Mogambi
JF-Expert Member
- May 25, 2012
- 213
- 357
Kazi ya Mzungu
1
DAVID NGOCHO SAMSON
Miaka miwili iliyokuwa imepita, Masuke aliamua kuondoka kijijini kwao Malonje na kuingia jijini kutafuta maisha kama ilivyo kuwa desturi ya vijana wengi. Alifika jijini Dar es salaam na kufikia kwa dada ake Maimuna ambako kwa miezi miwili alokaa kwake alikuwa akifanya kazi ya kulisha ng’ombe wa tajiri Soud wa Masouud, kabla ya kuamua kuyatafuta maisha huko Zanzibar, kufuatia fununu alizosikia kwa rafikize kuwa huko maisha yalikuwa na uafadhali. Kazi kidogo kipato cha juu! Dada yake alipojaribu kumshauri aangalie kwanza hapo jijini, yeye alikuwa ameshaamua la kuamua. Hakusikiliza na alisisitiza maisha ni kutafuta. Ujira wake kwa bwana Soudi ulimwezesha kuabiri boti ya Azam na kuingia Zanzibar tayari kwa maisha. Hakubahatika kuonana na rafikize waliotangulia huko. Mawasiliano yalikatika walipoondoka Dar na hilo halikumtia wasiwasi bali aliamini wangekutana huko.
Alifikia nyumba ya kulala wageni nje kidogo ya feri ya Zanzibar. Usiku huo akautumia kutafakari. Alijiuliza ni nini angefanya. Alfajiri ya kesho yake, Masuke alijiamsha na kuanza harakati za kuzunguka kuufahamu mji aliofikia. Katika mizunguko hiyo ndipo alipopata wazo la nini cha kufanya. Angeweza kusukuma mkokoteni wenye mizigo ya abiria kwa ujira mdogo mdogo ambao kwa kutwa nzima ungemudu kumpa hela ya kujikimu. Wakati akitafakari hayo, alimuona ustadhi mmoja mwenye kuvalia kanzu na barakshia kama ilivyo kawaida ya wazanzibar wengi. Masuke alimsogelea na kumsabahi
‘Asalam aleikum sheikh!' Masuke alitoa salam
‘Aleikum msalam! Wa bara weye!’ Alijibu ustadhi na kuuliza kwa lafudhi yake ya kizenji, Ilikuwa dhahiri kuwa sheikh yule alitanabahi kuwa Masu alikuwa mtu wa bara, na sio bara TU,bara huko nyikani na sio Pwani.
‘Naam sheikh na kazi yangu kubeba mizigo kwa ujira kidogo tu!’ Masu alilazimu kujinadi. Biashara matangazo ati.
Ustadhi alimtazama na bila shaka akaona imani.
‘Mizigo yenyewe mizito utaiweza weye?’
‘Naam sheikh, hii indo kazi yangu!’ Alizungumza kwa kujiamini.
‘Sawa, kwa mizigo hii utanitaka nikupe pesa ngapi?’
‘Mia tano tu itanifaa sheikh wangu!’
‘Haya basi, nipelekee hii kwenye ofisi hiyo ya Azam!’
Ni kama hakuamini bahati aliyokuwa nayo. Tayari ndoto zake alihisi zingetimia hapa. Kufikia magharibi, masuke alikuwa kamudu kujipatia buku nane. Hakutarajia. Sasa aliporejea pale guest alipofikia. Masuke alikuwa na wazo moja tu. Kesho angeamkia kazi yake mpya na saa za adhuhuri angezunguka kutafuta chumba cha kupanga maeneo ya jirani. Uzuri alikuwa na akiba kiasi ambacho angemudu kulipia chumba walau kwa mwezi mmoja. Akiba aliyomudu kukusanya alipomfanyia kazi bwana Soud wa Masoud kule jijini Dar.
**
Bwana Steve Curl alikuwa katinga suti yake mpya iliyomkaa vema, machoni alipachika miwani ya jua, nywele zake akiwa kazilaza kwa mafungu, na kutengeneza kijibarabara kidogo kwenye kichwa chake chenye nywele fupi nyeusi. Mkononi alikuwa na smartphone yake, na alionekana kutazama saa yake ya mkononi ya gharama kuonesha alikuwa anajaribu kupimana kasi na muda. Mwendo wake pia ulithibitisha kuwa, bwana huyo ama alikuwa anawahi ndege au basi kuna zito lilomtia mota miguuni hata aonekane kuvuja jasho kwa haraka alokuwa nayo. Aliikatiza mitaa ya mji mkongwe kwa haraka akielekea kwenye hotel aliyokuwa amefikia. Boda boda wala hawakuonekana mitaani, labda hicho ndicho kilichomfanya mzungu huyo kutoka marekani avuje jasho asubuhi hii ya saa kumi na mbili kwa kutumia usafiri nafuu, miguu yake.
