SEHEMU YA 158
Swala la Neema kukuta simu ya Ashura kwenye begi la Neema ni swala lililompa wasiwasi zaidi, akajikuta akitoka nayo kwa Patrick na kumueleza kuwa ile ni simu ya Ashura na ameikuta chumbani kwa Salome.
“Hivi umesema kuwa tangia Ashura aondoke umekuwa ukiwasiliana nae kwa njia ya ujumbe”
“Ndio, hata nikashangaa kusema kuwa eti umeona picha ya maiti yake ikiwa imeoza ila nimeshangaa zaidi kukuta simu ya Ashura kwenye pochi ya Salome na kunitia uwoga zaidi kuwa huenda Salome anajua kuhusu kifo cha Ashura au huenda ndio yeye mwenyewe aliyekuwa akiniandikia ujumbe mimi. Tuseme….”
Akafikiria kidogo kuwa Salome ndio kamuua Ashura, akajikuta akitikisa kichwa chake na kusema,
“Hapana, mwanangu sio mkatili kiasi hicho. Mwanangu hawezi kuwa amemuua Ashura, kwanza kwa lipi baya alilofanyiwa na Ashura hadi amuue? Hapana kwakweli, haiwezekani yani haiwezekani kabisa”
Patrick akamshauri Neema kuwa awashe ile simu ya Ashura ili wajaribu kuangalia kuwa ni namba gani zimewahi kupigwa na ujumbe mingapi iliyowahi kujibiwa kwenye simu hiyo. Basi Neema akajaribu kuwasha simu ile ila haikuwaka na kugundua kuwa haikuwa na chaji kwahiyo ikabidi aiweke kwenye chaji huku wakiwa na hamu ya kujua kuwa ni watu gani wamekuwa wakiwasiliana nae kwenye simu ile.
Muda kidogo alijaribu tena kuiwasha ila iliwaka na ilipowaka tu kuna ujumbe ambao inaonyesha ulikuwa unasubiri kuingia kwahiyo uliingia muda huo huo, ilionekana ni namba mpya ambayo haijatunzwa kwenye simu hiyo ndio imemtumia huo ujumbe, ujumbe ule ulisema,
“Umeona mambo uliyoyafanya sasa Ashura yani umenivurugia kila kitu, huyu Salome amekuwa mtihani mkubwa sana katika maisha yangu. Nilikutuma umamalize ila ukakimbia bila ya kummaliza, sasa huyu mtoto amekuwa na nguvu za ajabu na anataka kunimaliza mimi. Je utafurahi ukisikia ndugu yako nimemalizwa na huyu mtoto wa laana? Sijapendezewa kabisa na ulichofanya”
Neema na Patrick walitazamana kwani kuelewa huo ujumbe moja kwa moja ilikuwa ngumu kabisa ukizingatia mtumaji wa ujumbe ule hawakumfahamu, hivyo wakaamua kufatia mazungumzo kwa namba hiyo na jumbe zilizotumwa, mwishowe waligundua kuwa mtuma ujumbe alikuwa ni Rose na walishangaa sana kwani waliona hadi jinsi Rose alivyopanga mipango ya kummaliza Salome kwa kushirikiana na Ashura yani hadi walijikuta wakishindwa kuangalia jumbe zingine zaidi ya zile kwani ziliwatisha kwakweli,
“Yani kumbe Ashura nilikuwa naishi nae halafu anajuana na Rose! Kumbe alipanga mipango ya kumuua mwanangu! Sielewi kabisa sielewi”
Patrick alikuwa kimya tu kwani yeye ndio hakuelewa zaidi, muda kidogo walisikia mlango wa sebleni ukigongwa kisha Neema kwenda kufungua, alikuwa ni Salome ila Neema alishindwa hata kumfokea Salome kwa kurudi usiku huo nyumbani kwani jumbe za kwenye simu ya Ashura zilikuwa zimemtisha sana, badala yake alijikuta akimkaribisha ndani na kumuuliza kuhusu Ashura kama ana mpango wa kumuua yeye alijuaje na je imekuwaje hadi simu ya Ashura ipo kwake,
“Mama na Baba naomba niwaeleze kwa ufasaha kabisa, kama mmesoma hizo jumbe mtakuwa mmapata maana kuwa Ashura alikuwa ni mtu wa aina gani katika maisha yetu. Mama ulimchukulia Ashura kama mdogo wako ila kiukweli kuna kazi alipewa ndiomana alikuja kukaa hapa, Ashura na Rose hawakumuweza Salome sababu alikuwa na kinga thabiti kutoka kwa marehemu mama yake na Patrick”
Walimshangaa kuwataja majina yao ila kwavile walitaka kujua zaidi ndiomana walikuwa wakimuuliza tu maswali kuhusu Ashura,
“Eeh mwanangu hebu nieleze vizuri, ilikuwaje tena yani ilikuwaje hadi kutaka kukuua wewe na ilikuwaje hadi simu yake ipo kwako?”
