Mitandao ya kijamii hasa hasa ndio imewafanya watu kuwa watumwa wa simu zao, ni wakati sasa wa kuweka kwenye mitaala kuhusu matumizi chanya ya simu na mitandao ya kijamii. Jamii inaangamia, tatizo linazidi kuwa kubwa kila kukicha. Leo hii mtu hahitaji kuzungumza lolote na mtu wanayesafiri naye pamoja kisa ameweka earphones yupo instagram na kwenye magroup ya whatsap.Simu ni moja ya kifaa cha msingi katika maisha yetu ya kila siku, ndiyo inatuunganisha kirahisi pale tunapokuwa hatupo katika uwepo wa wale tunaotakiwa kuwasiliana nao. Zaidi ya kuweza kuendesha maisha yetu kijamii na kikazi, simu ina uwezo wa kuboresha mahusiano kama ambavyo ina uwezo mkubwa wa kudhoofisha mahusiano hayohayo kutegemeana na matumizi yake.
Makala hii ni ya kwanza katika mlolongo wa makala nilizoandaa ikizingatia matumizi ya simu katika kujenga au kubomoa mahusiano ya mtumiaji kwa watu waliomzunguka katika jamii, iwe ni wenza, wapenzi, ndugu, jamaa, marafiki, wafanyakazi, n.k
Leo nitajikita kwa wazazi/walezi majumbani dhidi ya matumizi ya simu na mwenendo wao kwa familia haswa watoto hadi kupelekea tabia na taratibu zao nyingi kuendeshwa na simu za mkononi wanazomiliki aidha kwa kutambua ama kutotambua. Napenda nitumie fursa hii kutathmini yale nitakayowasilisha, tutoe maoni yanayolenga kuboresha.
Uimara na ukaribu wa wanafamilia unategemea kwa kiasi kikubwa namna ambavyo familia hiyo inahusiana. Kuhusiana vizuri huambatana na matendo ya upendo, heshima na mawasiliano. Hata hivyo, kwa dunia ya leo imekuwa ni Changamoto kuweza kuhusiana vema majumbani, simu ikiwa moja ya sababu kubwa ya upungufu huo. Swali la msingi la kujiuliza, wewe kama Mzazi/Mlezi matumizi yako ya simu yanajenga au kudhoofisha/kubomoa?
Kuweza kufahamu kwa urahisi nafasi zetu katika matumizi ya simu, ni muhimu kuangalia, makosa ambayo wazazi/walezi huyafanya na simu.
Baadhi ya Makosa ambayo wazazi/walezi huyafanya na simu.
1. Kuipa simu umiliki wa akili na msingi wa maamuzi awapo nyumbaniHili limekuwa suala la kawaida sana kwa wazazi/walezi wengi mara wafikapo nyumbani. Wanashinda kwenye shughuli siku nzima mbali na nyumbani, lakini bado wakifika nyumbani wanakuwa ‘busy’ na simu haswa kwenye ku-chati, kutembelea mitandao ya kijamii na kufuatilia masuala mbalimbali ya kiulimwengu kupitia kiganja na hivyo kupuuzia kabisa mwenza/mpenzi pamoja na watoto. Kiasi kwamba kuna wakati anaona kero hata pale mtoto anapokuwa anahitaji umakini (attention) yake kwake. Mbaya zaidi ni kwa zile familia ambazo wazazi/walezi wote wawili wametekwa na simu, hivyo watoto huleana wenyewe zaidi au na dada wa kazi (ikitokea naye hajatekwa na simu).
2. Kutumia simu wakati wa mlo (meals)Wakati wa mlo ni moja la wakati wa msingi wa familia kujamiiana, kufahamu nini kinaendelea katika maisha ya wanao/wanafamilia na ni wakati mzuri pia wa ku re-connect haswa kwa wazazi ambao siku zote wapo makazini na uwepo wao nyumbani kuwa mfinyu. Pamoja na kuwa mzazi hawekewi masharti ya jinsi ya kulea mtoto wake, na kipi cha kufanya ama kutofanya - kitendo cha mzazi kutumia simu akiwa na familia yake wakati wa mlo ni moja ya njia ya wazi inayoonesha kuwa, wale unaowasiliana nao kwenye simu au kile unachokifanya kuwa muhimu zaidi ya kuwapa ‘full-attention’ familia yako kwa ile nafasi ndogo unayobahatika kuwa nao. Heshima ni ya pande zote mbili, mkubwa anapaswa kumuheshimu mtoto kama vile ambavyo watoto wanatarajiwa kuwaheshimu wakubwa zao. Njia rahisi ya kumuonesha heshima mtoto hata mwenza/mpenzi ni kumsikiliza na kumpa usikivu, kujali kile kinachomgusa katika maisha yake ya kila siku na pia kuelewa kile anachokutana nacho kila siku bila kujalisha unaweza kutatua au hutoweza.
