Simulizi Mpya: Mnyama ndani yangu

fleha

Senior Member
Oct 9, 2014
111
103
MNYAMA NDANI YANGU!

SEHEMU YA KWANZA

Na Nira Saire

Ilikuwa ni siku ya Alhamis majira ya saa nne za asubuhi nikiwa darasani nikisoma na wanafunzi wenzangu, mara hali yangu kiafya ikaanza kubadilika! Ikawa nahisi maumivu ya kichwa yakinianza polepole huku yakiambatana na kizunguzungu!. Nikaamua kulaza kichwa changu kwenye meza ya kusomea iliyokuwa mbele yangu ili kuweza kujisikilizia, nikiamini kuwa maumivu yale yangepita lakini hali ilikuwa tofauti na matarajio yangu,kwani maumivu yalizidi mara dufu hadi nikaanza kujihisi kuchanganyikiwa!. Akili ikanituma kuelekea kwenye vyoo vya shule ili niweze kupata maji ambayo niliamini kama ningeyatia kichwani basi yangeweza kunisaidia kupata unafuu, wakati huu rafiki yangu Majoba alikuwa amegundua kuwa sikuwa sawa hivyo akanifuata nilipokuwa natoka nje ya darasa lile huku akiniuliza nilikuwa na tatizo gani, sikuweza hata kumjibu, mimi niliendelea kukazana kuelekea maeneo ya vyoo naye akaendelea kunifuata kwa kasi akizidi kunisemesha, hata sikuweza kumsikia tena alikuwa anasema nini na wala sikuweza kujua nini kiliendelea kwani nilipoteza fahamu!......

Fahamu zilipokuja kunirudia nilijikuta katika mazingira ambayo yalikuwa ni mageni sana kwangu, lilikuwa ni eneo ambalo lilikuwa na miti mingi sana na kwa haraka haraka sikukumbuka kama nilishawahi kuwepo kwenye eneo lile abla, wakati huo fahamu ziliendelea kunirudia taratibu nikaanza kukumbuka safari yangu ya kutoka darasani na kuelekea eneo la vyoo vya shule, lakini kila nilipojaribu kukumbuka nini kilifuata nilibaki kuishia gizani. “unajisikiaje?” ilisikika sauti ikizungumza kutoka nyuma yangu, nilishtushwa sana na sauti ile kwa maana sikutegemea kama kuliuwa na mtu pale! Nikageuka na kumtizama mtu yule ambaye alikuwa ni mzee, “shikamoo” nikajikuta nimemsalimia, nikiwa bado nipo katika hali ya wasiwasi, mzee yule akaoesha tabasamu ambalo bila shaka lilidhamiria kunitoa wasiwasi kisha akaitikia “Marahaba Musa, maumivu ya kichwa yameisha?” Nikazidi kushangazwa baada ya kuona kuwa mzee yule alikuwa akinifahamu,kwani kwangu ilikuwa ni mara ya kwanza kumuona! “ndio, lakini bado nahisi kizungu” nilijibu. Mzee yule akanipa kikombe ambacho kilikuwa na kimiminika ambacho kwa muonekano wa rangi yake kilitokana na kusagwa majani fulani,”kunywa hii dawa itakupa nguvu” alisema mzee yule wakati akinikabidhi, nami nikaipokea dawa ile na kuinywa kidogo kabla sijasitisha haraka baada ya kugundua kuwa ilikuwa chungu mno! “jitahidi uimalize yote hiyo dawa” alisema mzee yule kisha akaongeza “wala usijisikilizie, kunywa yote haraka kama maji” Sijui kwanini nilikuwa namsikiliza mzee yule ambaye sikuwa nikimjua lakini nilijikuta nikitii maelekezo yake na kuimaliza ile dawa mara moja, mwili wangu ulisisimka sana wakati nikisikilizia uchungu wa ule dawa lakini msisimko ule ukaondoka na kizunguzungu kilichokuwa kimeniandama kwa muda mrefu. “inabidi nikurudishe maana sasa utakuwa unatafutwa” alisema yule mzee! “Usithubutu kumuelezea mtu yeyote juu ya jambo hili, ninajua una maswali mengi ila kesho tutaongea vizuri na utaelewa kila kitu, alinielezea mzee yule kisha akanishika kwenye paji la uso na kunisukuma kwanguvu, nikaangukia mgongo nikiwa nimekaa pale chini, nikapoteza tena fahamu!

