Simulizi: Mauaji ya Mfanyabiashara Musa Hamis Mtwara, Machozi na Damu

Kurunzi

JF-Expert Member
Jul 31, 2009
9,257
9,878
Dar/mikoani. Ni machozi ya damu, ndivyo unavyoweza kueleza katika simulizi ya vifo vya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis anayedaiwa kuuawa na maofisa wa polisi, huku ofisa wa jeshi hilo, Grayson Mahembe aliyekuwa akishikiliwa kwa tuhuma hizo akidaiwa kujinyonga hadi kufa akiwa mahabusu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mtwara jana, Hawa Ally ambaye ni mama mzazi wa Mussa, alisema mtoto wake (aliyezaliwa mwaka 1996), alikuwa mfanyabiashara wa madini na biashara nyingine baada ya kuacha shule akiwa kidato cha pili.

Alisema awali walikuwa wakiishi wote katika Kijiji cha Luponda wilayani Nachingwea Mkoa wa Lindi pamoja na mume wake ambaye ni baba wa kambo wa Mussa.

Akizungumzia mauaji hayo, alisema sakata hilo lilianza baada ya mafanikio ya Mussa alipopata madini na kuyauza kwa fedha za kigeni.

“Kwa sababu alikuwa ameshapata fedha za kigeni, yaani Dola za Mzungu (Dola za Marekani) sijui Mhindi kwa sababu mimi alikuwa hanisimulii zaidi, si mnajua vijana,” alisema Hawa. Alisema ilikuwa Oktoba 2021 wakati mwanawe anakwenda Mtwara, baba yake wa kambo alimuunganisha kwa mjukuu wake ambaye ameposwa na mtu anayeitwa Mmanga na anaishi mkoani hapo.

“Alichofanya bwana wangu (mume), ni kumpigia simu Mmanga kama mjukuu wake, akamwambia huko kuna mwanangu anakuja lakini anafuatana na shemeji yako, ambaye ndiye dada yake huyu marehemu.

Walipokwenda walipokewa, wakachenji fedha na kurudi kijijini, kisha wakaenda tena Mtwara ndipo wakashikwa. Lakini cha kushangaza, mmoja walimficha, lakini huyo wa kwangu akaonekana ameshikwa na polisi,” alisimulia Hawa.

Alimtaja mzee mmoja (jina tunalihifadhi) kuwa ndiye aliyewapigia simu kuwajulisha kuwa mtoto wao amekamatwa na wanatakiwa watume Sh300,000 ili atolewe kisha wakatuma.

“Baadaye akapiga tena simu (huyo mzee), akatuambia kuwa mtoto wenu ameshatoka, lakini inaonyesha ana hela nyingine anakuja kuonyesha huko nyumbani. Ikabidi tuziangalie kwenye nguo zake, naona mzee (mumewe) akaziona akaziweka sehemu, lengo azichukue,” alisema Hawa.

Alisema baada ya muda polisi walifika wakiwa na mtoto wao wamemfunga pingu.

“Wakatuuliza huyu ni mtoto wenu? Tukasema ndiyo, wakauliza ni wa ngapi? Nikasema ni mtoto wangu wa kwanza, huyu bwana (mume) ni mtoto wake wa kufikia. Wakasema huyu ana hela za dola (Dola za Marekani) na nyingine ameziweka ndani. Wakaingia ndani wakatafuta kwenye begi hela wakazikosa.

“Wakamuuliza hela umeweka wapi, akasema kwenye begi, wakamuonyesha bunduki, maana walikuja na bunduki. Kwa hiyo kwa kuona mimi nina uchungu wa mtoto wasimpige wasimuue wakati mimi niko pale, ndipo nikamwambia (mume wangu) katoe hela uwape. Ndipo wakapewa, wakazichukua wakawa wanazihesabu, mimi nilikuwa nalia kwa sababu ya uchungu, mtoto ametiwa pingu.”

Wakati huo maofisa hao wa polisi walimchukua mumewe na mtoto wao na kuondoka kuelekea Kituo cha Polisi cha Nachingwea.

“Nikauliza mnaenda naye wapi? Wakasema anakwenda kuisaidia polisi. Akaisaidie polisi kivipi, wakasema huyu ni baba mzazi (mume wake) tunakwenda naye, wewe unabaki,” alisema Hawa.

Aliendelea kusimulia kuwa, walipokuwa Mtwara maofisa wa polisi walimwambia kosa lake ni kukutwa na Dola za Marekani, lakini wakamkataza kutangaza suala hilo, badala yake wakampa kesi ya wizi wa pikipiki.

“Yule mtoto (marehemu Mussa) akasema nimeelewa, lakini sio haki yangu, nitasemaje kama nimeshikwa na pikipiki? Wakamwambia umeshikwa na pikipiki, tunakupa Sh100,000 nenda nyumbani kwenu. Halafu ukienda nyumbani kwenu, Novemba 6 urudi tena,” alisimulia Hawa.

Alisema hata Novemba 6, 2021 aliporudi polisi akiwa na mjomba wake, aliishia kufukuzwa.

“Alipofika nyumbani, yule mtoto akaanza kuumwa, aliumwa sana, nimezunguka naye hospitalini ili atulie. Hospitali wakasema mara BP (shinikizo la damu), mara sijui UTI, mara typhoid. Nilipokwenda kwa waganga wa kienyeji wakasema ni BP kwa kufikiria vitu alivyonyang’anywa,” alisema Hawa.

Baada ya kuzungushwa huku, mzee aliyewapigia simu aliwashauri wamtumie mwanasheria aliyeko mkoani Lindi.

“Lakini wakati anataka kwenda kwa mwanasheria wa Lindi, wale polisi wakamwita tena wakasema njoo uchukue vitu vyako kwa sababu utatusababishia tuachishwe kazi. Yule akapiga simu kwa mwanasheria aliyemwambia asiende mpaka ampe karatasi za kupeleka polisi.

“Kwa hiyo akaenda Lindi kwa yule mwanasheria akampa hiyo karatasi, kisha akarudi Mtwara akaipeleka polisi,” alisema Hawa.

Alisema baada ya kwenda kituo cha polisi akiwa na ndugu yake mwingine na zile karatasi alizopewa na mwanasheria wake, huo ndio ulikuwa mwisho wake kuonekana tena.

“Mwenzake anasema walipofika hapo aliambiwa akae nje wakati wanamhoji. Akauliza kwa nini akae nje wakati amekwenda naye? Wakasema wewe kaa nje tutakuita,” alisema Hawa.

Alijuaje amefariki dunia?

Hawa alisema tangu wakati huo wamekuwa wakimtafuta mtoto wao, hadi gazeti la Mwananchi lilipoandika jana, ndipo walipojua kuwa mtoto wao amefariki dunia.

“Kwa hiyo huyu kaka akaniambia kuwa mimi nimepata taarifa magazetini kwamba huyo kijana ameshauawa, kuna polisi amekufa pia. Mimi ndiyo nimepata nguvu ya kulia baada ya huyu kuniambia bayana kuwa mtoto ameshakufa na amezikwa,” alisema Hawa.

Ofisa anayedaiwa kujinyonga mahabusu

Wakati mkaguzi msaidizi wa polisi, Grayson Gaitan Mahembe akidaiwa kujinyonga akiwa mahabusu, amezikwa mkoani Iringa jana, huku wazazi wake wakilitaka Jeshi la Polisi kuchunguza kifo chake hicho chenye utata.

Mwili wa Grayson ulizikwa kijijini kwao Iladutwa wilayani Iringa, huku mamia ya waombolezaji wakishiriki msiba huo.

Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi aliyefika kwenye maziko ya Grayson, baba mzazi wa marehemu, Gaitan Mahembe alisema wiki mbili zilizopita alisikia sakata hilo kuwa marehemu alitumwa kwenda kukamata mhalifu sehemu.

Grayson alikuwa anadaiwa ni miongoni mwa watuhumiwa wa mauaji ya Mussa.

“Aliporudi akamweka ndani (Mussa), kisha akarudi nyumbani, lakini baada ya siku mbili tatu, akafuatwa akaambiwa unatakiwa kituoni,” alisema Mahembe.

Alisema mara ya mwisho alizungumza na mwanawe Januari 21 mwaka huu baada ya kumpigia simu.

“Inaniuma kwa kweli, kwa sababu ukweli wake umemponza. Yeye ni mkweli, yeye siyo mtuhumiwa, kutoka moyoni imeniuma sana. Yeye sawa ameshiriki lakini kwa maelekezo.

“Hatimaye nasikia ndiyo akawataja (alioshirikiana nao) mpaka mwisho ndiyo nasikia wapo ndani hao maofisa saba.

“Sasa kinachotuuma, wakamwambia tunaomba upumzike leo (siku hiyo), ili kesho usaini fomu utoke, baada ya kusema ukweli wa tukio lilivyotokea. Lakini hakutoka, mbaya zaidi tunasikia amejinyonga,” alisema Mahembe, ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Hata hivyo alisema, walimtuma mwakilishi wa familia kuchukua maiti ambaye pia ni mwanajeshi, lakini hakuonyeshwa eneo alilojinyongea.

