Siasa na wasomi kulikoni....?

Siasa na wasomi kulikoni....?

RUV ACTVIST.

JF-Expert Member
Joined
Jan 14, 2012
Posts
472
Reaction score
111
KIONAMBALI alikuwa akisoma kitu
kwenye mtandao. Mwandishi wa
kitu kile alikuwa anasema kwamba
wanafunzi wenye akili nyingi
husoma na kuwa wahandisi.
Wenye akili za wastani husoma na
kuwa wahasibu na wanasheria, na
katika mfumo wa utawala wa
taasisi, hawa huwaongoza
wahandisi.
Wale wenye akili zisizo nyingi sana
huingia katika siasa na kuwaongoza
wale wenye akili zilizowazidi, na
wale wasio na uwezo wa kiakili
kabisa huingia katika biashara na
wakawa matajiri, kisha
wakaabudiwa na wasomi na
wanasiasa.
Haya si maneno yangu,
nimeyanukuu na bahati mbaya
simjui mtunzi. Ni wazi kuna kiasi
fulani cha ukweli kwenye maneno
haya ingawa sio ukweli
uliokamilika.
Wakati akipewa shahada ya
heshima katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, mwanafasihi mkongwe,
Ngugi wa Thing’o, alitumia maneno
makali.
Alisema wasomi wa Afrika ni
wasaliti. Naungana naye nikisema
wasomi wengi wa Afrika na
Tanzania ikiwa sehemu ya Afrika ni
wasaliti.
Wengi wao hawajaweza kuwa
sehemu ya ukombozi wa kweli wa
raia wa kawaida.
Hawajaweza kutumia elimu yao
kuifanya Afrika nayo isikike kwa
mema. Vita ya wenyewe kwa
wenyewe, mauaji ya halaiki, njaa,
ukosefu wa demokrasia na
utoroshaji wa utajiri kutoka Afrika
kwenda sehemu nyingine duniani
umeendelea licha ya bara hili kuwa
na wasomi wengi waliosomea
ndani au nje ya Afrika.
Wasomi hawataki kujitia najisi ya
kisiasa! Wamebaki mbali
wakiendelea na nadharia zao za
uongo na kweli, na wengi wao
wakijikomba kwa watawala labda
nao watabahatika kupata makombo
ya vinono vinavyodondoka mezani
kwa wakubwa.
Na hata wasomi walioingia katika
siasa, wengi wameingia sio kusaidia
kubadilisha hali halisi ya watu, bali
kuwa sehemu ya mfumo ule ule
ambao wengi tunasema una tatizo.
Wasomi wanaharakati
wanahesabika kwenye viganja vya
mikono. Na bahati mbaya wale
waliokuwa na uwezo wa kusema
kweli bila kuogopa watawala,
wengi wao wameshatangulia mbele
ya haki.
Nikiwataja kwa uchache ni akina
Profesa Haroub Othman, Profesa
Chachage S. Chachage, Dk.
Seng’ondo Mvungi na wakili
maarufu Juan Mwaikyusa.
Wasomi wachache waliojaribu
kuingia katika harakati za
mabadiliko waliamua kufanya
“ajua”, wakageuka na kurudi
walikokuwa wanapinga. Hawa ni
pamoja na Dk. Masumbuko Lamwai
na Dk. Walid Aman Kabouru.
Wasomi wamebaki wachache sana
ambao wanatumia usomi wao
kuikomboa jamii hii kutoka katika
madhila yanayoikumba.
Wasomi wetu pamoja na kukalia
madawati miaka mingi, hawajaweza
kuja na suluhu ya kweli kuhusu
umaskini wetu.
Hata ukiwapa uwaziri, badala ya
kuleta suluhu ndio wanatangaza
kabisa Waafrika hatuwezi! Sijui
tafiti hizi wamezifanyia wapi.
Lakini hata hao wasomi ambao
hawajajiingiza moja kwa moja
katika siasa wanashindwa hata
kutoa machapisho na kuzua
mijadala ya namna tunavyoweza
kujikwamua hapa tulipo na
kusonga mbele.
Wakifanya chambuzi zao mara
nyingi ni nadhari tupu! Ukisikia
wakichambua hali ya kisiasa
Tanzania utashangaa.
Wataeleza namna ambavyo
wapinzani hawawezi kuchukua
nchi, lakini hawataeleza wafanye
nini ili mabadiliko ya kisiasa
yatokee. Wamekaa mbali kama vile
wakishiriki siasa watapata najisi.
Wananyoosha vidole na kubashiri
chama hiki au kile cha upinzani
kitasambaratika. Lakini hawajadili
kama virusi vikiachwa ndani ya
vyama hivyo matokeo yake ni yapi.
Wasomi Watanzania wamekubali
akili ndogo ziendelee kuongoza
akili kubwa. Wengi wao
wanaogopa kukaa upande wa
kukosoa watawala.
Wachache walioamua kuingia
kwenye siasa wamefuata mkondo
ule ule ambako matumbo yao
yatashiba.
Tatizo kubwa la mfumo kama huu
ambapo wasomi wanaogopa kukaa
upande wa mabadiliko, ni kwamba
mabadiliko ni lazima yatakuja bila
kujali wasomi wako upande upi.
Inapofika wakati wa mabadiliko na
wanaochukua hatamu ni vichaa,
ndio utaona yaliyotokea Uganda
wakati wa Iddi Amin. Ni muda sasa
wa wasomi kushirikisha jamii kile
walichojaliwa kichwani mwao na
kukitumia kuleta mabadiliko.
Wasikae tu kimya au kuwapamba
watawala. Tulidhani wasomi ndio
wanaopaswa kuwa watu wa kuibua
mijadala muhimu ya kijamii. Ni
wasomi ndio wangetuambia
kwanini gesi itoke Mtwara kwenda
inakokwenda.
Ni wasomi ndio wangetuambia
namna Watanzania tunavyoweza
kuwekeza katika maliasili zetu gesi
ikiwemo. Ni wasomi ndio
wangetusaidia kutuonyesha namna
mfumo wa demokrasia ulivyo na
upungufu na uwanja wa
mapambano ya kisiasa usivyo na
ulinganifu.
Hatuhitaji wasomi wa kutuimbia
ngonjera kutuonyesha rais
amepanda umaarufu kwa asilimia
ngapi. Tunataka wasomi wa
kutuambia kwanini rushwa
inaongezeka kila kukicha licha ya
kelele za wanasiasa, kwamba
wanapambana nayo.
Tunataka wasomi wa
kutuchambulia inawezekana vipi
tukawa maskini tuliozungukwa na
utajiri. Tunataka wasomi wa
kutuambia tunaweza vipi kubadili
mfumo uliopo kwa uhalali na
usalama.
Tunataka wasomi wanaotekenya
akili zao badala ya kukaa pembeni
na kutoa ubashiri kama wapiga
ramli!
Na bahati mbaya ni kwamba hata
vijana wanaosoma katika vyuo vya
elimu ya juu hawatupi matumaini
yoyote. Unaweza kusema wengi
wao wanatumika tu na wanasiasa
kama mtaji wa kisiasa.
Ukichanganya na aina ya makuzi
wanayopata siku hizi, wanakuwa
kama bendera inayofuata upepo
unakovuma. Sijaona wanafunzi wa
vyuo vikuu wakiandaa midahalo
isiyokuwa na upande wakajadili
mustakabali wa kisiasa wa taifa
letu.
Wanasubiri Godbless Lema au Nape
Nnauye aende kuzungumza nao na
wao washangilie au wazomee.
Wanaingia katika vyama kwa
kuchungulia wapi kunaonekana
kwenye matunda ya uwezekano wa
kushibisha njaa zao.
Wengi wanakubali kutumiwa. Ni
wachache wanaojitambua na
kusimama wenyewe kwa kuamini
katika misingi inayofahamika
badala ya ushabiki wa juu juu wa
kisiasa.
Kama wasomi hawataingia katika
siasa kwa maana ya kutoa
michango yao ya mawazo na hata
kushiriki moja kwa moja katika
harakati za mabadiliko, bado safari
ya kubadili mfumo huu
unaoonekana kushindwa kutoa
majibu ya matatizo yetu ni ndefu.
Nani awaelimishe wale ambao
hawakubahatika kwenda shule
kupata elimu? Au wasomi wetu
walipokuwa wanasoma akili yao
haikupanuliwa kuweza kujadili
masuala mapana ya jamii badala
yake wakabaki tu waking’ang’ania
wanachosoma bila kujua
kinatumika vipi kuisaidia jamii
yetu? Au usomi wao bado
umeathiriwa na kasumba ya
kikoloni?
Tunajiandaa kuingia katika
uchaguzi mkuu mwakani. Mwaka
huu kutakuwa na mchakato wa
kumalizia kupata katiba mpya. Nini
nafasi ya wasomi?
Au wao wanajiona wateule walio
nje ya jamii wakisubiri kufanya
uchambuzi baada ya matukio
badala ya kusaidia kuwezesha
matukio muhimu kutokea salama
na kwa weledi?
Wasomi wetu wasipojitambua sisi
wa kisomo cha akina ngumbaru si
ndio tutapotea kabisa? Bila maarifa
kizazi cha mwanadamu
kitaangamia.
Wasomi wetu wasikae pembeni
wakati wanaona tunakwenda njia
isiyo sahihi. Waingie ndani na
walete mabadiliko. Na wanasiasa
nao wawape nafasi wasomi ili
washiriki kwa namna chanya katika
siasa zetu.
Natamani kuanzia mwaka huu
tuone nguvu ya wasomi katika
kuleta mabadiliko ya kweli sio
kuwashabikia mabeberu na
watawala!
 
Wasomi wetu wamelala wakiamka labda watayaona masikitiko yako.Kwa sasa tujipe pole wamelala usingizi wa pona na walioamka wamelewa kilevi kinaitwa MADARAKA.Ni kweli wametusaliti hawa wenzetu.
 
Back
Top Bottom