Kanungila Karim
JF-Expert Member
- Apr 29, 2016
- 20,746
- 25,638
MTUNZI :ERIC SHIGONGO
SEHEMU YA 01
GENEVIEVE aliwaangalia watoto wake mapacha na kujikuta akitabasamu, ujio wao duniani ulifuta machozi yake na kumuondolea aibu ya kuitwa mwanamke tasa kila alikokwenda. Alipoikumbuka safari ndefu aliyosafiri kuwatafuta watoto hao ghafla huzuni ikamuingia na kujikuta akilengwalengwa na machozi.
Kabla hajaendelea sana na mawazo hayo mlango wa chumba ulifunguliwa, mume wake Phillip akatokeza nje akiwa amevaa shati lake jeupe, tai ya rangi ya kahawia na suruali iliyonyoshwa vizuri pamoja na viatu vilivyong’arishwa vyema, begani mwake alikuwa na begi la kompyuta yake ndogo.
“Nini tena?”
“Basi tu.”
“Basi tu nini?”
“Yaani kila siku ninapowaangalia Dorice na Dorica siamini kama hatimaye na mimi nina watoto tena wazuri kiasi hiki, badala ya kufurahi huwa naishia kuingiwa na huzuni.”
“Mwaaa!” Phillip alimbusu mkewe kwenye paji la uso huku akitabasamu.
“Asante.”
“Usijali darling, ni jambo la kumshukuru Mungu. Usiiangalie sana historia, wewe furahia kwamba hatimaye sasa tuna watoto na leo wanakwenda kuanza darasa la kwanza kwa mara ya kwanza.”
Phillip aliongea kwa sauti ya upole huku wote wawili wakiwaangalia watoto wao wazuri wa kike mapacha wakiwa wamekaa kwenye meza wakinywa chai, tayari walikuwa na miaka mitano, walikuwa na hamu kubwa ya kufika shuleni kuanza darasa la kwanza baada ya kusoma chekechea kwa miaka miwili.
“Daddy!” Dorice alimuita baba yake.
“Yes, darling.”
“Guess what?” (Hebu buni kuna nini?)
“What is it my sweetie!” (Nini mpenzi wangu?)
“Today we are going to school!” (Leo tunakwenda shule.)
“I know darling, make sure you do good in writing, reading and counting, okay?” (Najua mpenzi wangu, hakikisheni mnafanya vizuri kwenye kuandika, kusoma na kuhesabu, sawa?)
“Yes daddy, I am going to be the first and Dorica the second.” (Sawa baba, mimi nitakuwa wa kwanza na Dorica wa pili.)
“No! I will be the first and you the second.” (Hapana! Nitakuwa wa kwanza halafu wewe wa pili.) Dorica alijibu.
Genevieve na Phillip wakacheka kwa sauti kisha kunyanyuka kwa pamoja mahali walipoketi kwenda kuwakumbatia watoto wao, wakawabusu na hapohapo kuanza kusali wakiwaombea wafanye vizuri shuleni.
Zoezi hilo lilipomalizika, Phillip aliwaaga wote na kuwatakia siku njema kisha kutoka hadi nje ambapo aliingia ndani ya gari lake na kuondoka akiamini saa mbili kamili ikifika mke wake angewachukua watoto hadi barabarani ambako basi la shule lingepita na kuwabeba.
Waliishi Upanga karibu kabisa na eneo la katikati la jiji la Dar es Salaam, lakini ofisini kwa Phillip ilikuwa ni maeneo ya Victoria kilomita kama ishirini hivi kutoka katikati ya jiji. Wakati watu wengi waliteseka kwenye msongamano wa magari asubuhi kwenda kazini sababu ofisi nyingi zilikuwa katikati ya jiji, yeye hakuelewa hata kama kulikuwa na msongamano, alipishana nao asubuhi akielekea kazini nje ya jiji.
