Sehemu ya 108
Christina alikuwa akipambana kivyakevyake, ilikuwa ni lazima mwisho wa siku afanikiwe kwa kile alichokuwa akikihitaji, kuwa na John na kumfanya mwanaume wake.
Kipindi hicho alikuwa bize sana lakini baada ya kuambiwa na Amanda kulikuwa na mwanaume mwenye pesa aliyekuwa naye akaamua kurudi na kuwa naye karibu kama ilivyokuwa chuoni.
Kila siku walikuwa wakionana na kuzungumza mambo mengi, alichokuwa akikihitaji ni namba ya mwanaume huyo tu. Alijua jina lake aliitwa John, japokuwa kulikuwa na John wengi lakini aliamini baada ya kuliona jina hilo na namba angejua tu ndiye mwenyewe.
Kama walikuwa wapenzi basi John huyo ndiye aliyekuwa akiongoza kupigiwa ama kupiga hivyo ilikuwa rahisi sana kuipata namba hiyo.
Siku moja wakiwa chumbani kwa Amanda na msichana huyo kuitwa na mama yake ndiyo ilikuwa siku ambayo aliichukua simu yake na kuichukua namba hiyo.
Haikuwa kazi kutoa loki ya simu hiyo, aliijua kwa kuwa walikuwa karibu, akaiandika namba hiyo na kuisevu kwa jina jingine kabisa na sasa kazi ikabaki kwake, kuhakikisha anafanikiwa kulichukua penzi la mwanaume huyo.
Alivumilia, hakutaka kuingia kwa pupa, aliamini tu kwamba baada ya kukaa na Amanda kwa kipindi fulani angejua mengi kuhusu John.
Na hilo ndilo lililotokea, bila msichana huyo kujua akamwambia kuhusu ofisi yake ilipokuwa na mambo mengine.
Hiyo ndiyo nafasi ambayo msichana huyo alihitaji kuitumia, hakutaka kufanya jambo jingine zaidi ya kumfuata John huko Posta alipokuwa akifanya kazi.
Hakuwa akijuana naye, aliamini baada ya kuonekana mbele ya macho yake angekuwa mtu mpya na kama angekuwa kama wanaume wengine inawezekana mwanaume huyo angeusha ndoano yake na kuhitaji penzi lake.
Siku hiyo alivalia vilivyo, akaamua kuelekea huko. Kwa kuwa alikuwa na kiwowowo cha kishkaji, akavalia kisketi cha kubana kilichoishia juu ya magoti, blauzi na viatu virefu kidogo.
Kila alipokuwa akipita, alivutia, alionekana kama msichana fulani aliyekuwa na pigo za hatari mno. Wanaume wote waliokuwa wakipishana naye walikuwa wakiangalia nyuma kuangalia kijungu chake.