Shibuda hayo ndiyo uliyotumwa CHADEMA? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Shibuda hayo ndiyo uliyotumwa CHADEMA?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by JOHN MADIBA, Jul 13, 2011.

 1. JOHN MADIBA

  JOHN MADIBA JF-Expert Member

  #1
  Jul 13, 2011
  Joined: Jan 30, 2011
  Messages: 251
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  KAKA yangu Shibuda, John Shibuda, umenishangaza. Umenishangaza na kunikatisha tamaa kwa kuwa wewe ni kiongozi na mwanasiasa ninayekubali siasa zako ingawa imani yangu kwako inaporomoka kwa kasi ya kutisha mithili ya gunia la ndizi ubavuni mwa mlima.

  Inaporomoka kwa kuwa ninakuheshimu na kukupenda sana kisiasa lakini kwa hili, hapana; hapana Shibuda siamini kama hili unalifanya peke yako, labda unihakikishie kuwa kuna remote control inakuongoza kuyafanya haya.

  Shibuda; Mbunge wa Maswa Magharibi (CHADEMA), ungesaini kuchukua posho za vikao vya Bunge tu ukaondoka, nisingekuwa na la kukuambia wala kuhofu juu yako kwamba labda ulitumwa kwa kazi maalumu CHADEMA, lakini kwa kuuambia umma wa Watanzania maneno haya, nimechoka.

  Nimechoka na kupoteza haraka imani yangu kwako. Hivi Shibuda ulikwenda kwa wananchi kuwaomba wakuchague uwe Mbunge wa Maswa Magharibi ili ukagange njaa? Shibuda!

  Hayo si maoni yangu mwenyewe, bali vyombo vya habari vilivyokukariri ukisema kuwa posho za vikao bungeni hazitoshi na badala yake, unapendekeza ziongezwe toka kiasi cha shiling 70,000 za sasa kwa madai eti, posho hizo ndicho kipozeo cha wabunge maskini kama wewe ambao eti hamna biashara kuendesha majimbo yenu. Shibuda, hayo yanatoka moyoni mwako kabisa au ni kinywani mwako tu?

  Shibuda, umeshindwa nini kuyajadili hayo ndani ya chama chako hadi uamue kuyapeleka bungeni ili Watanzania wote wakuone na kukusikia namna unavyotofautiana na wengi ukijua kuwa asiyekubali ya wengi…. Lakini, mchuma janga hula na wa kwao.

  Kulisemea hilo bungeni, umeuambia umma wa Watanzania na dunia nzima kwamba upo kwa ajili ya kutumia ubunge kupooza umaskini wako na sio kuwatumikia wanajimbo wako.

  Kama kwamba hiyo haitoshi, Shibuda, mbunge na mwanasiasa maarufu na mwenye uzoefu wa kutosha namna hiyo, unachukua mambo ya “chumbani kwenu” na kuyapeleka kwenye mkutano wa hadhara?

  Kwa hekima zote na busara ulizo nazo ukaona ni vyema uende nje uanze kuwarushia makombora ya lawama Mwenyekiti wa chama chako cha CHADEMA Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe kwa madai kuwa, wanahatarisha demokrasia ndani ya chama hicho kwa vile wanakiendesha kama chama chao binafsi (NGO).

  Haya mambo ndiyo yanavyofanyika hata katika familia kwamba msipoelewana unaenda kwenye mkutano kijijini na kuelezea mapungufu ya familia yako?

  Shibuda! Umenishangaza kwelikweli. Ninashangaa ingawa ninajua mbinu za wanasiasa katika kujitafutia umaarfu ni nyingi, lakini nyingi pia ni chafu sana ndiyo maana wengi wanasema siasa ni mchezo mchafu.

  Kwamba sio kweli kwamba kukataa posho ni msimamo wa chama, bali eti msimamo wa Zitto na Mbowe ambao wanaonekana kuendesha chama kwa ubabe, hujuma, kubomoa umoja na kujenga makundi ndani ya chama.

  Mheshimiwa Mbunge John Shibuda, hivi wewe ungekuwa Mwana CHADEMA au hasahasa, mwanasiasa imara na uliyeiva kisiasa ungeona kuwa huo ni ustaarabu?

  Angalia sasa umekalia kuti kavu. Umekalia kuti kavu ukiwa ni miongoni mwa wanasiasa (wabunge) wachache ninaovutiwa na siasa zao za msimamo wa kusimamia kile wanachoamini kuwa ni sawa haijalishi wangapi wanakiunga mkono au wanakipinga.

  Msimamo huo ndio uliokufanya utoke ndani ya chama ulichokuwamo awali; Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenda “uhamishoni” (CHADEMA). Hiki kilikuwa kipindi cha mpito kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

  Nakumbuka namna ulivyoamua kusema sasa basi; nimechoka; nimechoka kukaa CCM, ukatia jembe mpini na kufunga virago vyako, ukaenda, ukabisha hodi na kupokelewa CHADEMA.

  Ukaongeza nguvu katika kambi ya upinzani na kusababisha mvuto maana hata katika kipindi cha kampeni, wengi walitaka kujua una lipi jipya unalolipeleka CHADEMA ilhali awali ulikuwa kama vile umekunywa maji ya bendera ya CCM.

  Shibuda! Mtazamo wa watu kwako ulikuwa tofauti na ule waliokuwa nao dhidi ya Fred Mpendazoe; aliyekuwa Mbunge wa Kishapu (CCM). Fred, alionesha wazi kuwa, kwake maslahi ya kifedha si chochote si lolote kama nafsi yake inakiri kuwa hajapata nafasi ya kuutumikia umma ipasavyo.

  Mpendazoe, akafunga virago, akajitwisha na kuondoka, bila kujali wala kugeuka kuangalia nyuma kwamba anapoteza maslahi yake ya kibunge bungeni.

  Wakati huo, nilimpenda Shibuda kwani alisimamia msimamo wake wa kutumia haki yake ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa kwa nafasi yoyote iwezekanayo; ukaonyesha nia ya kutaka hata siku moja, aitwe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  Ingawa kwa wana CCM wengi hili lilikuwa likiwauma mithili ya kung’oa jino bila sindano ya ganzi, kwangu mimi lilikuwa tamu mithili ya asali; lazima kila mtu aoneshe na kutafuta nafasi ya kutumia kipaji chake bwana kwani nani kasema kuna watu walizaliwa mapacha na uongozi.

  Tazama ndugu yangu Shibuda; sasa imekuwa nongwa maana kuna tetesi kwa wadadisi wa kisiasa walioanza kukutabiria “kifo” cha kisiasa wakisema hivi sasa umekalia kuti kavu lililoning’inia katika mto wenye mamba wenye njaa kali wakikusubiri wakutafune kisiasa.

  Kiongozi wangu Shibuda, umekuwa msumbufu ndani ya vyama vya siasa unavyokuwamo.

  Hebu jitazame vizuri kwanini kila unapokuwa kunaibuka mengi; kwani wewe hauambiliki wala kushaurika. Ndugu yangu Shibuda, jenga tabia ya kuwa na sikio kubwa, lakini uwe na mdomo mdogo yaani, toa nafasi kubwa kuwasikiliza wengine na utoe nafasi ya kusema kidogo.

  Usipende kuwa msemaji na mwamuzi peke yako katika vyama; hakuna chama utakachokuta cha hivyo labda uanzishe chako binafsi na hicho nacho, usikiite chama, kitafutie jina lingine labda taasisi isiyo ya kieriali (NGO).

  Shibuda umekuwa tatizo sana maana siasa zako zinaonesha ni mtu usiyetaka kuonyeka, haushauriki wala haupuuziki lakini kubwa, huambiliki; umekuwa mwiba ndani ya vyama unavyokuwapo kikiwamo CHADEMA ambacho si siri nadhani, “kinajuta kukufahamu.”

  Kama kwamba hiyo haitoshi, wadadisi wanakuwa na hofu kuwa huenda kuondoka kwako CCM kulikuwa ni mkakati wa makusudi wa chama hicho ili kukutuma ukachunguze wapinzani wanafanya nini na “ukipata ulichotumwa”, utafute njia ya kurudi na “mzigo” yaani furushi la siri na mikakati ya upinzani.