“Lakini yeye amekwenda kuonyeshwa Hospitali ya Ligula. Kwa nini msingeniita kwenye tukio? Ndiyo hicho kinachotuuma familia. Tunaomba uchunguzi wa kina ufanyike, kama ni kweli mwanangu amehusika,” alisema.

Mama mzazi wa Grayson alisema alipata taarifa za kifo cha mwanawe akiwa Moshi mkoani Kilimanjaro alikokwenda kwenye maombi milimani.

“Sasa siku ya Ijumaa, kule Moshi kulikuwa na upepo mvua mvua. Mchungaji wetu akasema huu mlima hatuwezi kuumaliza wote kwa sababu gari tunaliacha kule chini halafu tunapandisha juu.

“Basi tukashuka kwenye gari, tukanywa chai tukamaliza maombi pale. Tukaenda kule kuchukua mizigo yetu, yule mama aliyekuwa anatupikia chai tulikuwa naye safari moja anakuja huku Dar es Salaam, basi tukamwambia twende tukachukue mizigo yako, halafu turudi ili tuondoke, kweli tukaenda na yule mama mpaka kule nyumbani kwake kachukua mizigo kaingia kwenye gari,” alisema mama mzazi.

Alisema baada ya kuingia kwenye gari akasikia simu inaita, akapokea, “hallo wewe nani, George… akasema sio mimi mama, mimi Gray, akasema kesho RPC atakuja halafu nitatoka mimi mzima mama usiwe na wasiwasi,” alisema akinukuu sauti ya mwanawe.

Alimuuliza baada ya kutoka itakuwaje? “Akasema haina shida nitakuja tu nyumbani kukueleza.”

Alisimulia kuwa ilikuwa usiku saa mbili alipozungumza kwa mara ya mwisho na mwanawe.

“Sisi tunaondoka tulipofika Mkata tukalala mpaka saa 11 asubuhi tukaanza safari,” alisema mama mzazi wa Gray.

Alisema alipofika Mbezi mwanawe alipiga simu, hata hivyo alishindwa kuongea naye baada ya kusikia kelele na vilio.

“Tulipofika kanisani, akapiga tena simu, wakati huo mchungaji alisema shusheni mizigo halafu tumalize ibada tuondoke. Mtoto alivyopiga simu akaniambia mpe mtu yeyote hapo kanisani, nikampa msichana mmoja nilikuwa karibu naye, baadaye akampa mchungaji msaidizi, sasa walichoelezwa sijui.

“Mimi nikaenda chooni, nikarudi nikamuaga mchungaji akasema haya, sasa yule mchungaji msaidizi akaniambia ingiza mizigo kwenye gari inayowasindikiza kila mmoja kwake, wakanifikisha nyumbani. Sasa nafika mtoto wangu msichana akatoka akawasukuma watu, akaniambia mama Grey hatunaye,” alisema.

Hata hivyo, mama huyo alisema hakukubaliana kwamba mwanawe amefariki dunia kwa kuwa aliongea naye siku moja tu iliyopita.

“Kusema kweli nilikataa na mpaka kesho nakataa mtoto umeongea naye saa mbili Ijumaa, unaamka asubuhi unaambiwa amekufa hapana siamini, amekufa na nini wakati alikuwa mzima wamemfanya nini. Hili halipo akilini mwangu, nikikaa nikiwaza naumia sana. Mimi siamini hilo na sitaamini, nataka mwanangu mnaniambia amekufa na nini?”

Nyumbani kwake Dar

Waandishi wa Mwananchi walifika nyumbani kwa Grayson Tabata Segerea jijini Dar es Salaam na kuwakuta wapangaji katika nyumba hiyo ambao walisema msiba umepelekwa mkoani Iringa.

Akizungumza akiwa ndani ya uzio wa nyumba, mpangaji mmoja alisema kwa sasa ndugu wote wamesafiri Iringa kwa ajili ya kuzika, waliobaki kwenye nyumba hiyo ni wapangaji tu.

“Ni kweli hapa palikuwa na msiba wa huyu baba, alikuwa haishi hapa, polisi walikuja na maiti juzi saa tisa usiku, na alfajiri waliondoka kwenda Iringa kwa ajili ya mazishi yanayofanyika leo (jana),” alisema mpangaji huyo.

