Shule za Serikali zitakosa wanafunzi kidato cha tano

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,322
33,126
mwananchi-logo.jpg


HABARI kwamba idadi ya wanafunzi waliotarajiwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu imepungua kwa zaidi ya asilimia 13 kutokana na ufaulu mdogo wa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana bila shaka zitakuwa zimewashtua watu wengi. Habari hizo zilizotangazwa juzi na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo zimeibua maswali mengi kuliko majibu kuhusu mustakabali wa sekta ya elimu katika nchi yetu.


Wakati wizara hiyo ilipotangaza majibu ya kidato cha nne mapema mwaka huu na kusema kiwango cha ufaulu kilikuwa kimeshuka, wengi hawakujua hali hiyo ingeathiri idadi ya wanafunzi wa kuingia kidato cha tano kwa kiwango kikubwa kiasi hicho. Ndiyo maana habari hizo zilizotangazwa na naibu waziri huyo juzi siyo tu zimewaacha wadau wengi wa sekta ya elimu katika mshangao na mfadhaiko mkubwa, bali pia zimeibua hisia kwamba Serikali isipochukua hatua za dhati na haraka kusuka upya mfumo wa elimu uliopo hivi sasa, viwango vya elimu vitazidi kushuka kwa kasi ya ajabu.

Inatia hofu kufikiria athari zinazoweza kutokea kutokana na hali hiyo. Kama ufaulu huu mdogo umepunguza idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano kutoka wanafunzi 36,366 mwaka jana hadi wanafunzi 31,516 mwaka huu kama alivyosema Waziri Mulugo juzi, tujiulize upungufu huu wa wanafunzi 4,850 sawa na asilimia 13.34 utaleta athari gani katika shule za sekondari za Serikali ambazo hasa ndiyo kimbilio pekee la watoto wa wakulima? Uko wapi muujiza utakaowezesha shule hizo siyo tu kuziba pengo hilo, bali pia kubakiza wanafunzi waliofaulu kwa viwango vya juu katika madaraja ya kwanza na ya pili?

Hofu yetu kubwa inatokana na ukweli ufuatao ambao tunausema hapa pasipo kutafuna maneno. Ukweli huo ni kwamba sekondari za Serikali zitapata pigo kubwa la uhaba wa wanafunzi wenye sifa katika kidato cha tano. Hii ni kwa sababu idadi kubwa ya wanafunzi waliopata madaraja ya kwanza na ya pili katika mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana na kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano mwaka huu katika sekondari za Serikali watajiunga na sekondari za watu binafsi. Habari zinasema tangu matokeo ya mtihani huo yatolewe mapema mwaka huu, wanafunzi wengi waliofanya vizuri tayari wamejiunga na shule hizo.

Nini basi matokeo ya hali hiyo ya kutisha na kusikitisha? Kwanza, Serikali italazimika kuteremsha viwango vya ufaulu kwa kiasi kikubwa ili angalao shule zake zenye kidato cha tano zipate angalao asilimia 95 ya ujazo wa wanafunzi. Pili, kutokana na hali hiyo, uchaguzi wa wanafunzi wa kuingia kidato cha tano katika shule za Serikali itabidi urudiwe ifikapo katikati ya Aprili ili kujaza nafasi za wanafunzi waliojiunga na walio mbioni kujiunga na shule za watu binafsi kwa sababu idadi na majina yao yatakuwa tayari yamejulikana.

Tatizo hilo bila shaka litaziweka shule hizo za Serikali katika hali ya sintofahamu kwa sababu matokeo ya kuingiza wanafunzi ambao hawana sifa katika kidato cha tano yatajidhihirisha pindi watakapofanya mtihani wa kidato cha sita. Hatuhitaji mtabiri kutudhihirishia kwamba matokeo ya mtihani wao wa kidato cha sita yatavunja rekodi kwa wanafunzi hao kuambulia sufuri.

Ndiyo maana tunasema Serikali hivi sasa iko katika wakati mgumu na ingefaa itambue kwamba huu sasa ni wakati wa kusuka au kunyoa, kwani itasababisha balaa iwapo haitatumia busara na hekima kutafuta jawabu la kudumu la hali hiyo tata. Tunashauri kwamba Serikali iweke mikakati ya muda mfupi na muda mrefu, lengo likiwa ni kuinua viwango vya elimu kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu na isifanye hivyo kwa maono ya kisiasa kama ilivyokuwa katika uanzishaji wa sekondari za kata.

Shule za Serikali zitakosa wanafunzi kidato cha tano
 
Back
Top Bottom