Zanzibar inajifunza nini toka Bolivia.
KAMA kuna kura yoyote ya maoni inayohitajika huko Tanzania Visiwani basi ni ile ya kuwauliza Wapemba je wanataka kuwa jimbo huru ndani ya Zanzibar na Tanzania.
Mantiki ya hili ni kutokana na ukweli ambao CCM imeshindwa hadi leo kuuona. Na ukweli huo si mwingine ila Pemba nzima inaikubali na CUF na wanataka kutawaliwa na serikali ya CUF na sio SMZ.
Somo ambalo bado ni bichi kabisa ni lile la Santa Cruz [Pemba ya Bolivia] ambayo wananchi wake wametumia demokrasia kumpasha kiongozi wa nchi nzima, Bw. Evo Morales [Amani Abeid Karume wa Bolivia] kuwa wao wanataka kuliendesha jimbo lao wao wenyewe ili wahakikishe wanautumia uchumi wao kunufaisha watu wao.
Hili limewezekana kutokana na vuguvugu na harakati za wananchi, wafanyabiashara, wanasiasa jasiri na wasomi wa jimbo hilo la Santa Cruz kudai haki ya kuliendesha jimbo lao kwa namna ambayo wao wanaamini itakuwa bora zaidi kwao kuliko kushurutishwa kufuata kile uongozi wa nchi nzima unachokitaka [ambao wanaamini ni gharama na hasara kubwa kwao].
Tayari wana Santa Cruz sasa wanajiita wa-Crucenos na ushindi wao katika kura ya maoni ni tiketi ya kuwa na jimbo linalotawaliwa na watu waliowachagua wao na sio vinginevyo.
Kwa miaka mingi Bolivia nchi yenye utajiri mkubwa wa maliasili lakini ni masikini wakubwa imekuwa ikitawaliwa na madikteta na viongozi wabinafsi, mafisadi na wasioona mbali na mbele.
Wakazi wa Santa Cruz kama walivyo Wapemba wanaamini kwamba wana uwezo wa kufanya jimbo lao kuwa Dubai ya huko kwao.
Kama kawaida ya viongozi wabovu wanapoona sehemu fulani ya nchi yao inataka kujitenga na kujiendesha yenyewe kwa ustawi na ufanisi zaidi kwa watu wao, Bw. Morales na wafuasi wake walianza kuwahujumu wana Santa Cruz mara baada ya matokeo ya kura ya maoni kutangazwa. Achilia mbali maelfu ya watu waliokwaza katika kujiandikisha na kupiga kura kabla ya hapo.
Kinachotokea huko Bolivia ni mwanzo tu wa utabiri wa watu kama Alvin Toffler ambao wanaamini miaka ya 2010 kuendelea mbele itakuwa ni miaka ya watu na maeneo mengi zaidi toka Afrika hadi Uchina kudai haki ya kujitawala na kuendesha maisha yao wenyewe hata wakiwa wachache namna gani. Sababu kubwa ikiwa kukosa viongozi wanaoweza kuongoza watu wengi na maeneo makubwa vizuri.
Uwezo wa kuongoza duniani hivi leo umezidi kuwa dini kadri miaka inavyokwenda.
Ni dhahiri baada ya Santa Cruz majimbo mengine kadhaa ya Bolivia yanaweza nayo kuamua pia kuendesha mambo yao wenyewe chini ya serikali ya shirikisho.
Ujumbe kwa SMZ na serikali ya Muungano ya Tanzania ni kuwa wananchi wa Pemba wanashindwa kuwaelewa kwa kukataa muafaka na kutoa mwanya kwa watu wenye itikadi kama za wa-Crucenos wa Santa Cruz [Pemba ya Bolivia] na wao kuamua kudai haki ya kuongozwa na wale waliowachagua na sio vinginevyo. Hii ni haki yao, na hii ni demokrasia!
Hakika mkataa pema pabaya panamuita. Chagueni kati ya serikali ya mseto au Wapemba kuiga kutoka Santa Cruz siku moja ambayo si mbali sana kutoka sasa!
Tukiulize Chama cha Mafisadi [CCM] ni wapi zaidi ya kwa Robert Mugabe, huko Zimbabwe, wamewahi kuona mtu anashinda uchaguzi kisha anazuiwa kuwatawala waliomchagua kama sio tu Zanzibar!
mwisho