Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Bishop mimi nna ombi mkuu wangu mtunzi uliebobea, ikikupendeza tumalizie hii TAHARUKI yani samahani boss ni ombi tu ukiipost uipost yoote tujimwaemwae nayo af sasa tubadili mkao wa zifuatazo apa natoa ombi ila naogopa samahani kwa usumbufu mkuu natanguliza shukrani. Wako mtiifu Litro
 
Duh pole sana mkuu maana mtu unaweza kuumwa kichwa kumbe kuna ugonjwa mwingine umejichimbia. Nakumbuka kuna kashemeji kangu kalitutesa sana na maradhi ya kichwa mwisho wa siku anakuja kupona kwa mawani ya macho.
 
Naanza kumuonea huruma Mambo, naona kama atakata moto kabla ya kukutana na Sizya!! Ngoja tuone...Jason nae muda wote anawaza utamu kipenyo mwenzie utamcost.
Haha! Naona umeamua kutangulia mbele, mkuu. Leo nina nafuu kidogo. Baadaye kidogo nitashusha vitu..
 
Kwasiku tatu Mfululizo kila nikishika simu free naingia jf ni apa tu nakuwa na hatimae nimefka apa kwenye taharuki,bishop eroo Wee hii kazi unaiweza asee kipaji haswa, kaka arosto tupunguzie Ina raha kinyama kuisoma ndefu kama kitabu yaan, big up man
 
taharuki..jpg

327

Saa 12:35 jioni…

Gari la Luteni Lister liliniteremsha katika Kituo cha Mafuta cha Lake kilichopo mkabala na Malaika Beach Club, Kigamboni, dakika ishirini na tano kabla ya muda nilioahidiana na Sajenti Mambo kukutana hapo.

Sajenti Mambo alinipigia simu wakati tukitoka makaburi ya Kinondoni akanisisitiza kuwepo Malaika Beach Club, Kigamboni, saa moja kamili jioni, nami sikuwa tayari kufuata matakwa yake ya kufika kwa muda uliopangwa wa saa moja jioni kana kwamba nilikuwa nakwenda kwenye ibada kanisani. Kati ya mambo ambayo niliyathamini sana katika maisha yangu ya kipelelezi ni tabia ya kutomwamini mtu yeyote na kumshuku kila mtu, hata marehemu.

Mara zote nilijikumbusha kuwa kupanga muda wa kukutana ni kati ya makosa makubwa kwani unaweza kuwa unashirikishwa kupanga muda wa kifo chako mwenyewe. Hivyo, ni vizuri kukifumania kifo wakati kikijiandaa kukuchukua au kukichelewesha kidogo.

Baada ya kushuka toka kwenye gari la Luteni Lister nikaanza kupiga hatua zangu kwa utulivu nikikatisha barabara na kuelekea ng’ambo ya pili ya barabara ilipo Club ya Malaika. Wakati nikitembea na kukatisha katika ile barabara niliishusha vyema kofia ya pama niliyovaa kuufunika uso wangu huku macho yangu yakiwa makini zaidi kuzichunguza sura za watu waliokuwa eneo lile na mijongeo yao.

Mwili wangu ulikuwa bado mchovu mno kutokana na pilika pilika na kukosa mapumziko kwa siku kadhaa tangu lilipotokea tukio la kigaidi kwenye jengo la Alpha Mall, katika eneo la Makumbusho.

Kisha nilianza kukatiza kwenye viunga vya maegesho ya magari vya Malaika Beach Club ili kwenda kwenye mlango wa mbele wa Club. Hata hivyo wakati nikitembea kuelekea kwenye Club ile nikawa nikiyatembeza macho yangu kwa makini kupeleleza mandhari ya eneo lile ili kuona kama nilikuwa nimewekewa mtego wowote.

Niliona magari machache yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la maegesho ya magari la Club ile na nilipoyachunguza vizuri magari yale nikagundua kuwa yalikuwa ya watu wenye kipato cha kueleweka, ambao kwa vyovyote walikuwa mle ndani ya Club wakijipatia vinywaji au starehe yoyote iliyokuwa ikipatikana mle.

Kulikuwa na watu wawili watatu waliokuwa wamesimama pale nje ya Club ile wakiwa na mazungumzo. Watu wale waligeuka kidogo kunitazama wakati nilipokuwa nikiwapita kuelekea kwenye mlango wa kuingilia ndani ya ile Club, sikuonesha kuwatilia maanani lakini nilikuwa makini sana kunusa hatari.

Niliingia ndani ya Club na hapo nikajikuta nikikabiliana na macho ya watu waliokuwa wameketi kwa utulivu mle ndani wakiendelea na starehe zao. Walikuwa watu wachache. Niliangaza macho yangu huku na huko katika namna ya kutafuta sehemu nzuri ya kukaa na wakati nikiyatembeza macho yangu nikawa nikiwachunguza pia watu waliokuwa mle ndani. Kwa haraka nikagundua kuwa wengi wao walikuwa Wahindi.

Kisha nilipiga hatua taratibu kutafuta meza na kwenda kujitenga mbali na watu wengine, nikiketi kwenye meza ya peke yangu iliyokuwa pembeni kabisa ya ule ukumbi, karibu kabisa na mawimbi ya bahari, nikifaidi upepo mwanana wa baharini ambao ulikuwa ukinipuliza mwilini, lakini pia ilikuwa sehemu iliyoniwezesha kuona vizuri pande zote, kule baharini na hata mbele ya Club ile ambako magari yalikuwa yakiingilia. Niliketi huku macho yangu yakiwa yanachambua mazingira.