Masuke alikuwa keshaamka mapema. Sasa na yeye alikuwa kwenye harakati za kuwahi kivukoni, huko huenda angepata kazi ya kumbebea mtu kitu ili apate kitu kidogo kama ujira wake. Alishaanza kuzoea kutengeneza hela ya kutosha tu hasa alipowahi alfajiri. Kwa kazi yake hii ambayo alijipachika, alijikuta akipata kuzoeleka hasa kutokana na lafudhi yake, waliyoipa jina wenyeji, ‘lafudhi ya kibara.’ Asubuhi hii aliamka akiwa na tabasamu. Jana ilikuwa njema, ikimfanya ahisi leo itakuwa bora zaidi.
Kwenye kichochoro hapo mji mkongwe, Masuke akamuona mzungu akihangaika na mabegi. Akachanua tabasamu murua, hii ndio kazi yake. Ila sasa, akajikuta lile tabasamu likiyeyuka ghafla. Nini? Akakumbuka wakati wenzake wanajifunza alfabeti na kiingereza, yeye alikuwa kwenye mabanda ya kubeti akitengeneza hela na kuliwa hela. Mwisho wa siku, hakuna cha maana alichopata. Anaanzaje sasa kumuomba hiyo kazi huyu mzungu aliyekuwa mbele yake? ‘Ah, kwani nini! Nitaongea Kiswahili changu cha bara, asiponielewa potelea mbali, hata yeye alipokuja nchi za wenyewe alipaswa kujua lugha yao pia’ hivo ndivyo alivyowaza, huku akiongeza kasi kumfuata Yule mzungu. Tabasamu mwanana kabisa likiambaa ambaa kwenye midomo yake. Alishajua siri, siri ya kufanikiwa kwenye kazi yake, ilikuwa ni tabasamu lake. Hakuna aliyeliona akagoma kutoa kazi. Hiyo ilikuwa siri yake kuu.
‘Halo mzungu, unaweza kuongea Kiswahili? Mimi kazi yangu ni kubebea watu mizigo na kuwafikishia wanapotaka kwa pesa kidogo sana. Naweza kukusaidia, naona hiyo mizigo yako inakuelemea bosi wangu.’ Masuke alitamka huku akiliachia lile tabasamu lake.
‘Sawa, sawa. Ni shilingi ngapi?’ bwana Steve Curl alitamka maneno hayo mithili ya mtoto mdogo anayejifunza kusoma. Neno moja moja kwa tuo.
‘Oh, mefurahi sana unazungumza Kiswahili. Pesa itategemea ni wapi unapoenda.’
‘Nazungumza kidogo sana. Nataka kufika kwa taksi!’ Curl aliongea kwa ishara ya kuonesha kwa vidole vyake kwamba Kiswahili chake kilikuwa kiduchu sana.
‘Hapo bosi utanipa elfu mbili tu!’
‘Elfu mbili, hiyo ni kidogo sana. Nitakupa elfu tano’ Curl alizungumza tena kwa mtindo wake ule wa kusoma. Lakini ikaonekana kama kutangaza dau hilo kubwa ingemsaidia kuwahi alikokuwa anaenda, kwa vile kuzungumza na mswahili kulionekana kunamchelewesha. Hivyo alitumia vitendo zaidi kumhamasisha Masuke abebe haraka na wawahi huko walikokuwa wanaenda. Masuke alielewa, fasta sana akabeba mabegi yake, akanyanyuka kwa mwendo wa haraka, kumwahisha mteja wake.
Hakutaka kuongea, nadhani aliona kabisa kwamba huyo bwana wa kizungu, alikuwa na haraka isiyohitaji soga za kupoteza muda. Alipomfikisha, na kuiweka mizigo kwenye taksi, Masuke akatoa tabasamu lake akipokea buku tano yake, halafu akatamka;
‘Ukirudi, ukiwa na kazi yoyote, mimi nipo tayari kufanya kwa ujira mdogo’
‘Uko tayari, kazi yoyote? Sawa sawa, mimi natafuta wewe nikirudi. Naitwa nani wewe?’
‘Niite Masu, ukinitafuta, tumia ‘M’bara’ watu wanafahamu M’bara zaidi kuliko Masu!’
‘Mubara, mubara!’ Steve alitamka jina hilo huku akiliandika kwenye shajara yake ndogo.
‘Asante sana, hii itakusaidia pia’ Steve aliongea huku akimuongezea shilingi elfu kumi. Akazama kwenye gari, taksi ile ikaondolewa kwa mwendo wa kasi. Steve alikuwa anawahi sehemu bila shaka.