“Musa... Musa....we Musa” Fahamu zilikuwa zikinirudia huku nikisikia sauti ya mtu ikiniita kwa mbali kama vile nilikuwa naota, mtu yule alikuwa akiendelea kuita huku akinitikisa, nilipopata kujielewa zivuri niligundua mtu yule alikuwa ni mmoja wa walimu wangu, mwalimu Mdharuba ambaye alikuwa akinifundisha somo la hisabati, nilipojaribu kutizama huku na huko nikagundua kuwa nilikuwa katika eneo la mashamba ya shule nikiwa nimezungukwa na watu wengi sana miongoni mwao wakiwemo walimu, wanafunzi pamoja na skari polisi. Mwalimu Mdharuba akanisaidia kunyanyuka pale chini na tukaanza kutembea kuelekea wenye ofisi za waalimu, moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya mkuu wa shule ambapo kundi kubwa la watu lilibaki nje huko ndani nikaingia mimi pamoja na walimu wawili na askari polisi wawili, humo ndani tukamkuta mkuu wa shule na maongezi yakaanza! Watu wote waliokuwemo mule ndani walitaka kujua nini kilikuwa kimetokea, hivyo wakawa wananiulza maswali ambayo mengi sikuwa na uwezo wa kuyajibu. Lakini katika maswali yao yale nkagundua kuwa rafiki yangu Majoba hakuwa salama kwani walikuwa wakitaka kujua alishambuliwa na nini, hilo pia lilikuwa swali gumu sana kwangu kwani mara ya mwisho mimi kumuona Majoba alikuwa salama tu! Hivyo nikajibu kuwa sikuwa najua chochote kuhusu Majoba “lakini kwa maelezo ya wanafunzi wenzenu inasemekana wewe na Majoba mlitoka darasani pamoja, je mlienda wapi baada ya kutoka darasani?” aliuliza mmoja wa maasakari. “tulitoka tukaelekea chooni” hilo ndilo jibu pekee ambalo niliweza kulitoa. “enhee, nini kikatokea huko chooni?” aliendelea kuuliza yule askari! “kwakweli sikumbuki, nimekuja kujikuta tu mkiniamsha kule kweye mashamba” nilijibu huku nikiruka sehemu ya makutano yangu na yule mzee katika pori ambalo sikuwa nikilijua!. Labda tumpeleke eneo la tukio, anaweza kuona mazingira akakumbuka nini kilitokea, alishauri askari yule mwingine ambaye alikuwa msikilizaji zaidi kwenye maongezi yale, wazo wale likapita bila kupingwa na safari ya kuelekea eneo la vyoo vya shule ikaanza!.. tulipofika eneo ambalo fahamu yangu ilipotelea nilishangaa kuona eneo lile likiwa limetapakaa damu, damu ile ilikuwa nyingi sana kiasi cha kunitia hofu juu ya usalama wa Majoba ambaye tayari nilikuwa najua alikuwa ameshambuliwa ingawa sikujua alikuwa ameshambuliwa na nani..........

Usikose sehemu ya pili!

Nipate kupita:

+255653686008

nirasaire@gmail.com

facebook.com/nira.saire

@nira_saire(instagram)
 
MNYAMA NDANI YANGU!