Runinga pana iliyokuwa imetundikwa ukutani mle ukumbini ilikuwa imejikita katika kurusha matangazo ya kandanda la Ulaya. Sikuwa mfuatiliaji mzuri wa mchezo wa kandanda, hivyo wala sikujua ni timu zipi zilizokuwa zinacheza.

Kisha nikamwita mhudumu mmoja na kumwagiza aniletee mvinyo aina ya Dompo na baada ya dakika mbili mvinyo ukaletwa, nikaanza kunywa taratibu huku nikiusubiria muda mwafaka ambao Sajenti Mambo angefika. Nilikuwa na shauku kubwa ya kumsikia Sajenti Mambo akinieleza kile alichokifahamu huku nikitaraji kuwa mazungumzo yetu yangenipa mwanga zaidi katika kulitatua suala zito lililokuwa likinisumbua. Japokuwa nilijionya kutomwamini mtu yeyote lakini kwa bahati mbaya, sikuwa na jinsi.

Tangu lilipotokea lile tukio la bomu kwenye jengo la Alpha Mall nilijikuta kila hatua niliyoipiga kwenye upelelezi wangu ilifanya kazi ya uchunguzi iwe ngumu na ya hatari zaidi. Hivyo, kuna muda nikajikuta nikiwa mhitaji zaidi wa kichwa chenye kufikiri kwa upeo mpana zaidi katika masuala ya aina hii. Tayari nilishakuwa na vichwa kama Luteni Lister na Pamela, lakini sasa nilihitaji kichwa ambacho kilikuwemo ndani ya mtandao huo hatari na kilijua mambo mengi zaidi yaliyohusu mtandao huu. Kwa mtazamo wangu kichwa cha Sajenti Mambo kilikuwa mwafaka zaidi.

Luteni Lister baada ya kuliegesha gari lake mbali kidogo na eneo lile la Club alirudi na kutafuta meza iliyokuwa mbali na meza yangu, akaketi na kuagiza mvinyo aina ya Dodoma Wine, akiwa pale kwa ajili ya kuhakikisha ninakuwa salama.

Niliendelea kunywa mvinyo wangu taratibu huku nikitafakari hili na lile katika namna ya kubashiri ni kipi alichotaka kuniambia Sajenti Mambo. Nilianza kuyaona mafanikio ya upelelezi wetu kupitia Sajenti Mambo, nikashusha pumzi na kuitazama saa yangu ya mkononi, nikagundua kuwa bado nilisaliwa na dakika tano kabla ya muda tuliokubaliana. Nikamimina mvinyo katika bilauri na kuendelea kunywa taratibu huku nikiyasafirisha macho yangu kutazama nje ya ukumbi ule.

Ni muda huo huo wakati nikitazama kule nje, macho yangu yalipoliona gari aina ya Lexus la rangi ya fedha lililokuwa na vioo vyeusi visivyoonesha ndani likifika pale Club na kuegeshwa kwenye sehemu maalumu ya maegesho ya magari. Mara moja nikalikumbuka gari lile. Lilikuwa ni lile gari nililoliona nyumbani kwangu usiku wa siku iliyokuwa imetangulia. Gari ambalo Sajenti Mambo na Daniella walilitumia kuniletea ujumbe na kumwachia mlinzi wa nyumba yangu.

Sasa macho yangu yakawa makini zaidi kulitazama lile gari ili nione nani angeteremka, na wakati huo huo nikaliona gari lingine aina ya Nissan Patrol jeusi lenye vioo vyeusi visivyomruhusu mtu kuona waliomo ndani likiingia pale Club na kuegeshwa mbali kidogo na lile gari aina ya Lexus la rangi ya fedha.

Nikiwa makini kuyatazama magari yote mawili mara nikamwona mwanamume mmoja akishuka toka kwenye gari lile aina ya Lexus la rangi ya fedha akiwa ameshikilia briefcase ndogo mkononi. Ingawa macho yake alikuwa ameyafunika kwa miwani myeusi sikushindwa kumtambua mara moja. Alikuwa Sajenti Albert Mambo wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay.

Aliposhuka alitazama huku na kule, huenda alikuwa anahakikisha usalama wa eneo lile, kisha akashika briefcase yake vizuri mkononi na kuanza kutembea kwa mwendo wa haraka haraka kuelekea kwenye lango la kuingilia Malaika Beach Club.

Ni wakati huo huo kilipotokea kitu kilichonishtua sana, kwani ghafla nilimshuhudia Sajenti Mambo akisombwa hewani na kisha kutupwa chini kama gunia wakati akiwa hatua chache tu kufika mbele ya lango la kuingilia Club. Na hapo nikawashuhudia watu wachache waliokuwa pale nje ya Club na wengine walioliona tukio lile wakishikwa na taharuki, hata hivyo, mimi sikuwa miongoni mwao na badala yake fikra zangu zilijikita katika kuchukua tahadhari.

Endelea...
 
taharuki..jpg

328

Sikutaka kusubiri, nilinyanyuka haraka toka kwenye kiti changu huku nikimpa ishara Luteni Lister kwa kunyanyua mkono wangu wa kushoto na kugusa upande wa kulia wa ncha ya kola ya shati nililokuwa nimeivaa ndani ya suti kumuashiria kuwa mambo hayakuwa shwari. Bila kusita naye akanijibu kwa kugusa sikio lake la kushoto kuashiria kuwa alishaitambua hali hiyo.