‘Yyess, ah leo zari leo. Hesabu ya siku nimeshaingiza kwa kazi ya kwanza tu? Mungu mkubwa wallah! Naamini leo naweza kulaza hata hamsini. Leo, ah Asante Mungu.’ Masu alimaarufu M’bara, alijiongelesha huku akipanga mipango lukuki kichwani mwake. Alianza kuona mpango wake wa kumiliki guta unaelekea kuwa kweli. Alishaulizia dukani, akaambiwa laki moja na nusu angeweza kujipatia guta la kutengenezwa na mafundi welding, lenye tairi za baiskeli. Na sasa kwa muda mfupi aliokuwa amefanya kazi tayari alikuwa keshajiwekea akiba ya elfu themanini, ukiongezea na hii, hii aliyojipatia alfajiri hii, basi alikuwa na shilingi elfu tisini na tano akiba. M’bara akadhamiria siku hiyo ajitume angalau aingize kama elfu kumi na tano nyingine.
Akajiendea zake akiimba wimbo wa hip hop wa msanii wa Kenya Jua kali, mwoto sana! Si kama aliimba kweli, basi ni ile tu kusema alipenda mdundo na hivyo alijiwekea maneno anayojua mwenyewe kwa rhythm ya wimbo ule. Safari na mdundo.
Aliingia kivukoni saa kumi na mbili unusu hivi, harakati zilikuwa zinaendelea. Leo alichelewa kwa nusu saa hivi, hata hivyo haikuwa bure, ilikuwa nusu saa sawa na siku nzima ya kazi. Tabasamu lake lilichanua vema.
‘We M’bara, kuja hapa, nataka ubebe mizigo hii uipeleke kwa duka yangu. Fanya haraka.’ Babu G, ilikuwa jina la duka lake, mhindi aliyekuwa na duka la kuuza vifaa vya ujenzi. Mara nyingi mizigo yake ilifikia hapa kabla ya kwenda dukani, maana muhindi huyu kama walivyo wafanyabiashara wengine pia, alikuwa hapa kaweka stoo. Na kuna wakati alificha mali humo na kuwaambia wateja imeadimika halafu tena angewaambia kuna kidogo amepata lakini gharama ikiwa imepanda. Hivyo ndivyo alivyojipangia bei na kutengeneza faida maradufu. Hapa, kulikuwa na mzigo wa saruji. Mifuko hamsini. Yote ilikuwa imepata wateja na kilichofanyika ni kuipeleka dukani wateja wachukue mali yao.
Kawaida Masu alipopata tenda kama hizi basi alilazimika kukodi maguta au torori kwa mkinga aliyekuwa ashakuwa mzanzibar bwana Faustine Kyando. Hadi lugha na mavazi yake sasa yalikuwa ya kizanzibar kabisa. Usingemtambua. Huyu alijua kutumia fursa. Kama ilivyokuwa kwa Masu, Kyando naye aliingia Zanzibar kama mtu aliyepotea njia. Kutahamaki akakuta wazanzibar ni watu wa kupenda sana maisha hadi ikawa si kuyapenda tena bali kuyaendekeza. Hawakuwa na muda wa kufanya kazi hizi ndogo ndogo, kwao kazi za kuvuja jasho zilikuwa na wafuasi wachache sana. Na hata hao, walizifanya watimize kusudi, walipolikamilisha usingewaona tena.
Kwake, Kyando hiyo ilikuwa ni fursa. Aliitumia vema akajikuta anafungua duka kubwa na kuwekeza pia kwenye vifaa vya welding. Akajitengenezea bidhaa na kuuza. Akatengeneza pia mikokoteni na maguta kwa ajili ya kukodisha. Akawatonya marafikize waje, walipokuja wakawa wanaitumia mikokoteni na maguta kufanya zile kazi alizoanza nazo. Yeye akawa ashinda dukani na kupokea hesabu ya kukodisha mikokoteni yake jioni.
Masu alikuta huo utaratibu ukiwa umeshawekwa mahali pake. Alijihimu haraka na kumfuata rafiki yake Paulo, ambaye sasa alijiita Bakari. Wakachukukua mkokoteni mmoja walioupa jina ‘moto faya’. Kazi ikaanza. Tabasamu mwanana likienea usoni mwake. Alijipangia hesabu ya siku kuwa kumi na tano, lakini hapa walipewa mifuko hamsini. Mfuko mmoja kawaida walibeba kwa shilingi mia tano. Elfu ishirini na tano. Bakari angeambulia elfu tano tu na yeye angetia kibindoni shilingi elfu ishirini. Huo ndio utaratibu waliojiwekea. Kama aliona ndogo basi angetafutwa mwingine. Bahati nzuri, haikuwa siku njema kwa Bakari, alikuwa majalala mbaya. Alihitaji hela kama alivyohitaji oksijeni. Kwake elfu tano ilikuwa kubwa sana. Naye alikubali kwa tabasamu akimshukuru nduguye huyu kwa kumpa mchongo.
Siku yake ilikuwa njema, na sasa aliamini marafiki waliomwambia Zanzibar kunazo fursa.
Fuatilia episode 2 Kesho
DAVID NGOCHO SAMSON
Facebook: David Samson
Sent using Jamii Forums mobile app

DAVID NGOCHO SAMSONFacebook: David Samson
Sent using Jamii Forums mobile app
!