“Mama, nilimsikia kwa masikio yangu akiongea na simu kuhusu dawa ya kuweka ili wanimalize, ndipo akaandaa chakula na kuniwekea hiyo dawa kwenye chakula ila mimi nilifanya mchezo wa kumbadilishia sahani ya chakula na ndipo alipokula alianza kutoka povu na kutapatapa na akawa kimya hapo hapo kumbe ilikuwa ni sumu kali sana ya kuua kwa muda mfupi. Nikachukua simu yake na kugundua kuwa kuna vijana alizungumza nao kuja kubeba mwili wangu, kwahiyo nikampakia yeye kwenye viroba na kuwatumia wale vijana ujumbe kuwa waje wabebe tayari ila mimi niliondoka kwani nilipata pesa kwenye begi la Ashura na kuja kutafuta nyumba. Kwahiyo wale vijana walijua wameenda kunitupa mimi. Nilifanya hivyo kwasababu ni kesi kukutwa na maiti tena imeuwawa kwa sumu, nilifanya hivyo kuficha ushahidi kwani hata yeye alipanga kufanya hivyo”
Neema alishindwa kuwa alie au acheke kwani hakujielewa kabisa, siku zote alimchukulia Ashura kama mdogo wake ila hakuelewa kama Ashura alikuwa akimzunguka, ndipo akaelewa jinsi alivyoulizia habari za Ashura kwa mamake wa kambo na kuambiwa kuwa huyo mtu hawamtambui kabisa, alijaribu kuunganisha picha ya jinsi alivyokutana na Ashura na kupata jibu ya maswali aliyokuwa akimuuliza na kujua kuwa Ashura alitumwa katika maisha yake.
Salome akawaeleza vingi sana kuhusu Ashura na kuwafanya wabaki wameduwaa tu na hawakuelewa chochote kile, yani Neeema hakujua alie kwa kupata uhakika wa kifo cha Ashura au acheke sababu mwanae kanusurika na kifo, walijikuta wakikaa kimya tu wakitafakari kuhusu Ashura na kutumwa na Rose, yani Patrick alijikuta akijutia maisha yake,
“Najuta kumfahamu Rose, najuta kuanza kufanya biashara na mwanamke huyu. Alinifanya niifukuze familia yangu, amefanya nisiwathamini wanangu, amefanya mamangu auwawe kikatili, amenifanya niwasahau ndugu zangu, amefanya niwe kama ndondocha kwenye mali zangu mwenyewe. Najuta, amefanya niamini maneno ya Ashura kuwa ni ya ukweli sababu ni ndugu yako kumbe ni mtu ambaye amempanga kuja kuharibu maisha yetu, huyu mwanamke sijui nimfanye nini? Yeye ni mchawi ila mimi nitamfanyia kitu cha kawaida tu ambacho hatokisahau maishani mwake”
Patrick alionyesha kutokufurahishwa kabisa na mambo ya Rose, waliinuka na kwenda kulala ila si Patrick wala si Neema waliopata usingizi, kwani usingizi haukuwajia hata kidogo, muda wote Neema aliwaza alivyokuwa akiishi na Ashura jinsi alivyokuwa akishauriana nae halafu kumbe alikuwa na mipango ya kuuwa mtoto wake, ila tu alijiuliza kuwa kama alikuwa na mpango huo kwanini hakuweza kumuua mtoto wake wakati akiwa mdogo kabisa ndio kutaka kumuua mkubwa vile, aliwaza sana bila ya jibu la aina yoyote ile. Kwa upande wa Patrick nae alikuwa akiwaza tu toka siku ya kwanza alivyomfahamu Rose na jinsi alivyotelekeza familia yake.