Kisha sikusubiri, nikakimbilia kule nje alikokuwa ameangukia Sajenti Mambo, bastola yangu ikiwa mkononi tayari kwa lolote. Nilimkuta Sajenti Mambo akiwa amelala chali chini juu ya dimbwi la damu. Nilipofika nilimtazama kwa makini na hapo nikabaini kitu. Sajenti Mambo alikuwa hapumui!

Nikainama kwa tahadhari na kunyoosha mkono wangu wa kushoto kumgusa upande wake wa kushoto wa kifua kwa mgongo wa kiganja changu ili kusikiliza mapigo ya moyo wake, lakini wakati wote macho yangu yalikuwa makini kutazama huku na kule. Kwa haraka nikagundua kuwa Sajenti Mambo hakuwa na uhai.

Hali ile ikanifanya ninyanyuke haraka na kuanza kulichunguza eneo lote huku na huko na kuambulia kukutana na macho ya mshangao ya watu waliokuwepo eneo lile ambao walikuwa wameduwaa, baadhi yao walikuwa wakitetemeka kwa hofu ya tukio hilo ambalo hawakuweza kulitafsiri.

Muda huo nikamwona Luteni Lister akielekea upande wa mwingine wa ile Club katika namna ya kulikagua eneo kisha akakimbilia kuja pale nilipokuwepo huku macho yake yakiendelea kuwa makini kulichunguza eneo lote.

Nikiwa nimesimama nikawa najiuliza pasipo kupata majibu na mara wazo fulani likanijia akilini. Nikageuka haraka kutazama kwenye eneo la maegesho ya magari, kule lilikoegeshwa lile gari aina ya Nissan jeusi lenye vioo vyeusi visivyomruhusu mtu kuona ndani, nikaliona gari hilo likiondoka na kuyaacha maegesho ya magari.

Mlango wangu wa sita wa fahamu ukafunguka, hivyo nikamwambia Luteni Lister aikague maiti ya Sajenti Mambo kuona kama kulikuwa na chochote cha kutusaidia halafu nikaanza kutimua mbio nikilifukuza lile gari ambalo lilikuwa likiondoka kwa kasi toka katika eneo lile na kuingia barabarani.

Wakati nikiwa nafika barabarani lile gari aina ya Nissan Patrol lilikuwa linapita mbele ya Kituo cha Mafuta cha Lake na kabla halijafika kwenye Kituo cha Chekechea cha Malaika (Malaika Day Care) likakunja kuingia kushoto, wakati huo mimi nilikuwa upande wa pili wa barabara, umbali usiopungua mita therathini kutoka lilipo lile gari, nikiendelea kutimua mbio kulifukuza lakini nilikuwa kama mtu niliyechanganyikiwa.

Lile gari liliingia katika ile barabara ndogo ya vumbi iliyokuwa ikielekea kwenye maeneo ya makazi ya watu. Nikataka kuvuka barabara lakini sikufanikiwa kuvuka kwani muda huo magari mengi yalikuwa yanapita yakitokea upande wa Kigamboni na kukatisha mbele yangu hali iliyofanya yanizuie kama si kunichelewesha. Sikutaka kuendelea kuyasubiri yale magari yamalize kupita ndiyo nivuke ile barabara, hivyo nikaamua kufanya jambo la hatari, kwa kasi nilijirusha juu kimgongo mgongo na kutua juu ya boneti la gari dogo aina ya Mazda lililokuwa likikatisha mbele yangu.

Kuona vile, dereva wa lile gari aina ya Mazda akawahi kukanyaga breki na gari likaserereka barabarani huku sauti kali ya magurudumu yaliyokuwa yakisota juu ya lami ikisikika, hata hivyo wakati lile gari likisimama mimi tayari nilikuwa nimeshatua chini upande wa pili wa ile barabara na kuendelea kutimua mbio, lakini nikagundua kuwa hapakuwepo uwiano wowote kati ya mbio zangu za miguuni na kasi ya magurudumu ya gari lile nililokuwa nikilifukuza, kwani magurudumu yake yalikuwa yakizunguka kwa kasi ya ajabu.

Hatimaye wale wauaji wakawa wameniacha huku nikiwa siamini macho yangu. Nilisimama huku nikihema, nililitazama gari lile namna lilivyokuwa likitokomea na kupotelea kwenye eneo la makazi ya watu huku donge la hasira likiwa limenikaba kooni. Kwani kwa mara nyingine tena nilikuwa nimepoteza pointi muhimu za ushindi katika pambano langu.

Nilianza kutembea kivivu vivu nikirudi kule Malaika Beach Club huku mawazo mengi yakianza kupita kichwani mwangu. Nilipofika pale Club nikakuta watu wameshajaa wakishangaa. Nilimkuta Luteni Lister akiwa amemaliza kuipekua maiti ya Sajenti Mambo na sasa alikuwa anawapigia simu polisi kuwajulisha kuhusu tukio lile, na mara aliponiona akaniashiria kuwa nitangulie kwenye gari kisha akawataka watu waliokuwa wameanza kujazana eneo lile kutoigusa ile maiti.

Nikageuka kurudi nilikotoka nikilifuata gari letu lililokuwa limeegeshwa jirani na Malaika Day Care. Wakati nalifikia lile gari Luteni Lister naye akawa amefika, tukaingia kwenye gari na kabla hatujaondoka Luteni Lister akanikabidhi briefcase ya Sajenti Mambo, daftari dogo la kumbukumbu, flash yenye ukubwa wa kidole cha shahada, kalamu na kadi mbili za biashara huku akiniambia hivyo vitu alivitoa kwa marehemu baada ya kumkagua.