Baada ya kuingia tu ndani ya gari lake aliendesha kwa kasi ya kawaida akiwahurumia watu wa upande wa pili wa barabara ambao magari yao yalikuwa yamesimama bila hata kusogea mbele, kichwani mwake aliwaza sana juu ya watoto wake wa pekee Dorice na Dorica, wao ndiyo waliomfanya afanye kazi kwa nguvu sana kwa sababu hakutaka wapate shida maishani mwao.
Katika umri wa miaka mitano tu tayari kila mmoja kwenye akauti yake ya Jumbo kwenye Benki ya CRDB alikuwa na kiasi cha milioni nane ambazo Phillip na mke wake walipanga kuendelea kuziongeza wakiwa wamedhamiria zifike milioni mia moja kwenye kila akaunti ya kila mtoto watakapokuwa na umri wa miaka kumi na minane.
Mawazo hayo aliendelea nayo mpaka alipokuwa anakata kona kuingia ofisini kwake ambako aliegesha na kushuka, kabla hajaondoka simu yake ya mkononi ikalia, akifunga mlango aliibana kwa bega sikioni na kuanza kusikiliza taratibu akiwa bado hajaelewa ni nani aliyempigia kwani namba haikuonyesha jina bali maandishi “Call” peke yake ndiyo yaliyoonekana, ishara kuwa simu hiyo ilitoka nje ya nchi.
“Naongea na Phillip?”
“Ndiyo, nani mwenzangu?”
“Huhitaji sana kufahamu jina langu, ila nimekupigia kukutaarifu kuwa kama kuna uwezekano naomba usiwapandishe watoto wako kwenye basi la shule, kuna bomu limetegwa ndani yake litalipuka muda mfupi tu wakishapanda, watakufa hapo hapo! Nimekupigia kwa sababu najua ni kiasi gani unawapenda watoto wako.” simu ikakatwa.
Mwanzoni Phillip alidhani labda siku hiyo ilikuwa ni tarehe moja mwezi wa Nne, Siku ya Wajinga Duniani lakini alipoangalia saa yake mkononi alikuta ilikuwa ni tarehe tofauti. Upande mmoja wa moyo wake ukamwambia apuuze maneno hayo lakini upande mwingine ukamtaka ampigie simu mkewe haraka iwezekanavyo na kumsimulia habari hiyo ya kuogofya.
Simu iliita sana lakini haikupokelewa, akaendelea kupiga tena na tena lakini hali ilikuwa hiyo hiyo. Akathibitisha haikuwa tabia ya Genevieve kutopokea simu yake hasa alipopigiwa na mume wake maana hawakuwa na tabia ya kupigiana simu zisizo na maana, hii ilimfanya Phillip aingie ndani ya gari lake haraka na kugeuza akiwa amepuuza hata muda wa kuwahi kazini, kwake familia kilikuwa kitu cha kwanza.
Haraka akaanza kuendesha kuelekea mjini, hakwenda umbali mrefu akakutana na msongamano wa magari ambao wala ulikuwa hausongi mbele. Kwa mkono wa kuume akiwa ameshika usukani na kwa mkono wa kushoto simu ikiwa sikioni akiendelea kuwasiliana na Genevieve bila mafanikio, bado simu ilikuwa haipokelewi.
Alipofika maeneo ya Morocco aliamua kuiingiza gari yake kwenye kituo cha mafuta cha Bonjour, kando tu mwa kibanda ambacho hutumika kuuza baga, akashuka haraka na kukimbia upande wa pili ambako alimkodisha mtu wa Bajaj aliyekuwa akipita na kumtaka amwahishe haraka sana mjini.
Akiwa ndani ya Bajaj aliendelea kupiga simu huku wasiwasi wake ukiendelea kuongezeka, isingewezekana mke wake muda wote huo awe mbali na simu. Hakumpata Genevieve na Bajaj ilikuwa ikienda kwa mwendo mdogo sana, alipofika eneo liitwalo Mbuyuni alilazimika kumlipa dereva wa Bajaj ujira wake, akashuka na kukodisha pikipiki hiyo ndiyo ilimpeleka moja kwa moja hadi nyumbani kwake.
“Genevieve! Genevieve!” Aliita akigonga mlangoni lakini hakuitikiwa na mlango ulikuwa umefungwa.
Akaendelea kupiga simu, alipousikia mlio kutoka ndani tena sebuleni, alielewa mke wake alikuwa ameisahau simu ndani na kupeleka watoto barabarani. Haraka akarukia juu ya pikipiki na kumwamuru dereva aondoke kwenda barabarani mahali ambapo basi la shule hupita kuchukua wanafunzi.
Walipokaribia eneo hilo aliliona gari la mke wake likiwa limeegeshwa kando ya barabara, yeye mwenyewe akiwa amesimama nje akiliangalia gari la shule likiondoka mwendo wa taratibu, tayari Phillip akawa amefika na kuruka kwenye pikipiki. Genevieve alipomuona alishituka sana.
“Nini tena?”
“Watoto wako wapi?”
“Wako kwenye gari la shule.”
“Mungu wangu!”
“Nini?”
Phillip akadandia tena pikipiki na kumwamuru dereva aanze kulifuata basi la shule wakimwacha Genevieve mahali alipokuwa, hawakwenda mbali sana, gari likiwa umbali wa kama mita hamsini kabla hawajalifikia, walisikia kishindo cha ajabu “Puuuuuu”. Wakaanguka chini, gari la wanafunzi lilikuwa limelipuliwa na bomu.
Nani amefanya unyama huu? Dorice na Dorica wamekufa?
Mlipuko huo uliwafanya Phillip na mwendesha pikipiki waanguke kando ya barabara, fahamu za Phillip zikapotea. Alipozinduka alijikuta kitandani, mkononi akiwa na dripu iliyodondosha matone kwa haraka kuingiza kwenye mishipa yake. Awali hakuelewa ni kwa nini alikuwa pale lakini alipotulia ndipo akakumbuka picha nzima ya tukio la kulipuka kwa basi lililobeba wanafunzi, wakiwemo watoto wake Dorice na Dorica.
“Mamaaaaa! Watoto wanguuu! Nani amefanya kitendo hiki? Nitamjua,” aliongea kwa sauti ya juu huku akilia, wauguzi wakafika haraka na kuanza kumtuliza.
Faraja zao hazikusaidia, alitaka aoneshwe mahali mke wake Genevieve alipokuwa. Wauguzi hawakuwa tayari, moyoni akaingiwa na wasiwasi kuwa huenda hata yeye alikuwa marehemu. Phillip akiwa kama mtu aliyechanganyikiwa, alinyanyuka kitandani na kusimama wima, dripu ikachomoka.
Hakutaka kuongea kitu kingine zaidi, akatoka kuanza kukimbia kuelekea barabara ya Umoja wa Mataifa, karibu kabisa na Shule ya Al-Muntazir, ambako basi lililobeba wanafunzi lililipukia. Mbele kidogo alisimamisha gari ambalo kwa juu liliandikwa “Taxi”, likaegesha pembeni naye akaingia na kuketi kiti cha mbele kando ya dereva aliyemwangalia kwa jicho la wasiwasi.
“Wapi braza?”
“Pale chini.”
“Wapi?”
“Wewe twende.”
“Nipe kabisa changu,” dereva alisema baada ya kuhisi abiria wake asingemlipa kwani alionekana ni mtu aliyechanganyikiwa.
“Shilingi ngapi?”
“Niambie kwanza unakwenda wapi.”
“Kwenye basi lililolipukiwa na bomu.”
“Ahaa! Shilingi elfu moja.”
Phillip akaingiza mkono mfukoni na kukuta bahati nzuri pochi yake ilikuwepo, akaitoa na kuchomoa noti ya shilingi elfu kumi na kumkabidhi dereva wa teksi. Safari ikaanza kuelekea Al-Muntazir, mbele kidogo walikuta msongamano wa magari, barabara ilikuwa imefungwa kwa sababu ya ajali hiyo.
