Serikali kuanza kutumia umeme wa Luku

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
SERIKALI imetangaza hatua kadhaa za kudhibiti matumizi ya fedha za umma, ikiwemo kutumia mfumo wa malipo kabla katika huduma za umeme na simu kuanzia mwaka wa fedha wa 2010/11.

Mbali na hatua hiyo, serikali pia itapunguza idadi ya magari yatakayonunuliwa na itaimarisha Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini (GPSA) na kulipa posho za nyumba kutokana na uwezo wa bajeti.

Akiwasilisha bungeni mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2010/2011, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kulipa ankara za simu na umeme kwa wizara, idara za serikali zinazojitegemea na halmashauri nchini.

"Katika mwaka ujao wa fedha serikali kwa kushirikina na kampuni za simu na umeme (TTCL, Tanesco) inadhamiria kuanza kutumia mfumo wa malipo kabla ya huduma (kama luku) kwa wizara, Idara za serikali zinazojitegemea na mikoa ili kudhibiti ulimbikizaji wa madeni ya huduma hizo. Hatua hii pia inalenga kuyaimarisha mashirika haya kimapato," alisema.

Kuhusu magari, Waziri Mkulo alisema serikali itaimarisha GPSA ili iweze kuratibu ununuzi wa magari ya Serikali ikiwa ni pamoja na kuainisha aina za magari yatakayonunuliwa kwa lengo la kupunguza gharama za ununuzi, uendeshaji na matengenezo.

Mkulo alisema pia kwamba serikali italipa posho za nyumba kutokana na uwezo wa bajeti na zitatolewa kwa wafanyakazi wenye stahili pekee na kwa viwango maalum badala ya asilimia ya mshahara kama ilivyo sasa.

"Pia fedha zilizopangwa kwa ajili ya posho mbalimbali katika wizara, idara za serikali, mikoa na halmashauri zitapunguzwa na kudhibitiwa ili kuepuka matumizi yasiyo ya lazima," alisema waziri huyo.

Mkakati mwingine wa kubana matumizi uliotajwa na Waziri Mkulo ni kuhakikisha kuwa mfumo wa kutayarisha na kutoa taarifa za hesabu (IMFS) unasambaa katika serikali zilizobaki za mitaa zilizobaki kwa lengo la "kuhakikisha kuwa fedha zinatumika kama zilivyopangwa".

Alisema kwamba kuanzia mwaka 2010/11, halmashauri zitatakiwa kuonyesha bakaa katika akaunti ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha ili zijumuishwe kwenye bajeti ya mwaka unaofuata kama chanzo cha mapato.

Hatua nyingine iliyochukuliwa kudhibiti matumizi kuanzia mwaka ujao wa fedha ni kutumia utaratibu wa malipo unaosimamiwa na Benki Kuu (BoT) unaojulikana kama Tanzania Interbank Settlement System (TISS) kwa malipo yatakayofanywa na wizara zote zilizopo Dar es Salaam ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ili kuharakisha malipo ya serikali.

Mkulo alisema hatua zimechukuliwa kulinda mfumo huo kutokana na athari zinazoweza kutokea.

Serikali kuanza kutumia umeme wa Luku
 
Back
Top Bottom