Nilivitazama vile vitu na kilichonivutia zaidi ilikuwa ni maandishi madogo juu ya ile flash; yaliandikwa ‘Top Secret’. Luteni Lister akaniambia kuwa katika mfuko wa ndani kabisa wa koti la Sajenti Mambo alikuta bastola lakini aliiacha, na kwenye mifuko ya suruali hakukuwa na chochote cha muhimu zaidi ya pochi iliyokuwa na kibunda cha noti za elfu kumi kumi ambazo hazikupungua shilingi laki moja.

Nikiwa bado naviangalia vile vitu Luteni Lister akaliwasha gari na kuliondoa kwa kasi. Wakati yeye akiwa makini kwenye usukani, mimi nikaanza kucheza na namba za briefcase ile na muda mfupi baadaye nikafanikiwa kuifungua. Ilikuwa briefcase ndogo ya kisasa iliyokuwa ikifunguliwa kwa namba. Kwangu haikuwa kazi kubwa kucheza na namba zile kabla ya kuipata ile iliyokusudiwa.

Baada ya kuifungua ile briefcase na kutazama ndani nikashangaa kutokuona chochote. Briefcase ilikuwa tupu kabisa! Na hapo nikatambua kuwa Sajenti Mambo alikuwa ameibeba kwa ajili ya kuzugia au kuwapoteza maboya watu ambao wangejaribu kumfuatilia.

Muda huo tulikuwa tukipishana na gari moja la polisi lililokuwa likitokea Kigamboni kwa mwendo wa kasi huku king’ora kikibweka na kimwelumwelu kikimetemeta, tukahisi kuwa lilikuwa linaelekea kule Malaika Beach Club kwenye tukio la mauaji.

* * *

Endelea...
 
taharuki..jpg

329

Uso kwa uso…




Saa 4:30 usiku…

ILIKUWA rahisi sana kuitambua nyumba nambari 70 iliyopo kwenye bikoni nambari 2603 katika eneo la Mbezi Beach, ilikuwa imejengwa katika ufukwe wa Bahari ya Hindi. Haikuwa kazi ngumu kulitambua eneo lile kwa sababu simu yangu ya mkononi na hata saa yangu zilikuwa zinatumia mfumo wa kisasa kabisa wa utambuzi wa TracerMark.

Eneo ilipojengwa nyumba hiyo ambayo ilistahili kuitwa kasri, lilikuwa na barabara pana ya lami yenye usafi wa hali ya juu, na kulipandwa miti mizuri ya kivuli kando ya barabara ile. Pilika pilika za watu na magari zilikuwa hafifu sana katika eneo lile huku ustaarabu ukionekana kuzingatiwa kwa asilimia zote. Muda huo wa usiku eneo hilo lilikuwa na utulivu mkubwa sana huku likimulikwa na taa nzuri zenye mwanga mkali.

Ilikuwa kasumba kwa wafanyabiashara wakubwa na viongozi wengi wa bara la Afrika kupenda kuishi kwenye maeneo ya mijini yenye hadhi ya juu kiuchumi na kiusalama yenye majumba makubwa ya kisasa ya watu wakwasi yakiwa yamezungukwa na kuta ndefu za uzio na mageti makubwa yenye vifaa vyote vya usalama vya kuwahakikishia wakazi wake usalama wa hali ya juu.

Nyumba ile ilikuwa ya kisasa sana na kupita nyumba nyingine zote za jirani katika eneo lile la ufukweni mwa Bahari ya Hindi. Nyumba ile ilikuwa katika eneo tulivu mno na ilikuwa ya ghorofa mbili.

Mimi, Luteni Lister na Pamela tulikwenda Mbezi Beach baada ya mimi na Luteni Lister kutoka Kigamboni tulikoshuhudia Sajenti Mambo akiuawa na kisha tukampitia Pamela sehemu na kuelekea makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa, Oysterbay ambako tulimkuta mkurugenzi mkuu mzee Rajabu Kaunda akitusubiri, tukamwachia vile vitu tulivyovichukua toka kwa Sajenti Mambo. Ndipo tukaja Mbezi Beach.

Muda wote mzee Rajabu Kaunda alikuwa ofisini akisubiri kupokea taarifa na aliahidi kuwa asingekwenda nyumbani kulala hadi ahakikishe kila kitu kimeenda sawa na sisi tupo salama.

Baada ya kuipata ile nyumba ya mfanyabiashara Rashid Mrutu tulipita barabarani pasipo kufanya chochote tukiwa na lengo la kuchunguza mazingira ya eneo lile, na hapo tukagundua kuwa nyumba hiyo ilikuwa kimya sana na hivyo tukashindwa kujua kama ilikuwa ikikaliwa na mtu au la!

Ila kwa haraka haraka tu tuliweza kubaini kuwa nyumba ile ilikuwa na ulinzi madhubuti kwa kujengewa ukuta mrefu uliofungwa mfumo maalumu wa umeme kwa ajili ya kuzuia wezi, ukuta ambao haukumruhusu mtu yeyote kuona mle ndani. Pia ilikuwa imefungwa kamera maalumu za ulinzi.

Lakini pia tuligundua uwepo wa uchochoro uliokuwa ukipita eneo lile na kutokea mtaa wa pili, nikamshauri Luteni Lister aliyekuwa anaendesha gari aende akaliegeshe gari mtaa wa nyuma, nikiwa na lengo la kurudi kwa njia ile ya uchochoro ili niwe karibu na ile nyumba, nilihitaji kuwa ndani ya mita mia moja ili niweze kuzidukua zile kamera za ulinzi kwenye lile jumba jambo ambalo lingetusaidia kubaini kilichokuwa kikiendelea mle ndani.

Wakati nikishuka toka kwenye lile gari Luteni Lister na Pamela walibaki kwenye gari kwa ajili ya kuchunga usalama wangu na usalama wa eneo lote na pia kufuatilia kila ambacho kingekuwa kinaendelea kule ndani kupitia runinga ndogo iliyokuwemo mle garini endapo ningefanikiwa kudukua zile kamera.

Nikiwa nimeshika simu yangu ya mkononi iliyokuwa na programu maalumu ya utambuzi ya TracerMark ambayo ningeitumia kuzidukua zile kamera za ulinzi na kisha kusafirisha picha hadi kwenye runinga ndogo iliyokuwemo kwenye gari letu, bastola yangu ilikuwa imetuama nyuma kiunoni, nikawa natembea taratibu kama mtu aliyekuwa akipita njia kuelekea mtaa wa pili huku akiperuzi kwenye simu yake kufuatilia jambo kwenye mitandao ya kijamii.

“Kuwa mwangalifu sana, Jason, kwani huwenda hali ikawa tofauti kabisa na vile tunavyofikiria.” Pamela aliniasa kupitia kifaa maalumu cha mawasiliano wakati nikikatiza kwenye uchochoro ule wenye giza hafifu ulionipitisha jirani na ile nyumba ya Rashid Mrutu. Hata hivyo niliwatoa wasiwasi nikiwaambia kuwa niliamini Mungu angekuwa upande wetu.

Wakati nikiwa kwenye ule uchochoro kabla ya kuifikia nyumba ile nikaamua kufanya uchunguzi wa kutaka kujiridhisha kuwa nyumba ile ilikuwa salama na hapakuwa na mtu yeyote eneo lile. Hata hivyo sikuweza kumwona mtu yeyote na hali ilikuwa ya ukimya sana.

Wakati nilipokuwa napita kwenye ule uchochoro nikaanza utundu wangu kwa kuifungua simu yangu na kuingia kwenye mfumo wa TracerMark nikibofya hiki na kile kisha nikaingiza code fulani na muda mfupi uliofuata nikawa nimeshazidukua zile kamera za usalama za lile jumba la Rashid Mrutu, na hapo tabasamu pana likaupamba uso wangu.

Utundu wangu katika kucheza na mifumo ya kiusalama ulikuwa wa kiwango cha juu sana, na nilipofanikiwa kuzidukua zile kamera za ulinzi katika nyumba ile nikagundua kuwa nyumba hiyo ilikuwa na kamera nne za ulinzi; kamera moja ilikuwa imefungwa sehemu ya mbele kwenye geti kubwa la kuingilia ndani ya uzio mpana wa lile jumba. Kamera ya pili ilifungwa ndani ya uzio ili kuonesha mazingira ya ndani ya ule uzio, kamera ya tatu ilifungwa kwenye eneo la sebuleni na kamera ya nne ilifungwa juu kabisa na ilichukua eneo kubwa zaidi ikiwemo watu waliokuwa wakipita kwenye ule uchochoro.

Sasa nilikuwa na uwezo wa kuziendesha zile kamera kwa kutumia simu yangu kana kwamba nilikuwa ndani ya chumba maalumu chenye tarakilishi inayoongoza mfumo mzima wa zile kamera za ulinzi. Na katika kuchunguza niliweza kuona kila kilichokuwemo ndani ya uzio wa jumba lile ambako kuliegeshwa magari matatu ya kifahari sana. Kisha nilimwona mlinzi wa jumba lile, mtu mmoja mrefu na mweupe kiasi ambaye kwa mtazamo wa haraka tu niligundua kuwa alizidi futi sita na alikuwa na mwili wa kimazoezi na mikono yenye misuli imara ya mikononi iliyotuna kikamilifu.

Muda huo wa usiku alikuwa ndani ya koti kubwa jeusi lililomfika magotini, suruali nyeusi ya dengrizi, buti ngumu miguuni aina ya ‘safari boot’ za rangi nyeusi na kichwani alivaa kofia pana nyeusi ya pama iliyokishika vyema kichwa chake na kifuani alikuwa amening’iniza mkufu wa dhahabu ambao kwa kuuangalia tu nilibaini ulikuwa ni wa thamani kubwa sana.

Na nilipoitazama vizuri sura yake niliweza kubaini kuwa alikuwa na sura ndefu na macho yaliyoingia ndani na ndevu zake alizichonga mtindo wa “O”. Muda huo mtu yule alikuwa ameketi kwenye kibanda maalumu cha mlinzi akisinzia. Ndani ya kibanda kile kulikuwa na runinga kubwa, na hapo nikagundua kwamba runinga ile ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya usalama.

Endelea...
 
taharuki..jpg

330

Niliporudia tena kuitazama sura ya yule mtu mara moja nikahisi kumfahamu lakini tatizo likaja, ni nani na nilimwona wapi? Hata hivyo sikutaka kuendelea kujiuliza kwa kuwa nilijua kuwa eneo lile halikuwa eneo salama hivyo muda wote nilitakiwa kuwa katika tahadhari kubwa sana. Nikawasiliana na akina Luteni Lister kupitia kile kifaa maalumu cha mawasiliano kuwauliza kama walikuwa wanaona chochote, wakaniambia kuwa walikuwa wanaona kila kitu kupitia ile runinga ndogo iliyofungwa ndani ya lile gari.