Mmoja wa waendesha bodaboda katika eneo hilo, alisema alisikia kwenye nyumba hiyo kuna msiba lakini hafahamu kama umeshazikwa au kusafirishwa kwa kuwa hajaona shughuli zozote zikiendelea.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Mark Njera alisema jana kuwa tukio la mauaji lilitokea Januari 5 baada ya Hamis (Mussa) kufuatilia fedha zake zilizochukuliwa na maofisa wa polisi.

“Katika uchunguzi tulioufanya huyu Hamis alikamatwa Oktoba 2021, baada ya kupatikana taarifa kwamba alipanga kwenye lodge iitwayo Sadina ya hapa Mtwara na alionekana kuwa na matumizi makubwa ya fedha,” alisema Kamanda Njera.

Alisema maofisa hao walikwenda kumpekua hapo lodge, zilipatikana Sh2.3 milioni, lakini katika mahojiano alieleza kuwa hizo fedha alikuwa akifanya kazi zake Dar es Salaam na marafiki zake walifanya tukio huko wakapata fedha hizo.

“Pia, alikiri kuwa na fedha wilayani Nachingwea; na maofisa niliowataja walikwenda kumpekua na walipata Dola 13,500 za Marekani (Sh33,748,980). Baadaye wakarudi Mtwara, wakamweka mahabusu kwa siku tatu kisha wakampa dhamana.

“Tangu hapo hapakuwa na mawasiliano, lakini aliamini kuwa kama amefanya makosa basi sheria itachukua mkondo wake, lakini hicho hakikufanyika,” alisema.

Hata hivyo, alisema Januari 5, Hamisi alifika Kituo Kikuu cha Polisi kufuatilia hatima ya fedha zake, lakini alipofika kituoni hakuonekana tena.

“Ndipo tulipopata taarifa na kwa mujibu wa uchunguzi na bado tunaendelea, tumebaini kuwa ameshafariki dunia,” alisema.

Aliwataja maofisa waliokamatwa kuwa ni Mrakibu wa Polisi Gilbert Kalanje, (Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara), Mrakibu msaidizi wa Polisi, Charles Onyango aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mtwara, Mrakibu wa Polisi Nicolas Kisinza aliyekuwa Mkuu wa Intelijensia wa Mkoa.

Wengine ni Mkaguzi wa Polisi John Msuya, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Marko Mbuta, Mkaguzi wa Polisi Shiraz Ally Mkupa na askari mwenye namba G5158 Koplo Salum Juma Mbalu.

Chanzo: Mwananchi

PIA SOMA:
- Mtwara: Maafisa Saba(7) wa Polisi wafikishwa Mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya Kijana aliyekuwa akiwadai zaidi ya Tsh milioni 33.7 (25/01/2022)
- Mtwara: Askari Polisi mmoja kati watuhumiwa wa mauaji ya mfanyabiashara alikutwa mahabusu akiwa amejinyonga tarehe 22 Jan 2022
- Mtwara: Askari saba wanaotuhumiwa kumuua mfanyabiashara na kupora fedha wafikishwa Mahakamani
 
Screenshot_20220128-105848.jpg
 
"Nilipokwenda kwa waganga wa kienyeji wakasema ni BP kwa kufikiria vitu alivyonyang’anywa,"-Alisema Hawa.

Hawa waganga wa kienyeji wanapaswa kupewa heshima ya degree ya PhD kwani hata Hospitali hawakuweza kugundua tatizo la huyu jamaa vizuri kiasi hiki!😁😁😁
 
Njaa polisi. Mtu kumiliki million 33 tu imekuwa nongwa. Hawa polisi wanatakiwa wafinywe pumbu hadi kinyesi kiwatoke. Sasa million 33 tu ndo wanamuua kijana wa watu mchapa kazi anaetafuta kwa jasho lake. Sijui waligawana ngapi ngapi. Hatari kwa kweli.
 
Waliwauwa wafanyabiashara ya Madini toka Morogoro. Walimbabika Professor kesi ya kughusi ya nyara za taifa na sasa wameuwa tena mfanyabiashara za madini. Yote hayo hakuna aliyejiuzulu wala kuwajibika. Sisi tuko kimya tukidhani wanaofanyiwa ni WAO na SISI hayatatukuta.
 
Kiukweli serikali inahitaji kulifumua kabisa jeshi la polisi.Ni full of Thugs walio kwenye uniform.
Wengi Sana wanaumizwa na kuangamia kwenye mikono ya Hawa watu.
Ajabu utakuta Hawa watalindwa lindwa na kutochukuliwa hatua yoyote
 
Back
Top Bottom