho lakini si kuwakosa maishani mwake, hakika aliwapenda kupita kawaida katika maisha yake yote yaliyobaki duniani, aliamini hakuwa na ndugu mwingine zaidi ya watoto hao.

Siku hiyo ikapita kukiwa hakuna dalili zozote za kuwapata watoto wake na hata alipojaribu kurejea nyumbani na kuangalia bado walikuwa hawajaonekana, akiwa hapo akamkumbuka Ditrov na kuamini kwamba pengine asingemuua angekuwa msaada mkubwa katika kupatikana kwa watoto wake.

“Ditrov angekua hai hakika ninaamini watoto wangu wangepatikana,” aliwaza akijifuta machozi.
Kwa siku tatu mfululizo bado watoto waliendelea kusakwa huku na kule nchini Urusi pamoja na machafuko yaliyokuwepo, nchi hiyo ilibinuliwa nje ndani, msaada mkubwa ukifanywa na polisi lakini bado hawakupatikana.

Hatimaye siku ya nne asubuhi Victor Fedorov akiwa ameshakata tamaa juu ya kuwapata watoto wake, wazo likamjia kichwani mwake kwamba ajaribu kutangaza katika vyombo vya habari juu ya kupotea kwa watoto.

Huku akiwa mwenye mawazo mengi akakubaliana na wazo hilo.
“Nitakwenda kwenye televisheni ya taifa na kutangaza pengine kuna mtu amewaona sehemu fulani,” aliwaza akilini mwake.

Ndani ya nyumba yake hakukulika wala kukakalika, mawazo na akili yote ilielekea kwa watoto wake. Hivyo asubuhi hiyo alitoka nyumbani kwake na jambo moja tu; tangazo.

Akaingia ndani ya gari lake na kuliwasha bila kusema chochote akamwonyesha mlinzi ishara na lango likafunguliwa, taratibu akaanza kutoka nje, lakini kabla hajafika mbali mbele yake aliona kitu ambacho hakikuwa cha kawaida.

“Mh ni kitu gani kile?” alijiuliza akizima gari lake na kushuka kukielekea kitu hicho moyoni mwake akiwa na wasiwasi mwingi.


JASHO jingi lilikuwa kitiririka mwilini mwake, akatembea taratibu kukielekea kitu kilichokuwa mbele yake hatua chache tu tayari akawa amekifikia, alipotupa macho yake vyema kuangalia aligundua ilikuwa ni bahasha kubwa nyeupe na juu yake iliandikwa kwa maandishi ya rangi nyekundu akasimama kwa muda akijaribu kusoma ni kitu gani kiliandikwa juu yake.

“Victor Fedorov!” Moyo wake ukazidi kumwenda mbio, kitendo cha kukuta bahasha hiyo nje ya lango lake hakikuwa cha kawaida tena na jina lake kwa maandishi ya rangi nyekundu? Likawa ni swali jingine kichwani mwake akazidi kuchanganyikiwa.

Bila kupoteza wakati akiwa haelewi ni kitu gani kingetokea akapiga moyo konde na kuinama kuikota bahasha hiyo na kwa ujasiri wa hali ya juu haraka akaifungua ndani na kutoa kipande kidogo cha karatasi nacho pia kiliandikwa kwa rangi nyekundu.
“Anayeua kwa upanga naye hufa kwa upanga” Kilisomeka kipande hicho cha karatasi.

Victor Fedorov akiwa haamini maneno aliyokutana nayo ndani ya karatasi hiyo akapikicha macho yake tena na kurudia bado yaliendelea kusomeka hivyo hivyo kama mwanzo.
“Mungu wangu!” Akasema kimoyomoyo akiketi chini na kuendelea kusoma zaidi.

“Ninachohitaji kwako ni fedha, ili uweze kuwapata watoto wako Merina na Mariya kama unawahitaji wakiwa hai. Ninatoa muda wa saa ishirini na nne tu kuanzia sasa vinginevyo watakuwa marehemu, nakuhakikishia watakufa kifo kibaya kwa kuwakata kiungo kimoja baada ya kingine hadi umauti uwafike.
Kumbuka kama unawapenda watoto wako ni vyema ukafanya kila unachoweza ili uweze kuwapata na usijaribu kutumia jeshi la polisi kwa usalama zaidi.