Nikawaambia kuwa nilikuwa napanga kuingia mle ndani, hivyo Luteni Lister awe tayari kuja kulinda usalama wangu wakati nikigonga pale kwenye geti. Na wakati huo nikimtaka Pamela abakie kwenye gari ili kama ingetokea dharura yoyote basi aweze kuwasiliana na makao makuu kwa ajili ya msaada. Kisha nikaanza kulisogelea lile geti huku nikiwa makini halafu nikabonyeza kitufe cha kengele ya getini, nikaisikia kengele ikiita kule ndani. Nikasimama kwa kujiamini pale getini nikiifanya sura yangu ionekane ya kawaida isiyo na wasiwasi wowote.

Kupitia simu yangu ya mkononi niliyokuwa nikiitazama kama niliyekuwa naperuzi mitandao ya kijamii, nikamwona yule mlinzi akishtuka na kuipapasa bastola yake kiunoni kisha akawa kama aliyekuwa anasikilizia. Kitendo kile kikanifanya nirudie kubofya tena ile swichi ya kengele kwa mara ya pili, na hapo nikamwona yule mlinzi akiinuka haraka na kugeuka kuitazama ile runinga kubwa iliyokuwemo ndani ya kibanda cha mlinzi, aliitazama kwa makini kwa sekunde kadhaa, na hapo akaniona wakati nilipokuwa nimesimama pale nje ya geti nikiwa sina wasiwasi wowote.

Nikamshuhudia akijaribu kuwa makini kunitazama huku akiwa kama aliyekuwa akinitathmini. Sikujua alikuwa anawaza nini. Kisha nikamwona akishusha pumzi, huenda mavazi yangu ya gharama, suti nzuri ya kijivu niliyokuwa nimeivaa na kofia ya pama kichwani na namna nilivyokuwa nimesimama kwa kujiamini pale nje ya geti vilimchanganya.

Muda huo nilikuwa naomba asije akanishtukia, na nilijiuliza haraka haraka vipi endapo angenishtukia ningefanya nini! Lakini kabla sijapata jibu nikamwona akipiga hatua kuja pale getini. Alipofika pale getini akalifungua lile geti na hapo akajikuta akitazamana nami uso kwa uso, akanitazama kuanzia chini hadi juu kwa macho yenye kuashiria shari muda wote. Nikamtambua.

Nilijikuta nikitazamana uso kwa uso na yule mwanamume mrefu aliyekuwa amevaa ovaroli la rangi ya samawati, kofia ya pama ya rangi ya samawati aliyoishusha hadi usawa wa macho ili kuficha paji la uso wake, miwani mikubwa myeusi iliyoyafunika macho yake na buti ngumu miguuni aina ya ‘safari boot’ za rangi ya hudhurungi, aliyefika kwenye jengo la Alpha Mall na kuegesha pikipiki yake ya magurudumu matatu kwenye nafasi finyu iliyokuwa katikati ya magari ya Waziri Ummi Mrutu na Daniel Kayera!

Ndiyo… alikuwa yeye na niliweza kubaini kuwa macho yake yalikuwa na dalili zote za ukatili, dharau, unyama na dhihaka ya hali ya juu. Dah…! Mara moja nikajikuta nikisisimkwa mwili wangu na damu ikaanza kumchemka na kukimbia kwenye mishipa yangu ya damu, vinyweleo mwilini na nywele kichwani zikanisisimka kwa hasira na hali ile ikasababisha mapigo ya moyo wangu yaanze kwenda mbio! Nikapeleka mkono wangu kiunoni kwa uficho kuipapasa bastola yangu.

“Nikusaidie nini, ndugu?” yule mlinzi aliniuliza kwa sauti yake nzito inayokwaruza huku akinitazama kwa umakini usoni.

Akili ya haraka haraka ikanijia kwamba nilipaswa kufanya jambo la haraka pasipo kuchelewa kwani sikuwa na muda, hivyo badala ya kumjibu kwa maneno, kwa kasi ya aina yake nikampiga ngumi nzito ya usoni iliyomfanya apepesuke. Kufumba na kufumbua nikaruka na kumpiga teke kali sana la shingo lililomtupa mita kadhaa.

Haraka sana nikatoa bastola na kuishika vizuri tayari kwa kummaliza endapo angeleta matata, lakini nikamwona akiwa ametulia. Nilikuwa nimempiga teke baya sana la shingoni na hivyo sikuwa na imani kama angeweza kuamka tena kwa pigo lile. Hata hivyo bado sikuwa na imani naye, nikasimama na kumwangalia kwa umakini pale chini alipokuwa amelala kimya kisha nikamwendea kwa tahadhari na kumchunguza. Nikagundua kuwa mapigo ya moyo wake yalikuwa yanapiga kwa mbali kuashiria kuwa alikuwa bado ana uhai.

Muda huo huo nikahisi kama kulikuwa na mtu mwingine nyuma yangu, nikageuka haraka huku nikiruka kando na kwa kufanya vile macho yangu yakakutana na macho ya Luteni Lister akiwa amesimama akinitazama kwa tabasamu.

Good job,” Luteni Lister alisema. Sikujibu kitu nikasimama na kuangaza angaza ndani ya ule uzio mpana na lile jumba la kifahari, kisha ndani ya kile kibanda cha mlinzi kuona kama kulikuwa na chochote ambacho kingeweza kutusaidia lakini hakukuwa na chochote cha maana kuweza kutusadia kwa wakati ule.

Kwa kusaidiana na Luteni Lister tukamfunga pingu miguuni yule jamaa na kumvutia ndani ya kile kibanda cha mlinzi kisha tukampekua haraka haraka na kumkuta akiwa na bastola mbili, kete kadhaa za dawa za kulevya na kitambulisho cha kazi kilichoonesha kuwa alikuwa akiitwa Luis Ryoba, mwajiriwa wa kampuni ya ulinzi ya Gadi Security Agency kama mlinzi maalumu.

“Hii kampuni ya ulinzi ya Gadi Security Agency itabidi ichunguzwe ili tujue ni ya nani na ina uhusiano gani na mtandao huu hatari,” nilimwambia Luteni Lister kisha nikaongeza, “Sasa… mimi natangulia kuingia ndani kwa kutumia mlango huo mkubwa wa mbele. Naomba unilinde.”

Na hapo, kwa tahadhari ya aina yake, nikakiacha kile kibanda cha mlinzi na kuanza kuelekea pale barazani lakini machale yakanicheza nikaamua kubadili uelekeo na kuanza kutembea kwa tahadhari kuelekea upande wa kulia wa ile nyumba nikiizunguka katika namna ya kupata uhakika wa hali ya usalama wa eneo lile. Bastola yangu ikiwa mkononi, sikutaka tena kurudi nyuma.

Wakati nikitembea niliyatembeza macho yangu kupeleleza mandhari ya ile nyumba. Ilikuwa nyumba kubwa ya kisasa ya ghorofa mbili yenye madirisha makubwa ya kisasa na baraza kubwa mbele yake iliyopangwa seti moja ya makochi ya sofa.

Sehemu ya mandhari ya nyumba ile ilizungukwa na miti midogo kadhaa na miwili mikubwa ya kivuli na matawi ya miti ile usiku ule yalikuwa makubwa yaliyotengeneza vichaka vya giza la kutisha. Sehemu ya mbele ya ile nyumba ilikuwa imezungukwa na bustani nzuri ya maua ya kupendeza na katikati ya bustani ile kulitengenezwa njia nzuri ya kutembea kwa miguu kwa vitofali vidogo vinavyovutia.

Bastola yangu ikiwa imetulia vyema kwenye kiganja cha mkono wangu wa kulia nilizidi kusonga mbele kwa tahadhari huku masikio yangu yakiwa makini kusikiliza kama mbwa mwindaji. Nilichogundua ni kwamba nyumba ile ilikuwa kimya kabisa na hapakuwa na dalili zozote za uwepo wa kiumbe hai mle ndani, hisia zangu zikaniambia vile, hata hivyo sikutaka kuridhika na hali ile.

Mwishowe nikaifikia sehemu ya nyuma ya ile nyumba na kuanza kupanda ngazi chache za kibaraza cha nyuma kuelekea mlango wa nyuma wa nyumba ile, halafu nikageuka na kumwona Luteni Lister akiwa amejibanza katika pembe fulani akiwa makini kufuatilia nyendo zangu. Nikiwa pale kwenye baraza ya jikoni nikatafuta japo upenyo na kuchungulia ndani lakini sikuweza kuona chochote kwa sababu mle ndani kulikuwa na giza. Taratibu nikausogelea ule mlango na kutega sikio langu, bado hapakuwa na dalili zozote za uwepo wa kiumbe hai.

Endelea...
 
taharuki..jpg

331

Na kitendo cha kuiona nyumba ile ikiwa giza mle ndani halafu ipo kimya kabisa kikaniridhisha kuwa hapakuwa na mtu yeyote ndani, hivyo nikapanga kuingia ndani kwa kupitia upande ule wa nyuma wa nyumba. Nikashika kitasa cha mlango na kujaribu kukinyonga na kuusukuma, ajabu mlango ukafunguka na kujisukuma ndani kirahisi kabisa!

Kengele ya hatari ikaanza kugonga kichwani mwangu. Hisia zangu zikaniambia nigeuzie pale pale nirudi nilikotoka lakini udadisi ukaniambia vinginevyo. Nikausukuma zaidi ule mlango na kujidhihirisha kuwa kile kilikuwa chumba cha jiko na kilikuwa kimegubikwa na giza. Haraka nikaingia mle ndani na kuusukuma taratibu ule mlango nyuma yangu kuufunga huku nikiwa nimechukua tahadhari zote za kukwepa kumshtua kiumbe yeyote ambaye angekuwa ameniwekea mtego mle ndani.

Huku bastola yangu ikiwa mkononi, nilianza kutembea kwa kutumia hisia kwa sababu ya giza lililotanda mle ndani japokuwa taa za kule nje zilikuwa zinawaka, lakini kutokana na mapazia mazito yaliyofunika madirisha ilikuwa tabu kidogo kuona mle ndani. Mara tu nilipokiacha kile chumba cha jiko nikaingia upande wa kulia nikiifuata korido.

Nilipokuwa natokea kwenye chumba kikubwa ambacho hisia zangu ziliniambia kuwa ilikuwa ni sebule milango yangu ya fahamu ikanigutusha kuwa mle ndani sikuwa peke yangu, bali kulikuwa na mtu kama si watu wengine. Wakati nikipambana na hisia zangu mara nikahisi kitu kama chuma cha baridi kikikigusa kisogo changu. Nikahisi moyo wangu ukisimama ghafla kabla ya kuanza kwenda mbio na jasho jepesi kunitoka.

