SEHEMU YA 33
Kwenye gari ambalo Neema alikuwa amepanda na mtoto wake Salome huku akimpeleka hospitali, machozi yalikuwa yanamtoka mfululizo kwani aliamini kuwa mwanae alikuwa amekufa ukizingatia alikuwa amekauka kabisa kama aliyepigwa na shoti ya umeme. Kijana aliyewabeba kwenye gari alikuwa anaendesha haraka haraka ili awahi hospitali kwani hata yeye alipatwa na huruma kwa mtoto Yule ila walipokuwa wanakaribia hospitali, ikawa kama miujiza kwani Salome aliamka gafla na kumfanya mama yake hata machozi yamkatike, kwani alipoamka tu alimwambia mama yake,
“Msinipeleke hospitali tafadhali, nirudisheni nyumbani”
Mama yake alimuangalia kwa kustaajabu sana,
“Ila mwanangu tunatakiwa tukupime kwanza”
“Nirudisheni nyumbani, sitaki kwenda hospitali. Huko mkinipeleka nitakufa”
Hata Yule dereva alipatwa na mshangao tu, Neema alimuangalia dereva na kuanza kumuelekeza ili waende nyumbani.
Kwahiyo safari ilibadilika haikuwa ya hospitali tena bali safari ya nyumbani, kwakweli Neema alikuwa anamuangalia mwanae bila ya kummaliza kwani alimuona kama amebadilika hivi. Mpaka wanafika nyumbani na kushuka,
WAkati wanashuka, Salome alimwambia mama yake,
“”Tafadhali usimwambie yeyote kilichonipata”
“Kwanini?”
“Sitaki wajue mama wataniogopa, tafadhali usimwambie yeyote”
“Nakuahidi sitamwambia yeyote mwanangu, uzima wako ndio furaha yangu”
“Niahidi tena mama kuwa hutomwambia yeyote”
“Nakuahidi kweli mwanangu, hakuna yeyote nitakayemwambia”
Salome alionekana akishangaa shangaa tu mazingira ya pale kwao, mpaka mama yake akamuuliza,
“Mbona unashangaa hivyo Salome?”
“Naona kumebadilika”
“Hapana hakujabadilika, ni huku huku ndio nyumbani kwetu”
Waliingia ndani na Ashura ndio alikuwepo nyumbani na wale mapacha wadogo zake Salome, ila Salome alipomuona Ashura alimwambia,
“Khee Ashura bado upo huku?”
Mama yake alishangaa na kumwambia kwa mshangao,
“Kheee wee Salome, toka lini mama yako mdogo umemuita kwa jina lake? Adabu ya wapi hiyo? Halafu unamuuliza bado upo huku, ulifikiri mamako mdogo atakuwa wapi! Yani usingekuwa umepatwa na matatizo leo ningekupiga sana”
“Nisamehe mama”
Ikabidi Ashura nae aulize,
“Matatizo, kwani amepatwa na matatizo gani?”
“Mwenzangu makubwa”
“Yapi hayo?”
Salome akamuangalia mama yake na kumwambia,
“Kumbuka umeniahidi mama”
“Naelewa mwanangu”
Sasa Ashura akabaki na bumbuwazi na kuzidi kuuliza kulikoni imekuwaje kuwaje,
“Aaah si huyu Salome, kagombana na wenzie shuleni huko ndio leo niliitwa shuleni kwao”
“Kheee kwahiyo muda ule mnaondoka hapa ilikuwa mnaenda shuleni kwakina Salome? Imekuwaje leo kwenye kesi zake amekuchukua wewe badala ya kunichukua mimi?”
“Anaelewa makosa yake, tuachane na hizo habari mdogo wangu. Hebu tufikirie leo tutakula nini?”
“Tumuulize huyo mpenda ugomvi, leo anataka kula nini?”
“Nataka ugali, mlenda wa kuchanganywa na ngoga na samaki”
Neema na Ashura wote waliangaliana na kumuuliza Salome kwa mshangao tena kwa pamoja,
“Wewe ngoga unaijua?”
“Ndio, si ndio nyanyachungu”
“Toka lini ukala ugali Salome? Mpenda wali wewe, leo hii unataka ugali makubwa!”
“Tena ugali na ngoga, mbona makubwa haya ya leo dada”
“Makubwa haswaaa, huyu Salome wangu wa leo ni kiboko”
Salome akainuka na kwenda chumbani, ambapo alifika na kujilaza.
Baada ya muda mama yake akawa anamtafuta,
“Salome kaenda wapi jamani?”
“Ila sijamuona akitoka”
Mara wakaja wale mapacha wawili na kumwambia mama yao,
“Kalala chumbani kwetu”
“Kheee kalala chumbani kwenu, hivi Salome mzima akili yake kweli leo? Ameshasahau kama analalaga na mamake mdogo”
Neema akainuka na kwenda kumuasha Salome, alipoamka alikaa nae na kuzungumza nae
“Hivi Salome umeanzaje kuja kulala huku? Tuseme hujui chumba unacholala au? Hujui kama unalala na mamako mdogo wewe? Halafu hata kuoga hujaoga, hivi yale mambo yaliyotokea unaona ni madogo yale mwanangu? Naomba uinuke ukaoge halafu kama kulala ukalale chumbani kwenu”
“Mama naomba unisaidie kitu”
“Kitu gani hicho?”
“naomba msaada wako ila usimshirikishe mtu yeyote”
“Wewe niambie tu, simwambii mtu mwanangu”
“Kwakifupi mama kuna vitu mimi nimesahau, vitu vingine naomba unipe maelekezo”
“Sasa mwanangu, lile tukio halikuwa la kawaida ndiomana nikakwambia twende hospitali wakakucheki”
“Mama nitakuwa sawa tu, naomba vitu vingine unielekezage na usimwambie mtu yeyote. Lile tukio lililonitokea mimi kweli halikuwa la kawaida na limehusika haswa na mambo ya kishirikina ndiomana sitaki unipeleke hospitali maana huko utanipoteza kabisa, je upo tayari mwanao nife?”
“Sipo tayari mwanangu, nitaumia sana”
“Basi naomba iwe siri yako, mtu yeyote asijue, hata mabadiliko yangu asijue mtu yeyote. Wewe ndio mama yangu nakutegemea, naomba unielekezage tu cha kufanya”
“Haya niambie unataka nikuelekeze nini”
“Nielekeze chumba ninacholalaga, nielekeze nguo zangu za kuvaa, nielekeze choo chetu kilipo nikaoge”
“Mmh mwanangu inamaana vyote hivyo umesahau? Mbona unanitisha?”
“Usiogope mama yangu, nifanyie hivyo tu”
Neema aliinuka na kuanza kumuelekeza mwanae, ambapo aliporudi sebleni na kumuacha Salome anaoga ndipo Ashura nae akauliza,
“Imekuwaje tena, mbona Salome kama haeleweki hivi!”
“Achana nae, akili yake inawaza kupigana tu hapo”
Ashura akawa kimya ila alihisi kuna kitu cha tofauti kimempata Salome ingawa hakujua ni kitu gani.