Mara tu utakapokuwa tayari nitapenda unitaarifu kwa namba hizo hapo chini ili tukubaliane, sawa?
Tahadhari mimi ni mtu hatari sana, ukigeuka nyuma utaniona , kushoto, kulia na mbele pia nipo hivyo kabla hujafanya maamuzi yoyote tumia busara zako zote vinginevyo utajuta…
Kwa heri.” Ilisema sehemu ya barua hiyo.

“Ni Ditrov.”Alinong’ona.
Victor Fedorov akahisi vitu kama maji maji vikitiririka ndani ya suruali yake, hakika hakuamini alichokisoma kichwani mwake taswira ya Ditrov ikamjia akahisi pengine mtu huyo hakufa kama alivyofahamu.
“Noooo!” Akapaza sauti.

Akatupa macho yake pande zote nne bila kuona kitu akayerejesha tena kwenye saa yake ya mkononi akasoma akagundua amebakiza saa kumi na tisa tu muda aliokuwa amepewa na mtu aliyedai kuwa na watoto wake uwadie vinginevyo wangekufa.
“Mariya! Merina!” Akaita akikimbia kuelekea ndani ya nyumba yake, bila kukumbuka gari alilokuwa ameliegesha pembeni kidogo.

Moja kwa moja akagonga lango na mlinzi kulifungua bila kusema chochote akazama ndani akikimbia huku akilia.
“Kuna nini tena?” Mlinzi aliuliza lakini hakujibiwa kitu chochote.
Tayari Victor Fedorov alishazama ndani, kitu cha kwanza bila kupoteza wakati akaisogelea simu akainyanyua ili apige namba aliyokuwa ameisoma kwenye kipande cha barua kilichokuwa mkononi mwake.

Huku machozi yakimbubujika akakikunjua kipande hicho na kuanza kuzisoma namba na kubonyeza moja baada ya nyingine kisha kuweka mkono wa simu sikioni akisikiliza upande wa pili.

Takribani dakika tatu nzima simu hiyo iliita bila kupokelewa akili yake ikazidi kuvurugika akiwa haelewi ni kitu gani angefanya upande mmoja wa akili yake ukimwambia atoe taarifa hiyo kwa Jeshi la Polisi na mwingine ukimwambia kufanya hivyo ni kuwapoteza watoto wake wapendwa Mariya na Merina kwani alishapewa onyo juu ya jambo hilo.

“Hapana ngoja niwe mvumilivu nitawapata tu, isije kuwa ni Ditrov hana huruma mtu huyu anachokisema kinakuwa kweli, atawaua watoto wangu!” Alijiuliza maswali mengi mfululizo bila kupata majibu.
Dakika tano nzima baadaye alikuwa tena katika simu akibonyeza namba zile zile na kusikiliza ghafla akasikia sauti nzito upande wa pili ikapokea.

“Ah!Ah!” Kigugumizi kikamshika pamoja na ukatili wake wote Victor Fedorov hapo alikuwa hana ujanja tena, alikuwa tayari kupoteza kila kitu alichokuwa nacho lakini si watoto wake, aliwapenda kupita maelezo.

“Niko tayari...sawa…ndiyo…hapana…usiwaue…nitakupa hata kama ni utajiri wangu wote….Mungu wangu…niambie unapatikana wapi…nimekuelewa sitafanya hivyo… niambie unataka kiasi gani?” Yalikuwa ni maongezi katika simu na mtu mwingine upande wa pili ambaye hakuonekana na baada ya maongezi hayo simu ikakatwa.

Akiwa amepigwa na butwaa, taswira za watoto wake Mariya na Merina zikamjia, masikioni mwake akasikia sauti zao wakimwita na kumwomba asiwaache wafe, Victor Fedorov akalia kama mtoto mdogo. ITAENDELEA
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom