SEHEMU YA 58
Salome akiwa amefika nyumbani kwao, akamkuta mama yake yupo ndani, kisha Salome alipoingia tu akamuanza na maswali,
“Unajua sehemu niliyokuaga naenda asubuhi, nimeenda na kurudi. Ila sasa niambie ukweli wewe ulikuwa wapi?”
“Nilienda kwa baba”
Neema akashtuka na kujikuta akimuuliza tena,
“Unasemaje Salome?”
“Nilienda kwa baba”
“Unaoajua?”
“Napajua ndio, si mamdogo Ashura alinielekeza!”
“Wewe mtoto wewe usiniletee makubwa mimi”
“Makubwa yapi mama? Yani baba kafurahi sana kuniona na alitaka nikae pale moja kwa moja nikamwambia bado sijamuaga mama”
“Nitolee balaa lako hilo Salome”
“Sio balaa mama, yani baba kwa furaha aliyokuwa nayo kanipa hadi pesa za matumizi”
“Pesa za matumizi? Ziko wapi?”
Salome akatoa pesa ambazo zilikuwa ni elfu kumi kumi, akampa mama yake. Kwakweli Neema aliishiwa nguvu kabisa kuona zile hela akataka aanze kuzihesabu,
“Hata usijisumbue kuhesabu, kaniambia ziko milioni tatu”
“Milioni tatu? Yani Patrick akupe wewe milioni tatu! Wakati huo mke wake alikuwa wapi?”
“Mkewe alikuwepo na mbona kasapoti tu, tena alitaka niongezewe ila baba akasema hizo za kuanzia”
“Mmh Salome wewe unanishangaza”
“Mama hata usishangae ila nieleze ukweli kwanini ulinificha kuhusu baba yangu?”
“Aaah unajua mwanangu, aaah yani hata sijui nianzie wapi. Achana na hizo habari bhana”
Salome akachukua zile hela kwa mama yake,
“Sasa mbona umechukua tena wakati ulinikabidhi mwanangu!”
“Mpaka uniambie ukweli, mimi ni binti mkubwa sasa. Nataka kujua ukweli wa kwanini ulikuwa unanificha kuhusu baba yangu”
“Basi naomba nikuelezee kwa kifupi, si utanipa hizo hela eeh!”
“Mi nitakupa ila niambie ukweli”
“Ni hivi, Patrick amewahi kuwa mume wangu, tena ni mume wa ndoa kabisa. Nilifunga nae ndoa ya kanisani huko kijijini kwao. Ila niliishi nae muda mrefu sana bila ya kupata mtoto, yani mimi na Patrick tulioana mapema sana. Kipindi hicho nilikuwa na miaka kumi na sita halafu yeye alikuwa na miaka ishirini. Baada ya kuishi muda mrefu bila kuzaa takribani miaka kumi ilipita ndipo tulipohamia mjini na kuendelea tena na maisha ila sikuwahi kupata mimba hata ya kusingiziwa hata mwenyewe nilikuwa nashangaa maana sikuwahi kutoa mimba maishani mwangu. Miaka ilienda tu sibebi mimba wala mdudu wa mimba, basi mjini hapa biashara za Patrick zikaanza kutanuka akawa na mali nyingi na biashara kubwa kubwa ila kilichokosesha furaha ndoa yetu ni mtoto tu. Siku moja mume wangu alizna kufanya biashara na mwanamama aitwaye Rose, Yule Rose alikuwa Rose kweli kipindi hicho alikuwa mzuri haswaaa sio kama siku hizi hata mimi mwenyewe nikawa na mashaka ya kuibiwa penzi langu na rose ingawa alikuwa ni mkubwa sana tu kwangu. Ila naye alikuwa mfanyabiashara, gafla nikaja kusikia Patrick kuna mjengo amejenga huko anaishi na Rose kumbe mimi ananiaga kuwa anasafiri halafu anaenda kuishi na Rose, kuna kipindi alipotea kama miaka mitatu kumbe ndio yupo huko anaishi na Rose. Akarudi na kuishi na mimi kama wiki kumbe ananitafutia sababu ya kunifukuza. Siku hiyo Patrick alikuja na kuniambia wazi kuwa amechoka kuishi na mwanamke asiyezaa, miaka inaenda lakini mwanamke sizai na akaniambia ameamua kuwa na huyo Rose mwenye watoto tayari kwani anaamini huyo atamzalia ukizingatia tayari ameshazaa watoto watatu, nilisononeka sana. Patrick akanifukuza pale nyumbani kama mbwa kisha ile nyumba nasikia alipangisha. Nilianza maisha ya kutangatanga na badae nikajigundua kuwa nina ujauzito, nilijua ile mimba ni ya Patrick nikawa nataka niende kumwambia ila siku hiyo nilikutana na Rose akaniambia nikithubutu kusema basi ataninyonga na kukinyongelea mbali kitoto changu. Ila bado nilijipa matumaini kuwa Patrick akigundua atafurahi, nilihangaika na ile mimba, nakumbuka nilienda kujifungulia kijijini kwa kina Patrick, na mtoto nilimuita Maria Patrick. Jina Maria ni jina ambalo mwanangu ulipewa na bibi yako yani mama mzazi wa Patrick nami nililifurahia sana. Yule mama alinipenda na ndio akaanza kumsumbua Patrick kuwa anirudie mimi na tulee mtoto wetu lakini mambo yakawa si mambo tena, siku hiyo isiyo na jina walikuja vijana na kuvamia pale nyumbani kwa mama Patrick na ndani tulikuwa tunaishi mimi, na mtoto mdogo ambaye ni wewe pamoja na mama yake Patrick. Wale vijana walimchinja mama Patrick mbele ya macho yangu, kwa hakika siwezi kusahau kamwe na nikaambiwa niondoke tena nisionekane kabisa hapo kijijini kwani nitachinjwa na mwanangu kama walivyofanya kwa huyo mama. Walinitishia na niliogopa sana, ingawa ulikuwa ni usiku nikatoka na kukimbia kwa bahati nilikuta watu njiani wakisubiri gari lao nikawaomba lifti na kuja nao mjini. Niliteseka sana na wewe mwanangu yani sikuwa na raha ya maisha kabisa, sikutaka tena kurudi kwa Patrick wala ndugu zake kwani nilihofia yasije yakawapata kama kilichompata mama Patrick. Nilikaa kama miaka mitatu au mine mjini nikitangatanga, ndio kwa bahati nikampata Ashura aliyejitambulisha kama mdogo wangu na toka siku hiyo nikaanza kuishi na Ashura tena ni yeye aliyenishauri nikubadilishe jina ili tusifatiliwe tena. Badala ya Maria tukuite Salome tena akaniambia kuwa Rose amezaa na Patrick mtoto anaitwa Ana basi nikajua furaha ya Patrick imetimia sasa maana kama mtoto ameshapata, basi ndio imekuwa hivyo hadi leo. Naomba nisiendelee sana mwanangu, mengine utayajua taratibu tu. Basi nipe hizo hela”
Salome alichukua zile hela na kumkabidhi mama yake, kisha akainuka na kwenda chumbani ambako alikuwa akipanga mipango mipya sababu ameshajua yote aliyotaka kuyajua.
“Sasa nimeelewa kwanini Ashura alitumwa, lakini lazima kuna kitu kilikuwa kizuizi cha kuwachinja wahusika na kuishia kumchinja mamake Patrick. Hivi Patrick anajua kweli kama Yule mwanamke ndiye alimuulia mama yake? Najua hajui ila atajua tu”
Ila kumbe alikuwa anawaza kwa sauti halafu Neema nae alikuwa amekuja chumbani kwa Salome na kujikuta akimuuliza,
“Kujua nini?”
“Hamna mama kuna kitu nafikiria tu, ila mama na wewe jiwekee utaratibu basi wa kugonga mlango kabla ya kuingia ninapolala”
“Hivi wewe Salome utanificha nini mimi, maana mimi ni mwanamke na wewe ni mwanamke. Hakuna cha kufichana”
“Hatakama mama ila ni vizuri kuwe na utaratibu huo”
“Basi nitakuwa najitahidi, ila hizi pesa zimenichanganya yani hadi najiona kama namiliki dunia vile”
“Yani mama milioni tatu tu ndio inakuchanganya hivyo!”
“Kwa mimi ni kubwa sana, ten asana yani hapa hadi sina maneno. Ngoja kesho nikafungue akaunti benki”
Salome akacheka tu jinsi mama yake alivyopagawa na zile hela ila ukweli wa hela zile angeujua sijui angefanyeje.