Simamisha na kufukuza, je ndio kipimo cha uongozi bora?

Simamisha na kufukuza, je ndio kipimo cha uongozi bora?

activisty

JF-Expert Member
Joined
Apr 1, 2012
Posts
315
Reaction score
107
SIMAMISHA NA FUKUZAFUKUZA JE NDIO KIPIMO CHA UONGOZI BORA? SHERIA ZISIPOFUATWA TUTAJENGA TAIFA LA CHUKI NA HOFU.

Nianze waraka huu mfupi, kama salamu zangu kwa serikali ya awamu ya tano ya chama cha mapinduzi na kwa watanzania wote kwa ujumla. Ni wazi kwamba sasa idadi ya wafanyakazi wa umma wanaosimamishwa na kufukuzwa kazi imekua kubwa. Tokea serikali hii imeingia madarakani ni dhahiri kwamba kazi kubwa iliyofanya ni kusimamisha ama kufukuza watu kazi.

Na hakika nitakua sio mkweli na mzalendo kwa taifa langu nikisema kazi hii ya kuwaondoa watumishi wazembe na mafisadi sio kazi nzuri ambayo serikali hii inaifanya. Lakini Lengo la waraka huu ni moja tu, kuelezea ukweli na uhalisia wa mambo mbalimbali yanayofanyika chini ya serikali hii, na matokeo yake katika kulijenga taifa imara la Tanzania.

Kila mtu anataka mafisadi waondolewe, wazembe waondolewe lakini kwa kufuata taratibu za kisheria na katiba ya nchi. Kazi hii ya kupambana na ufisadi haiwezi kufanywa kimazingara tu. Lazima watu waandaliwe na sheria imara ziundwe ili zidhibiti watumishi wazembe na wezi.

Leo Rais anafukuza watu hadharani, watanzania tunampigia makofi tunasema kweli huyu ni kiongozi bora. Swali ni je, kipimo cha uongozi bora ni kufukuza watu au kuwasimamisha watu kazi? Nani kakwambia wote watakaoondolewa au kufukuzwa basi watakua ni wezi, watakua ni wazembe kama wewe mtanzania unamjenga kiongozi tena mwanasiasa kuamini kwamba nikisimamisha watu kazi na kuwafukuza basi nitakuwa kiongozi bora kwa wananchi wangu. Ni kipi sasa kitamzuia kufanya ivo bila kufuata sheria, bila kujali utu na haki za binadamu ili aipate sifa na heshima hiyo toka kwako wewe mwananchi?

Leo wakuu wa wilaya,mikoa,wakurugenzi,mawaziri kwao imekua sasa, ndio mtindo wa kufanya kazi. Kuita waandishi wa habari na kuwaondoa watumishi wa chini yao basi tu kwa ajili ya kuyatafuta makofi na shangwe za wananchi na wateuzi wao kwamba wanafanya kazi. Wanafanya hivi kwa sababu wananchi tumekua wadhaifu, hatufikiri na kutenda kwa hoja bali kwa mihemko na ushabiki wa kisiasa. Viongozi nao wanafanya hivo hivo.

Najiuliza ni taifa gani tunalijenga? Kama hoja ni watumishi hewa nauliza ni mfumo upi sasa unaondaliwa ili kuhakiki, na kufanya tathimini kwa watumishi, ili wakiondolewa sasa miaka miwili ijayo tusije kufanya kazi nyingine ya kuwaondoa tena watumishi hewa wapya. Na tena ni kwa vipi wakuu wa wilaya, mikoa wamehakiki idadi ya watu wote wanaodaiwa kuwa ni watumishi hewa katika maeneo yao ni sahihi? Tusije kuwa tunapokea idadi ya watimishi walioko likizo, wagonjwa n.k ati kuwa ni watumishi hewa kwa lengo lile lile la kuonekana serikali inafanya kazi.