SEHEMU YA PILI

Na Nira Saire

Kila mtu pale alikuwa amegundua kuwa sikuwa na jibu lolote la kuwapa,baadala yake nilikuwa nikishangaa tu, hivyo wakaniacha nikapumzike kwenye hostel za shule ambapo ndipo nilipokuwa nikiishi.
Nilipofika hostel ndipo nilipokuja kugundua kuwa Majoba alikuwa ameshambuliwa na myama ambaye hakukuwa na mtu yeyote aliyejua alikuwa ni mnyama gani, wanafunzi wenzangu walikuwa wakiongelea namna mwili wake ulivyokutwa ukiwa umeshambuliwa, ulikuwa uchanwachanwa kwa makucha na alikuwa na kovu kubwa sana shingoni. Nilikuwa nikisikiliza maelezo yale kimya kimya kama vile sikuwa nikifuatilia kitu lakini nilikuwa makini sana!.
Wanafunzi wenzangu walipotaka kujua nini nilikuwa najua juu ya shambulio lile kwa mwanafunzi mwenzetu niliwajibu kwa kifupi sana kuwa sikuwa najua kitu na nilikuwa nimechoka hivyo waniache nikapumzike. Hivyo nikaingia kwenye vyumba,moja kwa moja mpaka kitandani kwangu, nikajilaza! Mwili wangu ulikuwa na uchovu sana lakini ilinichukua muda kupata usingizi kwa maana kichwa changu kilikuwa kinasumbuliwa na mawazo ambayo yalikuwa yameuzidi uwezo wangu wa kufikiri, lakini baada ya dakika chache nilipata usingizi.

