Serikali yampuuza Masha | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali yampuuza Masha

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Teamo, Feb 16, 2009.

 1. Teamo

  Teamo JF-Expert Member

  #1
  Feb 16, 2009
  Joined: Jan 9, 2009
  Messages: 12,286
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 145
  Hatimaye imethibitika rasmi kwamba kampuni ya aliyodaiwa kuipendelea Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, ya Sagem Securite katika mchakato wa zabuni ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa, sasa imeenguliwa rasmi.

  Waziri Masha anatuhumiwa kuingilia kati mchakato huo baada ya kubaini kuwa kampuni hiyo imeenguliwa na Bodi ya Zabuni ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutokana na kukosa sifa.

  Hatua ya kuiengua kampuni hiyo ilimlazimisha Masha kumlalamikia Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa madai kuwa yeye (Masha) hakuhusishwa katika mchakato huo kama waziri mwenye dhamana.

  Taarifa ya kuthibitisha kuenguliwa kwa kampuni hiyo ya nchini Hispania, ilitolewa jana kwa vyombo vya habari na Bodi ya Zabuni ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kutaja kampuni sita zilizobakizwa kwa ajili ya kuendelea kuchujwa kati ya kampuni 54 zilizoomba zabuni hiyo yenye thamani ya Sh. bilioni 200.

  ``Bodi ya Zabuni ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeteua kampuni sita ambazo zitaendelea kuchujwa ili kupata kampuni moja itakayopewa kazi ya kuandaa mfumo wa Vitambulisho vya Taifa unaotumia teknolojia ya `smart card`,`` ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga.

  Kampuni zilizobakizwa katika mchakato huo baada ya mchujo wa kwanza ulioshirikisha kampuni 54 ambazo zilituma maombi ya kazi hiyo ni Unisys ya Afrika Kusini, Giesecke & Devrient Fze ya Dubai, Iris Corporation Berhad ya Malaysia, Madras Security Printers ya India, Marubeni Corporation ikishirikiana na Zetes na Nec ya Japan, na Tata Consultancy Services ikishirikiana na Ontrack Innovations LTD ya India.

  Taarifa hiyo ya Bodi ya Zabuni ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliongeza kuwa mchujo wa pili unatarajiwa kuanza mara moja na kukamilika haraka iwezekanavyo.

  Sakata la tuhuma kuwa Waziri Masha ameingilia mchakato huo lilipamba moto baada ya Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbrood Slaa, kumuuliza swali la papo kwa papo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akimtaka aeleze sababu za Masha kuingilia mchakato wa vitambulisho vya Taifa kwa maslahi yake binafsi na kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA).

  Katika majibu yake, Pinda alisema kuwa Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliiwahi serikali kuzungumziamchakato huo, lakini akakiri kuwa kuna taarifa za kunyofolewa kwa nyaraka za siri zinazohusu suala hilo katika jalada moja, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

  Baada ya Dk. Slaa kuendelea kutaka maelezo kutoka kwa Pinda, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alimshauri mbunge huyo kuandaa na kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili Wabunge wote wapate fursa ya kulijadili suala hilo.

  Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iliwahoji Dk. Slaa na Masha kuhusiana na tuhuma hizo, lakini hakuna kilichowekwa wazi.

  Aidha, Spika Sitta alitangaza kusitisha kujadiliwa kwa suala hilo kwa siku chache kabla ya kuahirishwa kwa mkutano wa 14 wa Bunge wiki iliyopita kwa maelezo kuwa ni kutaka kwahisha mchakato wa vitambulisho badala ya kuendelea kuhoji nani anauchelewesha.

  Kabla ya Sitta kusitisha suala hilo kujadiliwa bungeni, kulikuwepo na taarifa kuwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilijaribu kutaka kumuokoa Masha, dhidi ya hoja ya Dk. Slaa, kwamba ameingilia mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya taifa.

  Mpango huo ulikwama baada ya Pinda kuuzuia mpango huo.

  Waziri Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, alitoa angalizo hilo mapema wakati wa kikao cha wabunge hao.

  Habari ambazo Nipashe ilizipata kutoka ndani ya kikao hicho, zilieleza kuwa wabunge wengi walionyesha kuwa na hamu ya kuhoji suala hilo, hali iliyomfanya Pinda kugundua mapema na kuamua kulizima kabla halijaanza.

  Aliwaeleza Wabunge hao kuwa suala hilo lipo kwenye Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, hivyo hatua yoyote ya kulijadili, ingekuwa sawa na kuliingilia Bunge na kwamba hatua yoyote ya kujadili jambo hilo, ingeweza kuzua malalamiko mbele ya safari na kudhaniwa kwamba kamati ya wabunge wa CCM inaingilia kamati za Bunge.

  Nipashe ilidokezwa kuwa kabla ya kuanza kwa kikao, baadhi ya wabunge walikuwa wamejipanga kuhakikisha wanazima hoja ya Dk. Slaa Na kwamba baadhi yao walijiandaa kujenga hoja kuwa Masha hakuwa na kosa kuingilia mchakato huo, na kwamba kwa kutumia idadi kubwa ya wabunge wa CCM ndani ya Bunge wamlazimishe Dk. Slaa amwombe radhi Waziri Masha, pamoja na serikali kwa tuhuma alizotoa.

  Awali, Dk. Slaa aliliripotiwa na Nipashe akishangaa kuona Waziri Masha akiingilia shughuli ambayo anajua fika kuwa hana mamlaka nayo kisheria. Dk. Slaa alisema anashangazwa na hatua ya Waziri Masha kuandika barua ya malalamiko kwa Waziri Mkuu kutetea kampuni ya Sagem Securite.

  Dk. Slaa alisema kama Masha angeona kuna taratibu zimekiukwa alipaswa kumwelekeza mlalamikaji (Sagem Securite), hatua za kuchukua ikiwa ni pamoja na kuwasilisha malalamiko badala ya kulalamika kwa niaba ya kampuni hiyo.

  Imegundulika pia kuwa kampuni ya Sagem Securite, ambayo Masha anadaiwa kuwahi kukutana na maofisa wake waandamizi nchini Uswisi kwa siri mwaka jana, ilipata kuwaletea matata mawaziri watatu nchini Nigeria, ambao walifukuzwa kazi na kushitakiwa mahakamani kutokana na tuhuma za kupokea rushwa kutoka kampuni hiyo ili ipate zabuni ya kutengeneza vitambulisho vya taifa.

  Mawaziri hao walifukuzwa wakati wa utawala wa Rais Olusegun Obasanjo.
   
 2. Susuviri

  Susuviri JF-Expert Member

  #2
  Feb 16, 2009
  Joined: Oct 6, 2007
  Messages: 3,713
  Likes Received: 224
  Trophy Points: 160
  Mkuu, tunaomba ufanye kazi ya kuhariri na kutumia font yenye rangi nyeusi maana wazee unazidikutuharibia macho! Natanguliza shukrani zangu!
   
 3. Teamo

  Teamo JF-Expert Member

  #3
  Feb 16, 2009
  Joined: Jan 9, 2009
  Messages: 12,286
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 145
  asante mr susuviri,NIMEKUSOMA ILE MBAYA
   
 4. Fidel80

  Fidel80 JF-Expert Member

  #4
  Feb 16, 2009
  Joined: May 3, 2008
  Messages: 21,976
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 145
  Mkuu dgeouff nakushauri hii rangi uliyo tumia sio nzuri kwa sisi wenye macho ya kufifia.
  Tunakuomba uedit upya.
   
 5. Kandambilimbili

  Kandambilimbili R I P

  #5
  Feb 16, 2009
  Joined: Nov 11, 2008
  Messages: 782
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 0
  Naweza kufananisha habari hii sawa na magazeti yetu Tanzania, kichwa cha habari na habari yenyewe tofauti kabisa, huyu mwandishi amejaribu kufanya utafiti ajue sababu za kuondolewa hii kampuni? mwaka huu watu wengi watajiunga JF na habari za propaganzda zisizofanyiwa uchunguzi tutegemee kuziona sana.
   
Loading...