Hata hivyo sikutaka kufa kikondoo nikataka kuitumia bastola yangu niliyoishika mkononi ili kujihami lakini sikufanikiwa nia yangu kwani mkono wangu ulipigwa kwa pigo ambalo sikulielewa kwa haraka lilikuwa la mtindo gani, lilikuwa pigo lisiloelezeka gizani na hapo bastola ikaniponyoka mkononi na kungukia sehemu fulani sakafuni, na nilipotaka kuidaka nikajikuta nikichezea pigo moja makini la teke la kifua lililonitupa chini na kuniacha nikigugumia kwa maumivu makali.

Nikawahi kusimama ili nimfanyie shambulizi la kushtukiza yule mtu lakini nikasikia sauti ya kilimi cha bastola nyuma yangu ikipenya masikioni mwangu na kunionya. Kabla sijajua nifanye nini nikajikuta nikipokea pigo lingine la ngumi ya shingoni iliyonipepesua na kunifanya nirudi nyuma lakini ulikuwa mtego kwani nilishangaa nikichotwa mtama na mtu wa nyuma yangu na kupaishwa hewani. Nilitua chini kwa mgongo na kupata maumivu ambayo yalikuwa hayasemeki.

Hapo nikagundua kuwa nilikuwa napambana na watu wawili mle ndani na hivyo nikaona nisijilegeze vinginevyo ningekufa kizembe, nikaamua kufungua ukurasa mpya wa mapambano badala ya kutegemea Luteni Lister aje kuniokoa. Sikuwa tayari kuruhusu shambulizi lolote tena na hivyo nikajiviringisha haraka pale sakafuni kama gurudumu na kwenda upande wa pili wa ile sebule nikiwa tayari kuanzisha mapambano ya ana kwa ana.

Nilikuwa natumia hisia kwani kwa giza lile nilikuwa naona kitu mfano wa kivuli gizani. Wale watu wakanifuata haraka, jambo hilo nililitaraji na hivyo, nikiwa bado pale sakafuni nikauzungusha mguu wangu kwa kasi ya ajabu na kumchota mmoja wao mtama maridadi uliomwinua juu na kumtupa chini, akaanguka kama gunia juu ya meza ya kioo na kuivunja na wakati huo huo nikawa nimeshasimama, nikamchapa teke la shingoni yule mwenzake mara tu aliponifikia, akayumba kidogo na hapo nikamkita mguu wa tumbo. Akaguna kwa maumivu.

Nikataka nimalize mchezo mapema ili hata Luteni Lister akiingia akute nimeshamaliza kazi, nikatupa pigo la ngumi usawa wa shingo ya mtu aliyekuwa mbele yangu lakini ilikuwa kazi bure kwani yule mtu alikuwa mwepesi kulishtukia pigo langu ambalo lilikata hewa. Kisha nikajikuta nikipokea kipigo cha ngumi tatu kavu za haraka haraka.

Kabla sijakaa sawa pigo jingine la teke lilirushwa lakini nikawahi kulikwepa kwa kuruka hewani na kujipinda, kisha nilipokuwa natua chini nikaachia teke kali lililotua sehemu nyeti, na hapo nikamsikia yule mtu akigugumia kwa maumivu makali.

Yule mwenzake tayari alishanifikia kisha akaanza kunitupia mapigo ya mfululizo ambayo nilijitahidi kuyakwepa kwa kadiri nilivyoweza huku nami nikimtupia mateke yaliyomfanya apepesuke na kugugumia kwa maumivu. Alipotupa ngumi nyingine nikaihisi ikija usoni na kuikwepa kisha nikaudaka mkono wake na kuunyonga kwa ufundi wa hali ya juu kwa mtindo judo halafu nikauvunja. Yule mtu akapiga yowe kali la maumivu.

Na muda huo huo nikamsikia yule mwenzake akiangushwa chini kwa kushindo kikubwa kisha akapiga yowe hafifu la maumivu halafu sauti ikashindwa kutoka tena. Mara hali mle ndani ikawa kimya kwa sekunde kadhaa, nikayatega masikio yangu mle ndani kusikilizia chochote. Nilichoweza kusikia ni sauti za mguno wa maumivu tu toka kwa yule mtu niliyemvunja mkono.

Ghafla taa za pale sebuleni zikawaka na kunifanya nishtuke sana na kuruka kando huku nikijiviringisha kwa tahadhari, macho yangu yalikuwa makini kutazama huku na kule. Nikamwona Luteni Lister akiwa amesimama kando ya swichi ya kuwashia taa, bastola yake ikiwa mkononi. Wale watu waliokuwa mle ndani niliokuwa napambana nao walikuwa wamelala chini sakafuni, mmoja alikuwa akigugumia kwa maumivu huku akiwa ameushika mkono wake wa kushoto uliovunjika, alikuwa akihema ovyo, na mwingine alikuwa ametulia akiwa hana fahamu.

Nikawasogelea na kuanza kuwachunguza vizuri wale watu. Mshtuko ukanijia haraka baada ya kuzitambua sura zao vizuri. Mmoja alikuwa ni Inspekta Thomas Dilunga wa Kituo Kikuu cha Polisi na mwingine alikuwa ni Bosco Gahizi, gaidi hatari wa kukodiwa aliyekuwa akijihusisha na kazi za matukio yenye utata.

Inspekta Tom tayari alikwisha kufa kutokana na pigo kali la judo alilopigwa na Luteni Lister. Luteni Lister alimfuata Bosco Gahizi na kukwapua toka pale sakafuni, bila kujali kilio chake cha maumivu, akamfunga pingu mikono yake kwa nyuma.

Endelea...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom