Short story: Hisia

dawa yenu

JF-Expert Member
Joined
Jan 7, 2014
Posts
2,833
Reaction score
3,753

Naitwa Hamisa Stephen. Leo ni siku muhimu sana kwangu. Ni siku ya kuzaliwa kwangu pia leo ni siku ya mia moja tokea niwe mkazi ndani ya gereza hili. Tazama mwili wangu ulivyodhoofika hata nafsi yangu haina nguvu. Roho yangu imekata tamaa. Nahisi moyo wangu unararuka kwa maumivu makali yanayonikabili. Nimebakiza siku elfu tatu mia tisa ili niachiwe huru. Sioni tumaini lolote mbele yangu. Mboni za macho yangu zimepoteza nuru. Sina imani, nimechoka. Najua nitafia ndani ya kuta za gereza hili ila kabla mauti hayajanifika naomba niseme nawe leo.

Nimekuambia leo ni siku muhimu kwangu. Sihitaji zawadi kubwa kutoka kwako bali muda na usikivu wako vinanitosha na hakika nitashukuru sana. Hali yangu taabani, ona sina siha njema. Nazihesabu pumzi zangu, kila inayoingia inakuwa chungu kuliko inayotoka hakika nimechoka!Maisha ni safari ya walio hai lakini uhai ni nini? Hakika siuoni uhai ndani yangu. Kila pumzi inayotoka natamani iwe ya mwisho ichukue maisha yangu. Historia ya maisha yangu ni ndefu ila nitaanzia pale kwenye kisa kitamu cha mapenzi.

Mvuto wa penzi lake ulizinasa hisia zangu. Faraja ya moyo wangu alikuwa yeye, nilimpenda kwa dhati ya nafsi yangu. Tuliunganishwa na mengi ila nguvu ya upendo baina yetu haikuwa na kifani. Alinifunika kwa huba nami nakamtunukia zawadi ya penzi motomoto lililoutakasa mtima wake. Nilimpenda sana na yeye akanipenda kuliko alivyoyapenda maisha yake lakini mkasa ulianza hivi.

Ilikuwa jioni tulivu iliyoambatana na kaubaridi kwa mbali. Ilitupendeza kuitumia jioni hii pamoja nje ya hoteli hii ya kifahari. Tulipuliziana mahaba taratibu kwa manjonjo tele huku vinywaji vikisindikiza maongezi yetu. Wakati huo wote hisia zetu ziliburudishwa na mashairi mwanana ya mwanadada Maua Sama kutoka kwenye spika kubwa zilizokuwa katika eneo lile. Nikafuatisha mashairi yale, kwa sauti laini nikamuimbia mpenzi wangu,

“Sisikii,

Kwa penzi lako lako sioni,

Ooh baby please…

Love me like you do”

Ilipendeza sana. Nilihisi naelea juu ya bahari ya mapenzi. Basi akatabasamu kisha akanipiga busu jepesi shavuni lililoambatana na neno, “I love you Hamisa!” nilisisimka, sikuweza kujibu nilihisi nimemwagiwa maji ya baridi. Ilikuwa kama filamu ya kihindi yenye kisa murua cha mapenzi, alikuwa Shah ruh khan na mimi nilikuwa Kajol.

“Ooh sorry baby, I will be back” aliongea Patrick huku akinyanyuka taratibu. Alisimama kwa sekunde kadhaa akaniangalia usoni bila kusema chochote. Ni kama vile alikuwa na kitu moyoni ila hakujua ni maneno gani ayatumie katika uwasilishaji. Nilimstahi nikiamini wakati ukifika ataniambia lililopo moyoni mwake.

“Mmh I will be back darling” Aliniaga tena nikatabasamu kumkumbusha kuwa aliishaniaga. Alitikisa kichwa kwa soni kisha kwa hatua za taratibu huku akibonyeza simu akawa anaelekea ndani ya jengo lile la hoteli. Kila hatua aliyopiga macho yangu hayakubanduka kwake, nilipenda kumuangalia, zaidi ya yote nilipenda kujua anaenda wapi.

Nakumbuka njiani alionana na muhudumu wa hoteli. Waliongea kidogo ila hilo lisingenipa hofu yoyote kama wasingeshikana mikono na kuingia ndani. Sikupenda nilichokiona, sikupenda hata kidogo. Ile scene haikunivutia na laiti kama ingekuwa movie basi ningeshurutisha ile scene ifutwe maana haina maadili. Nilimeza mate kwa wivu ulichanganyika na hasira kisha nikashusha pumzi kudhibiti hisia zangu.

Sekunde ziliyoyoma, dakika zikapotea! Taratibu furaha yangu ikaanza kuyeyuka. Niliutazama ule mlango kwa uchu ya kuwaona wawili wale wakitoka ila hayo yalibaki kuwa matamanio yangu tu! Mapigo ya moyo wangu yakabadirika! Nikashindwa kuzidhibiti pumzi zangu! Sikupenda ile scene. Ana biashara gani na yule muhudumu? Wanafanya nini humo ndani? Kwanini sishirikishwi?

Nilihisi shetani anaranda randa maeneo yale name sikutaka kumpa nafasi. Nikachukua simu na kumpigia! Simu iliita, simu ikaita tena, ikaita tena na tena ila haikupokelewa. Hii ilinichanganya. Nikatabasamu kwa dharau huku nikitikisa kichwa na kukunja nne. Nikatetemeka kwa hasira, kifua kikajaa. Nikaishika tena simu na kupiga kwa mara nyingine. Nakumbuka iliita mara mbili halafu akakatwa. Sio siri sikuamini ninachokishuhudia. Nilitamani kuondoka kurudi nyumbani ila niliona huo utakuwa udhaifu wa kiwango cha lami.

Sikuweza kuvumilia dharau ile. Ule ni utovu wa nidhamu. Ni udhalilishaji! Nikanyanyuka kishujaa kwa hatua nikaelekea ndani ya lile hoteli. Nilipoingia tu nikakuta mlango wa lift unafunguka kisha anatoka Patrick na yule muhudumu. Wametokea vyumba vya ghorofani! Kwa sekunde kadhaa tulibaki tunatazamana. Hakuna aliyekuwa na ujasiri wa kumsemesha mwenzake. Niliona hofu iliyokuwa ikiwatafuna ndani yao.

Maswali yalitesa akili yangu. Walienda kufanya nini ghorofani? kwanini waende wawili tu? Kuna siri gani baina yao? Mbaya zaidi shati la mpenzi wangu lilikuwa limechomolewa, mwanzo halikuwa hivyo! Nini hiki jamani? Walikuwa wanafanya nini? Hisia zangu zilinipa majibu. Nimemkosea nini Patrick hata aniadhibu kiasi hiki? Mbona hana huruma? Ameniabisha Patrick! Nimekosa nini mimi Hamisa? Nililia sana.

Patrick alinisogelea akinisihi nisilie! Alitaka kunibembeleza. Unafki wa aina hiyo sikutaka kuuruhusu mbele ya macho yangu. Sikumbuki na wala sielewi nguvu zilitoka wapi! Nilimsukuma kwa nguvu Patrick! Alipepesuka akaenda kujigonga ukutani akapasuka paji la uso damu zikaruka. Wakati akiendelea kupepesuka akateleza kichwa kikaenda kujigonga kwenye meza ya kioo iliyokuwa eneo lile! Nilishuhudia kwa macho yangu kipande cha kioo kikiwa kimezama kwenye shingo yake.

Nilipata hofu damu zilipoanza kutapakaa eneo lile, ilitisha! Yule muhudumu aliogopa, alirudi nyuma huku anatetemeka kisha akaingia kwenye lifti akairuhusu ipande juu. Niliogopa sana nikamsogelea Patrick alikuwa anatoa povu mdomoni, nilichanganyikiwa! Nilijaribu kumuita Patrick ila hakuitika, nilimtikisa ila hakuamka. Alikuwa na jeraha kubwa shingoni.

Nikiwa sijui cha kufanya mlango wa lift ukafunguka akatoka yule muhudumu akiwa ameongozana na wanaume nane! Niliwatambua wale wanaume ni marafiki wa Patrick. Walishangaa kuona hali ile. Kila mtu alichanganyikiwa. Bila kupoteza muda wakashirikiana kumnyanyua ili kumuwahisha hospitali. Naumia kila nikikumbuka hili tukio. Moyo unaniuma sana. Hisia mbaya zilinifanya nichukue maamuzi ambayo sikupaswa kuyafanya. Leo najuta mimi! Nipo ndani ya jengo hili natumikia kifungo! Patrick alifariki njiani tukiwa tunampeleka hospitali. Sitokuja kusahau ile siku. Nililia sana. Nilihusika moja kwa moja na kifo cha Patrick. Ushahidi ulijitosheleza kabisa ni mimi ndiye muuaji.

Wakati kesi ikiendelea ndipo nikaujua ukweli. Siku ile ilikuwa muhimu kwa Patrick. Ni siku aliyokuwa akitaka kunivesha pete ya uchumba. Yule muhudumu alikuwa amepewa jukumu la kuandaa ukumbi wa hiyo hafla ambao ulikuwa ghorofa ya tatu ya ile hoteli. Ilitarajiwa iwe sherehe ya aina yake ila mimi nilivuruga kila kitu kisa hisia zangu. Masikini hisia zangu zimenifanya nidhurumu maisha ya mtu asie na hatia. Moyo wangu unanisuta, sitamani kuendelea kuishi. Najua mauti yatanikuta nikiwa humu! Najua nitakufa!

Leo nimekusimulia haya, nataka ukawasimulie na wengine. Kawaambie wasiruhusu hisia zao zikatawala maamuzi yao. Ni hatari sana maana hisia ni hisia tu zinaweza ziwe au zisiwe sahihi. Kawaambie wasifanye maamuzi wakiwa na hasira, huzuni au furaha sana maana itaadhiri fikra zao na maamuzi yanaweza yasiwe sahihi. Kawaambie waishi kwa upendo na amani! Maisha ni mafupi ila ukifanya maamuzi sahihi katu hutojutia.

HAYA NENDA KAWAAMBIE!
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…