  Ndiyo maana licha ya kukupenda kisiasa, lakini unayoyafanya sasa ndani ya CHADEMA yananifanya nikuulize kimyakimya kwamba, “hayo ndiyo uliyotumwa kwenda kuyafanya CHADEMA?”, kwamba ukawe mwiba ndani ya chama, ukawe mvurugaji ndani ya chama, ukaendekeze tofauti na wenzako wakati hata wahenga walisema silaha ya mnyonge ni umoja!

  Ndiyo hayo uliyotumwa kwenda kufanya huko CHADEMA ili ndani ya nyumba unyamaze, lakini ukifika bungeni unaposikika na kutazamwa kupitia luninga na vyombo vingine vya habari, uwaumbue viongozi wa chama ambacho bado umo na umeingia katika Bunge kwa tikiti ya chama hicho. Hivi mapungufu hayo umeyaona leo?

  Ina maana kaka yangu Shibuda ulikurupuka wakati unahamia huko toka CCM, au ulikwenda kwa makusudi na kazi maalumu. Hivi una mpango wa kurudi CCM sasa unatafuta gia ya kuondokea au utakwenda kuchafua hali ya hewa katika chama kingine?

  Kama unaona huko uliko hamwelewani, kwanini usihamie kwingine na kuonesha ujasiri wako kama alivyofanya Mpendazoe hata kama ni kwa kupoteza maslahi yako, lakini ulinde maslahi ya umma?

  Ndugu yangu Shibuda, badili mtazamo vinginevyo, kwako hizi zitakuwa ni harakati za kumaliza bucha mitaani, lakini ukakuta nyama ni ileile. Kwa mtindo huu, unatengeneza hatari ya kila chama kukuogopa na mwisho, ukirudi CCM utarudi ukiwa umebaki “makapi” ya kisiasa na kwa mtindo huo, hata ukianzisha chama, watu watakiogopa kama ukimwi.

  Epuka na utibiwe kabisa “ugonjwa” wa kupenda kufanya mapambano dhidi ya msimamo wa chama unachokuwapo. Hili ninalisema wazi bila kuzunguka zunguka; kwamba haushikiki, haukamatiki wala hauambiliki.

  Kumbuka hata namna ulivyoibuka ndani ya CCM, ukaibua agenda yako mwenyewe ya kushindana na Mwenyekiti wa Chama chako (CCM), Jakaya Kikwete katika kinyang’anyiro cha kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia ana “malaria ya mara kwa mara ya kukosoa” chama na kujitoa ili uonekane wewe pekee ndiye msafi miongoni mwa wanachama wa chama husika.

  Kumbuka uliyoyasema wakati ukichangia bungeni Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha wa 2011/ 12 bungeni mjini Dodoma.

  Ni wewe mbunge aliyetofautiana na msimamo wa chama chako wa kuwataka wabunge wa chama chenu (CHADEMA) kutopokea posho za vikao vya Bunge (sitting allowance).

  Viongozi wa CHADEMA na Watanzania wengi, wanapinga suala la kuwapo posho za vikao kwa wabunge wawapo bungeni kwa sababu mbunge kuwa bungeni, ni sehemu ya kazi yake hivyo hakuna anayestahili kupata mshahara wa kazi yake na kisha akapewa posho kwa kazi hiyohiyo anayolipwa mshahara.

  Wewe ukaenda mbali na kusema, uamuzi huo wa CHADEMA kukataa posho haukuwa sahihi kwa sababu posho ndicho kipozeo cha wabunge maskini kama yeye ambao hawana biashara kuendesha majimbo yao.

  Ndugu yangu, kiufupi kama anayaona magumu ndani ya CHADEMA kama ulivyoyaainisha, unasubiri nini kuchukua uamuzi kama alioufanya Mpendazoe na kuuthibitishia umma wa Watanzania kuwa hapendi malumbano? Ondoka CHADEMA, nenda kwingine au rudisha taarifa kama ulitumwa na CCM usichafue vyama vya upinzani na kuvipaka matope.