Ndugu zangu watanzania niseme tu kuwa tusiwe wepesi wa kuamini kila lisemwalo au lifanywalo na wanasiasa. Tusiweke taaluma zetu mifukoni, tusisahau dhiki inayotukabili, tusisahau ahadi na mbwembwe za uchaguzi, na tusisahau kuwa viongozi tunawachagua sisi,ili wasimamie yale yaliyo sahihi na muhimu kwetu kwa kufuata misingi ya haki na sheria na hatuwachagui ili tuwe mashabiki wao. Tukiendeleza ushabiki huu, tukawajenga viongozi katika jeuri na sifa tutajenga taifa la hofu na chuki.

Nasema tutalijenga taifa la hofu na chuki kwa sababu mfano leo hii wewe ni mama mwenye nyumba, ambaye hauna kazi, unazurura mchana kutwa kusaka na kusambaza umbea huku mumeo ambaye anajituma kwa kufanya kazi kwa bidii ili akiondoka asubuhi akuachie hela ya matumizi kwa ajili ya familia na mwisho wa mwezi amlipe dada wa kazi mliomuajiri ili akusaidie kazi, anarudi nyumbani jioni akiwa amechoka unampokea kwa maneno kwamba huyu dada afanyi kazi, ni mvivu, jeuri n.k na tena anapoenda mezani ili atizame chakula anakuta ugali na maharage ambayo yameungua na kuzidi chumvi, na wewe bila aibu unarusha lawama kwa dada wa kazi ati amekuibia hela aliyokuachia.

Mmumeo ananyanyuka na kukuchapa makofi huku na wewe ukinyanyuka kwa jazba na kumrarua makofi dada wa watu. Mumeo anakuamini na kukusikiliza kumbe dada wa watu kutoka pale njombe iringa uliyeletewa na rafiki yako,anajituma na kufanya kazi kwa hofu na uoga siku hadi siku, maumivu yanazidi anashindwa kuvumilia, hasira inamjaa na hatimaye chuki inamchukua.

Nauliza ni nini dada huyu kitakachomshinda kukifanya ili kulipa uovu huo unaomtendea? Je utarudi jioni na kumkuta mwanao ndani ya friji na dada haonekani? Ama je utarudi nyumbani, na kula chakula chenye sumu wewe, mumeo na watoto kisha mpoteze maisha wote, huku dada wa watu naye akijitoa uhai?Nani wa kulaumiwa hapo baba ambaye anamuamini na kumsikiliza mkewe, mke ambaye ni muongo na mnafiki, au dada wa kazi ambaye ni mtumwa na kiraka cha manyanyaso?

Sisi wananchi ndio ambao tumemwajiri Baba, kwa kodi zetu analipwa yeye na serikali na viongozi wote ambao tumewachagua, kuanzia na yeye kiongozi mkuu wa familia hii ya Tanzania ambaye tumempa madaraka makubwa zaidi, tukimsikiliza na kumuamini.(Baba) yeye naye anawasaidizi wake ambao wanafanya kazi na kumletea taarifa anawasikiliza na kuwaamini (mama)
wapo pia watumishi wadogo zaidi yao, wazembe, wezi, wavivu n.k (dada wa kazi)

Fanya tathimini ya familia ya namna hii ambayo baba anampiga mama mbele ya mtoto na dada wa kazi, mama naye anampiga dada wa kazi mbele ya mtoto. Nani atamuheshimu mwenzie hapa? Nini hatma ya familia ya namna hii? Inayoishi pasipo utaratibu na ustaarabu? Nimalizie tu kwa kusema kama nchi haitaongozwa kwa utarabu wa kisheria na maadili ya kufata katiba, basi tutambue tunajenga taifa la hofu na chuki kama familia hiyo hapo juu. Na zaidi kama matatizo yanayosababishwa na sheria mbovu yataendelea kutatuliwa kiholela bila kuundiwa suluhu ya kidumu ambayo ni sheria imara, basi kilio cha kero na matatizo haya hakitokwisha."Tanzania ni ya kwetu sote, kazi ya viongozi si kutuamulia ama kutufanyia maamuzi bali ni kushauri, kusimamia, na kutekeleza maamuzi yetu sote kwa pamoja"

By Mwanaharakati Huru
@activistyi@yahoo.com
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom