Shairi: Samaki huyu analiwaje? (Fumbo)

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,498
40,046
Nawauliza malenga, ninyi mlio bobea,
Magwiji kutoka Tanga, na hata wa kule Mbeya,
Hata Tabora Igunga, swali ninawatolea,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Nimempata Mwaloni, ni pale Mwanza sokoni,
Ninaye hapa jikoni, mwenzenu ninabaini,
Ninayo njaa tumboni, samaki namtamani,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Magamba nimeparua, namwandaa samaki,
Na tumbo nikatumbua, nikapata taharuki,
Hewa akaichafua, nikapigwa tahamaki,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Njaa miya inauma, moyo konde nikapiga,
Ndipo mimi nikasema, nitaandaa mafiga,
Na nitampika vyema, nikaondoa uwoga,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Limao nikanyunyiza, saumu na pilipili,
Nikadhani nimeweza, samaki kumkabili,
Nimewazoea pweza, hawahitaji shubili,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Wala sikufua dafu, juhudi hazikufaa,
Na ilizidi harufu, pote ilitapakaa,
Imezidi maradufu, nimebaki kushangaa,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Nimejipikia wali, na uko kwenye sinia,
Naandaa maakuli, samaki namhofia,
Dua zangu nikasali, na uma nitatumia,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Nikamleta kinywani, harufu ikazidia,
Amenishinda jamani, miye ninawakiria,
Nifanye nini jamani, samaki nilopikia,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Kijijini wanicheka, na wengine wanong”ona,
Na hamu imenitoka, njaa bado ninaona,
Kipande kimedondoka, miye simtaki tena,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Ninacho kichefuchefu, naweka mbali sahani,
Imenishinda harufu, ya samaki wa Mwaloni,
Sasa nimejawa hofu, samaki siwatamani,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)
 
Fumbo mfumbie jinga, mwerevu huling'amua
Hata ulitie kinga, za ndui na za surua
Kwa lugha za kimachinga,watani wasozijua
Samaki aliyenuka, si wa kula maadili

Samaki aliyenuka, si wa kula maadili
Usije shindwa nyanyuka, kosa wa kukusetiri
Domo likakuchachuka,ukapoteza nawiri
Samaki aliyenuka, si wa kula maadili

Samaki aliyenuka, si wa maadili kula
Ni kitu cha kuepuka, tumbo lisije kufura
Utakuja kubabuka, uje laumu gagula
Samaki aliyenuka, si wa kula maadili

Si wa maadili kula, samaki aliyenuka
Ukijifanya u-mullah, watani tutasituka
Hata kipewa na Pula,siibadilishi hulka
Samaki aliyenuka, si wa kula maadili
 
samaki huliwa kwa raha, hawezi liwa kwa karaha
huwezi kumla kwa kuhaha, bali moyo ukiwa na furaha
samaki alonuka ni karaha, humnyima mtu furaha
tafuta samaki mwingine, wako wengi baharini

Hamu yako isikutoke kwa mmoja, maana wako wengi mwaloni
lililoharibika ni mmoja, mwingine hubanwi asilani
kama huyo mmoja ni kioja, rudi tena kule mwaloni
tafuta samaki mwingine, wako wengi baharini

samaki hutambulika uzuri,kwa macho yenye wepesi
mbaya akitiwa uturi, hujulikana kwa upesi
usijawe na kiburi, kazi hii si nyepesi
tafuta samaki mwingine, wako wengi baharini

mnunuzi hung'amua, hawezi nunua mmoja
ni mwepesi kuamua, huyu wa mchuzi ni mmoja
mwingine hawezi gundua, wa hamu kanunua mmoja
tafuta samaki mwingine, wako wengi baharini

ubovu hujulikana mwaloni, siyo kwenye sufuria
si mpaka jikoni, ubovu kugundulia
mafunzo ukiweka kapuni, wengi hawatakuaminia
samaki wawili wawili, ujifunze kununua
 
Kama usingelificha
kwa hiyo lugha ya picha
ukafungua pakacha
mambo yakawa mchicha
walaji tungekwambia,huyo samaki kachacha
na kama kweli kachacha
kumla budi kuacha
 
Mzee Mwanakijiji, huu ushauri wangu,
Usitafute magwiji, huku waunguza chungu,
Bahari ingali maji, kuna wengi kina changu,
Shida ni ya mlaji, li wazi tangu na tangu.

Usumbufu waupata, na wako huyo samaki,
Viungo kuvitafuta, mdalasini hiliki,
Kwanini bado wasita, huku wanena humtaki?
Waachie wale paka, wasodhuriwa na shombo.

Waachie wale paka, wasodhuriwa na shombo,
Hutaki huku wataka, bure wachafua vyombo,
Kijijini wakucheka, na utaumiza tumbo,
Acha kumng'ang'ania, samaki asokufaa.

Acha kumng'ang'ania, samaki asokufaa,
Nguvu nyingi watumia, kwa samaki kumpaa,
Lengolo hutofikia, na harufu yasambaa,
Kamtafute mwingine, ni uchu umekwingia.

Kamtafute mwingine, ni uchu umekwingia,
Wawili watatu wane, hata watano sawia,
Waache waja wanene, hiyo ni yao tabia,
Mzee Mwanakijiji, huo wangu ushauri.
 
Samaki huyu aliwaje?(jibu)

Mmekula na kusaza,chakula kukisifia.
Doa samaki unamtia,baada yakushibia.
Mnakua mfadhilaka,fadhia mna kimbia.
Hajaoza walakuchina,samaki lake shombo nukia.

Shombo wameumbiwa,kunuka mwasingizia.
Huo niwake uvumba,ndio maana mwang'ang'ania.
Nafasi mkiipata,pwani kwenda nunua.
Hajaoza walakuchina,samaki lake shombo nukia.

Kolekole si Koana,Uvundo kunukilia.
Mbawasi kinenge papa,mauongo wamenonea.
Sahanini wapendeza,tumboni kuanza kutia.
Hajaoza walakuchina,samaki lake shombo nukia.

Mkono na wako uma,pia waweza tumia.
Vyuma vyaleta uzia,mkono bora tumia.
Bora silete kasumba,matumbo vyema mtoa.
Mdomoni kimuweka,uvundo hauto sikia.
Hajaoza
walakuchina,samaki lake shombo nukia.
 
Wajumbe nimesikia, majibu mlochambua,
Samaki nitajilia, huku nikiziba pua,
Harufu ntavumilia, ya huyu niloparua,
Maji nimeyavulia, sina budi kuyaoga!

Shombo nitavumilia, samaki nikirarua,
Mwingine sitapania, baharini sitovua,
Sitaki kumwachia, utamuwe naujua,
Maji nimeyavulia, sina budi kuyaoga!

Mbinu nitazitumia, siri yangu naijua,
Samaki ataka nia, madirisha nafungua,
Upepo utaingia, harufu itapungua,
Maji nimeyavulia, sina budi kuyaoga.

Njaa imenizidia, ubishoo nauvua,
Samaki aniitia, mwenzenu nimeamua,
Nitamla naapia, magwiji nimeng'amua,
Maji nimeyavulia, sina budi kuyaoga.
 
Back
Top Bottom