  Hata hivyo, vyama vyote havina budi kuwa makini dhidi ya “wahamiaji” wanaotoka chama kimoja kwenda kingine maana wengine si wanasiasa, bali wanaingia chama fulani wakiwa wametumwa kufanya kazi maalumu ya kuvuruga na kuchafua.

  Kama alivyosema Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu umefika wakati CHADEMA kikujadili kwa umakini na wewe uwe tayari kupokea uamuzi wowote wa chama ama chanya au hasi juu yako maana unalikoroga mwenyewe, huna budi kulinywa mwenyewe.

  Ukiwa binadamu, umejiamini kupita kiasi na bahati mbaya hujui kuwa kadiri muda unavyopita, wapiga kura wako wanazidi kukufahamu vizuri. Hivi Shibuda hayo ndiyo uliyotumwa CHADEMA?
   
 2. Echolima

  Echolima JF-Expert Member

  #2
  Jul 13, 2011
  Joined: Oct 28, 2007
  Messages: 3,169
  Likes Received: 531
  Trophy Points: 280
  Safi sana mkuu mpe vidonge vyake avimeze asimeze shauri yake,Inaonekana wazi kabisa Shibuda ni pandikizi la MAGAMBA.
   
 3. THINKINGBEING

  THINKINGBEING JF-Expert Member

  #3
  Jul 13, 2011
  Joined: Aug 9, 2010
  Messages: 2,726
  Likes Received: 854
  Trophy Points: 280
  Sikio la kufa......
   
 4. ndetichia

  ndetichia JF-Expert Member

  #4
  Jul 13, 2011
  Joined: Mar 18, 2011
  Messages: 27,641
  Likes Received: 236
  Trophy Points: 160
  duu hii kali sasa..
   
 5. Technician

  Technician JF-Expert Member

  #5
  Jul 13, 2011
  Joined: Mar 30, 2010
  Messages: 843
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Mkuu John Madiba,
  Unaonaje hii barua ikaenda moja kwa moja kwenye vichwa vya habari vya magazeti
  ya Tanzania kwa garama yoyote ili kuonesha jinsi gani huyu mdudu aliyetumwa
  kuvisambaratisha vyama vya upinzani.
   
 6. BPM

  BPM JF-Expert Member

  #6
  Jul 13, 2011
  Joined: Mar 10, 2011
  Messages: 2,766
  Likes Received: 15
  Trophy Points: 135
  huyu mheshimiwa ana lake jambo na mara nyingi anapenda kuwa tofauti na wengine .. cjui huwa ana mlengo gani
   
 7. k

  kiloni JF-Expert Member

  #7
  Jul 13, 2011
  Joined: Oct 28, 2010
  Messages: 575
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Huyu Shibuda ni mgonjwa wa akili!
  Anyang'anywe kadi haraka aende akachunge ng'ombe.
  HATUMUHITAJI
   
 8. M

  Msengapavi JF-Expert Member

  #8
  Jul 13, 2011
  Joined: Oct 23, 2008
  Messages: 4,802
  Likes Received: 2,749
  Trophy Points: 280
  Well written, well said! Bravo!!
   
 9. The Emils

  The Emils JF-Expert Member

  #9
  Jul 13, 2011
  Joined: Apr 16, 2011
  Messages: 570
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Shibuda ni nani hebu wana jamvi mwenye CV yake atuwekee hapa pengine tunamzungumzia mmoja wa wagonjwa wa mirembe hapa
   
 10. s

  smz JF-Expert Member

  #10
  Jul 13, 2011
  Joined: Dec 18, 2010
  Messages: 251
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Halafu wewe Shibuda,

  Sisi wapigakura wako - kama wengi wenu mnvyotuita, ndiyo tuliyokutuma hayo?? Yana manufaa gani kwa wananchi waliokuchagua?? Subiri Kamati kuu iamue, hukumu itakayotolewa sisi tuko tayari kuiunga mkono, shauri yako utaenda kumlaumu aliyekutuma kuropoka yote hayo.

  Halafu Shibuda nakuona kama mjanja: Hivi hukuchanganya na za kwako??
   
Loading...