3. Kuwapatia watoto simu kwa ajili ya kuchezeaKatika hoja hii tunajikita kwenye yeye kutumia simu ‘yako’ kama kifaa cha kuchezea (siku nyingine nitagusia umri sahihi unaoshauriwa mtoto kuwa na simu). Kuna tofauti ya mtoto kumiliki simu akiwa kanunuliwa na mzazi, na mzazi kumpatia mtoto simu awe anachezea. Kumpa mtoto simu achezee ni njia mojawapo rahisi ya kumridhisha mtoto kiasi kwamba atatulia hapo bila usumbufu wowote ule. Mzazi gani hataki apumzike mtoto asimkere au kumsumbua ? Ni wengi. Bahati mbaya, ni wazazi wachache ambao wanafahamu namna ya kuweka/kubadilisha matumizi ya vifaa hivyo ili viwe kwenye mfumo wa matumizi ya mtoto (kid mode). Na mbaya zaidi, wazazi wengi huitumia kama kumtuliza mtoto wakifuata njia rahisi na badala ya ile ndefu ya kuweza kumkatalia mwanae kwa kumwelewesha kuwa si wakati wote ni wa kuchezea simu na hivyo kujenga mtoto ambaye anaona anastahili kila kitu kilichopo machoni pake bila kujali simu hiyo ni ya mgeni ama lah.
Athari
1. Kutojenga nidhamu ndani ya familia. Watoto wanakua katika mazingira ya kuonyweshwa kutokuwepo na umuhimu na haja ya muda wa familia na thamani yake. Na pia mtoto kuona ni sawa kudharau ‘ignore’ watu pale ambapo umakini wake unahitajika.
2. Kama mzazi/mlezi unakuwa unapitwa kwa kiasi kikubwa na yale yanayojiri katika maisha ya watoto haswa kama ni wadogo. Watoto wanapenda kusililizwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa. Kuna changamoto ya mapenzi yanayopaswa kuelekezwa kwa mzazi yakatolewa kwa mtu ambaye anaweza kuwa si salama kwa mwanao.
3. Kukosekana kwa nyakati za msingi za kifamilia ambazo hujenga kumbukumbu za msingi kwa mtoto. Kama vile kukaa na kula pamoja, kusali sala ya usiku pamoja, kukaa na kufurahia kitu kwa pamoja.
4. Wazazi/Walezi kutofahamu yale yanayojiri kila siku katika maisha ya watoto wao. Inaweza kuonekana ni sawa, ila watoto nao wana changamoto zao wanazozipitia kila siku ambazo zinahitaji umakini na ukaribu wa wazazi na walezi patika kuwajenga kuwa vijana wazuri katika maisha yao. Wengine hupatwa na unyanyasaji wa kijinsia, na mtoto hutakiwa kujengewa kujiamini na kumuamini mzazi ili kueleza tatizo analokutana nalo, wakati mwingine hata ndani ya familia.
Ushauri
Tumekuwa wazazi na walezi ambao tupo Katika wakati ambao teknolojia imekuwa kubwa kuliko wakati wowote ule hapa duniani. Ni muhimu sana kuwa karibu sana na watoto wetu, na kuhakikisha hizi simu hazitufanyi mazezeta kiasi kwamba tunasahau majukumu na nafasi zetu pale tunapokuwa majumbani na familia zetu.
Kwa wale ambao kazi zinachukua maisha yako kwa kiasi kikubwa, wanaweza pia kujenga tabia ya kuwa na simu mbili. Simu ya kazi na simu ya nyumbani. Pale unapokuwa umefika nyumbani unazima kabisa simu na kutumia vema muda huo kwa ajili ya nyumbani ili kupunguza usumbufu. Nidhamu hutokana na kujiwekea misingi ya matumizi mazuri ya simu ambayo kwa namna yoyote ile hayataingiliana na nafasi yako kama mzazi/mlezi nyumbani.
Ni muhimu pia kwa familia kujiwekea taratibu za kuhakikisha simu haziruhusiwi kwenye baadhi ya nyakati za ‘family time’ ili kujenga mazingira ya kuwa karibu na kuzingatia wale walio mbele yako na si wanaopatikana kwenye simu.
Nimewasilisha hayo kwa uchache, una maoni, mawazo, ushauri au marekebisho? Tafadhali usisite kuchangia.
Karibuni katika kufahamishana zaidi,