Sijui nililala kwa muda gani lakini nikiwa usingizini nilipatwa na ndoto ya ajabu,ndoto ile ilikuwa na matukio yote yaliyonitokea toka nilipoanza kuugua nikiwa darasani mpaka nilipotoka kuelekea kwenye vyoo huku Majoba akinifuata, kwenye ndoto hii kulikuwa na muendelezo ambao haukuwepo wakati tukio lile likitokea, nilishangaa kuona ngozi ya mwili wangu ikibadilika, ikawa na manyoya kama ya mbwa, nikajikuta nina hasira na njaa kali sana, wakati huo Majoba alikuwa amenifikia na hakuwa na ufahamu juu ya mabadiko yangu na alikuwa akijaribu kunisemesha, mimi nikageuka kwa kasi ya ajabu na kumkamata,nilikuwa najua fika kuwa nilikuwa nataka kumnyonya damu lakini sikujua kwanini nilikuwa nataka kumfanyia vile, kuna sehemu ya moyo wangu ulikuwa ikijaribu kupingana na jambo lile ambalo upande huo wa moyo ulikuwa ukiliona kuwa la kinyama lakini kuna upande mwingine ambao ulikuwa una nguvu zaidi ukaendelea kunisukuma kufanya kitendo kile. Majoba alikuwa katika mshangao, akajaribu kupambana kuniponyoka lakini nilikuwa imara kumdhibiti huku nikimrarua kwa makucha marefu na makali ambayo yalikuwa yameniota ghafla, nikamjeruhi vibaya sana,akawa anapiga kelele huku akibubujigwa na damu kwenye maeneo mbalimbali ya mwili wake tukokana na majeraha makubwa ambayo nilikuwa nikimsababishia kila nilipokuwa namgusa! Lakini sikuacha, niliendelea kumdhibiti mpaka akaishiwa nguvu na hapo nikatekeleza adhma yangu, nikakamata shingo yake kisha nikaitoboa kwa meno makali ambayo nayo hayakuwa meno yangu ya kawaida, halafu nikaanza kumnyonya damu! Kwa mbali nilisikia sauti za watu wakikimbia kuja eneo lile, nadhani walikuwa wakifuta kelele ambazo alikuwa amezitoa Majoba hapo mwanzoni wakati akijitahidi kukabiliana na mimi, sikujali ujio wa watu wale ambao walikuwa wamekaribia, mimi niliendelea kumnyonya damu rafiki yangu Majoba, na wala sikutamani kuacha kwani kunyonya kule kulikuwa kiburudisho kikubwa sana kwangu. Mara nilisikia kishindo kikubwa sana nyuma yangu, nikasitisha zoezi nililokuwa nalifanya na kuangalia kulikuwa na nini, nikakutana macho kwa macho na mnyama ambaye kwa harakaharaka niliona alikuwa ni sokwe, ila alikuwa mkubwa sana. Macho yake yalionesha wazi kuwa hakuwa pale kiurafiki, bali alikuwa tayari kwa mapambano. Mnyama yule akaanza kunisogelea polepole na kwa tahadhari kubwa, akilini mwangu nikajua kuwa vita ilikuwa imeanza, lakini sikuwa naogopa, nikajikuta nautupa mwili wa Majoba chini na kutoka mbio kuelekea kumvamia mnyama yule, nilikuwa tayari kwa mapambano, mnyama yule aliponiona nikimuendea mbio akasimama palepale alipokuwa, nilipomfikia nikiwa nimejiandaa kumrarua kwa makucha yangu akaniwahi yeye na kuidaka shingo yangu, kisha akaninyanyua juu na kuacha miguu yangu ikining'inia. Nilijaribu kumponyoka lakini sikufanikiwa, nilimjeruhi mikono yake kwa makucha yangu lakini bado hakuniachia, baadala yake akanipiga kofi kubwa sana kwa kutumia mikono yake ambayo ilikuwa mikubwa mno ya yenye nguvu sana!!
Kofi lile likanizindua kutoka usingizini, nikashangaa kujikuta nilikuwa nje, na ulikuwa usiku wa giza nene, nikanyanyuka kutoka pale chini ambapo nilikuwa nimelala na kuanza kuangaza huku na huko, nilipogeuka nyuma yangu nikamuona yule sokwe mkubwa wa kwenye ndoto akiwa amesimama hatua chache tu kutoka nilipokuwepo. Nilishituka sana, sokwe yule akawa ananisogelea polepole na moyo wangu ukajaa hofu zaidi, nikaanza kurudi nyuma polepole lakini nikaona nachelewa, nikageuka na kuanza kukimbia kuelekea ambako hata sikuwa napajua, na sokwe yule akafuata nyuma yangu akinikimbiza nikaongeza mwendo huku nikiwa nageuka na kuangalia nilikuwa nimemuacha mbali kiasi gani, lakini niligundua kuwa alikuwa na kasi zaidi yangu kwani alikuwa karibu zaidi kadri sekunde zilivyokuwa zinasonga, hofu ikazidi kunitawala,miguu yangu ikawa inatetemeka kwa uoga huku ikiishiwa nguvu, nikajikwaa na kuanguka chini huku nikimsikia myama yule akiwa amenifikia,nikajigeuza pale chini na kulala chali nikijiandaa kujitetea lakini nilipomtizama aliyekuwa akinijia hakuwa yule sokwe tena, alionekana kuwa mwanadamu wa kawaida tu ingawa sikumona vizuri kutokana na giza. “unakimbia nini Musa?” aliuliza mtu yule mara baada ya kuwa karibu na mimi kiasi cha kuweza kutambuana. Alikuwa ni yule mzee ambaye nilionana naye na akanipa dawa kabla ya kunirudisha shuleni. Kidogo nikapata ahuweni, nikakaa pale chini huku nikipumua kwa kasi kujaribu kutosheleza mahitaji ya pumzi ndani ya mwili wangu. Mzee yule akaja na kuka pembeni yangu, ukweli ni kuwa nilikuwa namuogopa, lakini uoga niliokuwanao juu ya sokwe aliyekuwa akinikimbiza ambaye nilimuona ndotoni na nikaona ambacho alikuwa anaweza kukifanya ulikuwa ni uoga mkubwa zaidi. Tulikaa kimya kwa muda, mimi sikujua namna ya kuanzisha maongezi na mzee yule,lakini sikujua kwanini yule mzee naye alikuwa kimya.
“bila shaka utakuwa umepata majibu ya baadhi ya maswali yako kutoka kwenye ndoto ambayo umeiota” hatimaye mzee yule akavunja ukimya akaanza kuzungumza. “kila ambacho umekiona kwenye ndoto ile ndicho ambacho kilitokea kabla sijaja na kukutoa pale” alielezea mzee yule,akazidi kunichanganya,nikawa najiuliza kweli ni mimi ambaye nilimuua Majoba? Na kwanini nimfanyie unyama ule rafiki yangu?! “najua una maswali mengi sana, ila niko hapa kukupa maelezo ambayo yatakupa majibu ya maswali yak”, alielezea yule mzee kisha akaanza kunipa historia ya miaka kadhaa iliyopita..
“Baada ya wazazi wako kuoana, waliishi maisha ya furaha sana maana walikuwa wanapendana kwa dhati na walikuwa na mali za kutosha. Mambo yaliendelea kuwa shwari mpaka miaka mitatu baadae, hali ilianza kubadilika baada ya subira ya kupata mtoto kuonekana kutozaa matunda,wakaanza kuangaika kubadili madaktari kwaajili ya kuweza kutatua tatizo hilo ila kila walipopimwa ilionekana kuwa mama yako hakuwa na uwezo wa kupata mtoto, baadae wakahamia kwenye maombi lakini pia hakukuwa na mafanikio, hatimaye wakaanza kwenda na kwa waganga wa kienyeji lakini bado jitihada hizo hazikuzaa matunda. Mama yako alipata mateso sana kutokana na hali yake ya kutokuwa na uweza wa kuzaa, hasa kutoka kwa ndugu wa upande wa baba yako ambao walikuwa wakitamani baba yako angetafuta mwanamke mwingine ili amzalie watoto, lakini baba yako alikuwa na msimamo maana alimpenda mama yako kwa dhati na alikwishaamua kuwa ni bora akose mtoto milele kuliko kumsononesha mkewe kwa kujihusisha na wanawake wengine. Baada ya kukata tamaa,hata mama yako alianza kumshauri baba yako kuoa mke mwingine ili angalau aweze kupata mtoto maaha ilikuwa wazi kuwa pamoja na kila kitu ambacho walikuwa wanacho,kukosekana kwa mtoto kulipunguza kitu,lakini bado baba yako alisema hapana, na akashikilia msimamo wake huo wa kutojihusisha na mwanake mwingine yeyote zaidi ya mke wake, lakini hawakuacha kujaribu kila ambacho walishauriwa kuwa huenda kingewasaidia kutatua tatizo lao.
Siku moja baba yako akiwa anasafiri alikaa kwenye basi na mzee mmoja ambaye alikuwa na afya dhaifu, muda wote alikuwa kimya sana na hakuonekana kuwa na furaha, walipofika mahali ambapo wangeweza kupata chakula, baba yako akamtaka mzee yule washuke wakapate chakula lakini mzee yule alikataa akidai hakuwa na pesa baba yako akamwambia kuwa alikuwa tayari kumsaidia pesa kwaajili ya chakula lakini bado mzee yule aligoma kushuka kwenye gari, akashukuru na kudai kuwa hakuwa na njaa. Baba yako akaenda kupata chakula,lakini aliporudi akamletea mzee yule chakula,mzee yule akakipokea na kukila na hapo ukawa mwanzo wa mazungumzo yao.
Mzee yule akaelezea kuwa alikuwa anakwenda kwenye safari ile kumfuatilia mwanaye ambaye alikuwa ametoweka nyumbani kwao kwa miaka mingi na sasa alikuwa amepewa taarifa kuwa mwanaye huyo alikuwa ameonekana, akapewa maelekezo ya namna ya kumpata na sasa alikuwa anakwenda kuona kama atafanikiwa kumuona mwanaye huyo,akidai kuwa alitaka kumuona japo mara moja tu ya mwisho kabla ya kufa kwake, akielezea maelezo yale hakuweza kuzuia machozi yake yasitirirke, hali iliyomfanya baba yako kumuhurumia sana na kuahidi kumsaidia mzee yule kumpata mwanaye.
Walipofika mwisho wa safari ile baba yako akamuomba mzee yule afikie nyumbani kwake kisha kazi ya kumtafuta mwanaye ianze kesho yake kwani muda ulikuwa umekwenda sana na walikuwa wamechoka na safari,mzee yule akakubali,akampeleka nyumbani kwake ambapo mzee yule alikarimiwa sana, baba na mama yako wakamuhudumia kama vile alikuwa ni mzazi wao.
Kesho yake baba yako akatoka na yule mzee kwenda kumtafuta mtoto wake, wakifuata maelekezo ambayo mzee yule alikuwanayo lakini safari yao haikuwa ya mafanikio kwani welikwenda kugundua kuwa mtoto wa mzee yule alifariki wiki moja iliyopita, mzee yule aliumia sana kwa taarifa zile akalia sana kwa uchungu,wakaoneshwa marehemu alipozikwa kisha wakarudi nyumbani na zee yule, mzee yule hakutaka tena kukaa pale nyumbani akaomba aruhusiwe ili arudi kijijini kuelezea taarifa za msiba lakini wazazi wako walimzuia wakimtaka apumzike mpaka kesho yake ambapo wangempeleka, mzee akakubali.
Usiku wa siku hiyo yule mzee akaumwa sana, wazazi wako wakampeleka hospitali ambako alilazwa nao wakawa wanamuhudumia kwa kila kitu mpaka alipopona, ndipo wakafanya safari kwa gari binafsi kumrudisha mzee kijijini kwao. Walipomfikisha nao walipokelewa na kukarimiwa vizuri na ndugu wa mzee yule, walipokuwa tayari kuondoka mzee akawaeleza jambo. Akawaeleza kuwa kwa muda mfupi aliokuwanao amegundua upungufu kwenye furaha zao, na amegundua kuwa sababu ni kukosefu wa mtoto na kuwa alikuwa tayari kusaidia, kwa maana alikuwa na uwezo wa kusaidia jambo hilo ila hakutaka kutoa msaada huo kwakuwa mashariti yake ni magumu lakini nafsi inamsuta kuacha kuwasaidia pamoja na wema waliomtendea. Wazazi wako wakaona kuwa zile zilikuwa ni habari njema,na wakawa tayari kwa msaada huo hata baada kuambiwa malipo yake na makubwa sana, walipotaka kujua malipo yenyewe wakaambiwa kuwa wangetakiwa kutoa malipo baada ya kufanikiwa kupata mtoto nao wakaridhia na kufanyiwa dawa na mzee yule, wakaondoka.
Kweli baada ya muda mfupi mama yako alipata ujauzito na wewe ukazaliwa. Baada ya kuzaliwa kwako ikawabidi kwenda kwa yule mzee kwaajili ya malipo kama makubaliano yalivyokuwa. Mzee yule akawaambia kuwa dawa ilikuwa imefanya kazi, na kuanzia pale mama yako angeweza kujifungua watoto wengine wengi ila alitakiwa kumtoa mtoto huyu wa kwanza kama sadaka kwa mizimu!...
Hapo ndipo utata ulipoanzia, wazazi wako hawakuwa tayari kwa hilo,wakamjia juu sana mzee yule, lakini mzee yule alisisitiza kuwa jambo lile halikuwa na ujanja, lazima lifanyike na hakukuwa na namna ya kulizuia lisitokee kwani mtoto yule alikuwa mali ya mizimu na lazima watamchukua”..

Usikose sehemu ya tatu

Nipate kupita:

+255653686008

nirasaire@gmail.com

facebook.com/nira.saire

@nira_saire(instagram)
 
Back
Top Bottom