Phillip akashuka bila hata kudai chenji yake na kuanza kukimbia kwenda mbele. Mtu yeyote aliyemwona lazima alijua akili yake haikuwa sawa, hakujali, akazidi kukimbia akimfikiria mke wake na pia watoto wake. Kila kitu kilichotokea kwake kilikuwa ni ndoto, isingewezekana hata kidogo watoto wake wazuri, tena mapacha, waliofanana kila kitu kwa sura kuwa wamekufa ghafla kiasi hicho?
Alijiuliza bila kupata majibu akiamini muda si mrefu angezinduka ili amsimulie mke wake Genevieve ndoto hiyo, lakini ukweli haukubadilika. Alifika eneo la tukio na kukuta magari ya zimamoto na mamia ya watu wakiwa wamekusanyika kushuhudia kilichotokea. Lilikuwa tukio baya na polisi walikuwa kila mahali wakizuia watu kupita.
Hawakuweza kumzuia Phillip ambaye alipenya mpaka mbele na kuanguka chini akilia baada ya kuyaona mabaki ya watoto wazuri waliokufa kinyama, kiatu kimoja cha Dorica alikitambua, pia chupa ya chai ya Dorice aliyowekewa maziwa na mama yake ilikuwa juu ya lami.
Miili ya watoto wote ilikuwa imelazwa juu ya ardhi ikiwa imefunikwa na mashuka meupe, haikuwa rahisi hata kidogo kuitambua kwani iliharibika kupita kiasi. Phillip akanyanyuka na kuanza kuzunguka kwenye miili hiyo akifunua ili angalau aweze kuwaona watoto wake. Hapakuonekana mwili wa Dorice au Dorica, miili iliyokuwepo ilikuwa imesambaratishwa na kubaki kiungo kimoja kimoja.
“Nani amefanya unyama huu? Nitamjua, sitarudi kazini mpaka siku nitakapomtia mikononi mwangu,” alijisemea Phillip akilia, kisha akakaa chini na kuanza kuiangalia miili hiyo huku akimfikiria mke wake Genevieve ambaye mpaka wakati huo alikuwa hajamwona.
Siku iliyoanza vizuri hatimaye ilikuwa imeharibika, watu walikuwa wakilia kwa uchungu mkubwa, lilikuwa ni tukio baya kuliko jingine lolote kutokea. Phillip hakuwa tayari kuongea na waandishi wa habari walipomfuata. Tayari wazazi wa watoto wote waliokufa walikuwa eneo hilo, vilio vilienea.
Baadaye miili ilianza kubebwa na kuingizwa kwenye gari tayari kupelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Muhimbili. Phillip aliamua kutangulia huko ili akaone mahali ambapo watoto wake wangelazwa. Alifika wakati magari yameshawasili, watu wengi wakiwa wamekusanyika na wafanyakazi wenzake ambao tayari walishapata habari walikuwepo kumfariji lakini alikuwa hafarijiki.
“Jamani nisaidieni kujua mahali mke wangu alipo,” aliwaomba.
Badala ya kumjibu au kusema chochote, wafanyakazi wenzake walikaa kimya, jambo lililoonesha kabisa walikuwa na kitu moyoni. Wasiwasi wa Phillip ukaongezeka, hakuelewa maisha yake yangeendeleaje bila kuwa na familia. Alikitamani kifo kama ingethibitika kuwa, watu wote aliowapenda hawakuwepo duniani.
“Jamani niwaulize kama mnaweza kuwa mnafahamu mahali aliko Genevieve.”
“Tunajua lakini...”
“Lakini nini jamani, hebu nielezeni tu mahali aliko mke wangu, amekufa? Kwa mshtuko huu ukizingatia ana shinikizo la damu, anaweza kuwa amenitoka.
Nitafanyaje mimi? Nitaishije mimi? Eee Mungu, ni kwa nini umeruhusu nipite kwenye jambo hili wakati unaelewa moyo wangu ni mdogo?” Aliuliza maswali mengi akiwa ameshikiliwa na wafanyakazi wenzake walioonekana kuwa na siri nzito mioyoni mwao.
JE NI SIRI GANI NA NINI KITAENDELEA