SEHEMU YA 88
Sara akaanza kusogea akitaka kufungua, ila gafla akashtuliwa na sauti iliyotokea nyuma yake ilikuwa ni sauti ya mama yake.
“Unafanya nini hapo?”
Sara aligeuka na kumtazama mama yake ambaye alikuwa amemkazia sura vilivyo, ila cha kushangaza alivyoangaza huku na huku hakumuona Salome.
Sara alishangaa sana kwa kutokumuona Salome hadi mama yake akamuuliza,
“Mbona unashangaa hivyo?”
Akataka kumwambia mama yake kuwa alikuwa na Salome ila akashangaa mdomo unakuwa mzito kupita maelezo, akabaki tu kimya na mara akamuuliza mama yake,
“umeingiaje humu?”
“Badala nikuulize wewe umeingiaje humu eti unaniuliza mimi! Badala uniulize utatokaje humu unauliza nimeingiaje? Hujui kama humu ni ndani kwangu, popote nina uhuru wa kuingia. Haya umeingiaje humu? Na umefuata nini”
Sara alikuwa kimya tu akimuangalia mama yake kwani kiukweli hata yeye mwenyewe hajui humo amefuata nini maana alikuwa akimfuata tu Salome ndiye aliyempeleka humo ingawa hakumuona tena, mama yake alimuangalia tena kwa hasira na kumuuliza,
“Ulikuwa unafata nini humu? Unashida gani humu wewe mtoto lakini? Yani yote uliyonitendea leo unaona hayatoshi zaidi ya kuendelea kunichokonoa chokonoa? Ngoja nisiongee kwanza humu tutoke kwanza”
Rose alimvuta mwanae mkono kisha akafungua mlango tu kawaida kanakwamba haukufungwa na funguo halafu akatoka nae ila Sara alimchoropoka mama yake kwani bado alikuwa akijiuliza kuwa Salome yuko wapi, alienda moja kwa moja kwenye chumba ambacho huwa analala Moza na kufungua mlango ilia one kama Salome yupo ila alifungua mlango na hakumuona yoyote, mama yake alikuwa nyuma yake na kumuuliza,
“Sasa unatafuta nini?”
Sara alitamani kumwambia mama yake kuwa kwenye chumba kile aliingia na Salome na hakumuona tena kwahiyo alitaka kumuangalia kama chumbani kwake yupo, ila mdomo ulikuwa mzito kusema hayo na alishindwa. Mama yake alipoona mwanae anabung’aa bung’aaa akamvuta tena mkono na kupita nae sebleni, halafu akaenda nae kwenye sebule nyingine ambayo wale mapacha hupenda kuitumia. Akakaa nae na kumuuliza,
“Sara, mimi ni mama yako au sio mama yako?”
“Wewe ni mama yangu”
“Kwanini huniheshimu sasa?”
“Mama sio kwamba sikuheshimu ila linapokuja kwa wewe kuhusishwa na habari za kichawi ndio huogopa”
“Una uhakika kama mimi ni mchawi?”
“Mbona Ana ni mchawi mama”
“Kwahiyo kama Ana ni mchawi huo uchawi nimempa mimi?”
“Hapana mama sijamaanisha hivyo”
“Na kama nimempa Ana uchawi basi nyie wote kwenye nyumba hii ni wachawi, unaponaje kuwa mchawi wakati mama yako mzazi ni mchawi? Uchawi unaujua wewe? Kwanza nani aliyekuambia kama mimi ni mchawi?”
“Sijui mama”
“Sara mwanangu, acha fikra mbaya. Wewe ni mwanangu wa kwanza na mambo mengi nafanya kwaajili ya maisha yenu, kumbuka baba yako alikukataa wewe toka upo tumboni mwangu. Je alikukataa kwavile nilikuwa mchawi? Nimehangaika mimi nimeteseka, nikawapata kaka zako nao wakakataliwa na baba yao. Sasa mimi kumpata mtu na kumdhibiti asifurukute kwenye himaya yangu na awajali nyie na kuwapenda na kuwapa chochote mtakacho ni uchawi huo? Kumtafuta mtoto kama Ana ili kuongeza upendo kwa mwanaume niliyempata, ni uchawi huo? Unaacha kujiuliza kwanini huolewi na umri umeenda umekazana kutafuta uchawi wa mama yako. Sitaki yakukute yaliyonikuta mimi, usiamini maneno au vitendo vya kusema mimi ni mchawi ila nafanya vitu kwaajili na maisha yenu yani wewe na wadogo zako. Sina tatizo na Ana, ni wa tofauti na nyie Yule. Sahau katika maisha yako kama utakuja kuolewa, na kaka zako wasahau maishani mwao kama watakuja kuoa, ila Ana ataolewa na ataolewa sababu nataka amtese mume wake. Mimi sio mchawi mwanangu, na sitaki unifatilie tena. Nadhani tumeelewana!”
“Nimekuelewa mama na ninakuahidi sitakufatilia tena, ila kwanini unasema kuwa mimi sitaolewa wala kaka zangu hawataoa?”
“Nitakwambia sababu ila sio leo, nyie mtaishi name miaka yote”
Rose aliondoka na kumuacha mwanae kwenye dimbwi la mawazo, alikosa jibu kuwa kwanini hatoolewa ila aliweza kuolewa kuwa ni kwanini kila mwanaume anayemleta mama yake anampinga mwanaume huyo, yani hapo ndio akaelewa kuwa mama yake hataki yeye aolewe, akasema lazima awataarifu kaka zake kuhusiana na hicho alichoambiwa na mama yao.
Kisha Sara aliinuka pale na kutoka.