SEHEMU YA 85
Rose alikuwa kwenye maua akifanya dawa kwaajili ya mzimu wa Moza usifike kwenye nyumba yake maana alianza kupata hisia kuwa huenda mzimu wa Moza ndio unaosumbua akili yake, basi alipiga magoti kwenye lile ua ambalo moza aliwahi kulifukua na kutoa kile kimpira kilichopelekea mpaka kifo chake, kwa upande wa Rose hili ua lilikuwa na maana kubwa sana kwake na lilikuwa likimsaidia vitu vingi sana kwahiyo alipiga magoti na kuanza kusema maneno ambayo hayatakiwi yakatishwe akianza kuyasema mpaka ayamalize, akiwa katikati yay ale maneno alishikwa bega na Sara,
“Mama, mama”
Rose hakumjibu chochote Sara na aliendelea na kusema maneno yake ila Sara nae hakuacha kumuita mama yake hadi akawa anamtingisha,
“Mama, mama jamani mama ndio uchawi gani huu sasa mpaka umeanza kufanya peupe ili tujue kama mama yetu ni mchawi jamani!”
“Mama, namuhitaji Ommy wangu, nirudishie Ommy mama. Nipo tayari kuachana nae ila nirudishie Ommy mama”
Alipoona mama yake hamjibu chochote zaidi ya kuendelea na kitu anachofanya, akapata wazo la kuchukua maji na kumwagia hivyo akafanya kama wazo lake lilivyomtuma. Akafungua bomba na kukinga maji kwenye ndoo kisha akaenda kummwagia mama yake.
Kwakweli hakuna siku ambayo Rose aliwahi kuchukia kama siku ya leo maana aliinuka kwa hasira halafu alimpiga mwanae hadi alizimia yani kipigo alichompiga haikuwahi kutokea, mlinzi alisikia kelele tu na kumfanya azunguke nyuma ambako kelele zilitokea ila akaona Sara akipigwa na mama yake hadi kuzimia kisha mama yake alimuacha Sara hapo na kwenda ndani, yani Rose hakujali kama mwanae amezimia au nini alikuwa na hasira zilizopindukia.
Mlinzi alijaribu kumuinua Sara pale, sema sababu alikuwa na nguvu kwahiyo aliweza kumuinua na kumuweka pembeni kwenye kivuli kisha akaanza kumpepea ila hakuzinduka kwa muda huo.
Salome nae alitoka ndani na kukuta yale yaliyopo kisha akachukua maji na kummwagia Sara, yale maji yalimfanya Sara azinduke ila alikuwa na maumivu makali sana ya kupigwa na mama yake, kisha Salome na mlinzi wakasaidiana kumshika Sara na kumtembeza hadi chumbani ambako walimuweka kitandani apumzike. Mlinzi alitoka na kumuacha Salome akiwa na Sara chumbani, kwakweli Sara alikuwa na maumivu mwili mzima kiasi kwamba hata alivyopigwa pigwa na mama yake hakukumbuka vizuri huku akijiuliza mwenyewe,
“Hivi kilichonipeleka nyuma kule na kuanza kumfanyia fujo mama ni nini? Hivi kilichofanya nichungulie mama anachofanya ni nini?”
“Usijilaumu kwa chochote Sara, katika maisha kila kitu huwa kinapangwa na kinakuwa na maana yake kwahiyo usijipe lawama za bure”
“Hapana Salome, nimejitakia mwenyewe. Mwili wote unaniuma yani wote unaniuma. Mama yangu hajawahi kunipiga kiasi kile, mama yangu hajawahi kuwa na hasira na mimi kiasi kile. Hata kama mama yangu ni mchawi ila sikutakiwa kumfanyia fujo kiasi kile”
Salome alimuangalia Sara kisha akaondoka na kumuacha Sara mwenyewe chumbani akijilaumu tu kwanini amemfanyia fujo mama yake maana mwili wote ulikuwa unamuuma,
“Eti nampigia kelele mama amrudishe Ommy wa kazi gani sasa Ommy, janaume Malaya vile la nini? Kama limewekwa msukule na liwe tu msukule, ona nilivyopigwa na mama, huyu Salome nae sio wa kumsikiliza ushauri wake. Hivi yeye anaweza kufanya kwa mama yake ujinga kama huu! Mama ni mama hata akiwa mchawi, natakiwa kwenda kumuomba msamaha mama”
Sara aliinuka kwa kujikongoja akajivuta hadi chumbani kwa mama yake ambapo aligonga bila kufunguliwa, ikabidi afungue mwenyewe. Alishtuka na kushangaa mama yake akiwa mtupu kabisa ila Rose alizidi kupatwa na hasira kwa mwanae na kuongea kwa hasira,
“Hivi wewe mtoto una nini wewe? Unataka upate laana yangu au?”
sara aliondoka kwa aibu hata hakuweza kuzungumza na mama yake kwani hakutegemea kama angemkuta mama yake akiwa mtupu kabisa, Sara alirudi chumbani kwake huku akijiongezea makosa aliyomkosea mama yake kwa siku hiyo na kujiona ni mtoto mpumbavu asiye na maadili halafu ndio mtoto wa kwanza wa mama yake halafu maadili hana anafanya mambo ya ajabu kama yale.
“Nimemdhalilisha mama yangu, sifai mimi yani sifai kabisa”
Alikuwa akijilaumu tu kwa wakati huo.